Ezekiel 28:13-15 “Ulikuwa ndani
ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako,
akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na
yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na
filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa
tayari. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka
hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe
ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata
uovu ulipoonekana ndani yako.”
Utangulizi
Leo tutachukua Muda
kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusu Shetani, inawezekana kuwa ni mara
nyingi sana umewahi kusikia kuhusu shetani na huenda anatajwa sana na kila
mwanadamu na katika mahubiri anatajwa mara nyingi kila kona ya dunia, lakini
uko uwezekano kuwa hujawahi kupata mafundisho ya kutosha kuhusu shetani, Leo
Roho Mtakatifu anatutaka tuchukue muda kidogo kujifunza na kujikumbusha kuhusu
shetani pamoja na kazi zake zote anazozifanya na kuhakikisha kuwa wakati wote
tunamuelewa vema na kujifunza mikakati yake na mbinu zake anazozitumia ili
asipate kustushinda kwa kukosa kuzijua fikra zake.
2Wakorintho 2:10-11
“Lakini
kama mkimsamehe mtu neno lo lote, nami nimemsamehe; kwa maana mimi nami, ikiwa
nimemsamehe mtu neno lo lote, nimemsamehe kwa ajili yenu mbele za Kristo,
Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.”
Kujifunza na kumfahamu
shetani, asili yake, kwanini yuko na hatima yake pamoja na utendaji wake wote
ni swala la muhimu sana kwa kila Mkristo, kwa sababu shetani licha ya kuwa adui
wa Mungu ni adui mkubwa wa wanadamu na adui hatari zaidi kwa watu waliookoka,
kwa hiyo utambuzi kuhusu shetani ni agenda Muhimu itakayotusaidia kumtambua
adui yetu na namna tunavyoweza kumshinda, kwa msingi huo basi tutajifunza somo
hili Muhimu Mafundisho kuhusu shetani kwa kuzingatia vipengele vinne
vifuatavyo:-
·
Asili ya Shetani.
·
Mafundisho kuhusu
shetani.
·
Uwezo na utendaji
wa shetani.
·
Hatima ya shetani.
Asili ya Shetani
Ni muhimu kufahamu kuwa
shetani kwa asili anajulikana kama malaika aliyeasi dhidi ya Mungu na kupoteza
heshima yake kutoka mbinguni, na kulaaniwa pamoja na malaika wengine waovu,
Imani kubwa tatu zilizoko duniani, ambazo asili yake ni Abraham zinamtambua shetani
kama mshitaki na adui mkubwa wa wanadamu aliyepoteza heshima yake kutoka
mbinguni, na kuwa yeye ni sababu kubwa ya mwanadamu wa kwanza kufukuzwa kutoka
katika uwepo wa Mungu yaani Bustani ya Edeni. Maandiko hayajawahi kutuambia
kuwa sio malaika, kwa hiyo anatambulika kuwa ni malaika na moja ya malaika wakubwa
sana ambao kimsingi, wako karibu na kiti cha enzi cha Mungu, kuondolewa kwake
katika mpango huo na kuhukumiwa kwake kumempa hasira kubwa sana na kumfanya awe
mpinzani wa mipango yote ya Mungu na uumbaji wa Mungu akiwepo Mwanadamu. Jina
lake aliitwa Lucifer yaani mwenye kuangaza au mfano wa nyota ya alfajiri, na
hili ndio jina lake. Kutokana na kuanguka kwake shetani Lucifer aliitwa Ibilisi
kwa sababu ya kiburi chake na majivuno na mwenendo wake wa moyoni wa kutaka
kujiinua kuliko Mungu.
1Timotheo 3:6-7 “Wala asiwe mtu
aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.Tena
imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na
mtego wa Ibilisi.”
Kwa msingi huo endapo
shetani ni ana asili ya malika ni wazi kuwa yeye ni kiumbe aliyeumbwa na Mungu
wakati fulani pamoja na malaika wengine kwa amri ya neno lake Mungu ona
Zaburi 148:2-5 “Msifuni, enyi
malaika wake wote; Msifuni, majeshi yake yote. Msifuni, jua na mwezi; Msifuni,
nyota zote zenye mwanga. Msifuni, enyi mbingu za mbingu, Nanyi maji mlioko juu
ya mbingu. Na vilisifu jina la Bwana, Kwa maana aliamuru, vikaumbwa.”
Kwa msingi huo tunapata
ufahamu ya kuwa malaika pamoja na Lucifer waliumbwa kwa amri ya Mungu, kwa
sababu hiyo malaika wote wema au malaika wateule na malaika wote waovu yaani
mashetani hawastahili kuabudiwa kwa kuwa wao ni viumbe tu, hawana tofauti na
sisi katika mtazamo wa kuwa Mungu
aliwaumba kwa kusudi na kuwa sehemu mojawapo ya utumishi wao ni pamoja na kujihusisha
na wanadamu na kuwahudumia hii ni kwa malaika wateule na wale walioasi, wako
karibu nasi kwa kusudi la kuharibu makusudi yote ya Mungu na mpango wa Mungu
kwa wanadamu wote. Tofauti na sisi viumbe hawa ni wa kiroho na hawafi, hawana
uwezo kuoa, kuolewa.
Luka 20:36 “Yesu
akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa;lakini, wale wahesabiwao kuwa
wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala
hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni
wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo.”
Wakati shetani na
mashetani wakiwa ni maadui wakubwa wa wanadamu, malaika wateule wao hufanya
kazi kwa karibu na wanadamu na kuwahudumia wale watakaourithi wokovu
Waebrania 1:13-14 “Je! Yuko
malaika aliyemwambia wakati wo wote, Uketi mkono wangu wa kuume Hata
nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako? Je! Hao wote si roho watumikao,
wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?”
Kama wote tunakubaliana
na msimamo wa kimaandiko ya kwamba shetani aliumbwa kama mojawapo ya malaika ni
Muhimu tukafahamu basi sifa kadhaa za malaika ambazo kimsingi hata shetani na
majeshi yake wanazo.
·
Malaika ni roho ambao kimsingi waliumbwa wawepo milele, kwa
sababu hiyo malaika hawafi, wataendelea kuwepo milele na milele, Maandiko
yanatufundisha hivyo kuwa hawakuweko toka milele ni viumbe waliumbwa na Mungu
wakati fulani lakini waliumbwa wawepo milele, kwa hiyo malaika wote wema au
wabaya wanaendelea kuwepo milele, na ndio maana wako watu wanajiuliza kwa nini
Mungu hamuui shetani? Jibu lake ni kuwa Mungu aliwakusudia malaika wawepo
milele kwa hiyo wanaendelea kuwepo siku zote mpaka pale Mungu atakapomuhukumu
shetani katika wakati ambao ameutenga yeye mwenyewe, kwa sababu Yesu
anatutaarifu ya kuwa uko moto wa milele ambao Mungu ameuandaa kwaajili ya
shetani na malaika zake.
Luka 20:36 “Yesu
akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa;lakini, wale wahesabiwao kuwa
wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala
hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni
wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo.”
Mathayo 25:41 “Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto,
Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari
Ibilisi na malaika zake;”
·
Malaika wana nguvu kimsingi malaika wana nguvu lakini hawana
nguvu zote, yaani wana uwezo Fulani, kama jinsi ambavyo wanadamu wana uwezo
Fulani na nguvu Fulani, lakini nguvu zao hazizidi za Mungu mwenye enzi na Nguvu
zote Katika 2Wathesalonike 1:7 tunataarifiwa kuwa Yesu Kristo atarudi
kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake neno uweza au malaika wa
uweza wake kwa kiingereza linasomeka with his MIGHTY angels, ambalo kwa
kiyunani ni DUNAMIS – ambalo maana yake ni ability, power, strength sawa
na neno Uweza, Nguvu na mamlaka kwa hiyo utaweza kuona ya kuwa viumbe hao wana
nguvu, ukilinganisha na wanadamu malaika ni askari ni majemadari ni wanajeshi
na wanatajwa kuwa na ukuu, uwezo na nguvu na wenye uwezo wa kupigana au kupiga
ni Hodari kwa kiingereza “Angels that excel in strength” wana weledi mkubwa kivita ni majenerali. Malaika
mmoja tu kwa mfano aliweza kupiga watu zaidi ya laki moja na themanini na tao
elfu 185,000 ambao walikuwa askari wa majeshi ya waashuru
2Wafalme 19:35 “Ikawa usiku uo huo malaika wa Bwana alitoka, akakiingia
kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia na themanini na tano elfu. Na watu
walipoondoka asubuhi na mapema, kumbe! Hao walikuwa maiti wote pia.”
2Wathesalonike 1:6-9 “Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale
wawatesao ninyi; na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; wakati wa
kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake
katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao
wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele,
kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake;”
2Petro 2:11 “Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana
matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti
mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana.”
Zaburi 103:20 “Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari,
mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake.”
Daniel 10:12-17 “Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku
ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu
wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini
mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo
Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko
pamoja na wafalme wa Uajemi. Sasa nimekuja kukufahamisha mambo yatakayowapata
watu wako katika siku za mwisho; maana maono hayo ni ya siku nyingi bado. Na
alipokwisha kusema nami maneno hayo, nikauelekeza uso wangu chini, nikawa bubu.
Na kumbe, mmoja mfano wa wanadamu akanigusa midomo yangu; ndipo nikafumbua
kinywa changu, nikanena, nikamwambia yeye aliyesimama karibu nami, Ee Bwana
wangu, kwa sababu ya maono haya huzuni zangu zimenipata tena; hata sikusaziwa
nguvu. Maana, mtumishi wa Bwana wangu huyu atawezaje kusema na Bwana wangu
huyu? Kwa maana kwangu mimi, mara hazikusalia nguvu ndani yangu, wala pumzi
haikusalia ndani yangu.”
·
Malaika wana akili
na hekima – 2Samuel 14:20b “…; na bwana wangu anayo akili, kama akili ya malaika wa Mungu,
hata ajue mambo yote ya duniani.”
Malaika wana akili na hekina na wanajua mambo
na mafumbo kadhaa kwa kina na kwa ukamilifu wake kwa hiyo tunapojifunza kuhusu
shetani ni lazima ukumbuke ya kuwa naye anazo sifa hizi, zote kama walivyo na
malaika wengine kwa hiyo kamwe usifikiri unaposhughulika na shetani
unashughulika na kitu tu cha kawaida hapana unashughulika na malaika mwenye
uwezo mkubwa, akili nguvu na maarifa na ni rahisi kwake kukudanganya na kukuingiza
mtegoni na kukupoteza na hata na hayuko hovyo katika utendaji wake, ana
mpangilio mzuri wa kiserikali kisera, kiuchumi, na kiutendaji, huyu ndiye
Lucifer ambaye leo tunachukua muda kujifunza habari zake.
·
Malaika wana
utaratibu wa kiserikali – Kule mbinguni Bwana pia huitwa Bwana wa Majeshi, na uko ufalme
mbinguni na iko serikali mbinguni na uko utaratibu mbinguni, katika mpangilio
kama huo mfano malaika Mikael ambaye hujulikana kama malaika mkuu yeye pia ni
mkuu wa anga la nchi ya Israel, maana yake anashughulika pia na ulinzi wa
wayahudi
Daniel 10:13 “Akaniambia, Ee Danieli, mtu upendwaye sana, yafahamu maneno
nikuambiayo, ukasimame kiwima-wima; maana kwako nimetumwa sasa. Na aliponiambia
neno hili, nalisimama nikitetemeka. Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa
maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele
za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako.
Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama,
huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha
huko pamoja na wafalme wa Uajemi.”
Daniel 10:20-21 “Ndipo akasema, Je! Unajua sababu hata nikakujia? Na sasa
nitarudi ili nipigane na mkuu wa Uajemi; nami nitakapotoka huku, tazama, mkuu
wa Uyunani atakuja.Lakini nitakuambia yaliyoandikwa katika maandiko ya kweli;
wala hapana anisaidiaye juu ya hao ila huyo Mikaeli, mkuu wenu.”
Waefeso 6:10-12 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa
nguvu zake.Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za
Shetani.Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya
falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya
katika ulimwengu wa roho.”
Maandiko yanatufahamisha kuwa mkao wa
kishetani hauko hovyo, kuna mpangilio wa maswala mbali mbali ya kiutawala yaani
Dola, neno falme, mamlaka, wakuu wa giza, na majeshi katika biblia ya kiyunani
yanatajwa kama archē, - Chief (Magistrate power principality, principle
rule) kuna utawala wa kimahakama, kuna jaji mkuu, waendesha mashitaka na
mahakimu, kisha exousia – wenye mamlaka, kisha Kosmokratōr – watawala
kwa kila nchi, mkoa, wilaya, taifa na mahali, Kratos – Dominion might Wakuu
wa Dola au Himaya (empires)Mabara, au tawala kubwa zaidi ya nchi,
Pneumatikos – viongozi wa kidini au kiimani, na epouranios – majeshi
ya pepo wengi wabaya ambao ni ponēria wenye kuendesha ukatili na uovu au
ubaya na kupanga utendekaji wa dhambi, kwa hiyo utendaji wa kimamlaka wa
kishetani uko katika taratibu za kiserikali na kimamlaka na unatenda kazi
katika mtiririko maalumu
Mafundisho kuhusu
shetani.
Ni muhimu kufahamu kuwa
Mafundisho kuhusu shetani na asili yake yanaonekana kuwa kama dhana flani hivi
hasa kwa sababu ya matumizi ya maandiko yanayoonyesha asili ya Shetani,
kuwataja wafalme halisi wa Babeli, na Tiro, jambo ambalo katika muktadha wa
kibiblia ni kweli kabisa kuwa maandiko hayo yanaonekana kuwataja wafalme
wanadamu wa Babeli na Tiro mfano
Isaya 14:12-15 “Jinsi
ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi
ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako,
Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu;
Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini.
Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu. Lakini
utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo.”
Ezekiel 28:13-19 “Ulikuwa ndani
ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako,
akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na
yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na
filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa
tayari. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka
hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe
ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata
uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza
udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu
katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe
kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu
ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa
chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama. Kwa wingi wa maovu yako,
katika uovu wa uchuuzi wako, umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza
moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya
nchi, machoni pa watu wote wakutazamao. Wote wakujuao kati ya kabila za watu
watakustaajabia; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele.”
Isaya 14:12-15 ni kifungu ambacho kimsingi kweli
kinamzungumzia Mfalme wa Babeli, lakini katika uhalisia kifungu hiki kinatumiwa
kwa kina katika lugha ya kinabii kwa undani kumuelezea shetani, kwa sababu ile
roho ya kutaka kuabudiwa baada ya kuinuliwa na Mungu, na kuumbwa vema na Mungu
na kufanikishwa na Mungu sasa roho hiyo haitaki tena kujinyenyekeza kwa Mungu
na badala yake inataka ibada ielekezwe kwake maana yake ile tamaa na shauku
aliyokuwa nayo mfalme kuwa atakiinua kiti chake juu kuliko Mungu na atakuwa
kama Mungu Nabii anaiona sio tu kuwa ni roho iliyokuwa imemuathiri mfalme
lakini ni ukweli kuwa mfalme alikuwa amepagawa na roho ambayo ni sawasawa na
ile ile iliyomuathiri shetani kutukuka kwake mfalme huyu kulimfanya awe
anajiona anang’aa kama nyota ya alfajiri (Lucifer) Je ni kweli kuwa katika
Babeli mfalme alifikia ngazi ya kutaka kuabudiwa kama Mungu? Jibu ni ndio Je
mfalme huyu aliyekuwa mtawala wa dunia nzima hakutumia kuinuliwa kwake
kuwapotosha watu wote wa dunia waache kumuabudu Mungu aliye hai na badala yake
waabudu miungu yake na sanamu yake aliyoisimamisha? Jibu ni ndio na ni kitu
gani shetani huwa anakifanya hapa duniani?
je filimbi na ngoma na zumari na machezo zilikuwa zinaelekezwa wapi? Kwa
Mungu aliye hai au kwa mungu wa Nebukadreza na sanamu yake?
Daniel 3:1-14 “Nebukadreza,
mfalme, alifanya sanamu ya dhahabu, ambayo urefu wake ulikuwa ni dhiraa sitini,
na upana wake dhiraa sita; akaisimamisha katika uwanda wa Dura, katika wilaya ya
Babeli. Ndipo Nebukadreza akatuma watu kuwakusanya maamiri, na manaibu, na
maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa
wilaya zote, ili wahudhurie wakati wa kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadneza
aliyoisimamisha. Ndipo maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza
hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, wakakusanyika ili
kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha; wakasimama mbele ya
ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha. Ndipo mpiga mbiu akapiga kelele
akisema, Enyi watu wa kabila zote, na taifa, na lugha, mmeamriwa hivi, wakati
mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na
zomari, na namna zote za ngoma, lazima kuanguka na kuiabudu sanamu ya dhahabu,
mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha. Na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa
saa iyo hiyo katika tanuru ya moto uwakao. Basi wakati huo, watu wa kabila zote
walipoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari,
na namna zote za ngoma, watu wote na mataifa na lugha wakaanguka, wakaiabudu
ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha. Basi baadhi ya Wakaldayo
wakakaribia, wakaleta mashitaka juu ya Wayahudi. Wakajibu, wakamwambia mfalme
Nebukadreza, Ee mfalme, uishi milele. Wewe, Ee mfalme, ulitoa amri ya kwamba
kila mtu atakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na
santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, ni lazima aanguke na kuiabudu ile
sanamu ya dhahabu; na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa katika tanuru ya
moto uwakao. Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya
Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme,
hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu
uliyoisimamisha. Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe
hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya
mfalme. Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na
Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia
sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? ”
Ezekiel
28:13-19 kifungu hiki hali kadhalika kinaelekezwa na
nabii moja kwa moja kwa mfalme wa Tiro katika frikra nyembamba, Lakini katika
fikra pana anazungumziwa Kerubi malaika wa ngazi ya juu sana aliyeumbwa kwa
uhodari na ubora akiwa na hekima kubwa na uzuri lakini aliharibiwa kwa kiburi
ambacho kimsingi ndicho kilichopelekea anguko lake ufafanuzi huu pia kama
ulivyo ule wa Nyota ya Alfajiri katika Isaya na huuwa Kerubi mwenye kutiwa
mafuta moja kwa moja katika fikra pana unamzungumzia shetani ambaye ndiye
kimsingi aliwapagaa wafalme hawa kutaka kuabudiwa kama Mungu, kwa hiyo katika
mtazamo mwembaba wanazungumzwa wafalme wa Tiro, na Babeli, Lakini katika
mtazamo mpana anazungumzwa shetani na utendaji wake ambao uliwaathiri wanadamu
hawa wafalme
Ezekiel 28:2 “Mwanadamu,
mwambie mkuu wa Tiro, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe
umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari;
lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa
Mungu.”
Wakati ni kweli vifungu
hivyo vinawazungumzia wafalme wanadamu waliotawala Babeli na Tiro, Lakini ni
ukweli ulio wazi kuwa dhambi zao na kuzama kwao katika haribiko la kiroho
uliruhusu wao kwenda ndani zaidi na manabii wanawaona katika ulimwengu wa roho
wakifanya dhambi sawa tu na ile aliyoifanya shetani, waliangukia katika mtego
wa ibilisi, walijawa na kiburi, sawa tu na kile alichokuwa nacho shetani,
walijiona ni nyota ya alifajiri na walijiona ni makerubi, kwa hiyo kwa jicho la
kinabii Mungu anawaona wafalme hao kuwa wamefikia kiwango cha juu cha dhambi
sawa na ile aliyoifanya shetani na ndio maana kwa miaka mingi vifungu hivi
vimekuwa vikitafasiriwa na wanatheolojia wa kiyahudi na Kikrsto ya kuwa
vinamzungumzia shetani hasa kwa sababu manabii waliweza kuona mambo yaliyopo,
yaliyopita na yajayo, kwa hiyo wakati manabii wakitangulia kuwaonya wafalme hao
wanazungumza pia katika wakati uliopita wakitafakari au kuunganisha maonyo yao
na kile alichokuwa amekifanya na kikampata Lucifer mwenyewe kwa hiyo vifungu
hivi ndio vinavyokubalika kutupa historia iliyojificha kuhusu anguko la Shetani
na sababu zake.
Mungu hatakuja kuvumilia
hata siku moja mtawala mwanadamu, kujitukuza na kujiinua kama Mungu au kutaka
kuwaongoza watu na kuwapotosha wamuache Mungu aliye hao hayo kimsingi yanaweza
kufanywa na Shetani na mara kadhaa amezitumia serikali au wafalme wakubwa na
wenye nguvu duniani kuwalazimisha watu kufanya maovu, na hii ndio kazi ya
shetani, endapo mfalme mwanadamu atafanya kama hayo atashushwa hata kuzimu mara
moja
Ufunuo 13:13-15 “Naye afanya
ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele
ya wanadamu.Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa
kuzifanya mbele ya huyo mnyama, akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu
yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi.Akapewa kutia pumzi
katika ile sanamu ya mnyama, hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya hao
wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe.”
Matendo 12:21-24 “Basi siku moja
iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi,
akatoa hotuba mbele yao. Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si
sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu
utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho. Neno la Bwana likazidi na kuenea.”
Ushawishi huu wa wafalme
na watawala na wenye mamlaka na wanadamu kuwa na dhana ya kujifikiri kuwa wao
ni Mungu, kwa asili inatoka kwa shetani, kwa hiyo maonyo kwa wafalme wa Babeli
na Tiro wanayoonywa kuwa yatawapata manabii walitumia kuwa hukumu ile
itakayowapata itakuwa sawa tu na ile iliyompata aliyewashawishi wanadamu kutaka
kuwa kama Mungu tangu mwanzo ambaye kimsingi ni shetani, wapi wanadamu wanatoa
au kupokea ushawishi huu wa kutamani kuwa kama Mungu? Ni kwa mwanzilishi wa
uovu huo ambaye ni shetani!
Mwanzo 3:1-5 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa
mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema
Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda
ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya
bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia
mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula
matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema
na mabaya.”
Kwa hiyo unaweza kumuona
shetani katika picha ya kiburi na ubora kuwapitia viongozi wa dunia wasio mcha
Mungu na namna na jinsi wanavyojiinua kinyume na Mungu, tumekwisha kujifunza
sifa za malaika ambazo kimsingi shetani pia anazo, lakini ni vema pia tukaangalia
na kumchambua shetani ni nani na alivyo na hali yake kibinafsi namna ilivyo ni
kiumbe wa namna gani hasa?
1.
Jina lake: Katika maandiko jina analopewa mtu au kiumbe
huwa linafunua na kuelezea uhalisia wa jinsi na namna mtu huyo alivyo, hii ni
hali ya kawaida ukitaka kumjua Mungu, Bwana Yesu na Roho Mtakatifu utaweza
kujua kupitia majina anayopewa katika maandiko, hali kadhalika tunapojifunza
somo kuhusu Lucifer au shetani leo tutapitia pia majina yake ili tuweze kupata
picha na kujihoji ni kwanini shetani ameitwa namna hiyo:
a.
Shetani - Jina shetani kwa kiibrania ώâtân kiingereza
Adversary – “the arch enemy of good” katika Kiswahili ni shetani yaani adui
wa mema neno hili limetumika mara 19 katika Biblia ya kiingereza ya KJV kazi
yake ni kuharibu kila mpango mwema ambao Mungu ameukusudia katika jamii ya
wanadamu, ukiacha ya kuwa aliwaharibu wanadamu, lakini pia alikuwa anataka
kuharibu mpango wa Mungu wa ukombozi kupitia mwanamke kwa kutaka kuua uzao wa
mwanamke ili kumuua masihi na kuacha hai wa kwake
Mwanzo 3:14-15. “BWANA Mungu
akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama
wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi
utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo
mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe
utamponda kisigino.”
1Yohana 3:11-12 “Maana, hii
ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi; si kama
Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Naye alimwua kwa sababu
gani? Kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya, na ya ndugu yake yalikuwa ya
haki.”
Shetani ni mpinzani na adui wa kila mpango mwema wa Mungu uliokusudiwa
katika maandiko, anapambana katika ulimwengu wa roho akiratibu kila kitu
kinachoonekana katika ulimwengu wa mwili, alikusudia kuwaharibu wanadamu wote
wakaao juu ya uso wa nchi, alikusudia kuwaharibu, wana wa Israel kwa
kuwatumikisha huko Misri kupitia Farao, alikusudia kumuangamiza Yakobo kupitia
Esau, hata leo anachukizwa na uwepo wa taifa la Israel na anatumia mataifa
adui, kutamani au kutaka kuifuta Israel ili kuharibu Historia ya Mungu na
mpango wake wa baadaye wa utawala wa Masihi, na anachukizwa na kanisa na
anatumia kila mbinu kutaka kuliangamiza, na kama yule aliyezaliwa kwa mwili
alivyomuudhi yule aliyezaliwa kwa roho ndivyo ilivyo hata sasa.
Wagalatia 4:29 “Lakini kama
vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa
Roho, ndivyo ilivyo na sasa.”
Shetani amekuwa akishambulia kila kilicho cha Mungu na kutaka kukiangamiza
kabisa, analishambulia kanisa kupitia njia ya mateso na njia ya mafundisho ya
uongo, ana watu wake kama jinsi ambavyo Mungu ana watu wake, wako wanaofanya
kazi upande wake akiwatumia kama Mungu anavyotumia watu wake wanaofanya kazi
upande wake, kwa bahati mbaya watu wengi hawajui kuwa shetani ana watu wake
duniani, wanafikiri kuwa kila mtu ni mwema na hawachukui tahadhari kwa sababu
hawajui!
1Timotheo 4:1 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho
wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya
mashetani;”
Mathayo 13:38-39 “lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa
ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni
Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika.”
Ufunuo 2:10 “Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi
atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi.
Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.”
b.
Ibilisi – Shetani anaitwa ibilisi au yule joka la zamani,
jina ibilisi kwa kiingereza Devil kwa
Kiyunani “diabolos” ambalo
kiingereza tafasiri yake ni false accuser, au slanderer kwa Kiswahili ni
Mshitaki kwa hiyo jina ibilisi linatumika sana akiwa anafanya kazi ya
kuwashitaji wateule wa Mungu, kila mtu wa Mungu shetani humtafuta kwa udi na
uvumba apate jambo la kumshitaki, Shetani humshitaki Mungu kwetu na kutushitaki
sisi kwa Mungu, kama u mwema atafanya kila aliwezalo kuhakisha kuwa anakuchafua
anawaaminisha watu kuwa wewe hufai, atakushambulia kutoka ndani na nje kuhakikisha
kuwa unaonekana hufai hasa kama una kitu cha Mungu ndani yako, shetani
atakushitaki au atasimama kama mwendesha mashitaka kuhakikisha hukubaliki kwa
Mungu na kwa wanadamu, ili kupingana na kitu cha kiungu kilichomo ndani yako
au kumshawishi Mungu aachane na mpango wake juu yako.
Mwanzo 3:2-5
“Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula;
lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala
msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana
Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho,
nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
Ufunuo 12:9-10 “Yule joka
akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye
ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.
Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na
ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini
mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.”
Ayubu 1:8-11 “Kisha Bwana
akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana
mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu
na kuepukana na uovu.Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu
yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba
yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali
yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote
aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.”
Zekaria 3:1-2 “Kisha
akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na
Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye.Bwana akamwambia
Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na
akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni? ”
1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na
kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye,
huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”
c.
Mharabu au
mharibifu – Shetani anaitwa Mharabu, kwa kiyunani ni “Apollyon” apolioni na
kwa kiebrania ni “Abaddon” abadoni hii inadhihirisha hasira kubwa sana
aliyonayo na chuki dhidi ya Muumba na kazi yake, na mipango yote ya Mungu yeye
anabainishwa kama muharibifu naye amejiweka kwa kazi hiyo
Ufunuo 9:9-11 “Nao walikuwa na
dirii kifuani kama dirii za chuma. Na sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya
magari, ya farasi wengi waendao kasi vitani. Nao wana mikia kama ya nge, na
miiba; na nguvu yao ya kuwadhuru wanadamu miezi mitano ilikuwa katika mikia
yao. Na juu yao wanaye mfalme, naye ni malaika wa kuzimu, jina lake kwa
Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani analo jina lake Apolioni.”
Yohana 10:10-11 “Mwivi haji ila
aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao
tele. Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya
kondoo.”
d.
Nyoka au
Joka – Shetani anaitwa nyoka hivyo katika maandiko kama nembo ya kumbukumbu ya yale
aliyoyafanya zamani yaani kwa wivu wake na uharibifu wake kuleta anguko kwa
mwanadamu kwa kujibadilisha au kujivika umbo la nyoka, lakini pia kama neno ya
werevu na hila au ujanja wake alionao
Ufunuo 12:9-10 “Yule joka
akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani,
audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa
pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na
nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa
chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na
usiku.”
Mwanzo 3:1-5 “Basi nyoka
alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu.
Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti
yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini
twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema,
Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika
hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti
huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
e.
Mjaribu – Shetani anaitwa mjaribu, kwa sababu ndiye chanzo cha majaribu yote
yenye ushawishi wa kuwafanya watu watende maovu kwa Mungu kwa mtindo wa
kuwaonea, ni kazi yake kuwajaribu watu na kuwatia katika udhaifu na
kuwashawishi wamkosee Mungu, majaribio anayoyatoa shetani ni kuhakikisha
anakuoenea ili kuangalia uwe mwaminifu au usiwe mwaminifu kwa Mungu, hakuna
mwanadamu wa ngazi yoyote ile ambaye shatani ataacha kumjaribu, shetani
anatumia ushawishi, mvuto, uchochezi, na wakati wote anakudanganya kuwa unaweza
kufanya dhambi bila kupata madhara ilihali dhambi ina madhara makubwa sana
katika maisha ya mwanadamu, Mjaribu kwa kiingereza Tempter kwa kiyunani
“Peirazō” sawa na neno “scrutinizer” – a person who examines
something with great care or investigator who observes carefully hii maana
yake ni nini shetani ni mjaribu ambaye anatumia akili sana ni mwangalifu
katika jambo analolifanya ni mjanja mno kama mwindaji anavyotega mtego wa
kukamata ndege au paa kwa hiyo unahitaji kuwa na hekima sana kujichomoa kutoka
katika mitego ya adui,
Mathayo 4:1-3 “Kisha Yesu
alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi. Akafunga siku arobaini
mchana na usiku, mwisho akaona njaa. Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe
Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.”
Mithali 6:4-5 “Usiache macho
yako kupata usingizi, Wala kope za macho yako kusinzia.Ujiponye kama paa na
mkono wa mwindaji, Na kama ndege katika mkono wa mtega mitego.”
f.
Mdanganyifu
– Ni muhimu pia kufahamu kuwa shetani anaitwa mdanganyifu kwa sababu kadhaa
ikiwa ni pamoja na maneno na matendo na mafundisho yake kama inavyofundishwa katika maandiko, uongo
ndio moja ya silaha yake kubwa sana anayoitumia akitumia akili, hila na ujanja
mkubwa sana katika kuhakikisha anafanikisha kazi yake hiyo.
§ Alimdanganya Hawa – Mwanzo 3:1-5 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa
mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema
Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka,
Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati
ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia
mwanamke, Hakika hamtakufa,kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula
matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema
na mabaya.”
§ Hupotosha ukweli - Shetani ni mtaalamu wa kupotosha ukweli na
kuufanya uonekane uongo na uwongo uonekane kama kweli, shetani ana mafundisho
yake ambayo huyatumia kuliharibu kanisa kwa kutumia mafundisho ya uongo na roho
zidanganyazo
1Timotheo 4:1-5 “Basi Roho anena
waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza
roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao
uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na
kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani
na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni
kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; kwa kuwa
kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.”
§ Hujaribu kuficha ukweli kuhusu Mungu – Shetani siku zote atajaribu kuuficha upendo na
rehema na fadhili za Mungu kwa wanadamu, siku zote atawafanya wanadamu waamini
ya kuwa Mungu ni mkali, mwenye kuhukumu na hajali kuhusu maisha ya wanadamu,
ndio maana watu wengi nyakati za agano la kale kila walipopatwa na mabaya
walidhani Mungu ndiye anayesababisha hayo, hii ni kwa sababu shetani hujaribu
kumshitaki Mungu kwetu ili yamkini sisi nasi tuweze kujenga chuki kwa Mungu na
kumuona Mungu kama asiyetenda haki asiyejali na katili kwa watu wake aliowaumba
yeye mwenyewe.
Ruthu 1:19-21 “Hivyo hao
wakaendelea wote wawili hata walipofika Bethlehemu. Na ikawa walipofika
Bethlehemu, mji wote ulitaharuki kwa habari zao. Nao wanawake wakasema, Je!
Huyu ni Naomi?Akawaambia, Msiniite Naomi niiteni Mara,kwa sababu Mwenyezi Mungu
amenitenda mambo machungu sana,Mimi nalitoka hali nimejaa, naye Bwana
amenirudisha sina kitu, kwani kuniita Naomi, ikiwa Bwana ameshuhudia juu yangu,
na Mwenyezi Mungu amenitesa? ”
Mwanzo 16:1-2 “Basi Sarai
mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake
Hajiri.Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae,
umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza
sauti ya Sarai.”
1Samuel 1:1-6 “Palikuwa na mtu
mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa
Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu,
Mwefraimu naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina
lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa
na watoto. Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili
kuabudu, na kumtolea Bwana wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili
wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa Bwana, walikuwako huko.Hata siku ile
ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto
wake wote, waume kwa wake, sehemu zao; lakini Hana humpa sehemu mara mbili;
maana alimpenda Hana, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo. Ila mwenzake
humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo.”
Ayubu 1:16 “Huyo alipokuwa
akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka
mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke
yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.”
§ Hujaribu kututenganisha na Mungu – Lengo lingine la shetani ni kuhakikisha anatumia kila aina ya mbinu
anayoweza kututenganisha na Mungu, anatumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na
mashaka, hofu, kukata tamaa, dhambi, na tamaa ili kufanikisha tuwe mbali na
Mungu, Shetani anajua wazi kuwa usalama wetu uko kwa Mungu na kuwa akifanikiwa
kututenga na uwepo wa Mungu anaweza kusababisha madhara makubwa kwa wanadamu.
1Nyakati 21:1-3 “Tena shetani
akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Israeli.Basi Daudi
akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni kawahesabu Israeli toka Beer-sheba
mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao. Naye Yoabu akasema,
Bwana na awaongeze watu wake mara mia hesabu yao ilivyo; lakini, bwana wangu
mfalme, si wote watumishi wa bwana wangu? Mbona basi bwana wangu analitaka neno
hili? Mbona awe sababu ya hatia kwa Israeli?”
§ Hujaribu kuwafanya watu waamini uongo – anatoa matumaini hewa na kupotosha ukweli
kuhusu Maisha, furaha na mafanikio, anatufanya tuamini ya kuwa tunaweza kuwa na
furaha katika vitu vya dunia badala ya uhusiano na Mungu.
2Wakorintho
11:14-15 “Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa
nuru.Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi
wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.”
2Wakorintho 11:3-4
“Lakini
nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu
fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo. Maana yeye ajaye akihubiri
Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea,
au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye!”
g.
Mkuu wa
ulimwengu huu, Mungu wa dunia hii – Shetani anaitwa hivgio Mungu wa dunia hii katika maana ya kuwa kwa sasa
ni mtawala wa dunia hii, lakini Mungu ambaye ni mtawala wa yote amemuwekea
mipaka, hakuna anachoweza kukifanya bila Mungu kuruhusu au kunyamaza kimya, ni
kama tu vile alipozungumza na Mungu kuhusu Ayubu kuna mipaka Mungu alimuwekea
shetani.
2Wakorintho 4:3-4 “Lakini ikiwa
injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu
wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya
utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”
Yohana 12:31 “Sasa hukumu ya
ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.”
Waefeso 2:1-2 “Nanyi mlikuwa
wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata
kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule
atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;”
1Yohana 5:19 “Twajua ya kuwa
sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu.”
Tangu baada ya anguko la mwanadamu ambaye ndiye aliyepewa na Mungu
kuutawala ulimwengu huu na vyote viujazavyo, Shetani aliweza kuwa na nguvu ya
kimamlaka ya kutawala ulimwengu na kuingiza mawazo, elimu, falsafa, na
utaratibu mzima wa kuhakikisha kuwa anaitawala dunia kwa kutumia uwongo bila
wanadamu kuelewa akitumia hila na ujanja wa hali ya juu kuhakikisha kuwa
wanadamu hawaijui njia ya Mungu kwa usahihi, kwa hiyo usidhani wala kufikiri
kuwa kila kitu duniani hata kinachoonekana kuwa kina ukweli ni kweli, shetani
anatumia malengo na mitazamo na wakati mwingine mitazamo ya wengi, biashara na
kuweka mifumo ambayo kamwe haitaruhusu watu kujali kitu kuhusu Mungu.
Shetani sio mtawala wa ulimwengu mzima kwa ukamilifu wake, Mungu ndiye
anayetawala lakini yeye kama mkuu wa anga ameachiliwa na Mungu kufanya kazi
chini ya mipaka Fulani, wakati ikisubiriwa siku ya hukumu yake kamili kwa hiyo
ana mamlaka katika ulimwengu lakini chini ya udhibiti wa Mungu.
Ayubu 1:7-12 “Bwana
akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema,
Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.
Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa
kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye
kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je!
Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na
nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo
mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo
yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako. Bwana akamwambia Shetani,
Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu
yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana.”
Aidha ni muhimu kufahamu kuwa shetani ana utaratibu, wa kiserikali wenye
kila kitu na mengi akiwa ameyaigiza kutoka mbinguni kwa Mungu, isipokuwa tu
anauweka utaratibu wake utende kazi kijanja sana kwa kusudi la kuwanasa na
kuwashika wanadamu ili yamkini waweze kupotea na kwenda naye wakati wa hukumu
katika lile ziwa liwakalo moto aliloandaliwa yeye.
Uwezo na utendaji
wa shetani
Baada ya kuwa tumejifunza
mafundisho kuhusu shetani sasa ni muhimu kwetu kuangalia uwezo na utendaji wa
shetani yaani sifa zake na utendaji wake, tunaweza kumuelewa vizuri zaidi kwa
kuangalia uwezo wa utendaji wake, lengo kubwa sio kumtukuza lakini lengo kubwa
ni kuelewa kuwa Msaada wetu ni katika bwana na Mungu ndiye anayetusaidia
tunapokuwa tunamshinda adui shetani ni lazima tuelewe kuwa ni kwa msaada wa
Roho Mtakatifu.
1.
Shetani ana akili –
Watu wengi sana wanafikiri kuwa shetani ni
kiumbe kisicho na akili na kinachokurupuka tu lakini maandiko yanamuelezea
shetani kuwa ana akili “He has intelligence” intelligence maana yake kwa
kiingereza the ability to acquire and apply knowledge and skills yaani
ni ana uwezo wa kuelewa na kutumia akili zake au maarifa yake kwa usahihi na
ustadi mkubwa
2Wakorintho 2:11 “Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi
kuzijua fikira zake.”
Maandiko yanamuonyesha shetani kuwa ana FIKRA
neno fikra katika lugha ya kiyunani linatumika neno noēma ambalo maana
yake ni the intellect disposition yaani ni mwenye weledi katika
kutumia akili, elimu na mbinu nyingine kwa uangalifu mkubwa na kwa bidii, pia
ana mbinu, Stategic plans (Mpango mkakati) kwa msingi huo kama ni mikakati vita
shetani angependa sana kutumia vita laini sana ya kukuzidi fikra na kukunasa
hata bila wewe kujielewa, kwa hiyo ili kumshinda shetani watu wa Mungu hawana
budi kujiandaa na kujipanga kwa sababu sasa unajua ni aina gani ya adui ambaye
unakwenda kukabiliana naye, wakati wote tunapaswa kujifunza kuwa hodari kwa
sababu tunayekwenda kupambana naye ni Hodari na mjuzi wa vita
Waefeso 6:10-11. “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa
nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.”
Matumizi ya akili kubwa ni moja ya silaha yake
kubwa sana anayoitumia bila kujali wewe ni wa rohoni kwa kiwango gani, anauwezo
wa kuisoma akili yako na kukuharibu na kukuharibia hata kabla hujafikiri, vita
zake nyingi sana hutumia akili na uongo au hila na kwa hila anaweza
kukusababishia madhara Shetani anatajwa tangu mwanzo kuwa alikuwa mwerevu,
kuliko hayawani wote walioumbwa na Mungu
Mwanzo 3:1 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu
aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema
Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?”
Neno hilo mwerevu katika lugha ya kiibrania ni
ârûm ambalo kwa kiingereza ni cunning, au subtil, au prudent
au crafty yaani ni mjanja, mwerevu, mwenye kutumia busara, na msanii mkubwa,
kama umewahi kuwachunguza wachawi, waganga, wanamazingaombwe na matapeli,
majambazi, makahaba, na kama umewahi kutapeliwa utaelewa akili kubwa walizonazo
au wanazozitumia waganga utaweza kuona kuna ujanja mwingi, lugha nzuri, na akili
kubwa sana wanayoitumia kuiongoza akili yako mpaka wakutapeli au uweze kuamini,
kwa hiyo utapeli ni moja ya kazi kubwa na mbinu kubwa sana anayoitumia shetani
ndio maana anaitwa muongo na baba wa uongo yaani mwanzilishi wa uongo wote.
Ufunuo12:9 “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye
Ibilisi na Shetani,audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika
zake wakatupwa pamoja naye.”
Shetani anaweza kujua atamalizana nawe vipi
hata baada ya miaka kumi ijayo, anaweza kushughulika na wewe katika mtindo
ambao hautakuja ugundue kuwa uko vitani, na mbinu hizi hizi wanazo watumishi
wake wote anaowapagaa kutekeleza mpango wake huu, kumshinda shetani lazima uwe
na akili sana ujue fikra zake. Na akili hizo na maarifa hayo utayapata kwa
kusoma neno la Mungu na kuelewa kwa msaada wa Roho Mtakatifu, Shetani haogopi
dini yako, haogopi unashika vipi maandiko, haogopi wewe uko katika ngazi ya
ukuhani mkuu, haogopi umaalumu wako na hatakuja kwako katika njia utakayogundua
kuwa amekuja. Atajaribu kwa kiwango kikubwa kuharibu, kubomoa, kuchelewesha,
kuzuia, na kusimamisha huduma yako na ukristo wako kama unataka kukataa jiulize
wale mafarisayo washika dini waligeukaje kuwa wana wa Ibilisi? Ilihali walikuwa
washika dini? Jiulize hawa wana wa Ibrahimu, hawa washika maandiko, hawa
washika dini, ni lini na ilikuwaje wakawa wana wa ibilisi? Na je hawakumuua
Yesu? Je hawakupingana na kweli ya Mungu? Je hawakumsingizia Yesu uongo mbele
ya Pilato? Je hawakumuwekea vikao vya majungu na kutafuta namna watakavyomuangamiza?
au wadhani Yesu alikuwa anasema uongo kuwa wao wamekuwa wa ibilisi? Na
wanatekeleza mapenzi ya baba yao ibilisi? Shetani anatumia akili ona
Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo
mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika
kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake
mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo”
2.
Shetani analijua neno – Wakati anamkabili Yesu Kristo alipokuwa katika
mlima wa majaribu, tena akiwa amefunga siku 40 usiku na mchana yaani Yesu akiwa
kiroho kweli kweli akiwa amejaa Roho Mtakatifu na unajua Yesu alikuwa amejaa
neno la Mungu pia na alikua anajua kulitumia kwa usahihi, Shetani alicheza na
maandiko pia alipokuwa akimjaribu bwana Yesu
Mathayo 4:5-7 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu
ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana
imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije
ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu
Bwana Mungu wako.”
Unaona wakati akimjaribu Yesu Shetani alinukuu
andiko kama lilivyo, je unadhani alikuwa na biblia mkononi? Je unadhani alikuwa
na simu, au tablet au computer bila shaka alinukuu kutoka kichwani, hii maana
yake ni nini Shetani amejaa neno la Mungu, sijui wewe umejaa neno kwa kiasi
gani lakini elewa ya kuwa shetani analijua neno na ameweka katika kichwa tu we
hauogopi? Huoni kuwa ni jambo la kutisha kama huna bidii katika kujifunza neno
la Mungu, yeye amelishika na ni kwa sababu gani? Ni ili aweze kulitumia wakati
wowote na mda wowote autakao, anayajua maeneo yote ya udhaifu wako, anayajua
maeneo yote yenye udhaifu katika ndoa yako, anayajua maeneo yote ya dhambi zako
anakumbuka kila kitu kiovu ambacho umewahi kukifanya na anauwezo wa kumkumbusha
Mungu yale uliyoyafanya wakati wa kukushitaki, anajua wakati gani una nguvu na
wakati gani umechoka, alimjia Yesu wakati anasikia njaa, kwa hiyo anakujua ni
wakati gani utampinga na ni wakati gani utamlegezea na atapata ushindi, katika
kumjaribu Yesu sio kuwa aliishia pale maandiko yanasema alimuacha kwa muda, hii
maana yake alimjia tena na tena mara nyingine, shetani atakucheki mara kwa mara
taratibu tu wala hana haraka na wewe.
Luka 4:13 “Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.”
3.
Shetani ana maarifa
- ni muhimu kuelewa ya kuwa shetani anajua na ana maarifa ni mwelewa neno
maarifa katika kiebrania linatumika neno “yādha” na “da’ath” ambalo katika
kiyunani ni “oīda” na “ginōskō” yaani
“knows” and “to know fully” kwa hiyo
shetani sio kuwa ana maoni au mawazo anajua na anauelewa mpana sana ana
maarifa, anajenga hoja, ana uwezo wa kufikiri, anachunguza na kuelewa kwa hiyo
anamjua kila mtu duniani, anajua Baraka zako, anajua nguvu yako na anajua apige
wapi ili akuharibu kiimani, ana namna ya maarifa anajua afanye nini kwako na
asirudie tena na awe amekupata!
Ufunuo 12:12 “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa
nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi,
akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”
Ayubu 1:8-11 “Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo
mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu
mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.Ndipo Shetani
akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira
kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi
za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini
nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za
uso wako.”
Ayubu 2:3-6 “Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi
wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na
mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa
anashikamana na utimilifu wake, ujapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize
pasipokuwa na sababu. Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam,
yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake. Lakini sasa nyosha mkono
wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako.Bwana
akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake”
Unaweza kuona shetani alikuwa anamjua Ayubu,
alikuwa amemsoma na kujua kila kitu alichokuwa nacho, anajua aguse wapi na
kutokee nini unaona, anajua wewe ukinyimwa tendo la ndoa, nini kitatokea,
anajua wewe ukiwa na cheo nini kitatokea, anajua wewe ukiwa masikini nini
kitatokea, anajua wewe ukiwa mgonjwa utaenda kwa mganga, anajua wewe ukitegeshewa
hela utaiba, anajua wewe mumeo akiwa dhaifu utazini, anajua mumeo akiwa mzinzi utakimbia
ndoa, anajua hasira yako, anajua wivu wako, anajua tamaa yako na anajua
taratibu namna na jinsi anavyoweza kukuleta katika dhambi, anajua namna na
jinsi anavyoweza kukufanya dhaifu kwa nini kwa sababu anajua na ana maarifa ya
wewe ni nani, na afanye nini aguse kipi ili kuyababaisha maisha yako, kwa hiyo
haogopi maombi yako, wala ujuzi wako kuhusu neno na anajua namna ya kukunasa
katika dhambi na wala humpi shida anaweza kukupa hata kiburi tu ukajiona wewe
ndio wewe kama mafarisayo kumbe wameshakuwa watoto wa ibilisi siku nyingi bila
kufanya dhambi.
4.
Shetani ana mapenzi
yake - kama jinsi ambavyo Mungu ana mapenzi yake na
wakati mwingine tunaomba kuwa mapenzi yake yatimizwe hapa duniani kama huko
mbinguni, ni muhimu kufahamu kuwa shetani naye ana mapenzi yake na huenda
akataka yatimizwe hapa Duniani, na yatimizwe wakati mwingine hata na watu wa
Mungu aliowanasa katika mtego wake.
2Timotheo 2:24-26 “Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa
mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; akiwaonya kwa upole wao
washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;
wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa
naye, hata kuyafanya mapenzi yake.”
Isaya 14:12-14 “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri,
mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe
