Zaburi 15:1-5 “Bwana, ni nani atakayekaa Katika hema yako? Ni nani
atakayefanya maskani yake Katika kilima chako kitakatifu? Ni mtu aendaye kwa
ukamilifu, Na kutenda haki. Asemaye kweli kwa moyo wake, Asiyesingizia kwa
ulimi wake. Wala hakumtenda mwenziwe mabaya, Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa, Bali huwaheshimu wamchao Bwana Ingawa
ameapa kwa hasara yake, Hayabadili maneno yake. Hakutoa fedha yake apate kula
riba, Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo
Hataondoshwa milele.”
Utangulizi:
Mojawapo ya siri muhimu ya
mafanikio yetu na ustawi wetu wa kiroho na kimwili ni pamoja na kuwepo katika
uwepo wa Mungu, uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu unaunganishwa na uhai
wake, adhabu kubwa na mbaya kuliko zote anazoweza kuwa nayo mwanadamu ni
kufukuzwa katika uwepo wa Mungu au Mungu kuondoa uwepo wake katika maisha yetu,
Mungu akiondoa uwepo wake katika maisha yetu yeyote yule atakayetuona atatuua,
Kaini alielewa ubaya wa kuondoka au kuondolewa katika uwepo wa Mungu
(Kusitirika mbali na Uso wake).
Mwanzo 4:11-14 “Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa
chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; utakapoilima ardhi haitakupa
mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani. Kaini akamwambia
BWANA, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo
katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu
asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.”
Kuwa mbali na Uso wa Mungu
kungeweza kusababisha kifo wakati wowote cha kiroho na kimwili pia, sio hivyo
tu mambo yetu kuharibika, Na kutembea na kuwa katika uwepo wa Mungu kungeweza
kusababisha mafanikio na ustawi katika maisha ya kila mwanadamu, na ndio maana
kutengwa na Mungu ni kifo, ni adhabu mbaya na ya juu kabisa katika mamlaka ya uungu,
tunawezaje kutoboa katika maisha haya, huduma, familia, uchumi na kila kitu
bila uwepo wa Mungu?, Na ndio maana mwandishi wa zaburi anatupa kanuni kadhaa
zitakazotusaidia kuendelea kukaa katika uwepo wa Mungu kwa kujibu swali hilo
Bwana ni nani atakayekaa katika hema yako? Kwa msingi huo basi leo tutachukua
muda kujifunza namna na jinsi tunavyoweza kukaa katika uwepo wa Mungu katika
maisha yetu, na tutajifunza somo hili Bwana ni nani atakayekaa katika hema yako
kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya kukaa katika Hema ya Bwana
·
Bwana ni nani atakayekaa katika hema yako?
·
Faida za kukaa katika Hema ya Bwana.
Maana ya kukaa katika Hema ya Bwana.
Nyakati za agano la kale Mungu
alipotaka kukutana au kuzungumza na kujifunua kwa watu wake alitoa maelekezo maalumu
kwa Musa namna na jinsi ya kutengeneza nyumba maalumu yaani Hema ambayo
ilitengenezwa kwa maelekezo ya Mungu kwa kusudi la kukutana na watu wake, au
kwa kusudi la kuwa pamoja nao, Hema hii ilijulikana kama Hema ya kukutania,
yaani mahali ambapo Mungu alikutana na watu wake kwa sababu zozote zile za
kimwili na kiroho, kwa sababu hiyo awaye yote alipokuwa na changamoto yoyote na
akawa anataka kusikia kutoka kwa Bwana alimjilia Musa na kuhani mkuu Haruni ambaye angeingia katika hema hiyo na
kupata maekezo kutoka kwa Bwana
Hesabu 12:4-5 “Bwana akanena ghafula na Musa, na Haruni na Miriamu, na
kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao
watatu wakatoka nje.Bwana akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale
mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili.”
Kwa hiyo kimsingi hema ya Bwana
ilikuwa ni mahali Muhimu pa kukutanisha uwepo wa Mungu na wanadamu hususani
Israel kwa wakati ule walipokuwa safarini jangwani, na ni katika uwepo wa Mungu
majibu ya changamoto zozote za kibinadamu yangeweza kutatuliwa, kwa ufupi hema
ya bwana ilikuwa inawakilisha UWEPO WA
MUNGU, na kwa bahati nzuri sasa uwepo huu wa Mungu katika nyakati za agano
jipya unakaa ndani yetu. Kwa hiyo tunapodumisha uhusiano wetu na Mungu pia
tunadumisha uwepo wake kwetu
Neno uwepo wa Mungu, katika kiingereza
Gods’ Presence katika lugha ya
kiebrania linatumika neno “Pānīm”
ambalo maana yake ni USO yaani
uwepo wa Mungu pia ulitambulika kama uso
wa Mungu
Kutoka 33:14-16 “Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa
raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka
hapa. Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu
wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na
watu wote walio juu ya uso wa nchi?”
Unaona? Kwa hiyo nyakati za agano
la kale watu waliotutangulia walikuwa na ufahamu wa kutosha kuwa bila uso wa
Mungu, bila uwepo wa Mungu hawawezi kufanikiwa na wala hawawezi kupata neema,
lakini sio hivyo tu uwepo wa Mungu ungeweza kuwatofautisha watu wa Mungu na
watu wengine wote wakaao juu ya uso wa nchi.
Uwepo wa Mungu au uso wa Mungu
pia ulikuwa unamwakilisha Roho Mtakatifu ambaye katika agano la kale vilevile
alijulikana kama Malaika wa uso wake. (The
Angel of his Presence).
Isaya 63:9-10 “Katika mateso yao yote yeye aliteswa, na malaika wa uso
wake akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake, aliwakomboa mwenyewe;
akawainua, akawachukua siku zote za kale. Lakini wakaasi, wakamhuzunisha Roho
yake Mtakatifu; kwa hiyo akawageukia, akawa adui, akapigana nao.”
Unaweza kuona; Kwa hiyo swali
kama hili la mwandishi wa zaburi Bwana ni nani atakayekaa katika hema yako? Ni
sawa na kuuliza ni nani atakayetembea na uwepo wa Mungu, ni nani atakayekaa
mbele za uso wako, ni nani atakuwa na Roho wako Mtakatifu, kwa hiyo ni zaburi Muhimu
inayotuonyesha na kutukumbusha namna ya kukaa katika uwepo wa Mungu na
kuhakikisha kuwa katika maisha yetu Bwana hatuondolei Roho wake Mtakatifu
ambaye kimsingi tukitengwa naye kila kitu kitakuwa kimefikia mwisho na
mafanikio yetu ya kiroho na hata kimwili yanaweza kuwa matatani, kwa hiyo
kutengwa na Uso wa Mungu ilikuwa pia ina maana ya kuondoka kwa Roho Mtakatifu
katika maisha yetu Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuendelea kukaa katika
uwepo wa Mungu siku zote za maisha yetu Katika jina la Yesu Kristo Amen
Zaburi 51:10-12 “Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia
ndani yangu Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.
Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi.”
1Samuel 16:14 “Basi, roho ya Bwana ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya
kutoka kwa Bwana ikamsumbua.”
Bwana ni nani atakayekaa katika hema yako?
Zaburi 15:1-5 “Bwana, ni nani atakayekaa Katika hema yako? Ni nani
atakayefanya maskani yake Katika kilima chako kitakatifu? Ni mtu aendaye kwa
ukamilifu, Na kutenda haki. Asemaye kweli kwa moyo wake, Asiyesingizia kwa
ulimi wake. Wala hakumtenda mwenziwe mabaya, Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa, Bali huwaheshimu wamchao Bwana Ingawa
ameapa kwa hasara yake, Hayabadili maneno yake. Hakutoa fedha yake apate kula
riba, Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo
Hataondoshwa milele.”
Mwandishi wa zaburi ameandika
katika mtindo wa kuuliza swali, na kisha anajaribu kutoa majibu ya swali hilo
yeye mwenyewe, anauliza ni Ni mtu wa namna gani anayeweza kudumisha uhusiano wa
ukaribu na Mungu, ni nani anayeweza kutunza uwepo wa Mungu, ni mtu wa namna
gani ambaye Roho Mtakatifu atapenda kufanya makazi naye na anataja maswala kadhaa
ambayo kwa mtazamo wake yanaweza kuleta huzuni kwa Roho Mtakatifu au
kusababisha uwepo wake upungue au kuondoka katika maisha yetu? Kwani kupoteza
uwepo wa Mungu ni kupoteza kila kitu katika maisha yetu Mwandishi anatupa mambo
kadhaa ya kufanya au ya kujiepusha nayo ili kutunza uwepo wa Mungu katika
maisha yetu na kunufaika na uwepo wa Mungu ambao ni wa Muhimu sana katika
maisha yetu.
1.
Kuenenda
kwa ukamilifu – Mwandishi anaeleza kuwa sifa mojawapo ya mtu anayeweza
kukaa katika uwepo wa Mungu ni pamoja na mtu aendaye kwa ukamilifu hii maana
yake ni nini? Tunawezaje kuenenda kwa ukamilifu, neno kwa ukamilifu katika
biblia ya kiebrania linasomeka kama “tâmîym”
ambalo maana yake mtu aendaye kwa
usahihi katika mawazo na maneno na matendo, huyu ni mtu ambaye anachokisema
ndicho alichokimaanisha na ndicho atakachotenda kwa hiyo ni mtu asiye na hila,
tunaishi katika nyakati ambazo watu wengi wamekuwa wanafiki au wenye hila, kile
anachokisema na moyo wake hauendani au muonekano wake na matendo yake ni vitu
viwili tofauti, tabia ya unafiki ambao kimsingi anayeweza kuichungulia ni Mungu
ni tabia inayomuhuzunisha sana Roho Mtakatifu, Dunia inakabiliwa na ombwe kubwa
la watu ambao hawajanyooka Jambo ambalo Yesu aliliona katika mioyo na matendo
ya Mafarisayo
Mathayo 23:1-3 “Kisha Yesu akawaambia makutano na
wanafunzi wake, akasema, Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa;
basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa
matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi.”
2.
Kutenda
Haki – Kutenda haki katika lugha ya kiebrania wanatumia neno “tsedeq” ambalo kwa kiingereza ni “equity” au Fairness au Justice in the
way people are treated yaani ni kutenda haki, na usawa unapowahudumia watu
yaani bila upendeleo, kwa hiyo kama mtu huyu ni hakimu basi maana yake
anasimamia haki, kama ni mwana siasa anasimamia usawa anatoa haki sawa, Katika
agano jipya neno hilo linaenda mbali zaidi kwani neno linalotumika katika
kiyunani ni “Poieō” ambalo maana yake ni kutoa haki
ya mtu kwa uwazi bila kuichelewesha to
make an apparently justice or equity without prolonged, Mtu anayetenda haki
bila kuichelewesha hakuna udhalimu kwake amenyooka siku za leo kuna changamoto
kubwa sana katika sehemu nyingi kwa sababu hata kama kitu ni haki yako unaweza
ukakipata kwa kucheleweshwa sana, au kwa kuzungusha zungushwa njoo leo njoo
kesho hii ni aina ya udhalimu ambayo inaondoa sana na kupoteza uwepo wa Mungu
kila mahali kuna urasimu, wengine wanapewa haki yao upesi wengine
unawachelewesha, kutokutoa haki ya mtu upesi ni mojawapo ya udhalimu mkubwa
kimaandiko:-
Luka 18:1-8 “Akawaambia mfano, ya kwamba
imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na
kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo
palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki
na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa
simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi,
nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema,
Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule
wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia
haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? ”
Haki iliyocheleweshwa
ni sawa na haki iliyonyimwa, Mungu hacheleweshi haki ya Mtu, lakini watu
dhalimu wasiomcha Mungu huchelewesha huduma kwa watu, unaweza kucheleweshwa
hospitali, unaweza kucheleweshwa polisi, unaweza kucheleweshwa mahakamani,
unaweza kuchelewesha benki na fedha ni ya kwako, unaweza kucheleweshwa kwenye
maofisi ya watu na asiwepo wa kukujali wala kukuhudumia, unaweza kuchelewesha
standi na mnasafiri lakini basi haliondoki kwa wakati, mnaweza kucheleweshwa
malipo yako ya kustaafu, mnaweza kucheleweshwa mshahara, na kadhalika wako watu
ambao wakifanya hayo na kuweka mlolongo mrefu wa kuwahudumia watu wanadhani
ndio sifa lakini maandiko yanaonyesha ya kuwa urasimu na upendeleo sio tabia ya
uungu na inafifisha uwepo wake wahudumie watu kwa haraka sana wapatie haki yao
upesi, na usione sifa kuwapanga watu kwenye foleni, au kuchelewesha malipo ya
watu na hili ni mojawapo ya tatizo kubwa sana hasa kwa wahasibu katika maeneno
mbalimbali.
1Yohana 3:7 “Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye;
atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki;”
3.
Asemaye
kweli kwa moyo wake - Mtu anayesema
kweli moyoni mwake kwa kiebrania anaitwa “Emeth”
yaani ni mtu wa kuaminika
“trustworthiness” mtu anayesema anachokitenda, changamoto kama hii ilimgharimu
sana Sauli na huenda Daudi alikuwa amejifunza kuwa ni lazima mtu usimamie kile
unachokitamka, watu wanaovunja ahadi sio
watu wa kuaminika, lakini wale wanaotunza ahadi hao tunaweza kuwaamini na uwepo
wa Mungu hukaa na watu ambao wanasema kweli, kutoka moyoni anachokisema ndicho
atakachokitekeleza, je kiongozi wako wewe anachokisema ndicho anachotekeleza?
Wewe mwenyewe na mimi je tunaweza kuaminiwa hata katika ngazi ya familia yetu?
Mumeo, mkeo au watoto wako wanaweza kukuamini kwamba ukisema kitu unakisimamia?
Kiongozi wa kisiasa uliyemchagua au kokote kule je anasema kweli kwa moyo wake?
Anachokiahidi anakitekeleza? Dunia inakosa watu wa aina hii katika nyakati za
leo ambao anachokisema sio wanachokitekeleza, Mungu anasikitishwa sana na uwepo
wake unaweza kumuacha mtu asiyeaminika, mtu ambaye ndio yake si ndio na sio
yake ni ndio ndumilakuwili
1Samuel 15:1-14 “Wakati huo Samweli akamwambia Sauli,
Bwana alinipeleka nikutie mafuta, uwe mfalme wa watu wake Israeli; basi sasa,
isikilize sauti na maneno ya Bwana. Bwana wa majeshi asema hivi, Nimeyatia
moyoni mwangu mambo hayo Amaleki waliyowatenda Israeli, jinsi walivyowapinga
njiani, hapo walipopanda kutoka Misri. Basi sasa enda ukawapige Amaleki, na
kuviharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo, wala msiwaachilie; bali waueni,
mwanamume na mwanamke, mtoto naye anyonyaye, ng'ombe na kondoo, ngamia na
punda. Ndipo Sauli akawaita watu, akawahesabu huko Telemu, askari waliopanda
farasi mia mbili elfu, na watu wa Yuda kumi elfu. Sauli akaufikilia mji wa Amaleki,
akauvizia bondeni. Sauli akawaambia Wakeni, Haya! Enendeni zenu, mkashuke ili
kujitenga na Waamaleki, nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao; maana
mliwatendea wana wa Israeli mema, walipopanda kutoka Misri. Basi hao Wakeni
wakaondoka, wakajitenga na Waamaleki. Sauli akawapiga Waamaleki, toka Havila
uendapo Shuri, unaokabili Misri. Akamkamata Agagi, mfalme wa Waamaleki, yu hai,
akawaangamiza hao watu wote kwa upanga. Lakini Sauli na watu wake wakamwacha
Agagi hai, na katika kondoo walio wazuri, na ng'ombe, na vinono, na
wana-kondoo, na cho chote kilicho chema, wala hawakukubali kuwaangamiza; bali
cho chote kilichokuwa kibaya na kibovu, ndicho walichokiangamiza kabisa. Ndipo
neno la Bwana likamjia Samweli, kusema, Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe
mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli
akasikitika, akamlilia Bwana usiku kucha. Samweli akaondoka asubuhi na mapema
ili aonane na Sauli; Samweli akaambiwa ya kwamba, Sauli alifika Karmeli, na
tazama, akajisimamishia ukumbusho, akageuka, akapita, akatelemkia Gilgali.
Samweli akamwendea Sauli; naye Sauli akamwambia, Ubarikiwe na Bwana,
nimeitimiza amri ya Bwana. Samweli akasema, Maana yake nini, basi, hiki kilio
cha kondoo masikioni mwangu, na huu mlio wa ng'ombe ninaousikia? ”
4.
Asiyesingizia
kwa ulimi wake - Kusingizia kwa ulimi katika lugha ya kiebrania linatumika
neno “Râgal”
ambalo kwa kiingereza tunapata neno
“Slander” na “backbite” ambalo maana yake ni kusengenya, au kumtengezea mtu
Kashfa, kutengeneza maswala ya uongo dhidi ya mtu mwingine kwa kusudi la
kuharibu sifa zake au kumchafua au kumuharibia hii iko kinyume na amri ya Mungu
usishuhudie uongo Kutoka 20:16 “Usimshuhudie
jirani yako uongo.” Mtu anayesengenya na kutoa ushahidi wa uongo kwa
nia ya kuharibu heshima ya mtu mwingine mtu huyo anaingizwa kwenye kundi la
vitu vinavyomchukiza sana Mungu, Roho Mtakatifu ni Roho wa kweli,
tunaposhuhudia uongo anaumia sana na anaweza kujiondoa taratibu katika maisha
yetu na ukakosa kukaa katika uwepo wake, watu wengi waliookoka wanasengenya
sana, wamepona katika maeneo mengi lakini kusengenya inaonekana kama jambo la
kawaida hakuna anayechukia kusengenya, unakuta watu waliookoka ndio wanaongoza
kusema mabaya ya walokole wenzao na kuwachafua, Masengenyo, kusingizia
kuwchafua watu na kuwaema watu vibaya ni kawaida tu katika kanisa
Mithali 6:16-19 “Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana;
Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na
mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo
myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu
za fitina kati ya ndugu.”
Dalili za kilele
cha uharibifu wa moyo wa mwanadamu, au kuonyesha kuwa watu ni waovu ni pamoja
na kusingizia, Je leo hakuna malalamiko ya watu wanaowasingizia wengine? Au
kuzungumza mambo ambayo hawana uhakika nayo, wala wasiyoyajua kwa usahihi, Wako
watu wengi sana wamesingiziwa mambo yasiyofaa, wengine wamefungwa kwa sababu ya
kusingiziwa, wengine wameharibiwa heshima zao, Daudi anaona kuwa kusingizia
watu kutengenezea watu uongo (skendo) kama moja ya changamoto itakayomkosesha
mtu anayetaka kukaa katika hema ya Mungu, kumbuka Yezebeli alivyofanya kwa
Nabothi na kusababisha mauti yake kwa sababu ya moyo wa tamaa, wako watu wengi
sana wanaumizwa katika maisha kwa sababu tu ya watu ambao wanasingizia wengine,
au kutoa ushahidi wa uongo na kuharibia watu maisha yao na haki kupindishwa,
usitoe maneno ya uwongo kwa kusudi la kumdhuru mtu mwingine.
1Wafalme 21:1-16 “Ikawa baada ya hayo, Nabothi
Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya
kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe
shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba
yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au
ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. Nabothi akamwambia Ahabu,
Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. Basi Ahabu akaenda
nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile
aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu.
Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula. Lakini Yezebeli
mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula?
Akamwambia, Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia, Unipe shamba
lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine
badala yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu. Yezebeli mkewe
akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula,
moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. Basi,
akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile
nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa
pamoja na Nabothi. Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu
kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, mkainue watu wawili, watu wasiofaa,
ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha
mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe. Wale wazee wa mji wake, na walio
wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama
ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu kufunga,
wakamweka Nabothi juu mbele ya watu.Na hao watu wawili, watu wasiofaa,
wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele
ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya
mji, wakampiga kwa mawe hata akafa. Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema,
Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa.Ikawa Yezebeli aliposikia ya kwamba Nabothi
amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka, ulitamalaki shamba
la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa fedha, maana Nabothi
hako hai, lakini amekufa.Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa,
akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili alitamalaki.”
5.
Wala
hakumtenda mwenziwe mabaya – Kumtenda mtu mabaya katika lugha ya kiebrania
kunatumika neno “ra’ râ’âh”
kwa kiingereza wickedness, bad au evil ni mtindo mzima wa maisha yasiyo ya haki, yasiyoheshimu utu,
yasiyo ya kweli, ya tamaa, ya uovu, yaliyojaa dhambi, ni mfumo mzima
usiokubalika kwa Mungu, kuanzia mawazo mabaya mpaka na matendo yake hali hii
inaweza kupelekea Mungu kuangamiza ulimwengu au kuondoa uwepo wake kwa
mwanadamu na kumuacha aenende katika upotofu wake.
Mwanzo 6:5-6 “BWANA akaona ya kuwa maovu ya
mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni
baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani,
akahuzunika moyo.”
Hakisha wakati
wote haumleti mwanadamu mwenzio katika hatua ambayo atajutia na kuhuzunkia na
kuwa na msongo wa mawazo na kusikitika kutokana na dhuluma atakayokuwa
ametendewa
6.
Muovu
ni muovu na mwema ni mwema – Zaburi
15:4 “Machoni
pake mtu asiyefaa hudharauliwa, Bali huwaheshimu wamchao Bwana Ingawa ameapa
kwa hasara yake, Hayabadili maneno yake.” Uwepo wa Mungu unakaa na watu ambao kwao
sheria ya Mungu na maneno yao hayabadiliki, kama kitu ni uovu husimama kama
kiovu na kama kitu ni chema husimama katika wema huo, uwepo wa Mungu haukai na
watu wanaobadili haki ya Mungu kuwa kitu kingine wala hawana upendeleo,
hawawezi kuwafurahia wanaotenda udhalimu na kuwakubali kana kwamba wanasimama
na kweli, wao husimama na kweli na kuifurahia kweli wakati wote, wanadamu wanapoharibika huwa na tabia ya
kubadilisha mambo, jambo linaweza kuwa baya na jamii iliyokengeuka ikaona kuwa
jambo hilo ni sawa tabia za aina hiyo huondoa uwepo wa Mungu, mfano kule
Korintho katika kanisa lililokuwako kuna mtu alikuwa na mke wa baba yake na
kanisa lilikuwa linaona poa tu, watu wanavaa nusu uchi na unaona poa tu, watu
wanakula rushwa na unaona poa tu yaani hawasikitiki pale ukengeufu unapotokea,
maovu yanaweza kutendeka na ikaonekana sawa tu
1Wakorintho 5:1-3 “Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu
kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe
na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe
miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo. Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa
mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye
aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo.”
Isaya 5:20 “Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema,
na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza;
watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu! ”
Mungu
anapendezwa na jamii iliyonyooka hakuna kubadili badili, kama ndoa za jinsi
moja ni mbaya dunia isimame na kukemea kuwa huu ni uovu usiokubalika,
haiwezekanani jambo likawa baya alafu kanisa linapata kigugumizi cha kukemea na
kusema hili ni baya ndoa za jinsi moja haziruhusiwi kufungwa kanisani wala
kanisa haliwezi kuhalalisha ni muhimu kulikemea hilo kama lilivyo bila kupaka
mafuta kwa kisingizi cha haki za binadamu, kama kitu ni kiovu tukikemee, na
kama kitu ni chema tikitie moyo, Mtu atakayekaa katika uwepo wa Mungu ni mtu
asiyepinda pinda kwake yeye mwema ni mwema na muovu ni muovu hakuna kupaka
rangi, hakuna kujivunia, kumekuweko na makanisa ambayo yanatetea ushoga na
usagaji ati kwa sababu watu hao wana fedha sana na kwa hila wanaingiza aina ya
mafundisho Fulani ya kutaka kanisa likubaliane na jambo hilo Maandiko yanasema
hata sadaka na malipo ya watu hao yasipokelewe wala kuletwa katika nyumba ya
Mungu angalia maandiko
Kumbukumbu 23:18 “Usilete ujira wa kahaba, wala
mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo
yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili.”
Fedha za
makahaba na mshahara wa mbwa ni fedha za watu wanaoishi maisha ya kimalaya,
kisagaji na kishoga hawa Mungu amekataa kukubaliana nao na kusema ni watu wema
tukikaribisha hali hii kokote pale uwepo wa Mungu utaondoka, tuwanyooshee
maelezo kwamba watubu na kubadilika na kumpokea Yesu na kuwa watu wema vinginevyo
neno la Mungu halikubali kuchukuliana na uovu, uovu ni uovu na wema ni wema
7.
Hakutoa
fedha yake apate kula riba – Nyakati za Agano la kale Mungu alikuwa
amewakataza wana wa Israel, wanapokopesha waisrael wenzao wasitwae riba, lakini
wangeweza kuchukua riba kwa wageni, sheria hii inafanya kazi pia kwa waislamu,
muislamu hapaswi kumkopesha muislamu mwenzake kwa riba, na hata akiweka fedha
Benki na ikazalisha faida hachukui ile faida na ndio maana wana benki maalumu
za kutokuchukua riba, hii inaweza kuwa sawa kwa Mkristo pia kwamba asichukue
riba kwa Mkristo mwenzake, leo hii dunia imeingia katika wimbi kubwa sana la
mikopo yenye riba kubwa sana na ambazo zimesababisha mateso makubwa sana katika
jamii, iko mikopo ambayo ina riba kubwa sana kwa sababu watu wanataka faida
kubwa kupitia fedha aliyoazimisha, maisha ya watu wengi yameumizwa, watu
wameweka rehani vitu vyao na watu wameaibishana kwa sababu ya moyo wa tamaa wa
kutaka Riba, watu wengi sana wamejikosesha Baraka kwa sababu ya kutaka riba
kubwa na faida kubwa hata kwa ndugu zao
bila kujali uchaji wa Mungu, na ndio maana hali inazidi kuwa mbaya duniani kila
iitwapo leo, unakopa laki moja mtu anataka arudishiwe laki na nusu au zaidi,
kwa hiyo kwa sababu ya shida watu hukopa lakini wanashindwa kuzalisha ile riba
na hivyo kujikuta wakiwa wahanga wa mikopo na kudhalilika vibaya Mungu alikataa
jambo hili. Unaweza kulifanya kwa mtu
asiye wa imani yako lakini sio kwa ndugu yako kumbuka hilo usisahau. Daudi
anasema atoaye fedha ili apate kula riba uwepo wa Mungu huondoka kake na Bwana
hawezi kufanya maskiani na mtu wa namna hiyo, mikopo imetesa wengi katika miaka
ya hivi karibuni kuliko lolote, tumesikia leo hii mikopo yenye majina ya
kukomoa sana na kusikitisha mfano mkopo kausha damu, au mikopo umiza na
kadhalikamikopo hiyo imeumiza watu na watu
wanadaiana mpaka wanauana, huku ndiko jamii inakokwenda leo kwa sababu ya
kutaka riba kubwa sana wakati wa marejesho,
na wakati mwingine mikopo hiyo umiza ina masharti yasiyo wazi na wala
haioneshi kiwango cha marejesho, watu wamedhalilishwa, watu wamepoteza mali
zao, watu wamekimbia miji, na wengine kupoteza maisha wengine nyumba
zimeandikwa ukutani nyumba inauzwa, au rejesha mkopo wa watu banki na kadhalika
maumivu haya wanayoyapata watu yanachangia kuleta laana katika taifa na kuondoa
uwepo wa Mungu, ndio maana Mungu hakutaka riba.
Kumbukumbu 23:19-20 “Usimkopeshe
ndugu yako kwa riba; riba ya fedha, riba ya vyakula, riba ya kitu cho chote
kikopeshwacho kwa riba; mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu
yako kwa riba; ili Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika yote utiayo
mkono wako, katika nchi uingiayo kuimiliki.”
8.
Hakutwaa
rushwa amwangamize asiye na hatia – Moja ya changamoto kubwa ambayo
inaikabli jamii inayoharibika ni pamoja na Rushwa, rushwa katika mazingira
yoyote ile inaaathiri utoaji wa haki na kusababisha dhuluma, lakini sio hivyo
tu upendeleo pia ni dhuluma ni rushwa maandiko yamekataza, ni kupitia rushwa
unaweza kuona jamii ikiumziwa kila iitwapo leo na haki ikipindishwa rushwa ni
adui wa haki
Kumbukumbu 16:18-20 “Weka waamuzi na
maakida katika malango yako yote akupayo Bwana, Mungu wako, kwa hesabu ya
kabila zako; nao wawaamue watu kwa maamuzi ya haki.Usipotoe maamuzi; wala
usipendelee uso wa mtu; wala usitwae rushwa; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya
wenye akili, na kugeuza daawa ya wenye haki.Yaliyo haki kabisa ndiyo
utakayoyafuata, ili upate kuishi na kuirithi nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.”
Yakobo 2:1-4 “Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu
Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu.Maana akiingia
katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha
akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi
mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini,
Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu,
mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? ”
Je wewe unapokea
rushwa? Je wewe unapendelea watu? Ukitaka kujua ubaya wa maamuzi mabaya
shabikia mpira kisha uone timu yako ikifungwa goli la uonevu tu aidha kwa
sababu refa yaani mwamuzi ameamua kuipendelea timu Fulani, au kuibeba ule uchungu na maumivu
yanayowapata wale waliofungwa kwa kukosa haki ndio uchungu ambao maandiko
unataka tuyaepuke, au pale mnaenda kwenye sanduku la kura na kumchagua mtu
Fulani kisha anayetangwazwa kwenye matokeo kama mshindi ni mtu mwingine ndio
maana neno linatutaka kuhakikisha kuwa tunatenda haki na kutokupokea rushwa au
kupendelea watu na kupotosha hukumu ya yule asiye na hatia, Bwana ni nani
atakayekaa katika uwepo wa bwana ni mtu asiyepotosha hukumu mtu atendaye haki.
Faida za kukaa katika Hema ya Bwana
Neno la Mungu linahitimisha kwa
kuonyesha ya kuwa kama tutayatendea kazi yale ambayo Mungu ametufunza hapo
maana yake ni nini kila kitu katika maisha yetu kitadumu na uwepo wa Mungu
utakuwa pamoja nasi siku zote hata milele angalia Daudi anasema atendayo hayo
hataondoshwa.
Zaburi 15:1-5 “Bwana, ni nani atakayekaa Katika hema yako? Ni nani
atakayefanya maskani yake Katika kilima chako kitakatifu? Ni mtu aendaye kwa
ukamilifu, Na kutenda haki. Asemaye kweli kwa moyo wake, Asiyesingizia kwa
ulimi wake. Wala hakumtenda mwenziwe mabaya, Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa, Bali huwaheshimu wamchao Bwana Ingawa
ameapa kwa hasara yake, Hayabadili maneno yake. Hakutoa fedha yake apate kula
riba, Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo
Hataondoshwa milele.”
Unaona mtu atendaye mambo hayo
hataondoshwa milele, mtu huyu atakuwa imara katika roho, mwili na ustawi kwa
sababu uwepo wa Mungu utakuwa pamoja naye, uhusiano wake na Mungu utadumu na
Mungu atakaa na mtu huyo, kwa vyovyote vile mtu hawezi kuna na sifa alizozitaja
Daudi katika zaburi yake kama halijui neno la Mungu, maagizo hayo yote yako
katika neno na ni mtu anayeyaangalia maagizo ya Bwana ni lazima atakuwa mtu
mwenye roho iliyopondeka na anayelicha jina la Bwana au kutetemeka asikiapo
neno lake mtu wa namna hii Bwana ameahidi kukaa naye katika uwepo wake
Isaya 66:2 “Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi
vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia,
mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.”
Mtu wa namna hii ni lazima
atakuwa anamjua sana Mungu, na ni lazima atafanikwa na amani ya Mungu itakuwa
juu yake, Ayubu 22:21 “Mjue sana
Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.” Unapokuwa na
uwepo wa Mungu Amani ya Mungu inakuwa ni sehemu ya maisha yako.
Mtu wa namna hii ni lazima
atakuwa ni mtu anayemtumainia Mungu, na hana namna ya kupita shortcut – njia ya
mkato kwa rushwa na kupindisha hukumu za watu, wala kutoa ushahidi wa uongo,
kuishi kwa haki na ukamilifu wa moyo kunataka wakati wote uwe ni mtu
unayemtegemea Mungu na Mungu hataacha kumbariki mtu wa namna hiyo kwa hiyo mtu
huyo hufunikwa na Baraka za Mungu.
Yeremia 17:7-8. “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini
Lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake
karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa
bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa
matunda.”
Zaidi ya yote mtu huyu ataurithi
uzima wa milele kukaa katika hema ya Mungu maana yake sio tu kufurahia uwepo
wake tuwapo duniani, lakini vile vile Mungu atakaa pamoja nasi Daima kumbuka
wazo la Mungu la ile hema ya kukutania ilikuwa ile maskani ya Mungu iwe pamoja
na wanadamu Milele.
Ufunuo 21:3 “Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi
ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani
yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.”
Hitimisho:
Zaburi hii ya 15 inatupa picha ya
wazi ya Mtu ambaye Mungu angependa kumkaribisha katika uwepo wake, Neema ya
Mungu inamualika kila mmoja wetu kujifunza na kukubali kuitikia mwitikio huu na
kujiuliza na kujipima kama tunaishi kile ambacho Mungu Roho Mtakatifu
anatufundisha kubwa zaidi na lenye furaha ni kukaa katika uwepo wa Mungu na
kuwa na urafiki wa kudumu na Mungu. Uongezewe neema unapoyatendea kazi maneno
ya Mungu.
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.