Alhamisi, 13 Agosti 2020

Imba wewe uliye tasa!

Isaya 54:1-4Imba, wewe uliye tasa, wewe usiyezaa; paza sauti yako kwa kuimba, piga kelele, wewe usiyekuwa na utungu; maana watoto wake aliyeachwa ni wengi kuliko watoto wake yeye aliyeolewa, asema Bwana. Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze; ongeza urefu wa kamba zako; vikaze vigingi vya hema yako. Kwa maana utaenea upande wa kuume na upande wa kushoto; na wazao wako watawamiliki mataifa; wataifanya miji iliyokuwa ukiwa kukaliwa na watu. Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena”.


Utangulizi.

Katika changamoto mbaya sana duniani, tunazoweza kuorodhesha na zinazotesa sana watu utasa inaweza kuwa mojawapo, Utasa ni moja ya tatizo baya sana katika historia ya mwanadamu, utasa ni hali ya mwanamke au mwanaume kushiriki tendo la ndoa bila kinga yoyote kwa zaidi ya miezi kumi na mbili bila kupata matokeo!, Tatizo la utasa ni tatizo gumu sana na linaweza kusababishwa na kutokuwa sawa kwa homoni za mwanamke au mwanaume kunakopolekea kuleta shida katika mfumo wa uzazi. Tatizo kubwa linalozaliwa ni uwezo mdogo wa kubeba ujauzito na kunaweza kusiwepo ugonjwa mwingine. Kwa kuwa utasa sio ugonjwa lakini ni tatizo na lina uwezo wa kuathiri eneo kubwa sana la maisha ya mwanadamu, linasababisha kuweko kwa Mauvimbe ya ajabu kuzalishwa tumboni, fadhaa kubwa kwa mtu anayehitaji matokeo, matatizo ya kisaikolojia, wasiwasi, kupoteza matumaini, msongo wa mawazo, hatia, na kujihisi kama mtu usiyefaa kitu na hata kujisikia kufa, licha ya matatizo ya ndani anayoyapitia mtu aliye tasa pia kuna shutuma kutoka nje wanazopitia watu wasio na uwezo wa kuzaa

Wataalamu wa maswala ya uzazi wanaeleza kuwa katika utafiti walioufanya kwa wagonjwa 200 wanandoa wanaohudhuria clinic kwaajili ya kutaia uzao asilimia 50% ya wanawake na asilimia 15% ya wanaume walibainika kuwa na matatizo ya kiakili yaani kisaikolojia, aidha walipitia aina fulaninya mateso na manyanyaso na hayo yaliwapotezea furaha na kusababisha utasa, aidha katika utafiti mwingine wanawake 488 waliokuwa na tatizo la utasa walipoulizwa maswali walibainika kuwa na tatizo la msongo wa mawazo linalopelekea wao kuwa tasa.

Kwa ufupi utasa ni tatizo baya sana  ambalo wakati mwingine matabibu hawana uwezo nalo, na wakati mwingine ni Mpaka Mungu mwenyewe aingilie kati, Katika jamii ya Israel Mtu alipokuwa tasa alinyanyaswa sana na alijiona duni na mtu asiyefaa katika Israel utasa lilikuwa ni kama jambo la aibu kubwa na fedhea na watu waliokuwa tasa walinyanyapaliwa hata na wanawake wenzao kwa hiyo maumivu ya wanawake tasa katika jamii yalikuwa makubwa na yenye uchungu mno

a.       Sara alinyanyaswa na kijakazi wake ambaye alishika mimba ilihali bibi yake akiwa hana kitu mara baada ya hajiri kupokea ujauzito alimdharau sana Sara na kumdhihaki huku akijiona yeye kuwa ni bora zaidi ona Mwanzo 16:1-5Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake. Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe.”

b.      Rebbeca alikuwa ni mwanamke mwingine anayetajwa katika Biblia kuwa alikuwa tasa mwanamke huyu kutokana na manyanyaso katika jamii alimsumbua mumewe akimwambia nipe watoto, alilewa Isaka akiwa na miaka 40 na alipata mtoto akiwa na mika 60 ona Mwanzo 25:20-26Isaka akawa mwenye miaka arobaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake. Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba.Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yamo tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo. Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake. Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau. Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake unamshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa.”

c.       Hanna aliteseka na hali ya utasa inaonekana mumewe pamoja na upendo mkubwa sana alishauriwa aoe mke mwingine na kama haitoshi mwanamke huyo alizaam, Hana hakuwa na mtoto hivyo alichokozwa na kutendewa vibaya na mke mwenza hali hii ilisababisha maumivu makubwa sana        kiasi cha kumfanya mwanamke huyu kushinda hekaluni akilia na kumuomba Mungu ona 1Samuel 1:1-10Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea Bwana wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa Bwana, walikuwako huko. Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, waume kwa wake, sehemu zao; lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo. Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo. Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa Bwana, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula. Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi? Ndipo Hana akainuka, walipokwisha kula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la Bwana.Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana.”

Unaona wanawake hao na wengine wengi wanatajwa katika maandiko kuwa walipitia changamoto ngumu sana ya utasa, utasa ni tatizo bay asana kila mwanadamu na mwanamke mwenye akili timamu anatamani kuzaa, tena anatamani kuzaa kwa kiwango cha kutosha uzao ni Baraka kubwa nay a kwanza ya mwanadamu Mwanzo 1:28 “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.” ili mwanadamu aendelee kuwepo juu ya uso wan chi anapaswa kuwa na uzao, uzao ndio unaoendeleza ukoo, mali na shughuli zote ntunazozifanya zitakosa warithi kama hatuna uzao, Mungu akikupa uzao amekupa urithi juu ya nchi  amekupa silaha tena hasa watotowanaozaliwa ujanani Zaburi 127:3-4” Tazama, wana ndio urithi wa Bwana, Uzao wa tumbo ni thawabu. Kama mishale mkononi mwa shujaa, Ndivyo walivyo wana wa ujanani.” Kukosa watoto ilihesabika kama adhabu kubwa sana duniani ilikuwa kama laana, utasa ni kitu kibaya sana aidha pia kuharibika kwa mimba ni tukio bay asana Mungu aliwaahidi watu wake kama watamtumikia ataondoa kabisa utasa kabisa na kuwa hatakuwako aliye tasa wala mwenye kuharibu mimba ona Kutoka 23:25-26 “Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako.   Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.

Katika mstari wa msingi Mungu analiona taifa la Israel na mataifa mengine na kumtumia Isaya nabii kuwaletea habari njema Israel walikwenda utumwani, katika hali ngumu sana wakidharauliwa na watu kama ilivyo kwa mwanamke aliye tasa, Na mataifa mengine wakiwa kama mwanamke asiyeolewa kila mmoja kwa jinsi yake anapitia hali Fulani katika maisha ambayo haizai, inaweza kuwa taifa, inaweza kuwa mtu, unapokuwa na hali ya umasikini, kile unachotaka kukitimiza au kukifanya hakifanikiwi, uko katika hali ya kushindwa kuzalisha au mipango isiyofanikiwa ni kama unataka mpenyo na hupati mpenyo unaokusudiwa hiyo ni hali ya utasa, huna furaha huna amani ni hali ya utasa, huna unalilifanya likafanikiwa ni hali ya utasa Nabii Isaya anawataka wote wanaopitia hali kama hiyo waimbe kwa maana Mungu anaahidi kuuondoa utasa, utasa ni tatizo ambalo linaweza kukabiliwa na Mungu pekee, yeye ndiye anayeweza khbadili hali ya mambo katika maisha yako, huduma yako, ukoo wako kijiji chako, taifa lako, familia yako, kushindwa kuzalisha kumekuletea fadhaa kubwa Isaya anasimama leo kutoa habari njema anasema imba wewe uliye tasa kwa maana watoto wako ni wengi mno watoto wako wanakuja , hakuna sababu ya kufadhaika yeye aliyebadili maisha ya Sara, akabadili maisha ya Rebbeka, akabadili maisha ya Hanna akabadili masiha ya Manoa akabadili maisha ya Elizabeth ana uwezo wa kubadili maisha yako leo na kuyafuta machozi yako na kukufanya uwe productive uwe mwenye faida mahali ambako umeonekana huna faida yoyote Mungu anajua fadhaa zako anajua uchungu wako anajua unayoyapitia na yuko tayari kutoa msaada unaolinga na na mahitaji yako! Kwa kawaida mambo yanapokuwa magumu mwanadamu hulia na hawezi kuimba lakini Isaya anatangaza mtu aimbe mtu achangamke kwa kuwa bwana anaahidi kubadilisha mambo katika maisha yako! Ni maombi yangu kuwa unapomaliza kusoma ujumbe huuu Mungu abadilishe mtazamo wako na kukupa uzao, uwe ni uzao wa tumbo lako, huduma yako, kanisa lako, biashara yako, kazini kwako shambani kwako na amani yako Mungu na akufanie muujiza akupobnye na kuondoa fedhea katika kila eneo la maisha yako akupe nguvu kwa upya ili uwe na uzalishaji katika maisha yako amen!

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: