1Petro 4:15 “Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya,
au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kwamba ili mtu wa Mungu
aweze kuwa imara kiroho anahitaji muda mwingi wa kukaa katika uwepo wa Mungu,
kuomba, kujisomea neno na kutafakari na kuimba na kujizatiti kiroho kuliko
tunavyoweza kufikiri, maandalizi yetu ya kiroho binafsi ni muhimu kwa ushindi
dhidi ya ibilisi kuliko hata huduma, Mojawapo ya mbinu kubwa sana anayoitumia
ibilisi ili kuwamaliza watu wengi kiroho na hatimaye ili aweze kuwaangusha ni
kuwaingiza katika MTEGO WA SHUGHULI NYINGI kwa msingi huo ni muhimu kwetu
kuijua mbinu hii ili shetani asipate kutushinda kwa kutokuzijua mbinu zake
angalia 2Wakoritho 2:11 “Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira
zake” Biblia ya
kiingereza inatumia maneno “Let Satan should get advantege of us – yaani asije
akapata faida, akapata kitu kwetu, akafaidika, kwa mbinu “Fikra” zenye hila
zenye kuumiza zenye ujanja cunning strategies mbinu anazitumia adui ili aweze
kutushinda, Biblia inatutahadharisha kuwa wajuzi na wajanja katika mbinu za
ibilisi ili asitunase, moja ya mbinu hii ni mtego wa shughuli nyingi!
Shetani anajua nguvu
zako na uweza wako ulio nao, anajua wazi kuwa asili ya nguvu zako iko katika
chanzo cha ngubu za Roho Mtakatifu unachokitegemea, ambacho kimeungwa katika
kujityoa kwako binafsi kwa Mungu self devotional kwa msingi huo hataki na wala
hatakubali upate nafasi ya kurudi magotini na katika kulisoma neno la Mungu na
badala yake atakupa kitu mbadala ili akutumie kwenye hilo na baada ya muda
flani aje na mbinu zilezile za kukuangusha ukiwa mtupu kabisa, mtego huu na
mbinu hii anayoitumia shetani ni Mtego wa shughuli Nyingi.
Ni muhimu kufahamu
kuwa unaweza kuwa unampenda Mungu sana na unapenda sana uwe na Muda wa kuomba
na kububujika katika uwepo wa Mungu, unapenda upate nafasi ya kufunga na kuomba
na kutafakari neno na kuhudhuria ibada na kufanya mambo yote yatakayokuweka
karibu na Mungu na kuna uwezekano kabisa umekomaa kiroho na umefikia ngazi
ambayo hakuna jaribu jipya litakuja kwako usilibaini, Shetani akiisha kufahamu
hilo hatakuwa na Majaribu ambayo anajua kuwa utashituka kwa haraka bali atakuja
na Mtego wa shughuli nyingi, kwa mtego huu atakutumia kwa muda mrefu uwe
unashughulika na mambi mengi sana ambayo yanaweza kuwa kama ya kiroho hivi
lakini baada ya Muda utagundua kuwa umepungukiwa sana na uwepo wa Mungu na
katika wakati huu anaweza kukusambaratisha atakavyo akihakikisha kuwa hauna na
wala haupati nguu ya kuinuka tena!
Binafsi Kuna jambo
nimekuwa nikimuomba Mungu sana, kuhusu maisha yangu katika siku za karibuni ili
kwamba Mungu aweze kuingilia kati na kunisaidia, nampenda sana Mungu, napenda
sana neno lake na napenda sana kuomba na pia kuandaa jumbe za neno la Mungu kwa
kusudi la kuwasaidia watu wake, napenda kukaa uweponi mwake, hiyo ni kazi yangu, ni wajibu wangu ndio kazi
niliyoitiwa, nimeitwa kuujenga mwili wa Kristo na hili nalifanya kwa uaminifu,
Lakini nahisi kuna kitu kimepungua kwangu, nahisi kiu ya kumuhitaji Mungu, nafanya
kazi yake lakini nahisi nimemmisi Mungu, sio yeye tu nimemisi pia baadhi ya
watu, ndugu zangu jamaa zangu na hata marafiki zangu nahisi kama kuna jambo
ninapoteza sio kiroho bali na hata kimwili, kwa sababu hata ratiba ya kula
haiko sawasawa nimekuwa na shughuli nyingi mno mno nikiwa natafakari hilo siku
moja nikaelewa kuwa ni mtego wa Ibilisi!
Fikiaria
kama unaweza kuwa na shughuli nyingi, kiasi cha kutokuwa na Muda na marafiki,
jamaa, familia, mkeo, wanao, na hata muda wa kula au ahata kufanya mazoezi na
unarejea nyumbani ukiwa umechoka mno, hata kula kwenyewe unaona uvivu! Kumbuka
shughuli ulizokuwqa ukizifanya sio dhambi hata kidogo ni shughuli zilizoko
katikati yako na huduma yako, kwa hiyo ni kama za huduma yako, wale watu
waliofikia ngazi ya kuwa viongozi, Maasskofu, waangalizi, mitume na manabii
watakubaliana nami katika hili kuwa kadiri unavyokuwa na majukumu haya makubwa
na shughuli zionaongezeaka mno ni shughuli za kati kati katika ya uwepo wa
Mungu na uwepo wa dunia hapa ndipo shetani anapokuweka kwa kusudi la kukuingiza
katika mtego huu ninaouzungumzia shetani anaogopa sana akuachie mtu kama wewe
ukae katika uwepo wa Mungu anajua utampa shida sana angalia mistari ifuatayo:-
Luka
4:1-2 “Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani,
akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na
siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa”
Luka
4:14-15 “Yesu akarudi kwa nguvu
za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika
masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote.”
Katika
maandiko hayo hapo juu Yesu alikaa katika uwepo wa Mungu kwa muda wa kutosha
alikuwa anafunga na kuomba alishinda majaribu yote makubwa ya ibilisi, na sasa
anaingia katika jamii akiwa na NGUVU ZA ROHO nguvu hizi ndio zinazomfanya Yesu
anakuwa maarufu kil a mahali habari zake zinaenea kila sehemu na watu wote
wanamsifu na kumtukuza, Kukaa katika kuutafuta uwepo wa Mungu ni jambo la
muhimu na lenye kumuogopesha sana shetani kuliko jambo lolote lile shetania
anajua ni vigumu kumshinda mtu anayekaa katika uwepo wa Mungu lakini ni rahisi
sana kumpata mtu kwa kumfanya ashighulike na mambo ya wengine kuliko
kushughulika na yeye binafsi
Jambo hili hunitokea
na mimi bila kupenda unakuwa busy unakuwa na shughuli nyingi tu zenye
kuchosha nikitafakari wakati mwingine
naingia shaka kama yanafanana na kile Mungu ameniitia au nimeingia katika metgo
wa ibilisi? Siku moja nikiwa nimechoka majira ya saa tatu usiku nikiwa nimevaa
suti niliyoivaa tangu asubuhi, na nikiwa sijachukua mazoezi wala kuoga nikiwa
nawasubiri watu fulani ambao nilikuwa na kikao nao tangu asubuhi mpaka saa sita
nikaenda kunywa chai ya mchana, kisha wao wakenda mjini na kuniahidi watarejea
na hivyo nikawa nawasubiri warejee mpaka ilipofika saa tatu usiku waliniahidi
wanakuja nikaendelea kusubiri sikubadilisha nguo sikutaka kuondoa nguo nzito
mwilini mwangu nawasubiri watu wa Mungu niwahudumie, nilipompigia simu mmoja
akaniambia ndio yuko mezani anakula ameshindwa kurudi kha mimi nilikuwa
sijaweza kufanya jambo lolote namshubiri yeye, nilimweleza mke wangu naye
akaniambia omba ili kwamba roho ya Masumbufu ikuachie unakuwa busy sana lakini
ni ubize ambao ni kama unakutesa wewe, ratiba za kula hazikai vizuri, ratiba za
mazoezi huzifuati sawasawa, kukaa na familia na hata muda wako wa kuandaa neno
la Mungu kaa sawa alinieleza mke wangu!
Nikaomba na
kumuuliza Mungu mbona maswala yasiyo ya muhimu lakini yanayoonekana kama ni ya
muhimu sana yananiandama maisha yangu naona nashughulika nayo kuliko yale
niyapendayo kuyatenda? Ndipo Roho Mtakatifu akaniambia “UMEINGIA KATIKA MTEGO
WA SHUGHULI NYINGI”
Nilifikiri
ninamtumikia Mungu na ninafanya kazi zake sasa nimeingiaje kwenye mtego
washughuli nyingi? Nilikuwa najiuliza mbona kazi zimeongezeka sana nyingine
njema ni za kazini, na taasisi yetu ni ya kimungu tunamtumikia Mungu sasa
nimeingiaje kwenye mtego wa shughuli nyingi? Ni Mungu ndiye aliyeniita
nilidhani kuwa wakati huu nimekuwa na shughuli nyingi kwa sababu nimekuwa mtu
mzima kwa hiyo majukumu yananipeleka nisikokutaka nilijipa moyo kwa neno la
Mungu Yesu alimwambia Petro ulipokuwa kijana ulikwenda kokote ulikotaka wewe
utakapokuwa mtu mzima mtu mwingine atakufunga na kukupeleka usikotaka, Yesu
alikuwa anaongelea juu ya mauti ya Petro katika Yohana 21:18 “Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa
ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha
mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka.” Tafasiri ya Maneno haya ya Yesu ipo katika mstari wa 19 Yesu
alitabiri namna Patro atakavyokufa akimtukuza Yesu, Mimi niliutumia mstari wa
18 pekee kukubali tu ukweli kuwa ukiwa kijana unakuwa na uhuru mkubwa wa
kujifanyia lolote ulipendalo nafasi inakuwa nyingi mno na unaweza kwenda kokote utakako ukiisha kuwa mtu
mzima na mwenye majukumu shughuli zinakufunga kiasi ambacho huwezi kufanya
utakalo, bali majukumu yanakulazimisha uyafanye nilitumia maandiko haya kujipa
moyo kuwa huenda ndio mambo yalivyo lakini Roho Mtakatifu alisisitiza tu “UMEINGIA
KATIKA MTEGO WA SHUGHULI NYINGI” UMEINGIA KATIKA MTEGO WA SHUGHULI NYINGI?
Sasa niliamua kuwa
mpole na kumsikiliza Roho Mtakatifu, lakini pia safari hii nilimsikiliza mke
wangu, ni nadra sana kwangu kusikiliza mwanamke narudia tena ni nadra sana
kwangu kumsikiliza mwanamke hii niachie mwenyewe labda yatokana na athari zangu
za kimaandiko na kimaisha huwa simsikilizi mwanamke aaa huwa namsikiliza sana lakini kwa vile
niko na shughuli nyingi (busy) na huwa
anazungumza habari nyingine za kwenye mitandao ya kujamii huwa nahesabu kama
mtu anayeweza kunipotezea Muda lakini safari hii alichoniambia “omba ili kwamba
roho ya Masumbufu ikuachie u nakuwa busy sana lakini ni ubize ambao ni kama
unakutesa wewe,” akili ilinijia kuwa nachoka sana na kufadhaika sana kwa
shughuli nizifanyazo kila siku nikihangaikia watu na taasisi nimekuwa na shughuli nyingi kweli kweli busy mno hakuna
wakati wakupumzika, shughuli zenyewe
ukizitafakari sio dhambi ila ziko katikati ya shughuli za kimungu ni shughuli
za kanisa kabisa lakini hazikupi nafasi ya kuukaribia uwepo wa Mungu hizi ndio
zinaitwa Mtego wa shughuli nyingi, Mtego huu ndio Ibilisi anautumia kulikamata
kanisa la leo, chunguza kwa undani makanisani kila idara ina shughuli, kanisa
lina shughuli wachungaji wanashughuli, kuna shughuli za VIJANA, Kuna shughuli
za WAMAMA, kuna shughuli za WABABA, kuna shughuli za UJENZI, kuna shughuli za UINJILISTI,
kuna shughuli za Vikao vywa WACHUNGAJI, Kuna shughuli za WAANGALIZI, kuna
shughuli za MAASKOFU kuna shughuli za UMOJA WA MAKANISA, kuna shughuli, Kuna
mipango kadhaa ya maswala kadhaa, kuna shughuli nyingi mno, siku moja nilifika
kwenye kituo Fulani cha Polisi kwenye shughuli nikamuona rafiki yangu mmoja
ASKOFU wa kanisa Fulani aliwa pale POLISI mimi nilikwenda kutoa taarifa ya
mhasibu wetu alikuwa amechukua fedha nyingi za taasisi yetu zilizotakiwa kwenda
TRA na tulipokuwa tunambana azirudishe akawa hato maelezo yaliyonyooka kwa hiyo
nilimpeleka POLISI na ilinipasa kufika hapo kuandikisha maelezo sikuwa na nania
ya kumfunga lakini nilitaka pesa zirudi tu zilikuwa milioni 16, sikuwahi
kufikiri kuwa nitafika Polisi hata siku moja, Nilishangaa kumuona Askofu yuko
pale, Nilimuuliza Mchungaji Vipi mbona uko hapa akaniambia kuna Mchungaji wangu
yuko Ndani amefungwa nimekuja kumletea chakula tulikaa sana pale kituoni wakati
huu somo hili lilikuwa ndio linafunuliwa kwangu upesi nikajisemea Moyoni ni “ULE
MTEGO WA SHUGHULI NYINGI” ulimwengu umekuwa wa shughuli nyingi, ninasimamia
shule ya Seminary mahali ambapo injili inahubiriwa wanafunzi wetu ni wa kiume
tu baadhi ya wanafunzi watatu walijihusisha na dhambi ya USHOGA tukawafukuza,
wazazi wao wakapingana nasi vikali, wakitaka vijana wao warudishwe shuleni,
Afisa Elimu wilaya na Mkoa pia walisimama na wazazi ili kuwatetea warejee
shuleni, Msimamo wetu ni kuwa hatuwezi kuwarudhisha shuleni wanafunzi
waliokiuka maswala ya uadilifu kwa kiwango kama hiki, ilikuwa shughuli kubwa
sana, vikaoa kadhaa vilikaliwa, vikao vya Kamati ya nidhamu, vikao vya walimu,
vikao vya bodi ya shule, vikaoa na wazazi vikao na maafisa Elimu, vikaoa na
watu wa usalama wa taifa ilichukua miezi
mitatu kuumaliza mgogoro huo wa kuvutana sisi HAWARUDI maafisa Elimu wanasema WATARUDI
lilikuwa jambo la kushangaza viongozi wakubwa wanaotakiwa kusimamia uadilifu
katika maswala ya Elimu wakitetea ujinga na uchafu, tena wakisema haifai
Mchungaji kuwa mkuu wa shule? Nilikuwa naumia moyoni nilitamani Mungu afanye
kitu flani na Mungu alifanya lakini mapambano hayo dhidi ya uovu yalichukua
miezi mitatu kumalizika na kumbuka maafisa Elimu wote walikuwa wakristo na
wazazi wa watoto walioshiriki uovu ule walikuwa wakristo kwa nini shetani
alikuwa akitusumbua hivi dunia imeharibika ibilisi alikuwa anataka tuwe na
shughuli nyingi tujiumize na kujichosha kwa jambo rahisi la walioshiriki
vitendo viovu kinyume na sheria za shule na imani yetu na neno la Mungu
walitakiwa kuondoka mara moja lakini tulitumia miezi mitatu kuvutana shetani
alitaka kuleta usumbufu na kutuingiza katika mtego wa shughuli nyingi. Sasa
basi ni muhimu kujihoji basi mtego wa shughuli nyingi ni nini?
Maana ya Mtego wa
shughuli Nyingi.
Nilijiuliza
kwanza huu mtego wa shughuli nyingi ni upi? Katika moja ya mafunzo ya awali
sana ya wokovu tulijifunza kuhusu kuwa na shughuli nyingi kunavyozuia ukuaji wa
mtu kiroho hasa kupitia mfano wa Mpanzi ambapo zile mbegu zilizoangukia katika
miiba humaanisha watu wanaolipokea neno la Mungu, lakini kwa sababu ya kusongwa
na shughuli za ulimwengu wanashindwa kukua vizuri na hatimaye kushindwa kuzaa
matunda! tujikumbushe maana za mfano ule
Mathayo
13:18-23 “Basi ninyi sikilizeni
mfano wa mpanzi.Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule
mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na
njia. Naye aliyepandwa penye miamba, huyo
ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi
ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile
neno, mara huchukizwa. Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile
neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa
halizai. Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno,
na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu
thelathini.”
Nilitafakari
sana kifungu hiki cha maandiko kwamba je inawezekana kwamba nimegeuka kuwa
kundi la wale waliopandwa kwenye miiba? Ambao shughuli za dunia na udanganyifu
wa mali hulisonga neno lisikue?au lisizae, sitaki kujihesabia haki sitafuti
vitu vya dunia nimeridhika Mungu amenipa kila kitu ambacho mwanadamu wa kawaida
anatakiwa kuwa nacho sitaki mambo makubwa kwa hiyo udanganyifu wa mali hauwezi
kunisumbua lakini naweza kukiri kuwa shughuli za dunia zimenifunga, shughuli za
dunia ni nyingi na sio lazima ziwe dhambi, lakini ni kazi za kawaida lakini
hili silo lile ambalo Roho Mtakatifu alimaanisha.
Kwa
hiyo nilitafakari kifungu kingine Katika wimbo uliobora 1:6 “Msinichunguze kwa kuwa ni mweusi-mweusi, Kwa sababu jua
limeniunguza. Wana wa mamangu walinikasirikia, Waliniweka niwe mlinzi wa
mashamba ya mizabibu; Bali shamba langu mwenyewe sikulilinda.“
Kifungu
hiki pia sio tatizo kubwa sana huyu ni mtu ameajiriwa na au amefanywa mtumwa
maisha yake yamemlazimisha kuwa mtumishi wa wengine kiasi ambacho ameshindwa
kutimiza wajibu wa kuangalia mambo muhimu yanayiomuhusu yaani shamba lake
mwenyewe la mizabibu, huu sio mtego wqa shughuli nyingi ni mazingira flani tu ya kuajiriwa na
kutokufanya maswala yako mwenyewe, hili halikuwa lile ambalo Roho Mtakatifu
alikuwa analikemea kwangu “UMEINGIA KATIKA MTEGO WA SHUGHULI NYINGI”
Kwa
hiyo nilitafakari kifungu kingine tena kuhusu siku ile Yesu alipomtembela
Martha na Mariamu ona
Luka 10:38- 42 ”Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke
mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake
aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini
Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana,
huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie
anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika
kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu
amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”
Hichi
alichokisema Yesu kwa Martha kilikuwa ni cha Muhimu sana angeweza kuketi kama
Mariam na kumsikiliza Yesu ambaye anauwezo hata wa kushusha chakula kutoka
mbinguni, Yeye alikuwa akisumbuka kwaajilya kumpikia Yesu hakikuwa tatizo kama
Martha angepika na kuleta chakula kwa Yesu angekula yeye ni mwanadamu kwa wakati
ule angekula lakini tatizo la Martha alinung’unika na kushitaki kuhusu Mariamu Hivyo
Yesu alitaka kuonyesha ubora wa Mariamu kwa upande mwingine kumsikiliza Yesu na
kukaa minguuni pake ni shughuli muhimu sana, Kuliko alichokuwa anakifanya
Martha, Martha alikuwa na shughuli nyingi (busy) lakini hili halikuwa
tatizo isipokuwa kama tu amenung’unika lakini shughuli yake ilikuwa ni sahihi
kimila na kitamaduni kushughulika kwaajili ya Yesu aliyekuwa mgeni wao haikuwa tatizo kama
tutakuwa na shughuli nyingi bila kuwanu;gunikia wengine sio tatizo, mimi
ninashughulika kwaajili ya Yesu na sitaki kumlaumu Mtu lakini hili sio lile ambalo
Roho Mtakatifi analikemea kwetu Mungu anatuonya na kutukemea kuhusu hili “UMEINGIA KATIKA MTEGO WA SHUGHULI NYINGI”
Andiko
la msingi hasa linasema hivi 1Petro 4:15 “Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya,
au KAMA MTU AJISHUGHULISHAYE NA MAMBO YA WATU WENGINE.”
Nitalinukuu andiko hili pia kwa lugha ya kiingereza uweze
kuliona vizuri kile kinachomaanishwa hapa 1Peter 4:15 “If you suffer, It should not
be as a murderer or thief or any other kind of criminal or EVEN AS A MEDDLER”
Neno Meddler – maana yake mwenye kujishughulisha na mambo ya watu katika njia
isiyo sahihi, au yenye kuingiliana na shughuli muhimu za kazi, au
kujishughulisha ma maswala yasiyopaswa au yasiyotakiwa toleo lingine la
kiingereza linatumia neno “Busybody” mtu anayeteseka kwa kujishughulisha na
mambo ya wengine yanayoonekana kama mambo yake au ya Mungu lakini sio ya Mungu KJV inasema
hivi 1Peter 4:15 “But let none of you
suffer as a murderer, or as a thief, or as an evildoer, or as a busybody in
other men's matters.”
Mtu aliyeingia katika
mtego wa shughuli nyingi ni mtu anayejishughulisha na maisha ya wengine lakini
mtego huu ni mtego wa dhambi isiyokusudiwa, hili ni tatizo kubwa sana
unajishughulisha na mambo ambayo sio kazi ya wito wako Mungu aliokuitia na hili
pekee ni tatizo tosha na mbaya zaidi mtu mwenye kujishughulisha na mambo ya
wengine ana muda mchache au hana muda kabisa wa kushughulikia mambo yake,
hawafanyi dhambi lakini wakati wote hufukiri kuhusu wengine hawana muda wa
kutubu husaidia wengine kutubu, hawana muda wa kusoma neno husaidia wengine
kuelewa neno, hawana Muda kuomba huhamasisha watu kuomba, hawana muda hata wa
kula huhudumia watu walioshiba huku yeye akiwa na njaa, hutatua matatizo ya
wengine huku yake hakuna anayeyajali kwa ujumla wanapoteza lengo na hawana muda
hata wa kujitathimini, wanaweza kunyoosha kidole kwa wengine huku vitatu
vikiwarejea wenyewe ikiwa ni ishara ya Mungu Baba Mwana na Roho Mtakatifu
wakitusihi kujiangalia wenyewe zaidi kujitathimini na kujilinda na kujihami
Huu ni mtego wa
Ibilisi anatufanya tupeleke mawazo yetu kwenye kitu vitu ambavyo havitaweza
kubadilika ili kwamba tusiweke mawazo yetu katika mabadiliko yetu wenyewe, ni
kwaajili ya haya Shetani anataka tuangalie mambo ya wengine ambao ni vigumu
kuwabadilisha ili kwamba tusijiangalie wenyewe ambao tunauwezo wa kubadilika
kwa haraka kumbuka mtu aliyebadilika yeye mwenyewe ndio mwenye uwezo mkubwa
zaidi wa kuwabadilisha wengine, shetani haogopi mtu anayeshughulikia mambo ya
wengine bali anaogopeshwa zaidi na mtu anayetumia muda mwingi kwa mabadiliko
yake mwenyewe
Kwa hiyo utaweza
kuona kuwa na shughuli nyingi sio sifa bali ni wazi kuwa ni mtego wa Ibilisi,
kukaa kwetu katika uwepo wa Mungu na kubadilika kwetu ndio kwa muhimu zaidi na
kunakoweza kubadilisha wengine kuliko shughuli zetu za kushughulika katika
kubadilisha mambo!
Shetani amefanikiwa
kwa kiwango kikubwa sana kulipa kanisa kuwa na shughuli, makanisa mengi leo yana mipango na shughuli na watumishi
wengi wa Mungu leo wanashughulikia mipango na shughuli, vijana wako kwenye
mipango na shughuli, wamama wako kwenye mipango na shughuli, wababa wako kwenye
mipango na shughuli, waangalizi wa makanisa wako kwenye mipango na shughuli,
maaskofu na viongozi wako kwenye mipango na shughuli, Muda mwingi unaotumika ni
wa vikao vya mipango na shughuli wajkati mwingine vikao vya mipango na shughuli
ndio huwa vinakuwa virefu kuliko hata ibada yenyewe leo washirika wanakwenda
katika ibada lakini wakiwa wamejaa mawazo ya mipango na shughuli, penginepo
watatakiwa kutoa taarifa ya mipango na shughuli sasa haya nyanapozidi kuliko yale
tutakayoyatolea Hesabu atakapokuja mwana wa Adamu ndio yanaitwa mtego wa
Ibilisi na mtego huu una madhara yake angalia kisa kifuatacho:-
Baba Mtakatifu
Gregory the great (Pichani hapo Juu) wakati wa mwisho wa huduma yake ya
kichungaji alikuwa akitafakari kuhusu swala zima na kujishughulisha na mambo ya
wengine yeye alitumia mfano wa stori ya Dina katika Biblia hakutumia neno Mtego
wa shughuli nyingi bali alifananaisha na kile kinachomtokea mtu aliyenaswa na
mtego wa shughuli nyingi, alisema kwanza shetani hutoa mawazo yenye ushawishi
kwa mtu ili kumuhakikishia ulinzi na usalama wa uongo kwa kusudi la kumbomoa
mtu huyo polepole na mfano huu ni sawa na yake yaliyomtokea Dina.
Mwanzo 34:1-3 “Basi Dina, binti Lea,
ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi. Shekemu, mwana wa
Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri. Moyo
wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu
msichana kwa maneno mazuri.”
Dina alitoka kwenda
kuwaona mabinti wa nchi, kila mara mtu anapoacha kuifikiri nafsi yake na kuanza
kujishughulisha na wengine Shekemu mtawala wa dunia ataiwinda nafsi hiyo na
kuibikiri au kuitia unajisi, shetani nwakati wote huitia unajisi nafsi ya mtu
inayojishughulisha na mambo ya nje wakati mwingine bila yeye kujua na shetani
atazungumza na wewe kwa maneno mazuri, kwa sababu shetani anatufikiri sisi kuwa
watu wenye kufaa kwake shetani wakati
wote atatupa tumaini la uongo lakini hatima yake ni kututia unajisi tu, habari
ya Dina ni sawa na mtu anayeingizwa taabuni na shetani, Shetani ataendelea
kuzungumza vizuri na mtu anayejishughulisha na mambo ya wengine ili aweze
kumnasa katika mtego wake (Binti Bikira wakati wote huwakilisha Kanisa, Binti
za nchi huwakilisha wana wa dunia hii na Mfalme wao huwakilisha Mungu wa dunia
hii yaani Shetani)
Inawezekana tukawa
hatufanyi dhambi, lakini tukanaswa katika mtego wa shughuli nyingi, tukionana na kukutana na watu wa dunia hii wenye dhambi
na wakatutia unajisi kwaajili ya kushughulika nao, tunapaswa kulinda nafsi zetu
zisiondoke katika ushirika na Mungu, shetani anataka tuwe na shughuli nyingi (busy)
na shughuli za dunia tushughulike na wenye dhambi na kujisahau taratibu,
anataka atunase duniani taratibu tutapungua katika kusimamia neno la Mungu,
tutapungua katika kuomba, tutapungua katika kuhudumu, kuhudhuria ibada, kutenda
mema kuona wagonjwa, kuhudumia yatima, kujenga ushirika, kujenga umoja, kukuza
familia kuimarisha ndoa, kukuza ndugu kuonyesha kuwajali baba na mama na
washirika weengine, tutakuwa na shughuli nyingi kiasi cha kushindwa kusimamia
watoto wetu na malezi yao na masomo yao, tutakuwa na shughuli mno mpaka
tunachoka na kushindwa kuona umuhimu wa wa kuwa karibu na Mungu, Kumbuka Dunia
haibadilishwi na watu wanaobadilisha wengine bali inaweza kubadilishwa na watu
waliobadilika wao wenyewe kwanza, “unapojaribu
kubadilisha wengine utayeyuka mwenyewe kama sabuni” tunaposhughulika na
wengine tunaweza kuingia vilevile katika mtego wa kujilinganisha nao na kuona
aaa mimi sio mbaya sana ukilinganisha na hawa na shetani anaweza kutunasa
kijanja sana na kuzungumza lugha nzuri na sisi bila sisi kuelewa kuwa tumeingia
katika mtego wa shughuli nyingi,
Mtu aliyechoka kwa
shughuli nyingi anapoteza uwezo wa kuona mambo ya Msingi ya kiroho, Kutokana na
kuchoshwa kwa shughuli nyingi tunapoteza kujitambua kuwa sisi ni nani kwa
Mungu, tunaweza kujikuta tunapuuzima mambo ya msingi kwa sababu tu shughuli
nyingi zimetuzinga, mtu mwenye utulivu wa nafsi anaweza kuina kwa jicho lingine
na kuyapima mambo kwa uzito unaiostahiki kuliko mtu aliyechoka, Shetani anajua
nguvu zako na uwezo wako wa kiroho anajua kuwa unatambua mbinu zake zote kwa
kiwango kikubwa anajua uzoefu wako hivyo hawezi kukupata tena vilabuni, hawezi
kukupata tena kwa zinaa, hawezi kukupata tena kwa majaribu na mateso lakini
anajua akikuacha ufanye shughuli nyingi sana utachoka na kwa urahisi sana
atakubembeleza wakati umechoka na kukuchukulia kitu chako cha thamani kile
ambacho Mungu amekupa ni wakati gani Esau aliuza urithi wake wa Mzaliwa wa
Kwanza ni wakati amechoka na uwezo wa kufikiri umepungua
Mwanzo 25:29-34 “Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye
alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula
chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu.Yakobo
akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema,
Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? Yakobo
akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya
mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala,
akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya
mzaliwa wa kwanza.”
Jinsi ya kujitoa katika Mtego wa shughuli nyingi!.
Ni lazima tuchukizwe
na hali ya kudhalilishwa na kubakwa na na kunajisiwa na ibilisi na kukataa
kumuacha azungumze nasi lugha nzuri ya kutupendezesha, Lazima uamke na kujipima
na siku za mwanzoni mwa wokovu wako tulipokuwa tunaomba sana na kusoma neno la
Mungu sana mambo yalirahisishwa na wala hatukuwa na shughuli nyingi, sasa
angalia tuna shughuli nyingi lakini je tunaomba kama zamani je haujihisi
kupungukiwa na kitu? Sasa basi tufanye nini lazima tukubali kujipima sawa na
neno la Mungu!
Ni lazima
tujishughulishe sana katika kuomba ili Mungu atuepushe na mtego wa shughuli
nyingi na kuhakikisha kuwa hatukubali kuwa washirika wa shughuli nyingi na kumpa Ibilisi nafasi, jambo moja la
msingi la kukumbuka ni kuwa mtu mwenye shughuli nyingi ni mawindo rahisi sana ya
ibilisi, kwa kuwa tunaangalia sana mambo ya wengine kiasi cha kusahau kuangalia
mambo yako mwenyewe, ni rahisi kunajisiwa na kuingia katika taabu kwa sababu ya
kushughulika na mambo ya wengine, unaweza tu kusahaulishwa na ule mpango wa
ibilisi wa kukulinganisha kuwa hata hivyo mimi sio mbaya sana ukilinganisha na
wengine, unaweza tu kujifikiri kuwa wewe ni bora sana ukijilinganisha na
wengine kumbuka kuwa kiwango cha ubora wetu si watu wengine bali ni Yesu Kristo
yeye ndio kielelezo chetu na kiwango cha ubora wetu na ni kupitia neema na
rehema tunaweza kufikia kiwango chake tatizo kubwa la watu walioingia katika
mtego wa shughuli nyingi ni kuwa wanajishughulisha sana na mambo ya wengine na
wanasahau kujihukumu wenyewe kwa msingi huo basi ni muhimu kwanza
1.
1Wakoritho 11:31 “Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa.” Kila mtu aliyeokoka
anapaswa kujipima mwenyewe na kujiangalia mara kwa mara kwamba yuko katika
kiwango gani cha kumpenda Mungu na kuacha shughuli nyingi na kujitoa zaidia
katika dua na sala na maombi na kulia sana machozi
2.
Tunapaswa kujilinda na kujihami na sifa tunapofanya
kazi ya Mungu wakati mwingine watu watatusifu na wenye mahitaji yao wengi
watatujia tutajikuta tunawahudumia sana wao na kusahau kuwa nguvu za
kuwahudumia hazitokani na nafsi zetu tuuige mfano wa Yesu ambaye mara kadhaa
alijitenga na umati wa watu waliokuja kwa nia njema ili awahudumie lakini yeye
alikumbuka kwenda kuomba angalia Luka 5:15-16
“Lakini habari zake
zikazidi kuenea, wakakutanika makutano mengi wamsikilize na kuponywa magonjwa
yao. Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba.” Leo hii wako watu wanafanya huduma na kushinda wakishughulika na
watu kuanzia asubuhi mpaka jioni wanasahahu kuwa ni mtego wa shughuli nyingi
Yesu alikumbuka mara kwa mara kujiepusha na kwenda kuomba
3.
Kila unapojiandaaa na jukumu kubwa ni muhimu
kutanguliza maombi, Dr David Yong Cho wa kanisa la Full Gospel of Yoido kule
Korea kusini huomba masaa matatu asubuhi kabla ya kuingia katika shughuli za
kila siku, Martin Luther aliomba masaa matatu asubuhi kabla ya kuingia katika
shughuli za kila siku Yesu mwana wa Mungu kwa maandalizi ya huduma yake
alifunga na kuomba kwa siku 40 Luka
4:1-2, 14-15 “Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani,
akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na
siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa.” “Yesu akarudi kwa
nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za
kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu
wote.”
4.
Ni muhimunpia kuwaamini wengine na kugawa majukumu
si vema kila kitu ukakifanya wewe, kwa mamlaka uliyonayo unaweza kuwapa
majukumu wengine na kuwaelekeza wakafanya kama ambavyo wewe ungefanya Yesu aliwatuma wale 12 na wakafanya kazi
nzuri wakamletea ripoti na akawaagiza wapumzike ona Marko 6:30-32 “Na mitume wakakusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote
waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha. Akawaambia, Njoni ninyi peke
yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu
walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula.Wakaenda
zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu.” Unaona Yesu
alitambua kuwa watu wanaofanya hduma wabahitaji muda wa kuwa faragha na
kupumzika
5.
Kunapokuwa na mambo ya kuhuzunisha au habari ngumu
pia huna budi kuhakikisha kuwa unajitenga na shughuli nyingi upate nguvu mpya Mathayo 14:1-13 “Wakati ule mfalme Herode
alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, Huyo ndiye Yohana
Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani
yake. Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa
ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye. Kwa sababu Yohana alimwambia, Si
halali kwako kuwa naye. Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona
Yohana kuwa nabii. Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti
Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya
kwamba atampa lo lote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema,
Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika;
lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani
pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani. Kichwa
chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye. Wanafunzi
wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha
Yesu habari. Naye Yesu aliposikia; hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda
mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu
kutoka mijini mwao.”
6.
Hatuwezi kufanya maamuzi muhimu huku tukiwa katika
shughuli nyingi ni muhimu kukumbuka kuwa kila maamuzi muhimu yanahitaji maombi
ili kwamba Mungu aweze kuingilia kati, viongozi nwengi sana wamefanya maamuzi
mengi mabaya bila kufikiri wala kuwaza kwa sababu wako kwenye mtego wa shughuli
nyingi kisha linawajia jambo linalohitaji maamuzi na wanaamua bila kuwa katika
uwepo wa Mungu Yesu alipotaka kuamua
hata kuchagua viongozi aliomba usiku kucha Luka
6:12-13 “Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku
kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake;
akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume;”
7. Tunapokuwa
na Msongo wa mawazo inatupasa kuomba kwa masaa ya kutosha na hasa tunapotambua
kuwa kuna mambio magumu mbeleni yanatukabili Luka 22:39-44 “Akatoka akaenda mpaka mlima wa
Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye. Alipofika
mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe akajitenga
nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa
ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako
yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu. Naye kwa vile
alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya
damu yakidondoka nchini.]”
8. Kumbuka
wakati wote Maombi ndiyo yanayotuweka karibu na Mungu, kusoma neno la ke na
kulitafakari na kumtii yeye hutupa nguzu za rohoni kwa hiyo ni muhimu sana
kwetu kuhakikisha kuwa tunaufurahia uwepo wa Mungu zaidi ya kukubali kuwa na
shughuli nyingi Luka 5:16 “Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na
watu, akaomba."
Kama tutakuwa na shughuli nyingi na Mungu, Mungu ataweka wepesi
katika yale tunayoyashughulikia kwa hiyo tusikubali kuingia katika mtego wa
shughuli Nyingi
Mchungaji: Innocent
Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni