Jumanne, 17 Septemba 2024

Msaidizi Mwingine!


Yohana 14:16-18 “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu.”



Utangulizi:

Leo tutachukua Muda tena kujifunza kwa kina na mapana na marefu, tukikazia tena na tena umuhimu wa Mungu Roho Mtakatifu katika maisha yetu, Ambaye Bwana Yesu alimuita Msaidizi mwingine, kanisa ni muhimu sana sana kufahamu na kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu kwa sababu yeye ni msaada mkubwa sana wa kutuondolea mashaka na kutupa neema ya kuishi kwa Amani.

Yohana 14:16-18 “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu.”

Wanafunzi wa Bwana wakiwa pamoja naye katika karamu yake ya mwisho pamoja nao. Yesu anawaeleza kuwa amekamilisha kazi aliyotumwa na baba na kuwa kilele cha kazi aliyotumwa ni kufa msalabani kwaajili ya wengi, wanafunzi waliposikia kuwa Yesu anazungumza maswala mengi yanayohusu kuhitimisha huduma yake duniani, walipata mashaka na huzuni nyingi, walifadhaika na kujiona kupwaya na kuwa dhaifu, itakuwaje maisha yao bila Yesu?, nani atakuwa pamoja nao, nani atawasaidia, nani atawashauri, nani atakuwa karibu nao, nani atawatia moyo, nani atawafundisha na kuwaelekeza, na wanawezaje kuukabili ulimwengu ambao ni mgumu bila msaada wa Mungu, kukabiliana na wakuu wa dini za kiyahudi, kukabiliana na upinzani wa kiimani na kidhehebu, watu wenye kuipinga injili na habari za Mungu, akijua kila kilichokuwa kinaendelea katika mioyo yao, Yesu aliwathibitishia kuwa atamuomba baba naye atawapa msaidizi mwingine ili akae nasi milele.

Roho Mtakatifu ndiye Msaidizi huyo, Roho Mtakatifu ni wa Muhimu sana sana katika maisha yetu, hakuna lugha ya kuweza kuelezea vya kutosha lakini ikiwa Yesu anasema yafaa au yatufaa au yawafaa yeye aondoke kwa kuwa asipoondoka msaidizi hatakuja kwetu, maana yake Msaidizi huyu ni wa Muhimu na msaada ulio karibu zaidi tukinena kiwazimu kuliko uwepo wa Yesu Kristo duniani, Uwepo wa Yesu Kristo duniani akiwa kama mwanadamu ulimfunga na kumpa mipaka ya kuwepo katika inchi ya Israel tu, vilevile kutokuweza kukaa moyoni mwa kila muumini, Lakini uwepo wa Roho Mtakatifu ambaye hayuko katika mwili, unamuwezesha kuwepo kila mahali na kuwepo ndani ya moyo wa kila aaminiye na kutimiza mambo makubwa sana katika kiwango kile kile alichokuwa anakifanya Yesu Duniani kwa uweza wa Roho Mtakatifu, Ndio maana Yesu akasema yafaa yeye aende, ili Roho Mtakatifu aweze kuchukua nafsi na kukaa nasi hata milele unaona ?

Yohana 16:6-7 “Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu. Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.”

Neno yawafaa, au yafaa Katika kiingereza linatumika neno expedient ambalo kwa kiyunani linasomeka kama Sumpherō ambalo tafasiri yake kwa kiingereza ni to be good, Be profit, be profitable, be better yaani kwa Kiswahili, yafaa, ni afadhali, ni faida, ni vema zaidi, ni bora zaidi kwa hiyo kuondoka kwa Yesu ni bora zaidi, ili aje Roho Mtakatifu kuliko kuendelea kuweko kwa Yesu Duniani, katika jinsi ya mwili, ikiwa Yesu aliona umuhimu wa swala hili basi kanisa ni muhimu kwetu kuelewa kuwa Yesu alikuwa Mwalimu bora zaidi kuliko wote duniani, ni mwafalasafa mkubwa zaidi kuliko wote, ni mtenda miujiza mikubwa kuliko mtu awaye yote duniani ana sifa ambazo hakuna mwanadamu awaye yote anazo duniani lakini anasema ni afadhali yeye aende kuliko kubaki ili aje Roho Mtakatifu ambaye ndiye msaidizi, basi kuna umuhimu mkubwa sana wa kulizingatia hili, kwa sababu hiyo leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu somo hili muhimu Msaidizi mwingine kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Msaidizi mwingine.

·         Umuhimu wa kuwa na Msaidizi mwingine.

·         Jinsi ya kuwa na msaidizi mwingine.     

Msaidizi mwingine

Yohana 14:16-18 “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu.”

Msaidizi mwingine anayetajwa katika maandiko haya ni Roho Mtakatifu, neno Msaidizi mwingine katika kiingereza linatumika kama neno “Another Comforter” ambalo kimsingi katika kiyunani linasomeka kama Parakletōs  ambalo katika kiingereza tafasiri zake ni Consoler, an intercessor, advocate, tafasiri zake one called to the side of another for the purpose of helping him in any way Kwa Kiswahili sasa maana ya Msaidizi mwingine ni Mfariji, mtetezi, mwanasheria, wakili, rafiki, na mshauri, Kwa hiyo ni wazi kuwa Yesu anamuelezea Roho Mtakatifu kama nafsi nyingine itakayosimama kwa niaba ya kanisa na kuwatetea, kuwafariji, kuwatia nguvu, kuwashauri na kuwapa cha kusema au kusema kwa niaba yao hata wanapokuwa katika kumbi za kimahakama, au katika mabaraza na mbele ya maliwali, Roho Mtakatifu atakuwa kama wakili wakati huo. Na sio wakili atakayehitaji malipo bali anayefanya hivyo kwa sababu ya upendo wake Mungu, na kuwashauri watu wake kipi cha kutamka na kwa jinsi gani watamke na kuwashinda wale wanaowashambulia, Biblia ya kiingereza the Amplified Bible inatumia maneno haya katika kiingereza  And I will ask the Father, and he will give you another Helper (comforter, Advocate, Intercessor, Counselor, Strengthener, standby ) to be with you forever ” na Biblia ya kiaramu the Aramaic Bible inasema hivi katika kiiingereza “ And I shall request from my Father and he will give you another Redeemer of the accursed, that he will be with you for eternity” kwa hiyo Roho Mtakatifu ni Mfariji, ni wakili, ni muombezi, ni kiongozi, ni mtia moyo, ni msaada ulio karibu, Roho Mtakatifu ni Mkombozi mwingine dhidi ya mshitaki wetu. Kwa hiyo Roho Mtakatifu ambaye atakaa ndani yetu atatusaidia kutimiliza kile kile ambacho Kristo angetenda akiwa pembeni yetu.

Mathayo 10:17-20 “Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.”

Matendo 6:8-10 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano;lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.”

Katika lugha ya kiebrania neno hilo Msaidizi linatajwa kama neno “Ezer” ambalo maana yake ni Msaada au msaada ulio karibu kwa hiyo Roho Mtakatifu ni Msaada ulio karibu, ni msaada wa kimwili na kiroho  na kihekima na kiushauri na kimuelekeo, na kiuaffanuzi, na kiualimu, na hutusaidia katika udhaifu wetu, hutusaidia na kututia nguvu wakati wa mateso na kutuongoza katika kweli yote, Kimsingi Roho wa Mungu ni msaada kamili kama ule tu ambao ungepatikana kwa Mungu baba na Mungu mwana yaani Yesu kristo. Roho Mtakatifu ndani yetu katika roho ni muhimu kuliko Yesu Kristo pembeni yetu katika mwili.

Zaburi 46:1-2 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.”

Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.”

Kwa hiyo Roho Mtakatifu ni msaada wa karibu katika kutoa ushauri wa hekima, ushauri wa nini cha kusema, kipi cha kufanya, anazungumza kwa niaba yetu, anashughulika kwa niaba yetu, anatutia nguvu, anatupa wepesi anatusaidia wakati wa majaribu na wakati wa mambo magumu, na wakati wa mateso, na wakati wa hatari, na wakati wa upinzani, kwa maana nyingine msaada ule ule aliokuwa akiutoa Yesu Kristo alipokuwa Duniani pamoja na wanafunzi wake, ndio msaada anaoutoa Roho Mtakatifu kwa kila mwamini kokote aliko, na msaada ule ule anaoutoa Mungu baba tunaupata kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu, kwa hiyo utaweza kuona umuhimu wake katika maisha yetu

Ni muhimu vile vile kufahamu kuwa neno Msaidizi mwingine yaani neno mwingine katika kiyunani linatumika neno “Allos” ambalo maana yake, The other, another, more one, yaani mwingine, tofauti na Yesu lakini akiwa katika kiwango kimoja au sawa na yeye kwa hiyo lugha hii pia inatufundisha kuwa huyu Msaidizi mwingine yaani Roho Mtakatifu ni nafsi tofauti na Yesu na ni nafsi nyingine tofauti na Baba lakini ni watenda kazi pamoja katika kukamilisha kusudi lile lile na hii inatuthibitishia kuwepo kwa utatu wa Mungu katika maana nyingine angalia maneno yale  Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwinginehii inathibitisha ukweli kuwa yuko Baba, Mwana na Roho Mtakatifu kwa hiyo mafundisho kuhusu utatu wa Mungu sio swala la kizushi lakini ni fundisho jepesi na rahisi la kimaandiko na bwana hajawahi kutukemea au kutufunulia kuwa hakuna usahihi katika hilo,

Mathayo 28:19-20 “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

Luka 3:21-22 “Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”

Kwa hiyo msaidizi mwingine huyu ni nafsi nyingine mbali na baba na mwana Huyu ni Roho Mtakatifu, ukweli huu kuhusu namna Mungu alivyo katika utatu haupingiki kimaandiko kwa sababu neno la Mungu ndio linavyotuambia na kutuelekeza na kutufundisha, kwa hiyo Msaidizi mwingine ni Roho Mtakatifu, ni Roho wa Mungu, ni Mungu ndani yetu.                        

Umuhimu wa kuwa na Msaidizi mwingine

Ni muhimu kufahamu kuwa kuna umuhimu mkubwa sana wa kila mtu aliyeokolewa kuwa na uhusiano na Msaidizi mwingine yaani Roho Mtakatifu, Yesu alikuwa na maana pana sana ya kusisitiza kuwa atamuomba Baba ili atupatie Msaidizi mwingine yaani Roho Mtakatifu ili akae nasi, Yesu alikuwa anafahamu umuhimu wa Roho wa Mungu katika maisha yetu kwa sababu Yeye aliishi duniani kama Mwanadamu kwa asilimia 100% na akiwa Mungu kwa asilimia 100% Lakini kama mwanadamu alikuwa anataka kutufundisha namna ya kuishi na kutenda kama wana wa Mungu tukiwa hapa Duniani, alipokuwa Duniani Yesu alimtegemea Roho Mtakatifu kwa kila jambo kwa hiyo kila alichokifanya alikifanya kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Sasa ikiwa Bwana Yesu alimuhitaji Roho Mtakatifu katika maisha yake ni zaidi sana wewe na mimi tunamuhitaji zaidi.  Katika maisha yetu ili aweze kutusaidia katika kila jambo, Na ni muhimu kuelewa kuwa Roho Mtakatifu sio ushawishi, wala sio nguvu tu kama watu wengine wanavyofundisha bali ni Mungu kamili, Roho wa Mungu ni Mungu ona:-

Matendo 5:3-4 “Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.”

Mathayo 12:22-28 “Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu. Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.”

Yesu Kristo alitoa kipaumbele kwa Roho Mtakatifu, alimtegemea Roho Mtakatifu hata kufanya miujiza na kutoa pepo, Nyakati za kanisa la kwanza walitoa kipaumbele kikubwa kwa Roho Mtakatifu, kwa msingi huo basi ni muhimu kwetu, kuhakikisha kuwa tunatoa nafasi kwa Roho Mtakatifu kwa sababu gani yeye anashughulika na maswala yote muhimu yanayohusiana na maisha yetu mfano:-

1.       Roho Mtakatifu huuisha Maisha mapya -  Roho Mtakatifu ndiye anayehusika kuweka mfumo wa maisha mapya katika roho zetu, ni yeye anayehusika katika wokovu wetu, na anakuwa kama anatuzaa upya kwa Roho, anatufufua kutoka katika hali ya kufa, anatupa uhai anatuhuuisha anaweka ndani yetu kiu ya kumcha Mungu na kumtafuta Mungu, hatuwezi kupata uamsho wowote ndani yetu ambao pia unaweza kuwa uamsho wa kanisa zima kama hatutamtii na kumsikiliza Roho Mtakatifu, mwanadamu anazaliwa akiwa ni mwenye dhambi kwa sababu ya kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, Dhambi hutufarikisha na Mungu, mbele za Mungu mtu mwenye dhambi au aliyepotea huhesabiwa kama mfu, kwa sababu ametengwa mbali na uwepo wa Mungu

 

Waefeso 2:1-6 “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda;hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu;”

 

Yohana 7:37-39 “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake. Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa.”

 

Uhai wote wa kimwili na wa kiroho uko katika uweza wa Roho Mtakatifu, bila Roho wa Mungu ni vigumu kitu chochote kuwa hai na maisha yetu ya kiroho kuwa hai, hatuwezi kuendelea, hatuwezi kujutia, hatuwezi kutubu, hatuwezi kuomba, hatuwezi kusoma neno la Mungu endapo Roho Mtakatifu hatahusika katika maisha yetu, kama ilivyo kwamba Bila Yesu hatuwezi kufanya neno lolote hali kadhalika Bila Roho wa Bwana sisi nasi hatuwezi kufanya jambo lolote, kwa hiyo Kristo alijua kuwa wanafunzi wake wamemuamini, lakini wasipokuwa na Roho Mtakatifu ni vigumu kwao kuendelea na imani ile bila ya msaada ulio karibu na msaada huo ni Roho Mtakatifu ambaye ndiye anayehuisha Roho zetu, Na kutupa msaada wa kuwa hai katika maswala ya kiroho.         

 

2.       Roho Mtakatifu hukaa ndani ya Mwamini – Kuna umuhimu mkubwa sana wa Roho Mtakatifu kukaa ndani yetu, Katika mstari wa Msingi tunamuona Yesu akisema atamuomba baba atupe msaidizi mwingine, ili msaidizi huyo akae ndani yetu

 

Yohana 14:16-18 “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu.”

 

Kukaa ndani yetu kwa Roho Mtakatifu kuna faida kubwa sana kwa sababu sisi ni hekalu la Roho Mtakatifu na akiwa ndani yetu tunapata nafasi ya kudumisha uhusiano wetu na Mungu kwa kuabudu, kuomba, kutafakari na kutuvuta tuwe karibu na yeye, Roho Mtakatifu anatumika kama daraja linalounganisha mioyo yetu na moyo wa Mungu, huku akibadilisha tabia zetu kwa kadiri tunavyojitoa kwake kwa kutii anatusababishia kuzaa matunda ya Roho na kuwa na sifa zinazomfanania Yesu Kristo.

 

Wagalatia 5:22-23 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”

 

3.       Roho Mtakatifu hutupa hakika ya wokovu -  Tunapa hakika ya wokovu kwa Imani kupitia Roho wa Mungu ndani yetu, aidha na neno la Mungu kwa hiyo  wokovu wetu hautegemei hisia zetu namna tunavyojisikia lakini unategemea namna Neno la Mungu linavyotuambia tukithibitishiwa na Roho wake Mtakatifu

 

Warumi 8:15-16 “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;”

 

4.       Roho Mtakatifu hubatiza mwamini – Neno la Mungu liliahidi ya kuwa sote tutabatizwa katika Roho Mtakatifu, Yohana mbatizaji anasema ajaye nyuma yangu ana nguvu kwa sababu yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu, kwa hiyo ni kazi ya Mungu kutubatiza kwa Roho wake Mtakatifu, lugha inayofahamika kama kujazwa, kutujaza,  lugha nzuri ya maana sana ni ubatizo wa Roho Mtakatifu, na hata hivyo, anapotubatiza Roho mwenyewe huusika katika kutubatiza, tunazamishwa ndani yake na kila kitu mpaka lugha zetu zinaingizwa katika uwepo wa Roho Mtakatifu bila kutupagaa, “we are filled without possessed”

 

Mathayo 3:11 “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.”

 

Yohana 1:33 “Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu.”

 

Matendo 1:5 “ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache.”

 

Matendo 2:4 “Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”

               

Matendo 10:44-47 “Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno. Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu, Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?

               

Matendo 19:1-6 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.”

               

Marko 16:17 “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;”

 

1Wakorintho 12:13 “Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.”

 

1Wakorintho 14:2 “Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.”

 

1Wakorintho 14:4 “Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa.”

 

5.       Roho Mtakatifu huzungumza na waamini – Roho Mtakatifu huzungumza, hunena na kuelekeza wazi wazi, ni jambo la kushangaza wale wanaodhani kuwa Roho Mtakatifu ni nguvu tu za Mungu na kumuondolea haki ya kuwa nafsi ni muhimu kujikumbusha kuwa huyu ni Msaidizi mwingine ni nafsi nyingine lakini anafanya kazi moja na Baba na Mwana na hivyo hutoa maelekezo, huzungumza, na hutoa maonyo.

 

Matendo 8:27-29 “Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu, akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya. Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.”

 

Matendo 13:1-2 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli.Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.”         

 

1Timotheo 4:1-3 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.”

               

Ufunuo 2:7 “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu.”

               

Ufunuo 2:11Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili.”        

 

Ufunuo 2:17Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea.”               

 

Ufunuo 2:29 “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.”

 

6.       Roho Mtakatifu hujihusisha na uongozi wa kiroho – Wakati wanafunzi wakiwa Pamoja na Yesu Kristo Duniani yeye ndiye alikuwa kiongozi wao katika maswala yote ya kiroho na ibada, sasa Yesu anapokuwa Mbinguni huku akiwa pamoja nasi katika ulimwengu wa Roho, kila wajibu na kazi alizokuwa akizifanya sasa Roho Mtakatifu hufanya hivyo ndani yetu

 

Yohana 16:7 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.”            

 

7.       Roho Mtakatifu hufundisha na Kuongoza katika kweli – Roho Mtakatifu ni Mwalimu mkuu, ambaye anapokuwa ndani yetu anatufundisha na kutukumbusha wote tuliomuamini katika neno la Kristo, jambo ambalo ni muhimu sana kwa ukuaji wetu kiroho na kudumu katika neno la Mungu na kuisimamia Imani, angalia leo wako watu wanaoukana utatu wazi wazi wakisema kuwa ni jambo lililoingizwa na Warumi wakati wa utawala wa Mfalme Constantino, wanasahahu kuwa mfalme huyo aliokoka baada ya kuona alama ya msalaba mbinguni wakati wa usiku na sauti iliyomuambia kuwa kwa alama hii utashinda na ndipo alipoukubali Ukristo, Mungu alimtumia kusimamia kweli kadhaa pamoja na wazee wetu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, ni kweli kuwa kanisa katoliki lina madhaifu kadhaa kama yalivyo makanisa mengine na kama yalivyokuwa yale makanisa saba ya eneo la Asia ndogo ambayo Yesu aliyakemea mapungufu yao na kuwatia moyo uwezo wao, hata hivyo pamoja na udhaifu unaoweza kuuona kwa wakatoliki hawajawahi kufikia ngazi ya kukana uungu wa Yesu au uungu wa Roho Mtakatifu, kwa hiyo katika wakati huu wa kuishi  kwetu tunapaswa kumtegemea sana Roho Mtakatifu kutuongoza katika kweli badala ya kushiba maharagwe na kuropoka, maandiko yako wazi kuhusu utatu wa Mungu likiwemo hili ya kuwa Roho Mtakatifu ni Mwalimu kama vile vile ilivyokuwa kwa Yesu Kristo, na atatukumbusha  na kutuongoza na kututia katika kweli yote.  

 

Yohana 14:26 “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”

 

Yohana 16:13-15 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri Lake Mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari

 

8.       Roho Mtakatifu huita watu katika huduma – Roho Mtakatifu huita watu katika huduma na kuwaongoza katika huduma hiyo sawasawa na Yesu alivyokuwa akiita watu na wote wanaongoza katika kazi ileile kwa misingi ile ile, mfano unaweza kumuona Yesu akimuita Sauli kwa kazi yake na unaweza kumuona Roho wa Mungu akimuita sauli yule yule aliyeitwa na Yesu kwa kazi ile iole iliyokusudiwa na Bwan Yesu! Ona :-

 

Matendo 9:1-6 “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu,akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi?Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.”

 

Matendo 13:1-4 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro.”    

 

Matendo 16:6-10 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.”

 

9.       Roho Mtakatifu hutupa uhakika wa uwepo wa Mungu – Roho Mtakatifu anakaa ndani yetu na anafanya kazi ya kutupa uhakika wa uwepo wa Mungu na uwepo halisi wa Yesu Kristo na asili zao na zaidi ya yote anatuunga katika ushirika na Mungu Baba na Mwana  na ndio maana maandiko yana wasiwasi sana na mtu ambaye anaharibu asili ya Mungu baba na Mungu mwana na wakati mwingine watu wanaofanya hivyo huenda hawana Roho wa Mungu ndani yao kama maandiko yanavyotuonya wazi wazi

 

1Yohana 2:22-29 “Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana.Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia.Ninyi basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana, na ndani ya Baba. Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele. Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza. Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake. Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake.Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye.”

 

Warumi 8:9-16 “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu. Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;”

 

10.   Roho Mtakatifu hutia nguvu – Roho wa Mungu hututia nguvu kukamilisha majukumu yote tuliyopewa na Mungu hapa duniani hasa ya kuhudumia watu, pamoja na kukabiliana na nguvu zote pinzani zinazotukabili kwa kusudi la kuzuia kusudi la Mungu, na kutimiza majukumu yote ambayo Mungu anataka tuwatendee watu wake

 

Luka 4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

 

Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

 

11.   Roho Mtakatifu husaidia katika maombi – Tangu zamani uwezo wa kuomba hauko katika uweza wa wanadamu, Roho Mtakatifu ndiye anayetuwezesha kuomba kwa kuugua kusikoweza kutamkwa au kwa kuomboleza, waamini wanapoomba pamoja na Roho Mtakatifu hawachoki, na sio hivyo tu huomba katika namna iliyo sahihi, Yeye anaitwa Roho wa neema na kuomba maana yake hutusaidia au kutupa neema ya kuomba, Maisha ya mtu aliyeokoka yatapata usitawi mkubwa sana endapo watu wake wataomba wakisaidiwa na Roho Mtakatifu.

 

Zekaria 12:10 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.”

 

Warumi 8:26-28 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”

 

Yuda 1:20 “Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu,”                       

 

12.   Roho Mtakatifu huwezesha kuabudu – Mungu ni Roho nao waabuduo halisi wanapaswa kumuabudu yeye katika Roho na kweli, kimsingi hatuwezi kuabudu vizuri bila msaada wa Roho Mtakatifu kama tu vile jinsi ambavyo hatuwezi kuomba vizuri bila Roho Mtakatifu, muunganiko wetu na usikivu wetu katika kumuabudu Mungu na kupokea kutoka kwake unatuhitaji wakati wa kuabudu tuwe rohoni

 

Ufunuo 1:9-11 “Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu. Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu,ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia.”

 

Yohana 4:23-24 “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

               

Wafilipi 3:3 “Maana sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili.”

 

1Wakorintho 14:15 “Imekuwaje, basi? Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia.”               

 

13.   Roho Mtakatifu hutoa karama – Kwaajili ya kuifanikisha kazi ya Mungu Roho wa Mungu hutupa karama ambazo kazi yake ni kuujenga mwili wa Kristo na kulithibitisha neno la Mungu, miujiza yote, uponyaji utoaji wa pepo ni kazi zinazofanywa na Roho Mtakatifu kupitia karama mbalimbalia anazoziweka kwa waamini

 

1Wakorintho 12:7-11 “Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.”

               

Kuna na mambo mengine mengi sana ambayo msaidizi mwingine huyafanya katika maisha yetu ya kila siku, hapa nimechagua machache lakini ni msaada kwa wanafunzi wakati wa mitihani, ni msaada kwa wanajeshi wakiwa vitani, ni msaada kwa usalama wa taifa na wapelelezi,  ni msaada wa wafalme katika maamuzi, ni msaada kwa wafanya biashara, ni msaada kwa wakulima, ni msaada kwa wachumi na ni msaada katika michezo na kila eneo ambalo Mtu wa Mungu analifanyia kazi, ni msaada kwa mafundi wa cherahani na wajenzi alitoa hekima kwa ujenzi wa hekalu, mavazi ya Haruni, wajenzi wa hema, ujenzi wa Meli wakati wa Nuhu, ukulima wakati wa Isaka, utawala wakati wa Suleimani, vitani wakati wa wamaamuzi na Daudi, upelelezi wakati wa Elisha,  kimsingi Roho wa Mungu ni msaada katika maisha yetu hata kitu kinapopotea Roho Mtakatifu, anahusika kionekane kumbuka habari ya kuelea kwa chuma cha shoka wakati wa Elisha na matukio mengine chungu nzima muimbaji na wapigaji kinubi kama Daudi mpaka pepo wanakimbia, vitani ngao zilipakwa mafuta kupata neema na upako kwaajili ya ushindi na ulinzi, unaweza kuhitaji msaada wa Roho Mtakatifu katika kila eneo bila kumuwekea Mungu mipaka.  Na ni kazi yake kutupa msaada tunaoutaka

Jinsi ya kuwa na msaidizi mwingine.

Roho Mtakatifu ili umpokee ni lazima uwe umemuamini Bwana Yesu kama mwokozi wako aliyekufa msalabani kwaajili yako, tendo la kumuamini Bwana Yesu ndilo linalotuunganisha na Mungu na kutufanya tuwe wana wa Mungu na kwa imani tunajiweka katika nafasi ya kumpokea Roho Mtakatifu

Matendo 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.”     

Matendo 19:1-6 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.”

Yohana 7:38-39 “Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa.”

Ni lazima mtu anayemuhitaji Roho Mtakatidu awe na shauku, liwe ni hitaji, iwe ni kiu yako na hivyo hua budi kuwa muhitaji na kumuomba Mungu baada ya kujifunza umuhimu wake unaingia katika maombi unaomba na Mungu anapoiona shauku yako na kiu yako atakupa Roho Mtakatifu.

Luka 11:13 “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?

Yohana 7:37-39 “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa.”

Ni lazima ukae katika neno la Mungu, Roho Mtakatifu hafanyi kazi nje ya neno lake lililowekwa ndani yetu kwa hiyo hakikisha unajaa neno na kwa jinsi hii utaruhusu Roho Mtakatifu kufanya makazi ndani yako na utaiona na kufurahia faida zake zote katika maisha yako

Yohana 15:7-8 “Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.”

Utii kwa neno la Mungu husafisha njia ya Roho Mtakatifi kukaa ndani yetu Zaburi 51:4-11“Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu.Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani. Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanijulisha hekima kwa siri, Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji Unifanye kusikia furaha na shangwe, Mifupa uliyoiponda ifurahi. Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; Uzifute hatia zangu zote. Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yanguUsinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.”

Jihadhari usiasi Isaya 63:10 “Lakini wakaasi, wakamhuzunisha Roho yake Mtakatifu; kwa hiyo akawageukia, akawa adui, akapigana nao.”

Kwa kuwa msaidizi mwingine ni wa Muhimu na ni zawadi kubwa sana kutoka kwa Mungu wakristo ni lazima tukubali kuruhusu Mungu atende kazi pamoja nasi kupitia Roho wake Mtakatifu kwaajili ya utukufu wake, hatuwezi lolote katika maisha haya na bila Mungu hatuwezi kutoboa kwa sababu hiyo ni muhimu kwetu kuhakikisha kuwa wakati wote tunampa Roho Mtakatifu kipaumbele katika maisha yetu na tunamtii kwa kila mzigo anaouweka ndani yetu na tuutimize kwa wakati. Uongezewe neema

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima        

Jumamosi, 7 Septemba 2024

Umuhimu wa kunena kwa lugha


Marko 16:15-18 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”



Utangulizi:

Kunena kwa lugha ni moja ya kipawa cha Roho Mtakatifu kinachotolewa kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo, kuwa na uwezo wa kuzungumza lugha nyingine ya wanadamu au malaika kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kipawa hiki kinatajwa na kuelezewa mara kadhaa katika maandiko hususani ya Agano Jipya na kwa sababu hiyo ni muhimu kwetu, kuchukua muda na kujifunza kwa kina na mapana na marefu, ili tuweze kuelewa umuhimu wake, faida zake na uhalisia wake, hii ni kwa sababu kama ilivyo kwa fundisho la utatu, na uungu wa Yesu, na hata uwepo wa Roho Mtakatifu, kitheolojia yamekuwa na mijadala mikubwa sana ambayo inapelekea watu kutilia shaka kuhusu mafundisho hayo hali kadhalika swala la kunena kwa Lugha. Na hivyo kupelekea kuwepo na upungufu wa kuzingatia umuhimu na faida za karama hii ya kunena kwa lugha, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kufuatilia na kuelewa kwa kina ili tuweze kufaidika na uwepo wa kipawa hiki kwa faida ya ufalme wa Mungu: Tutajifunza somo hili  Umuhimu kwa kunena kwa lugha kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-


·         Ukweli kuhusu kunena kwa lugha.

·         Umuhimu wa kunena kwa lugha.


Ukweli kuhusu kunena kwa lugha.

Ni muhimu kufahamu kuwa swala la kunena kwa lugha sio swala la mzaha na dhihaka kama watu wengine wanavyofikiri, kunena kwa lugha ni ishara kamili na ni kipawa kamili kutoka kwa Baba wa mianga kama jinsi ambavyo Yesu Kristo mwenyewe alivyoahidi na kusema kuhusu swala hilo, sio hivyo tu, maandiko yamelitaja swala la kunena kwa lugha katika mazingira toshelevu ya kuwa na uwezo wa kufanya fundisho kupitia swala hilo:-

Marko 16:15-18 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

Yakobo 1:16-17 “Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike.Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.”

Kunena kwa lugha kupo, na ni karama au kipawa kutoka kwa Mungu, maandiko hayo hayako kwa bahati mbaya, Yesu mwenyewe aliahidi ya kuwa wale wanaomuamini watafuatiwa na ishara mbalimbali, ikiwemo hii ya kunena kwa lugha mpya, hiki ni kipawa kamili kutoka kwa baba wa mianga ambaye kwake hakuna kivuli cha kugeuka geuka, kwa msingi huo ni ukweli usiopingika kuwa zawadi hii ya kunena kwa lugha ipo na imethibitishwa katika maandiko,  bahati mbaya Makanisa mengi na baadhi ya madhehebu wana maoni tofauti tofauti kuhusu kunena kwa lugha hata hivyo eneo pekee ambalo tunaweza kujifunza na kuelewa kwa kina kuhusu karama hii ni kwenye neno la Mungu tu.

-          Matendo 2:3-4 “Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”

 

-          Matendo 10:44-46 “Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,”

 

-          Matendo 19:1-6 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.”

 

-          1Wakorintho 14:2 “Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.”

                               

-          1Wakorintho 13:1 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.”                       

Kwa ushahidi wa maandiko kadhaa hapo tunaweza kukubaliana ya kuwa maandiko yanatambua kuwa iko ishara ya kunena kwa lugha na nyakati za kanisa la kwanza ilikuwa ni jambo la kawaida kwa wakristo waliobatizwa kwa Roho Mtakatifu kunena kwa lugha, na maandiko yameweka wazi hilo, kwa hiyo hatuwezi kupingana na neno kuhusu hili.


Umuhimu wa kunena kwa lugha


Ni muhimu kufahamu kuwa katika makanisa mengi sana watu wengi wanapuuzia swala zima la kunena kwa lugha kwa sababu wanadhani au kufikiri kuwa neno la Mungu linasema kuwa kunena kwa lugha kutakoma, lakini hiyo haimaanishi tukiwa ulimwenguni, kunena kwa lugha kutakoma tutakapofika mbinguni, kwa sababu tukifika mbinguni kunena kwa lugha kutapoteza umuhimu wake kwa sababu kule kila kitu kitakuwa kamili au kitakamilika kwa Mungu


1Wakorintho 13:9-12 “Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika.Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto.Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.”


Wako pia wale wanaoamini katika kunena kwa lugha lakini pia hawaoni umuhimu wa kuendelea kunena kwa lugha aidha kwa kufikiri kuwa kunena kwa lugha hakuna umuhimu, hapa sizungumzii karama ya aina za lugha, nazungumzia kunena kwa lugha ambako ni fungu la kila mtu aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu, Kunena kwa lugha hakutokei mara moja pale tu mtu anapokuwa amebatizwa kwa Roho Mtakatifu lakini linapaswa kuwa swala endelevu ambalo lina faida kubwa sana, hapa yako maswala kadhaa yanayosisitiza umuhimu wa kunena kwa lugha sawa na neno la Mungu.


1.       Kusema na Mungu. -  Kunena kwa lugha uwe unajua hiyo lugha au huitambui lakini kuna kupa neema ya kuzungumza na Mungu na sio wanadamu, kwa hiyo kunena kwa lugha ni mawasiliano ya siri kati ya mtu na Mungu ambayo mwanadamu hawezi kuyaelewa, kwa hiyo roho ya mtu aliyeokoka na kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, inawasiliana na Mungu moja kwa moja japokuwa huwezi kupanga kuhusu kunena kwa lugha lakini hatuna budi kuchochea kwa kina swala zima la kunena kwa lugha kutokana na umuhimu wake.kwani Mtu anaponena kwa lugha anazungumza na Mungu moja kwa moja maswala yote ya siri katika roho yake.

 

1Wakorintho 14:2 “Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.”

 

2.       Kujijenga kiroho  - Kunena kwa lugha pia kunamjenga kiroho, yeye anenaye kwa lugha, kujijenga kiroho kuna maanisha nini kunamaanisha kuwa unaponena kwa lugha unaimarisha imani yako na kuijimarisha kiroho wakati huo akili yako haina matunda yaani haijui kile unachokizungumza lakini roho yako ndani yako inaomba katika kiwango kilicho bora zaidi, ambacho kimsingi kinaimarisha hali yako ya kiroho unajijenga. Kumbuka pia kunena ka lugha pia kunaitwa kuomba kwa roho katika maandiko.

 

1Wakorintho 14:3-4 “Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo.Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa.”

 

Yuda 1:20 “Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu,”

 

1Wakorintho 14:14-15 “Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda. Imekuwaje, basi? Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia.”

 

3.       Kumwadhimisha Mungu – Kunena kwa lugha kunakufanya umwadhimishe Mungu yaani umuabudu Mungu katika namna ya ndani sana, Na kumshukuru, Roho Mtakatifu anatusaidia kumuabudu Mungu katika namna ambayo kibinadamu ni ngumu kuelezea naweza kusema ni kama mnenaji kwa lugha ni kama anazungumza akiwa mbinguni katika ulimwengu wa roho, na ndio maana tunaambiwa katika maandiko kuwa mara baada ya Kornelio na watu wa nyumbani mwake kubatizwa katika Roho Mtakatifu walianza kumwadhimisha Mungu yaani kuuabudu kwa ndani na kumshukuru Mungu, lugha inakusaidia kumuabudu Mungu kwa usahihi.

 

Matendo 10:44-47 “Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno. Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu, Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?     

 

4.       Mlango wa maisha ya ushindi – Moja ya siri kubwa sana ya mafanikio ya kunena kwa lugha ni pamoja na kukupa maisha ya ushindi, na kukupandisha kiroho pamoja na kuchochewa kwa karama za Rohoni, Kama unataka kuona hayo katika maisha yako chochea zoezi hili la kunena kwa lugha na utakuja kukubaliana nami kuwa kadiri unavyonena kwa lugha sana utagundua kuwa unapanda juu sana kiroho na kuchochea karama nyingi sana za rohoni, na kadiri unavyoacha utaona upungufu, watu wa Korintho walikuwa wananena kwa lugha na walikuwa na karama nyingi sana za rohoni lakini Paulo Mtume aliwaambia watamani sana karama zilizo kuu, karama zilizokuu maana yake kadiri mtu anavyotumia lugha katika mawasiliano na Mungu anajiweka katika nafasi ya kuchochea uwepo wa Mungu na karama za Roho na kutumiwa na Mungu zaidi.

 

1Wakorintho 14:1 “Ufuateni upendo, na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu.”

 

1Wakorintho 12:31 “Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora.”

 

Kunena kwa lugha ni njia ya kipekee sana ambayo Mungu ametupa kwaajili ya kujijenga binafsi, kujenga roho zetu, hii ni njia ya kujiimarisha kiroho na kuimarisha mahusiano yetu, na kumuabudu Mungu, tunapoomba kwa roho yaani kunena kwa lugha roho iliyoko ndani yetu na Roho wa Mungu yaani Roho Mtakatifu anatusaidia kutuombea na kujiweka katika nafasi nzuri kwaajili ya mambo yajayo kwani yeye anayajua

 

Yohana 16:13-14 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.”

 

1Wakorintho 2:19-15 “Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho Huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana Ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu.”

 

5.       Kuomba kwa usahihi zaidi – Kunena kwa lugha kunamsaidia mnenaji kuomba kwa njia inayomlingana Mungu, na hasa kuomba sawa na mapenzi ya Mungu kwa sababu kwa akili zetu na nguvu zetu kibinadamu hatujui kuomba kama jinsi itupaswavyo kuomba, kwa hiyo tunapoomba katika Roho Mtakatifu yaani kwa kunena kwa lugha tunajiweka katika nafasi ya kuomba kwa usahihi na kuboresha maisha ya maombi, bila Roho Mtakatifu ni vugumu kuwa waombaji lakini ni Roho wa Mungu ndani yetu na kupitia kunena kwa lugha tunaweza kuboresha kwa kiwango kikubwa sana maisha ya maombi, na kuongezea neema ya kuwa waombaji wenye maombi yenye kutosheleza na yenye kutuletea majibu na utaratibu ulio sahihi zaidi.

 

Warumi 8:26-27 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.”

 

Zecharia 12:10 -11 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.”

 

6.       Kuimarisha uhusiano wetu na Mungu - Wote tunafahamu jinsi lugha yoyote duniani ilivyo ya muhimu, iwe ni ya kuzungumza, au ya alama, au ya kimatendo, wote tunafahamu kuwa ubora na uzuri mkubwa wa lugha ni katika kuwasiliana na kujenga uhusiano, lugha ndiyo inayoruhusu kujielezea, na kuelezea hisia zetu, mawazo yetu shauku yetu na matakwa yetu. Kama hatuna ujuzi wa mawasiliano ni vigumu kwetu kueleweka ipaswavyo, ndani ya lugha kuna msingi wa mawasiliano, uhusiano, utamaduni, ukaribu, silaha, usalama, na nafasi, na kuunganisha, hii ndicho kinachotokea kati ya mtu aliyeokoka na Mungu pale tunaponena kwa lugha tunaimarika kila kitu katika uhusiano wetu na Mungu, hii haimaanishi kuwa Mungu hasikii lugha nyingine hapana lakini kwa njia rahisi tunaweza kusema kunena kwa Lugha ni lugha ya rohoni au ni lugha ya Mungu, ni Lugha ya Roho Mtakatifu, wote tunafahamu pale inapotokea ukikutana na mtu wa ngozi yako, rangi yako na lugha yako katika eneo la ugenini, jinsi inavyoleta msisimko mkubwa sana na kutaka kujuana na kuwasiliana ndicho kinachotokea pale unapozungumza na Mungu kwa kunena kwa lugha.  

 

1Wakorintho 14:2 “Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.”               

 

7.       Kukabiliana na changamoto za kiroho – Kunena kwa lugha kunazalisha nguvu na nguvu mpya na kunazalisha upako kutoka kwa Roho Mtakatifu unaotusaidia kukabiliana na changamoto zozote za kiroho, Paulo mtume alikabiliana na changamoto nyingi sana, alifanya kazi kuliko mitume wote, alitumiwa na Mungu kwa viwango vikubwa sana lakini moja ya sababu kubwa ya yeye kuwa imara sana ni kwa sababu alinena sana kwa lugha, kunena kwa lugha sana au kuliko wengine ni wazi kuwa pia alikuwa na maisha ya maombi sana kuliko wengine na unaweza kuona utajiri wa kila karama aliokuwa nao, na utendaji au kutumiwa na Mungu kwa viwango vikubwa zaidi.  

 

Yuda 1:20 “Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu,”

 

1Wakorintho 14:18-19 “Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote; lakini katika kanisa napenda kunena maneno matano kwa akili zangu, nipate kuwafundisha wengine, zaidi ya kunena maneno kumi elfu kwa lugha.”

 

1Wakorintho 15:9-10 “Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.”                

 

Matendo 19:11-12 “Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.”                

 

Unaweza kuona muunganiko ulioko kati ya kunena kwa lugha sana, kufanya kazi sana na kutumiwa na Mungu sana siri ya kutumiwa na Mungu katika neema yake na kumsaidia mtu kuishi maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu, na kumtumikia Mungu sana na kutumiwa sana katika ishara na miujiza iko katika kunena kwa lugha sana.

 

 

8.       Kupokea maelekezo ya kiroho – kwa kuwa kunena kwa lugha kunaimarisha uhusiano wetu na Mungu ni wazi kuwa kila anayenena kwa lugha anazungumza na Mungu na kwa sababu hiyo ni rahisi kupokea maelekezo, mafunuo, Elimu na hata unabii na maelekezo ya kimafundisho, kwa hiyo kunena kwa lugha hutuletea ufunuo mkubwa sana na maelekezo kutoka kwa Mungu ambayo yatatusaidia katika maisha yetu na huduma na utumishi kwa Mungu.

 

1Wakorintho 14:5-6 “Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha, lakini zaidi sana mpate kuhutubu, maana yeye ahutubuye ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi kanisa lipate kujengwa. Ila sasa, ndugu, nikija kwenu na kunena kwa lugha, nitawafaidia nini, isipokuwa nasema nanyi kwa njia ya ufunuo, au kwa njia ya elimu, au kwa njia ya hotuba, au kwa njia ya fundisho?

 

9.       Kwaajili ya kuyatimiza maandiko – Hakuna jambo la msingi na la muhimu kama kutii maandiko, wakati mwingine utii unaleta Baraka kubwa sana hata kama jambo tulifanyalo linaonekana kama la kipuuzi, tukumbuke tu kuwa upumbavu wa Mungu una hekima kuliko maarifa ya kibinadamu, maandiko yanapotutaka tujae Roho, tutembee kwa Roho, tuishi kwa Roho, tuabudu katika roho na kweli hayo yote hayawezi kukamilika kama tutaachia nje swala hili la msingi sana la kunena kwa lugha.

 

Yohana 4:23-24 “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

 

Warumi 8:11-16 “Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu. Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu

 

Wagalatia 5:16-18 “Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria

 

Waefeso 5:18 “ .Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;”

 

10.   Kwaajili ya vita vya kiroho – Kunena kwa lugha ni silaha, tunawasiliana kwa siri na Mungu na kwa sababu hiyo roho zetu huelewana vizuri na Mungu, na kwa sababu hiyo kutusaidia kupigana vita vya kiroho tukisaidiwa na Mungu kwa namna ya ajabu sana, kuomba katika roho yaani kunena kwa lugha kumetajwa na Paulo mtume kama miongoni mwa silaha za Rohoni zinazotusaidia kupata ushindi katika vita vyetu dhidi ya giza

 

Waefeso 6:10-18 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

 

Aidha utafiti wa kisayansi uliofanyika mnamo mwaka 2006  na kuandikwa katika gazeti la The new York Times limethibitisha kuwa watu wanaonena kwa lugha ni mara chache sana kupatwa na tatizo la kiakili, kule uingereza katika utafiti uliofanywa kwa watu 1000 wanaonena kwa lugha ilibainika kuwa watu wanaonena kwa lugha wako sawa kihisia kuliko wale wasionena kwa lugha, na huku kundi linalofuata likiwa ni wale wanaokaa kimya na kufanya tafakari, kwa hiyo kunena kwa lugha licha ya kukupa ushindi dhidi ya nguvu za giza unakufanya uwe imara kihisia na kiakili, kisaikolojia na kukufanya uishi maisha yaliyo sahihi. Kwa hiyo ile hali ya kufikiriwa kuwa wanaonena kwa lugha labda hawako sawa kiakili imebainika kuwa sio dhana sahihi.

 

Kwa msingi huo wote tunakubaliana ya kuwa swala hili ni swala la Muhimu sana, kwamba kunena kwa lugha kuna faida kubwa sana za kiroho, kwa kila Mkristo aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu kwani kunatujenga kiroho, kunatufanya kuomba kwa usahihi, kunaimarisha ushirika wetu na Mungu, kunatupa mafunuo, kunajenga mahusiano na mawasiliano, na Ndio maana Paulo mtume aliitumia sana zawadi hii ya kunena kwa lugha wewe na mimi hatunabudi kuhakikisha ya kuwa tunauiga mfano wa Paulo mtume na kuliweka swala hili katika vitendo kwa kumuhitaji sana Roho Mtakatifu katika kunena kwa lugha na kuimarisha uhusiano wetu na Mungu na kupata faida zote zinazoambatana na kunena kwa lugha. Ni kawaida yangu tu kufundisha neno la Mungu bila kuweka shuhuda lakini nnazo shuhuda nyingi zinazoashiria kunena kwa lugha kunabadilisha mfumo wa maisha yetu jambo la msingi tu lifanyie kazi neno hili na utabaini kuwa nisemayo ni kweli.

Yakobo 1:22-24 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.”  

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!