Warumi 8:35-39 “Ni nani atakayetutenga na
upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari,
au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa,
Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote
tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba,
wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo,
wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho
chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana
wetu”
Utangulizi:
Nyakati za kanisa la Kwanza na
hata katika siku zetu za leo ni rahisi sana watu kufikiri kuwa wanapopitia
mambo magumu au changamoto za aina mbalimbali hudhani kuwa labda Mungu huwa anaadhibu
au anakomesha au amepunguza upendo wake kwetu, Lakini ni muhimu kufahamu kuwa
hakuna kituchochote tunachokipitia ambacho kinaweza kumaanisha kuwa Upendo wa
Mungu umepungua kwetu HAPANA, Paulo
Mtume alikuwa anawaandikia Wakristo wa makanisa ya Rumi na maeneo mengine ambao wakati huo
walikuwa wakipitia majaribu ya namna mbalimbali na kuwataka wajifunze kuwa
hakuna jambo baya linaloweza kumtokea mtu wa Mungu kisha likamaanisha kuwa labda Mungu amemuacha ! Paulo aliandika
waraka huu akitaka kuitambulisha injili anayoihubiri hasa kwa sababu alitaka
kufika rumi mara kadhaa lakini shetani alimzuia, na katika kutaka kuwafikia
aliandika waraka huu akiwafunulia maswala mbalimbali anayoyahubiri na pia
alitaka kujibu maswali kadhaa ikiwa ni pamoja na hoja ya kuteseka kwa wakristo
ili wakristo wasijenge dhana kuwa au
labda upendo wa Mungu umepungua na kuwa njia ya Mungu ni njia sahihi, Kulikuwa na maswali kadhaa wa kadhaa kwamba
mbona sasa tumefuata njia iliyo njema
lakini Serikali ya kirumi na mahakama zilizokuwepo zilikuwa na wakuu wa dini
walikuwa kinyume na Imani hii,
1. Je
kweli imani hii ni sahihi? Kweli Mungu yuko upande wetu?
2. Kweli
Mungu anasikia maombi na kukutana na mahitaji yetu
3. Mbona
watu wa Mungu wanashitakiwa?
4. Mbona
sasa watu wa Mungu wanahukumiwa?
5. Na
je njia sahihi ni kuachana na imani ?
Maswali hayo yalilitatiza sana
kanisa la kwanza kwa sababu walikutana na upinzani mzito kwaajili ya injili na
hivyo Mitume wliifanya kazi ya kujaribu kulijibu swali hilo kwa ufasaha Matendo
4:1-3, 23-26
Matendo 4:1-3, “Hata walipokuwa wakisema na
watu wale, makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo wakawatokea, wakifadhaika
sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu.
Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni.”
Matendo 4:23-26 “Hata walipofunguliwa,
wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu
wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo
mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na
bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha
babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila
wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri
pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake.”
Kwa kadiri imani katika Kristo
ilivyozidi kuenea hali ilizidi kuwa ngumu sana, kwani wakristo walipigwa kwa
mawe na kuuawa na kutiwa magerezani na
hivyo kuendelea kuleta maswali mengi sana miongoni mwa wanatheolojia wa wakati
ule ya kwamba imani ni nzuri lakini mbona inaleta majaribu magumu na maswali
yasiyoweza kujibika ?
Matendo 8:1-3 “Siku ile kukatukia adha kuu
ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya
Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano,
wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba,
na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani ”
Dhiki na mateso, usumbufu na
taabu zilizokuwa zinalikumba Kanisa la kwanza zilipelekea Mitume kujenga hoja
na kujibu hoja ili wakristo waweze kuelewa kuwa kinachowatokea kina maana pana sana
katika Mungu:-
1.
Wasione
ni ajabu 1Petro 4:12 “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu
ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni
kitu kigeni kiwapatacho.”
2.
Imani
huwa inajaribiwa 1Petro 1:7 “Nanyi mnalindwa na
nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa
wakati wa mwisho. Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo,
ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;”
3.
Dhiki
inatuumbia uwezo wa kuvumilia Yakobo 1:2-3 “Ndugu
zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali;
mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na
kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.”
4.
Ufalme
wa Mungu sio bei rahisi Matendo 14:
21-22 “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika
mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na
Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani,
na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.”
5.
Hakuna
wa kututenga na Upendo wa Kristo Warumi 8:35-39 “Ni
nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au
njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili
yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini
katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye
aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua
hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka,
wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala
yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa
Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu”
Kwa sababu hiyo ni Muhimu kufahamu kuwa kwa kadiri unavyojitoa kwa Mungu na kuendelea kuwasaidia wengine kukua katika imani na kwa kadiri siku zinavyokwenda utagundua kuwa njia ya Mungu sio nyepesi kama tunavyoweza kudhani lakini hatuna budi kuhakikisha kuwa tunafurahia wakati wote na wala hatupaswi kuhuzunika Pale Mungu wetu anaporuhusu Mambo yakawa tofauti na namna tunavyodhani, hivyo ni muhimu kuufahamu upendo wa Kristo katika kile eneo na kukumbuka kuwa wakati wote tunapopitia sintofahamu ya aina yoyote ile Mungu yuko Karibu mno kuliko tunavyodhani, usifikiri kuwa hayuko upande wetu, usifikirikuwa hatakutana na mahitaji yetu, Usifikiri kuwa kuna mwanadamu anaweza kutuhukumu, wala usifikiri kuwa Upendo wa Mungu umepungua kwetu upendo wa Mungu ni mpana sana na wakati wote anaandaa Mambo mazuri zaidi kwaajili yetu. Hakuna lolote lenye nguvu ya kututenga na upendo wa Mungu. Wakati mwingine kwa kadiri unavyojitoa zaidi kwa Mungu ndivyo unavyokutana na changamoto zilizokubwa zaidi 2Wakorintho 11:21-33, CV ya ufalme wa Mungu inatengenezwa kwa kupitia mambo magumu na sio hizi changamoto ndogo ndogo.
Na Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima .
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni