Jumanne, 31 Oktoba 2017

Aonavyo mtu nafsini mwake Ndivyo alivyo!


 Mithali 23:7 aMaana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.”

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu, kwamba Biblia inaonyesha ya kuwa maisha yetu yanaweza kutabiriwa na kila tunachokifikiri au kukiwaza, yale tunayoruhusu yaingie katika mioyo yetu ndiyo yenye nafasi kubwa sana katika kuamua hatima na muelekeo wa maisha yetu, kwa msingi huo kile tunachokisema na kukitenda ni matokeo ya pili ya kile tunachokiwaza, hatuwezi kujificha kuwa sisi ni watu wa namna gani, kwani kusema kwetu na kutenda kwetu kutafunua hatimaye kuwa sisi tukoje, ndio maana ni vigumu sana kumsoma mtu anayenyamaza. Mtu halisi ni vile tunavyofikiri, Biblia inaonyesha udhahiri wa watoto wa Mungu na watoto wa ibilisi kutokana na utendaji waoa au usemaji wao.  1Yohana 3:10Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.

Mkuu wa wajenzi Rev. Innocent Kamote wa pili Kutoka kushoto akiwa na waalimu wa Living Stone, Mwalimu Oscar, Kushoto, Nicolous Luchenja watatu kushoto na Jimmy Molel wanne kutoka kushoto wakiwa katika mazoezi ya Taekondoo. Aonavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo!

Mithali 23:7a “ Maana aonavyo mtu ndivyo alivyo”

Proverbs 23:7a “For as he thinketh in his heart, so he is”

Kwa msingi huo vile tunavyofikiri ndivyo, uhalisia wa utu wetu

I.                    Wewe ni matokeo ya kile unachokifikiri na kwa sababu hiyo ni muhimu kufikiri pia kuhusu nini unakiwaza na kama kina kibali mbele za Mungu Zaburi 19:13-14 Biblia inasema “Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi, Yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, Nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa. Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu”. Kwanini mwandishi wa Zaburi anataka mawazo ya moyo wake yapate kibali mbele za Mungu? Maana yake ni kama anamuomba Mungu amsaidie kuwaza sawasawa, hii ni Muhimu sana vile tunavyowaza ndivyo tunavyoweza kusema na kutenda, kama tutawaza sawasawa tutakuwa tumejizuia, kutenda, kutawaliwa, kusema na kijiepusha na makosa makubwa na uovu.

Yale tunayoyafikiri yana vyanzo, Mtu ili aweze kuwa kama alivyo ni lazima kuweko maswala kadhaa ynayochangia katika kumjenga moja ikiwa ni wakati wa kuzaliwa kwetu, lakinimengine ni vile tunavyopokea kutoka ulimwenguni kutokana na mazingira na milango yetu mitano ya fahamu kwa msingihuo ni muhimu kwetu kujilinda na vyanzo vinavyoingiza taarifa katika nafsi zetu na akili zetu mfano :-

a.       Yale tunayoyasoma?- Tunayoyasoma yanaingia katika akili zetu na kwa hivyo yana mchango mkubwa sana katika kuyajenga maisha yetu na ndio maana biblia inasema tujae nenola Mungu mioyoni mwetu Wakolosai 3:16-17 “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.” 2Timotheo 3:14-17 “14. Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” Maandiko matakatifu yanaweza kutuhekimisha na kutuongoza katika haki, kwa msingi huo yale tunayoyasoma yanaweza kuathiri maisha yetu na hivyo ni muhimu kwa mtu mwema kuhakikisha anaingiza mambo yaliyo mema katika moyo waake “Ubongo”
b.      Yale tunayoyaangalia Ayubu 31:1 “Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana?Ayubu aliweka agano na macho yake kuwa hataangalia mwanamke kwa tamaa yaani kumwangalia kwa nia mbaya, kumbe kuangalia kunaweza kuathiri mitazamo yetu na mfumo wa maisha yetu ni muhimu kwetu pia kujilinda katika yale tunayoyaangalia.
i.                     Kuyaangalia kupitia Internet,jihanadhari angalia vitu vyema
ii.                   Kuyaangalia kupitia Movies, TV, na kadhalika watoto wetu wengi siku hizi wanangalia sana ngumi na uharibifu wa kwenye sinema na hivyo vijana wengi sana wa leo wamekuwa ni waharibifu wakubwa wa vitu na vifaa majumbani na mashuleni
c.       Yale tunayoyatafakari Wafilipi 4:8.” Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Kuna maswala ya kutafakari ambayo biblia inayapendekeza hapa kwenye kutafakari ndipo panapoweza kutusaidia kujenga misimamo yetu iliyo thabiti, ni muhimu kwa kila mmoja kujipima kuwa anatafakari nini.
d.      Yale tunayoyasikia, ukisikia taarifa zisizo sahihi hutakuwa sahihi na ukisikia taarifa sahihi unakuwa sahihi. Hakikisha kuwa unasikiliza mambo ya msingi, Biblia ya Kiswahili inasema Mazungumzo mabaya huaribu tabia njema, kwa maana ya kuwa tunapozungumza pia tunasikia, Biblia ya kiingereza inasema “Bad Company corrupt Good Character”  sawa na kusema marafiki wabaya huaribu tabia njema kwa msingi huo ni muhimu kwetu kuangalia wale wanaotuzunguka kwa vile wanahusika kwa kiwango kikubwa katika kuyajenga maisha yetu
II.                  Mioyo yetu ndio chemichemi ya tabia zetu.
a.       Mti hutambulikana kwa matunda yake Luka 6:43-45Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake”. Unaona kile Yesu anakizungumza hapa ni kama anasema aonavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo! Kumbe kusema kwetu na kutenda kwetu ni matokeo ya asili yetu ya moyoni, tunza saba moyo wako! Kuna athari kubwa sana katika kuwaza kwetu au katika yale tunayoyajaza mioyoni mwetu kwani hatima yeke ni kuyazalia matunda. Kipengele kifuatacho kinasaidia kutujulisha namna tutakavyokua endapo tutaielekeza mioyo yetu katika maswala mhaya:-    
III.                Maisha yako yanafafanuliwa na moyo wako na fikira zako:-
1.       Kama unajifikiri mwenyewe sana utakuwa mbinafsi sana 2Timotheo 3:1-2 “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,”    
2.       Kama utafikiri sana kuhusu wengine utakuwa mkarimu, na mwenye kujali Warumi12:10-13. “Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana; kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu; kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni mkijitahidi.”, Waefeso 4:32
3.       Kama unafikiri sana kuhusu fedha utakuwa mtu mwenye tamaa 1Timotheo 6:9-10 “. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”               
4.       Kama utakuwa mwenye kushukuru sana utakuwa mtu mwenye kuridhika 1Timotheo 6:6-8 “6. Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa.  Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.”
5.       Kama utafikiri sana kuhusu ngono utakuwa  mwenye tamaa au kahaba Mathayo 5: 27-28 “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.”
6.       Kama tutafikiri sana kuhusu uadilifu tutakuwa wenye moyo safi  1Wakoritho 6:18, Mathayo 5:8 “Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.”
7.       Kama utafikiri sana kuhusu kutenda hila utakuwa muongo mkubwa Wakolosai 3:9-10 “Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba.”
8.       Kama utakuwa mwenye kufikiri kuhusu ukweli utakuwa mtu muaminifu Waefeso 4:25 “Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.”
9.       Kama utakuwa mwenye kutaka sifa kutoka kwa watu utakuwa mnafiki Mathayo 6:5,23:12  Mathayo 6:5 “Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao.”
10.   Kama utakuwa mwenye kufikiri sana kuhusu kumuinua Mungu, utakuwa mtumishi wake mkubwa sana 1Petro 2:1-3. “Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;  ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana ni mwenye fadhili.
  
Hitimisho.

Wewe ni mtu wa namna gani, na je Mungu anaona nini kwako? Matendo 1:24, Waebrania 4:13
Ni lazima uamue kuwa mtu wa aina gani kwa kuhakikisha kuwa unawaza vema wakati wote
Kila unachokitafakari na jinis unavyojiona ndani ndivyo unavyoamua maisha yako yawe Mungu alichukizwa na wana wa Israel ambao walijiona nafsi zao kama panzi walipojilinganisha na wakanaani na kusahau ukuu wa Mungu na hivyo Mungu alichukizwa nao Mafanikio yetu na maisha yetu ya kiroho na kimwili yanategemeana sana na namna tunavyojiona ndani na namna tunavyojiona ndani inategemeana sana na yake  tunayoyaingiza katika mioyo yetu, ukijiona duni wewe ni duni, ukijiona shujaa wewe ni shujaa, ukijiona huwezi wewe hutaweza, ukijiona mbaya wewe ni mbaya, ukijiona mwema wewe utakuwa mwema,ukijichukia hakuna mtu atakayekupenda, ukijipenda utapendwa, ukiwa na amani, utazalisha amani ukiwa na uchungu utazalisha uchungu, Aonavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo

Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Rev. Innocent Kamote.

Jumatatu, 23 Oktoba 2017

Kwa bidii si walegevu!



Mstari wa Msingi: Warumi 12:11kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;”

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa kila tunalolifanya duniani Mungu anataka tulifanye kwa bidii, kufanya kazi ya Mungu kwa bidii, kuabudu, kwa bidii, kuomba kwa bidii, kusoma kwa bidii, kufanya kazi za kawaida, kwa bidii Mungu anataka tuwe na bidii, tuwe na Juhudi, katika kila jambo, Haya ni mapenzi ya Mungu kabisa ni kanuni ya mafanikio. Kama mtu anataka kufanikiwa katika kila jambo basi ni muhimu jambo analolifanya likafanyika kwa bidii, Neno la Mungu linaunga mkono utendaji wa kazi kwa bidii na linaeleza faida za kuwa na bidii katika kila jambo.

Kwa kuanzia na Mstari wa msingi 

Warumi 12:11 SUV, Inasema kwa bidii, si walegevu, mkiwa na juhudi
Romans 12:11 NIV, Never be lacking in Zeal, but keep your spiritual fervor
Romans 12:11 KJV, Not slothful in business; fervent in spirit;

Neno hilo Kwa bidii, kwa juhudi katika Biblia ya kiyunani linasomeka kama AGONIZOMAI ambalo kwa kiingereza kuna maneno kadhaa yanaingiliana kuhusu neno hilo

Kwa ujumla maneno hayo yote yanakazia kufanya kazi kwa bidii, kufanya kazi kwa juhudi,kwa wivu, kwa moto, kwa muwako, kwa shauku, kwa viwango, kwa ufundi na kwa njia nyingine zozote lakini hakuna lugha ya kueleza vema katika Kiswahili zaidi ya kukazia bidii na juhudi, au kwa moyo wako wote.

Mfano Biblia inazungumza kumpenda Mungu kwa Moyo wetu wote

1.      Kumbukumbu 6:5Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.” Kwa maana nyingine Biblia inataka tumpende Mungu kwa moyo, kwa roho na kwa nguvu hii maana yake nini kwa bidii

2.      Yakobo 5:16Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.”Kumbe hata katika kuomba Biblia inatutaka tuombe kwa bidii unaona 

3.      Matendo 12:5Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake.” Maombi yaliyomtoa Petro gerezani yalikuwa ni maombi yaliyofanyika kwa juhudi

4.      Matendo 18:24-25Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu.” Apolo alikuwa hodari yaani alikuwa na juhudi na hata alipoanza kuhubiri alikuwa na “zeal” yaani alikuwa anawakwa anahubiri kuhusu Yesu kwa nguvu.

5.      Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”Biblia inatutia Moyo vilevile ikitakam bidii katika kuwa na amani na watu wote, kumbe kila kitu kinahitaji bidii

6.      Mithali 8:17Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.” Biblia inatia moyo kwamba tumtafute Mungu kwa bidii, bidii inahitajika katika kila eneo

Kwa msingi huo basi kama kila kitu kitafanyika kwa bidii maana yake mafanikio ni lazima, ni lazima kila mwanafunzi ajifunze kusoma kwa bidii, wanaofanya kazi wafanye kwa bidii, “USITAMANI KUTEMBEA IKIWA UNAUWEZO WA KURUKA” “do not desire to walk when you have wings to fly”

Mfano:

Wakati fulani kulikuwa na Mfalme aliyekuwa mkarimu sana na mwenye moyo Mzuri, lakini pia alikuwa rafiki wa wanyama na ndege, aliwapenda kiasi ambacho hakufurahi hata kuona mnyama akichinjwa

Kutokana na ukarimu wake kwa wanyama na ndege siku moja mfanya biashara mmoja alimpatia  zawadi ya mwewe  wawili “Falcon” Mfalme alifurahi sana na kumuomba kiongozi wa wa mifugo kuwatunza mwewe hao wawili na kuhakikisha kuwa wanaishi kwa fuaha na faraja lakini wakiwa na uwezo na mpaka wawe na uwezo wa kuruka, kwani walikuwa hawawezi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na wakati wa ukamatwaji walipunguzwa baadhi ya manyoya ili wasiruke



Baada ya Muda Mfalme alitamani kuwaona mwewe wale wakiruka, lakini kiongozi wa mifugo alimueleza kuwa ni mwewe mmoja tu ndiye aliyeweza kuruka kwa kasi na huwa anarejea kwa kasi ya ajabu lakini mwingine hajawahi kuruka hata siku moja,

Mfalme alishangaa sana na alitoa zawadi kwa mtunzaji wa mifugo kutokana na kuruka kwa mwewe wa kwanza, hata hivyo alisisitiza kuwa ni lazima ahakikishe kuwa na mwewe wa pili anaruka. Lakini hata hivyo mwewe wa pili hakuweza kuruka bali alikaa tu kwa upole katika tawi la mti na kutulia alijaribu kila mbinu lakini ndege yule hakuweza kuruka.
Mfalme alimwambia usisikitike nitaita mtu mmoja atakayeweza kumfanya mwewe aweze kuruka mfalme alitangaza kama yuko mtu anayeweza kumfanya mwewe yule aweze kuruka ajitokeze na atapewa zawadi


Baada ya kusikia tangazo hilo Mzee mmoja wa miaka alijitokeza na kufika ikulu na kumuhakikishia mfalme kuwa yeye anaweza kumfanya mwewe kuruka, Mfalm,e alimuagiza mkuu wa wanyama kumchukua Mzee yule na kumpeleka kwenye eneo la mifugo na ndege na kuifanya hiyo kazi na kuwa yeye atatembelea siku inayofuata kuona itakavyokua na kama kuna mabadiliko.

Siku ya pili Mfalme alishangaa sana kuona kweli mwewe ameruka kwa mara ya kwanza  na akaenda mbali sana kwa spidi ya ajabu na kurejea, Mfalme alifurahi sana na kumpa zawadi mzee yule, kisha akamuuliza Mzee umewezaje kumfanya ndege huyu kuruka Mzee alicheka na kujibu Nilikata tawi alilokuwa analitegemea kwa kukaa.

Wengi wetu tuna mbawa za kurukia, tunajua kuruka na tunajua wapi kwa kurukia lakini tumekaa bila sababu na hatufanyi lolote na tunabakia duni.

Kila mmoja anaweza kufanya jambo kwa bidii, kila mwanafunzi anaweza kujisomea kwa bidii watu wengi na wanafunzi wengi wanao uwezo, wanauwezo wa kupata hata maxi kubwa zaidi ya hizi wanazozipata lakini kuna mahali wamekaa, 

Mithali 10: 4Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.” Ndugu hakuna muujiza wa mafanikio unaokuja kwa kuambiwa pokea! Pokea! Mafanikio yoyote yanakuja kwa kufanya kazi kwa bidii, Yeye aliye na sikio na asikie neno hili ambalo mkuu wa wajenzi anawaambia wasomaji wake.

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Jumamosi, 21 Oktoba 2017

Madhabahu Iliyoleta Utata!


Yoshua 22: 9-10.
Basi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase wakarudi, wakatoka kwa wana wa Israeli katika Shilo, ulioko nchi ya Kanaani, ili waende nchi ya Gileadi, hiyo nchi ya milki yao, waliyokuwa wanaimiliki, sawasawa na amri ya Bwana kwa mkono wa Musa. Nao walipofika pande za Yordani, zilizo katika nchi ya Kanaani, hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na nusu ya kabila ya Manase, wakajenga madhabahu huko karibu na Yordani, iliyoonekana kuwa ni madhabahu kubwa.”

Utangulizi. 

Mara baada ya kuingia katika nchi ya kanaani wakati wa Yoshua Wana wa Israel yaani walioishi ng’ambo ya Yordan ambao ni kabila la Wareuben, Gadi na Nusu ya Manase, walimjengea Bwana Madhabahu kubwa sana ambayo ilileta utata na kutaka kusababisha vita ya wenyewe kwa wenyewe, Mungu alipompa Musa sheria alieleza wazi kuwa watu wasijenge madhabahu isipokuwa ile iliyoamriwa.
 
Kumbukumbu 12:1-14 “Hizi ndizo amri na hukumu mtakazotunza kuzifanya katika nchi aliyokupa Bwana, Mungu wa baba zako, uimiliki, siku zote mtakazoishi juu ya nchi. Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo. Wala msimfanyie hivyo Bwana, Mungu wenu. Lakini mahali atakapochagua Bwana, Mungu wenu, katika kabila zenu zote, apaweke jina lake, maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe wende huko; pelekeni huko sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng'ombe na ya kondoo; na huko mtakula mbele za Bwana, Mungu wenu, nanyi furahini katika yote mtakayotia mikono yenu, ninyi na wa nyumbani mwenu, aliyokubarikia Bwana, Mungu wako. Msifanye kwa kufuata mambo yote tuyafanyayo hapa leo, kila mtu kama aonavyo vema machoni pake; kwani hamjafikilia bado katika raha na urithi akupao Bwana, Mungu wako. Lakini mtakapovuka Yordani na kukaa katika nchi anayowarithisha Bwana, Mungu wenu, akawapeni raha, akiwaokoa na adui zenu pande zote, mkakaa salama; wakati huo itakuwa kwamba mahali pale atakapopachagua Bwana, Mungu wenu, alikalishe jina lake, hapo ndipo mtakapoleta kila kitu ninachowaamuru; sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu zote teule mtakazoweka kwa Bwana. Nanyi mtafurahi mbele za Bwana, Mungu wenu, ninyi, na wana wenu, na binti zenu, na watumishi wenu wanawaume na wanawake, na Mlawi aliyemo malangoni mwenu; kwa kuwa hana sehemu wala urithi kwenu. Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo; bali katika mahali atakapopachagua Bwana katika kabila zako mojawapo, ndipo utakapotoa sadaka zako za kuteketezwa, ndipo utakapotenda yote nikuamuruyo.

Kutokana na mtazamo huo wana wa Israel walitambua kuwa ndugu zao wamekiuka agizo la Mungu, kwa kujenga madhabahu iliyoleta utata na hivyo walipaswa kupigwa na kufutiliwa mbali , wazo la kuwapiga na kuwafutilia mbali  lilikuwa sawa na agizo la Torati.

Kumbukumbu 13:12-16 “Ukisikia yasemwa habari ya miji yako mmojawapo, akupayo Bwana, Mungu wako, ukae humo, ukiambiwa, Kumetoka katikati yako mabaradhuli kadha wa kadha, wamewapotoa wenyeji wa mji wao, wakisema, Twendeni tukaabudu miungu mingine msiyoijua; ndipo nawe uulize na kutafuta, ukiuliza kwa bidii; nawe angalia, ikiwa kweli, na jambo lile halina shaka, kwamba machukizo mfano wa haya yafanyika katikati yako; hakika yako uwapige wenyeji wa mji ule kwa makali ya upanga, kwa kuwaangamiza kabisa, pamoja na vitu vyote vilivyomo, na wanyama walio humo, kwa makali ya upanga. Na nyara zake zote uzikusanyie katikati ya njia yake; na mji uuteketeze kwa moto, na nyara zake zote, kuwe sadaka kamili ya kuteketezwa kwa Bwana, Mungu wako; nao utakuwa magofu milele; usijengwe tena.” 

Israel na uongozi wa Magharibi ulikuwa umezingatia maagizo haya ya Mungu, wao walikuwa wametafasiri kuwa ndugu zao wamekusudia kuabudu miungu mingine na kuwa wamekiuka agizo la Mungu kupitia torati ya Musa, lakini jambo lililokuwa jema zaidi ni kwamba walitaka kufanya uchunguzi ili kujiridhisha kabla ya kuingia vitani, Kabila la Warubeni na Gadi na Manase, walifafanua matumizi ya madhabahu hiyo kuwa ulikuwa ni ukumbusho kwa Bwana Mungu wao, wao walikuwa wametenganishwa na mto kijiografia , Lakini walitaka kuonyesha muungano wao wa kiroho, Madhabahu yao ilikuwa ni Ishara ya umoja na sio uasi, wao walikuwa na nia ya kutunza maisha ya kiroho ya watoto wao Yoshua 22:12-29 “Basi, wana wa Israeli waliposikia habari hiyo, mkutano wote wa wana wa Israeli wakakutanika pamoja huko Shilo, ili waende kupigana nao. Kisha wana wa Israeli wakatuma wajumbe waende kwa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, hata nchi ya Gileadi; nao ni hawa, Finehasi mwana wa Eleazari kuhani; na pamoja naye wakuu kumi, mkuu mmoja wa nyumba ya mababa kwa ajili ya kila kabila ya Israeli; nao kila mmoja alikuwa ni kichwa cha nyumba ya mababa katika maelfu ya Israeli.  Nao wakawafikilia hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, katika nchi ya Gileadi, na wakasema nao, wakinena, Mkutano wote wa Bwana wanena, Ni kosa gani hili mlilolikosa juu ya Mungu wa Israeli, hata mkakengeuka hivi leo na kuacha kumwandama Bwana, katika kujijengea madhabahu, na kuasi hivi leo juu ya Bwana? Je! Ule uovu wa Peori haututoshi, ambao hamjajitakasa nafsi zenu katika huo hata hivi leo, ijapokuwa ilikuja tauni juu ya mkutano wa Bwana, hata ikawa hamna budi hivi leo kugeuka na kuacha kumwandama Bwana? Kisha itakuwa, kwa kuwa ninyi mwamwasi Bwana hivi leo, kwamba kesho yeye atakasirika na mkutano wote wa Israeli. Basi kwamba hiyo nchi ya milki yenu si tohara, ndipo ninyi vukeni na kuingia nchi ya milki yake Bwana, ambayo maskani ya Bwana inakaa ndani yake, nanyi twaeni milki kati yetu; lakini msimwasi Bwana, wala msituasi sisi, kwa kujijengea madhabahu zaidi ya hiyo madhabahu ya Bwana, Mungu wetu. Je! Huyo Akani mwana wa Zera hakukosa katika vile vitu vilivyowekwa wakfu, na hasira ikauangukia mkutano wote wa Israeli? Kisha mtu huyo hakuangamia peke yake katika uovu wake? Ndipo hapo wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wakajibu, na kuwaambia hao waliokuwa ni vichwa vya maelfu ya Israeli, wakasema,  Mungu, Mungu Bwana, naam, Mungu, Mungu Bwana, yeye yuajua, na Israeli naye atajua; kama ni katika uasi, au kama ni katika kosa juu ya Bwana, (usituokoe hivi leo); sisi kujijengea madhabahu ili kukengeuka na kuacha kumwandama Bwana; au kama ni kusongeza juu yake sadaka ya kuteketezwa, au sadaka ya unga, au kama ni kusongeza sadaka za amani juu yake, yeye Bwana mwenyewe na alitake jambo hili; au kama sisi tumefanya jambo hili kwa hadhari sana, tena makusudi, huku tukisema, Katika siku zijazo wana wenu yamkini wakanena na wana wetu, na kusema, Ninyi mna nini na Bwana, yeye Mungu wa Israeli? Kwa kuwa yeye Bwana ameufanya huu mto wa Yordani uwe mpaka katikati ya sisi na ninyi, enyi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, hamna fungu katika Bwana; basi hivyo wana wenu wangewakomesha wana wetu wasimche Bwana. Kwa ajili ya hayo tulisema, Na tufanye tayari ili kujijengea madhabahu, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, wala kwa sadaka yo yote; bali itakuwa ni ushahidi kati ya sisi na ninyi, tena kati ya vizazi vyetu baada yetu, ili kwamba tufanye huo utumishi wa Bwana mbele yake kwa njia ya sadaka zetu za kuteketezwa, na kwa dhabihu zetu, na kwa sadaka zetu za amani; ili kwamba wana wenu wasiwaambie wana wetu katika zamani zijazo, Ninyi hamna fungu katika Bwana. Kwa hiyo tulisema, Itakuwa, hapo watakapotuambia neno kama hilo, au kuwaambia watu wa vizazi vyetu katika zamani zijazo neno kama hilo, ndipo sisi tutawaambia, Angalieni huu mfano wa madhabahu ya Bwana, walioufanya baba zetu, si kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, wala kwa ajili ya dhabihu; lakini ni ushahidi kati ya sisi na ninyi. Mungu na atuzuie msimwasi Bwana, na kukengeuka hivi leo na kuacha kumwandama Bwana, hata mkajenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, au sadaka za unga, au dhabihu, mbali na ile madhabahu ya Bwana, Mungu wetu, iliyo huko mbele ya maskani yake”. 

Walipogundua hilo,Kuhani mkuu Finehasi na makuhani na wazee waliwaambia Reuben na Gadi na Manase  walipata amani Yoshua 22:30-34 “Basi Finehasi kuhani, na wakuu wa mkutano, maana, ni hao waliokuwa vichwa vya maelfu ya Israeli waliokuwa pamoja naye, hapo walipoyasikia hayo maneno waliyoyasema hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, maneno hayo yaliwaridhia sana. Naye Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, akawaambia wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, akasema, Siku hii ya leo twajua ya kwamba Bwana yu kati yetu, kwa sababu hamkukosa katika jambo hili mbele ya Bwana; sasa ninyi mmewaokoa wana wa Israeli na mkono wa Bwana. Kisha Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, na hao wakuu, wakarudi na kuwaacha wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakatoka katika nchi ya Gileadi, na kuingia nchi ya Kanaani; wakawarudia wana wa Israeli, wakawapa habari. Wana wa Israeli nao wakaliridhia jambo hilo; nao wana wa Israeli wakamhimidi Mungu, wala hawakusema tena habari ya kuwaendea juu yao kupigana nao, wala kuiharibu nchi waliyoikaa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi. Basi hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakaiita madhabahu hiyo Edi; wakasema, Kwa kuwa ni ushahidi kati yetu ya kwamba yeye Bwana ndiye Mungu”.   
            
Mgogoro ulimalizika, tukio hili linatufunza kuwa Hatupaswi kuhukumu kwa haraka na kufikia katika hatima ya jambo kabla kwanza ya kusikiliza, Nikodemo alimtetea Yesu kwamba sheria yetu haimuhukumu mtu kwanza kabla ya kumsikiliza na kuangalia kile anachokifanya Yohana 7:51, “Je! Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo?”  Mithali 18:13. “Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake.”

Mara nyingi tumewahukumu watu kutokana na mitazamo iliyoko ndani yetu tu na hatujawapa Muda wa kuwasikiliza, hatuwezi kufikia suluhu ya jambo lolote kwa kudhani kuwa mawaazo yetu ni sahihi tu wakati wote, ni lazima tuwasikilize na wengine

Wakati wote unapofanya mambo makubwa na ya kushangaza, lazima watakuweko watu watakaotafasiri tofauti lolote ulifanyalo, Hakikisha unaweka alama kubwa katika maisha yako, unaacha wasifu mkubwa katika maisha yako, unapata maxi kubwa katika masomo yako, unafanya makubwa katika kila eneo, ukijenga kanisa jenga kanisa kubwa, ukiombea watu fanya miujiza mikubwa, ukiomba mamombi toa maombi makubwa, ukitoa sadaka toa sadaka kubwa, ukiwa na uhusiano na mungu uwe na uhusiano mkubwa, fanya kila kitu kikubwa utashangaza watu hata watu wa Mungu watakushangaa.

 Wana wa Reuben na Gadi na Manase walijenga madhabahu kubwa, kila mtu ni lazima adhamirie kufanya mambo makubwa na mara zote unapokusudia kutenda mambo makubwa watu watachanganyikiwa,  watatoa maneno ya kipuuzi, bila kuchunguza kuwa nini kinachofanyika

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote