Jumapili, 19 Aprili 2015

Nikamkeshea Akapoteza Kazi Baada Ya Siku Nne!



Naitwa Sulemani  Mdeni , sipendi kuzungumza mengi sana kwa sababu habari yenyewe imejaa vitu vingi vidogovidogo, nitasema yale ya muhimu tu ambayo ndiyo hasa  yamenifanya niandike habari hii, Nilizaliwa Tanga mjini mwaka 1954, nilikulia na kusomea Tanga ambapo nilipofika darasa la nne pale Chumbageni , nilianguka mtihani ambapo nilichukuliwa na mjomba kwenda Hedaru huko upareni, mjomba wangu alikuwa ni fundi cherehani, nilipofika Hedaru mwaka 1966 nilianza kujifunza kushona  wakati huo Hedaru kalikuwa ni kamji kadogo sana , nilijifunza uufundi hapo na kuwa fundi mzuri sana, Mwaka 1975 nilikwenda Korogwe ambapo nilipata kazi dukani kwa mzee mmoja pale Manundu. Siku moja mwaka 1977 niliamua kwenda Tanga kumsalimu mzazi wangu mama.

Nikiwa hapo nyumbani siku moja mama aliniambia kwamba kuna mtoto anateswa sana nyumba ya jirani, Nilimuuliza sababu ya kuteswa, mama akaniambia ni mtoto wa kaka wa huyo jirani ambapo mtoto wa huyo alikuweko, Niliambiawa alifika hapo  baada ya wazazi wake kufa na huyo ndugu ndiyo akamchukua, niliuliza mateso yake nikaambiwa kwamba alikuwa anafanyishwa kazi kama punda, anapigwa sana na kusimangwa  na kuna wakati watoto wa huyo jirani yetu wanataka kumlawiti, mama aliniambia kuwa kwa wakati ule Yule mtoto alikuwa anaumwa sana , niliambiwa kwamaba alikuwa na kidonda kikubwa sana ambacho alikipata kwa kujikata na ndoo iliyomwangukia wakati akichota maji, nilisimuliwa mengi sana kuhusu maswala ya mtoto Yule na roho ikaniuma sana , hasa baada ya kuambiwa pamoja na hali aliyonayo bado anafanyishwa kazi sana , hata watoto wa kike wa ile nyumba ya jirani walikuwa hawafanyi kazi isipokuwa mtoto tule ambaye niliambiwa alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili tu. Nilipiga akili hatimaye niliipata, (nilikuwa na rafiki yangu polisi naomba nisitaje kituo) pale Tanga niliamua nikamwambie aje awatishe wale majirani zetu na kumchukua mtoto kwa lengo la kumpeleka Hospitali, haja yangu ilikuwa ni kumchukua mtoto Yule na kwenda naye Korogwe.

Ni kweli mpango wangu ulifanikiwa bila wale majirani kujua kuwa kwamba nilikuwa nimeusuka mimi, mtoto Yule alichukuliwa na polisi na kupelekwa kweli Bombo Hospitali kuu mkoano hapa , baada ya siku nne ambapo muda wangu wa kuondoka ulikuwa umefika  niliondoka na Yule mtoto, alikuwa ni mtoto mwenye mwili mkubwa licha ya kuonewa na alionyesha pia kuwa na akili, nilimuuliza kama mangependa kusoma  na alikubali, nilimtafutia shule ambapo alianza darasa la nne  kama nilivyokuwa nimefikiria mtoto alikuwa na akili  sana kwani alianza kuongoza , alimaliza la saba mwaka 1980 na kufaulu kwenda shule ya sekondari Magamba Lushotoalisoma hapo hadi mwaka 1985 ambapo alimaliza kidato cha nne, hakufaulu vizuri sana , lakini ilikuwa inaeleweka , alipokuwa kidato cha pili alianza uhuni wa mambo ya kutafuta wasichana na kuvuta sigara. Niliitwa mara mbili shuleni na alisimamishwa shule mara moja ,hata mimi alianza kunidharau sasa, lakini jinsi maisha yake yalivyokuwa  niliona sina budi kuendelea kumsaidia , alipomaliza shule alikuwa ni mtu wa vijiwe tu na ukimsemesha anasema hawezi kuzungumza na watu wasiosoma , yaani alibadilika sana.  

                   ziko nguvu Duniani za kulipiza katika yale tunayoyafanya Dua ni sehemu ya hilo


Niliamua kumsaidia apate kazi , nilipata bahati siku moja ya kukutana na mzee mmoja amabaye nilimshonea suti ya sherehe ya miaka 20 ya ndoa yake, pamoja na familia yake , amabaye aliafurahishwa sana na kazi yangu, mzee huyu zamania alikuwa serikalini, nilimuombea kazi huyu kijana , ambaye kwangu alikuwa kama mdogo wangu hasa kwa kuzingatia kuwa sikuwa na mdogo wa kiume , huyu mzee alinisaidia  nikapata kazi kwaajili ya huyu ndugu yangu kwenye kampuni moija pale (Tanga naomba nisiitaje)ilikuwa kama bahati kwani alipata kazi mahali pazuri sana , nikisema pazuri kwa mazingira ya kijinga  ni mahali ambapo aliweza kuiba  hii ilikuwa ni mwaka 1990. Baada ya kuanza kazi sikumuona tena hadi mwaka 1993 nilipoenda Tanga  nilimpitia kazini kwake kumjulia hali, ambapo hakuchangamka kabisa, ilikuwa kama vile hakuwa akinifahamu, Sikujali kwani hata mama aliniambia kwamba kuna siku alipatwa na dharula akaenda kumuomba msaada, akamwambia mama kwamba hana kitu, ikiwa ni uongo mkubwa, wakati huu huyu bwana mdogo alishajenga nyumba Muheza na alishanunua kiwanja pale Korogwe na alikuwa na teksi Dar hiyo ni kwa miaka mitatu tu, sikujali niliumia lakini nilijiambia lengo langu la kumsaidia lilikuwa limetimia Nilisema hayo kutoka moyoni kabisa

Mwaka 1996 nilikuwa ndio kwanza nimeoa mke wa pili baada ya Yule wa kwanza kunishinda, siku moja jioni wakati mimi na mke wangu tunatembea pale Tanga nilikutana na Yule bwana mdogo , Nilishangaa kwamba alinichangamkia sana , Aliniomba radhi kuwa hanitembelei kule Korogwe  kwa sababau yuko bize, sana amepandishwa cheo kazini , Nilimtambulisha kwa mke wangu mpya  na aliuliza kwa mshangao kama nimemuacha Yule shemeji yake (mke wangu wa kwanza)niliomwambia ndio  hakusema nenoi  lakini nadhaniu alifurahi, kwani walikuwa hawaelewani kabisa, alinipa hela nakumbuka kwa mara ya kwanza kabisa  tangu kuanza kazi,nilityaka kuzikataa lakini niliona haitakuwa vizuri zilikuwa ni 12,000 kwa wakati ule zilikuwa nyingi kidogo, halafu alihaidi kwamba angenitembelea Korogwe.

Alinitembelea kweli siku nne tu baadaye , alifika nyumbani kwanza mimi nikiwa kazini, Kuanzia hapo akawa anakuja nyumbani kwangu  haipiti wiki amekuja kusalimu, Akawa analeta vyakula , samaki na hata nguo anatununulia , hatimaye akanisaidia nikapata zabuni ya kushona nguo za kazini kwao. Niliweza kumalizia nyumba yangu pale Pongwe kwa fedha hizo, lakini siku moja  mwaka 1997 jirani yangu mmoja tena mtu mzima  aliniomba tuzungumze nikamkubalia , aliniambia jioni nikifunga kazi tukae mahali tuzungumze. Huyu mzee alianza kwanza kwa maneno ya hekima  na busara , halafu alisema alichoniitia , Sikuwa nategemea alichiniambia  kwamba mke wangu alikuwa ananiendea kinyume , alisema wazi kwamba  alikuwa akitembea na Yule kijana ambaye huyu mzee alikuwa anamjua tangu namleta pale akiwa ananuka kidonda , sikuamini kwani kwa jinsi nilivyokuwa namjua Yule mzee niliamini kuwa kuna ukweli. Niliporudi nyumbani sikumuuliza mke wangu ingawa nilikuwa na maumivu ambayo nina sitakuja kuyahisi tena maishani mwangu, Yule mzee alinishauri nisiseme chochote  nyumbani kwani kumfumania mke wangu kwenye tendo ingekuwa rahisi sana .

Siku mbili tu baada ya taarifa ile Yule mzee alinifuata kazini kwangu na kuniambia kwamba mke wangu yuko na Yule bwana mdogo nyumba ya wageni, Alinitajia nyumba yenyewe na tuliondoka naye kwenda huko, Ni kweli alikuwa hapo na Yule kijana, sikuumia palepale  sijui kwanini, nilipohakikisha nilifunga mlango na kuondoka. Yule mzee alinisaidia kufanya utaratibu wa talaka , nilitoa talaka siku ileile na baada ya kutoa talaka  ndipo hasa nilipohisi maumivu ya kweli, niliumia kiasi kwamba niliona ni lazima ningekufa , hguwa sinywi pombe lakini nilitaka kwenda kunywa, ilipofika saa nne usiku  niliingia chumbani kwangu na kuzima taa  halafu nilichukua mswala  na kukaa chini nilianza kumshitakia Mungu nilianza kunuia mabaya  kwayule kijana  nilipotea kabisa kwenye sala ile  ya kunuia ubaya hadi majogoo yanawika . Nilisali hadi nikaona mwanga nisioujua , nililenga ubaya tu.

Najua hutaamini , siku ya nne tangu tukio lile  nikiwa nyumbani kwa mama yangu ambapo nilienda kupumzika  nililetewa taarifa kwamba  Yule kijana alikuwa ameshakamatawa na yuko Polisi, niliambia alikuwa amekamatwa kwa tuhuma za wizi,wiki moja baadaye kilakitu alichokuwa anakimiliki kilikamatwa  na alikuwa rumande , lakini wiki mbili baadaye aliachiwa  huru baada ya mwenye kampuni  kumuomba polisi wamwachie maana amepata mali zake , aliachiwa akiwa hana hata senti tano, alihamia mji wa Tanga . Mwaka huohuo nilihama kutoka Korogwe kuja Tanga na kuanzisha shughuli pale Pongwe, Lakini nilipofikiria kuwa nyumba ile nimeijenga kwa zabuni ya dhambi niliiuza, mwaka 2002 nikiwa nyumbani pamoja na mama na ndugu zangu wawili wa kike tuliona mtu akija. alikuwa ni  mwanaume ambaye wazi alikuwa anaumwa , alikuwa mchafu, kupindukia na alikuwa na kidonda mguuni, baada ya kutusalimia ndipo polepole  tulipobaini kwamba alikuwa ni Yule kijana, Mahali alipokuwa na kidonda mguuni ni palepale ambapo alikuwa na kile kidonda  wakati namchukua, alipokwisha kusalimu alipiga magoti  na kusema kaka najua ni vigumu kunisamehe, lakini naomba uendelee kufikiria kunisamehe  siku moja hata nikiwa nimeshakufa , nilikuwa mjinga , kichaa, mnyama asiyefaa hata kuliwa…” alianza kulia , mimi nilinyamaza kimya  nikimtazama sikuwa na hasira naye kabisa, dada zangu na mama ndio walikuwa wakimzonga huku wakimcheka kwa kebehi, Naomba kaka uniombee heri niwe binadamu tena , ni wewe ulinifanya nikawa binadamu nikakosa shukuraninaomba uniombee niwe mwenye hekima  tu nipate hekima tu si utajiri..’

Akina dada na mama walimcheka  na kuanza kumtukana Mimi sikufanya hivyo nilimsjhika mkono Yule kijana na kumuinua Ni kweli umekosa  na umejua kosa lako , mimi na wewe tutaomba pamoja  kwa Mungu urejewe Ufahamu , Dada zangu walipiga kelele  za mshangao na kupinga jambo lile  nilimsaidia Yule kijana kuoga  na alipewa chakula ingawa kwa masimango, usiku nilimwomba aingie chumbani kwake aombe anachokitaka kimtokee, name nliingia chumbani mwangu na kuanza kusali  nikimwombea mabadiliko, Najua wakati mwingine ni vigumu kuamini mambo haya lakini nasema hivi yapo, huyu kijana alikaa pele nyumbani na kidonda chake kilikauka  baada ya wiki tatu tu, wakati alikuwa amehangaika nacho kwa mwaka mzima , unajua huyu kijana siku hizi yuko wapi? Ukiona watu wanaokuja Dar wakitokea Mombasa kama wafanya biashara ulizia Bwana Abuubakar au jitu kubwa, Amerudi kwenye hali yake ya kawaida ya zamani bwana mafedha lakini hivi sasa anajua kuheshimu nwatu hata watoto wadogo, na mimi nimepata ndugu hivi sasa. Je nguvu ya maombi iko wapi? Je kumtendea mtu uovu ni swala unalolichukuaje na unalielezea vipi? Je huoni kwamba Kusamehe ni jambo la muhimu sana? najua kuwa unakodoma mimacho kwa mshangao lakini Kristo alisema waombeeni wanaowaudhi watendeeni mema adui zenu.
Na Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima Rev. Innocent Kamote
0718990796, ikamote@yahoo.com

Hakuna maoni: