Mathayo 12: 38-42 Biblia inasema “38. Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako. 39. Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. 40. Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi. 41. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona. 42. Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.”
Yesu Kristo akitambua hilo alitoa hutuba kali sana ya maonyo dhidi ya watu wanaopinga kazi ya Mungu Roho Mtakatifu, na zaidi ya yote aliwaonya watu kuhusu kuzungumza maneno yasiyo na maana kwa vile watatoa hesabu kwa kila neno lisilo na maana wanalolitoa katika vinywa vyao,
Mathayo 12:33-37. “Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana. Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa”
Baada ya hutuba hii ya Yesu ambayo ilikuwa kali na yenye maonyo baadhi ya Mafarisayo waliogopa sana Lugha “Hapo” inatumika kuonyesha kuwa iliwalazimu sasa waombe ishara ya kumfahamu Yesu vema kuwa yeye ni nani, Tupe ishara itakayotusaidia kukutambua wewe ni nani? Ndipo Yesu aliwajibu kwamba watamtabua kupitia Ishara kuu mbili.
1. Ishara ya Nabii Yona.
Yesu aliwaeleza kwa uwazi kuwa Ishara ya kumtambua Masihi iko wazi, ishara hii ndiyo iliyowavutia watu wa Ninawi wakatubu na kumgeukia Mungu kupitia mahubiri ya Yona, Mathayo 12:38-41, “Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako. Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona.”
Kimsingi Yesu alitaka kukazia kuwa kile kilichomtokea Yona kilikuwa ni ishara halisi, na kilikuwa ni kivuli cha kumtambua Masihi, ambaye Yesu alikazia kuwa ni mkuu kuliko Yona, Yesu alikazia kuwa namna njema ya kumtambua yeye ni pale atakapokufa na kufufuka siku ya tatu, hii ndio kazi kubwa ya ukombozi itakayowavuta wengi katika ufalme wa Mungu. Nguvu kubwa ya masihi ni kukishinda kifo, kuishinda mauti, hii ni ishara kubwa waliyopewa watu.
2. Ishara ya Malkia wa Sheba.
Yesu aliwapa Mafarisayo Ishara nyingine ya muhimu. Ambapo sasa anaeleza kuhusu Malkia wa kusini yaani Sheba kwamba alitoka mbali sana pande zamwisho wa Nchi kuja kusikiliza Hekima ya Sulemani, Yesu ni kama alikuwa anakazia kuwa njia nyingine ya kumtambua ni kumsikiliza, usikivu ungeliwasaidia kujua kuwa hakuna mwingine anayeweza kunena au kutenda katika kiwango kama cha Yesu, Mathayo 12:42 “ Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.”
hata hivyo mahali hapa ndipo paliponisukuma zaidi kufanya Uchambuzi hususani Yesu alipohitimisha kuwa malikia huyu alisafiri kutoka mbali kusikiliza Hekima ya Sulemani, hata hivyo Yesu alitamka wazi kuwa Yeye ni mkuu kuliko Sulemani.
Suleimani ni mfalme aliyeishi kwa anasa na ufahari wa hali ya juu, mfalme huyo alikuwa na Hekima na ufahamu na maarifa ya hali ya juu sana kuliko wafalme wote ambao wamepata kuweko, Biblia inasema kabla yake hajakuweko na badala yake hatokuweko 1Wafalme 3:9-13, “Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi? Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili. Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu; basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe. Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.”
1Wafalme 4;29-34 “Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani.Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, na hekima zote za Misri.Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka. Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano. Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki. Wakaja wa mataifa yote ili waisikie hekima ya Sulemani, toka wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamepata habari za hekima yake.”
unaweza kuona!, wengi waliosikia Hekima ya Suleimani katika enzi zake walisafiri kutoka mbali ili kwenda kumsikiliza, Lakini ziara ya kifahari na maarufu sana na iliyoelezewa kwa kina ni safari ya Malkia wa Sheba au Ethiopia ambaye alikwenda kwa mikogo mingi na mikubwa 1Wafalme 10:1,”Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la Bwana, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo.” 2Nyakati 9:1-6 “Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani, alikuja ili amjaribu Sulemani kwa maswali ya fumbo huko Yerusalemu, mwenye wafuasi wengi, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akamwambia mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala halikuwako neno alilofichiwa Sulemani, asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima ya Sulemani, na nyumba aliyoijenga, na vyakula vya mezani mwake, na kikao cha watumishi wake, na usimamizi wao wangoje wake, na mavazi yao; na wanyweshaji wake, na mavazi yao; na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana; roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia.”
Biblia inasema malkia huyu alikwenda akiwa na maswali magumu sana The Amplified Bible inasema kwa lugha ya kiingereza“She came to Jerusalem to test him with Hard Questions” na Biblia ya kiingereza ya NIV “she came to Prove Solomon with Hard Questions” pamoja na ziara yake ya kifahari na zawadi kibao alizozibeba alipofika Yerusalem kwa Suleimani alijibiwa maswali yake yote na mambo yake yote hata aliyokuwa ameyaficha sirini, hakuna kilichofichika kwa Suleimani, alitosheleza mahitaji yake yote na hisia zake zote zilijibiwa na kuzidi.
Dunia ya leo ina maswali magumu mengi yasiyo na majibu, pamoja na kuendelea na kukua kwa maarifa na uvumbuzi wa kisayansi na Teknolojia, Watu wanazidi kuharibikiwa dunia imejawa na hekima ya uharibifu, wizi, ufisadi, uchochezi, uchoinganishi, majungu na fitina, kuliza wengine, kutoa mimba udanganyifu, na hakuna majibu ya maswala muhimu katika matatizo ya watu, Sulemani alikuwa na ujuzi zaidi ya wa kibailojia, Chemistry, Physics, aliishi kwa anasa kuliko mtu yeyote, mwisho aliona hekima na maarifa bila ya Mungu ni upuuzi au ubatili, alishauri watu kumkumbuka Muumba wao siku za ujana wao, Muumba huyu ndiye mkuu kuliko Sulemani, Yesu Kristo anatajwa kama Hekima yetu
1Wakoritho 1:30 “Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi;”
kwa kiyunani Epignosis sofia, Full of wisdom Knowledge and Understanding, Yesu aliposema Hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani alimaanisha Yeye ndiye aliyemuumba huyo Sulemani, Yeye ndiye mwenye majibu yote hata ya mambo magumu, Yeye ndiye Masihi, ni zaidi ya mfalme Sulemani, watu watatoka kila pande za dunia kumjia yeye, na atawahukumu wote waliomkataa yeye atakuwa na majibu ya kutosha na kushangaza ulimwengu kwa hao wanaomjia
Hapa yupo aliye mkuu Kuliko Sulemani.
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.
0718990796
ikamote@yahoo.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni