Jumatatu, 12 Desemba 2016

“Gimpel the fool” Gimpel mpumbafu au fala!



Naitwa Gimpel  mjinga au fala, Ingawa sifikiri kabisa mwenyewe kuwa ni fala au mjinga, kama watu wanavyonifikiri, Lakini ndivyo wazushi wanavyoniita, walinipa majina tangu nikiwa shuleni, nilipewa majina kama saba hivi waliniita Jinga, Punda, Bichwa maji, Levi, Mshamba, Wakuja, na Fala, na jina la mwisho ndio likawa maarufu zaidi, nilikuwa najiuliza kwa nini naitwa fala? Eti kwa sababu nadanganyika kirahisi, siku moja waliniambia Gimpel unajua kuwa mke wa Rabbbi amejifungua? Niliondoka shuleni mara moja ili kwenda kumuangalia, lakini kumbe ulikuwa ni uongo! Nilijiuliza nilipaswa kuangalia nini je tumbo lake kwamba halikuwa kubwa? au nilipaswa kuangalia nini ningejuaje kama ana mimba? Je ulikuwa ni ujinga nilioufanya? Aaah sijui lakini kundi lote la watu walinicheka, waligonga mikono yao na kurukaruka na kunizomea mpaka saa ya maombi ya usiku, haikunidhoofisha kwa sababu sikuwa mjinga lakini nafikiri walikuwa wamenipatia siku hiyo, mimi namcha sana Mungu, nikasema litapiata tu.

Nilipokuwa nikitoka shuleni kurejea nyumbani nilisikia mbwa wakibweka, kwa vile nilikuwa siogopi mbwa sikujali, lakini nilifikiri moyoni je kama mbwa hao ni kichaa na wataning’ata itakuwaje najua madhara ya kung’atwa na mbwa mwenye kichaa, hivyo niliamua kutimua mbio kama niliyenunua gari, lakini jambo la ajabu nilishangaa watu waliokuwa sokoni na madukani waliangua kicheko kikubwa sana, kumbe mtu mmoja aliiigiza mlio kama wa mbwa je ningewezaje kujua kuwa ni mtu? Lakini nilionekana kuwa mjinga pia.

Watu wengi walipogundua kuwa mimi ni mtu ambaye ninaweza kudanganyika kirahisi basi kila mmoja alijaribu anachoweza kukifanya ili mradi kunidanganya, wengine waliniambia Kaisari anakuja kwenu, wengine mwezi umeanguka huko Turbeen, tumegundua sanduku la thamani nyuma ya bafuni kwenu, na mengineyo mengi ili mradi tu walijua kuwa naweza kumuamini kila mmoja, na ndivyo ilivyo nilimuamini kila mtu na niliamini hakuna lisilowezekana kama ilivyoandikwa katika hekima za mababa, si hivyo tu niliamini katika wingi wa watu mfano kama kijiji kizima wangeniambia jambo ningeamini mpaka pale waliponiambia kuwa tunakutania, niliwaamini na nilijua ni jambo jema kuwaamini watu kuliko kuwa na mashaka nao.

Mimi nilikuwa yatima na bibi yangu aliyenilea alikuwa amezeeka sana na mwenye kukaribia kufa, hivyo nilipewa kazi ya kusaidia kuuza mikate kwa mtu mmoja aliyekuwa na baker ya mikate, nilipokuwa zamu pale karibu kila msichana aliyekuja kuoka mikate aliweza kunidanganya kama sio mara moja na zaidi, wengine wakiniambia kuna thawabu kubwa mbinguni kama ukiwa muungwana, wengine waliniambia mke wa kuhani amejifungua dume la ngombe tangu mwezi july, Ngo’mbe ameruka juu ya dari na kutaga yai, ili mradi tu wanidanganye, kijana mmoja aliyekuwa mwanafunzi wa Yashiva alikuja na kuniambia Gimpel ulipokuwa umesimama pale Masihi alikuja na kufufua watu wote makaburini na baba yako na mama yako wamesimama makaburini wakikuita, 

Kusema ukweli nilifahamu wazi kuwa jambo kama hilo haliwezi kutokea, lakini nilipoambiwa niliingia shaka kuwa labda huenda kuna kitu na nikashindwa kukishuhudia kwa macho yangu mwenyewe, lakini wakati wote nilidanganywa dahaa niliamua kuwa sitaamini jambo lolote na niliweka Nadhiri kutokuamini mtu, lakini hata hivyo walinichanganya sana nisingeweza kujua mwisho wa jambo kubwa mpaka lililo dogo nimelielewa kwanza.

Niliamua kwenda kwa Rabbi mmoja ili kupata ushauri, aliniambia “ni afadhali kuwa mjinga siku zote kuliko kuwa mwovu kwa saa moja” “wewe sio mjinga” alisema “wao ndio wajinga” kwa sababu yeye anayemsababishia ndugu yake makwazo na aibu Jehanamu inamuhusu, Kama haitoshi Binti wa rabbi alinichukua mpaka ndani, tukiwa tunaondoka katika sebule ya Rabbi binti yake aliniambia umeshawahi kubusu ukuta? Nikamwambia hapana kwanini hasa? Akaniambia ni sheria na unapaswa kuitimiza kila unapotembelea hapa, daah hilo halikuwa na madhara ati lakini aliangua kicheko naona alikuwa amenipata tena

Nilitamani sasa kuhamia mji mwingine, lakini kila mtu alikuwa akijishughulisha kunitafuta mimi, walinitafuta walinivuta koti langu mpaka wakararibia kulichana walinisemesha mpaka masikio yangu yalikuwa kama yanataka kulowa mate, alikuwa kama mwenye kulea mtoto hivi lakini niliambiwa kuwa huyu hakuwa mtoto wake ni mtoto wa ndugu yake na yeye ni bikira na bado ni msafi hajanajisika, niliwaambia mnapoteza muda wenu siwezi kumuoa mwanamke huyo, hata hivyo waliniambia unajiaibisha mwenyewe na kuwa watanipeleka kwa Rabi na kunishitaki kuwa ninataka kumchafulia jina lake, niliwatazama na kujua kuwa nnaweza kuwakimbia kwa vile wamenifanya kama mtani wao, waliniambia inaweza kuwa heshima kubwa kwa Mwalimu wako Rabbi kama tu utamuoa mwanamke huyu aliyelelewa na Rabbi itakujengea heshima, lilikuwa jambo zuri kidogo kwangu kwa vile nilijihoji kuwa huwezi kuvuka maisha haya pasi na kupitia hatua hii ya kuoa 

Nilimfuata katika nyumba yake ya udongo iliyokuwa imejengwa eneo kubwa la mchangani na kuingia ndani, kundi kubwa la watu walinifuata wakiimba nyimbo walikuwa kama nyuki wanaotaka kuingia mzingani, nilipofika karibu walisimama na kuniacha niingine mwenyewe, niliingia na kupenya katika kuta nyembaba za nyumba hiyo huku nguo nyingi zikiwa zimeanikwa, huku nyuma walikaa kimya na waliogopa kumsemesha chochote Elka maana ndio jina lake, wanamjua kuwa hapendi kuzungumza lakini akizunhgumza ana maneno makali sana, niliingia ndani na kumkuta akiwa anaosha miguu yake akiwa hajavaa viatu, alikuwa amevaa nguo ya kitani ambayo ilikuwa imefunuka upande mmoja, nywele zake zilikuwa nimebanwa vizuri kwa nyuma na chache zikiwa zinaning’inia usoni, alikuwa ameumbika vizuri, nilivuta pumzi na kukaribia kuzimia, alikuwa ananijua vema bila shaka, aliniangalia na kuniambia angalia nnani anayekuja kisha? alifuta kiti na kuniamuru nikae

Tuliongea swala zima la kuoana lakini nilimwambia sikatai lolote lakini ninaomba uniambie ukweli kabisa  wewe kweli ni bikira? Na je huyu mtoto kweli ni wa ndugu yako? Usinidanganye tafadhali kwa sababu mimi ni Yatima

Mimi pia ni yatima alijibu, kila atakayejaribu kukudanganya na yeye mwishoni na apinde pua yake, ni imani yangu kuwa watu hawawezi kutuchukulia kwa faida zao, mimi nataka ulipe mahari ya Elfu Hamsini tu sina makuu, na ngoja nikusanye michango mwenyewe unajua kwa nini alizungumza kwa uwazi kuwa ni mwanamke ndiye anayelipa mahari na sio wewe, kwa hiyo usianze kupiga bajeti kuwa nitafanyaje wewe kubali tu tuoane, kisha aliniambia waweza kurejea ulikotoka

Niliwaza du leo huenda nitaachana na kazi ya kuoka mikate, na mji wetu haukuwa mji wa watu masikini,waliandaa kila kitu na kuendelea na maandalizi ya harusi, haikuwa jambo gumu kwa harusi kuandaliwa wakati ule maandalizi yalifana na siku ya harusi iliwadia kumbuka harusi yetu ilikuwa ya kiyahudi kwa vile wote tulikuwa wayahudi, siku ya harusi ilipofika tulijiandaa kama kawaida, Harusi ilifanyika katika geti la uwanja wa makaburi, watu walifurahi kuimba na kunywa kweli kweli, wakati agano la ndoa lilipokuwa likifanyika nilisikia Rabbi mkuu aliuliza Bibi harusi ni mjane au mwanamke aliyeachwa, mwanamke aliyekuwa akimsaidia bi harusi alijibu kwa niaba yake ni yote mjane na aliyeachika, dah ulikuwa wakati wa giza nene kwangu, lakini sikuwa na jinsi wakati hu je ningetimua mbio wakati wa shughuli za harusi? Hali ilikuwa ngumu kwangu.

Watu waliiimba huku wakiwa wamevaa mavazi meupe na baada ya mahubiri wengine walirusha Maputo meupe juu wakimsifu Mungu na kwaajili ya kuwakumbuka marehemu, wengine walifurahi na kucheza mpaka karibu na mimi na wengine walinikumbatia kwaajili ya kunipongeza, zawadi zilitolewa nyingi sana lakini katika moja ya vitu vilinishangaza vijana wawili walikuwa wamebeba kijikitanda kidogo cha mtoto, niliuliza je tunahitaji hii kitu? Ni ya nini hii? Waliniambia usijali wala usiumize ubongo wako kitanda kitakuwa mikononi mwako, nilijiuliza sana maswali mmh hii nini tena naenda kupata utani mwingine, lakini nilijipa moyo kuwa mji mzima hawawezi kuwa vichaa kiasi hiki na haiwezekani mji mzima waamua kunifanya mjinga.

Jioni nilikwenda kugonga katika chumba cha mke wangu lakini hakuniruhusu kuingia kwake nilisema nini hiki sasa kwani tuliozwa ili kuja kutazamana? Aliniambia hapana lakini niko katika siku zangu! Nilimwambia lakini jana ulichukuliwa kwenda kuogeshwa ina maana hawakuliona hili? Alinijibu jana sio leo, na leo sio jana unaweza kuipiga leo kama unaiweza mmh kwa kifupi ilibidi nisubiri

Baada ya miezi minne alishikwa na uchungu wa kujifungua  mtoto, kha wanakijiji walikuwa kimya tu wala hawakunicheka sielewi aina hii ya unafiki, uchungu ulikuwa umemshika  na alikuwa amejiegemeza katika ukuta na kujaribu kutembea aliita Gimpel nakufa tafhadhali nisaidie alilia nisamehe, wanawake walikuja na kuingia chumbani mwake na wengine walianza kuchota maji na kutafuta beiseni la maji ahaa ningefanya nini nilikwenda kwenye sinagogi na kuanza kuomba nikirudia Zaburi kadhaa

Mji mzima walisikia jambo lile na habari zilitapakaa, nilisimama kwenye kona nikumuomba Mungu na kuimba zaburi hilo ndio nililoweza kulifanya katika wakati ule mgumu wa kufikiri mke niliyeoa anajifungua ndani ya miezi minne

Watu waliosikia walisikitika na kusema maombi maombi maombi, maombi hayawezi kumfanya mwanamke akawa mjamzito, mmoja alisema maneno mazito kwangu yaani wewe ni sawasawa na Ngo’mbe, kuna jambo zaidi ya hilo kwa Mungu!

Mke wangu alijifungua mtoto wa kiume, siku ya ijumaa tuliingia kwenye sinagozi na kiongozi wa sinagogi wakati wa matangazo alisema kuna sherehe kubwa sana kwa tajiri Gimpel kwani kwake kumezaliwa mtoto wa kiume, watu wote katika sinagogi waliangua kicheko, nilijisikia vibaya sana , lakini sikuwa na la kufanya maswala yote ya ibada ya mtoto na swala la kumtahiri yalikuwa yananihusu mimi

Mji mzima walihudhuria sherehe na shughuli nzima ya tohara ya mtoto, watu walikuja na vinywaji na zawadi na wengi walinipongeza na nilitakiwa kutoa jina nilimpa jina la marehemu baba yangu mzazi roho yake na istarehe kwa amani masikini, dah Baada ya sherehe watu wote waliondoka na nilibaki peke yangu na mke wangu alichungulia kwenye pazia na kuniita Gimpel

Mbona uko kimya meli yako imezama?
Nitasema nini? Umenifanyia jambo jema sana mara ya pili hii kama mama yangu angelikuwa hai na kulisikia hili angefariki mara ya pili nilimjibu
We chizi nini? Unawezaje kusema ujinga kiasi hicho alijibu kwa ukali sana Nilimwambia nani anapaswa kuwa Bwana hapa?
Unanini wewe eeh unawaza nini kwani? aliuliza tena kwa ukali Nilimwambia wazi kwamba je hii ndio njia sahii ya kumfanyia Yatima? Umefanya unyama wa hali ya juu nilimwambia
Aliniambia ondoa ujinga huu kichwani mwako mtoto ni wako!, anawezaje kuwa wangu nilihoji, amezaliwa wiki kama kumi na nne tu tangu tumeoana?

Aliniambia kuwa amini mtoto huyu ni wako akanieleza kuwa huyu mtoto alizaliwa akiwa hajatimiza siku zake, akaniambia nilikuwa na bibi yangu ambaye pia aliwahi kuzaa mtoto ambaye alikuwa hajatimiza umri wake kwa hiyo maji hufuata mkondo hata huyu hajatimiza umri wake kabisa na kisha alianza kuapa kwa mwenyezi Mungu kuwa hajaniambia uongo hata kidogo, sikuweza kumuamini nilimuita Rabbi na tukazungumza siku ya pili na aliniambia ni jambo la kawaida lilimtokea hata Adamu na Eva walienda kitandani wawili na wakajikuta wamekuwa wane, je hakuna mwanamke duniani ambaye sio uzao wa Eva? Walinihoji kiasi cha kuninyamazisha nilinyamaza lakini nani ajuaye mambo yanavyokuwa? na nilikuwa namuheshimu Rabbi na sikufikiri kama anaweza kunidanganya pia hivyo nilikuwa mpole


Taratibu nilianza kusahau machungu yangu, nilimlea mtoto kama wangu nilicheza naye alinizoea akitiwa zongo niliweza kumpeleka haraka wa watoa zongo na kalikuwa kananipokea na nilifanya kazi kwa bidii sana ili kumtunza mtoto huyu kama unavyoelewa ni gharama sana swala la malezi, nilifanya kazi kama ngo’mbe au punda na nataka nikwambie sijawahi kumchukia Elka kutokana na uovu ule, maisha yaliendelea ni kilea mwanangu na mke wangu kila siku jioni niliwaletea zawadi ya mkate, pia niliwaletea zawadi mbalimbali na mapocho pocho wakati mwingine niliiba ili niwaletee zawadi zenye kufaa naamini nitasamehewa kwa wizi huo lakini hii ilitokana na upendo wangu kwa familia yangu na kuonyesha kuwajali.

Nilikuwa nalazimika kulala mbali na nyumbani kutokana na kazi zangu na siku za ijumaa nilirudi hata hivyo mke wangu alikuwa akitoa udhuru wa namna mbalimbali katika kunipatia unyumba akitoa sababu mara kichwa kinauma, mara kiungulia na mara hivi au vile, kama mnavyojua wanawake walivyo, nilijisikia uchungu moyoni kwaajili ya hilo, zaidi ya hilo alikuwa na kaka yake mdogo ambaye alikuwa amekuwa na ni kijana katili sana aliposikia nikimkoromea aliwasha taa na kunimulika alinionya kuwa anaweza kunipiga vibaya na kwakuwa alikuwa na nguvu kunizidi nilinyamaza, walinitishia kunipa talaka pia hali ilikuwa ngumu, Nilihisi kuna mwanaume mwengine anayekula chakula changu na kuondoka lakini nitafanyaje mimi ni wale watu wanaoachia kila kitu mikononi mwa Mungu nilisema kama yuko mtu ananiibia Mungu atamlipa!

Siku moja usiku mashine yetu ya kuokea mikate ilipata shida na hivyo nilitakiwa kurudi nyumbani usiku nilifurahi kwani nilisema leo nitalala na mimi usingizi japo kidogo na mke wangu, lakini nilipofika karibu na nyumbani nilisikia kama watu wanaokoroma zaidi ya mmoja sikufurahi alikuwa mke wangu na mwingine alikuwa anakoroma kama Ngo’mbe alikuwa ni jamaa amelala na mke wangu nilipotaka kulala ilileta shida kubwa sana na makelele yalizidi kuwa makubwa kiasi ambacho niliona itakuwa aibu mji mzima na pia nitamwamsha mtoto hivyo nilirejea Kazini na kuchukua safleti za magunia nikatandika na kulala, hata hivyo sikupata usingizi nilikuwa nikijiuliza usiku kucha kuwa uonevuu huu uitaisha lini ni lini mimi nitaendelea kuwa mjinga, je hata ujinga na wajinga kama mimi hivi hakuna mwisho wao nilijiwazia Gimpel hataendelea kuwa mjinga nafikiri kuna mwisho wa kila kitu.



Asubuhi nilikwenda kwa Rabbi kwaajili ya maswala haya kesi hii ilikuwa na mvuto mkubwa sana na hivyo ilivutia watu wengi Elka aliposikia alikuja akiwa na mtoto, na alikanusha kila kitu na kusema huenda uko nje ya akili zako umerukwa na akili,Rabi alimkemea na kusema anajua maswala ya ndoto, maono na kupamabanua mambo, alimkemea huku akigonga meza, lakini alisimamia msimamo wake kuwa hakufanya jambo hilo ni uzushi tu alisema Elka.

Wauza nyama na wafanya biashara ya farasi wote walisimama upande wake na kumtetea, mwanamke mmoja alijitokeza na kuniambia tumeshakufahamu tabia zako, mara mtoto alianza kujikojolea na hivyo Elka alitakiwa kuondoka haraka kwa sababu katika sinagogi kuna sanduku la agano na haipaswi kitendo kile kutendeka katika sinagogi. Hivyo Elka alitolewa,

Nilimwambia Rabii nifenye nini sasa?
Lazima umpe talaka mara moja alinijibu Rabbi
Nikamuuliza je akikataa?
Aliniambia lazima utoe talaka hilo ndio la msingi na si vinginevyo
Nikamwambia sawa Rabbi ngoja nifikiri
Hakuna cha kufikiri ndugu yangu vinginevyo utabaki naye katika paa moja na tabia ileile
Je nikitaka kumuona mtoto niliuliza?
Achana naye huyo kahaba mwache aendelee na huyo mjinga wake
Alikazia hakikisha unalifanyia kazi hilo na si vinginevyo maadamu mimi ni hai sitaki kusikia tena
Wakati huo ulikuwa mchana na nilijiambia kuwa nitahakikisha ninalifanyia kazi.

Usiku nilipokuwa nimejituliza kwenye magunia nililifikiri jambo hilo kwa uchungu sana, nilimtafakari yeye na mtoto pia, Hasira zangu zilipanda sana lakini pia nilitafakari kuwa mimi sio mtu wa kukasirika kiasi kile, niliwaza na kutafakari kuwa wakati mwingine wanadamu hawawezi kuishi bila kukosea na kwa vile amekataa kabisa kwa kiapo huenda labda mimi niliona maluweluwe tu yaani unaweza kuona kama mtu halisi kumbe hakukuwa na mtu na kama ndivyo nitakuwa simtendei haki Elka na nilipotafakari hilo nilianza kububujikwa na Machozi, kisha asubuhi nilikwenda kwa Rabbi na kumwambia kuwa huenda nilikosea, Rabi aliniambia kama ni hivyo sina la kuamua katika kesi yako na unachopaswa kukifanya labda uendelee kumtunza mkeo lakini usilale naye tena na unapotuma matumizi tumia mtu na usionane naye tena.

Miezi tisa ilipita kabla marabi wote hawajafikia muafaka na mwisho walikubaliana na maoni yangu na waliandika barua sikufahamu kama lingechukua muda mrefu hivyo, hata hivyo baada ya miezi hii tisa Mke wangu alijifungua mtoto mwingine na sasa alikuwa mtoto wa kike, siku ya sabato nilimpeleka mtoto kwaajili ya Baraka za kikuhani na nilikaribishwa karibu na Torati na na kuombwa nitoe jina na nilimpa mtoto jina la mama mkwe wangu,watu walionifahamu walinitia moyo kuendelea na maswala yangu kwani walihisi labda nitaelemewa na huzuni wakinicheka, nilijiapiza kuwa sasa nitaamini kila neno atakaloniambia mke wangu kwani nisipomuamini yeye leo kesho nitashindwa kumuamini hata Mungu

Niliendelea kuitunza familia yangu na kuwasaidia chakula na kila kitu kilichowafaa, pia niliendelea kumsaidia kijana mmoja aliyekuwa jirani yangu na aliyekuwa anajifunza kazi, siku moja kijana huyu aliniembelea nyumbani na kuniambia Gimpel una mke mzuri kijana na watoto wawili wazuri sana ambao kwa kweli hustahili lakini kile watu wanachokisema kuhusu mkeo, kha watu wana midomo mirefu nafikiri unachopaswa kufanya ni kuwapuuza kama kama ulivyopuuzia msimu wa baridi uliopita.

Siku moja Rabbi alinitumia ujumbe na kuniuliza una uhakika kuwa uliwaza vibaya kuhusu mkeo? Nilimwambia ndio nina uhakika, aliniambia kwa nini sasa ulikuja ukishuhudia kuona mwenyewe kwa macho? Nika mwambia yalikuwa ji maruweruwe tu, aliniambia sasa unaweza kwenda nyumbani na kuendelea na maisha maana marabi wamekuruhusu nilibusu mkono wa rabi na kuondoka.

Nilitamani kwenda nyumbani mara moja sio jambo dogo kuishi mbali na familia, lakini nilijitia moyo kwenda kazini na kisha nitakwenda nyumbani jioni, jua lilipokuchwa nilifanya maandalizi na kubeba zawadi kibao na mikate na nikaanza kuelekea nyumbani, kulikuwa na mbaramwezi ya kutosha siku ile kulikuwa na kabaridi na barafu zilikuwa zinaanguka, niliona nyota kwa mbali na nilikuwa nikitembea kichwani kawimbo kalinijia na nilitamani kutembea huku ninaimba lakini nilihofia kuwaamsha watu waliokuwa wamelala, lakini nilikuwa nauwaza maana ni wimbo unaofukuza mashetani, niliendelea na safari, nilipokaribia nyumbani moyo wangu ulianza kudunda kwa kasi kama moyo wa mtu mhalifu, niliingiwa na hofu ya ghafla moyo wangu ukidunda kwa kasi sana, nilifika na kuona mwangaza ndani kutokana na Nuru ya mbaramwezi niliweza kuona mtoto mpya aliyezaliwa kakiwa kamelazwa aidha pia nilimuona mke wangu Elka akiwa amelala na nilipokaribia kabisa nilimuona my amelala karibu na mke wangu Elka na nilipoangalia vizuri unaweza kuhisi alikuwa nani? Alikuwa ni yule kijana niliyekuwa ninamsaidia, Ghafla ingawa mbaramwezi inawaka niliona giza kali,nilitetemeka na meno yalianza kugongana, mikate na zawadi zilizokuwa mkononi zilianguka ghafla na mke wangu alishituka usingizini huku akuliza nanii? Kwa sauti Gimpel? Imekuwaje umerudi na uko hapa? Mi nilijua umekatazwa? Sasa fanya jambo moja tafadhali nenda kaangalie kama mbuzi na kondoo hapo zizini wako salama maana mmoja alikuwa anaumwa, nilikwenda nilikuwa nimesahau kama tuna mbuzi na nilipozikia kuwa anaumwa nilimuonea huruma, nilipofungua mlango wa zizi, mbuzi yule alisimama na inaonekana alikuwa salama na wengine wote,baada ya hilo nilirejea ndani na kuuliza yuko wapi yule mjinga mke wangu aliniuliza mjinga gani? Nilimwambia yule kijana akaniambia hizo ndoto zako inaonekana una mapepo mjinga mkubwa we nitapiga kelele utokezako sasa hivi tokaa nilipotaka kuleta fujo Yule ndugun yake aliamka na kuja kutaka kunishambulia alinipiga vibaya kwa nyuma na nikafikiri amevunja shingo yangu nilitulia na kujiuliza kuna kitu hakiko sawa kwangu, mara yule nduguye aliniambia usije ukafanya kasfha nyingine hapa na hiyo mikate yako hakuna atakayekula hapa, Nilitulia 

 Sawa inatosha sasa Elka alisema na aliniamuru kulala kimya mpaka asubuhi bila kufanya lolote, asubuhi nilimuona yule kijana na nilitaka kumuonya lakini alinikemea kwa sauti kubwa kama mbwa na kuniambia nisikilize inakupasa uende kwa mganga au mtu yeyote mwenye uwezo wa kutibu akutibu kwa sababu nafikiri kuna misumari kicwani mwako haiku sawasawa duh, jamani kufupisha hii habari niliishi na mke wangu katika hali hizo kwa miaka 20, alizaa watoto sita wakiume wawili na wakike wane kwa mtindo huohuo mimi nikiamini tu kuwa ni wa kwangu, marabi waliniambia endelea kutenda mema kwani wenye haki huishi kwa imani

Ghafla mke wangu alianza kuugua kuanzia kwenye maziwa na kushuka chini kadiri siku zilivyoenda hali ilizidi kuwa mbaya, na ilionekana wazi kuwa hawezi kuishi, nilijaribu kuwaita madaktari na waganga kumtibu na kila siku walikuja kumwangalia na kumtibu nilimuuguza na kuacha kwenda kazini wakati huu nilikuwa na Bakeri yangu ya mikate na nilikuwa mtu tajiri lakini nilikuwa sijamwambia, pamoja na juhudi za kitabibu hakuna nafuu yoyote mke wangu aliipata hali ilizidi kuwa mbaya kabla hajafa aliniita kitandani na kuniambia Nisamehe sana Gimpel 

Nilimwambia unaomba msamaha kwa lipi?
Umekuwa mke mwaminifu na mwema sana
Ole wangu Gimpel alijibu mimi sio mwema Gimpel nimekudanganya kwa miaka hii yote sasa nataka kupatana na Muumba na leo nataka nikuweke wazi kuwa watoto hawa wote sio wa kwako, yaani kama kichwani mwangu ningekuwa ana akili ya mbao ingekuwa vizuri
Nilidakia ni wa nani sasa?
Sijui Gimpel tafadhali  nimetembea na wanaume wengi sana na sifahamu lakini nina uhakika sio wa kwako huna hata mmoja hapa, wakati ninashangaa aligeuka na kukata roho uso wake ukiwa na tabasamu ni kama alikufa akiwa ananiambia nimemdanganya Gimpel maisha yangu yote.

Siku moja baada ya kipindi cha maombolezo kuisha raho chafu ilinijia ikiwa na sura yake ikaniambia Gimpel mbonma unalala? ulimwengu mzima umekudanganya na ukaamua kuulipa kwa kuudanganya, nilimuuliza mimi nimeudanganyaje ulimwengu? Unawezaje kubeba mkojo katika kapu usiku na mchana na kutokuachie uende chooni? Kivipi?

Mimi nilikuwa nakudanganya kuwa hawa ni watoto wako na nilikuwa nalala na wanaume wengine lakini nawe ulikuwa unaudanganya ulimwengu kuwa hawa ni watoto wako na mimi ni mkeo
Nilimwambia je hujui kuwa kuna hukumu ya mwisho? 

Aliniambia hakuna hukumu ya mwisho ulimwengu umekudanganya, umetoa fedha nyingi ukaaminishwa kuwa umenunua paka tumboni mwako wakati hakuna paka hicho ndio kilichokukuta nikamwambia vipi kuhusu Mungu? 

Akaniambia hakuna Mungu pia ninachokuambia ni cha kusadikika tu.  Nilitamani kumpiga kwa nguvu lakini nilikuwa nimejaa hofu na nilitaka kupiga kelele kuelezea kilichotokea, mara yule kijana alikuja niliyekuwa nikimsaidia na baadaye alilala na mke wangu nilimkamata na kumtupia katika tanuru la moto la mikate kwa hasira nilimuua na kumzika pamoja na tanuru alisikika akisema leo umejilipizia kisasi, baada ya tukio hilo niliinamisha kichwa na  nilijikaza nikalala usingizi mara tena Elka akanijia katika ndoto akiwa na sanda akaniambia umefanya nini Gimpel 

Nilimwambia ni kwa sababu ya makosa yako kisha, nikaanza kulia akaniambia we we ni mjinga wewe ni mjinga kwa sababu mimi nilikuwa muongo kwenye kila kitu cha uongo na nilijidanganya hata nafsi yangu na sasa ninalipwa yote ukweli sikuwa nimemdanganya yeyote nilikuwa najidanganya mwenyewe najuta najuta sana, nilimuangalia uso wake na alikuwa mweusi sana,  kwa kuwa alikuwa motoni lakini aliniambia huna nafasi tena peponi uliyokuwa umewekewa kwa muda mrefu imefutwa,niliamka na nikakaa nikagundua kuwa kumbe kila kitu kilikuwa kimekaa sawa anayedanganya anajidanganya khah 

Niliharibu kila kitu kwenye bakeri ya mikate nilikwenda nyumbani na kuchukua mali sehemu Fulani niliwagaia watoto wote niliwaambia nimemuona mama yenu usiku wa leo ameungua vibaya motoni niliwaambia kila mmoja asahau kabisa kuwa yuko mtu anaitwa Gimpel na wao hawakujibu neno lolote walibaki kushangaa

Niliwabussu na kuwatakia maisha mema na nilivaa mabuti yangu na kuanza kuondoka kila aliyeniona mjini alinishangaa na kuniuliza unaenda wapi niliwajibu naenda ulimwenguni na nilihama mji ule kabisa walioniuliza niliwaambia nimedanganywa miaka yote ya ujana wangu lakini kwa kuishi kwangu sana nimegundua kuwa watu hawa hawakuwa waongo kwani ndio mtindo wa maisha usipodanganywa leo utadanganywa kesho na kama sio mwaka huu basi mwaka ujao na kila mtu anaweza kudanganya hata bila kukusudia

Nilihamia mji mwingine na huko nilikuwa nikipokelewa na watu kadhaa wa kadha nilikula chakula katika meza kadhaa isipokuwa usiku nikilala mji nioondoka ulikuwa unanijia na Elka pia nilijiuliza ulimwengu huu ni ulimwengu wa namna gani, Nilikuwa nikiishi maisha ya kuwasimulia vijana hadithi mbalimbali katika maisha yangu na nilizisimulia kiasi ambacho nilikuwa nasahau na kuzirudia zingine na watoto waliokuwa wakinifuata babu tusimulie khadithi niliwasimulia na wengine waliniiambia haa babu hii tayari.



Stori hii imeandikwa na Isaack Bashevis, Mwimbaji na mtunzi wa kiyahudi
Akionyesha maisha ya zamani huko ulaya miaka ya 1800 hivi wakati jamii ya kiyahudi ilipokuwa inaishi ulaya na inakuonyesha jinsi Gimpel alivyoweza kuozwa binti wa Kikuhani na rabi, lakini akidanganywa kuwa ni bikira na jinsi alivyoendelea kudanganywa maisha yake yote watu wakiitumia nafasi yake ya kumcha Mungu kama njia ya kumhadaa bila kujali kuwa alikuwa yatima pia ulimwengu ni ulimwengu wa udanganyifu, na ni ulimwengu ambao hauwezi kukuhurumia kwa sababu zozote zile, unaweza kuwa muongo wakati unajaribu kuwa mkweli, wanadamu ni waongo, makuhani pia ni waongo, hakuna uadilifu, mashetani nao ni waongo ni nani wa kuaminiwa? Unamuamini sana mkeo, Mumeo? Mchungaji wako? Chagua wa kumuamini mkweli ni mmoja tu Mungu pekee.

Imetafasiriwa na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumamosi, 10 Desemba 2016

Mungu wa Faraja yote. (God of all Comfort).



Andiko: 2Wakoritho 1: 3-7

3. Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote

Utangulizi:

Neno Mungu wa faraja yote linalojitokeza hapa na sehemu nyingine katika agano jipya limetokana na neno la asili la kiyunani “Paraklesis” ambalo maana yake ni wakili au mtetezi au mtu anayesimama karibu na mtuhumiwa ili kumtetea na kumsaidia,Neno hili limetumiwa mara nyingi sana na Paulo mtume katika nyaraka zake, na Mwandishi Luka na baadhi ya waandishi n wengine wa nyaraka na katika waraka wa Waebrania, ambapo neno hilo hujitokeza Mara 12 au kwa maneno yanayofanana na hilo mara 28

Neno hili ni la muhimu sana kwa wakristo wanaopitia magumu na mapito ya aina mbalimbali lakini zaidi sana mapito a taabu zinazotokana na kazi ya injili, ni muhimu sana kufahamu kuwa maisha ya ukristo yanajumuisha pamoja na kuteseka kwaajili ya Kristo biblia inasema tumeitwa si kumwamini tu bali kuteseka pamoja na Kristo, lakini hata pamoja na mateso hayo wakati huu Mungu hujihusisha kwa namna ya kipekee katika kufariji na hiki ndicho Paulo anakikazia katika kifungu hiki tunachojifunza leo.



Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia maswala ya msingi yafuatayo:-

·         Ahimidiwe Mungu. Mstari 3
·         Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo Mstari 3
·         Baba wa Rehema Mstari wa 3
·         Mungu wa Faraja yote Mstari wa 3

Ahimidiwe Mungu.

Neno Ahimidiwe Mungu katika Biblia ya kiingereza ya NIV linasomeka “Praise be to the God” na Biblia ya kiingereza ya KJV ambaoyo ndiyo iliyotumika kutafasiri Biblia ya Kiswahili ya Union Version linasomeka katika lugha hiyohiyo ambayo Kiswahili chake kingesomeka “Abarikiwe Mungu” Hata hivyo Biblia ya kilatili Vulgate inatumia neno “Benedictus” ambalo kiingereza chake lingesomeka “Heartfelt thanks be to the God” ambalo lingesomeka kwa Kiswahili rahisi  Atukukuzwe au Ashukuriwe sana Mungu, unaweza kuona vema katika Waefeso 1:3 “Atukuzwe Mungu

Salamu hizi kwa ujumla zinafunua moyo wa Paulo mtume ambaye alikuwa amejawa na wingi wa shukurani, na hivyo anaonyesha kufurahi na kushukuru kwa kiwango cha juu sana kwa Mungu, kwa nini Paulo anajawa na wingi wa shukurani kiasi hiki kwa Mungu? Paulo alikuwa ni mtu mwenye mzigo na kazi ya Mungu, alikuwa ni mtume mwenye moyo wa kichungaji, alikuwa na mambo mengi sana ya kuwaonya na kuwafundisha wakoritho hasa baada ya kanisa kumuandikia na kumsimulia yale waliokuwa wakiyapitia wakati akiwa hayupo, na aliwajibu kwa kuandika waraka wa Wakoritho ule wa kwanza sasa anapata taarifa kuwa Kanisa la Koritho sasa linaendelea vizuri, Paulo mtume alikuwa amekemea mambo mengi katika waraka wake wa kwanza ambao ulileta huzuni na toba kwa kanisa la Koritho na waliweza kufanya marekebisho mengi, sasa Paulo amesikia taarifa kuwa Kanisa linaendelea vema na sasa anafarijika na kufurahi sana kutokana na maendeleo mazuri ya Kanisa la Koritho, habari za maendeleo mazuri Paulo alizipata kutoka kwa Tito aliyekuwa akisimamia makanisa ya Akaya au Macedonia 2Wakoritho 7:8-10,12-16, Ni kwasababu hii Paulo mtume anamtukuza Mungu, anafurahi anamhimidi Mungu, ni kama mtu uliyekuwa na mgonjwa kisha ukapewa taarifa kuwa mgojwa huyo sasa anaendelea vema, au ameruhusiwa, kila mchungaji mwenye mapenzi ya kweli na kanisa hawezi kufurahi kanisa linapoharibika, hafurahii watu wakienenda katika njia isiyopasa, lakini watu wanapoendelea vizuri kunakuwa na furaha kubwa sana hali kadhalika walimu watafurahi kusikia wanafunzi wao wanaendelea vizuri wanafanya vizuri, madaktari na manesi hawafurahii kuona wagonjwa wakipoteza maisha wanapenda kuona wagonjwa wanapona

Huu ndio ulikuwa moyo wa Paulo Mtume anafurahi, anamtukuza Mungu anamhimidi bwana Mungu anamsifu anaonyesha moyo wa kufurahi, mambo yanapokwenda vema, kila mmoja anapaswa kufurahia mabadiliko mema ya kila mmoja wetu katika kumpenda Mungu, hatutarajii watu watasababisha huzuni, kila mmoja ataonyesha ukomavu, maendeleo katika kila Nyanja ni jambo hilo linaleta faraja kubwa sana, hakuna mama anayefurahia kuwa na mtoto asiyekua, lakini kila mtoto anapopiga hatua kina mama hushangilia sana anakaa, anatambaa, anaota meno, anasimama, anatembea anazungumza na hatua nyinginezo zote huleta faraja kubwa sana kwa kina mama wanaofanya malezi ya watoto.

Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo Mstari 3

Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo – Mahali hapa Paulo anamtaja Mungu lakini anaunganisha Mungu Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, kwa nini ? sababu kubwa ni kuwa hakuna mtu anaweza kuunganishwa na rehema za Mungu baba pasipokuweko kwa Yesu Kristo, Ni muhimu kufahamu kuwa watu wengi sana duniani hata wapagani wanafahamu sana Mungu kama Baba wa rehema lakini tatizo kubwa ni kuwa hawa wanataka kwa vinywa vyao tu hawajui kuwa rehema hizi za Mungu zimepitia kwa Yesu Kristo, ni kwa mateso ya yesu Kristo tu, ni kwa kusulubiwa kwake tu ni kwa kuiamini kazi aliyoifanya Yesu Kristo tu ndipo watu wanaweza kufaidika na rehema za Mungu baba  na upendo wake hakuna njia nyingine, Upendo wa Mungu umeunganishwa kwa mwana wake wa pekee Yesu Kristo na hakuna namna nyingine, kama tunapitia mateso katka imani yetu ni kupitiamateso ya Kristo 2Wakoritho 1:5 kama tunafarijika faraja hiyo ni kwaajili ya Yesu Kristo tu, Pasipo Kristo hatuwezi kufanya neno lolote. Shukurani anazozitoa Mtume Paulo kwa Mungu baba pia zinaunganishwa na Yesu Kristo yeye pekee ndio kipatanisho cha kweli kati ya Mungu na wanadamu

Baba wa Rehema Mstari wa 3

Baba wa Rehema – Ni muhimu kufahamu kuwa Paulo mtume alikuwa Mwebrania na ingawa aliandika waraka huu kiyunani, ni wazi kuwa alikuwa anawaza kiebrania, katika tamaduni za Kiibrania neno Baba lilitumika pia kumaanisha MWANZILISHI au chanzo kwa msingi huo linapotumika hapa linamaanisha Rehema zinatoka kwa Mungu, asili yake ni kutoa Rehema  na ndiye mwenye kuitunza rehema, 

Rehema ni sifa kuu ya Mungu, Ndani ya rehema kuna huruma, neema uvumilivu usioelezeka tunaita Mungu wa Rehema na neema , mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli Zaburi 86: 15 na ni kupitia sifa hizo ndio Mungu husaidia na kufariji, Vitabu vya tamaduni za kiyahudi Talmud vinaeleza kuwa ndiye yeye huanza kwa rehema na kumaliza kwa rehema, kila sura ya Quran isipokuwa moja tu zinaanza kwa kusema Mungu ni mwingi wa Rehema, hii ilikuwa ni salamu ya kawaida kwa waru wa mashariki ya kati kuhusu tabia ya Mungu kwa kiibrania “RACHAMIM” likimaanisha huruma au rehema Warumi 12:1 ni kutokana na tamaduni hizi na sifa hii ya kweli ya Mungu ilikuwa ni utaratibu wa kawaida kwa nyakati za kanisa la kwanza kumtaja Mungu kama Baba wa rehema

