Jumapili, 22 Septemba 2019

Yeye aliye na Funguo za mauti na Kuzimu!

Ufunuo 1:17-18Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,  na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.


Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu wazi kwamba tunaishi katika kizazi ambacho watu wanajaribu kujisahaulisha kuhusu kifo, watu wanajaribu kusahau kuwa kifo kipo, na kwa namna fulani wanadamu wanajaribu kila siku kubadili mtazamo wa kifo, kwa kuboresha Majeneza mazuri na kuyapamba kwa maua kiasi ambacho kifo kinaonekana kama ni monawapo ya sherehe ya kumuaga mtu, na sio hivyo tu hata makaburi yanapambwa kwa kujengewa vizuri kwa kiasi cha kugeuka kuwa bustani na maeneo ya kutembelea, hii yote ni kujaribu kukifanya kifo kionekane kuwa sio kibaya ! Laiki ukweli unabaki pale pale kuwa kifo ni adui mkubwa sana wa Mwanadamu  1Wakoritho 15:25-26 “Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti
Kifo ni tamko la Mungu ambalo limetamkwa kuwa kama mwandamu angemuasi Mungu basi kifo kigekuwa moja ya sababu ya uharibifu mkubwawa mwanadamu, kwa hiyo tangu mwanadamu anapozaliwa adui mkubwa anayefuata na kuanza kupambana naye ni mauti.
Yesu aliwajulisha wanafunzi wake mapema kuwa nao watakufa, tena watakufa kwaajili ya imani katika yeye Yohana 21:18-23 “Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka. Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo akamwambia, Nifuate. Petro akageuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata; (ndiye huyo aliyeegama kifuani pake wakati wa kula chakula cha jioni, akasema, Bwana, ni nani akusalitiye?) Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je? Yesu akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi. Basi neno hilo lilienea katikati ya ndugu ya kwamba mwanafunzi yule hafi. Walakini Yesu hakumwambia ya kwamba hafi; bali, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe?

Yesu alikuwa amewatabiria wanafunzi wake namna watakavyokufa kwaajili ya imani, na sasa anamwambia Petro namna atakavyokufa kwa utukufu wa Mungu, Petro alimuuliza Yesu je vipi kuhusu Yohana Yesu alimjibu ikiwa nataka huyu akae hata nijapo imekuopasaje wewe? Yaani vyovyote ni takavyo kwamba afe au akae mpaka mimi nijapo wewe inakuhusu nini wewe nifuate!      Petron aliuawa huko Roma kwa kusulubiwa kichwa chini miguu juu kama alivyotabiri masihi.

Hata hivyo historia ya Kanisa inatuambia kuwa Yohana pekee ndie mtume ambaye hakuuawa bali alikufa kifo cha kawaida, lakini vilevile kwa mujibu wa mwana historia maarufu wa kanisa katoliki aitwae Jerome Mtume Yohana alipitia shida dhiki na mateso makubwa sana kwani yeye aliishi karibu miaka 100, na hivyo alipitia vipindi vya mateso makali sana, wakati wa utawala wa Tatulian aliweza kusokotwa kwenye majani na akachomwa moto na alipoamka alijikungu’ta tu na nkuendelea na safari za injili, wakati wa utawala wa Domitian alidumbukizwa kwenye pipa la mafuta ya lami na kuchemshwa lakini alitoka akiwa hai, kutokana na kuwa na ugumu wa kifo alipelekwa uhamishoni kwenye kisiwa kiitwacho patmo iali ateseke na kufia huko, hata hivyo baada ya muda walikwenda kumchungulia na kukuta akiandika kitabu cha ufunuo na walimkata mkono, waliporejea mara ya pili walimkuta akiwa na mikono yake yote, Yohana aliishi maisha ya upweke lakini aliendelea kumuabudu Mungu, hata siku ya bwana  jumapili aliiadhimisha akiwa katika roho, akiwa amechoka kwa mateso haya Ndipo Yesu alimtokea na kumuagiza aandike kitabu hiki cha ufunuo, na jambo la kwanza Yesu alilolifanya ilikuwa ni kumtia moyo, Yesu alitaka kumtia moyo Yohana na kila mmoja wetu kuwa “Yeye anazo funguo za mauti na kuzimu

Yeye aliye na Funguo za mauti na kuzimu.
Kuwa na funguo za mauti na za kuzimu maana yake ni kuwa na mamlaka, au uwezo au mamlaka ya mwiho ya kuamua kuhusu kifo, Yesu ana uwezo juu ya kifo, anauwezo wa kuamua ufe au usife, kama uwezo huu angelipewa adui yetu angetufutilia mbali mara moja, Lakini ni Yesu ndiye anayeamua ni yesu ndiye anyeruhusu yeye ndio mwenye mamlaka mwenye udhibiti Hata maisha yake aliamua yeye mwenyewe kuyatoa na hakuna mtu aliyaondoa maisha yake ilikuwa ni kwa hiyari yake mwenyewe

Yohana 10:17-18 “Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena.  Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.”

Yesu ana nguvu dhidi ya Mauti ana mamlaka nayo na ni yeye anayeamua kuwa wale wanaomuamini watakufa lini, yaani lini awachukue wakaungane naye na wakifa awapeleke wapi? Na ni yeye mwenye mamlaka ya kufufua  ni kama Yesu alikuwa anamwambia Yohana kuwa usiogope Mimi nalikufa na sasa ni hai yaani huoni mfano wangu? Mauti haina uwezo ndani yangu, kama jinsi ambavyo haikuwa na uwezo juu yako,

Nisikilize watu wanaweza kujaribu kukuua kwa maneno na matendo, wanaweza kusema ngoja tuone familia yake itakuwaje, ngoja tuone mwisho wake utakuaje? Wanaweza kusema hapa amepatikana hapa tumemuweza, huu ndio mwisho wake, hapa tumemkomesha, hapa hachomoki, hapa tumemaliza, safari hii tumemuweza, hapa ndio mwisho wa kila kitu, tutaona watasomaje, tutaona atakwepaje mtego huu, huduma yake itakufa, amekufa kiroho, ameishiwa hana jipya, duka lake linakufa, biashara yake haiwezi kusimama, hawezi kuzaa tena, jamaa kwishinei, zilikuwa kelele za bure tuna lolote wanaweza kusema lakini Neno la Mungu linatuambia ye kuwa yukomwenye funguo, hatupaswi kuogopa kelele za wasio na funguo, namuogopa mmoja tu mwenye funguo, mwenye mamlaka ambaye yeye akifunga hakuna afunguaye na akifungua hakuna afunguaye

Ufunuo 3:7 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye.



Nataka nikutie moyo leo kuwa usiogope yeye ndiye mwenye kufungua mlango na ndiye mwenye kufunga hakuna anyeweza kushindana naye kama ipo ipo tu, ana nguvu ya kuizuia mauti.
Alizuia mauti kwa shadrak, Meshak na Abednego wakatembea kati kati ya moto, aidha alizuia makanwa ya simba kwa Daniel aliyetupwa katika matundu ya simba Mungu akaifunga mauti, kumbuka wale simba walikuwa na njaa , huyu ndiye aliyemsaidia Yohana akaangwe kwenye pipa la lami na mauti isimuweze, yeye ndiye aliyakufa akafufuka changamka huna sababu ya kuogopa adui huyu ni mdogo tu.

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumatatu, 16 Septemba 2019

Usimwache Mchawi kuishi!


Mstari wa Msingi: Kutoka 22:18 “Usimwache mwanamke mchawi kuishi.”

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya amri kuu katika maandiko inasema “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yoteLuka 10:27, Amri hii inaonyesha wazi kuwa Mungu anataka aabudiwe yeye peke yake na kwamba kuabudu miungu mingine ni moja ya machukizo makubwa sana kwa Mungu; Kutoka 20:3-6Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,  nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.”

Swala la watu kutafuta miungu mingine nje ya Mungu mwenyezi ni swala la siku nyingi na la zamani sana na shetani amefanikiwa sana kuwafanya watu waabudu miungu mingine kupitia waganga na wachawi badala ya Mungu, shetani anatumia Waganga, wachawi, wanajimu na kadhalika ili kuwafanya watu wasimuabudu Mungu na badala yake wamuabudu yeye au washirikiane na mashetani. Maandiko yanakataza kwa mkazo mkubwa mno swala la kushirikiana na Mashetani yaani ushirikina na uganga na uchawi. 1 Wakoritho 10:20-21Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.”  Paulo mtume alikataza kabisa kwa herufi kuwa Kanisa kuwa na ushirika na Mashetani, Unaposikia mtu anaitwa mshirikina maana yake ni mtu mwenye ushirika na mashetani aidha kupitia wachawi au waganga wa kienyeji, swala hili ni katazo la kibiblia katika agano la kale Mungu aliwakataza kabisa wana wa Israel kujihusisha na maswala haya kabisa na mara kadhaa agizo la kuupinga uchawi na ushirikina liliambatana na kifo!

Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
1.       Msimamo wa agano la kale kuhusu wachwi
2.       Msimamo wa Agano jipya kuhusu Wachwi
3.       Wito na ushauri wa kimungu kwa wachawi na washirikina

Msimamo wa agano la kale kuhusu wachawi.

·         Walawi 19:31Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu

·         Walawi 20:6Na mtu yule atakayewaendea wenye pepo, na wachawi, ili kuzini pamoja nao, nitakaza uso wangu juu ya mtu yule, nitamtenga na watu wake”.

·         Walawi 20:27  Tena mtu mume au mtu mke aliye na pepo, au aliye mchawi, hakika atauawa; watawapiga kwa mawe; damu yao itakuwa juu yao.”

·         Kumbukumbu 18:10-14Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako. Uwe mkamilifu kwa Bwana, Mungu wako. Maana mataifa haya utakaowamiliki huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na kutazama bao; bali wewe, Bwana, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo.

·         1Nyakati 10:13 tunaelezwa wazi kuwa sababu za kifo cha mfalme wa kwanza wa Israel ilikuwa ni kwa sababu alikwenda kuuliza kwa wachwi “Basi Sauli alikufa kwa sababu ya kosa lake alilomkosa Bwana, kwa sababu ya neno la Bwana, asilolishika; na tena kwa kutaka shauri kwa mwenye pepo wa utambuzi, aulize kwake, asiulize kwa Bwana; kwa hiyo akamwua, na ufalme akamgeuzia Daudi, mwana wa Yese.”

·         Hasira ya Bwana Mungu huwaka kwa mtu anayejishughulisha na maswala ya ushirikina 2Nyakati 33:6 “Tena akawapitisha wanawe motoni katika bonde la mwana wa Hinomu; akatazama bao, akabashiri, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa Bwana, hata kumkasirisha.”

Msimamo wa agano jipya kuhusu wachawi.

·         Katika matendo ya mwili yanayotajwa katika agano jipya ya watu ambao hawataurithi ufalme wa Mungu na wachawi nao wamo Wagalatia 5:19-21 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.”

·         Agano jipya pia linaeleza wazi kuwa wachawi sehemu yao itakuwa ni katika lile ziwa la Moto Ufunuo 21:8 “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.

·         Hakuna lugha ya upole kwa wachawi Biblia inaonyesha wazi kuwa mitume hawajawi kuzungumza na wachawi kwa lugha ya kubembeleza wakati wote wachawi walikemewa na kuitwa katika toba ili waamini vinginevyoa adhabu kali ilikuwa ikiambatana nao ona kwa mfano Matendo 8:9-22 “Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu. Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake.Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka. Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema,Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali. Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wakoMungu ni mwingi wa Rehema na upendo lakini nataka nikueleze wazi kuwa hana huruma na wachawi hata kidogo, kila mtumishi wa Mungu mwenye mamlaka ya kimungu ameruhusiwa kuwafanya lolote wachawi kusema nao kwa ukali na kuwaamuru kuavcha hila zao mbaya maan wao ni wana wa ibilisi Matendo ya Mitume 13:8-11 “.Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.” Wachawi huzipotosha njia za Bwana zilizonyooka Paulo anamuadhibu vikali Mchawi kwa sababu anajua kuwa Mungu yuko kiyuma nao na kuwa wachwi wakati wote hupinga na shauri la Mungu, wako kinyume na Mapenzi ya Mungu, Mungu alipokuwa anataka kuwaokoa wana wa Israel kutoka Misri wachawi waliweza kuigiza miujiza ya Mungu vilevile na walichangia kwa kiasi nkikubwa ugumu wa mowyo wa farao kwa sababu farao aliona hakuna jipa angalia Kutoka 7:22 “Lakini waganga wa Misri wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na moyo wake Farao ukawa mgumu, wala hakuwasikiza, kama BWANA alivyonena”. Unaona Biblia ya habari njema BHN inasomeka vizuri katika Kutoka 7:22 inasemaLakini wachwi wa Misri kwa kutumia uchawi waowakafanyoa vivyo hivyo,Kwa hiyo moyo wa farao ukabaki kuwa mgumu naye hakuwasikiliza Mose na Aroni kama mwenyezi Mungu alivyokua amesemaWachawi hawa ni wapinzani wa mipango ya Mungu, na wakati mwingine kwa mtu mwenye moyo kama wa Farao ni vigumu kupambanua na kujua katika ya mtu wa Mungu na Mchawi, farao alifikiri Musa yuko sawa na wachawi wake tu Mpaka pale Mungu alipodhihirisha uwezo wake ndipo wachawi wa farao wakamueleza wazi kuwa hiki ni chanda cha Mungu    Kutoka 8:19 “Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni chanda cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.”  Hakuna popote katika Biblia mchawi au mganga ameonyeshwa kuwa ni mtumishi wa Mungu hakuna. Wote wanahukumiwa na Mungu kwa ukali na dhabu kuwa ni kifo au watubu na kumgeukia Mungu, Kazi kubwa ya wachawi ni kupinga na Mungu na makusudi yake, popote pale mtu wa Mungu unapofanya jambo na kuona kuwa kuna ushindani, kuna upinzani kuna ugumu usiokuwa wa kawaida, hakuna mtiririko unaokusudiwa funguka na kukemea nguvu za upinzani shetani ujue yupo au watumishi wake na wanafanya yao hivyo butua shughulika na Yane na Yambre ambao ndio hufanya hayo wanayoyafanya  yaani wanapingana na imani 2Timotheo 3:8Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani.

Wito na ushauri wa kimungu kwa  wachawi na washirikina
Biblia ina wito mmoja tu kwa wachawi, watubu ili yamkini Mungu awasamehe fikira yao mbaya, waache kuzipotoa njia za Bwana zilizonyooka na watubu na kugeuka na kuchomelea mbali vitabu vyao na mikoba yao na vifaa vyao vya uchawi Matendo ya Mitume 19:19 “Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.” Biblia inaonyesha kuwa wachawi kule Efeso walitubu na kuziharibu kabisa kazi mabaya za gharama kubwa hawakuwa na aibu waliviharibu na kuviteketeza vyote bila kujalia gharama vifaa vyote vya uchawi walivichoma moto wito wa kibiblia ni kila mtu mbaya aache njia yake mbaya na amgeukie Mungu naye Mungu atamsamehe Isaya 55:6-7Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.”
Biblia inaonya kwa ukali sana kuhusu kujihusisha na ushirikina ukweli ni kuwa hakuna neno la Huruma kwa wachawi awe mwanaume au awe mwanamke adhabu ya wachawi ni kifo tu, Katika agano jipya trehema tunayoweza kuiona ni wao kuacha uchawi na kumuamini Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yao, Neno la Mungu linaposema usimuache mwanamke mchawi kuishi, liko wazi kuwa hukumu ya wachawi ni kifo tu, kama unajihusiha na ushirikiana nakuonya kwa jina la Mwenyeji Mungu acha mara moja Mgeukie Yesu, mwambie akusamehe na kama unajihusisha na uganga acha acha mara moja na ili uweze kuwa salama Mgeukie Mungu acha kuwadanganya watu, acha kutumia pepo wa utambuzi, achana na mapepo ya uuguzi, acha kutumiwa na maimuna, subian, makata na vinyamkera na aina yoyote ya majini na mapepo yanayokutokea ua kukuotesha ndoto acha nakuonya, na kama unakwenda kwa waganga tubu na usirudie tena. Vinginevyo kifo cha kimwili na kiroho kinakuhusu.

