Jumatatu, 29 Aprili 2019

Imekwisha !



Yohana 19:28-30Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani.  Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, IMEKWISHA. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.


Utangulizi:
Mojawapo kati ya usemi wenye maana sana kati ya semi saba za Yesu alizozisema akiwa msalabani na ambazo zinatajwa katika sehemu mbalimbali za injili, moja ya usemi huo wa muhimu ni usemi wa sita wenye Neno IMEKWISHA  ambalo leo katika siku ya pasaka tutachukua muda kulijadili kwa undani na kupata maana iliyokusudiwa, maneno mengine kati ya maneno saba aliyoyasema Yesu msalabani ni pamoja na:-
·         Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34
·         Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43
·         Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27
·         Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46
·         Nina kiu Yohana 19:28
·         Imekwisha Yohana 19:30
·         Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46
Maana ya neno IMEKWISHA
Ni muhimu kufahamu kuwa Neno IMEKWISHA ambalo katika kiingereza kiingereza linasomeka “IT IS FINISHED  katika Biblia ya kiyunani yaani Kigiriki linasomeka kama “TETELESTAI  Neno hili ndio neno la Mwisho kabisa katika maneno aliyoyatamka Yesu pale msalabani kabla ya kutamka neno “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu” na kufariki dunia pale msalabani, Neno hili Imekwisha TETELESTAI limetokana na neno TELEO la kiyunani ambalo maana yake ni Kukamilisha kazi, kumaliza kazi, kutimiza kazi, to complete or to accomplish, neno hili lina umuhimu mkubwa kwa sababu linazungumzia kumaliza kazi kwa furaha, au kwa mafanikio, utamu wa neno hili ni kama vile mtu anapokuwa amemaliza mtihani wa mwisho katika kozi ya mwisho, au mtihani wa mwisho kabisa wa kumaliza shule au chuo au kama vile mtu aliyekamilisha malipo ya mwisho ya ununuzi wa nyumba au gari, (Paid in Full) au kukamilisha kwa usahihi kile ulichowaza au kufikiri kuwa utakifanya na ukakifanya kwa usahihi kabisa, Kama vile Mungu alivyosema tazama kila kitu kimekuwa chema, well done, kazi imefanyika kwa ufasaha.

Lakini ni muhimu kufahamu kuwa neno hili IMEKWISHA liko katika wakati uliopita kwa namna linavyoonekana hapa  lakini katika kiyunani ni sentensi kamili Perfect tense na kwa sababu hiyo neno hili linapata umuhimu mkubwa kwa sababu lina maanisha imekwisha katika wakati uliopita, uliopo na ujao kwa msingi huo neno hili linaendelea kufanya kazi kila siku na kila wakati, Neno hili pia lilimaanisha kuwa kama kulikuwa na deni, basi deni hilo limelipwa milele, wale wamuaminio Yesu hawana wanachodaiwa, kama ilikuwa ni kesi imefutwa na hati za mashitaka zimeharibiwa kabisa Wakolosai 2:14-15 akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo”.Neno hili ni kama kupewa ruhusa kutoka hospitalini baada ya kuugua kwa muda na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kila mtu akijua umekwisha kisha ukainuka tena ukiwa mzima wa afya. Ni neno muhimu sana katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu na wokovu wetu.

Umuhimu wa neno IMEKWISHA.

Yesu alipolia kwa sauti kuu IMEKWISHA alimaanisha katika wakati uliopita, sasa na itaendelea kuwa imekwisha hata baadaye. Kumbuka kuwa hakusema nimekwisha hii ingemaanisha kuwa ameshindwa na kifo, lakini alilia akisema IMEKWISHA! maana yake nimeikamilisha kwa ufasaha kazi niliyokuja kuifanya. Kwa msingi huo neno imekwisha lina maana ya hakuna kilichosazwa katika kazi ya ukombozi aliyokuja kuifanya na hivyo alikuwa akizungumza ukweli kuwa kila kitu kimekamilishwa sasa ni mambo gani Yesu aliyakamilisha yako mengi mno lakini baadhi ni pamoja na:-
1.       Alikamilisha kazi yote aliyokuwa ametumwa na baba yake kuja kuifanya duniani Yohana 17:4 “Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.

2.       Alikamilisha kazi ya kuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea Luka 19:10 “Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”

3.       Alikamilisha kazi ya kutukomboa sisi na adui zetu Luka 1:68-74 “Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu; Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote wanaotuchukia; Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake takatifu; Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu, Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu,

4.       Alikamilisha unabii katika torati na manabii uliozungumza kumuhusu yeye kwa unabii, ishara, alama na vivuli kuhusu ujio wake na kazi zake kutoka kitabu cha Mwanzo mpaka kitabu cha Malaki ambako kuna nabii zaidi ya 300 kuhusu Masihi Mwanzo 3:15 na Isaya 53

Kwa msingi huo hatupaswi tena kuteseka, kuwa watumwa, kukandamizwa, kuonewa, kuugua na kuteswa na magonjwa, kuwa watumwa wa dhambi na shetani, hatupaswi kumuogopa awaye yote, Nguvu za giza, na wachawi na washirikina na waganga, na mapepo na majini na mashetani na shetani hazina uwezo juu yetu kwa imani katika kazi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani, laana ya torati, na sheria, hatuna deni, hatuna deni la jana wala la leo wala la kesho kazi imekamilika yakikutokea majanga angalia msalaba kumbuka kazi iliyofanyika msalabani, kumbuka kuwa mwanaume huyu amemaliza amakamilisha kazi ya ukombozi huna hatia hata kidogo hakuna wa kukuhukumu, wewe hata kama ulikuwa na historia mbaya sana yeye anawweza kuifuta na kuiandika upya endapo utamwamini Bwan Yesu, Neno imekwisha ni neno lenye nguvu kama vile siku unapotangazwa uhuru wa taifa lililotawaliwa na wakoloni, tunapoadhimisha siku ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo yaani katika siku hii ya pasaka ni lazima tujikumbushe kuwa Yesu amekamilisha kazi ya kutuweka huru na kuvitangazia vifungo vinavyotuzunguka kwa kuvitangazia kuwa imekwisha, Mateso yamekwisha, kazi za shetani zimekwisha, majini na mapepo kazi zao zimekwisha kila aina ya vifungo na utumwa wa ibilisi ni lazima zisikie na kukumbuka kuwa imekwisha

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Wamisri wakatuonea, wakatutesa, !


Kumbukumbu la torati 26:6-9 “Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito.  Tukamlilia Bwana, Mungu wa baba zetu; Bwana akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu.  Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu; naye ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali.”

 Sinagogi la Kiyahudi huko San Diego, lililoshambuliwa kwa Risasi 28/04/2019

Utangulizi:
Jana tarehe 28 April 2019  sawa na mwezi Nisan 23 5779 kwa kalenda ya kiyahudi, nilipata habari ya kuuawa kwa Myahudi mmoja kutokana na shambulio la risasi lililofanyika huko San Diego katika mojawapo ya sinagogi la kiyahudi, na wengine watatu kujeruhiwa vibaya, nilikuwa bado sijasahau tukio la kuuawa kwa wakristo wakati wa Pasaka Nchini Sri-lanka nikafikiri na kuwaza kwamba bado dunia ya leo iliyoendelea kuna watu bado wanafikiri wanaweza kuwepo duniani peke yao bila kuchanganyika na watu wanaotofautiana nao kimawazo kifikira kiitikadi na kiimani? Dunia inapaswa kutafakari kwa kina kuhusu ukomavu na uwezo wa kuchukuliana katika jamii na kupendana bila kujali tofauti zetu,
Biblia inasema katika 1Yohana 4:8Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo.” Hii ni wazi kuwa bado dunia haijamjua Mungu, na kuwa jamii inapaswa kukumbuka na kuhimiza na kufundisha kuhusu upendo, ni muhimu kufanya kilalinalowezekana kuing’oa chuki miongoni mwa wakazi wa dunia, na kukumbuka kuwa Yesu hakuwa mjinga alipokuwa akifundisha Upendo, alikuwa anajua wazi kuwa dunia itakuja kufikia na kuwa na matukio haya tunayoyashuhudia leo katika jamii iliyoendelea.
Katika kifungu cha maandiko ya msingi, Musa alikuwa anawakumbusha wana wa Israel sheria za Mungu na hususani kwa kizazi kipya ambao wengi waoa walizaliwa Jangwani au na wale waliotoka Misri wakiwa vijana na waliokuwa wadogo, Musa alikuwa akizungmzia kumtolea Mungu sadaka za shukurani watakazomtolea Mungu watakapokuwa katika nchi ya amani nchi iliyojaa maziwa na asali nchi ya Israel aliwalekeza kwamba watakapotoa wamkumbushe Mungu kuwa walionewa huko Misri, lakini walipomlilia Mungu akawaokoa na kuwaleta katika inchi hii iliyojaa maziwa na asali
Katika kifungu hiki Kumbukumbu la Torati 26:6 ““Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito. .”
Biblia ya kiingereza  NIV inasomeka hivi Deuteronomy 26:6But the Egyptians mistreated us and made us suffer, subjecting us to harsh labor.”
Biblia ya Kiyahudi iitwayo (The Israel Bible) inasomeka hivi Deuteronomy 26:6The Egyptians DEALT HARSHLY WITH US and oppressed us; they imposed heavy labor upon us.”
Musa aliwakumbusha Jambo hili la msingi walikumbuke watakapokuwa wakiabudu, kwa sadaka ya shukurani, wamkumbushe Mungu kuwa walitendwa vibaya na wamisri neno kuonewa, kuteswa na kutendwa vibaya katika lugha ya Kiebrania linatumika neno “VAYAREIU”  likimaanisha kuwa lakini rafiki zetu walitugeuka,walitutenda mabaya, wakatuonea, wakatutesa, wakatudhulumu kisha wakatugeuza  kuwa watumwa kwa utumwa mbaya na mzito” Hii ilimaanisha kuwa Israel hawakushuka Misri wakiwa watumwa walikuwa rafiki wa wamisri, walikuwa wapendwa, walikuwa jamaa na ndugu wa waisrael, lakini hatimaye ukafika wakati wakawageuka, wakavunja urafiki, wakaanza kuwabagua na kutengeneza sheria za kuwabana, na kuwaonea na kuwatesa na kuwakandamiza na hatimaye kuwafanya watumwa wao, Ndipo ulipofika wakati wayahudi wakamlilia Mungu awatoe katika utumwa ule mzito na Mungu akawaokoa akawapeleka katika nchi ya ahadi, ambako huko npekee ndipo mahali ambapo Wayahudi watakuwa salama na wakamfurahia Mungu.
Leo hii sio Misri tu ambao wamewakaribisha Wayahudi kisha wakawaonea baadaye, ziko nchi nyingi tu ambazo zimewapokea wayahudi wakiwa kama marafiki, kama ilivyotokea Ujerumani na Uganda, lakini baadaye katika namna isiyoweza kueleweka watu hao waliwageuka nakuwaona wayahudi kama adui na watu wasiofaa, ili mtahudi aweze kuwa salama ni lazima popote pale walipo warudi katika nchi yao ya asili nchi yao ya ahadi ili wamuabudu Mungu pasipo hofu na watoe sadaka ya shukurani na mateso yao yote yatageuka kuwa historia
Wako watu wengi sana leo wanateseka lakini chanzo cha mateso yao hakikuwa chuki na majuto na dhuluma ambazo wanaziona sasa, inawezekana wewe ni House girl ulichukuliwa kama dada wa kazi kwa nia nzuri, ukaenda mjini kama rafiki na ndugu, na ukapokelewa vema huko ulikokwenda mama na baba wa nyuma uliyofikia walikataa kuitwa anko walisema utuite mama au baba, lakini baada ya siku kadhaa hali ilibadilika umeanza kuitwa hili, limbwa, paka , nyau. Fala na kadhalika.

Inawezekana ulioa au kuolewa kwa nia nzuri kabisa, wakati unachumbiwa ulikuwa ni rafiki, hukuwa mtumwa mliitana majina mazuri, sweetie, asali wangu, maua, dear, dally na kadhalika lakini hapa unaposoma ujumbe huu mambo yamegeuka wewe sasa ni jibwa, fala, lione, liangalie, sijui nililioa la nini, mlango wa nane, balaa nuksi, mwiba na kadhalika.
Inawezekana wakati uaajiliwa ulikaribishwa kwa furaha, bosi aliwataka wenyeji wakupe saada mkubwa utakaouhitaji, ulidekezwa, ulifanywa kama moja ya wamiliki wa kampuni, ulikuwa ni wakati wa furaha umepata kazi mpya, lakini baada ya sikukadhaa, Mambo yamebadilika, unaonekana kama mzigo, unateseka, unapelekeshwa unaonekana hifai tena.
Kila mahali walikokwenda Wayahudi walikaribishwa walipokelewa kwa ukarimu lakini leo watu wanawalipua, wanawapiga risasi, kama majambazi au watu wasiofaa, huko san diego wayahudi wameuawa katika sabato ya kwanza ya Pasaka walipokuwa katika ibada na mama mmoja mwenye miaka 60 alifariki na wengine watatu kujeruhiwa vibaya, mmoja akiwa kiongozi wa kidini Rabbi na mkuu wa sinagogi husika kinawafanya wengine wawe na chuki dhidi ya wengine, kwa nini wakristo wameuawa Srilanka na kwa nini waqyahudi wameshambuliwa nani atawasemea
Hujawahi kuona unakaribishwa mahali vizuri, unapeewa na ofisi, unasifiwa kila mahali unahesabika kama mtu mwema kisha baada ya muda wewe ndio unaonekana kama mwiba wa kila mmoja pale ulipo?
Hali hii ndio inayowatokea Israel Duniani kote, ndio inayoatokea Wakristo, watu wanaona kuwa ni haki kuvaa mabomu na kuwalipua
Iko siri moja kubwa na ya kipekee, ni kukaa katika ahadi za Mungu tu, Ili Israel iweze kuwa salama hawana budi kuungana na kukaa Israel pekee ili wajilinde wakae katika nchi ya ahadi waliyoahidiwa baba zao Ibrahimu Isaka na Yakobo ndio wanaweza kujithibitishia usalama wao.
Wako watu wengi leoa hawako salama kwa sababu walifanya urafiki na shetani, walipokelewa na shetani , ibilisi kwa furaha sana wakiwa kama marafiki, Lakini kumbuka kuwa shetani hana urafiki na mtu awaye yote lazima atakugeuka tu atakutesa atakugeuza kuwa mtumwa na atakudhulumu, shetani anataka ufanye mambo kwa faida yake na maslahi yake hakuna mafanikio ya kweli kwa shetani, ili uwe salama huna budi kurudi kwa Yesu kristo na kujificha kwake, yeye ndio nchi halisi ya ahadi na kwake kuna usalama, Kwa ibilisi haijalishi kuwa wewe ni mwenye haki au la kwake nifuraha kubwa ukiangamia yeye na watu wake hawatajali haki yako, wakati umefika wa wewe kukaa katika uwepo wa Mungu kwa usalama wako, ili amani ipatikane katika ndoa yako hakikisheni mnamkaribisha Mungu na kujifunza upendo kama yeye alivyoagiza.
Isaya 5:1 Mwenye haki hupotea, wala hakuna atiaye hayo moyoni; na watu watauwa huondolewa, wala hakuna afikiriye ya kuwa mwenye haki ameondolewa asipatikane na mabaya
Hakuna wanaojali kile kinachowapata wayahudi leo. Lakini Palestina ikiguswa tu dunia itapiga kelele hata kama wakati mwingine wao ndio wachokozi na ndio wanaoanzisha kurusha maroketi, Israel ikijibu kama sehemu na wajibu wa kujihami na kujilinda, Israel ikijilipizia kisasi kwa adui zake dunia inapiga kelele je wadhani Wayahudi sio watu, nani atawapigia kelele na kuielimsha jamii duniani kuwa nao wanastahili kutetewa na kuangaliwa kwa maslahi yao duniani, Mimi sisemi kwa sababu nina asili ya Kiebrania tu hapana bali nataka haki itetendeke duniani ifikie hatua tujifunze pendo lake Yesu na kuielimisha katika jamii yetu, kila mmoja anapaswa kujua kuwa kama tunampenda Mungu tutathamini uhai wa watu wake kuliko imani zetu, Dunia pia inapaswa kuelewa kuwa ili Israel iweze kuwa salama  nilazima waelekee katika nchi ya ahadi na kukaa katika taifa lao wenyewe, ili sisi nasi tuweze kuwa salama turudi katika uwepo wa Mungu. Tutafanikiwa. Israel walimlilia Mungu, akawasikia akaziona taabu zao na kuonewa kwao aakawaokoa kwa mkono wa nguvu ulionyooshwa na wakajiliwa na kipindi cha neema  I stand with Israel.”
Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima

Jumapili, 28 Aprili 2019

Sitakupungukia wala sitakuacha!

Mstari wa Msingi: Yoshua 1:5-8 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako”.



Jumatatu ijayo kidato cha sita kote Nchini wanatarajia kuanza mitihani yao ya kumaliza Elimu ya juu ya sekondari, nafahamu sana katika wakati huu wengi watakuwa wana hofu kwamba mambo yatakuwaje japo kweli wengi wamejiandaa vizuri na hawana wasowasi kabisa kukabiliana na mtihani huo, lakini hata hivyo Mungu alinipa neno hili maalumu kwaajili yao kwamba “Naye Bwana, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.” Kumbukumbu la Torati 31:8

Ni muhimu kufahamu kuwa katika maisha wakati mwingine tutakabiliana na changamoto za aina mbalimbali, ziko changamoto nyingi lakini mojawapo ya changamoto kubwa ni pale unapodhani kuwa uko peke yako au unakabiliana na muda ambao utabaki mwenyewe na wakati huo utapaswa kutatua changamoto zinazokukabili ukiwa peke yako, Bila mtu aliyekuwa anakupa msaada wa karibu, Mungu alifanya kazi na Musa kwa kiwango kikubwa na cha ajabu, Mungu pia alifanya kazi na Yesu Kristo kwa uweza mkubwa na waajabu, Musa alipokuwa ameondoka Yoshua alibaki mwenyewe na hivyo alikuwa na mashaka makubwa kuwa itakuwaje endapo atakabiliwa na changamoto nzito zilizoko mbele yake, sio hivyo tu hata wakati Yesu anaondoka wanafunzi wake walikuwa na wasiwasi mkubwa sana kwamba itakuwaje Jibu sahihi katika wakati huu lilikuwa ni kuwahakikishia kuwa nitakuwa pamoja nanyi, Mungu alimuhakikishia Yoshua kuwa atakuwa pamoja naye hatampungukia wala hatamuacha

Ni rahisi kwetu wanadamu tunapopita katika changamoto ngumu huku tukifikiri kuwa hakuna msaada ni rahisi kwetu kupiga kelele za kibinadamu kama zile alizopiga Yesu Kristo pale msalabani baada ya mateso mazito “Mungu wangu mungu wangu mbona umeniacha?” Mungu katika neno lake ameahidi mara kadhaa kwani anatujua vema umbo letu anajua udhaifu wetu na ameahidi kuwa hatatuacha kamwe, ushindi wetu katika maisha yetu unaanza na ujasiri huu kwamba Mungu yuko Pamoja nasi, Hatatuacha wala hatatupungukia.

Tunapokaribia kuingia katika vyumba vya mitihani wiki ijayo, ni kweli kuwa tutakaa wenyewe mbali na wenzetu mbali na walimu, tutakuwa tukikabiliana na maswali yaliyotungwa na watu tusiowajua sisi, wasio walimu wetu sisi na hivyo ni rahisi kuogopa mtihani kwa sababu tu umepewa jina la mtihani wa kitaifa, lakini hata ujapokuwa peke yako katika chumba chako cha mtihani kumbuka kuwa Bwana anatangulia mbele yako hatakuacha kabisa wala kukupungukia kabisa. Hakuna mtu alipewa wajibu wa kufanya na Mungu kisha Mungu asiwe pamoja nae, mmepewa wajibu wa kusoma kwa sasa na hilo ndio kusudi la Mungu kwaajili yenu katika kusudi hilo Bwana atakuwa pamoja nanyi, MSIOGOPE.

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; NA TAZAMA, MIMI NIPO PAMOJA NANYI SIKU ZOTE, HATA UKAMILIFU WA DAHARI

Hakuna maneno ya muhimu kama haya wakati tunakabiliana na changamoto yoyote mbeleni Mungu akikuambia kuwa yuko pamoja nawe tayari hii ni alama kubwa sana ya ushindi, lakini akikuambia kuwa hatakuacha wala nhatakupungukia ni zaidi ya ushindi, yeye atakuwa pamoja nawe ahadi hii imerejewa mara kadhaa katika maandiko kwa kusudi la kutuondolea woga na kutupa ujasiri na moyo wa kujiamini, kwamba atakuwa pamoja nasi, katikwa wakati wa msahaka na wasoiwasi kumbuka atakuwa pamoja nasi kwa uwepo mkubwa sana.

Mungu alimwambia Yakobo katika Mwanzo 28:11-17 “Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. NA TAZAMA, MIMI NIPO PAMOJA NAWE, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni.

Mungu anataka tuwe na ujuzi huu, kwamba yuko pamoja nasi, ujuzi wa aina hii ukiwa wazi mbele yetu hatutaogopa, tutakuwa na ujasiri, kwamba hata iweje yuko Mungu ambaye ni Mchungaji mwema na hivyo hatutapungukiwa na kitu, kwa vyovyote vile hatatupungukia wala hatakuacha hata tujapopita katika uvuli wa mauti

Daudi alipoifahamu siri hii hakuogopa alimtegemea Mungu na alijua wazi kuwa Mungu ni Mchungaji wake na kwamba hatapungukiwa, wala hataogopa mabaya au vitisho kwa maana yeye yupo pamoja naye, Hofu ni adui mkubwa wa mafanikio yetu, wanafunzi wengi wenye akili na uwezo wanaweza kufanya vema siku zote lakini wanaweza kuharibu wakati wa mitihani kwa sababu shetani huwatia hofu huwaogopesha lakini leo Bwana amenituma nikuamnbie kuwa usiogope Bwana yu pamoja nawe

Zaburi 23: 1-6 “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana WEWE UPO PAMOJA NAMI, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika.   Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.

Yoshua alichoambiwa na Mungu ni kuliamini neno lake tu, kwamba alisome, alitafakari na kulitii na kulifuata na kuwa akifanya hivyo haitakuja itokee amepungukiwa na kitu, Hutapungukiwa na kitu Yesu akikutuma, hii ni ahadi katika neno lake anapokuagiza Yesu hata kama huna kitu mfukoni hutapungukiwa 

Luka 22:35 “Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La!

Waebrania 13:5-6 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?

Jambo kubwa na la msingi ni kuamini neno lake, na kulitendea kazi, na ndio maana, Mungu alimwambia Yoshua aliangalie neno la kulitafakari na kulishika atafanikiwa katika kila alifanyalo na kila aendako na kuwa hakuna kiti au mtu atakayeweza kusimamam mbele yake siku zote za maisha yake, Hitler Dikteta mkubwa sana alikuwa ni mtu asiye na hofu askari wake pia hawakuogopa walikuwa watii mno kwa neno la Hitler kwa kiwango cha kufa lakini Hitler anasema alikuwa anaogopa mitihani, sisis hatupaswi kuogopa kwa sababu Mungu ameahidi kwamaba atakuwa pamoja nasi, hii ni ahadi yake kwetu, na ni neno lake kwetu tuamini tu na utaona mafanikio makubwa katika mitihani itakayoanza jumatatu ijayo ya tarehe 6/05/2019 Bwana hatakupungukia wala hatakuacha amini tu neno lake.

Mathayo 7:24-27 “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.

Sisi ni warithi wa Baraka zake Ibrahimu, Ibrahimu baba yetu wa imani alikuwa rafiki wa Mungu, Ibrahimu hakuishi maisha ya hofu Mungu alimtokea na kumwambia wazi kuwa yeye ni thawabu yake kubwa sana na Ngao yake

Mwanzo 15:1 “Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.

Baba katika jina la Yesu nawasogeza kidato cha sita nchi nzima nawaombea mtihani mwema, naamini neno lako litawafikia hata kama wengine wako shule za Bweni na hawajui Mungu amesema nao nini lakini mimi mtumwa wako kwa nenolako ulilonipa nawaombea wote uwe pamoja nao kama ulivyoahidi, katika neno lako, uwasaidie wote wanaokutegemea wewe Bwana nakuomba usiwaangushe ukawafanikishe na uwepo wako ukawe pamoja nao katika vyumba vyao vya mitihani kwaajili ya utukufu wako, asiwepo awaye yote wa kuwatisha wala kuwaingizia hofu, nawakinga kwa jina lako kutoka katika mashambulizi yote ya yule muovu nakusihi ukawe pamoja nao, Katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai, Amen!

Na. Rev Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.