Jumatano, 27 Machi 2019

Mungu aonaye!


Mwanzo 16:1-13 “Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake. Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe. Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako. Naye atakuwa kama punda-mwitu kati ya watu, mkono wake utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu wote utakuwa juu yake, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote. Akaliita jina la BWANA aliyesema naye, Wewe U Mungu uonaye, kwani alisema, Hata hapa nimemwona yeye anionaye?”


Utangulizi:

Ni muhimu kwa kila mwanadamu kuwa na ufahamu kwamba kila wakati tunapopitia Mateso na mambo  magumu ya kukatisha tamaa, kukumbuka kuwa hatuko wenyewe, Mungu aonaye “Jehoha Rohi” anaona kila tunalolipitia na kila kinachotokea katika maisha yetu, Mungu anajali sana  na anajishughulisha sana na mambo yetu, Yeye sio mwepesi wa hasira, wala sio Mungu aliye mbali, au asiyejali yeye anajali, anatamani sana tuwe na mambo mazuri na kila kitu kituendee vizuri katika maisha yetu, anataka kila mmoja wetu aweze kuwa na maisha ya ushindi na furaha, sisi ni watoto wake ni kondoo wa malisjo yake anawajibika kututunza na kushughulika na mahitaji yetu Bila upendeleo.

Mungu anajua na anaona kila unachopitia.

Mwanzo 16:1-6Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake. Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe. Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake.”

Katika kifungu cha maandiko wote tunaweza kuoina hali halisi, iliyojiyokeza katika familia ya Ibrahimu na Sara a mjakazi wao Hajiri, kwamba japo jambo hili lilikuwa sawa katika mila na desturi za kikaldayo, lakini haikuwa sawa katika macho ya Mungu, ziko mila na desturi ambazo watu baada ya kuwa na urafiki na Mungu wakizifuata zinaweza kuharibu mtiririko wetu wa imani katika kuonyesha kuwa tunamtegemea Mungu, Sara alikuwa amechoka kwa mapito aliyokuwa akiyapitia, Mungu alikuwa amemuona Sara na alikuwa amekwisha kumuahidi kuwa atamkumbuka lakini Sara alikuwa ameelemewa na huzuni na maumivu:-

·         Maumivu yamatumaini yaliyokuwa yakitarajiwa lakini yamechelewa
·         Maumivu yanayoashiria kana kwamba Mungu hajajibu mamombi au amechelewa kujibu maombi
·         Maumivu kwamba mikono yake haijawahi kushika mtoto wake mwenyewe
·         Maumivu ya aibu kujulikana kama mwanamke aliye tasa au mgumba na asiyezaa katika jamii
·         Maumivu ya kumlaumu Mungu kama asiyejali maumivu yake na mateso yake

Hali hii inampelekea Sara kuamua kutumia akili na njia za kibinadamu kutatua tatizo walilonalo katika familia yake, Usahwishi wake kama ilivyokuwa kwa Eva na Adamu unasikilizwa na Ibrahimu, wanaamua kuongeza mke ambaye ni Hajiri, Bila shaka ni moja ya watumwa (Kijakazi) wa Sara  aliyepewa huko Misri na Farao, Matumizi yao ya akili katika kutaka kutatua tatizo lao nje ya mfumo wa njia za kimungu kunaleta tatizo kubwa zaidi, Hajiri anashika Mimba, lakini yeye sasa anapoteza kutii, kule kushika Mimba kunampa kiburi, anasahaku kuwa aliinuliwa kwa mawazo ya Sara, mgogoro unakuwa mkubwa sara anaona Abrahamu kuwa pia ni sehemu ya tatizo, Abrahamu anamuonyesha sara kwamba hajiri bado ni mtumwa wake ni mjakazi wake anaweza kumfanya anachokitaka, sasa sara anamtesa Hajiri, huku Ibarahimu akiwa ameridhia kuteseka kwa Hajiri, mwanamke huyu mnyonge, na masikini sasa hana namna kibano kimezidi kuwa kikali sana na sasa anakimbia jangwani, Ni safari ngumu, ni safari ndefu, bila shaka alikuwa akijaribu kurejea kwao Misri lakini bila msaada wa wowote, hakuna anayejali wala hakuna anayetaka kubeba lawama kila mtu amechoka. Ni mwanamke mjamzito, anataka kiujaribu kurudi kwao, kupitia Jangwani, hana msaada kuna wanyama wakali, kilichoko kwenye kichwa chake “NI HERI KUFA KULIKO MATESO NINAYOYAPITIA KWA SARA” Biblia haijaeleza kuwa sara alimfanya nini lakini mwanatheolojia mmoja ametumia neno la Kiingereza “Sarai attacked Hagar with disproportionate cruelty,” Neno hilo “DIS-PRO-POR-TIONATE” maana yake ukatili usiopimika, na maneno mengine ya kiingereza “Harshly, Cruel, severe, Mistreated   ni aibu kwa mwanamke bosi kama Sara kuwa na ukatili wa aina ile ni aibu, japo haikuwa vema pia kwa Hajiri kuwa asiyetii, lakini hali hizi zote ziliweza kufikisha katika hatua hii, wako watu duniani wanajua kutesa, wako watu duniani wanajua kunyanyasa mpaka inapofikia hatua ya mtu kuchagua kujiua kuliko mateso unayoyapata, Mungu sio mjinga, Mungu sio kipofu, Mungu sio Mungu asiyejali, Mungu sio Mungu wa Upendeleo, Mungu ni Mungu aonaye, Hajiri anakuwa ni Mwanamke wa kwanza Duniani kumuona malaika wa Bwana, Hajiri anajulikana Mbinguni, Mungu anamtaja kwa jina lake… Munguanamjua anakotoka na anakokwenda Hajiri ni mwanamke wa Kwanza  kumpa Mungu Jina “YEHOVAH ROHI” alishuhudia kuwa Mungu alimuona.

Mungu ataingilia kati hali unayoipitia.
Mwanzo 16:7-13Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako. Naye atakuwa kama punda-mwitu kati ya watu, mkono wake utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu wote utakuwa juu yake, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote. Akaliita jina la BWANA aliyesema naye, Wewe U Mungu uonaye, kwani alisema, Hata hapa nimemwona yeye anionaye”

Unaweza kuona tayari hali ya Hajiri ilishaanza kuwa mashakani, ashukuriwe Mungu alikuwa amekwama kwenye kisima cha maji jangwani, kwa vyovyote vile hapo alipumzika kama angeendelea mbele hali ya hatari ilikuwa ikimkabili, Jangwa la shuri ni jangwa pan asana unapoliangalia huwezi kuna mwisho waka ukigeuka huwezi kuona utokako hii ilikuwa ni muelekeo wa kuangamia sasa kwa mwanamke kijana tena mwenye mimba alihitaji msaada na sasa Bwana mwenyewe anamtokea angalia maneno ha malaika wa Bwana:-

-          Wewe Hajiri Mjakazi wa Sarai
-          Unatoka wapi nawe unakwenda wapi
-          Rudi kwa bibi yako ukanyenyekee chini ya mikono yake
-          Nitauzidisha uzao wako wala hautahesabika kwa jinsi utakavyouwa mwingi
-          Utazaa mtoto wa kiume nawe utamwita Ishamel maana Bwana amesikia kilio cha Mateso yako
-          Atakuwa kama punda mwitu, atakaa mbele ya ndugu zake wote
-          Mkono wake utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu wote utakuwa juu yake.

Malaikia wa bwana alionyesha kuwa anamjua Hajiri vizuri sana kwa jina lake na kwa kazi yake, Malaika wa bwana alitaka kupima unyenyekevu ndani ya hajiri kwamba anajisikiaje kuitwa Mjakazi wa Sarai, Swali unatoka wapi na unakwenda wapi lilikuwa lina kusudi la kumrejesha Hajiri,katika toba na kuacha kiburi, kisha kurudi panapopaswa na kuwa Mnyenyekevu , kwa sababu kwa mila na tamaduni alikuwa na mtoto wa watu hao tumboni, na hivyo alipaswa kumrejesha, alimuakikishia kuwa uzao wake utakuwa mwingi, maneno haya huenda yalikuwa ni maneno aliyozoea kuyasikia katika familia ya Ibrahimu kuhusu ahadi za Mungu, ni wazi maneno hayo na ahadi hizo zilimfanya hajiri awe na utambuzi kuwa huyu hakuwa malaika wa bwana tu bali alikuwa ni Mungu mwenyewe alikuwa na ujuzi kuwa Mungu anaona, ujuzi huu una umuhimu mkubwa kwetu, Mungu mwenye kuhusika na mahitaji ya wanadamu anaona na anajua kila kitu na kila njia na aina ya mateso tunayoyapitia.

Hakuna mtu mwenye hati miliki ya Mungu, Mungu sii wa Ibrahimu na Sara tu, wala Mungu si wa matajiri peke yao, Mungu ni wa kila mtu, anajali na anamuhurumia kila mtu bila kujali kabila wala rangi yake, inapofikia ngazi ya kukata tamaa yuko Mungu anayesikia na kuona mateso yetu, yuko Mungu anayejua sida na mateso na changamoto unazozipitia, yeye atahusika na maisha yako, hana dini wala ukabila hana upendeleo, kila mtu anayemwendea na kuliitia jina lake anasikiwa, anaweza kumuongeza na kumzidisha awaye yote, hakuna mtu maalumu kwa Mungu, Mungu ni wa watu wote, Mungu anataka kumponya na kumganga na kumuhudumia kila mmoja wetu, Unaweza kuteswa, kunyanyaswa, kuonewa na kufanyiwa mabaya lakini liko Jicho lenye nguvu linalochungulia ulimwenguni na kuitafuta haki ili kuona ikitendeka na kama haitendeki, huingilia kati na kutokezea njia yeye ni Mungu aonaye

Kutoka 3:7-9BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.

Mungu aonaye Jehovah Rohi macho yake yako kila mahali hawezi kuvumilia kuona unateseka mpaka unalia na kuugua au kuchagua kufa kuliko kuishi, wakati mateso yako yanapozidi kupita uwezo wako, wakati mateso yako yanapokaribia kukutupa nje, unapokata tamaa ya kuishi kumbuka kuwa Mungu kupitia mwanaye Yesu ambaye ni Mwokozi atakutetea atashuka na kuingilia kati na kukurejesha kwenye furaha yako nawe utasimulia matendo yake makuu nimemuona yeye aonaye.
Na. Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima.

Alhamisi, 21 Machi 2019

Mtu atakayelitengeneza boma !



Ezekiel 22:30-31.Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu. Kwa sababu hiyo nimemwaga ghadhabu yangu juu yao; nimewateketeza kwa moto wa hasira yangu; nami nimeileta njia yao wenyewe juu ya vichwa vyao, asema Bwana MUNGU.”




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu katika mpango wake wa ukombozi, hapendi kufanya mambo duniani bila kuwahusisha wenyeji wa dunia, Mungu huwa anatafuta mtu ili aweze kumtumia katika kuujenga ufalme wake, inapotokea kuwa Familia, ukoo, jamii au hata taifa limemtenda Mungu dhambi ni wajibu wa Mungu, kuikemea, kuonya na hata kuhukumu wale waliofanya uovu, hata hivyo Kabla ya Mungu kuhukumu pia huwa anatafuta mtu, ili yamkini aweze kumtumia mtu huyo kutoa Maonyo ili kwamba kama watu watatubu aweze kuwasamehe, hii ni kwa sababu yeye pia ni mwingi wa huruma na neema.

Ezekiel 22:30-31.Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu. Kwa sababu hiyo nimemwaga ghadhabu yangu juu yao; nimewateketeza kwa moto wa hasira yangu; nami nimeileta njia yao wenyewe juu ya vichwa vyao, asema Bwana MUNGU.”

Katika kifungu hiki ambacho tunachukua Muda kujifunza leo, Tunaona Mungu akimueleza Mtumishi wake Ezekiel sababu za kuhukumiwa kwa utawala ya Yuda, na kufikia hatua ya Mungu kuliharibu taifa na hata kuruhusu vita na wao kuchukuliwa Mateka ni kwamba taifa lilipoteza watu wenye haki na waombezi, na waonyaji na wale waliokuwa na ushawishi wa kumuomba Mungu kwaajili ya watu hata Mungu akasikia.

A.     Hali ya taifa zima ilikuwa ni hali ya dhambi na watu walikuwa wameharibika

1.      Viongozi wa serikali walikuwa wameharibika sana
a.      Walifanya ufisadi na kupokea rushwa
b.      Makunani nao walikuwa wamejiingiza katika anasa za dunia na kuacha utumishi wao
c.       Watu wengi wa Mungu walijishughulisha na utafutaji mali, wakitafuta mali za ulimwengu
d.      Maswala ya ibada yalionekana kuwa ni ushamba, na kupoteza muda
e.      Walilitafasiri neno la Mungu kwa kusudi la kupata hekina na sio kuliamini
f.        Manabii wengi walikuwa hawakemei uovu bali waliwatabiria watu amani amani
g.      Walitabiri ushindi hata pale ambapo watu walikuwa wameshindwa vibaya kiroho
h.      Walitabiri amani wakati Mungu alikuwa amekusudia vita na hukumu
i.        Waliwatabiria watu kuwa na mali wakati Mungu alikusudia wawe mateka
j.        Watu walikosa Muongozo wa kiroho na walikuwa waliangukia katika 

B.      Mungu alikuwa anatafuta mtu atalayelitengeneza Boma na kusimama mahali palipobomoka

1.      Mungu ni mwingi wa rehema na neema angeweza kuwasamehe endapo angepatikana mtu wa kusimama mahali palipobomoka na kulitegeneza boma Yeremia 15:1Ndipo Bwana akaniambia, Hata wangesimama mbele zangu Musa na Samweli, moyo wangu usingewaelekea watu hawa; watupe, watoke mbele za macho yangu, wakaende zao.Mungu aliwakumbuka watu wenye haki walioweza kudumisha uhusiano wao na Mungu kiasi ambacho Mungu aliweza kuwasikiliza walipofanya maombezi kwaajili ya taifa na Mungu akasikia dua zao mfano Musa na Samuel, lakini kwa vile hakuona watu wa kiwango hicho aliweza kuwahukumu watu wake.

a.      Mungu hakupata watu au mtu wa kulitengeneza Boma, katika lugha ya kiingeza neno boma linasomeka kama “HEDGE” hii ni aina ya miti au maua magumu yaliyotumika kupandwa shambani au nyumbani kwa kusudi la kuweka uzio ili kuzuia uvamizi na uharibifu kwa mazao au uvamizi nyumbani au katika makazi yaliyokusudiwa kulindwa.

b.      Watu wanapofanya dhambi uzio huo unakuwa umebomoka katika ulimwengu wa roho na unaweza kuruhusu Hasira za Mungu kupita na kufanya uharibifu kwa hiyo ni lazima awepo MUOMBEZI, mtu atakayelia na kuomboleza kwaajili ya kuwaombea watu rehema kwa Mungu, ni aina hii ya watu ndio Mungu anawatafuta hapa Katika Yuda Mungu hakuwaona hao.

i.    Watu walikuwa busy na ujenzi wa makazi yao
ii.  Watu walikuwa wakijiimarisha kutafuta nguvu za kiuchumi na kujiongezea mapato
iii.Watu walijishughulisha na Mashamba yao, vyote havikuwa vitu vibaya lakini vitakuwa na faida gani kama Mungu ataruhusu Moto na uharibifu wa hukumu yake usambaratishe hayo yote na kwa kweli vilisambaratishwa.
c.       Mungu hakuona mtu na kwa sababu hiyo aliruhusu uharibifu kuiharibu Israel.

Hitimisho.

Ni muhimu kufahamu kuwa wanapokuwepo watu ambao Mungu anawaheshimu kwa kiwango cha Musa watu hao wana ushawishi mkubwa wa kuweza kumuomba Mungu au kumsihi Mungu kubadili maamuzi yake, Mara kadhaa Mungu alikusudia kuwafutilia Mbali wana wa Israel Pale walipomuudhi lakini Musa alisimama kwa nguvu na kumwambia Mungu HAPANA angalia  Zaburi 106:23 “Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa, mteule wake, asingalisimama, Mbele zake kama mahali palipobomoka, Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu.” Mungu anatafuta viongozi wa Kisiasa, viongozi wa dini na watu wacha Mungu watakaodumisha uhusiano wake na yeye na kuleta mapinduzi makubwa ya kijamii, kiroho na mabadiliko makubwa na kusababisha watu wamche Mungu na kumgeukia yeye, watakaoleta uamsho, wakataokomesha ufisadi, na kuifanya taifa kutembea katika uadilifu, Mungu anatafuta waombaji, watu watakaosimama kumshawishi aisamehe Familia, ukoo wako, taasisi yako kijiji chako na wilaya yako mkoa na taifa, wakikosekana watu wenye ushawishi wa iana hii katika Taifa lazima hasira ya Mungu itashuka na hukumu kubwa itafuata, Kama taifa halina viongozi wa kiserikali, waombaji na makuhani na manabii wanachekelea dhuluma ikifanyika, mizani zikivurugwa, haki zikipindishwa taifa lazimalitaanguka tu, Haki huinua taifa bali dhambi ni aibu ya watu wote, Hatuna budi kuhakikisha kuwa tunasimama katika zamu yetu kwa haki na kuliombea taifa.

Ni aibu Mungu kukosa waombaji, Mungu anapokosa waombaji katika jamii anaibomoa jamii hiyo na kuisambaratisha, anakuwa hana namna nyingine zaidi ya kuihukumu, Mungu anatoa wito wa watu kurudi magotini, kuomba kwa siri na kuwa watu wenye kuiombea jamii na taifa, watu wengi waombaji wametoweka Duniani leo na mambo yanakwenda Kombo, Mungu anatafuta mtu atakayesimama mahali palipobomoka na kulitengeneza Boma ili asiharibu Nchi.

*Rev. Innocent Kamote*
*Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima*.