Jumapili, 13 Juni 2021

Hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena Milele !


Msatri wa Msingi: Kutoka 14:14-14Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.”




Utangulizi:


Siku moja Bwana Mungu aliviita viungo vyote katika mwili wa mwanadamu na akataka kuwauliza ili kujua wanafanyaje kazi? Kichwa kilielezea yote, Moyo, mikono miguu na kila kiuongo kwa jinsi yake, Lakini kiungo kimoja kilikuwa na malalamiko dhidi ya kiungo kingine, kiungo kilichokuwa na malalamiko kilikuwa ni *Ulimi* na mlalamikiwa alikuwa ni *Meno*, Kesi iliposikilizwa, ulimi ulisema kuwa mimi ni laini sana Mzee na umeniweka na Meno ambaye kwaasili yeye ni mgumu, tunapokuwa katika kazi ya kulainisha chakula mara kwa mara Meno huning’ata na kuniumiza na hivyo nachukua siku kadhaa kupona na kuendelea na kazi zangu, Mungu alimwambia ulimi usilalamike, ulaini wako haumaanishi kuwa wewe ni dhaifu kuliko meno, wewe ni mgumu sana, kuliko unavyojifikiri utaumizwa na utapona, na utaendelea kuwepo,  lakini sivyo ilivyo kwa meno ambaye anaonekana kuwa mgumulakini ukweli yeye ni dhaifu, baada ya miaka kadhaa utahesabia meno na utakubaliana nami kuwa mengine yataliwa na wadudu na hutayaona tena na yatang’olewa, lakini wewe ulimi utadumu hata mwisho wa dahari, ni kweli ulimi ulivumilia na kutoa muda kwa meno na wakati wa uzee, ni ulimi pekee aliyeonekana kudumu na kutokuchoka tena ukiwa na nguvu zake vilevile!


Lolote lile linalokusumbua katika maisha yako, na kukuumiza lipe muda tu, iko siku litang’oka, Wamisri waliwaonea wana wa Israel na kuwatumikisha kama watumwa kwa miaka mia nne na thelathini, Lakini siku moja wakati Israel wakiivuka bahari ya shamu, Musa alitabiri kuwa hawa wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele, unabii huu ulidumu kwa muda mfupi tu, kwani hata Musa aliusema akiwa kama kiongozi na mwenye kuwatia moyo watu wake kama mchungaji, lakini yeye mwenyewe alimlilia Mungu kwa hali aliyokuwa anaiona, Mkono wa Mungu ulikuwa mwema kwani aliwafutilia mbali Wamisri wale waliokuwa wakiwaandama wana wa Israel ili kuwaonea.


Leo nakutangazia kwa jina la Yesu, Magumu yote yanayokukabili na changamoto zote unazozipitia hautakuja uzione tena milele, Bwana atakupigania nawe hutanung’unika milele, Bwana atakustarehesha, Bwana atakupigania nawe utanyamaza kimya, kila changamoto unayokutana nayo katika maisha yako na inayoonekana kuwa ngumu au tishio kwako, hayo ni kama magego tu na wewe ni kama ulimi wewe ni imara zaidi kuliko wao na kuliko changamoto zako, Mungu anayejua kuwa uko katikati ya magumu atakutetea, Changamoto hizo kwa mamlaka niliyopewa kama mtumishi wake natangaza  leo ziwe mwisho na usizione tena katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai, Natangaza kuwa changamoto zinazokukabili hautaziona tena, sema amina

Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Alhamisi, 3 Juni 2021

Ni mizuri kama nini miguu yao, wahubirio habari ya mema!


Isaya 52:7 “Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki!



Utangulizi:

Ujumbe huu wa Nabii Isaya ulikuwa ni ujumbe wa maono ya siku ya ukombozi wa Yerusalem ambao vilevile huitwa sayuni, Ni ujumbe unaohusiana na Israel (Wayahudi) kuletewa ujumbe wa amani kutoka kwa mfalme Koreshi ya kwamba Mungu amemtuma awatangazie uhuru wayahudi waliokuwa utumwani huko Babel kwamba warejee kwao na kuujenga tena mji wao na Hekalu la Mungu wao baada ya kuwa utumwani kwa miaka mingi, Nabii anaona maono ya ukombozi anawaona wajumbe juu ya milima ya Yudea wakiiletea Yerusalem habari za kufunguliwa kwake! Ona


Isaya 40:9-11 “Wewe uuhubiriye Sayuni habari njema, Panda juu ya mlima mrefu; Wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema, Paza sauti kwa nguvu; Paza sauti yako, usiogope; Iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu. Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa, Na mkono wake ndio utakaomtawalia; Tazameni, thawabu yake i pamoja naye, Na ijara yake i mbele zake. Atalilisha kundi lake kama mchungaji, Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake; Na kuwachukua kifuani mwake, Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.

Nabii Isaya hakupata nafasi ya kuona kile kilichowapata wana wa Israel (Wayahudi) waliochukuliwa utumwani wakati wa Mfalme Nebukadreza, lakini aliweza kuona na kutabiri katika ulimwengu wa kiroho na kuwaona wayahudi wakipelekwa utumwani lakini vilevile wakirejea, Unabii wake huu hasa unatoa matumaini kwa Wayahudi ambao wangechukuliwa utumwani na kuwatia moyo ya Kwamba Mungu angewatokea tena na kuwarejeza.

Wayahudi walichukuliwa utumwani na Mfalme aliyeitwa Nabukadreza kimsingi mfalme huyu wa wakaldayo, alikuwa ni mwana wa Nabopolassar na alipata utawala mwaka wa 604 Kabla ya Kristo baada ya kuanguka kwa utawala wa waashuru, Jina lake kamili hasa linaandikwa na kutamkwa kama Nebuchadrezzar ambalo kwaasili ni “Nabu-Kudurri-usur” ambalo maana yake ni Nebo linda mipaka yangu (Nebo ni mungu wa wakaldayo) Mfalme huyu aliyekuwa katili sana na aliyekuwa dikteta mkubwa mno ametajwa zaidi ya mara tisini katika agano la kale.

Wayahudi wanamkumbuka Mfalme huyu kama moja ya wafalme katili sana ambaye wao wanamuhesabu kuwa aliwafanya wayahudi kama moja ya wanyama, alipopata utawala alikuwa na kampeni ya kupanua mipaka yake ya kuitawala Dunia mpaka Misri na kuhakikisha kuwa kila mfalme anamtii yeye na akawa mfalme wa wafalme, Wayahudi pia walitawaliwa na mfalme huyu, na Yehoyakimu mfalme wa wayahudi alitakiwa kujinyenyekesha chini yake na alipoasi jamaa alimuharibu ona

2Wafalme 24:1-3 “Katika siku zake akakwea Nebukadreza, mfalme wa Babeli na Yehoyakimu akawa mtumishi wake muda wa miaka mitatu;kisha, akageuka,akamwasi.Naye Bwana akatuma juu yake vikosi vya Wakaldayo, na vikosi vya Washami, na vikosi vya Wamoabi, na vikosi vya wana wa Amoni, akawatuma juu ya Yuda ili kuiharibu, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa mkono wa watumishi wake manabii. Hakika kwa amri ya Bwana mambo hayo yalimpata Yuda, ili waondoshwe kutoka machoni pake, kwa sababu ya dhambi zake Manase, kadiri ya yote aliyoyafanya;


Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Nebukadreza vilevile aliliharibu Hekalu la Yerusalem na kuchukua vyombo vitakatifu na kuvipeleka katika hekalu lake huko Babeli wakati wa mfalme Yehoyakimu

2Nyakati 36:5-7 “Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja; akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, Mungu wake. Juu yake akakwea Nebukadreza, Nebukadreza akachukua baadhi ya vyombo vya nyumba ya Bwana mpaka Babeli, akavitia katika hekalu lake huko Babeli.”
Aidha alimuua mfalme wa wayahudi na kuutupa mwili wake bila kuuzika sawa na alivyotabiri nabii Yeremia ona

Yeremia 22:18-19 “Basi, Bwana asema hivi, katika habari ya Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; Hawatamwombolezea, wakisema, Aa! Ndugu yangu; au, Aa! Dada yangu; wala hawatamlilia, wakisema, Aa! Bwana wangu; au, Aa! Utukufu wake. Atazikwa maziko ya punda, akibururwa, na kutupwa nje ya malango ya Yerusalemu.” Ona pia

Yeremia 36:30-32 “Basi, Bwana aseme hivi, katika habari za Yehoyakimu, mfalme wa Yuda; Hatakuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Daudi; na mzoga wake utatupwa nje wakati wa mchana upigwe kwa hari, na wakati wa usiku upigwe kwa baridi. Nami nitamwadhibu yeye, na wazao wake, na watumishi wake, kwa sababu ya uovu wao, nami nitaleta juu yao, na juu ya wenyeji wa Yerusalemu, na juu ya watu wa Yuda, mabaya yote niliyoyatamka juu yao, lakini hawakukubali kusikiliza. Ndipo Yeremia akatwaa gombo lingine, akampa Baruku, mwandishi, mwana wa Neria, naye akayaandika maneno yote yaliyotoka katika kinywa cha Yeremia, ya kitabu kile alichokiteketeza Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika moto; tena maneno mengi zaidi kama yale yakatiwa ndani yake.
Licha ya kumuua mfalme wa wayahudi na kumtupa bila kuzikwa, Nebukadreza pia alichukua utumwani kundi la wayahudi wapatao 4,600 ona

Yeremiah 52:27-30 “Naye mfalme wa Babeli akawapiga na kuwaua huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Ndivyo Yuda alivyochukuliwa utumwani, akatolewa katika nchi yake. Watu hawa ndio wale ambao Nebukadreza aliwachukua mateka; katika mwaka wa saba, Wayahudi elfu tatu na ishirini na watatu; katika mwaka wa kumi na nane wa Nebukadreza aliwachukua toka Yerusalemu watu mia nane na thelathini na wawili;katika mwaka wa ishirini na tatu wa Nebukadreza, Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua mateka katika Wayahudi watu mia saba na arobaini na watano; jumla ya watu hao wote ni watu elfu nne na mia sita.” 

Mfalme huyu ambaye hakuwa na huruma aliamuru mateka watembee moja kwa moja bila mapumziko mpaka Ukaldayo bila kupumzika hata hatua moja, akiamini kuwa wayahudi wakipewa nafasi tu watapata muda wa kusali na kuomba na kutubu kwa Mungu wao na wanaweza kupata rehema, hivyo ili wakose pumzi ya kupata kanafasi ka toba na kusababisha Mungu wao kubadili mawazo alihakikisha kuwa wanakula kibano sawia, alipofika ukaldayo alifanya sherehe kubwa sana ya kufurahia ushindi wake na kuwalazimisha wayahudi waimbe nyimbo za Sayuni kwa miungu yake huko


Zaburi 137:1-3 “Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.”


Vijana wazuri wenye nguvu na hekima walihasiwa ili wawe watumishi wa mfalme yaani walifanywa kuwa matowashi, akiwepo Daniel, Hanania, Mishael na Azaria, walikuja kujulikana baadaye kama Shedrack, Meshak na Abednego ona Daniel 1:1-4 “Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadreza mfalme wa Babeli,alikwenda Yerusalemu akauhusuru. Bwana akamtia Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu; naye akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu wake. Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana; vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.”                

Licha ya mateso haya ya kiutu na kisaikolojia Mateka wengi waliachwa na njaa, walipigwa na jua kali, walitembezwa wakiwa uchi mpaka wakawa weusi, njaa ilisumbua watu wazima mpaka vitoto vichanga, ilifikia  hatua hata wanawake waliokuwa na huruma walikula watoto wao kwa zamu Maombolezo 4:8-10 “Nyuso zao ni nyeusi kuliko makaa; Hawajulikani katika njia kuu; Ngozi yao yagandamana na mifupa yao Imekauka, imekuwa kama mti. Heri wale waliouawa kwa upanga Kuliko wao waliouawa kwa njaa; Maana hao husinyaa, wakichomwa Kwa kukosa matunda ya mashamba. Mikono ya wanawake wenye huruma Imewatokosa watoto wao wenyewe; Walikuwa ndio chakula chao Katika uharibifu wa binti ya watu wangu.” Kuna maswala mengi sana ya kikatili yaliyofanywa na Mfalme huyu mkubwa sana na dikteta wa hali ya juu aliyekuwa amejaa kiburi mpaka aliponyenyekeshwa na Mungu, ukweli ni kuwa hata wayahudi walipofika utumwani hawakuwa na maisha salama waliendelea kutumikishwa katika shughuli ngumu na kali na mateso. Aidha kiimani walilazimishwa kuabudu na kuitumikia miungu migeni ya Ukaldayo kwa ujumla waliishi Maisha ya wasiwasi na kutokuelewa kuwa kesho yao itakuwaje jambo hili liliwafanya waikumbuke Sayuni, wakumbuke Yerusalem wawe na tamaa ya kurudi kwao, Kwa hiyo nabii Isaya licha ya kuona mateso haya kinabii vilevile alitabiri kuwa anawaona malaika wa Bwana wanashuka juu ya milima ya uyahudi wakitangaza habari njema, ni habari ya kuwekwa huru, ni habari ya kuamuriwa kurudi Yerusalem, ni habari ya kurudi nyumbani, ni habari ya kwenda kuwa na ushirika na Mungu wao ni habari ya kwenda sehemu ambako unabii wa kuja kwa masihi ungetimizwa ni habari ya kurejeshewa kwa matumaini yao, ni habari ya kuelezewa ya kuwa mambo yatakuwa mazuri, Nabii isaya anasema ni Mizuri kama nini Miguu yao juu ya milima ya uyahudi waletao habari za amani, waenezao habari njema wasemao habari za wokovu waambiao watu Mungu ndiye anayetawala yaani ufalme wa Mungu u karibu  hii ilikuwa ni kauli ya furaha kwa watu waliokata tamaa, kila mmoja anaweza akawa yuko katika hali ya mateso na hali isiyofurahisha wala kuridhisha kila mmoja anahitaji ukombozi, anahitaji kusikia habari njema Baada ya kutimizwa kwa unabii huu wa Isaya Mungu alimuinua mfalme mkuu Koreshi wa uajemi ambaye alitoa habari njema kwa kuwaruhusu Wayahudi warejee Yerusalem ili kulijenga tena hekalu na vilevile kukomesha utumwa wa wana wa Israel na mateso yao ona Isaya 44:28 “nimwambiaye Koreshi, Mchungaji wangu, naye atayatenda mapenzi yangu; hata ataunena Yerusalemu, Utajengwa; na hilo hekalu, Msingi wako utawekwa.” Isaya 45:1-5 “Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi, masihi wake, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume, ili kutiisha mataifa mbele yake, nami nitalegeza viuno vya wafalme; ili kufungua milango mbele yake, hata malango hayatafungwa. Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli. Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua. Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu; nitakufunga mshipi ijapokuwa hukunijua;” Unabii Isaya wa isaya ulitimizwa miaka 180 baadaye Isaya alikuwa na maono ya ajabu sana mpaka ya kutaja jina la Mfalme huyo mabaye Mungu alimuita Mtumishi wake na mpakwa mafuta waka na Mchungaji wake, hii ni wazi kuwa mtumishi awaye yote wa Mungu atakayetenda mapenzi halisi ya Mungu ni yule mwenye miguu mizuri anayetangaza habari njema na za amani na za wokovu na za kuwaweka watu huru, katika namna nyembamba kiongozi huyo ni Koreshi bali katika namna pana Kiongozi huyo ni Yesu Kristo, lakini wale wanaoihubiri habari njema yaani injili pia wanaitwa ni wenye miguu mizuri kwa sababu wanafanya yale mapenzi ya Mungu kwa watu wake.

Paulo anaitumia kauli hii ya Nabii Isaya katika Warumi 10:15b “Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya memaWahubiri katika agano jipya wanapaswa kuwatangazia watu habari njema za matumaini ya Kwamba Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai ndiye aliyekuwa anatabiriwa kutuletea habari njema ya ukombozi ya kuwekwa huru sio tu kwa Israel bali na kwa mataifa mengine, watu wameteseka vya kutosha chini ya utawala wa mfalme asiyekuwa katika mikono ya Mungu, shetani ni mfalme wa wafalme aliye katili sana mwenye kuwatesa watu na kutokuwapoa pumzi ya uhuru wala nafasi ya toba, Lakini Yesu ni Mfalme wa wa falme mwenye rehema, Wahubiri katika agano jipya hawapaswi kuwatisha watu, wala kuwabebesha watu mizigo, bali wanapaswa kuwafungua watu kutoka katika vifungo vyao, watu wa Mungu wana mahitaji ya aina mbalimbali na wanahitaji ukombozi wa kweli wala sio vitisho na migandamizo kutoka kwa watu waovu wanajipa mamlaka kubwa na kusahau kuwa yuko Mungu wa mbinguni na kuwa Mungu huyo ndiye anayetawala, Mungu anachokitaka kwa watu wake ni kuwatangazia habari njema huu ndio mpango wake Israel wote walikuwa wakiusubiri mpango huu ona Isaya 58:6 “ Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?       

Mungu anapenda watu wake wasamehewe, walegezewe mizigo yao inayowaelemea, wajisikie huru kutika kila aina ya uonevu na kila aina ya magereza inayowatesa hata kama ina nguvu kiasi gani nira yake ivunjwe mtu anayefanya hayo ndiye mwenye kuleta habari njema ndiye ambaye miguu yake ni mizuri kama nini, ndiye anayetangaza habari za kweli za wokovu, ni ujumbe kama huu ndio tunayaita maneno ya neema na nitangazo la namna hii ndio Yesu Kristo alikuja kulitimiza na kulifanya Luka 4;16-22 16. “Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu? unaona Masihi Yesu Kristo mwenyewe alipoianza kazi ya kuhubiri injili yaani habari njema alitangaza kufunguliwa kwa watu na jamii ya watu wa kwao WALISTAAJABIA MANENO YA NEEMA YALIYOTOKA KINYWANI MWAKE. Huyu ndiye ambaye kila mtu alikuwa anamgoja anayetangaza habari ya mema, habari za amani habari za kuwaweka huru waliosetwa, habari za kuwafungua waliofungwa, habari za vipofu kuona habari ya kutangaza jubilii yaani mwaka wa bwana wa neema, Mtu wa namna hii ndiye ambaye tunasema ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari njema, kutana sasa na wale wasiotangaza habari njema miguu yao ni mibaya utasikia Leo tunamtangaza dada fulani au kaka fulani kuwa tumemkabidhi kwa shetani, leo natangaza kumtega fulani, leo namfukuza fulani kutoka katika kanisa letu, leo tunaanza mfungo wa siku miamoja, leo ni siku ya kumtolea Bwana Isaka wako, leo ameondoka katika kanisa hili habari zake ndio kwishinei, leo nalaani wanaopingana nami, dhehebu hili ndilo bora kuliko lile, muhubiri yule anahubiri mafundisho potofu na yasiyofaa, yule ndio mzinzi namba moja, huyu jamaa si aliwahi kufumaniwa, yule hanizidi mimi kwa maombi,  sisi ndio waanzilishi wa imani, sisi tunauzoefu, mimi sibabaishwi na hiki ama kile, mimi nimetembea sana nimezunguka nchi nyingi sana duniani, mimi utaniambia nini, mimi nina miaka mingi sana katika wokovu au nimekutangulia sana katikla huduma na kadhalika nisikilize, watu hawahitaji kujua umezunguka nchi ngapi, hawahitaji kujua umesoma kiasi gani watu wanahitaji kustaajabia maneno ya neema yanayotoka kinywani mwako, watu wanahitaji kutangaziwa msamaha wa dhambi,  wanahitaji wokovu, wanahitaji utawala na ufalme wa Mungu, wanahitaji kufundishwa na kuwekwa huru kutoka katika vifungo mbalimbali, wanahitaji kuelekezwa kwa masihi ili awaponye na kuwaweka huru, watu wanaotangaza habari za namna hii ni adimu sana kuwapata siku hizi, watu watamleta Isaka wao na hata Yakobo kama tu watahudumiwa vema na kutangaziwa utawala na malamaka ya kiungu hawa ndio Isaya anawatabiri kuwa ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari njema, wanaoleta habari njema wanaotangaza amani, wanaotangaza mambo mema, wanaotangaza wokovu na kuwaambia watu uko ufalme wa Mungu na kuwaelekeza watu kwa Yesu!

Ni Mizuri kama nini miguu yao, wahubirio habari ya mema!

Isaya 52:7 “Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki!

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!