Isaya 62:1-3 “Kwa ajili ya Sayuni
sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea
kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. Na mataifa wataiona haki yako,
na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa
na kinywa cha Bwana. Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na
kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.”
Utangulizi:
Miaka mingi nyuma Muhubiri na
mtumishi wa Mungu Bill Bright
aliwahi kuhubiri ujumbe unaofanana na wa kwangu ambao aliuita “Why we cannot remain Silence” kwa
tafasiri isiyo rasimi “kwanini hatuwezi
kukaa kimya” ujumbe huo umehifadhiwa katika kitabu kiitwacho 50 Great sermon, Yeye alikuwa
akizungumzia kuhusu umuhimu wa kuihubiri injili kutokana na Agizo kuu la Bwana
wetu Yesu Kristo kwa kanisa na Dr Martin
Luther king Jr aliyekuwa mtumishi wa Mungu na mpigania haki za weusi wakati
wa ubaguzi wa rangi kule Marekani
aliwahi kusema “Our lives begin to end the
day we become silent” pia kwa tafasiri isiyo rasmi ni kama anasema “Maisha yetu huanza kuisha siku tutakapokaa
kimya” wote hawa walihubiri na kusema hayo katika mukhtadha tofauti na maandiko
tofauti, Bill akizungumzia umuhimu wa agizo kuu hatuwezi kukaa kimya bila
kuieneza injili, na Martin akizungumzia kutokuacha kukemea matendo ya ubaguzi, Hatuwezi kukaa kimya bila kukemea
matendo yasiyo ya haki ya kibaguzi, Leo
na mimi nakuja na ujumbe huu kwanini hatuwezi kunyamaza katika mlengo mwingine
hasa nikitaka kusisitiza jinsi Roho Mtakatifu anavyofanya kazi ndani yetu ya
kutufanya tutimize wajibu, alioweka ndani yetu; kwa hiyo mimi nazungumzia ni
nani anayesababisha tusikae kimya, Roho Mtakatifu ambaye amemuita kila mmoja
wetu kwa kazi zake maalumu pia anaweka ndani yetu Mzigo “burden” ambao anataka kila mmoja wetu aweze kuutimiza katika maisha
yetu hapa Duniani na kwaajili ya hayo utaweza kuona ni vigumu kwetu kuwa na
utulivu, bila kutimiza kile ambacho Mungu amekikusudia ndani yetu tutajifunza
somo hili kwanini hatuwezi kunyamaza kwa kuzingatia vipengele vitatu
vifuatavyo:-
·
Maana ya kunyamaza.
·
Kwanini hatuwezi kunyamaza.
·
Mifano ya kibiblia ya watu walioshindwa
kunyamaza.
Maana ya kunyamaza.
Ni muhimu kufahamu kuwa neno
kunyamaza halina misamiati mingi katika lugha ya Kiebrania na kiyunani
inayoweza kutosheleza kuelezea, Neno kunyamaza au kutulia au kukaa kimya katika
kingereza ni neno “Quiet”, ambalo
tafasiri yake ni without noise, absence of noise yaani paipo kelele, au bila ya
kelele, Lakini katika lugha ya kiebrania
neno linalotumika kuelezea ukimya au utulivu ni neno tām – kwa kiingereza “Gentle” ambalo maana yake ni kutokuchukua hatua, yaani kwa mfano
mtu anaweza kutenda kosa ambalo kiimani au kimila ni kosa kubwa sana ambalo
linahitaji uchukue hatua kali lakini badala yake unatulia bila kuchukua hatua
zozote wala kukemea wala kukosoa wala kusema, au mtu anaweza akawa
anakusingizia au kusema maneno ya uzushi na uongo kukuhusu, au akijifanya
anathibitisha kuwa wewe una kosa hili au lile kisha wewe hujibu kitu chochote
huko kunaitwa kunyamaza tām
kwa kiebrania, kunyamaza kwingineko ni kupuuzia na kut4okuchangia lolote kwa
kiyunani linatumika neno “Siōpaō”
ambalo maana yake kwa kiingereza ni “muteness”, na neno lingine
ni neno la Kiibrania “shākat” ambalo maana yake be “undisturbed” yaani kutokuwa na shughuli
na mtu, kutokujisumbua na maswala ya watu kuachia kile kitu kiende kama
kilivyo; huko ndio kunyamaza kunakotajwa katika maandiko. Mfano:-
Mwanzo 34:1-7 “Basi Dina, binti Lea, ambaye
Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi. Shekemu, mwana wa Hamori,
Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri.Moyo wake
ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu
msichana kwa maneno mazuri. Shekemu akamwambia Hamori, babaye, akasema,
Unipatie msichana huyu awe mke wangu. Basi Yakobo akasikia ya kwamba amembikiri
Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na wanyama wake nyikani. YAKOBO
AKANYAMAZA, hata walipokuja. Akatoka Hamori, babaye Shekemu, kumwendea Yakobo,
aseme naye.Wanawe Yakobo waliposikia hayo, wakaja kutoka nyikani; nao
wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu amefanya upumbavu katika
Israeli kwa kulala na binti Yakobo, neno lisilojuzu kutendeka.”
Mwanzo 35:21-22 “Kisha akasafiri Israeli akapiga hema yake upande wa pili
wa mnara wa Ederi. Ikawa Israeli alipokuwa akikaa katika nchi ile, Reubeni
akaenda akalala na Bilha, suria wa babaye; ISRAELI AKASIKIA HABARI. Basi hao
wana wa Yakobo walikuwa kumi na wawili.”
Mwanzo 25:23-27 “BWANA akamwambia, Mataifa
mawili yamo tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni
mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo.
Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake. Wa
kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita
jina lake Esau. Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake unamshika Esau
kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe
alipowazaa. Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa
nyikani, na YAKOBO ALIKUWA MTU MTULIVU, mwenye kukaa hemani.”
Mathayo 26:59-63 “Basi wakuu wa makuhani na
baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua;wasiuone
wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi. Hata baadaye wawili wakatokea,
wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku
tatu. Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia
nini? Lakini, YESU AKANYAMAZA. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu
aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.”
Marko 14:55-61 “Basi wakuu wa makuhani na
baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione. Kwa maana
wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana. Hata wengine
wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema, Sisi tulimsikia akisema, Mimi
nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga
jingine lisilofanyika kwa mikono. Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana. Kisha
Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa
wanakushuhudia nini? LAKINI AKANYAMAZA, WALA HAKUJIBU NENO. Kuhani Mkuu
akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu? ”
Waamuzi 18:7 “Ndipo hao watu watano
wakaenda zao, wakafika Laisha, wakawaona wale watu waliokuwamo ndani yake,
jinsi walivyokaa salama salimini kwa mfano wa walivyokaa hao Wasidoni, wenye
starehe na hifadhi, kwa maana hapakuwa na mtu katika nchi hiyo aliyekuwa na
amri, aliyeweza kuwatweza katika neno lo lote, nao walikuwa wa mbali na hao
Wasidoni, wala hawakuwa na shughuli na mtu ye yote.”
Katika vifungu vya maandiko hapo
juu tunaona sasa matumizi na neno kunyamaza. Linavyotumika kwa Yakobo
linatumika neno “tām” gentle hii inamaanisha kuwa
Yakobo au Israel alikuwa ni mkimya au mtulivu kwa kuzaliwa kwa hiyo kukaa kimya
ilikuwa ni tabia yake ambayo kimsingi watoto wake Simoni na Lawi hawakuwahi
kukubaliana nayo, waliona ni ukimya unaopelekea hata kuonewa. Binti yake
alipobakwa Yakobo alikaa kimya, nahata Reuben alipolala na suria wa baba yake
Yakobo alisikia lakini alikaa kimya, kwa hiyo ni wazi kuwa alikuwa ni mtulivu
mno upole uliokithiri, utulivu uliopittiliza, alikaa kimya.
Na kwa Bwana Yesu ukimya wake
wakati akiwa anashitakiwa mashitaka ya uongo mbele ya mahakama ya kiyahudi yeye
alinyamaza “Siōpaō” muteness Ukimya huu ni ukimya wa kupuuzia, au
kuamua kupuuzia na kutokutilia maanani maswala ya kipuuzi. Usipoteze muda wako
kujibu lolote unalozushiwa ambalo ni la uongo, Yesu watu walipomsingizia na
kusema uongo hakujibu lolote alitulia kimya
Na ukimya unaozungumzwa katika andiko
kutoka katika kitabu cha waamuzi linazunguiza utulivu wa kukaa kwa amani au
bila kusumbuana na maswala ya watu “shākat”
yaani “undisturbed” husumbuliwi
wala husumbui, hushughuliki na jambo lolote la mtu wala wao hawashughuliki na
wewe kwa hiyo unakaa salama kimyaa
Na neno lingine linalotumika
katika maandiko ambalo kisingi ndilo tutakalolitumia leo ni neno la kiibrania “Chậshậh” ambalo maana yake to keep quiet, to hold peace, au to keep
silence Hili ndio linalotumiwa na
Roho Mtakatifu kutokumfanya mtu atulie au awe na Amani au anyamaze wakati kuna
mzigo ambao Mungu ameuweka ndani yake
Isaya 62:1-3 “Kwa ajili ya Sayuni
sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea
kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. Na mataifa wataiona haki yako,
na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa
na kinywa cha Bwana. Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na
kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.”
Kwa nini hatuwezi kunyamaza
Roho Mtakatifu anapokuwa ndani
yetu, moja ya kazi anayoifanya ni kukutaharakisha, kukupeleka katika kutimiza
majukumu ambayo Mungu ameyakusudia na kuyaweka ndani yako, kwa hiyo yeye
hukufanya wewe na mimi tusiweze kukaa kimya, Ni kazi ya Roho Mtakatifu kuwatia
nguvu waamini na kuwasukuma moyoni kwa kuwanyima Amani, kwa kuwakoseha utulivu,
kwa kuwahimiza na kutowafanya wanyamaze mpaka wametimiza kile ambacho Mungu
amekikusudia kwa mtu huyo aweze kukitimiza, kwa hiyo Roho wa Mungu anafanyika “Catalyst” kichocheo ambaye anainua mioyo yetu na kuweka mzigo na
moyo na kutuwezesha kusema kile ambacho Mungu amekikusudia ili kitende kazi
ndani yetu mfano kama Mungu anaweka neno ndani yetu basi, Roho Mtakatifu
anachochea lile neno ambalo Mungu amelikusudia, tuliseme ili tuweze kulisema na
inapotokea utaamua kukaa kimya kunatokea changamoto ndani yako zinazokunyima
Amani itakayokupelekea ukaseme kila ambacho Mungu amekikusudia ni kwaajili ya
Roho Mtakatifu kuweka kitu ndani yako au ndani yangu ndio tunakosa utulivu au
uwezo wa kunyamaza “Chậshậh”
kwanini hatuwezi kunyamaza? Ni kwa sababu Roho Mtakatifu haachi kufanya
uchochezi ndani yetu!
Yeremia 1:6-8 “Ndipo niliposema, Aa, Bwana
MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini Bwana akaniambia,
Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe
utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo
pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana.”
Ezekiel 33:7-9 “Basi wewe, mwanadamu,
nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani
mwangu, ukawape maonyo yangu. Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika
utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya
huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.
Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye
asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako.”
Kwa hiyo kumbe Mungu anapoweka
neno lake au wajibu wake kwa mtumishi Fulani wa Mungu, Roho Mtakatifu huchochea
na kumfanya mtu huyo kukosa utulivu mpaka atakapotimiza kile ambacho Mungu
amekiweka, matukio ya aina hii yanaweza kuwekwa kwa waombaji, yanaweza kuwekwa
kwa wajumbe wa kinabii ambao Mungu anataka wapeleke maonyo na kutia moyo,
wajumbe wa kiinjilisti ambao Mungu anawataka waseme habari njema, wajumbe wa
kialimu ambao Mungu anawataka wafundishe, wajumbe wa kiandishi ambao Mungu
anawataka waandike “haya uyaonayo uyaandike!” , Wajumbe wa kichungaji ambao
Mungu anaweka mzigo ndani yao wachunge na kulisha kundi la kondoo wa Bwana,
wajumbe wa kitume ambao watapanda makanisa na kuipeleka injili kule Mungu
anakotaka, Wajumbe wa kitaaluma ambao Mungu anataka wawake na kupanda taaluma
katika jamii, wakati wote Mungu Roho Mtakatifu atawataharakisha watu wake
wasikae kimya kwaajili ya kazi zote katika ufalme wa Mungu, yeye huhimiza na kutoa
maelekezo kwa kila muhusika kwaajili ya kazi husika ambayo yeye anataka
itimizwe
Ezra 5:1-2 “Basi manabii, Hagai nabii, na
Zekaria mwana wa Ido, wakawafanyia unabii Wayahudi waliokuwako Yerusalemu na
Yuda; waliwafanyia unabii kwa jina la Mungu wa Israeli. Ndipo akaondoka
Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, wakaanza
kuijenga nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu; na pamoja nao walikuwa manabii wa
Mungu, wakiwasaidia.”
Matendo 8:26-29 “Malaika wa Bwana akasema
na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo
kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa. Naye akaondoka, akaenda; mara
akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa
Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu
kuabudu, akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya.
Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.”
Luka 2:25-35 “Na tazama, pale Yerusalemu
palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu,
akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.Naye alikuwa
ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa
Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto
Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe
alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema,Sasa, Bwana, wamruhusu
mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu
wako,Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa,
Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa
wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia
Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio
katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia
moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi”
2Petro 1:20-21 “Mkijua neno hili kwanza, ya
kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu
fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali
wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.”
Wakati wote Roho Mtakatifu
aliwapa uchochezi manabii, mitume na watumishi mbalimbali wa Mungu kuweza kutoa
ujumbe, kutabiri na kutia moyo au kuongoza katika haki ili mapenzi ya Mungu
yaweze kufahamika na kutendeka katika jamii ya watu ambao Mungu aliwakusudia,
Mungu Roho Mtakatifu anapokuwa amekusudia hilo na wewe ndie ambaye umekusudiwa
upeleke ujumbe huo basi yeye hatakuacha unyamaze atakusukuma kwa jambo hilo,
utaona moto ndani yako, utaona msukumo, utaona kukosa Amani, utaona kusumbuliwa
utasikia kushikwa, kukamatwa, kupelekwa kutaharakishwa kuuzishwa mpaka umetenda
kile ambacho kimekusudiwa naye
Mifano ya kibiblia ya watu walioshindwa kunyamaza.
Waamuzi 13:24-25 “Basi yule mwanamke
akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana
akambarikia. Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati
ya Sora na Eshtaoli.”
Wote tunafahamu kuwa Samsoni alizaliwa
kwa kusudi maalumu, na Mungu alikuwa amemuandaa kuwa mwokozi wa wana wa Israel
ambao walikuwa wanaonewa na Wafilisti kwa wakati huo, tunasoma tu kuwa mara
baada ya mtoto huyu kukua Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha maana yake ikamnyima
kutulia, ikamnyima kunyamaza Roho Mtakatifu alianza kuweka msukumo na kumfanya
ajione hawezi kutulia ni lazima aseme alijiona hawezi kuwa utumwani yeye wala
ndugu zake alijisikia kuwa ni lazima afanye kazi yake aliyopewa ya kuwaokoa
wana wa Israel kama Jeshi la Mtu mmoja na alikuwa na hisia zilizokuwa
zikimuelekeza au kumyima Amani mpaka atafute kisa ili mradi aweze kuwaokoa wana
wa Israel, kwa hiyo tunajifunza hapa kuwa Mungu akikupa agizo huwezi kutulia
kunakuwepo moto unaokutesa na kukusumbua ukikutaka utimize kusudi ambalo kwa
sababu ya hilo ulizaliwa.
Isaya 58:1-14 “Piga kelele, usiache, Paza
sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo
dhambi zao. Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile
taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za
haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona
tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu
mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu.
Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na
kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata
kuisikizisha sauti yenu juu. Je! Kufunga
namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi
yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini
yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana? Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii?
Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa,
na kwamba mvunje kila nira? Je! Siyo
kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani
kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu
moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea
mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo
utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa
nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama
ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo
nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye
Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na
kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama
chemchemi ambayo maji yake hayapungui.
Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa
ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza
mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia. Kama ukigeuza mguu
wako usihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita
sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa
kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema
maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika Bwana; nami
nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba
yako; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo.”
Nabii Isaya aliitwa na Mungu na
Mungu alimtaka awaonye wana wa Israel na kuwaeleza kosa lao ili yamkini waweze
kutubu, ujumbe wa makemeo wakati mwingine sio ujumbe mwepesi, kama mwanadamu
wakati mwingine alisita na au aliingia hofu
na labda alitaka kuacha lakini Roho wa Mungu alimwambia piga kelele wala
usiache paza sauti yako kama tarumbeta kwa nguvu onya juu ya unafiki, wa watu
wa Mungu, wakati mwingine ni ngumu kuhubiri maneno magumu watu wanaweza kusema
ya kuwa unawahukumu na hasa na wewe ukijijua kuwa u mwanadamu hivyo ilikuwa ni
sahihi kwa Isaya kusita sita Lakini aliambiwa apige kelele kama tarumbeta
awaonye watu, alipaswa kuwa muaminifu kuhubiri ujumbe wote wa Mungu kama ni
toba anyooshe, kama ni rehema anyoooshe na asiseme tu maneno laini kama watu
walivyokuwa wanataka kwaajili ya hayo Isaya hakunyamaza.
Isaya 58:1 “Piga kelele, usiache, Paza
sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo
dhambi zao.”
Wakati wote kumbe Roho wa Mungu
anapokuwa juu yako kwaajili ya huduma ambayo Mungu ameiweka ndani yako ni
ukweli ulio wazi hutatulia, wala hutanyamaza utafanya kile ambacho Mungu
amekikusudia, kama ni kuwafungua watu, kama ni kuponya kama ni kujenga mioyo ya
watu, kama ni kutangaza habari njema, yeye hatakuacha utulie atataka utangaze
kile ambacho Mungu anataka kukifanywa kupitia wewe ilikuwa hivyo kwa Isaya
nabii na ilikuwa hivyo kwa Masihi Bwana wetu Yesu.
Isaya 61:1-3 “Roho ya Bwana MUNGU i juu
yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema;
amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na
hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.Kutangaza mwaka wa Bwana
uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;
kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu,
mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito;
wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na Bwana, ili atukuzwe.”
Ni maneno ya Nabii Isaya lakini
vilevile ni ya Masihi, Yesu alipokuja duniani aliyatumia maneno haya, ni kazi
ileile ya Roho Mtakatifu ambaye hataki
mtu mwenye agizo kunyamaza, Roho wa Mungu kupitia Yesu alitaka afungue kinywa
chake na kuwahubiria wanyenyekevu habari njema, alitakiwa kuwaganga
waliovunjika moyo, alitakiwa kutangaza uhuru kwa mateka, na wafungwa
kuwatangazia kufunguliwa, na kuutangaza mwaka wa neema uliokubalika,
wasingeliweza kunyamaza kimya katika hayo, na ndio maana tunamuona Yesu
akizunguka toka mji mmoja kwenda mji mwingine na vijijini kila mahali akiifanya
kazi hii asingeliweza kutulia kwa sababu Roho Mtakatifu alimpaka mafuta
kwaajili ya hilo, kila mmoja kwa kusudi lake ambalo kwalo Mungu amekupaka
mafuta lifanye kwa bidii na kwa uaminifu wote na kwa usikivu mkubwa kwa Roho wa Mungu na
utaona kuwa huna sababu za kunyamaza!
Isaya 62:1-3 “Kwa ajili ya Sayuni
sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea
kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. Na mataifa wataiona haki yako,
na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa
na kinywa cha Bwana. Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na
kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.”
Isaya anazungumza kwa niaba ya
mji wa Yerusalem yaani Sayuni akimaanisha Israel, kwamba pamoja na kukumbwa na
matukio mbalimbali na kubomolewa na maadui lakini haitakuja itokee, mji huu
usisimame, ni mji ambao uko kwenye mapenzi ya Mungu, ni mji uliowekewa
waombezi, manabii, na waombolezaji maarufu, ambao wanauombea usiku na mchana
ili kwamba ufalme wa Mungu uweze kusimama, Kama Mungu alivyomuinua Isaya bado
anaendelea kuinua watu wanaoiombea Israel kila iitwapo leo katika kila kona za
Dunia, wanaoitakia mema Israel wako kama jeshi, Yerusalem ni mji ambao Utawala
halisi wa kimasihi utatawala na Kristo akiwa Mfalme wa utawala huo Wakristo
wanapoomba katika sala ya Bwana ufalme wako uje na mapenzi ya Mungu yatimizwe
hapa duniani kama mbinguni Mathayo 6:10
maana yake tunaomba pia kwamba Yesu arudi na kusimamisha utawala wake hapa
duniani na ufalme huo na kiti chake cha Enzi kitakuwa Israel,Pale Yerusalem,
Sayuni, Kwaajili ya Israel Hatuwezi kunyamaza
Yeremia 20:7-9 “Ee Bwana, umenihadaa, nami
nimehadaika; wewe una nguvu kuliko mimi, ukashinda; nimekuwa kitu cha
kuchekesha, mchana kutwa; kila mtu hunidhihaki.Maana kila ninenapo napiga
kelele, nalia, Dhuluma na uharibifu! Kwa kuwa neno la Bwana limefanywa shutumu
kwangu, na dhihaka, mchana kutwa. Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena
kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao,
uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi
kujizuia.”
Yeremia alitumwa na Mungu kumbuka
kuwa Mungu aliweka maneno ndani yake na kumuamuru kuyasema haikuwa kitu rahisi
kukubalika katika mioyo ya watu kiasi ambacho hata pamoja na kuwa Mungu
alimwambia nitakuwa pamoja naye alikutana na magumu sana alitiwa gerezani,
aliteswa alitupwa katika shimo la matope
ilifikia hatua alitaka kukaa kimya asiseme lakini kwa kadiri alivyokuwa
akijitahidi akae kimya kuna nguvu ya kiungu iliyokuwa inamlazimisha kusema wivu
wa kiungu ulijaa ndani yake na alipoona uovu uliokuwa ukiendelea na ujumbe
aliopewa kusema maneno yalimuunguza akawa hawezi kuyafumbia mdomo alilazimika
kutangaza kile ambacho Mungu alikuwa amemuagiza pamoja na kuwa ilimgharimu
mateso makali na maumivu makubwa.
Yeremia 47:6-7 “Ee upanga wa Bwana, Siku
ngapi zitapita kabla hujatulia? Ujitie katika ala yako; Pumzika,
utulie.Utawezaje kutulia, Ikiwa Bwana amekupa agizo? Juu ya Ashkeloni na juu ya
pwani, Ndipo alipoyaamuru hayo.”
Wafilisti walikuwa wanaikalia
pwani ya Yuda na mara nyingi kihistoria kulikuwa na ugomvi kati ya nchi ya
Israel na wafilisti, Yeremia alitakiwa
kutoa unabii wa kuwaonya wafilisti ya kuwa upanga wa Bwana utawahusu, ni kama
Mungu alikuwa ameamuru hukumu kwa wafilisti kuwa upanga wa Bwana uipige Gaza na
Ashkeloni, ilionekana kuwa hakutakuwa na utulivu kwa wafilisti, kila wakati
Gaza itapigwa, hatujui kama nabii aliwaombea wafilisti angalau upanga utulie
Lakini lilikuwa ni agizo la Mungu upanga ulikataa kutulia kwa sababu ulikuwa na
agizo la Mungu, utawezaje kutulia ikiwa Bwana amekupa agizo? Kupigwa kwa Gaza
ni agizo la kimaandiko na itaendelea kuwa hivyo kwa sababu ndivyo neno la Mungu
linavyosema na Roho wa Mungu husukuma hukumu juu ya Gaza kwa sababu ni agizo
lililoko katika neno lake.
Yoel 2:28-29 “Hata itakuwa, baada ya hayo,
ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume
kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;
tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina
roho yangu.”
Ni unabii wa maana sana kimsingi
unahusiana na siku za mwisho na ujio wa Roho Mtakatifu kama alivyoona Yoel Roho
Mtakatifu atakuja na kazi maalumu kwa kila watu na makundi na kila mmoja
hataweza kukaaa kimya atasema tu, watatabiri, wanaona maono, wataota ndoto, kwa
hiyo tunaweza kukubaliana wote ya kuwa ubatizo wa Roho Mtakatifu utasababisha
na kumfanya kila mwanadamu kutokutulia, neno la Mungu linasema tena juu ya
watumishi wangu, nini maana yake watumishi maana yake “Bond Servants” ni neno limetumika mara 800 katika maandiko
likimaanisha ni watu wa kazi watumwa hawatatulia, kila atakayepewa Roho wa
Mungu hataweza kuwa na utulivu atafanya kile ambacho Mungu ambaye ni bwana wetu
amekusudia akifanye.
Mika 3:8 “Bali mimi, hakika nimejaa nguvu
kwa roho ya Bwana; nimejaa hukumu na uwezo; nimhubiri Yakobo kosa lake, na
Israeli dhambi yake.”
Mika aliitwa kuwa msemaji kwa
niaba ya Mungu yaani nabii, alinena kwa uweza wa Roho Mtakatifu, alitakiwa
kuikemea dhambi katika nyumba ya Mungu na ilikuwa ni kazi aliyopewa pamoja na
kuonyesha moyo wa Mungu, kutia moyo na kukatisha tamaa uovu, wakati wa Mika
kulikuwa na manabii wa uongo wengi, waliokuwa wakiwakosesha watu wa Mungu kwa
jumbe zisizo za kweli, lakini uweza wa Roho wa Bwana haukumpa Amani Mika
alipewa kusema, alipewa kuonya, alipewa kutangaza hukumu, alipewa kutangaza
rehema asingeliweza kunyamaza
Mika 3:5 “Bwana asema hivi katika habari za
manabii wanaowakosesha watu wangu; hao waumao kwa meno yao, na kulia, Amani; na
mtu awaye yote asiyetia kitu vinywani mwao, wao humwandalia vita.”
Mungu alimtaka Mika kukemea na
kusema kweli, bila kujali kuwa liko kundi la manabii feki yaani wa uongo,
Kanisa halipaswi kufuata shinikizo la watu Fulani ndani au nje ya nchi
wanaotaka tuwe na mtindo Fulani unaofanana wa maisha hata kama mambo hayo ni
uovu yako kinyume na Mungu na mila zetu, Kanisa ni lazima likemee bila huruma
kile ambacho kinaonekana kuwa ni uongo na kuwa kiko kinyume na mapenzi ya
Mungu, Mika hakufuata mkumbo alibaki katika zamu yake na kukemea kweli kweli
kwa sababu nyuma yake kulikuwa na shinikizo la Roho Mtakatifu kwanini hatuwezi
kunyamaza kwa sababu Roho wa Mungu anafanya hivyo ndani yetu, hakuna anayeweza
kutulia!
Zekaria 4:6-9 “Akajibu akaniambia, akisema,
Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa
nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.Nani wewe, Ee mlima
mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la
kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie. Tena neno
la Bwana likanijia, kusema, Mikono yake Zerubabeli imeiweka misingi ya nyumba
hii, na mikono yake ndiyo itakayoimaliza; nawe utajua ya kuwa Bwana wa majeshi
amenituma kwenu.”
Mungu alimuinua Zerubabeli
kuijenga tena Nyumba ya Mungu katika mazingira magumu wakati Israel waliporejea
kutoka utumwani Babeli yaani wayahudi, kazi hii ilikuwa ngumu kiasi ambacho kuna
wakati watu walikuwa kama wameisusia, Lakini Mungu aliwainua manabii Habakuki,
Zekaria na Malaki kuwatia moyo viongozi waliokuwa wanahusika na agizo la
kuijenga nyumba ya Bwana walipokuwa wanasita sita Zekaria alipewa ujumbe kumtia
Moyo Zerubabeli kuwa nyumba hiyo itajengeka tu sio kwa uweza wa kiserikali wala
wa kijeshi bali Roho Mtakatifu, huyu atainua hari ya wajenzi na watajenga kwa
uwezo wake hakuna mtu atakayeweza kutulia kwa sababu Roho wa Mungu atasababisha
kazi yake itendeke na hakuna kikwazo chochote kitakachoweza kusimama mbele ya
wajenzi.
Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha
kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika
Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”
Ni tangazo la ujio wa Roho
Mtakatifu kwa kanisa, mitume waliagizwa kusubiria ubatizo huo na
walihakikishiwa kuwa watakapopokea ubatizo wa Roho Mtakatifu hawataweza kukaa
kimya watasema, watahubiri, watathibitisha na kuwa wao ni mashahidi wa kweli
kwaajili ya Yesu kristo, hatakuja kuwa na kizuizi watamtii Mungu kuliko
wanadamu katika swala zima la kuhubiri injili.
Matendo 5:17-32 “Akaondoka Kuhani Mkuu na
wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo),
wamejaa wivu, wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza; lakini malaika wa
Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame
hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu. Nao waliposikia wakaenda
alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha. Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja
naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli,
wakatuma watu gerezani ili wawalete. Hata watumishi walipofika hawakuwaona
gerezani, wakarudi wakatoa habari, wakisema, Gereza tumeikuta imefungwa salama,
nao walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu
ndani. Basi jemadari wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa
na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo. Mtu mmoja akaja akawapasha
habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu,
wamesimama wakiwafundisha watu. Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na
watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije
wakawapiga kwa mawe. Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu
akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina
hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta
damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii
Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua
mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe
Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu
mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote
wamtiio.”
Mitume walikuwa na agizo la
kuihubiri injili, na Mungu Roho Mtakatifu alikuwa amewabatiza kusudi waweze kulitimiza
kusudi hilo pana la Mungu, hata hivyo walikutana na upinzani mkali kutoka kwa
wazee wa kiyahudi wajulikanao kama Sanhedrin yaani mahakama kuu ya kiyahudi,
hawa waliwakataza wasihurbiri wala wasiseme kitu kuhusu Yesu, waliwatia
gerezani lakini hata hivyo malaika wa Bwana aliwafungulia hawawezi kunyamaza
waliagizwa waendelee kufundisha na walifanya hivyo, wazee walikasirika
sana wakiwataka wakae kimyaa Petro na mitume wakajibu hoja kuwa imetupasaa
kumtii Mungu kuliko wanadamu, Roho Mtakatifu hutuwezesha kuwa na utii wa
kiwango cha juu kwaajili ya kile ambacho tumeitiwa kukifanya na kufundisha na
kulisema neno lake tunawezaje kunyamaza? Kanisa ndio maana hatuwezi kunyamaza
na ndio maana hata mimi na wewe hatuwezi kunyamaza.
Matendo 17:16 “Paulo alipokuwa akiwangojea
huko Athene na kuona jinsi mji ule ulivyojaa sanamu, roho yake ilichukizwa sana
ndani yake.”
Paulo mtume aliihubiri injili
huko Thesalonike na Beroya, hata hivyo wayahudi wenye wivu walimuwinda na
kutaka kumua, kwa hiyo wanafunzi waliookoka walimpeleka Paulo katika mji wa
Athene ili awasubiri Timotheo na Sillas ambao walibaki katika miji ya awali,
Neno la Mungu linatuambia wakati
alipokuwa akiwasubiri huko Athene aliona mji ule umejaa sanamu, roho yake ilichukizwa sana Katika kiingereza
tunaambiwa hivi “his spirit was stirred
in him” neno stirred katika
kiyunani ni “Paroxunō” maana yake easily Provoked yaani alichochewa,
alipatwa na hasira ya kiungu au alisukumwa kutokukaa kimya, Roho Mtakatifu
ndani ya Paulo mtume alipoona sanamu hakusubiri aliona itachelewesha akaanza
kuhubiri, Roho wa Mungu hatakuacha unyamaze akiwa ameweka kitu au mzigo au
wajibu ambao unatakiwa uutekeleze. Je wewe roho yako inachukizwa? Unapoona
wanadamu wanaoana na mbwa? unachukizwa na kuona mwanaume akimpa binti yake
mimba?, wanadamu wakilala na wanyama, madaktari wakifanya ngono na wagonjwa,
watumishi wanapozini na washirika, matajiri wakipewa nafasi ya vyeo vikubwa
makanisani, washirika wakiibiwa fedha na kutajirisha wahubiri, Wahubiri
wakijilimbikizia mali, kampeni za kisiasa zikitapakaa makanisani, watu
wakipeana sumu kwaajili ya nafasi za uongozi, watu wakiombewa bila kuongozwa
sala ya toba, wanakwaya wakitembea wenyewe kwa wenyewe, wanamuziki wakiacha
waume zao na ndoa zao kwa kisingizio cha wito, unanyamazaje wakati utoaji wa
mimba umeingia makanisani hata wanandoa waliookoka siku hizi wanatoa mimba?,
madawa ya kuleywa yakiuzwa kila mahali, rushwa na ushoga umetapakaa kila
mahali, unanyamazaje wakati watu wakiwa wahanga wa picha za ngono? Uamsho
ukisisitizwa bila utakatifu, mafundisho potofu yakiwa hayakemewi, watu wakiwa
wanatekwa na kuuawa, mauaji ya kutisha yakisambaa, ulawiti na ubakaji
uliokithiri, hali ya uchumi ikiendelea kuwa mbaya? Paulo mtume angekuwepo leo
asingeliweza kunyamaza, ikiwa sanamu tu zilimsumbua sana sisi nasi hatunabudi
kuhakikisha kuwa tunaifikia jamii na kuijenga kwa gharama yoyote ile na kamwe
hatuwezi kunyamaza!, Roho Mtakatifu akiwa ndani yetu roho zetu zitachukizwa
hatuwezi kunyamaza!
Warumi 1:16-17 “Kwa maana siionei haya Injili;
kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi
kwanza, na kwa Myunani pia. Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake,
toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.”
Paulo mtume anaonyesha wazi kuwa
haionei haya injili kwa sababu ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa watu
waaminio, kutokana na uwezo mkubwa wa habari njema kuwasaidia wanadamu na
kuwapa uzima wa milele bure kwa Imani katika Kristo Yesu Paulo anaona ana
wajibu wa kutokuionea haya injili iwe ni kwa kufungwa au kudhaliliswa, au
kuteswa kwa sababu zozote zile hawezi kuona aibu kwa sababu ya injili, maana
yake pia hawezi kukaa kimya kwaajili ya injili ataendelea kuisema katika
mazingira yoyote.
2Timotheo 1:7-9 “Maana Mungu hakutupa roho
ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.Basi usiuonee haya
ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie
mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye
alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi,
bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika
Kristo Yesu tangu milele,”
Paulo anamkumbusha Timotheo kutokuonea
haya ushuhuda wa Bwana, kutokuionea haya ufungwa kwaajili ya injili, anamtaka
avumilie mabaya kwaajili ya injili aendelee kwa kadiri ya nguvu za Mungu
aliyewaita akimkumbusha kuwa Roho Mtakatifu sio Roho ya woga bali ni ya nguvu
na upendo na moyo wa kiasi kwa hiyo haijalishi ni magumu kiasi gani anakutana nayo
anamtaka aendelee na kazi ya wito mtakatifu kwa kusudi lile kuu, Roho Mtakatifu
huondoa woga wote na kutupa ujasiri, na nguvu na upendo ili tuweze kusonga
mbele kwa wito tulioitiwa hivyo hatuwezi kunyamaza, Ni yeye ambaye akiwa ndani
yetu tutavurugwa, tutachukizwa na sanamu, tutataharakishwa hatutakubali uonevu
wa ibilisi dhidi ya ndugu zetu, tutawaombea watu, tutawafungua watu, tutawapa
watu mahitaji yao kwa msukumo wa Roho Mtakatifu ndani yetu ni yeye ni yeye ni
yeye anayesababisha hatuwezi kunyamaza kamwe!
2Timotheo 2:8-9 “Mkumbuke Yesu Kristo,
aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu. Nami
katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu
halifungwi.”
Mwisho Paulo mtume akiwa
kifungoni anamkumbusha Timotheo kumkumbuka Yesu aliyefufuka katika wafu, ya
kuwa uko ushindi katika maisha yetu ya kazi ya injili kama Daudi alivyoshinda
Vita vyote kwa jinsi ya mwili, Yesu naye ameshinda vita vyote vya kiroho, kwa
hiyo hata ingawa Paulo mtume alikuwa kifungoni, alimwambia Timotheo kuwa neno
la Mungu halifungwi, akiwa kifungoni hakuweza kunyamaza na badala yake alianza
kuandika nyaraka zenye kuwatia moyo waamini na watumishi wa Mungu na kuendelea
kuwajenga, Katika nyakati zetu leo hata kama tutakuwa gerezani, injili
itaendelea kwa sababu Roho Mtakatifu hatatuacha kunyamaza. Neno la Mungu
halifungwi! Roho Mtakatifu hatatuacha tuwe na utulivu bila kutimiza ile huduma
ya upatanisho aliyoiweka ndani yetu haleluyaa!
Hitimisho
Usinyamaze kwaajili ya kile
ambacho Mungu amekuitia kukifanya uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha yetu
unatufanya kuwa na msaidizi wa karibu ndani yetu, kiongozi ndani yetu, mwenye
kututia nguvu, na anatutia nguvu na kutupa nguvu za ushawishi ndani yetu,
Hatuna budi kumtii na kukubali kuongozwa
naye katika kuyatii mapenzi yake na tunapomtii atasema nasi na kutusukuma kama
nguvu ya moto ndani yetu akiweka wivu, wa Bwana na kutusukuma katika kuyatii
mapenzi yake kwa hiyo ni lazima kuhakikisha kuwa tunaihubiri injili kwa namna
yoyote kila mmoja kwa kadiri ya wito wake alioitiwa na kamwe tusiache kwa
sababu tukiacha watu watakengeuka, mwenye kuomba asiache kuomba, mwenye
kuhubiri asinyamaze, mwenye kutoa asiache, mwenye kuangalia wafungwa asiache,
mwenye kufariji wajane na yatima asiache, mwenye kushuhudia asiache, mwenye
kufundisha asiache mwenye kusimamia asiache, mwenye kutia moyo asiache na
mwenye kuandika kama mimi asiache hakuna anayeweza kutunyamazisha kwa sababu
Roho wa Mungu anataka kila kitu kitimizwe ndani yetu kwa wakati wake!
2Timotheo 4:1-5 “Nakuagiza mbele za Mungu,
na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa
kwake na kwa ufalme wake; lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati
usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana
utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia
zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya
utafiti;nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za
uongo.Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya
mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.”
Warumi 12:4-8 “Kwa kuwa kama vile katika
mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; Vivyo
hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja
kwa mwenzake. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema
mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo
katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya,
katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa
bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.”
Roho wa Mungu hututia nguvu
katika maisha yetu kuishinda aibu, woga, na vikwazo na kutupa ujasiri na hali
ya kutokuweza kukaa kimya akitenda kazi ndani yetu na kututia nguvu na ujasiri
na kutuagiza kwa neno lake na kwa sababu hiyo hatuwezi kunyamaza, Martini Luther King Jr alikuwa
mchungaji lakini wakati huo ulikuwa ni wakati wa ubaguzi mkubwa wa rangi nchini
Marekani, alisimama sio tu kama Muhubiri lakini aliionyesha jamii kuwa matukio
ya kibaguzi sio kitu sahihi, hakunyamaza kila lilipojitokeza tukio la kibaguzi
na aliuawa kwaajili ya hilo, naamini kuwa Mungu alimtia nguvu, kutokukaa kimya
na yeye alisema tutakaa kimya pale tu tutakapokuwa tumekufa, au kwa lugha
nyingine Maisha yetu hufikia mwisho pale tu tunapoanza kukaa kimya kwaali ya
maswala ya msingi “Our lives begin to end the day we become
silent” Bill Bright yeye alisema
“Why we cannot remain Silence” kwanini hatuwezi kukaa kimya akikazia kwa
sababu tuna agizo kuu la kuihubiri injili, na mimi nimesema kwanini hatuwezi
kunyamaza kwa sababu Roho Mtakatifu yuko ndani yetu naye ndiye kichocheo na
sababu kwanini hatuwezi kunyamaza.
Wewe nawe kamwe usikae kimya kwa
kile ambacho Roho Mtakatifu amekuwekea ndani yako, Endelea kupiga kelele kama ni za uamsho, kemea
kama ni za kukemea manabii wa uongo, kama ni injili ihubiri, unazo sababu
lukuki kwanini hauwezi kukaa kimya, tunazo sababu nyingi kwanini hatuwezi kunyamaza
haleluyaaa! Uongezewe neema
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni