Adiko la Msingi: Mwanzo 14:14-16
“Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha
vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na
wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na
watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa
kushoto wa Dameski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu
nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu.”
Utangulizi:
Nimetumia neno operesheni ambalo kwa kawaida ni neno linalotumika
katika kampeni mbalimbali za kivita, mfano Tanzania,ilipokwenda kukomboa
visiwa vya Anjuan wakati wa utawala wa Kikwete ile iliitwa Operasheni
Demokrasi, Israel ilipokwenda kukomboa wayahudi kule Uganda wakati wa
idd Amin kampeni ile iliitwa Operasheni Entebbe au wakati wa kurejesha
Waethiopia wenye asili ya Kiyahudi ambao inasadikiwa kuwa walikuwa
watoto wa Suleiman iliitwa operesheni SOLOMON sasa Abrahamu alipigana
vita kumkomboa Lutu ndio maana nimeiita Operesheni Lutu sasa tuendelee
na somo
Ni muhimu kufahamu kwamba maandiko matakatifu
yanatukumbusha katika Wagalatia 5:13b kwa mba tutumikiane kwa Upendo,
“bali tumikianeni kwa upendo” moja ya maeneo yanayotufundisha kuhusu
maisha ya Abraham ni pamoja na kifungu hiki muhimu tulichokipitia
leo,kifungu hiki kinatukumbusha jinsi Abrahamu alivyokuwa mwenye kujali
sana Maisha ya ndugu zake na jamaa zake. Lakini vilevile tunajifunza
mambo mengine Makubwa sana kuhusu Mtu huyu wa Mungu ambayo yatatupa
uweza mpana wa kufukiri kuhusu utendaji wa Mungu katika maisha yake.
Wengi wetu tunaposikia kuhusu Maisha ya Abrahamu mara kadhaa tunaweza
kukumbuka matukio yake ya kidhaifu kama kusema uongo kwa kusudi la
kulinda uhai wake kwa kumtaja Sara kama dada yake jambo lililohatarisha
kupoteza ndoa yake, Lakini vilevile tunaweza kukumbuka ushujaa wake wa
kukubali kuitikia wito wa Mungu na kukubali kuitii Sauti yake kwenda
Katika nchi ya Kanaani, aidha tunaweza kukumbuka ushujaa wake wa
kuthubutu kumtoa Isaka kama sadaka ya kuteketezwa mpaka malaika
akamzuia, Pamoja na umuhimu wa Maswala hayo Leo ni muhimu tukajikumbusha
kuwa Ibrahimu vilevile alikuwa mtu wa Vita, alikuwa mpiganaji Hodari
mwenye mbinu kali sana za kivita, Abrahamu alikuwa mpiganaji.
Abrahamu si baba wa imani tu laikini ni baba wa vita!
Biblia inatufunulia siri hii kuhusu maisha ya Abrahamu kama mtu wa vita
na jemadari kwa habari tunayoweza kuiona katika Mwanzo 14:1-4. Ni
muhimu kufahamu kuwa sio tu kuwa Abraham alikuwa mpole tu lakini
vilevile alikuwa ni Jemadari wa vita ni mpiganaji, Lakini alikuwa na
Moyo wa kuwasaidia wengine, Mungu anapokuwa amekuita kuwa Baraka kwa
wengine maana yake pia amekuita kuwapigania wengine Abrahamu anaonekana
kuwa shujaa wa kipekee alipoingia katika vita ya kumuokoa Lutu Nduguye.
Mwanzo 14:1-4 “Ikawa siku za Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko
mfalme wa Elasari, na Kedorlaoma mfalme wa Elamu na Tidali mfalme wa
Goimu, walifanya vita na Bera mfalme wa Sodoma na Birsha mfalme wa
Gomora, na Shinabu mfalme wa Adma, na Shemeberi mfalme wa Seboimu, na
mfalme wa Bela, ndio Soari. Hawa wote wakakutana panapo bonde la Sidimu,
kwenye Bahari ya Chumvi. Miaka kumi na miwili walimtumikia Kedorlaoma,
hata mwaka wa kumi na tatu wakaasi.”
Maandiko yanaonyesha kuwa
kulikuwa na vita za kifalme wafalme Amrafel, Arioko, Elasari, Kedorlaoma
na tidal yaani combine ya Majeshi ya wafalme watano(5) walioungana
walikuja kupigana na Birsha, Shinabu, Shemeberi, na mfalme wa Bela jumla
ya wafalme (4) sababu kuu ya wafalme hawa wanne walikuwa wamekataa
kuendelea kulipa Kodi ya mfale Kedorlaoma wa Elamu aliyekuwa kinara wa
utawala huo, hii ilikuwa vita kali katika nchi ya kanaani hususani
kusini ya Israel liliko bonde la nchi ya chumvi lililojulikana kama
bonde la Siddim, wafalme hao wanne walikuwa watumwa kwa miaka 12 lakini
sasa wakaasi, hivyo Kedorlaoma alikuja kuwashambulia akiwa na wafalme
kadhaa wanaomuunga mkono.
Mwanzo 14:5-7 “Na mwaka wa kumi na nne
akaja Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja naye, wakawapiga Warefai
katika Ashteroth-karnaimu, na Wazuzi katika Hamu, na Waemi katika
Shawe-kiryathaimu, na Wahori katika mlima wao Seiri, mpaka Elparani
iliyo karibu na jangwa. Kisha wakarudi wakaja mpaka Enmisfati, ndio
Kadeshi, wakapiga nchi yote ya Waamaleki, na Waamori waliokaa
Hasason-tamari. Mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, na mfalme wa
Adma, na mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakatoka
wakapanga vita panapo bonde la Sidimu; wapigane na Kedorlaoma mfalme wa
Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, na Amrafeli mfalme wa Shinari, na
Arioko mfalme wa Elasari, wafalme wanne juu ya wale watano. Na bonde la
Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami. Nao wafalme wa Sodoma na Gomora
wakakimbia, wakaanguka huko, nao waliosalia wakakimbia milimani.
Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda
zao.”
Kinara wa vita hivi alikuwa ni mfalme KEDORLAOMA yeye
aliongoza muungano wa majeshi ya kifalme kwa zaidi ya wafalme wanne na
kabla ya kuanza na hawa watano walifagia miji mingina na kuwapiga vibaya
wote waliokuwa kinyume nao na walipofika katika miji ya Sodoma na
Gomora wafalme hao watano pia yaliwakuta magumu na wote walikimbia
mbele ya ufalme huu wenye nguvu. Nani angeweza kuwatetea wafalme hao
watano na wengine wote chini ya KEDORLAOMA? Hakuna mtu aliyeweza
kusimama mbele yake.
Kosa kuu la KEDORLAOMA.
Pamoja na
ushindi mkubwa aliokuwa nao KEDORLAOMA alifanya kosa ambalo liliweza
kumfanya ajutie utendaji wake kosa hili lilikuwa kumgusa Lutu Mwanzo
14:8-10, walichukua Mateka kila kitu lakini pia walimchukua Lutu na mali
zake na watoto wake na watu wake wote aliokuwa nao, Lutu alikuwa
amefiwa na baba yake na hivyo alilelewa na Abrahamu, Abrahamu hangeweza
kumuacha Lutu, amekulia kwake tangu utoto wake kusumbuliwa kwake
kulileta maumivu makubwa sana kwa Abrahamu naye alipopata habari aliona
aweze kufanya jambo.
Mwanzo 14:11-12 Biblia inasema “Wakachukua
mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao.
Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko Sodoma, na mali
yake, wakaenda zao.”
Abrahamu aliamuru Majeshi yake kwaajili ya Lutu.
Mwanzo 14:13-19 “Mtu mmoja aliyeponyoka akaenda, akampasha habari
Abramu Mwebrania; naye amekaa panapo mialoni ya Mamre, yule Mwamori,
ndugu ya Eshkoli, na ndugu ya Aneri, na hao walikuwa wamepatana na
Abramu. Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa
silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na
kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku,
yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande
wa kushoto wa Dameski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu
nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu. Abramu aliporudi kutoka
kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa
Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. Na
Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa
kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na
abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi.”
Mungu alimpa neema kubwa Abrahamu, alikuwa na vijana “318” ambao wao walikuwa wamejifunza vita Biblia inasema hawa wote walizaliwa katika nyumba yake hii ni wazi kuwa walilelewa na Ibrahimu, na ni wazi kuwa Ibrahimu alikuwa amewafunza kuhusu Mungu ushujaa wao ulikuwa umetokana na Mungu aliye juu Neema ya Mungu ilikuwa juu yao haiwezekani katika akili za kawaida Mtu mmoja aweze kupiga wafalme wanne waliokuwa na ushindi mkubwa wa ajabu, na wafalme wanne walikuwa wamekimbia Lakini Abrahamu na vijana wake 318 tu waliwapiga vibaya kundi kubwa la watu wenye uzoefu wa vita, siri kuu ya ushindi wa Abrahamu ilikuwa ni Muujiza wa Mungu, lakini vilevile alifanya sehemu yake alipigana na Mungu aliwaongezea hekima namna ya kupambana.
Abrahamu alifanikiwa kuwafuatia na
kuwavamia maadui na aliweza kufanikiwa kuwapokonya malizote
walizozipora kwa wafalme wanne na zaidi ya yote Abrahamu alikuwa
anamtaka Lutu awe salama, aliwafukuza maadui kwa zaidi ya maili 50
Abrahamu alifanya mashambulizi makali wakati wa usiku, hakupigana mchana, laziki zaidi ya yote aliwagawa vijana wake makundi makundi na wakaanza kushambulia kutoka sehemu mbalimbali, maadui walichanganyikiwa wakidhani ya kuwa ulikuwa uvamizi mkubwa sana na hivyo walikimbia na kuachia kila kitu hivyo Abrahamu alimshinda KEDORLAOMA, Abrahamu alirejea nyumbani na ushindi. Alirudi na vijana wote waliwa salama na alirejea na mali zote na alifanikiwa kumuokoa Lutu.
Wafalme kadhaa wakaja kumlaki
Mmoja alifikiri ushindi wa Abrahamu unatokana na vijana wake “318” na
akasema Mwanzo 14:21-22 “Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, Nipe mimi
hao watu, na hizo mali uchukue wewe. Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma,
Nimeinua mkono wangu kwa BWANA, Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na
nchi”
Lakini Mfalme mwingine aliyekuwa Kuhani wa Mungu aliya juu sana alijua siri ya ushindi wa Abrahamu
Mwanzo 14:17-20 “Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote”
Siri kubwa ya ushindi wa maisha yetu hautokani na uwezo wetu na akili
zetu, bali inatokana na uwezo na uhodari wetu katika Mungu, ni lazima
tujifunze kupambana na kushinda vita zote za kiroho, na kujitegemeza
katika uwepo wake na adui zetu watakimbia, Ibrahimu alikuwa ni mpole
sana lakini linapokuja swala la kuchokozwa na kuguswa kwa maisha ya
nduguze alihakikisha kuwa anapigana kwa hali na mali huku akimshirikisha
Mungu.
Ni ukweli ulio wazi kuwa tunapokuwa na Moyo wa kuwajali
wengine Mungu hutubariki na kutupa neema na Baraka tele, Abrahamu
hakuweza kusema Lutu shauri yake si amejitenga nani mwenyewe lakini bado
alitaka kuhakikisha usalama wa Lutu na jirani zake unakuwepo na hivyo
alimtetea Lutu hii ndio operesheni Lutu.
mfalme wa Sodoma
alitamani kumpa Ibrahu Mali zake ili achukue vijana 318, Ibrahimu
hakukubali, wako watu wa mataifa ya kigeni wakati mwingine
wanatulazimisha Afrika kufuata tabia zao mbaya kwa makusudi ya
kutuingiza katika mtego wa kukosa uadilifu, tukatae misaada hiyo na
tuendelee kumtegemea Mungu anatubariki na kutusaidia.
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Rev. Innocent Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni