Jumatatu, 27 Julai 2020

“Na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala”


Mwanzo 3:16Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.



Utangulizi:


September 4-15 Mwaka 1995 Kulifanyika mkutano mkubwa wa nne wa dunia wa wanawake huko Beijing nchini China.  Mkutano huo ulipewa jina la kiingereza “Action for Equality: development and peace”, yaani kwa tafasiri ya Kiswahili changu naweza kusema “Haki sawa kwa maendeleo na amani” Kongamano hili la wanawake lilipewa jina hilo na umoja wa mataifa, Katika mkutano huu mkubwa, serikali za dunia zilikusanyika zikiwakilishwa na wanawake maarufu kutoka sehemu mbalimbali duniani zikiwa na wito wa kuitaka dunia kufikia malengo ya usawa yaliyokubaliwa na jukwaa hilo la wanawake lililofanyika Beijing likijulikana kama “The Beijing Platform for Action”, Kutoka Tanzania mwakilishi mmojawapo maarufu alikuwa mama Gertrude Mongella (Kushoto pichani hapo juu) ambaye wakati huo pia alikuwa ni spika wa bunge la Africa kwa upande wa wanawake, pamoja na maswala mengine  swala kubwa lilosisitizwa ni usawa katika uwakilishi lakini kubwa zaidi ni haki za wanawake duniani. Mkutano huo wa Beijing ulihitimishwa kwa kutoa tamko la Beijing yaani “Beijing Declaration.” Na lilikuwa ni tamko lenye maazimio yapatayo 38 na mengi yakiwa na mkazo kuhusu haki za wanawake.


Je unapata picha gani unaposoma habari za mikutano mikubwa kama hii na maazimio makubwa ya wanawake? Hasa yanayodai haki na haki hii ni usawa baina yao na wanaume, ni ukweli ulio wazi na usiopingika kuwa katika jamii mwanamke amebaki nyuma kwa kiwango kikubwa na sehemu kubwa sana uwezo wao haufanani na ule wa wanaume, tangu katika malezi na hata ukuaji kumekuwa na kipaumbele zaidi kwa watoto wa kiume penginepo kuliko watoto wa kike, maumbile na maswala mengine ya kijamii mila na tamaduni zimemuacha mwanamke nyuma kwa kiwango kikubwa na kwa sababu hiyo kuna uwezekano mkubwa kuwa labda umoja wa mataifa umeliona hilo na hivyo ukaandaa makongamano kadhaa yenye maazimio ya kumuinua mwanamke,  hatuna shaka kabisa kuwa uko ukweli ulio wazi kuwa mwanamke akiendelea jamii inaeweza kuendelea na kupiga hatua kwa kiwango kikubwa, Mwanafalsafa mmoja maarufu wa Afrika nchini Ghana James Aggrey alisema ulimuelimisha mwanamke umeielimisha jamii, kwa hiyo wanawake wakiendelezwa na kupewa fursa sina shaka kabisa watakuwa msaada mkubwa kwa jamii duniani.


Hata hivyo ni muhimu kufahamu na kujiuliza kuwa kwa nini wanawake wamejikuta katika changamoto hizi na swala kubwa zaidi kwanini wanapigania haki na usawa linapokuja swala la ulinganifu na wanaume? Fahamu ya kuwa wanawake wanajaribu au wanataka kujikomboa, wanataka kujikomboa kutoka katika kile ambacho maandiko yametamka kuwahusu, Liko tatizo ambalo wala sio la mfumo dume, wala sio la mila na desturi wala sio la kitamaduni ni tatizo la kiroho ni tatizo ambalo msingi wake na chanzo chake kilisababishwa na wanawake wenyewe, na hii ni kwa mujibu wa maandiko matakatifu, wakati mwingine wanawake wanapokuwa katika harakati zao huwa wanatamka kirahisi tu kuwa hata tamaduni mila na kidini ziliwakandamiza! Lakini leo nataka itambulike wazi kiini cha tatizo ili kwamba mwanamke aweze kuwa na ukombozi sahihi anapaswa kujua haki zake za msingi kama zilivyotamkwa na Maandiko matakatifu au na Mungu mwenyewe ili ajue mipaka yake ya haki na ukombozi anaoupigania wakielewa hayo watakuwa na amani ya kweli na watapata uhuru wa kweli.


Chanzo cha tatizo.


Neno la Mungu linaonyesha wazi kabisa kuwa mwanamke na mwanaume waliumbwa wote wakiwa na haki sawa, wote wakiwa wakamilifu na wote wakiwa wamepokea tamko la Baraka za Mungu katika kuutawala ulimwengu ona Mwanzo 1:26-31 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.” 


Unaona maandiko yako wazi kabisa kuwa Mungu amewapa wanadamu namaanisha wanawake na wanaume kwa pamoja thamani kubwa sana wote walitamkiwa baraka ya kuongezeka na kuijaza nchi na kuitiisha na kuitawala wote walipewa mtaji sawa utawala sawa na uhuru sawa kwa msingi huo mwanamke na mwanaume walikuwa ni watawala wenza wenye usawa unaofanana, lakini wote pia walikuwa na jukumu la kumuabudu Mungu na kumtii kwa usawa na kwa pamoja, Hata hivyo Mwanamke alipaswa sio kumsikiliza Mungu tu, lakini alipaswa kumsikiliza na Mumewe sawasawa na kumsikiliza Mungu, agizo la kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya kimsingi lilitolewa kwa Adamu pekee na huenda labda mwanamke alisikia agizo hilo baadaye kutoka kwa mwanaume angalia 


Mwanzo 2:15-17 “BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika”. 


Unaposoma maandiko haya ya uchanganuzi wa uumbaji utaweza kuona kuwa agizo hili lilitolewa kwa Adamu na kisha baadaye Eva aliumbwa kwa hiyo ni wazi katazo la ule mti wa ujuzi wa mema na mabaya Eva alilisikia kutoka kwa mumewe, lakini haki ya utawala iliwahusu wote, hii maana yake kwa kuwa mwanaume aliumbwa kwanza kisha mwanamke baadaye na kwa kuwa mwanaume alipaswa kumfundisha mwanamke amri  na maagizo ya Mungu, ni wazi na haki utakubaliana nami kuwa Mwanaume, alikuwa na majukumu yenye ngazi ya juu zaidi ya mwanamke kutokana na kuwa aliumbwa kwanza, Lakini vilevile alikuwa mwalimu na amri ile alipewa yeye hivyo alikuwa ni msimamizi wa kazi ya uumbaji na maelekezo aliyopewa na Muumba. Ni wazi basi kuwa swala la Kufundisha na kutawala lilikuwa jukumu kuu la Mwanaume na swala la kusikiliza lilikuwa la mwanamke yaani Mungu angetoa maelekezo kwa Adamu na Adamu angeleta ufafanuzi na maelekzo kwa mwanamke naye pamoja na jamii wangetekeleza kile Mungu alichokusudia kwa hivyo kwa itifaki, Mungu ni kichwa cha kila mwanaume na mwanaume ni kichwa cha mwanamke hapo ndipo itifaki ya uumbaji na upokelewaji wa maagizo ya Mungu ungepaswa kwenda kwa namna hiyo ona 

1Wakoritho 11:3 “Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha kila mwanamume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha Kristo ni Mungu.Unaweza kuona kwa msingi huo ili Baraka za Mungu ziweze kutiririka lazima itifaki ya kiungu izingatiwe, hili lisipoeleweka vema na wala kuzingatiwa mambo mabaya sana yatatokea na uwepo wa Mungu utaondoka, Mungu ni Mungu wa utaratibu wala sio Mungu wa machafuko!


Sasa basi jambo mojawapo kubwa na la kusikitisha ni kuwa mwanamke alikuwa ni kiumbe mwenye udadisi mkubwa na akili za kuhoji na kutafiti kile kilichosemwa na Mungu na mumewe Adamu na kutokana na udadisi wake mwanamke akawa mwanadamu au kiumbe wa kwanza kuharibu utaratibu huo uliokusudiwa na Mungu ona sasa Mwanzo 3:1-6 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.” Hiki ndio chanzo cha tatizo, Mwanamke amekuwa mwanadamu wa kwanza kusababisha dhambi na mauti kuingia ulimwenguni, ndio kiumbe wa kwanza kuharibu utaratibu, ndie kumbe wa kwanza kutokutaka kumsikiliza Mungu wala mumewe na alichagua kumsikiliza ibilisi na kusababisha kuharibika kwa utaratibu na mpango kamili wa Mungu katika maisha ya wanadamu, Paulo mtume akimuasa Timotheo katika waraka wake anamtaka Timotheo kukumbuka habari hizi na kuwaonya wanawake wawe katika utulivu, akimkumbusha kile kilichotokea bustanini na namna ya kuhakikisha kuwa utaratibu unafuatwa kanisani ona 1Timotheo 2:12-14Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu. Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.”


Ni muhimu kufahamu kuwa katika kifungu hiki Paulo mtume hakumaanisha kuwa wanawake hawawezi kusimama na kufundisha katika kanisa, Nyakati za kanisa la kwanza wanawake walifanya kazi ya kuhubiri injili na kufundisha neno la Mungu na mfano mzuri ni Prisilla na mumewe Akila wanaotajwa katika Matendo ya Mitume 18:24-26 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.”  Lakini vilevile tunasoma habari za Fibi aliyekuwa na huduma katika kanisa huko Kenrea ona  katika Warumi 16:1 “Namkabidhi kwenu Fibi, ndugu yetu, aliye mhudumu wa kanisa lililoko Kenkrea;” Huenda muhudumu huyu alikuwa mwanamke na alifundisha katika kanisa lakini kimsingi lugha inayotumika katika 1Timotheo 2:12-14  kwamba simpi mwanamke nafasi ya kufundisha sio inayotokana na neno la Kiyunani “DIDASKEIN” (Didasko) Ambalo maana yake ni kufundisha yaani kutoa maarifa  na ujuzi na kuupeleka kwa wengine, Neno linalotumika pale simpi mwanamke nafasi ya kufundisha ni neno la Kiyunani “AUTHENTEIN” (Authenteo) ambalo kwa kiingereza lingeweza kusomeka kama “exercise authority” au “Dominate” yaani to have control over a place or person yaani wanawake wasishikishe adabu wanaume au wasitiishe wanaume, wasiwaamuru kama wenye mamlaka hii ndio lugha halisi ya kibiblia hapa wasiwatawale wasiwe na amri juu yao.


Hivyo basi tunapata picha kuwa ni Eva aliyekuwa wakwanza kutamani na kujaribu kula matunda ya mti ule wa ujuzi wa mema na mabaya ambao Mungu alikuwa amekataza, na ni yeye aliyeweza kutumia ushawishi wake na mamlaka yake kuamuru na kumkosesha na Mumewe Adamu naye akala ni sawa na kusema wazi kuwa dhambi iliingia ulimwenguni kupitia amri ya mwanamke na matokeo yake na athari zake zikawa nyingi ikiwemo kuvurugika kwa mpango kamili wa Mungu kwa mwanaume na mwanamke kama watawala wenza. Kwa hiyo dhambi ya mwanamke ilikuwa ni kujiamulia, kula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya na kumuamuru mumewe naye ale. Na hivyo kuingiza mauti ulimwenguni. 


Na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala


Mungu ni Mtakatifu na ni lazima aihukumu dhambi, imefanyika kwa kusudi au kwa bahati mbaya lazima ataishughulikia tu, Mungu aliwahukumu wote na kuwaadhibu wote kutokana na kosa walilolifanya lakini kila mmoja kwa namna yake, Adamu alimlaumu Eva kwa kosa lake, na Eva alimlaumu nyoka kwa kosa lake na wote akiwemo nyoka waliadhibiwa na Mungu kutokana na makosa yao, sisi nasi kila mmoja ataadhibiwa mbele za Mungu kutokana na makosa yake, bila kujali ni mazingira gani yamepelekea tukafanya dhambi lakini ni lazima tukae na kukumbuka kuwa mshahara wa dhambi ni mauti na kila dhambi ni lazima iadhibiwe na kuhukumiwa na Mungu mwenyewe mwenye haki!


1.       Kwa Nyoka.


Kwa kuwa Nyoka ndiye aliyetumiwa na Ibilisi moja kwa moja Mungu alimlaani, ni jambo gumu sana Mungu kutoa laana kwa kiumbe chake chochote, Lakini shetani alikuwa ana ujuzi kuwa wao ni malaika na malaika kama viumbe vya kiroho hawafi, na hivyo alistahili laana, kwani kupitia ushawishi wake amesababisha mwanadamu kuwa na mauti katika mwili wake hivyo shetani kama mwanzilishi wa dhambi alilaaniwa, Aidha nyoka ambaye alikuwa kiumbe wa kawaida aliyetumiwa na Shetani kuzungmza na mwanamke yeye alilaaniwa kutembea kwa tumbo na kula mavumbi lakini pia kuwa adui wa mwanadamu, Nyoka alitumiwa na shetani kuwashawishi wazazi wetu wa kwanza kufanya dhambi, kwa kusudi na kwa nia ovu kabisa na hivyo alilaaniwa bila mjadala na kupokea adhabu yake, adhabu ya nje ilimuhusu nyoka halisi na adhabu ya ndani kiroho ilimuhusu shetani na majeshi yake. Ona

Mwanzo 3:14BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.


2.        Kwa Mwanamke.


Eva alikuwa ni kiumbe wa pili kutamkiwa adhabu japo wanadamu hawakulaaniwa, Eva alipokea kifurushi cha adhabu chenye mafungu matatu, Ikiwa ni pamoja na kuzaa kwa uchungu, Tamaa yake kuwa kwa mumewe, na mumewe kumtawala, huu haukuwa mpango wa Mungu katika mahusiano, lakini ni mpango uliotokana na kuharibika kwa mwanadamu kutokana na kuingia kwa dhambi ulimwenguni, wanawake wote waliowahi kuzaa wanaujua au wameuonja uchungu huo, na uchungu huu unaendelea katika uhalisia wa maisha ya wanadamu wote


Mwanzo 3:16. “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.


Hata hivyo swala la tamaa yako itakuwa kwa mumeo naye atakutawala ndio mahali panapochanganya watu kwa miaka mingi na wasiweze kuelewa maana ya msemo huu, ili kuweza kuelewa jambo hili hatuna budi kuliangalia kwa jicho linguine Biblia ya kiingereza ya The New Living Translation ndio imetafasiri kwa namna iliyonyooka zaidi kwani inasomeka hivi “you will desire to control your husband, but he will rule over you” yaani kwa Kiswahili chake tungeweza kusema namna hii “Utatamani kumtawala mwanaume lakini yeye atakutawala wewe” unaweza kuona kumbuka kuwa Mungu alikuwa anatamka adhabu kutokana na anguko la mwanadamu kwa kila mmoja kulingana na kukosea kwake, kwa hiyo mwanamke hapa kutokana na kuwa wa kwanza kwa hiyo kwa neno hili dhambi inaathiri uhusiano wa mwanamke na mwanaume katika ndoa na laana moja wapo au adhabu mojawapo ya kudumu ambayo haiondoki hata kwa wokovu, ni hii wanawake watatafuata wawe wanajua au hawajui watatafuta kuwatawala wanaume na sio kuwatawala tu hata kuwaondoa au kuwaua, au kuwaondoa kabisa wasiwepo hata kama wanaume watawapenda vipi wake zao, wao badala ya kufurahia upendo na muungano huu ambao Mungu aliukusudia, Mungu hapa anatangaza mgogoro utakaokuwepo kati ya mwanaume na mwanamke kutokana na madhara ya dhambi, lakini pia anahitimisha kwa kuonyesha matokeo ya mgogoro huo, hiki ndio wanawake watakuwa wanakitafuta siku zote za maisha yao hata kama watakuwa wameokoka jaribu kubwa la wanawake litakuwa hilo na matokeo ya mgogoro huu ni wao ndio watakaotawalika, Lugha inayotumika hapo na mumeo atakutawala katika lugha ya kiibrania linatumika neno “Mashal” linasomeka “Maw-shal Maana yake ni KUTAWALIWA, kwa msingi huo sasa katika utaratibu mpya wa haki na utawala Mwanamke anapaswa kujinyenyekeza chini ya utawala wa mumewe ili aweze kuwa sawa na aweze kuwa na furaha na amani japo jambo hili halitawafurahishwa kwa vile ni adhabu kutoka kwa Mungu unaona! Waefeso 5:22-25 “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;Kwa msingi huo ni muhimu kufahamu kuwa swala la wanawake kujitiisha chini ya mwanaume ni adhabu na hivyo haliwezi kuleta furaha kwao, wao ndio wa kwanza kuleta dhambi na mauti na kutumia uwezo wao wa kushawishi na mwanaume akatii, adhabu yake ilikuwa awe mtii kwa mumewe japo hawatakuwa na furaha kwa sababu watajiona kama wamekuwa duni lakini vilevile heshima yao inapatikana kwa kuolewa na kupendwa, siri kubwa ya mafanikio ya mwanamke na ili aweze kuishi kwa furaha ni kujinyenyekeza kwa Bwana zao yaani waume zao, mwanamke hata awe na fedha kiasi gani, hata awe na mafanikio kwa kiwango gani au awe na cheo kikubwa kiasi gani jambo pekee linaloweza kumjengea heshima ni kuwa na mume na kujinyenyekeza kwa mumewe, endapo mwanamke atakataa jambo hili heshima yake na furaha yake haiwezi kuwa kamili. Kama wanawake hawatagundua siri hii watajikuta wanafanya mikutano mikubwa mingi na kupitisha maazimio mengi sana lakini wanapaswa kukumbuka kuwa mwanaume kuwa juu  na kuwa na mamlaka dhidi yao ni mgogoro uliotangazwa na Mungu katika bustani ya Adeni na dawa yake ni kuukubali mgogoro huo na kukubali kutawalika kinyume cha hapo watakuwa wanamuasi Mungu.


3.       Kwa Wanaume.


Mwanzo 3:17-18 “Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.”


Kiumbe wa mwisho kutamkiwa adhabu alikuwa Mwanadamu na kwa Mara ya kwanza Biblia inamtaja kwa jina lake Adam yeye anahukumiwa kutokana na kosa la kumsikiliza mwanamke na kukubali ushawishi wake Ushauri wa Mungu ni bora zaidi kuliko wa mwanamke Mithali 15:22-26 “Pasipo mashauri makusudi hubatilika; Bali kwa wingi wa washauri huthibithika. Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake; Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini! Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu chini. Bwana ataing'oa nyumba ya mwenye kiburi; Bali atauthibitisha mpaka wa mjane. Mashauri mabaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maneno yapendezayo ni safi Kuzungumza ukweli kuwa ni huyu mwanamke uliyenipa alinishawishi nikala hakukuwa na msaada kwa Adamu alikuwa amesikiliza ujinga na hivyo alikuwa amefanya machukizo kwa Mungu, hukumu yake itakuwa katika kujipatia riziki zake za kila siku, yaani kazi za mikono yake zitampa shida Adamu, wakati mwanamke familia itamtesa mwanaume atapatatabu kazini, atakula mkate kwa shida kazi ambazo zingempa raha nafsini mwake zitampa taabusiku zote za maisha yake, adhabu ya Eva inahusisha taabu za kifamilia na kuwa mtumwa wa mwanaume lakini adhabu ya Adamu inahusisha kuwa mtumwa wa mazingira na kuishi kwa shida au kwa jasho yaani lazima afanye kazi


Hitimisho.


Adhabu zilizotajwa hapo juu haziondoki kwa wokovu wala kwa maombezi, njia ya kweli ya kufanikiwa ni kufanya kazi kwa bidii, kila mwanaume anapaswa kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili aweze kuwa mwenye furaha lazima ajaribu kwa kila njia kuyatawala mazingira, ambayo ingekuwa rahisi kuyatawala kwa neema ya Mungu kabla ya anguko lakini sasa atayatawala kwa jasho, wanawake nao hawawezi kuwa na uwezo wa kufikia kilele cha mafanikio bila kuwa wanyenyekevu, Ndoa na kuheshimu mumeo hata kama una kitu gani ndiko kutakakomfanya mwanamke awe na furaha ya kweli huu ndio mpango wa Mungu uliokamili, hivyo wanawake wanapotafuta haki zao na usawa miongoni mwa jamii wasome kwa bidii, wasaidie katika kufanya kazi na wafanikiwe katika kila Nyanja lakini wakumbuke Mungu amemuweka mwanaume juu yao, wanawake wanapookolewa hawana tofauti na wanaume wote wana haki sawa. Wanawake wote hawajaamuliwa kuwanyenyekea wanaume, lakini ilivyo ni kuwa kila mwanamke aliyeolewa anapaswa kumtii mumewe na sio kila mwanaume, kwa hiyo ili furaha yako itimie mtii mumeo swala hili linatakiwa lifanyike kwa hiyari ili liweze kuleta Baraka kwa nini kwa wanawake kuwatii waume zao kunafananishwa na kumtii Kristo hivyo mwanamke anaweza kuyatenda mapenzi ya Mungu akiwa chini ya mumewe, na kwa nini hili lifanyike kwa sababu Mungu amemuweka mwanaume katika nafasi ya utawala, kwa hiyo yanapokuwepo makongamano ya haki sawa wanawaka wanapaswa kupigania haki zao ili wainuke na kutatua changamoto zao lakini katika muktadha wa kukumbuka kuheshimu utaratibu ambao Mungu ameuweka ili amani ya kweli iwatawale na waweze kupendwa na waume zao.

Na. Rev. Innocent Kamote. 

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima