Ijumaa, 16 Februari 2018

Je ! Mifupa hii yaweza kuishi?



Mstari wa Msingi: Ezekiel 37:1-3 “.Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa; akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana.  Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe”.


Je! mifupa hii yaweza Kuishi?
Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Wana wa Israel walikuwa wameokolewa na Mungu kwa uweza mkubwa sana wote tunakumbuka jinsi Mungu alivyomuadhibu farao kwa mapigo mazito chini ya mkono wa Mtumishi wake Musa na Haruni, mpaka Mungu alivyojipatia taifa na kulistawisha katika nchi ya mkanaani na kuwa na ustawi mkubwa sana chini ya waamuzi na wafalme. Hata hivyo ni jambo la kusikitisha kuwa baada ya muda mfupi, walimuacha Mungu na kuabudu miungu na kumpuuzia Mungu aliyewaokoa, ukweli ni kuwa walisahau historia nzima na kugeukia njia zao, Hivyo Mungu aliruhusu waweze kwenda utumwani tena.

Mwaka kama wa 722BK na 586BK  Mungu aliruhusu Israel kuchukuliwa uhamishoni na Yuda kuchukuliwa uhamishoni Babeli chini ya utawala wa mfalme Nebuchadnezer, Jeshi la Nebuchadnezer liliizingira Yerusalem na kuharibu na kusambaratisha vibaya Hekalu lililokuwako Yerusalem na kulichoma moto kuwa majivu, na wayahudi walichukuliwa kwenda Utumwani Babeli, hiki ndio kilikuwa kifo cha Taifa hili na mwisho wa matumaini yao. Huu ulikuwa ni msiba mkubwa sana ambao haukuwa na matumaini ya kuupoza.

Daniel 1:1-4 “Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadreza mfalme wa Babeli,alikwenda Yerusalemu akauhusuru.Bwana akamtia Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu; naye akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu wake.  Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana;  vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.    

Katika wakati huu watu wazuri na vijana wazuri na kila kitu kizuri kilichukuliwa utumwani Yerusalem ilibaki ukiwa huku kukiwa hakuna matumaini tena, Ezekiel nabii alikuwa ni miongozi mwa watu waliochukuliwa utumwani kwa mujibu wa historia.

Ni katika wakati huu sasa Ndipo Mungu alimwambia nabii Ezekiel katika maono aweze kuangalia bonde hili lisilo na matumaini, bonde lenye umauti usio na tumaini la kurejea tena na mifupa ilikuwa imetapakaa na ni mikavu hakukuwa na matumaini ya uhai na ndipo Mungu alipomuuliza Ezekiel swali hili Je mifupa hii mikavu yaweza kuishi?

Kwa ukweli maono haya yalikuwa yanalihusu Taifa la Israel kwa wakati huo kwa sababu walikuwa wamekata tamaa, walikuwa wamepoteza tumaini, waliona mauti na kujihisi kuwa ni kama wamekatiliwa mbali Ezekiel 37:11Kisha akaniambia, Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli; tazama, wao husema, Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea; tumekatiliwa mbali kabisa.”ni kweli kuwa hakukuwa na namna na jinsi ya kujiokoa kutoka katika msiba huo, kwani watu wengi waliuawa na wengine walichukuliwa kwenda utumwani , Israel iilikuwa tayari limegeuka kuwa bonde lisilo na uhani, na ni lenye mauti sisyo na matumaini hii ilikuwa ni picha ya kukosekana kwa matumaini.

Tukio la jinsi hii lilijirudia tena Israel waliporudi tena kutoka utumwani, walipata Hekalu na Yesu alikuja lakinimnamo mwaka wa 70 hivi walitawanywa kotekote uhamishoni duniani na hakukuwa na matumaini tena na hekalu lilibomolewa lakini ilipofika 1948 Israel ilipata uhuru wake na kufanyika taifa tena Mungu ni mwaminifu kwa watu wake Historia inatushuhudia.

Hali hii sio tu kuwa ilikuwa inaihusu Israel wakati ule, lakini inawezekana ikawa inatuhusu sisi nasi katika siku hii ya leo, inawezekana uko mahali hapa unaisikia sauti hii, au unasoma makala hii, lakini ukiwa katika hali ya uzuni nzito inayokukabili, moyoni mwako ukiwa umepoteza matumaini, huoni nuru mbele matumaini yako yamepotea, una vyeti kadhaa vya madaktari, una shuhuda kadhaa za watu wenye tatizo kama lako na wote mmeambia kuwa tatizo lako haliwezekani, inawezekana ni wachawi wameharibu ukoo wenu, ni adui zako wamesema wale tumewaweza kwa hali hii hawachomoki tena, hawainuki tena uko katika giza nene, inawezekana watu wakakuona una-smile lakini Moyoni huna amani ya kweli, moyoni ni misiba, moyoni ni kukavu, hufurahii uwepo wa Bwana, unalia kilio cha ndani unajiuliza matumaini yatatokea wapi? Unajiuliza kehso itakuwaje? Unajiuliza nawezaje kukabiliana na aibu hii? Kila kitu kimesambaratika hakuna matumaini ya kusimama tena, ndoto zako zimeyeyuka? Mambo unayotaka ni kama hayaendi?

Namshukuru Mungu kwa Jibu alilolitoa Ezekiel 37:3bNami nikajibu Ee Bwana Mungu wajua wewe.” Ezekiel yuko katika Bonde lililojaa mifupa mikavu tena iliyotawanyika na kwaakili za kibinadamu hakuna uwezekano wa kuweko uzima wala ufufuo, ni vigumu kukubali hali halisi ya uzima hapa ni vigumu hata kufariji we ungejibuje swali kama hili, Lakini jibu la nabii Ezekiel linaonyesha kwa sehemu alijua kuwa Mungu anaweza kuwa anaelewa zaidi.

Ezekiel ni kama alikuwa anajua kuwa Mungu anaelewa zaidi, ni yeye pekee anayeweza kuingilia kati na kufanya kitu katika mazingira ambayo akili ya mwanadamu imefika mwisho, Ezekiel alikuwa anajua kuwa Mungu anaweza kufanya lolote analolitaka, kwa Mungu hakuna linaloshindikana, Mungu akitaka mifupa hii mikavu iiishi itaishi.

Mungu amenituma leo nikutangazie kuwa yasiyowezekana kwa wanadamu, Kwa Mungu yanawezekana kwake liko tumaini kubwa sana na hupaswi kukata tamaa, kila matumaini yanayofifia katika moyo wako na ndoto zako Bwana anaweza kukuinua tena Ee bwana Mungu wajua wewe ilikuwa ni sauti ya Ezekiel akimjibu Mungu ashukuriwe Mungu Ezekiel hakusema haiwezekani, lakini alisema Mungu anajua liko tumaini katika yeye, atakufufua tena atakupa uhai, kama alivyoipa Israel uhai, wa kisiasa na kiroho na kuliponya taifa lile na kulilinda hata liko tena leo.

Mungu atakuinua tena, Simama tena changamka usikae chini na kusikitika kuwa itakuwaje iko pumzi ya uhai leo, Bwana atakuganga kwa upya, kila kilicho na uhai na kisicho na uhai kinasikia neno la Mungu leo neno la Mungu linakuja kwako kama pumzi ya uhai nawe utajua ya kuwa Bwana ndiye Mungu Ezekiel 37:4-6Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la Bwana. Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi. Nami nitatia mishipa juu yenu, nami nitaleta nyama iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.” 

Nakuomea ili kwamba Bwana afufue na kurejeza matumaini yako kila yanakoonekana kufifia aku kufa katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai.

Ni matumaini yangu kuwa umebarikiwa na ujumbe huu ningependa kupata maoni yako kama ujumbe huu umekubariki, na ni imani yangu utakubariki, au utabariki washirika wako usisite kumshukuru Mungu japo kwa ujumbe was sms

Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima.

0718990796        

HASIRA YA BWANA !



Zaburi 90:7-11Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako? Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima. Ee Bwana urudi, hata lini? Uwahurumie watumishi wako. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.  Utufurahishe kwa kadiri ya siku ulizotutesa, Kama miaka ile tuliyoona mabaya. Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, Na adhama yako kwa watoto wao. Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu, Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti, Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe.” 



  • ·         Mifano ya kibiblia inayoonyesha kuweko kwa Hasira ya Mungu.
  • ·         Sababu ya kuweko kwa hasira ya Mungu.
  • ·         Hasira ya Mungu inafunuliwa namna gani.
  • ·         Hatima ya Hasira ya Mungu.
  • ·         Namna ya kujiokoa na hasira ya Mungu ijayo:


Utangulizi:

“Hasira ni hisia kali zinazotokea wakati jambo linalofikiriwa kuwa baya au lisilofaa au lisilola haki linapokuwa limetendeka” wanadamu kwa kawaida huwa wana hasira, Na hali kadhalika Mungu katika nyakati fulani fulani hufikia kiwango cha kutokuendelea kuwavumilia wanadamu pale wanapotenda yasiyopaswa! Neno la Mungu limejaa mifano mingi inayoonyesha juu ya hasira za Mungu pale wanadamu walipotenda kinyume na mapenzi yake!

Musa alifahamu kuwa Mungu ndiye aliyekuwa akiwaongoza wana wa Israel, aliona jinsi Mungu alivyowaokoa Israel kwa uweza mkubwa, kupitia mapigo yale 10 na vilevile namna alivyowaokoa Israel kwa kuwavusha bahari ya shamu na kumwangamiza Farao na majeshi yake yote kwa sababu walikuwa wakijaribu kupingana na mpango wake dhidi ya watoto wake na taifa lake teule, lakini vilevile Musa alishuhudia Mungu akiwaangamiza walwi 250 baada ya kuivuka bahari ya shamu, kwa hiyo sasa Musa alikuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu Hasira za Mungu.

Mifano ya kibiblia inayoonyesha kuweko kwa Hasira ya Mungu.

Mungu anapokasirika hufanya matukio ya kutisha sana hasira za Mungu huja pale wanadamu wanaposimama kinyume na mpango wake na kutaka kuvuruga makusudi yake na kuishi maisha ya dhambi, Mungu aliiharibu miji ya Sodoma na Gomora kwa sababu ya maisha mabaya na machafu., Mungu alimuhurumia Lutu tu na familia yake kwa sababu ya Haki, lakini wengine wote na mji mzima aliusambaratisha Maandiko yanaonyesha katika sehemu kadhaa jinsi Mungu anavyochukizwa na dhambi

·       Mapema sana wanadamu walipokuwa wakiongezeka juu ya uso wa dunia na kuacha njia za Mungu Mungu aliweza kuifunua Hasira yake takatifu na kuwafutilia mbali wanadamu wote juu ya uso wa nchi Mwanzo 6:1-8 “.Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.  BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za binadamu, wakazaa nao wana; hao ndiyo waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. BWANA akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA.

·         Aidha Hasira takatifu ya Mungu ilifunuliwa pale wanadamu walipopingana na makusudi yake ya kutawanyika na kuijaza Dunia na hivyo Mungu alishuka na kuwachafulia usemi Mwanzo 11:1-9Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja. Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. Wakaambiana,Haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa.  Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote. BWANA akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. BWANA akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao. Basi BWANA akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji. Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo BWANA alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko BWANA akawatawanya waende usoni pa nchi yote.

·         Hasira ya Munguiliweza kudhihirika pale watu wa miji ya Sodoma na Gomora walipoanza kufuata uchafu na kushiriki ngono za jinsia moja, Mungu aliteketeza kila kitu katika mji wa Sodoma na Gomora , waona watoto wao na mali zao na kila walichokuwa wakikimiliki Mwanzo 18:17-21 BWANA akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake. BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua”. Kumbuka kuwa watu wa Sodoma hawakuwa na Biblia hawakuwa na manabii wala viongozi wa dini lakini hiyo haikuwa tiketi ya Mungu kuwaacha watu waishi bila uadilifu, Mungu anataka watu waishi kwa uadilifu ili kuepuka hasira zake.

·         Hasira za Mungu zinafunuliwa katika kitabu cha kutoka Pale Kora, Dathan na Abiramu waliposhindana na Mtumishi wa Mungu Musa katika Hesabu 16:1-21Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni; nao, pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa; nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, Bwana naye yu kati yao; n'nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa Bwana?  Musa aliposikia maneno haya, akapomoka kifudifudi; kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi Bwana ataonyesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake. Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote; vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za Bwana kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu Bwana atakayemchagua, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi.

Musa akamwambia Kora, Sikizeni basi, enyi Wana wa Lawi; Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mfanye utumishi wa maskani ya Bwana, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia; tena ya kuwa amekuleta uwe karibu, na ndugu zako wote wana wa Lawi pamoja nawe? Nanyi, je! Mwataka na ukuhani pia? Kwa sababu hii wewe na mkutano wako wote mmekusanyika kinyume cha Bwana; na Haruni, je! Yeye ni nani hata mkamnung'unikia? Kisha Musa akatuma kuwaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu; nao wakasema, Hatuji sisi; je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyojawa na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa? Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji. Musa akakasirika sana, akamwambia Bwana. Usiikubali sadaka yao; mimi sikutwaa hata punda mmoja kwao, wala sikumwumiza hata mtu mmoja miongoni mwao. Kisha Musa akamwambia Kora, Wewe na mkutano wako wote iweni hapa mbele ya Bwana kesho, wewe, na wao, na Haruni; mkatwae kila mtu chetezo chake, na kutia uvumba juu yake, mkavilete mbele za Bwana, vyetezo mia mbili na hamsini; wewe pia, na Haruni, kila mtu na awe na chetezo chake. Basi wakavitwaa kila mtu chetezo chake, wakatia na moto ndani yake, wakatia na uvumba juu ya moto, na kusimama pale mlangoni pa hema ya kukutania, pamoja na Musa na Haruni. Kisha Kora akakutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa Bwana ukatokea mbele ya mkutano wote. Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Jitengeni ninyi mkaondoke kati ya mkutano huu, ili nipate kuwaangamiza mara moja.”

·         Hasira za Mungu ziliweza kuainishwa tena kwa wana wa Israel waliposhindwa kumuamini kwamba wataingia katikia nchi ya mkanaani  Hesabu 14:1-9Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri. Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli. Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope.”

·         Wakati watu walipofanya dhambi ya manung’uniko kinyume na mpango wa Mungu Hasira za Mungu zliwaka na akaruhusu nyoka za moto kuwashughulikia Israel ingawa walikuwa watu wake Hesabu 21:4-6Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. Watu wakamnung'unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.

·         Katika agano jipya tunaweza kuona Jnsi mtu aliyeitwa anania na Safira walivyoweza kufanya dhambi na hatimaye walijikuta wakifutiliwa mbali wote mtu na mke wake kwa sababu ya kulidanganya kanisa Matendo 5:1-10Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya. Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika.     Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe.Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe.”

Sababu ya kuweko kwa hasira ya Mungu.

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu ni Mungu wa haki, na moja ya malipo anayoyafanya kwa wanadamu wanapokuwa wameasi au kwenda kinyume naye biblia imeweka wazi kuwa mshahara wa dhambi ni mauti  na zawadi ya utii ni uzima wa milele Warumi 6:23Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Maandiko yanatuthibitishia wazi kuwa tukifanya dhambi yako malipo yanayotukabili Hesabu 32:23Lakini kama hamtaki kufanya neno hilo, ninyi mmefanya dhambi mbele za Bwana, nanyi jueni ya kwamba hiyo dhambi yenu itawapata hapana budi.” Hakuna mtu anaweza kufanya dhambi kisha akakwepa Hasira za Mungu, Ni kweli kuwa Mungu ana uvumilivu mkubwa lakini maandiko bado yanatuonya kwa uwazi kwamba dhambi huamsha hasira za Mungu.

Hasira ya Mungu inafunuliwa namna gani.

Ni muhimu kufahamu kuwa Hasira za Mungu zinafunuliwa mara kadhaa kupitia nyuso au uso wa watumishi wake na maneno ya watumishi wake au matendo ya watumishi wake, mara kadhaa utaweza kuona kimaandiko jambo lilipokuwa baya aidha lilimuuzi Mungu na mtumishi wake pia Hesabu 16:28-35Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba Bwana amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe. Kama watu hawa wakifa kifo cha sikuzote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi Bwana hakunituma mimi. Lakini Bwana akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau Bwana Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka; nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote. Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wali hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni. Nao Israeli wote waliokuwa kando-kando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi. Kisha moto ukatoka kwa Bwana, ukawateketeza hao watu mia mbili hamsini waliofukiza uvumba.”

2Wafalme 1:1-17Ikawa, baada ya kufa kwake Ahabu, Moabu wakawaasi Israeli. Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu. Lakini malaika wa Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi sasa, Bwana asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka. Wale wajumbe wakarudi, na mfalme akawaambia, Mbona mmerudi? Wakamwambia, Mtu alitokea, akaonana nasi, akatuambia, Enendeni, rudini kwa mfalme yule aliyewatuma, mkamwambie, Bwana asema hivi Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi kwa ajili ya hayo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Akawaambia, Je! Mtu yule aliyetokea, akaonana nanyi, akawaambia maneno hayo, alikuwa mtu wa namna gani? Wakamwambia, Alikuwa amevaa vazi la manyoya, tena amejifunga shuka ya ngozi kiunoni mwake. Naye akasema, Ndiye yule Eliya Mtishbi. Ndipo mfalme akatuma akida wa askari hamsini pamoja na hamsini wake, wamwendee Eliya. Akamwendea, na tazama, ameketi juu ya kilima. Akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka.  Eliya akajibu, akamwambia yule akida wa hamsini, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto ukashuka, ukamteketeza, yeye na hamsini wake. Akatuma tena akida wa hamsini mwingine pamoja na hamsini wake, wamwendee. Akajibu, akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka upesi. Eliya akajibu, akamwambia, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza, yeye na hamsini wake. Tena akatuma akida wa hamsini wa tatu, pamoja na hamsini wake. Yule akida wa hamsini wa tatu akapanda, akaenda akapiga magoti mbele ya Eliya, akamsihi sana, akamwambia, Ee mtu wa Mungu, nakusihi, roho yangu, na roho za watumishi wako hawa hamsini, ziwe na thamani machoni pako. Tazama, moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawateketeza wale akida wa hamsini wawili wa kwanza pamoja na hamsini wao; laiti sasa roho yangu na iwe na thamani machoni pako. Malaika wa Bwana akamwambia Eliya, Shuka pamoja naye; usimwogope. Akaondoka, akashuka pamoja naye hata kwa mfalme. Akamwambia, Bwana asema hivi, Kwa kuwa umetuma wajumbe waulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, uulize neno lake? Kwa hiyo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Basi akafa, sawasawa na neno la Bwana alilolinena Eliya. Na Yoramu alianza kutawala mahali pake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda; kwa kuwa yeye hakuwa na mwana.”

Yohana 2:14-16 “Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng'ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng'ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao;  akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara”.  
             
Hatima ya Hasira ya Mungu.

Ni muhimu kufahamu kuwa hatima ya maswala yote haya ni kuwa Mungu ataifunua hasira yake kamili kwa wampingao katika jehanamu au ziwa la moto Zaburi 9:17Wadhalimu watarejea kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.” Kuzimu ni mbali na huruma ya Mungu maelezo ya kawaida kuhusu kuzimu maana yake ni mahali ambapo pamejaa moto na salfa na makaa na mawe ya moto ni shimo lenye giza huko nafsi za wote waliomkataa Mungu kwa matendo yao watahifadhiwa wakiwa katika hali ya kifo milele na milele pamoja na mashetani, Biblia inaelezea kuwa huko kutakuwa na kilio na kusaga meno ni wazi kuwa Mungu anayaandika majina ya watu wake wanaomuheshimu na kushika amri zake katika kitabu cha uzima na kama mtu hataoonekana siku ile ya hukumu atatupwa katika ziwa la Moto Ufunuo 20:15Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.”

Namna ya kujiokoa na hasira ya Mungu ijayo:

Biblia inaonyesha njia pekee ya kuikimbia hasira hii ni kuliitia jina la bwana ili tuokolewe Warumi 10:13kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.hatima ya kila mmoja wetu inategemeana na jinsi unavyoyatoa maisha yako kwa Yesu, kuliitia jina la Bwana maana yake ni kumuamini Yesu na kumuabudu na kuzishika njia zake na kufuata mafundisho yake na kuishi mbali na dhambi ambayo ndio husababisha hasira ya Mungu aidha dhambi mshahara wake ni Mauti Warumi 6:23, Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Njia pekee ya kujiokoa na na mauti hii ni sisi kumuamini Yesu Kristo na kumfanya kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yetu na kumuomba atuokoe na dhambi maana hii ndio kazi kubwa ya mwokozi Mathayo 1:21 “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao”

Tunaweza kuikwepa Hasira ya Bwana kwa toba na kumkimbilia Yeye, kumbuka kuwa Yeye ni mwaminifu kama tutajinyenyekeza kwake atatuangalia, katika Ghadhabu yake atakumbuka rehema, na kutusaidia, kama tukifanya dhambi kama watu wote tufanyavyo dhambi tusimkimbie Mungu bali tukimbilie kwa Mungu.

Ni muhimu kwetu tukajiokoa na kizazi hiki chenye ukaidi na uasi wa kila namna ili tuweze kuiepuka Hasira ya Mungu
Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa mbali na hasira ya Mungu katika Jina la Yesu.

Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.!

Jumatatu, 5 Februari 2018

Kama Mungu angekuwa Baba yako!



Yohana 8: 42Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma.”


Utangulizi

Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kujiuliza je Mungu ni baba yetu? Ni muhimu kufahamu kuwa sio kila mmoja wetu Mungu ni baba yake?, Yesu aliwahi kuwaambia ukweli mafarisayo na masadukayo pamoja na waalimu wa Torati waliodhani kuwa Mungu ni Baba yao kwamba wao sio wa Mungu, na aliwakemea kwa kuwaeleza wazi kuwa wao baba yao ni Ibilisi Yohana 8:44Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” Kama Mungu ni baba yetu tutampenda Yesu, tutamkubali Yesu, na tunaweza kuthibitisha kwamba sisi ni wa baba katika njia kuu saba zifuatazo:-

1.       Tutamwanimi yeye kama tunavyomwamini Mungu:-

Ni jambo la kusikitisha kwamba Yesu alitoka kwa Mungu, lakini hata hivyo wakuu wa dini, mafarisayo na masadukayo pamoja na waandishi yaani walimu wa torati hawakuwa wamemwamini, huwezi kusema kuwa unampenda mtu, lakini hata hivyo humuamini, kuamini kunaendana na kupenda Yesu anataka tumwamini yeye kwa kiwango kilekile cha kumuamini Mungu Yohana 14:1Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.”

Ishara kubwa ya kwamba tunamkubali Yesu na kwamba tunamwamini Mungu na tunampenda ni pamoja na kumuamini, na kama tunamwamini Yesu ni sawa na kuwa tumekubali zawadi kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu kupitia yeye na hivyo tutampenda.

2.       Tutazitii amri zake:-

Kiwango kikubwa na cha juu zaidi cha upendo wetu kwa Yesu ni pamoja na kutii amri zake, Yesu aliliweka wazi hili mapema tu ya kwamba kama Mungu ni baba yetu na amemtuma mwanaye wa pekee sio tu ili tumwamini lakini vilevile tumsikilize yeye ni ukweli ulio wazi kuwa Torati iliagiza kuwa Nabii huyu mkubwa aliyetumwa kwa mfano wa Musa anapaswa kusikilizwa maana yake tumtii Kumbukumbu la Torati 18:15,18-19Bwana, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye., Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.Hata itakuwa, mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake” Yesu alikuwa ndiye nabii yule ajaye aliyetabiriwa na Musa katika torati na katika manabii na swala hili lilieleweka wazi Yohana 1:45. “Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti” ni ukweli ulio wazi kuwa ilieleweka kwamba Yesu ndiye masihi lakini hata hivyo baadhi ya watu licha ya kuwa walikataa kumuamini lakini pia hawakuzishika amri zake, Yesu anaweka wazi kuwa kama tunampenda yeye basi tutazitii amri zake Yohana 14:15Mkinipenda, mtazishika amri zangu” Unaona kama Mungu ni baba yetu tutamwanini Yesu Kristo na tutazishika mari zake.Yesu hafurahii kuitwa Bwana na watu ambao hawako tayari kuyatenda asemayo Luka 6:46Na kwa nini mnaniita, Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo?” unaona Yesu kristo anahitaji kuaminiwa lakini vilevile kuyatii maagizo yake.

3.       Tutadumisha Ushirika wetu na Yesu!

Ni muhimu kufahamu kuwa uhusiano wetu na Mungu na bwana wetu Yesu Kristo ni uhusiano wa kudumu, awaye yote ambaye atamwamini Yesu au aliyeamua kumfuata Yesu hana budi kuhakikisha kuwa anashikamana na ushirika na Yesu bila kugeuka nyuma, Mungu anatarajia uhusiano wetu nay eye uwe wenye kudumu, na hafurahii kugeuka nyuma, kimsingi mtu anayemuacha Mungu biblia inamuita mtu mwenye moyo mbovu Waebrania 3:12-14 “Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.  Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho;” Kuanza safari ya kumuamini Yesu sio tatizo, watu wengi hulipokea neno kwa furaha na kumkubali Bwana yesu kwa msisimko, lakini hata hivyo kuendelea kukaa ndani yake ndio jambo la muhimu na zaidi ya umuhimu ni kustahimili mpaka mwisho na kuumaliza mwendo pamoja naye, Mathayo 24:13Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.”  Unaweza kuona kwamba mtu anamalizaje hilo ndio jambo la muhimu, Katika kutuongoza kuifuata imani Biblia inatutia moyo kuwaiga watu waliotuongoza na kuiiga imani yao Waebrania 13:7 “Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao.” Kumbe tunaweza kuiiga imani ya kiongozi wetu, wachungaji wetu, mashemasi wetu wazee wetu, maaskofu wetu na kadhalika lakini baada ya kuchunguza namna walivyohitimu katika imani, Mungu anataka tudumishe uhusiano nay eye hata mwisho.

4.       Tutazinena habari zake!

Hakuna namna yoyote ambayo kwayo tunaweza kusema kuwa tunampenda Mungu na Yesu Kristo kama hatuzisemi habari zake, Mitume walidhihirisha wazi kuwa wanampenda sio kwa kunyamaza kimya bali walizinena habari zake  kila siku na kila mahali Matendo 5:41-42Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo.  Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.Maandiko yanawasifia watu wanaonena habari za Yesu kuwa ni watu wema na kuisifia miguu yao kuwa ni mizuri, Yesu anataka tusambaze habari zake kwa watu wote ili waliitie jina lake na kuokolewa Warumi 10:14-15 “Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!Nyakati za kanisa la kwanza watu walimpenda sana Yesu na hivyo hawakuacha kuzungumza habari zake kila walikokwenda hata pale walipotawanyika kwa sababu ya dhiki bado walikuwa waaminifu kuelezea habari za Yesu Matendo 8:1-5 “Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume.  Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo.”  Kama Mungu ni baba yaetu tutampenda Yesu Kristo na kama tunampenda Yeu Kristo tutazungumza habari zake, Biblia inatutaka tuwe tayari wakati wote na siku zote 1Petro 3:15Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.” Wote waliompenda Yesu walikuwa tayari kuzishuhudia habari zake na hawakuona aibu.

5.       Tutakuwa tayari kuteseka kwaajili yake

Kile unachokipenda wakati mwingine unaweza kuwa tayari kukigharimikia, wazazi wanatoa nguvu zao na muda wao kujinyima kwaajli ya watoto wao kwa vile wanawapenda, wako watu ambao wako tayari kuyatoa maisha yao kwaajili ya wapendwa wao, katika hali kama hii wote wanaompenda Yesu wote ambao Mungu ni aba yao watakuwa tayari pia kuteseka kwaajili ya Yesu Kristo , Yeye alitupatia zawadi kuu ya wokovu kwa njia ya Mateso Waebrania 5:7-9 7. “Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii;unaweza kuona jinsi ambayo kiongozi mkuu wa wokovu wetu yaani Bwana Yesu alikamilishwa kwa njia ya Mateso, kila mmoja wetu ambaye ameitwa kumwandama Bwana ni lazima pia awe tayari kuteseka kwaajili yake kuwa ndani ya Yesu ni kukubali mateso ni kujiunga  na mateso yake 2Timotheo 1:7-12 “7. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele, na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili; ambayo kwa ajili ya hiyo naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu. Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile.” Unaweza kuona njia nyingine pekee yenye kuonyesha kuwa tunampenda Mungu na kwamba Mungu ni baba yetu ni kukubali kushiriki mateso kwaajili ya injili yake.

6.       Tutatamani kufanana naye.  
     
Lengo kubwa la neno la Mungu na mafundisho ya mitume ni sisi kuwa kama Yesu Kristo Wagalatia 4:19Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu;” Unaona Kristo kuumbika ndani yetu maana yake ni ile hali ya kukomaa na katika tabia na mwenendo na kufikia hatua ya kuwa kama Yesu Kristo mwenyewe, hili ndilo kusudi kuu kama tunampenda Yesu ni lazima tutafanana naye, mwelekeo na mkazo mkuu wa mitume na manabii ni kuhakikisha kuwa tunawafuata wao kama wanavyomfuata Kristo 1Wakoritho 11:1Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo.” Watoto wakati wote hujifunza kwa kuigiza tunaweza kuwaigiza wazazi wetu katika kila jambo liwe jema au baya, kwa sababu tunawapenda, sisi nasi kama tunampenda Bwana Yesu tutamuiga katika kila eneo la tabia na mwenendo wake, kuitwa wakristo kunatokana na mwenendo unaomfanania Yesu Kristo, Wakolosai 3:9-11Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake;           mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba. Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote.” Unaona tunapaswa kuvaa utu mpya sawasawa na mfano wa yeye aliyetuumba, wakati wote ni lazima tulenge kuwa kama Yesu na kufanana naye.

7.       Tutatamani kumpendeza Yeye.

Ni muhimu kufahamu kuwa watu wanaopendana hutamani sana kufurahishana, sisi nasi ni muhimu kuhakikisha kuwa tunatamani kumpendeza Bwana wetu Yesu, yeye alitupenda upeo nasi hatuna budi kumpenda 2Wakoritho 5:14-15 “Maana, upendo wa Kristo watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote; tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao.” Unaweza kuona haya ndio yalikuwa madai makubwa ya Bwana Yeye kuwa kila ambaye Mungu ni baba yake angampenda yeye maana yeye ametoka kwa Baba      Yohana 8: 42Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma.”

Hitimisho:
Ukweli ulio wazi ni kuwa kama mtu hampenzi Yesu nasikitika kumjulisha mtu huyo kuwa maandiko yanasema amelaaniwa 1Wakoritho 16:22 “Mtu awaye yote asiyempenda Bwana, na awe amelaaniwa. Maran atha.” Na kwa sababu hiyo hii kama humpendi Yesu Mungu sio baba yako na kama Mungu sio baba yako wewe ni wa ibilisi na unawezaje kuwa mwana wa Mungu ni kwa imani kupitia Yesu Kristo, Wagalatia 3:26 “Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.” Ni kupitia yeye pekee tunaweza kumfikia Mungu na ndio maana Yesu aliwataka viongozi wa dini kuelewa wazi kuwa hawana budi kumkubali yeye endapo wanadai wanamjua Mungu lakini kama wanamkataa Yeye hawawezi kwa njia yoyote kuwa wana wa Mungu.

“Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi”

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.