Mungu wa Faraja yote Mstari wa 3

Neno hili Mungu wa faraja yote ndio nenola Muhumu sana key word dhidi ya maneno yote katika kifungu hiki ni wazi kuwa kutoka mstari wa 3-7 neno faraja limetajwa mara kumi likiunganishwa na neno Mateso mara nne hivi au dhiki 

Mahali hapa panatupa matumaini yalkiyo wazi kuwa katika dhiki ya aina yoyote na mateso ya aina yoyote kamwe Mungu hawezi kutuacha wala kujitenga na upendo wake, Paulo ameona katika uzoefu wake kuwa wakati wote walipopita katika magumu Mungu alikuwa ni faraja , kwa msingi huo Mungu anafaraja yote, Mungu anaweza kuruhusu sisi kupita katika mateso na dhiki ili tuweze kuwafunza wenzetu jinsi Mungu alivyo mwema tuwe na ujasiri wa kuwashuhudia wengine upendo na neema ya Mungu, 

Mungu singeliweka faraja zake tungelikata tamaa, Dunia ni ngumu lakini kwaajili ya faraja zake tumejifunza kuvumilia kwa kuwa na tumaini Mungu anatufariji kwa Roho wake Mtakatifu, Paulo anaiona faraja nyingine kuwa ni kuendelea mbele na kukua wa kanisa la Koritho ambalo alilitaabikia, likaingiliwa na waalimu wa uongo, likaonyesha dalili mbaya akakemea ingawa alitumia waraka wake wa kwanza sasa wanaendelea vizuri, wanakua kiroho kwa kasi, kwa Paulo mtume hii ni aina ya faraja, Mungu anatufariji kwa viwango vikubwa anajua kutufariji katika kila aina ya dhiki na mateso, kila aina ya pito lisilo jema unalolipitia kumbuka kuwa Yuko Mungu wa faraka yote

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi.

Jumapili, 4 Desemba 2016

Mungu wa Kisasi Uangaze!



Andiko : Zaburi 94:1-3

“1. Ee Bwana, Mungu wa kisasi, Mungu wa kisasi, uangaze, 2. Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze, Uwape wenye kiburi stahili zao. 3. Bwana, hata lini wasio haki, Hata lini wasio haki watashangilia?



Utangulizi:

Je wewe umewahi kuona watu wakidhulumiwa? Umewahi kuona mahali haki haitendeki? Je hujawahi hata kusikia mahali watu wakionewa, wakiteswa, wajane na yatima na hata wageni au wakimbizi na wanyonge wakikandamizwa na kuonelewa huku wale wanaofanya dhuluma wakishangilia na kufurahi? Na hata wakidharau kuweko kwa Mungu na utetezi wake?

Jambo hili ndio hali halisi katika zaburi hii iliyoandikwa na Daudi, Hatuwezi kujua kuwa Daudi wakati huu alikuwa ameshuhudia nini katika mazingira yake, lakini kile anachokizungumza na kukililia katika zaburi hii kinafunua wazi aidha jambo ambalo amelishuhudia katika uzoefu wake wa maisha ama limewahi kumkuta, vyovyote vile iwavyo maswala haya yanaikumba hata jamii inayotuzunguka leo na Biblia hapa kupitia kinywa cha Mfalme Daudi ambaye pia Roho wa Kinabii alikaa ndani yake kuna mswala kadhaa muhimu ya kujifunza ambayo tutajifunza katika vipengele vifuatavyo:-

·         Kumuita Bwana kwaajili ya Haki (Zaburi ya 94:1-4)
·         Kushitaki kile wanachikifanya wadhalimu (Zaburi 94:5-7)
·         Kushangazwa na ujinga wa wadhalimu (Zaburi 94:8-11)
·         Baraka za kupitia katika magumu (Zaburi 94:12-13, 14-15)
·         Hatima ya kucheza na mwenye haki (Zaburi 94:16-23)

Kumuita Bwana kwaajili ya Haki (Zaburi ya 94:1-4)

Daudi anaiimba Zaburi hii katika mtazamo wa watu wanaoonewa, wanoteswa na kudhulumiwa na kutokutendewa haki watu hao wakimuangalia Mungu kama Jaji mkuu mwenye uwezo wa kutoa hukumu ya mwisho, wakati wengine wote wameshindwa kutoa msaada, Daudi anamuonyesha Mungu kuwa ndio mahakama ya juu zaidi tunayoweza kukata rufaa na tena mahakama hii ya juu zaidi inauwezo wa kutulipia Kisasi, Daudi anamtaka Mungu huyu mwenye uwezo wa kulipiza kisasi dhidi ya maadui zetu  aangaze, yaani aangalie kila kinachofanyika na kutoa haki

Wewe na mimi tumewahi kushuhudia kile ambacho Daudi alikishuhudia na kukililia katika Zaburi hii, inawezekana umewahi kushuhudia mume akifariki na kuacha mjane na yatima na Ndugu wa Mume wakiingilia kati na kudhulumu mali za yatima na kumuacha mjane huyo akiwa mikono mitupu wakiishi maisha ya dhiki, tumewahi kushuhudia wanawake wakorofi wakipora mali za waume zao na kujimilikisha, ndugu jamaa na hata watoto wakigombea hati za viwanja, kadi za magari, watu wakichongeana makazini na kusababisha wenngine wafukuzwe kazi, na kushangilia mafanikio ya anguko la mwingine, watu wakichafuana kwa faida na maslahi yao wenyewe na hila za aina nyingi zikifanyika duniani zinazofanana na hayo

Biblia inatufundisha kuwa endapo tumezulumiwa kila tunachokistahili na hakuna wa kututetea pako mahali ambapo tunaweza kudai haki zetu, Yesu alifundisha kwa msisitizo kuhusu madai ya haki zetu kwa Jaji mkuu wa majaji wote duniani, Mfalme wa wafalme mwenye uwezo sio tu wa kutoa haki bali pia kulipiza kisasi kwa watakaotudhulumu 

Luka 18: 1-81. Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. 2. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. 3. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. 4. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, 5. lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. 6. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. 7. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? 8. Nawaambia, atawapatia haki upesi;”

Daudi anamuomba Mungu haki iweze kupatikana, Yesu anatufundisha kuendelea Kumuomba Mungu mpaka haki yetu iweze kupatikana Yeye ni Jaji mkuu, ni Hakimu wa Dunia nzima, tunaweza kuimuendea yeye kwa ujasiri atupatie haki yetu, hatuhitaji kulalamika Yuko Mungu wa kisasi mwenye kuihukumu inchi na kuwapa stahili zao wenye kiburi, Yeye atawahukumu watu wote na pia ndiye mwenye kulipiza kisasi kwa wadhalimu na ndiye anayeteua majaji Warumi 13:4

Biblia inatufundisha kuwa tunapodhulumiwa tumuombe Mungu na kumsihi aangazie kile kinachoendelea, Hatupaswi kutumia njia yoyote ile yenye kutaka kujilipia kisasi wenyewe ni muhimu kumuachia Mungu yeye ndiye atakayetulipia kisasi.

 Warumi 12:19Wapenzi, Msijilipizie kisasi, Bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa Kisasi ni juu yangu mimi nitalipa anena Bwana

Kushitaki kile wanachikifanya wadhalimu (Zaburi 94:5-7)

Daudi mwandishi wa Zaburi anaendelea kumwambia Mungu kilie wanachokifanya wadhalimu, wote tunajua kuwa Mungu anafahamu kila kinachoendelea lakini Daudi anataka kufafanua, kuchamganua kile ambacho ameona kinaendelea na anataka Mungu akiangazie 

5. Ee Bwana, wanawaseta watu wako; Wanautesa urithi wako; 6. Wanamwua mjane na mgeni; Wanawafisha yatima. 7. Nao husema, Bwana haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri.”

Daudi anaelezea jinsi sifa ya wadhalimu hao walivyo, hawana huruma, wana kiburi na wanazungumza kwa kejeli na kiburi cha hali ya juu, hawajali hata kile wanachokizungumza, wanazungumza vibaya na wengine, sio watu wa dini wala hawamjali Mungu, wanajiamini wanajitegemea, wanavunja watu mioyo, wanagawa watu, wanawaua watu,hawajali huyu mjana wala yatima, wanajisemesha kuwa nani atatwatetea nani atawaokoa na uwezo walio nao ni makatili, hawajali wageni wala wakimbizi, Daudi aliwasoma vema maadui hawa na kuwaona jinsi walivyo wabaya na wakatili na alieleza Moyo wake kwa Mungu kuwahusu, wako watu Duniani ni wabaya na hawana haya unaweza kujiuliza ni roho ya namna gani waliyonayo na usipate majibu kwamba wanaongozwa na ibilisi au vipi wakati mwingine unaweza kuona ukatiliwao unazidi hata ule wa ibilisi mwenyewe Mungu atulinde na watu wa aina hii 

Kushangazwa na ujinga wa wadhalimu (Zaburi 94:8-11)

8. Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? 9. Aliyelitia sikio mahali pake asisikie? Aliyelifanya jicho asione?         10. Awaadibuye mataifa asikemee? Amfundishaye mwanadamu asijue? 11.  Bwana anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili.”

Daudi anashangwazwa na jinsi wadhalumu hao walivyojawa na roho ya udanganyifu wanafanya uovu mkubwa kwa kujiamini kiasi cha kupofuka macho na kuwa wajinga na wasiofikiri wala kuwa na akili Daudi anauzoefu kuwa Mungu Jaji mkuu atafanya kitu haiwezekani Yeye aliyemuumba mwanadamu awe na sikio kisha yeye mwenyewe asisikie, Yeye aliyemuumba mwanadamu kuwa na jicho kisha asiione yanayotendeka, yeye anayeshikisha watu adabu asikemee udhalimu unaoendelea, yeye anayewafundisha wanadamu sheria na jinsi iwapaswavyo kuenenda asijue uharibifu unaoendelea, anahitimisha kuwa Mungu anayajua mawazo ya wanadamu na anatambua kuwa ni ya ubatili

Wako watu wameharibika mioyo kiasi cha kutokutambua kuwa yuko Mungu anayeona na kusikia, wako watu wanafanya uovu kana kwamba wao ndio Miungu na hakuna awaye yote aliye juu yao, Daudi anasema huu ni ujinga wa watu na unaweza kufanywa na watu wasiofikiri, tena anawaita wapumbavu na anajiuliza ni lini watakapopata akili

Baraka za kupitia katika magumu (Zaburi 94:12-13, 14-15)

12. Ee Bwana, heri mtu yule umwadibuye, Na kumfundisha kwa sheria yako; 13. Upate kumstarehesha siku za mabaya, Hata asiye haki atakapochimbiwa shimo.14. Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake, Wala hutauacha urithi wake, 15. Maana hukumu itairejea haki, Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata.

Daudi anatumia mistari hii kumuita heri mtu anayepitia katika majaribu kwake yeye kupitia katika hali ngumu ni kuadibishwa na Mungu ni kufundishwa sheria na kanuni za Mungu na kuwa hatima ya Mungu ni kuja kutupa starehe wakati wa mabaya na kuwa mwisho wa adui upon a tutawaona adui zetu wakizikwa wakichimbiwa shimo, Daudi aonyesha ya kuwa Mungu hatawatupa watu wake hawezi kutuacha maana kila anayemcha yeye ni urithi wake, ana uhakika kuwa Mungu atafanya hukumu atarejea  na haki itapatikana na waliowanyofu wa moyo watanufaika nayo

Dhuluma zinazoendelea Duniani hazitadumu, uko wakati Mungu atakomesha , atahukumu kwa haki na kuwasterehesha wote walioonewa na mwisho wa wabaya tutauona Ndugu yangu kama asemavyo Daudi na kama lisemavyo neno la Mungu Bwana hatawatupa watu wake hawezi kuuachia Urithi wake 

Hatima ya kucheza na mwenye haki (Zaburi 94:16-23)

16. Ni nani atakayesimama Kwa ajili yangu juu ya wabaya? Ni nani atakayenisaidia Juu yao wafanyao maovu? 17. Kama Bwana asingalikuwa msaada wangu, Nafsi yangu kwa upesi ingalikaa penye kimya. 18. Niliposema, Mguu wangu unateleza; Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza. 19. Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako zaifurahisha roho yangu. 20. Je! Kiti cha udhalimu kishirikiane nawe, Kitungacho madhara kwa njia ya sheria? 21. Huishambulia nafsi yake mwenye haki, Na kuihukumu damu isiyo na hatia. 22. Lakini Bwana amekuwa ngome kwangu, Na Mungu wangu mwamba wangu wa kukimbilia. 23. Naye atawarudishia uovu wao, Atawaangamiza katika ubaya wao, Naam, Bwana, Mungu wetu, atawaangamiza

Mwandishi wa zaburi anahitimisha kwa kuuliza swali nani atasimama kunitetea dhidi ya adui zangu? Na ni atanisaidia dhidi ya waovu au wadhalimu? Kisha anaonyesha kuwa Bwana ni Msaada na kama asingelikuwa msaada waovu waneipoteza nafsi yake, Lakini fadhili za Bwana ni njema na zilimtegemeza Mungu alifanyika faraja kubwa  pamoja na udhalimu wanaoufanya Mungu akikimbiliwa anakuwa mwamba na atawarudisha waovu hawezi kukaa nao kiti kimoja atawaangamiza katika ubaya wao na hakika atawaangamiza 

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu anaona kila aina ya uonevu unaoendelea katika ulimwengu, inatupasa kukata rufaa na kudai haki zetu kwa dua sala na maombi, Mungu atatutetea, ataingilia kati jambo kubwa la msingi ni kumwambia mlipiza kisasi aangaze Tumuombe Mungu wa kisasi aangaze amulike aangalkie aone atazame na kukemea kila aina ya ubaya , uovu  na udhalimu wa watu walioota sugu walioharibika mioyo wasiojali wanaodhulumu, wanaoibia watu wakidhani kuwa hakuna utetezi dhidi ya wanyonge Bwana ana aliangalie jambo hilo na kulikemea Katika Jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!

+255718990796