Jumatatu, 23 Januari 2023

Ni nani atakayetutenga na Upendo wa Kristo?

Warumi 8:35-39 “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.  Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu


Utangulizi:

Nyakati za kanisa la Kwanza na hata katika siku zetu za leo ni rahisi sana watu kufikiri kuwa wanapopitia mambo magumu au changamoto za aina mbalimbali hudhani kuwa labda Mungu huwa anaadhibu au anakomesha au amepunguza upendo wake kwetu, Lakini ni muhimu kufahamu kuwa hakuna kituchochote tunachokipitia ambacho kinaweza kumaanisha kuwa Upendo wa Mungu umepungua kwetu HAPANA, Paulo Mtume alikuwa anawaandikia Wakristo wa makanisa ya  Rumi na maeneo mengine ambao wakati huo walikuwa wakipitia majaribu ya namna mbalimbali na kuwataka wajifunze kuwa hakuna jambo baya linaloweza kumtokea mtu wa Mungu kisha likamaanisha kuwa  labda Mungu amemuacha ! Paulo aliandika waraka huu akitaka kuitambulisha injili anayoihubiri hasa kwa sababu alitaka kufika rumi mara kadhaa lakini shetani alimzuia, na katika kutaka kuwafikia aliandika waraka huu akiwafunulia maswala mbalimbali anayoyahubiri na pia alitaka kujibu maswali kadhaa ikiwa ni pamoja na hoja ya kuteseka kwa wakristo ili wakristo wasijenge dhana kuwa  au labda upendo wa Mungu umepungua na kuwa njia ya Mungu ni njia sahihi,  Kulikuwa na maswali kadhaa wa kadhaa kwamba mbona  sasa tumefuata njia iliyo njema lakini Serikali ya kirumi na mahakama zilizokuwepo zilikuwa na wakuu wa dini walikuwa kinyume na Imani hii, 

1.       Je kweli imani hii ni sahihi? Kweli Mungu yuko upande wetu?

2.       Kweli Mungu anasikia maombi na kukutana na mahitaji yetu

3.       Mbona watu wa Mungu wanashitakiwa?

4.       Mbona sasa watu wa Mungu wanahukumiwa?

5.       Na je njia sahihi ni kuachana na imani ?

Maswali hayo yalilitatiza sana kanisa la kwanza kwa sababu walikutana na upinzani mzito kwaajili ya injili na hivyo Mitume wliifanya kazi ya kujaribu kulijibu swali hilo kwa ufasaha  Matendo 4:1-3, 23-26

Matendo 4:1-3, “Hata walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo wakawatokea, wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu. Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni.” 

Matendo 4:23-26 “Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake.” 

Kwa kadiri imani katika Kristo ilivyozidi kuenea hali ilizidi kuwa ngumu sana, kwani wakristo walipigwa kwa mawe na kuuawa na kutiwa magerezani  na hivyo kuendelea kuleta maswali mengi sana miongoni mwa wanatheolojia wa wakati ule ya kwamba imani ni nzuri lakini mbona inaleta majaribu magumu na maswali yasiyoweza kujibika ?

Matendo 8:1-3 “Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani

Dhiki na mateso, usumbufu na taabu zilizokuwa zinalikumba Kanisa la kwanza zilipelekea Mitume kujenga hoja na kujibu hoja ili wakristo waweze kuelewa kuwa kinachowatokea kina maana pana sana katika Mungu:-

1.       Wasione ni ajabu 1Petro 4:12 “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.”

               

2.       Imani huwa inajaribiwa 1Petro 1:7 “Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho. Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;”

 

3.       Dhiki inatuumbia uwezo wa kuvumilia Yakobo 1:2-3 “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.”   

 

4.       Ufalme wa Mungu  sio bei rahisi Matendo 14: 21-22 “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.”

 

5.       Hakuna wa kututenga na Upendo wa Kristo Warumi 8:35-39 “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.  Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu” 

Kwa sababu hiyo ni Muhimu kufahamu kuwa kwa kadiri unavyojitoa kwa Mungu na kuendelea kuwasaidia wengine kukua katika imani na kwa kadiri siku zinavyokwenda utagundua kuwa njia ya Mungu sio nyepesi kama tunavyoweza kudhani lakini hatuna budi kuhakikisha kuwa tunafurahia wakati wote na wala hatupaswi kuhuzunika Pale Mungu wetu anaporuhusu Mambo yakawa tofauti na namna tunavyodhani, hivyo ni muhimu kuufahamu upendo wa Kristo katika kile eneo na kukumbuka kuwa wakati wote tunapopitia sintofahamu ya aina yoyote ile Mungu yuko Karibu mno kuliko tunavyodhani, usifikiri kuwa hayuko upande wetu, usifikirikuwa hatakutana na mahitaji yetu, Usifikiri kuwa kuna mwanadamu anaweza kutuhukumu, wala usifikiri kuwa Upendo wa Mungu umepungua kwetu upendo wa Mungu ni mpana sana  na wakati wote anaandaa Mambo mazuri zaidi kwaajili yetu. Hakuna lolote lenye nguvu ya kututenga na upendo wa Mungu. Wakati mwingine kwa kadiri unavyojitoa zaidi kwa Mungu ndivyo unavyokutana na changamoto zilizokubwa zaidi 2Wakorintho 11:21-33, CV ya ufalme wa Mungu inatengenezwa kwa kupitia mambo magumu na sio hizi changamoto ndogo ndogo.


Na Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima .