Jumatatu, 31 Januari 2022

Haki huinua Taifa !


Mithali 14:34 “Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa maandiko yanatupa siri ya mafanikio makubwa sana katika maisha yetu ya kila siku na maisha ya kila mtu na maisha ya taifa lolote lile kwamba; Ili tuweze kuwa na ustawi tunapaswa kuwa watu wa haki, Mungu hawezi kumvumilia mtu au taifa lolote ikiwa watu wa taifa hilo wataacha na uadilifu na kumkataa Mungu, siri ya nguvu na mafanikio ya mtu watu jamii na taifa lolote iko katika kutenda uadilifu na kuyaishi mapenzi ya Mungu na wala sio nguvu za kijeshi na uchumi, siri ya mafanikio ya kweli iko kwenye uadilifu na kutenda haki, Taifa lolote likiandaa mipango na mikakati ya kiadilifu na ya kumcha Mungu na kumuheshimu na kukaa katika uadilifu kila kitu kitafanikiwa kwa mujibu wa maandiko Mithali 14:34 Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.” Tutajifunza somo hili Haki huinua taifa kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:- 

1.       Maana ya Taifa

2.       Jinsi haki inavyoinua taifa na Dhambi inavyoleta aibu

3.       Haki huinua taifa 

Maana ya Taifa

Ni muhimu kufahamu kuwa katika maandiko lugha inayotumika kumaanisha taifa inatumika katika maana pana sana unapoangalia maana ya Taifa kwa kiingereza yaani Nation maana yake katika Dictionary inasomeka hivi National means People who possess a common kinship, a social or political group and simply a people, kwa kiyunani ni Ethnos au Ethinic, ni jamii au watu wanaotokana na mtu, au kabila au dini au lugha na kadhalika, Kwa mfano watu wanaweza kuzaliwa na baba mmoja na mama mmoja au hata wakawa mapacha lakini katika jicho la kiungu hao wanaweza kuwa mataifa mawili tofauti na kabila mbili tofauti unaona!

Mwanzo 25:21-23 Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yamo tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo.”      

Unaona na pia unaweza kuiona lugha ya aina hii ikitumiwa na Yesu katika Mathayo 24:6-7 “Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali.”  

Kwa msingi huo sasa Taifa linaweza kuwa ni jamii ya watu wanaotokana na mtu mmoja mmoja, taifa ni watu wa karibu sana wakati ufalme na ufalme inaweza kuwa ni mipaka ya kiserikali, kwa hiyo Mungu yu aweza kumuona au kumuita mtu mmoja na mtu huyo akamfanya kuwa taifa, yaani kama wewe ni mtenda haki na unampendeza Mungu wewe ni asili ya taifa Mungu yu aweza kukufanya wewe kuwa taifa kubwa ona

Mwanzo 12:1-3 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”

Kwa msingi huo tunapozungumzia taifa tunamzungumzia mtu mmoja mmoja, na jamii au kabila au kundi la watu wa aina filani walio karibu sana hilo ndio taifa, na ufalme ni jamii ya watu wanaopakana kiserikali, kwa hiyo kila mmoja anapaswa kuwa mtenda haki na kuishi maisha ya kumcha Mungu kwa sababu Mungu hashindwi kukufanya wewe kuwa taifa kwa sababu taifa linaanzia na mtu mmoja kama Mungu akipendezwa nawe anaweza kukufanya kuwa taifa na kama Mungu akichukizwa nawe anaweza kukufuta ona

Kutoka 32:7-14BWANA akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Tena BWANA akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. Musa akamsihi sana BWANA, Mungu wake, na kusema, BWANA, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele. Na BWANA akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wakeunaweza kuona kwa msingi huo sasa swala la kutenda haki au kwa lugha nyingine nyepesi kutembea katika mapenzi ya Mungu halianzi na mtu Fulani tu linaanza na wewe na mimi

Jinsi haki inavyoinua taifa na Dhambi inavyoleta aibu

Maandiko sasa yanatuonyesha kupitia wana wa Israel na maisha yao kwamba pale watu walipotenda haki na walipotembea katika njia za Mungu, Mungu aliwafanya kuwa imara na pale watu walipoziacha njia za Mungu, na kuyaacha mapenzi yake  Mungu aliwaacha waanguke katika mikono ya adui zao na kunyanyaswa vibaya  ona kwa mfano

Waamuzi 2:11-23 Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakawatumikia Mabaali.Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika. Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na Maashtorethi. Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao. Kila walikokwenda mkono wa Bwana ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama Bwana alivyosema, na kama Bwana alivyowaapia; nao wakafadhaika sana. Kisha Bwana akawainua waamuzi, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara. Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za Bwana bali wao hawakufanya hivyo. Na wakati Bwana alipowainulia waamuzi, ndipo Bwana alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana Bwana alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua. Lakini ikawa, wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine ili kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi. Basi hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu; mimi nami tokea sasa sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa; ili kwa njia ya hayo nipate kuwajaribu Israeli, kwamba wataishika njia ya Bwana kwenda katika njia hiyo, au sivyo. Basi Bwana akawaacha mataifa yale, wala hakuwafukuza kwa upesi, wala hakuwatia katika mikono ya Yoshua.”

Unaweza kuona kwamba pale watu wa Mungu walipoziacha njia za Mungu na kuishi kwa dhuluma na  wakajifanyia kila wanachokiona kuwa chema katika macho yao  Mungu aliwadhibu vikali sana na kuwaacha katika mikono ya adui zao ili washughulikiwe na wakati mwingine aliruhusu wachukuliwe mateka na kwenda utumwani  na sio hivyo tu akliwaacha wadhalilike na kufedheheka nah ii ndio aibu kubwa iliyokuwa inawapata pale wanapoacha njia za Mungu ambayo ndio haki ya Mungu.

2Wafalme 17:6-12 “Katika mwaka wa kenda wa Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi. Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya Bwana, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine. Wakaziendea sheria za mataifa, ambao Bwana aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya. Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo yasiyokuwa mema juu ya Bwana, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma. Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; wakafukiza uvumba huko katika kila mahali pa juu, kama mataifa walivyofanya, ambao Bwana aliwafukuza mbele yao; wakaunda mambo mabaya, ili wamkasirishe Bwana; wakatumikia sanamu, ambazo Bwana aliwakataza, akasema, Msitende jambo hili.”

Pale Israel walipotubu na kucha dhambi zao na kutembea katika mapenzi ya Mungu Mungu aliwasaidia aliwapa Mwokozi, alileta ukombozi na kuwapa amani na kuondoa masumbufu yote

 Waamuzi 3:9-11 “Kisha wana wa Israeli walipomlingana Bwana, Bwana akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu. Roho ya Bwana ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye Bwana akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini. Kisha Othnieli, mwana wa Kenazi, akafa.” Unaweza kuona hii ndio kanuni ya Mungu, Mungu hawezi kukuinua na kukutumia katika hali ya uovu, hatunabudi kutubu, kujinyenyekesha mbele za Mungu na kumlingana Mungu yaani kutembea katika njia zake tukifanya hivyo hatutaingia katika aibu na fedhea ya aina yoyote ile na Mungu atakuwa pamoja nasi na tutakuwa na uhakika wa ulinzi wa kudumu wala Bwana hatatuuza tuumizwe na adui zetu

Haki huinua taifa

Mithali 14:15-34 “Mjinga huamini kila neno; Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo. Mwenye hekima huogopa, akajitenga na uovu; Bali mpumbavu ana ufidhuli, na kujitumai. Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga; Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa. Wajinga hurithi upumbavu; Bali wenye busara huvikwa taji ya maarifa. Wabaya huinama mbele ya wema, Na wasio haki malangoni mwao wenye haki. Maskini huchukiwa hata na jirani yake; Bali tajiri ana rafiki wengi. Amdharauye mwenzake afanya dhambi; Bali amhurumiaye maskini ana heri. Je! Hawakosi wawazao mabaya? Bali fadhili na kweli zina wao wawazao mema. Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu. Taji ya wenye hekima ni mali zao; Bali upumbavu wa wajinga ni upumbavu tu. Shahidi wa kweli huponya nafsi za watu; Bali atoaye uongo hudanganya. Kumcha Bwana ni tumaini imara; Watoto wake watakuwa na kimbilio. Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti. Utukufu wa mfalme ni wingi wa watu wake; Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao. Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi; Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu. Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili; Bali husuda ni ubovu wa mifupa. Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake; Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu. Mtu mbaya husukumwa chini katika kutenda mabaya kwake; Bali mwenye haki ana matumaini katika kufa kwake. Hekima hukaa katika moyo wake mwenye ufahamu; Bali yaliyo ndani ya wapumbavu hudhihirika. Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.”

Suleimani katika kitabu cha Mithali anaonyesha wazi namna mtu mwenye haki anavyoweza kufanikiwa na namna watu waovu wanavyoweza kujikuta katika mashaka kinachosisitizwa katika maandiko hapa ni kwamba wale wanaomkataa Mungu na kuacha kutenda haki na kuendelea na uovu wanafanya ujinga ambao utawaharibia maisha na wale wanaomkubali Mungu na njia zake wanajipatia hekima na maarifa  na kujitengenezea ulinzi wa uhakika , kwa msingi huo neno la Mungu linapozungumza kuhusu taifa linatuzungumzia wewe na mimi na baadaye jamii yetu na jamii ya dunia kwa ujumla lakini kanuni hii inaanza kufanya kazi kwa mtu mmoja mmoja

Mithali 3:5 -8 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu. Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako.” Ukiyajua hayo Heri wewe ukiyatenda!

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumatatu, 24 Januari 2022

Ni nani atakayewashitaki wateule


Warumi 8:31-33 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.  Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?  Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya kazi muhimu anayoifanya shetani katika maisha yetu ya kila siku, ukiacha kututia majaribuni pia anafanya kazi ya kutushitaki mara tunapoangukia katika majaribu, yeye anaitwa Mshitaki wetu  na kazi hii huifanya usiku na mchana ona katika

Ufunuo 12:10 “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.”  Unaona Mwandishi wa kitabu cha ufunuo anaonyesha kushindwa kwa Mshitaki huyu katika ulimwengu wa roho, lakini ni wazi maandiko yanatukumbusha kuwa shetani nimshitaji wetu  kwa kiingereza  The Accuser” kwa hiyo waweza kuona wazi kuwa ibilisi ni mshitaki wetu, Petro anawaonywa Wakristo kuwa makini usiku na mchana ni kama anasema wasilale wawe waangalifu kwa sababu huyu mshitaki yuko kazini akituwinda kama Simba ona 1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Maana ya neno Mshitaki wetu:-

·         Ni nani atakaye washitaki wateule:-

·         Madhara ya kuwashitaji wateule:-

Maana ya neno mshitaki.

Ni muhimu kufahamu kuwa Paulo Mtume anaonyesha kwanza uwazi kuhusu ukarimu mkuu wa Mungu kwa wateule wake  na jinsi anavyotuhesabia haki na namna alivyotupenda ona

Warumi 3:23-26 “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake,ili aonyeshe haki yake ,kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa. apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.”

Na pia unaweza kuona katika Yohana 3:16-18 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”       

Upendo wa Mungu kwa wateule ni mkuu sana kiasi ambacho hakutuachilia mwanaye wa pekee asiyekuwa na dhambi kwaajili yetu na kwa sababu hiyo Mungu hashindwi, kutukarimia na mambo mengine lakini Paulo mtume anakwenda ndani zaidi katika lugha ya kimahakama kwamba licha ya rehema na upendo wa Mungu wa kutukomboa lakini vilevile sio rahisi mtu kufanikiwa kuwashitaki watele wa Mungu hii ni ile hali ya mtu kusimama mahakamani na kuendesha mashitaka ya kutaka wewe usikubaliwe na Mungu, Maneno yanayotumika hapo katika lugha ya Kiyunani ni Kategoros kwa kiingereza Prosecutor  -  A person who institutes legal proceedings against someone ! or a Person who claims that someone has committed an Offence or done something wrong , ni mtu anayeendesha mashitaka kwaajili ya mtuhumiwa ili ahukumiwe  na kuonekana na hatia , Nyakati za agano la kale  wayahudi waliamini hivyo ya kuwa shetani hufanya kazi ya kuwashitaki watu wa Mungu ili waonekane kuwa na hatia ona kwa mfano

Ayubu 1:6-11 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.

Unaweza kuona pia katika tukio linguine mfano Zakaria 3:1-7 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni? Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika. Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi. Nikasema, Na wampige kilemba kizuri kichwani pake. Basi, wakampiga kilemba kizuri kichwani pake, wakamvika mavazi; naye malaika wa Bwana akasimama karibu. Kisha malaika wa Bwana akamshuhudia Yoshua, akisema, Bwana wa majeshi asema hivi, Kama ukienda katika njia zangu, na kama ukishika maagizo yangu, ndipo utakapoihukumu nyumba yangu, nawe utazilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi ya kunikaribia kati yao wasimamao karibu.”

Kwa msingi huo wanadamu wengi wanakuwa na hofu, na kutembea kwa kutokujiamini kwa sababu wanajua kuwa wana hatia na kuwa shetani akiwashitani katika kesi ni kuwa hawatatoboa, sio hivyo tu lakini hata pale itakapotokea huna hatia kama Ayubu bado shetani atahakikisha kuwa anakuchongea kwa Mungu ili upate shida ni kwaajili ya haya Paulo mtume anauliza kwa hoja zenye nguvu kubwa sana kuwa ni nani atakayewashitaki wateule ?  nan i nani atawahukumia adhabu? Yesu yuko mkono wa Kuume wa Mungu na kwa bei ya mauti yake ametukomboa na anatutetea kwa baba yake ili wewe na mi mi tuokolewe!

Ni nani atakaye washitaki wateule:-

Kama jinsi tulivyoweza kuona maana ya Mshitaki, vilevile kugundua kuwa ni shetani lakini vilevile shetani hutumia sana mioyo yetu kutuhukumu, kule kujua kuwa tumetenda dhambi kunatuuma sana moyoni na wakati mwingine tunaweza kumfikiri Mungu vibaya kwa kudhani kuwa hataweza kutukubali na kutuhesabia haki, kutokana na namna na jinsi tulivyomkosea, sio hivyo tu wakati mwingine pia tunaweza kusikia mashitaka kutoka kwa wanadamu wenzetu wakituhukumu kutokana na kosa hili au lile

Yohana 8:2-7 “Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha. Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje?  Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe

Kwa hiyo shetani anaweza kutushitaki, mioyo yetu inaweza kutushitaki lakini hata watu wengine wanaweza kutushitaki na kisha kutuhukumu, Paulo sasa ana jenga hoja kwa kuwa Mungu ametupenda upeo akatuokoa na kutusamehe dhambi zetu ni nani atakaye washitaki wateule ?  Paulo anajenga hoja hii kwa vile anakumbuka kuwa mtu akimuamini Yesu hakuna hukumu iwayo yote inaweza kuwa na nguvu juu yake, kwa kufa kwa yesu pale msalabani hati za mashitaka na hukumu zimeharibiwa hivyio hakuna copy of judgement Wakolosai 2:13-15 “Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”

Mtu akimuamini Yesu Kristo dhambi zake zinasamehewa ya kale yanapita na tazama kila kitu kina kuwa kipya

2Wakoritho 5: 17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.”

Hii maana yake ni kuwa kila aina ya mashitaka kwa mtu wa Mungu au kwa watu wa Mungu lazima yataanguka na kusambara tika na hayatafanikiwa ni Mungu ndiye anayetuhesabia haki, Mungu muumba wa ulimwengu, ni yeye anayemtangaza mtu kuwa na haki, kwa malipo ya ukombozi unaotokana na kazi ya Yesu Pale msalabani, ambaye amekwishalipa gharama ya dhambi zetu, ni yeye aliyeteswa badala yetu ni yeye aliyekufa naye yuko mkono wa kuume wa Nguvu mbinguni hivyo kikla anayemuamini anahesabiwa haki, kwa hiyo hatusimami kwa sababu ya shetani, au mioyo yetu au watu, twasimama kwa sababu Mungu yuko pamoja nasi na anatutetea kupitia kazi ya Bwana Yesu Pale Msalabani.

Madhara ya kuwashitaji wateule:-

Watu wa Mungu hawashitakiwi, unapojaribu kuwashitaki watu wa Mungu ni wewe ndiye utakayeumbuka, ukimhukumu mtu wa Mungu wewe ndiye utakayekuja kuonekana una hukumu na hatia maandiko yanaonya vikali sana swala zima la kuhukumiana  na yana ahadi ya kuwa hakuna mtu atakayekuhukumu akafanikiwa :-

·         Isaya 54:17 “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”

·         Mtu wa Mungu hata kama unamuna anaharibu sio jukumu lako kuhukumu  ni hatari sana kumuhukumu mtu wa Mungu kwa Mungu mwenyewe biblia inaonya vikali ona Warumi 14:4 “Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha.”

·         Kushitaki na kumuhukumu mtu mwingine ni kujifanya wewe ni Mungu ni kuchukua nafasi ya Mungu ni kujikweza kuliko kukubwa sana ni kujifanya ya kuwa wewe ndiwe mwenye hatima ya maisha ya mtu mwingine Yakobo 4:12 “Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine? Maandiko ni kama yanaonya vikali sana swala zima la kuhukumu watu wengine na kuna madhara makubwa sana kwa kuwa wewe sio Mungu

·         Kuhukumu wengine kutakufanya ukataliwe  au uonekane sio kitu Warumi 11:1-3 “Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? Hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazao wa Ibrahimu, mtu wa kabila ya Benyamini. Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali.”

Ndugu yangu Mungu ni mkubwa kuliko mioyo yetu, hakuna sababu ya kutembea kwa huzuni iwapo moyo wako unamtegemea Yesu, makosa ya kibinadamu yanaweza kuweko lakini tukimuomba Mungu msamaha kwa neema yake ataturehemu, na zaidi sana Mungu ni muhimu kuendelea na Yesu, kumshika na kumuamini dhambi kubwa sana kuliko yote ni kukataa neema ya Mungu kwa kumkana Yesu Kristo Mathayo 10:32-33 “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”

Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote.