Ijumaa, 29 Juni 2018

Vilivyotakaswa na Mungu Usiviite wewe najisi!


Andiko la Msingi: Matendo 10:15Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi.”


Ni muhimu kufahamu kwamba tunaishi katika nyakati za mwisho sana ambazo zina mawimbi mengi makubwa na ya kutisha ya uharibifu katika jamii, tunaweza kwa sehemu kuita nyakati hizi kuwa ni nyakati nzuri sana lakini kwa upande mwingine ni nyakati mbaya sana, kwa vile Dunia imeshuhudia mfumuko mkubwa sana wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, elimu ujuzi na uvumbuzi umepiga hatua kwa kiwango kikubwa sana, Hapo tunaweza kusema kuwa dunia imekuwa nzuri imeendelea,  lakini hata hivyo dunia imeshuhudia mmomonyoko mkubwa wa uadilifu na uvunjwaji mkubwa wa haki za kibinadamu katika mtazamo wa Mungu, moja ya matukio yenye kuhatarisha amani ya dunia na kukuza chuki miongoni mwa jamii ni pamoja na ubaguzi wa rangi na wa kimadaraja kwa aina binadamu, Makusudi makubwa ya somo hili ni kuwaita watu kurudi katika haki na upendo na kutokomeza maswala yote ya kibaguzi duniani.Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia maswala kadhaa yafuatayo:-

·         Wajibu wa Kutenda haki.
·         Mungu Hakuichagua Israel kwa sababu walikuwa bora kuliko wengine.
·         Vilivyotakaswa na Mungu usiviite wewe najisi.
·         Mashujaa waliosimama kupinga ubaguzi duniani.

Wajibu wa kutenda haki.

Neno la Mungu katika vifungu kadhaa vya Biblia limekazia juu ya wajibu wa kutenda haki, na kukataza maswala yoyote yenye uhusiano na kutokutenda haki, pamoja na kukataza upendeleo kwa sababu zozote zile Walawi 19:15Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki.” Mungu anapendezwa sana na watu watendao haki, lakini vilevile anachukizwa mno na watu wasiotenda haki Mika 6:8Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki na kupenda rehema na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako” Mtu anayetenda haki anabarikiwa katika maandiko Zaburi 106:3Heri wazishikao hukumu na kutenda haki siku zote” kinyume chake mtu asiyetenda haki amelaaniwa katika maandiko Kumbukumbu 27:19Na alaaniwe apotoaye hukumu ya mgeni, na yatima na mjane aliyefiliwa na mumewe. Na watu wote waseme Amina. Kulaaniwa maana yake mambo mabaya yampate mtu awaye yote asiyetenda haki unaweza kuona muda usingeliweza kutosha kuona maandiko yanavyokazia swala zima la kutenda haki na kuhukumu sawasawa bila sababu au upendeleo wa aina yoyote ule au kuchukua rushwa!

Mungu anataka watu wajifunze kutenda Mema kutenda haki na kwahurumia wanaoonewa Isaya 1:17 “jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.Kwa msingi huo Biblia inapozungumzia kutenda haki maana yake ni kuwa swala lolote la ubaguzi wa rangi au ubaguzi wa kijamii na kitamaduni unamaanisha kutokutenda haki, Katika Mstari wetu wa msingi Mungu alikuwa akimkemea na Kumuandaa Petro kwenda na kukubali kuwahudumia Mataifa ambao walikuwa wanahitaji injili na kwamba Mungu alikuwa amewakubali, Mungu alikuwa anashughulika na Petro ambaye ndani yake mila na tamaduni za kuwa Myahudi zilikuwa zimemfunga asiweze kuona Mpango kamili wa Mapenzi ya Mungu kuhusu Mataifa, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi alikemewa Petro.

Mungu Hakuichagua Israel kwa sababu walikuwa bora kuliko wengine.

Natambua wazi kabisa kuwa Israel ni taifa teule, ni watu ambao Mungu alijifunga kwao kwa kiapo na maagano aliyowaapia Baba zao Ibrahim, Isaka na Yakobo, naipenda Israel ni taifa ambalo limemleta Masihi kwetu Yesu mwana wa Mungu aliye hai, najivunia Israel naipenda Israel ni Mapenzi ya Mungu kuipenda Israel na kuiombea na kuomba kwaajili ya Yerusalem,  natambua mapenzi ya Mungu dhidi ya Israel, tumejifunza mengi kutoka kwao na uadilifu pia , Lakini maandiko yanakumbusha kuwa walichaguliwa kwa neema tu ni kwa neema ya Mungu ili aweze kupitisha mpango wake kwao Mungu anaonyesha kuwa hakuwachagua wao kwa sababu walikuwa bora zaidi ya mataifa mengine

Si kwa sababu ya wingi Kumbukumbu 7:7-9
Bwana hakuwapenda ninyi, wala hakuwachagua ninyi, kwa sababu mlikuwa wengi kuliko mataifa yote, maana mlikuwa wachache kuliko watu wote; bali kwa sababu Bwana anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia baba zenu, ndiyo sababu Bwana akawatoa kwa mkono wa nguvu, akawakomboa katika nyumba ya utumwa, katika mkono wa Farao, mfalme wa Misri. Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu;”

Si kwaajili ya Haki au usafi wao Kumbukumbu 9:4-6
Usiseme moyoni mwako, Bwana, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia Bwana niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya Bwana awafukuza nje mbele yako. Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya Bwana, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno Bwana alilowaapia baba zako Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Basi jua ya kuwa Bwana, Mungu wako, hakupi nchi hii nzuri uimiliki kwa ajili ya haki yako, kwa maana u taifa lenye shingo ngumu.”

Si kwa sababu wao walikuwa bora Warumi 3:9
“Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi;”

Sio kwaajili ya Matendo mema Tito 3:5
si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu;” 
     
Vilivyotakaswa na Mungu usiviite wewe najisi.

Matendo 10:1-29 “Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda. Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita wawili katika watumishi wake wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa katika wale waliomhudumia daima; na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa. Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana; akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule.  Lakini Petro akasema, Hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni. Hata Petro alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuiulizia nyumba ya Simoni, wakasimama mbele ya mlango, wakaita; wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro anakaa humo. Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta. Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma. Petro akawashukia wale watu, akanena, Mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani? Wakasema, Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, apate kusikiliza maneno kwako. Akawakaribisha wawe wageni wake. Hata siku ya pili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu waliokaa Yafa wakafuatana naye. Siku ya pili yake wakaingia Kaisaria. Na Kornelio alikuwa akiwangojea, hali amekusanya jamaa zake na rafiki zake. Petro alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguu, akamsujudia. Lakini Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu. Na katika kusema naye akaingia ndani, akaona watu wengi wamekusanyika. Akawaambia, Ninyi mnajua ya kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa taifa lingine wala kumwendea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu awaye yote mchafu wala najisi. Kwa sababu hiyo nalikuja nilipoitwa, nisikatae; basi nawauliza, ni neno gani mliloniitia?

Ukifuatilia mafundisho hayo hapo juu utaweza kuona kuwa Mungu alikuwa akishughulika na Petro, Petro alikuwa moja ya wanafunzi wakuu wa Yesu Kristo, alitembea na Yesu kwa muda mrefu alifundishwa mambo kadhaa kuhusu ufalme wa Mungu, Lakini sasa Mungu anamfundisha Petro kitu kingine cha ziada, Mungu anataka kuvunja mipaka ya mila na desturi na kidini na kikabila na rangi, Mungu anakataa kila aina ya ubaguzi, Petro hengekuwa radhi kuwahubiri watu wa mataifa mengine hata ama watu hao wanamkubali Mungu, Ni dhambi kuwabagua watu kwa sababu yoyote ile, Mungu hana upendeleo, Yesu aliwafundisha wayahudi kwenda zaidi ya mazoea yao aliwaambia kuwa Mungu baba huwapa jua lake na mvua yake wema na wabaya,

Ni wazi kuwa Mungu anakataa ubaguzi wa aina yoyote, Ulimwengu tulionao sio ulimwengu wa Mtu mmoja , Ni kweli kuwa Mungu amefanya mataifa ya aina mbali mbali na ni kweli kuwa Mungu ameumba watu kwa rangi mbalimbali, na ni kweli yako mataifa yameendelea sana kuliko mengine, wako watu wamefanikiwa sana kuliko wengine hata hivyo Mungu anataka watu wote wapewe huduma sawa na haki sawa, hakuna mtu asiyestahili injili, Petro alitakiwa kutoa injili kwa kila mtu na hivyo alipaswa aingilkiane na tamaduni nyingine na kuwafikishia habari njema 

Leo hii sehemu mbalimbali duniani zimekuwa na utamaduni huu wa kizamani sana wa kupiga marufuku watu wa jamii fulani wasiingie eneo fulani, au wasihubiri au wasijenge makanisa yako mataifa ya kidini na hayataki mtu wa dini nyingine aingie huko Makanisani kumekuweko na ubaguzi wa kikabila, watu wa kabila fulani, wana wabagua watu wa kabisa lingine, au wanadhani kuwa wao ndio wenye hati miliki ya Mungu, wengine wanabagua watu wengine kwa sababu sio wa Dini yao, dhehebu lao, kabila lao nchi yao n.k huu ni utamaduni uliopitwa na wakati Mungu yuko kinyume na “racism” Mungu yuko kinyume na madaraja, Mungu yuko kinyume na aina yoyote ile ya ubaguzi, Vilivyotakaswa na Mungu usibiite wewe Najisi.
 
Mifano ya Mashujaa waliosimama kupinga ubaguzi duniani.

Mohandas Karamchand GandhiMohandas Karamchand Gandhi (1869–1948)
Mwaka 2007 Umoja wa mataifa uliitangaza rasmi kuwa tarehe 2 kila mwezi wa kumi itakuwa ni siku ya Kimataifa ya Kutokufanya Fujo, hii ilitangazwa kwa kusudi la kuenzi na kukumbuka mwanzilishi wa maandamano ya amani ajulikanaye kama Mahatma Ghandi ambaye anajulikana kwa kuiletea India Uhuru, na aliyekuwa na ushawishi mku bwa wa kuwavuta watu kwenye maandamano ya amani, bila fujo duniani dhidi ya ukoloni wa Kiingereza bila chuki dhidi yao licha ya kuwa walifanya ukoloni nchini kwao

Rosa Parks (1913–2005)
Rosa Parks, with Dr. Martin Luther King Jr. in the background, around 1955.Rosa Louise Parks anafikiriwa kuwa Ndiye mama wa siku ya haki duniani huko Marekani, Yeye alijipatia umaarufu mkubwa kwa kukataa kupisha siti ya kwenye basi kwa mtu mweupe huko Alabama mwaka 1955, Jambo lililopelekea kukamatwa kwake, swala la mgomo wa kutokuachia siti au kuingia katika hoteli za watu weupe na kula kwa lazima lilianzia huko Montgomer na kuanza kuenea nchi nzima na katika majimbo ya kusini, Ujasiri wa Rosa ulimpatia umaarufu na kuanza kubadili mitazamo kuhusu watu weusi huko Marekani na kuanza kubadilisha mtazamo wa kihistoria, Rosa alikuwa mwanaharakati hata kabla ya kugoma kupisha siti ya basi kwa mzungu, Mwaka 1930 alimpigania kijana mmoja wa mweusi kati ya vijana weusi tisa walioshitakiwa kwa uongo kwamba walimbaka mwanamke mweupe ndani ya treni karibu na Scottboro, Alabama, Parks na mumewe Raymon Parks walifanya kazi katika shirika la umoja watu wasio weupe colored, Baadaye alihamia Detroit Michigan na kuwa shemasi katika kanisa la Methodist la watu weusi, alipewa Udaktari wa Heshima kwa degree 43 na mwaka 1996 Rais Clinton alimpa medali ya Uhuru Medal of Freedom.

Nelson Mandela (1918–2013)
Nelson MandelaMpinga ubaguzi na mwana mapinduzi aliyeyahamasisha mataifa kupinga vitendo vya kibaguzi, alifungwa kwa kusingiziwa kuwa alitaka kuipindua serikali ya kibaguzi na kuwekwa kizuizini, Mataifa mengi yalipiga kelele kwaajili yake, Baada ya kukaa Gerezani kwa miaka 27 aliachiliwa mnamo mwaka 1990, Miaka mitatu baadaye alipewa nishani ya  Amani ya Nobel Yeye pamoja na rais FW. De Klerk kwa kazi yao kubwa waliyoifanya huko Africa ya kusini ya kuutokomeza ubaguzi wa rangi na sera zake, Mwaka 1994 Mandela alitawazwa kuwa rais wa kwanza Mweusi mpaka mwaka 1999 alipoamua kung’atuka, kutokana na umaarufu wake alipewa Heshimamkama Baba wa taifa aliyeleta Democrasia ya kweli, wengine walimuita mpigania uhuru na wengine walimuita Mwokozi, wengine walisema Washingtona na Lincolin walioungana pamoja ndani yake.
Jimmy Carter (1924–)
 
Jimmy CarterRais wa 39 wa Marekani, aliacha Ofisi yake 1980, Mwaka 1982  yeye na mkewe Rosalynn alianzisha Carter Center  Huko Atlanta ambayo misingi yake ilikuwa ni kusimamia haki za binadamu hususani wanaaonewa na kuteseka, akilenga kutatua migogoro na kupata ufumbuzi, kukuza uhuru na demokrasia na kutunza afya za watu
Center yake ilianzisha mfuko wa usimamizi wa uchaguzi na kufanikiwa kusimamia chaguzi za mataifa mbalimbali katika chaguzi zaidi ya 94, alihusika katika uhamasishaji na ukuzaji wa demokrasia katika inchi za Ethiopia, Eritrea, Liberia, Sudan, Uganda,  Korean Peninsula, Haiti, Bosnia and Herzegovina, na Mashariki ya kati
Alijishughulisha na watu wenye kichaa, na kutia moyo viwango vya haki za binadamu katika jumuia za kimataifa, alipigia kelele dhidi ya uonevu wa mtu moja moja mwenye haki duniani na kwaajili ya haya mwaka 2002 kituo chake kilipewa Nishani ya Nobel kwaajili ya kazi yake muhimu ya kutatua migogoro ya kimataifa na kutunza haki za binadamu, kukuza uchumi na maendeleo ya jamii.

Martin Luther King Jr. (1929–1968)
Martin Luther King Jr. Mchungaji wa Marekani, aliyekuwa kiongozi wa Waamerika wenye asili ya Afrika wenye kupigania haki na usawa, Alijulikana sana kwa uwezo wake mkubwa wenye ushawishi na nguvu akipinga ubaguzi wa rangi Nchini Marekani, alijulikana sana kwa uwezo wake wa kushawishi na kuongoza maanadamano ya amani ya kupinga ubaguzi, Mwaka 1955 alikomesha ubaguzi wa rangi ndani ya mabasi, ilikuwa kama mkipanda basin a mwafrika amekaa akija Mzungu unampisha, Kwa kipindi cha miaka 11 tangu 1957-1968 Martin Luther King alitembea zaidi ya mile milioni sita, na kuzungumza katika hutuba mara 2500, alijitokeza kila eneo ambalo maswala ya haki na ubaguzi yalijitokeza na kupinga kivitendo, akiwa na umri wa miaka 35 Martin Luther King JR alikuwa kijana wa kwanza kupokea Nishani ya Nobel kutokana na umahiri wake, aliuawa na waliompinga kwa kupigwa risasi 1968.

14th Dalai Lama (1935)
14th Dalai LamaMtawa wa Kibudha na kiongozi wa Kiroho wa Tibet, anaitwa Tenzin Gyatso au Dalai Lama wa 14 yeye pia aliwahi kupata nishani ya Nobel mnamo mwaka 1989, kwaajili ya kuendeleza mapambano yasiyo ya uasi akitetea uhuru wa Tibet, Ameweza kusimamia amani na kupinga mambo bila kumwagika damu hata wakati wa maswala magumu au katikati ya hali ngumu amekuwa akijishughulisha huku na huku kuhamashisha amani na kutokana na umahiri wake amepewa Udaktari wa Heshima mara 150 akisifiwa kwa jumbe zake zenye kuhamasisha amani na usawa. Uelewa na uwezo wa kuchukuliana na watu wa dini nyingine na imani tofauti, huruma na uvumilivu, ameandika vitabu zaidi ya 110, na ana wafuasi zaidi ya milioni saba katika mtandao wa twiter duniani unaweza kuona @DalaiLama

Hitimisho

Kwa ujumla Mungu anataka walimwengu waishi kwa amani bila ubaguzi wa aina yoyote, Pale mtu anapojifikiri kwa namna yoyote kuwa Bora ukweli unabaki kuwa mtu huyo amejivuna tu, ana kiburi na Mungu yuko kinyume na mtu mwenye kiburi, Ili dunia iishi kwa amani ni lazima watu wache mambo ya kijinga, Kabila lako halina maana isipokuwa ya utambulisho tu kama lilivyo jina lako, dini yako haina maana isipokuwa kuonyesha mtazamo wako kuhusu Mungu au itikadi yako namna unavyomuona au husiana na Mungu, Utajiri wako hauna maana dhidi ya uwakili wa malia ambao Mungu amekuzawadia ili kukupima namna utakavyoishi na wengine, akili zako na cheo chako hakina maana dhidi ya dhamna a ambayo Mungu amekupa ili akupime utaitumiaje kwa upendo kuelekea wengine, rangi yako haina maana wala uzuri wako hauna maana kama utatumika kuwa alama ya kiburi na majivuno

Lazima watu wajifunze upenda na kutenda haki na kusimama katika kweli kwa gharama yoyote Paulo Mtume alipingwa sana kwa sababu eti alikuwa akihubiri injili kwa watu wanaodhaniwa kuwa hawafai 1Wakoritho 16:5-9 Lakini yeye aliwaona Mataifa kama mlango unaofaa mkubwa kwa injili. Mpango wa Mungu ni kuwa dunia yote ipate kumjua Mungu na kujawa na utukufu wake huku amani ikitawala ni kwaajili ya haya Yesu Kristo alikuja Isaya 11:1-9.

Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
0718990796