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Mungu na wakimbizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa kuwahudumia wakimbizi ni mpango wa Mungu!, Leo tutachukua Muda wa kutosha kwa kina na upana na urefu kuangalia huduma muhimu kwaajili ya wakimbizi Duniani, Mwaka 2004 pekee karibia watu milioni tatu na nusu walikuwa ni wakimbizi barani Afrika pekee, ambao walikimbia na kuishi nje ya nchi zao, na wengine zaidi ya milioni kumi walikuwa ni wakimbizi ndani ya nchi zao, wengi walikuwa hawakimbii tumatukio ya majanga ya kiasili nlakini walikuwa wanakimbia matatizo ya kisiasa, ugomvi wa kimadaraka, matatizo ya kidini, ukabila na maswala mengineyo je neno la Mungu linasema nini kuhusu wakimbizi, kanisa limewahi kutafakari nini kuhusu wakimbizi? Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Neno la Mungu na wakimbizi
·         Mungu anawajali wakimbizi
·         Wakimbizi na mafundisho ya agano jipya

Neno la Mungu na wakimbizi:

Biblia inatambua kuweko kwa watu ambao wamewahi kukimbia huko na huko mbali na Nchi zao, kaini alikuwa mtu wa kwanza kufahamu madhara ya ukimbizi Mwanzo 4:12,”Utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake, utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao Duniani” Neno utakuwa mtoro ni sawa na utakuwa mkimbizi. Yakobo na Familia yake waliishimaisha ya ukimbizi kutokana na majanga ya njaa nchini kwao Mwanzo 47:3-4, “Farao akawauliza hao nduguze Kazi yenu ni nini? Wakamwambia Farao, Tumekuja kukaa ugenini katika nchi hii, kwa sababu wanyama wa watumwa wako hawana malisho, maana njaa ni nzito sana katika nchi ya kanaani, Basi twakusihi uturuhusu sisi watumwa wako tukae katika nchi ya gosheni” Yesu pia alikuwa mkimbizi huko Misri kwaajili ya kuokoa Maisha yake yaliyokuwa yakitafuta na mfalme Herode Mathayo 2:13-14. “Na hao walipokwisha kwenda zao tazama malaika wa Bwana alimtokea yusufu katika ndoto, akasema  Ondoka umchukue mtoto na mama yake , ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie kwa maana Herode anataka amwangamize, Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku akaenda zake Misri” ziko sababu mbalimbali na mazingira ya aina mbalimbali yanayoweza kusababisha kila mmoja wetu kuwa mkimbizi kwa namna moja ama nyingine.

Mungu anawajali wakimbizi

Biblia iko wazi kuwa Mungu anawajali wakimbizi, alionyesha kujalia sana maisha ya Kaini hata pamoja na kuwa ukimbizi wake ulisababishwa na makosa yake mwenyewe Mwanzo 4:15. Mungu alimwambia Musa katika Torati kuandaa miji ya makimbilio kwaajili ya wakimbizi watakaokimbilia kutokana na sababu mbalimbali ama ambao watu wangelikuwa wanatafuta kuwaua, Kutoka  21:12-14, Hesabu 35:9-34, Mstari 10-13 inasema hivi  Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani,Ndipo mtajiwekea miji iwe miji ya makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua mtu, pasipo kukusudia kumwua, apate kukimbilia huko.Na hiyo miji itakuwa kwenu kuwa makimbilio, kumkimbia mwenye kutwaa kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu, hata atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe. Na hiyo miji mtakayowapa itakuwa kwenu ni miji sita ya makimbilio”.  Kumbukumbu 4:41-43, 19:3-13, Nyakati 6:42-55. Mungu aliagiza pia kuwa wageni walioambatana na Israel pia wanahitaji kuheshimiwa kimsingi tunapaswa kuwajali aina zote za wakimbizi waliokimbia nchi zao kwa sababu zozote zile ziwe za kisiasa, vita uchumi njaa  na ugumu mwingine wote wanapaswa kuheshimiwa kuhifadhiwa kutunzwa vizuri, kupendwa na kuhifadhiwa,kwa heshima na usawa sawa na raia wengine tukiwahesabu kuwa ni ndugu na jamaa zetu Walawi 25, Isaya 16:1-4, Ezekiel 47:21-23 Lawi 19:33-34. Isaya 16: 3-4 inasema “Lete shauri; kata neno; fanya kivuli chako kuwa kama usiku kati ya mchana; wafiche waliofukuzwa; usiwachongee waliopotea. Watu wangu waliofukuzwa waache wakae pamoja nawe; katika habari za Moabu, uwe sitara kwake mbele ya uso wake anayeharibu; maana yeye atozaye kwa nguvu amekoma; afanyaye ukiwa ametoweka; waliokanyaga watu wametoka katika nchi.”  

         
Wakimbizi na mafundisho ya agano jipya

Agano jipya linasisitiza sana kuwahudumia wageni kuwapenda na kuwajali wenye mateso na masikini Mathayo 25:35-40,  kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi”. tofauti ya ndugu na wakimbizi iliondolewa kabisa katika agano jipya Yohana 13:34 kutokana na umoja wa waamini Yohana 17:20-23 na kutokana na udugu na wote kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo.

Hivyo ni muhimu kwa kanisa kujihusisha na kuwahudumia wakimbizi punde linapotokea swala la wakimbizi na kukutana na mahitaji yao ya muhimu haraka , kama usalama, upendo, chakula mavazi, malazi, maji safi,madawa, Kumbuka kuwa Yesu atakuja kubagua Kondoo na mbuzi kwa misingi ya namna tunavyowajudumia wengine au wenye uhitaji Mathayo 25:31-46, bila huduma hizi ni vigumu kwa wakimbizi kuikubali injili, wanyarwanda wana usemi usemao “Inda irimo ubusa ntigira amatwi” yaani tumbo tupu halina masikio, Ni muhimu kanisa likakumbuka hilo likakumbuka kuwahubiri injili lakini pia kusikiliza injili kutoka kwao ikiwa wanauwezo wa kuhudumu ili kuwalea na kukuza huduma zao punde warudipo au kuwa wamisionari katika taifa letu, hivi ndivyo nyakati za kanisa la kwanza walivyofanya pia Matendo 8;1-4, 18:1-2, Hali hii itainua heshima yao na kuwatia moyo, kanisa pia linapaswa kufanya kitu cha ziada sio tu kuwaletea maji katika birika bali kuwaelekeza namna wanavyoweza kuchimba visima wenyewe ili kujipatia maji, kanisa linapaswa pia kujihusisha katika swala zima la kuangalia chanzo cha ukimbizi na kukishughulikia hii ina maana kuwa kanisa linapaswa kujishughulisha na swala la kufanya upatanisho na kutafuta majibu ya matatizo ili kuyatatua na watu waweze kurejea katika nchi zao kwa amani badala ya kuiacha kazi hiiikafanywa na serikali zaidi, Kanisa ni lazima lisimamie demokrasia, Haki, upatanisho na mswala ya uongozi kwa ujumla, unaweza kufikiri kuwa kazi hii ni ya kiserikali zaidi nay a kijamii zaidi kuliko ya kiroho, lakini nataka nikuambie kuwa ni ya Kiroho zaidi na inapaswa kanisa kuwa sambamba na mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na huduma kwa wakimbizi

Ni muhimu kuwahudumia vema wakimbizi wao pia ni binadamu, kuna historia za kutisha kuwa sehemu nyingine wakimbizi wanabakwa, wanakataliwa, wanawekewa uzio, au wanafanyiwa hila wafe,n.k. hivi karibuni katika nchi ya Syria kutokana na vita kumekuwa na wakimbizi wengi wanaokimbilia ulaya na wengine wanapitia Libiya lakini wengi wamefanyiwa hila wakikimbia kuokoa maisha yao wengine wameuawa na mataifa mengine yameingia hofu ya kuwapokea Mungu isaidie Dunia kuwa mahali panapofaa kukaa ni wajibu wetu kupiga vita kila kinachosababisha watu kukimbia nchi zao na kujaribu kutatua migogoro iliyoko Duniani ili kila Nchi ipate Ustawi unaokusudiwa na Mungu.
Yeye aliye na sikio na alisikie neno hili ambalo Roho aliambia kanisa.
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima

Msichoke katika kutenda Mema!

Wagalatia 6:9Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.


 Utangulizi:

Msichoke katika kutenda mema, Mstari huu katika biblia ya kiingereza unasomeka “And let us not grow weary while doing good, for in due season we shall reap if we do not lose heart”
Neno

“weary”
linalotumika hapo halizungumzii kuchoka kwa mwili ambako kunaweza kukarabatiwa kwa kula, kunywa maji mengi, kuoga maji ya baridi na kupumzika vya kutosha ambako kitaalamu kunaweza kuwa tiba ya kuchoka kwa mwili, Neno hili Weary maana yake spiritless, Exhausted, lose heart, despair hii inazungumzia kuchoka kwa nafsi huku ndio kuchoka kubaya zaidi kunakoweza kuleta madhara makubwa
Kuchoka huku ni hali ya kukata tamaa, ni hali ya kutokuendelea au hali ya kuvunjika moyo, Hali hii inatokana na kukosekana kwa muamko wa Moyo na sio kuchoka kwa mwili, Hali ya kukosa muamko inaweza kupelekea mtu kuchoka katika nafsi mwili na roho. Hivi karibuni watu tumeshuhudia huko Africa ya kusini watu waliochoka nafsi waliweza kuwavamia waafrika wenzao na kuharibu vitu na kuiba na kuchoma moto matendo ambayo yameleta aibu duniani lakini sababu kubwa inatokana watu kukata tamaa, watu wanapokata tamaa huweza kucha kutenda mema na wakatenda mabaya!

 Maandiko yanatuonya kutokukata tamaa kutokuchoka, kuchoka kunaweza kuletwa na Maswala mbalimbali makubwa katika maisha yetu, Nyakati za Kanisa la kwanza wakati mwingine Makanisa yalikata tamaa kutokana na kukamatwa kwa viongozi na kuwekwa ndani mara kwa mara Waefeso 3:13 “Basi naomba msikate tamaa kwa sababu ya dhiki zangu kwa ajili yenu, zilizo utukufu kwenu.” Watu wanapokosa mwamko ni rahisi sana kukata tamaa, wanafunzi wanapokosa mwamko ni rahisi kuchoka katika kusoma, walimu wanapokata tamaa ni rahisi sana kuendelea kuwafundisha wanafunzi kwa weledi, Baba anapochoka  anapochoshwa na tabia za watoto au mkewe  nyumbani anaweza kukata tamaa, kila tunalilofanya linahitaji motosha ili tusiweze kuchoka.

Msichoke Katika kutenda Mema.

Msichoke katika kutenda mema, hili ni swala ambalo neno la Mungu linatutia moyo, kwamba tuendelee kutenda mema kwa imani, kwa upendo, na nguvu tuliyonayo katika jina la Yesu, hii ni kanuni ambayo ina mavuno ndani yake , lakini sio hivyo tu ni jambo lenye kumpendeza Mungu; Hatupaswi kuchoka hata kidogo Mungu azitie moyo roho zetu na nia zetu, Hata tunapokutana na vikwazo vya namna mbalimbali, Mara nyingi ni vigumu kupata muelekeo na kuchoka kwa nafsi, Mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, Madeni, kupoteza maswala kadhaa katika ulimwengu, kukosekana kwa shukurani au kupongezwa au hata kutiwa Moyo ulimwengu unapokuwa sio ulimwengu wenye kutia moyo ni rahisi sana watu kukata tamaa na kuacha kufanya kile wanachojisikia kukifanya na hapo Biblia inatusukuma kutokuacha au kuchoka katika kutenda mema 2Wathesalonike 3:13 “Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema.”

Kunapotokea Maswala magumu ya kukatisha tamaa na kukosekana kwa motisha miongoni mwa wakristo ni rahisi sana kwa jamii ya kanisa kuacha kuendelea kutumika katika kiwango kile tulichokuwa nacho, ni rahisi kutoa udhuru, ni rahisi kupoteza mwelekeo na ni rahisi kuacha hii inatokana na kukata tamaa Tunahitaji neema ya Mungu na kutokukata tamaa kabisa Yakobo 5:7-8 “Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia

 Neno la Mungu linatutia moyo kuwa Kutenda mema kunalipa na kuwa tutavuna kwa wakati, aidha wakati huu wa sasa ama wakati ujao liko tumaini kubwa mbele yetu na kamwe hatupaswi kuzimia moyo uvumilivu wetu unapaswa kuwa sawa na ule wa mkulima Mungu atatulipa tu kwani kila tulifanyalo lililo jema ni mbegu kwa MUngu na kwa wakati wake tutavuna kama hatutazimia moyo

Mfano:

Katika mji mmoja kulikuwa na vijana wawili waliokuwa Ndugu, Ndugu mkubwa alimuonea sana na kumtendea vibaya ndugu yake mdogo na wala hakuwahi kumuonyesha upendo, na wakati mwingine alikula chakula chake, na pia alichukua nguo zote nzuri za ndugu yake mdogo na kuzivaa yeye, Nduguye aliendelea kuvumilia na kumuonyesha upendo hatahivyo, Siku moja Ndugu yule mkubwa alikwenda msituni kwa kusudi la kutafuta kuni na kuziuza, alipokuwa msituni akikata kuni, kutoka mti mmoja mpaka mti mwingine, alikutana na mti mmoja wa ajabu, na mti huu ulimwambia tafadhali sana usikate matawi kutoka kwangu na kama utafanya hivyo nitakupa peasi la dhahabu, Kijana yule mkubwa alikubali, Lakini hata hivyo mti ule wa ajabu ulimpa matunda machahe ya dhahabu,kwa uroho na uchungu na tamaa, aliamua kutisha ule mti kuwa ataukata!kama mti huu hautatoa peasi nyingi zaidi, Mti huu wa ajabu kwa namna iaisyoweza kuelezeka ulitoa miiba mingi sana na ikamchoma yule jama amwili mzima na akawa anagaa gaa kwaajili ya kujinasua kutoka katika kujitoa miiba ile

Ndugu yake mdogo alipoona kuwa jua linakuchwa alipata hofu na aliamua kumtafuta kaka yake, na alikwenda mpaka msituni na kumkuta akiwa katika hali ngumu sana na aliamua kumsaidia kwa upendo, na kumuondoa miiba yote mwilini alipomaliza kaka yake alitambua wazi kuwa mdogo wake alikuwa na upendo wa kweli, aliomba radhi,kwa jinsi alivyokuwa akimfanyia ubaya ndugu yake na alimuahidi kumtendea mema tangu siku ile , Mti ule wa ajabu uliona yote yaliyotendeka na ukaridhika na badilikola kaka mkubwa ukawapa wote mapeas ya dhahabu waliyohitaji, wote maisha yao yalibadilika na wakaishi maisha ya upendo

tunajifunza nini kutoka kwa ndugu yule mdogo angechoka kutenda mema aisngevuna kwa wakati muafaka  nay eye na kak ayake wasingeweza kuwa na maisha ya furaha na mafanikio

Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!