Jumamosi, 24 Septemba 2016

Umuhimu wa maombi wakati wa mambo magumu!



Andiko la msingi: Zaburi 46:1-2Mungu kwetu sisi ni kimbilio na Nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso, kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa Bahari

              Gereza ambalo Paulo na Sila walifungwa wakaomba na vifungo vikaachia huko Philipi


Utangulizi.
Kwa mujibu wa Mafundisho ya kibiblia kuhusu Maombi, Biblia inatoa maelekezo kwamba imetupasa kumuomba Mungu siku zote bila kukata tamaa Luka 18:1Akawaambia mfano ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote , wala wasikate tamaa” kwa lugha nyingine imetupasa kumuomba Mungu siku zote bila kukoma 1Wathesalonike 5:17Ombeni bila kukoma” ni wazi kuwa  Biblia inatia moyo kuwa waombaji na kila siku kumuomba Mungu na kushukuru, ni katika hali zote na kwa namna yoyote imetupasa kuomba Maombi ni muhimu sana katika maisha yetu, na katika kudumisha uhusiano wetu na Mungu, Yesu alikuwa Muombaji, hatuna budi kuunganisha ucha Mungu wetu na maombi, kuacha maombi ni sawa na kuacha Ukristo!

Lakini kila mmoja anaweza kujiuliza kwa nini leo mkuu wa wajenzi anataka au anazungumzia Umuhimu wa maombi wakati wa mambo Magumu, Kwa ujumla maombi yanapaswa kuwa sehemu na tabia ya kila amwaminiye Yesu Kristo, Na pamoja na hayo binafsi sipendi kuomba wakati wa mambo magumu, nafurahia sana kuomba wakati wa amani, hata hivyo kibiblia wakati wa mambo magumu sio wakati wa kuacha kuomba ni wakati wa kuongeza bidii katika kuomba. Biblia inatufundisha kuwa nyakati za Kanisa la kwanza wakristo wa Karne ya kwanza walikuwa waombaji, sehemu kuu ya ibada ya kawaida ya kanisa ilikuwa ni maombi, waliomba Mungu siku zote, Biblia inasema walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali Matendo 2:14Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali,pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu na ndugu zake” Unaona! Biblia inaonyesha kuwa wanafunzi na mama yake Yesu na ndugu zake walidumu katika kuomba hii ndio ilikuwa tabia ya nyakati za kanisa la kwanza.

Lakini hata hivyo tunaweza kuona katika biblia Kanisa la kwanza wakiongeza Maombi zaidi wakati wa mambo magumu, kama andiko la msingi pale juu linaonyesha kuwa Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, ni msaada utakaoonekana tele wakati wa Mateso, hii maana yake ni kuwa ni lazima na ni muhimu kuliitia jina la bwana zaidi wakati wa mateso na majaribu Matendo 4:23-31 Biblia inasema

 “23. Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. 24. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; 25. nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? 26. Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. 27. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, 28. ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. 29. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, 30. ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. 31. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.”

 Unaweza kuona Kumbe wakati wa majaribu na mateso pia ni wakati mzuri wa kuongeza bidii na kumuomba Mungu kwa nguvu zaidi, Muda usingeliweza kutosha kwa nyongeza ya mifano zaidi ya kibiblia lakini biblia inaonyesha pia Paulo na Sila walipokuwa Gerezani yaani wakati wa mateso waliendelea kukazia ibada Matendo 16:25Lakini panmapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu na wafungwa wengine walikuwa wakisikiliza” unaona ukiendelea kusoma utaweza kuona ni nini kilitokea Mungu alipowajibu maombi yao hivyo Biblia inatufundisha kuwa tusikate tamaa na kuwa hata wakati wa mambo magumu inatupasa kuomba 

1.       Kwa nini inatupasa kumuomba Mungu hata wakati wa Mambo Magumu
2.       Maombi ni msaada kutoka kwa Mungu wakati wa mambo Magumu Zaburi 3:3-8;34:4
1.Bwana, watesi wangu wamezidi kuwa wengi, Ni wengi wanaonishambulia, 2. Ni wengi wanaoiambia nafsi yangu, Hana wokovu huyu kwa Mungu. 3. Na Wewe, Bwana, U ngao yangu pande zote, Utukufu wangu na mwinua kichwa changu. 4. Kwa sauti yangu namwita Bwana Naye aniitikia toka mlima wake mtakatifu. 5. Nalijilaza nikalala usingizi, nikaamka, Kwa kuwa Bwana ananitegemeza. 6. Sitayaogopa makumi elfu ya watu, Waliojipanga juu yangu pande zote. 7. Bwana, uinuke, Mungu wangu, uniokoe, Maana umewapiga taya adui zangu wote; Umewavunja meno wasio haki. 8. Wokovu una Bwana; Baraka yako na iwe juu ya watu wako.

3.       Maombi ndio njia ya Mungu ya kutulinda na nguvu na utendaji wa yule muovu Mathayo 6:13, Efeso 6:12.
4.       Maombi ndio njia pekee ya kutuletea amani tunapokutana na Magumu na hali za kutisha na kukatisha tamaa Wafilipi 4:4-7
5.       Maombi yanaweza kupindulia mbali vikwazo vya aina zote Marko 11:23-24
6.       Maombi ndio njia ya kututia moyo wakati wa kuvunjika Moyo Wakolosai 1:9-11
7.       Maombi yana nguvu ya kuhairisha jambo baya Esta 4:15-17, Daniel 2:13-19
8.       Maombi ndio njia ya kupokea nguvu za kiroho na ujasiri wakati wa vita za kiroho Matendo 4:23-31

Bila shaka sasa unaweza kuona na kuamini kupitia maandiko, kuwa wakati wa mateso na Mapito na mambo magumu ya aina yoyote ile, huo sio wakati wa kukata tamaa na kuacha kuomba ni wakati wa kuzidisha maombi na kumtegemea Mungu, Na Mungu hujitokeza  kwa viwango vikubwa tukionyesha kumtegemea yeye katika maombi wakati wa Mahitaji yetu katika wakati mgumu.

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Jumapili, 18 Septemba 2016

MUNGU SI MTU ASEME UONGO


Wengi wetu tutakuwa tunafahamu kuwa Mungu wetu ana tabia ya uaminifu na mkweli anapokuwa ameahidi jambo ni muhimu kufahamu kuwa atalifanya (2 Koritho 1;20,)Biblia inasema hivi:-

“Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi.”

 Tabia za Mungu kamwe haziwezi kufananishwa na za wanadamu ambao wao hugeuka geuka kwa sababu ya kigeugeu

 (Yakobo 1;17)Biblia inasema hivi:-  Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.”

Kwa msingi huo basi hatupaswi hatupaswi kumdhani Mungu kuwa ni kama mwanadamu yeye anapohaidi au kusema ni lazima atatenda  na kulifikiliza na kamwe hawezi kujuta kama mwanadamu kuwa kwanini alihaidi YEYE SI MTU HATA ASEME UONGO Hesabu 23;19,katika kujifunza kwetu kuhusu uaminifu wa Mungu leo tutaangalia mfano wa maisha ya Yusufu tangu Mungu alipomuahidi kwa ndoto kuwa atawatawala ndugu zake  Hali ilikuwa tofauti kana kwamba ndoto za Yusufu zinakwenda kupotelea mbali je mambo yalikuaje? Miaka kumi na mitatu ilipita na ahadi za Mungu zikatimizwa angalia mchoro huu.

Maelezo kutoka katika picha ya Grafu ya maisha ya Yusufu



·         Mwanzo 37;5-11- Yusufu alipewa Ndoto Na Mungu kuwa atakuwa Kiongozi mkubwa kiasi ambacho Nduguze watamuinamia
·         Mwanzo 37;18-22 – Ndugu wa Yusufu kwa wivu uliosukumwa na Ibilisi walitaka kumuua
·         Mwanzo 37;26-27- Mungu alimuokoa Yusufu na Kifo kwa wazo la Yuda la kumuuza Ndugu yao
·         Mwanzo 39;2-6  - Yusufu alinunuliwa na Potifa Kamanda wa Jeshi la farao na kuwa mkubwa
·         Mwanzo 39;7-20  - Majaribu Makubwa yalimpata kwa kusingiziwa kubaka na akafungwa
·         Mwanzo 39;21-23  - Mungu aliyatunza maisha yake Gerezani akawa kiongozi wa wafungwa
·      Mwanzo 41;40,42,42;5-6,43;26 – Mungu aliiitimiza Ndoto ya Yusufu Na akawa mkubwa na nduguze walimsujudia ilichukua miaka 13 kwa ndoto ya Yusufu kuwa kweli, Mungu alitunza ahadi yake Mungu si Mtu hata aseme uongo  

    Kijana Yusufu akiwa anatupwa shimoni kwa kusudi la mkuuawa, na kijana Yusufu akiwa anauzwa utumwani
   Yusufu akisimikwa kumsaidia farao kama makamu wa rais wa Taifa kubwa Duniani nyakati hizo
 
 Mambo yatupasayo Kufanya
1. Kuendelea Kumuamini Mungu ( Yusufu alimuamini Mungu katika maisha yake)
2. Kuendelea kuwa mwaminifu Yusufu hakutaka kumtenda Mungu dhambi ambazo zingeweza kuharibu Ndoto yake, hata ingawa Mungu ni Mwaminifu katika upande wetu sisi nasi tunahitaji kutunza uaminifu wetu kwake kusudi aweze kutubariki
3. Ni lazima tuwe wavumilivu hakuna ahadi ya Mungu ambayo haitatimizwa kwetu, lakini kwa uvumilivu tutazipata ahadi, ni lazima tuwe kama wakulima ambao huvumilia tangu mvua ya kwanza



Waebrania 6:13-18 "13. Kwa maana Mungu, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake, 14.akisema, Hakikayangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza. 15. Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi. 16. Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na kwao ukomo wa mashindano yote ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha.  17. Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonyesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati;  18. ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu;"  

 Yakobo 5:7-8."7. Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho.   8. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia

Jumamosi, 3 Septemba 2016

MADHARA YA KUWAGUSA MASIHI WA BWANA.


Mstari wa Msingi: Zaburi 105: 14-15 Biblia inasema “Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwaajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu wala msiwadhuru nabii zangu

Kupakwa mafuta kuliunganisha unganisho la Kiroho na uwezo wa kufanya kazi uliyoitiwa na Mungu

He allowed no man to do them wrong Amplified, He allowed no one to oppress NIV, He permitted no one to do them wrong NKJV

Kusudi la Somo:- (uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka  na kutii na kuwa tayari kwa kila kazi njema Tito 3:1)

Watu wote duniani waliookoka na wasiookoka wanapaswa kuwa na ufahamu na kuwa na hekima juu ya ujumbe huu muhimu katika maisha yao ili wasije wakajikuta wanapoteza Neema ya Mungu na kuwa na maisha yaliyojawa na mikosi na mapigo mazito yasiyoweza kuzuilika kwa sababu ya kutokuwa na ufahamu katika neno la Mungu na tukajikuta tunamchukiza Mungu, Bwana na ampe neema na hekima kila mmoja wetu kuwa na ufahamu katika somo hili katika jina la Yesu amen. Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vine vifuatavyo:-
 
·         Maana ya Neno  masihi
·         Onyo la kutokuwagusa masihi wa Bwana
·         Madhara ya kuwagusa masihi wa Bwana
·         Jinsi ya kufanya.

MAANA YA NENO MASIHI

Neno masihi limetokana na neno la kiibrania MESIAH au MESSIAS  na limejitokeza kwa mara ya kwanza katika 1Samuel 2:10, ambalo maana yake ni mtiwa mafuta au mwenye kuwekwa wakfu kwa kutiwa mafuta ili awe Kuhani, Mfalme au nabii, kwa kiyunani ni Kristo, Neno masihi mahali hapo linatumika katika mazingira tofauti sana na ile tunayoitumia kwa Bwana Yesu Kristo, Nyakati za Agano la kale mtu alipochaguliwa na Mungu kuwa kuhani, mfalme au nabii aliwekwa wakfu kwa kutiwa mafuta na hivyo kuitwa masihi, mafuta hayo yaliyomiminwa juu yao kwa jinsi ya mwili yaliwakilisha maswala muhimu katika jinsi ya kiroho 1Samuel 16:1-13, Roho Mtakatifu alishuka juu ya mtu aliyepakwa mafuta kumuwezesha mtu huyo, kuwa na uwezo wa kiungu na wa kupita kawaida katika kuyatimiza majukumu yake, ilifanyika hivyo katika nyakati za agano la kale kwa vile Roho Mtakatifu alikuwa hajaja maalumu bado, Nyakati za sasa hatutiwi mafuta katika namna ya kimwili, Lakini Roho wa Mungu mwenyewe ndiye anayemchagua mtu kwa utumishi alioukusudia  na kumpaka Mafuta Matendo 13:1-3, aidha pia katika agano jipya watumishi wa Mungu wanapowekewa mikono na kubarikiwa wanakuwa wametiwa mafuta katika namna ya rohoni, Kumbuka kuwa ni Mungu mwenyewe ndiye anayechagua “Nitengeeni Barnaba na Saul kwa kazi ile niliyowaitia” watu wa Mungu

Mafuta ilikuwa na hata sasa ni alama ya Roho Mtakatifu, mtu alipopakwa mafuta Roho alimuwezesha kuwa na vipaji vya kiroho vya kuweza kutimiza jukumu alilokabidhiwa, Mfano Yesu Kristo kama Masihi hakupakwa mafuta kwa jinsi ya mwili, lakini alijiliwa na Roho Mtakatifu na kuongozwa katika kuyatekeleza majukumu yake Luka 3:21-22,4:1,18-19 Kupakwa mafuta kwa Yesu Kristo kulimfanya awe na uwezo wa kipekee katika kuitimiza huduma yake hivyo Yesu ni Masihi ni mpakwa mafuta ni Kristo, Mtu anapomwamini Yesu kuwa bwana na mwokozi wamaisha yake Roho wa Mungu anakaa ndani yake kwa hivyo kibiblia mafuta yanakaa ndani yake 1Yohana 2:26-27, Yohana 14:25-26, hivyo watu waliookolewa ni wapakwa mafuta roho Mtakatifu anakaa ndani yetu 1Wakoritho 3:10, Hata hivyo kutoka miongoni mwao Roho Mtakatifu ambaye ndiye Bwana wa Mavuno, huwaita watu katika huduma Matedno 13:2, watumishi wa Mungu wanaoitwa katika huduma maalumu za utumishi, Roho wa Mungu anakuwa juu yao kwaajili ya kutimiza huduma waliyoitiwa, kwa hiyo nao huitwa wapakwa mafuta, wapakwa mafuta hao wanakuwa wametumwa na Mungu na hivyo huyanena maneno ya Mungu Yohana 3:24 wao huubiri kweli yote kwa ujasiri bila kuichakachua injili, watasimamia kweli yote huku wenyewe wakiwa kielelezo cha injili wanayoihubiri, watakemea, wataonya, watatia moyo na hawatahubiri khadihi za kutungwa na wanadamu Mathayo 5:48, watahubiri utakatifu 1Petro 1:13-16,Waebrania 12:14 watafanya na kutenda kama Yesu Kristo mwenyewe, Masihi wa Bwana wanaishi kwa haki na utauwa, bila kuwa na lawama zilizo na ukweli 1Wakoritho 1:11, 1Wathesalonike 2:10, Biblia inasema tutawatambua kwa matunda yao.

Aidha masihi wa Bwana watafanya kazi ya kulitetea jina la Bwana lisichafuliwe au kutukanwa, Manabii makuhani na manabii nyakati za agano la kale hawakujali sana watu maadui zao wanasema nini juu yao bali, walijali sana maaduin au watu waliokuwa wakitaka au kumkufuru Mungu.

Masihi wa Bwana watahubiri Utakatifu, Ni  muhimu kufahamu kuwa shetani hawezi  kuhubiri  utakatifu na ni rahisi kupambambanua kati ya mtumishi wa shetani na  Mtumishi wa Mungu, sifa  mojawapo ya Mtumishi wa shetani ni kuhubiri maneno yake. ( maneno yao) na  watajifanya ni watumishi  wa haki na watahubiri   mambo   ambayo ukiwauliza kwa wameyapata wapi au yameandikwa wapi, watakuambia  hii  ndiyo  sheria au desturi ya kanisa:  watajitungia mambo yao  na  hawataihubiri  neno, shetani kamwe hawezi   kuhubiri  utakatifu   na watumishi wa shetani  hawawezi  kamwe  kuishi  katika  utakatifu  na akawa  kielelezo  na hawezi  kuwafanya  watu waokolewe na  kukaa  katika  usafi  na utakatifu: (shetani hawezi kumtoa  shetani )

ONYO LA KUTOKUWAGUSA MASIHI  WA BWANA. Zaburi 105: 14- 15,  I Nyakati  16: 21-22
Ni muhimu kufahamu kuwa Maandiko matakatifu yanatoa maonyo na yamejaa mafundisho na mifano ya kutosha yanayotoa maonyo dhidi ya kuwagusa masihi wa Bwana

Kuwagusa huku ni pamoja  na kuwasengenya, kuwanena  vibaya, kuwachafulia huduma zao ili waonekane  wabaya  hawafai kama walivyomchafua  Yesu  kwa  kusema  anatoa pepo kwa Nguvu za mkuu wa pepo Bezelzebul, kuwadhalilisha, mbele za  watu  wengine  kuwalia huduma zao ,  kuwaua moja kwa moja  au kuwadhuru kwa mabaya au kuwatukana huko ni kuwagusa  masihi wa Bwana au kuwanyanyasa, kuwavunjia Heshima, kuwadhulumu, na kuwatendea mabaya  kumgeuza  mkewe, hata  kama ni mfalme  atashughulikiwa  atadhibitiwa na  Mungu Zakaria 2: 8  kuwagusa hawa ni kugusa  mboni  ya jicho la Mungu;  Hivyo hata kama sisi ni  wachungaji tunapaswa kuangalia walio juu  yetu  kwani wao  ni masihi wa Bwana. Kwa nini Biblia inaonya kutokuwagusa masihi wa Bwana au wapakwa mafuta?

1.       Wao ni Mawakili wa Mungu- Tito. 1:7,8,9 “Maana imempasa askofu(mwangalizi) awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa Mungu; asiwe mtu wa kujipenda nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu; bali awe mkaribishaji, mpenda wema,mwenye kiasi,mwenye haki, mtakatifu,mwenye kudhibiti nafsi yake, akilishika lile neno la imani vilevile kama alivyofundishwa,apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.”

2.       Hawajichukulii wenyewe heshima hii Waebrania 5:4 “Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe Heshima hii ila yeye aitwaye na Mungu kama vile Haruni

3.       Biblia imeagiza kuwatii na kuwanyenyekea wanaotuongoza Waebrania 13:17 “watiini wenye kuwaongoza  na kuwanyenyekea  maana wao wanakesha kwaajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua maana isingeliwafaa ninyi

4.       Mungu huwaheshimu watu wanaomtumikia Yohana 12:26 “Mtu akinitumikia na anifuate nami nilipo na mtumishi wangu atakakapokuwepo, tena mtu akinitumikia Baba atamheshimu

MADHARA YA KUWAGUSA MASIHI WA BWANA.

Muda usingetutosha kuweza kuangalia mifano  mmoja moja katika Biblia juu ya watu waliowagusa masihi wa Bwana na kushughulikiwa kwa makini na Mungu alivyoonyesha  ghadhabu juu yao hata hivyo tutaangalia mifano kadhaa:

1.       MARIAMU: (Hesabu 12: 1- 9) Miriamu alikuwa nabii mke lakini alinena vibaya juu ya uongozi wake Musa na  alishughulikiwa kwa kupigwa ukoma.

2.       FARAO:  Alichukua mke wa Ibrahimu kwa kutumia mamlaka ya kifalme alivyokuwa nayo na alishughulikiwa kwa mapigo mazito sana.( Mwanzo. 12: 14- 17

3.       ABIMELEKI:  Alipotamani kumchukua Sarai mke wa Ibrahim Mungu alimtandika( MWANZO 20: 1- 4, 6-8,14)

4.       YEROBOAMU: ( I Falme 13: 1- 4

5.       ASKARI WALIOTAKA KUMKAMATA  ELIYA  Bila kuonnyesha unyenyekevu  ( 2 Falme 1: 5- 15)

6.       WATU WALIOMFANYIA MZAHA ELISHA  yaani vijana waliomtania Upara wake (2 Falme 2: 23- 25)

7.       MWAMLEKI Aliyejidai kuwa ameuua  SAULI ( 2  Samwel 1: 1-16)

8.       Herode Baada ya Kumuua Yakobo Matendo 12: 1-4,20-24

JINSI YA KUFANYA.

-          Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu anaheshimu sana mafuta na kwa sababu hiyo si vema kupuuzia mafuta yaliyo juu ya watumishi wake kwani kwa kufanya hivyo kuna madhara yawezayo kutupata
-          Ni muhimu pia kufahamu kuwa kupakwa mafuta haipaswi kuwa sababu ya kuwafanya wapakwa mafuta hao kutokuishi sawa na maadili ya injili na Neno la Mungu
-          Ni muhimu kuomba kwa ajili ya wapakwa mafuta kwa sababu nao ni wanadamu

Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote
Nilijifunza kutoka kwa Bishop Zachary Kakobe, Miaka zaidi ya 20 iliyopita.