Jumatatu, 21 Januari 2019

Operesheni Lutu !

Adiko la Msingi: Mwanzo 14:14-16 “Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu.”


Utangulizi:

Nimetumia neno operesheni ambalo kwa kawaida ni neno linalotumika katika kampeni mbalimbali za kivita, mfano Tanzania,ilipokwenda kukomboa visiwa vya Anjuan wakati wa utawala wa Kikwete ile iliitwa Operasheni Demokrasi, Israel ilipokwenda kukomboa wayahudi kule Uganda wakati wa idd Amin kampeni ile iliitwa Operasheni Entebbe au wakati wa kurejesha Waethiopia wenye asili ya Kiyahudi ambao inasadikiwa kuwa walikuwa watoto wa Suleiman iliitwa operesheni SOLOMON sasa Abrahamu alipigana vita kumkomboa Lutu ndio maana nimeiita Operesheni Lutu sasa tuendelee na somo 

Ni muhimu kufahamu kwamba maandiko matakatifu yanatukumbusha katika Wagalatia 5:13b kwa mba tutumikiane kwa Upendo, “bali tumikianeni kwa upendo” moja ya maeneo yanayotufundisha kuhusu maisha ya Abraham ni pamoja na kifungu hiki muhimu tulichokipitia leo,kifungu hiki kinatukumbusha jinsi Abrahamu alivyokuwa mwenye kujali sana Maisha ya ndugu zake na jamaa zake. Lakini vilevile tunajifunza mambo mengine Makubwa sana kuhusu Mtu huyu wa Mungu ambayo yatatupa uweza mpana wa kufukiri kuhusu utendaji wa Mungu katika maisha yake.

Wengi wetu tunaposikia kuhusu Maisha ya Abrahamu mara kadhaa tunaweza kukumbuka matukio yake ya kidhaifu kama kusema uongo kwa kusudi la kulinda uhai wake kwa kumtaja Sara kama dada yake jambo lililohatarisha kupoteza ndoa yake, Lakini vilevile tunaweza kukumbuka ushujaa wake wa kukubali kuitikia wito wa Mungu na kukubali kuitii Sauti yake kwenda Katika nchi ya Kanaani, aidha tunaweza kukumbuka ushujaa wake wa kuthubutu kumtoa Isaka kama sadaka ya kuteketezwa mpaka malaika akamzuia, Pamoja na umuhimu wa Maswala hayo Leo ni muhimu tukajikumbusha kuwa Ibrahimu vilevile alikuwa mtu wa Vita, alikuwa mpiganaji Hodari mwenye mbinu kali sana za kivita, Abrahamu alikuwa mpiganaji.

Abrahamu si baba wa imani tu laikini ni baba wa vita!

Biblia inatufunulia siri hii kuhusu maisha ya Abrahamu kama mtu wa vita na jemadari kwa habari tunayoweza kuiona katika Mwanzo 14:1-4. Ni muhimu kufahamu kuwa sio tu kuwa Abraham alikuwa mpole tu lakini vilevile alikuwa ni Jemadari wa vita ni mpiganaji, Lakini alikuwa na Moyo wa kuwasaidia wengine, Mungu anapokuwa amekuita kuwa Baraka kwa wengine maana yake pia amekuita kuwapigania wengine Abrahamu anaonekana kuwa shujaa wa kipekee alipoingia katika vita ya kumuokoa Lutu Nduguye.

Mwanzo 14:1-4Ikawa siku za Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, na Kedorlaoma mfalme wa Elamu na Tidali mfalme wa Goimu, walifanya vita na Bera mfalme wa Sodoma na Birsha mfalme wa Gomora, na Shinabu mfalme wa Adma, na Shemeberi mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari. Hawa wote wakakutana panapo bonde la Sidimu, kwenye Bahari ya Chumvi. Miaka kumi na miwili walimtumikia Kedorlaoma, hata mwaka wa kumi na tatu wakaasi.”

Maandiko yanaonyesha kuwa kulikuwa na vita za kifalme wafalme Amrafel, Arioko, Elasari, Kedorlaoma na tidal yaani combine ya Majeshi ya wafalme watano(5) walioungana walikuja kupigana na Birsha, Shinabu, Shemeberi, na mfalme wa Bela jumla ya wafalme (4) sababu kuu ya wafalme hawa wanne walikuwa wamekataa kuendelea kulipa Kodi ya mfale Kedorlaoma wa Elamu aliyekuwa kinara wa utawala huo, hii ilikuwa vita kali katika nchi ya kanaani hususani kusini ya Israel liliko bonde la nchi ya chumvi lililojulikana kama bonde la Siddim, wafalme hao wanne walikuwa watumwa kwa miaka 12 lakini sasa wakaasi, hivyo Kedorlaoma alikuja kuwashambulia akiwa na wafalme kadhaa wanaomuunga mkono.

Mwanzo 14:5-7 “Na mwaka wa kumi na nne akaja Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja naye, wakawapiga Warefai katika Ashteroth-karnaimu, na Wazuzi katika Hamu, na Waemi katika Shawe-kiryathaimu, na Wahori katika mlima wao Seiri, mpaka Elparani iliyo karibu na jangwa. Kisha wakarudi wakaja mpaka Enmisfati, ndio Kadeshi, wakapiga nchi yote ya Waamaleki, na Waamori waliokaa Hasason-tamari. Mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, na mfalme wa Adma, na mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakatoka wakapanga vita panapo bonde la Sidimu; wapigane na Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, na Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, wafalme wanne juu ya wale watano. Na bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami. Nao wafalme wa Sodoma na Gomora wakakimbia, wakaanguka huko, nao waliosalia wakakimbia milimani. Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao.

Kinara wa vita hivi alikuwa ni mfalme KEDORLAOMA yeye aliongoza muungano wa majeshi ya kifalme kwa zaidi ya wafalme wanne na kabla ya kuanza na hawa watano walifagia miji mingina na kuwapiga vibaya wote waliokuwa kinyume nao na walipofika katika miji ya Sodoma na Gomora wafalme hao watano pia yaliwakuta magumu na wote walikimbia mbele ya ufalme huu wenye nguvu. Nani angeweza kuwatetea wafalme hao watano na wengine wote chini ya KEDORLAOMA? Hakuna mtu aliyeweza kusimama mbele yake.

Kosa kuu la KEDORLAOMA

Pamoja na ushindi mkubwa aliokuwa nao KEDORLAOMA alifanya kosa ambalo liliweza kumfanya ajutie utendaji wake kosa hili lilikuwa kumgusa Lutu Mwanzo 14:8-10, walichukua Mateka kila kitu lakini pia walimchukua Lutu na mali zake na watoto wake na watu wake wote aliokuwa nao, Lutu alikuwa amefiwa na baba yake na hivyo alilelewa na Abrahamu, Abrahamu hangeweza kumuacha Lutu, amekulia kwake tangu utoto wake kusumbuliwa kwake kulileta maumivu makubwa sana kwa Abrahamu naye alipopata habari aliona aweze kufanya jambo.

Mwanzo 14:11-12 Biblia inasema “Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao. Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko Sodoma, na mali yake, wakaenda zao.”

Abrahamu aliamuru Majeshi yake kwaajili ya Lutu.

Mwanzo 14:13-19 “Mtu mmoja aliyeponyoka akaenda, akampasha habari Abramu Mwebrania; naye amekaa panapo mialoni ya Mamre, yule Mwamori, ndugu ya Eshkoli, na ndugu ya Aneri, na hao walikuwa wamepatana na Abramu. Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu. Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi.

Mungu alimpa neema kubwa Abrahamu, alikuwa na vijana “318” ambao wao walikuwa wamejifunza vita Biblia inasema hawa wote walizaliwa katika nyumba yake hii ni wazi kuwa walilelewa na Ibrahimu, na ni wazi kuwa Ibrahimu alikuwa amewafunza kuhusu Mungu ushujaa wao ulikuwa umetokana na Mungu aliye juu Neema ya Mungu ilikuwa juu yao haiwezekani katika akili za kawaida Mtu mmoja aweze kupiga wafalme wanne waliokuwa na ushindi mkubwa wa ajabu, na wafalme wanne walikuwa wamekimbia Lakini Abrahamu na vijana wake 318 tu waliwapiga vibaya kundi kubwa la watu wenye uzoefu wa vita, siri kuu ya ushindi wa Abrahamu ilikuwa ni Muujiza wa Mungu, lakini vilevile alifanya sehemu yake alipigana na Mungu aliwaongezea hekima namna ya kupambana.

Abrahamu alifanikiwa kuwafuatia na kuwavamia maadui na aliweza kufanikiwa kuwapokonya malizote walizozipora kwa wafalme wanne na zaidi ya yote Abrahamu alikuwa anamtaka Lutu awe salama, aliwafukuza maadui kwa zaidi ya maili 50

Abrahamu alifanya mashambulizi makali wakati wa usiku, hakupigana mchana, laziki zaidi ya yote aliwagawa vijana wake makundi makundi na wakaanza kushambulia kutoka sehemu mbalimbali, maadui walichanganyikiwa wakidhani ya kuwa ulikuwa uvamizi mkubwa sana na hivyo walikimbia na kuachia kila kitu hivyo Abrahamu alimshinda KEDORLAOMA, Abrahamu alirejea nyumbani na ushindi. Alirudi na vijana wote waliwa salama na alirejea na mali zote na alifanikiwa kumuokoa Lutu.

Wafalme kadhaa wakaja kumlaki

Mmoja alifikiri ushindi wa Abrahamu unatokana na vijana wake “318” na akasema Mwanzo 14:21-22Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, Nipe mimi hao watu, na hizo mali uchukue wewe. Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, Nimeinua mkono wangu kwa BWANA, Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi

Lakini Mfalme mwingine aliyekuwa Kuhani wa Mungu aliya juu sana alijua siri ya ushindi wa Abrahamu

Mwanzo 14:17-20 “Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote

Siri kubwa ya ushindi wa maisha yetu hautokani na uwezo wetu na akili zetu, bali inatokana na uwezo na uhodari wetu katika Mungu, ni lazima tujifunze kupambana na kushinda vita zote za kiroho, na kujitegemeza katika uwepo wake na adui zetu watakimbia, Ibrahimu alikuwa ni mpole sana lakini linapokuja swala la kuchokozwa na kuguswa kwa maisha ya nduguze alihakikisha kuwa anapigana kwa hali na mali huku akimshirikisha Mungu.

Ni ukweli ulio wazi kuwa tunapokuwa na Moyo wa kuwajali wengine Mungu hutubariki na kutupa neema na Baraka tele, Abrahamu hakuweza kusema Lutu shauri yake si amejitenga nani mwenyewe lakini bado alitaka kuhakikisha usalama wa Lutu na jirani zake unakuwepo na hivyo alimtetea Lutu hii ndio operesheni Lutu.

mfalme wa Sodoma alitamani kumpa Ibrahu Mali zake ili achukue vijana 318, Ibrahimu hakukubali, wako watu wa mataifa ya kigeni wakati mwingine wanatulazimisha Afrika kufuata tabia zao mbaya kwa makusudi ya kutuingiza katika mtego wa kukosa uadilifu, tukatae misaada hiyo na tuendelee kumtegemea Mungu anatubariki na kutusaidia. 

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima. 

Rev. Innocent Kamote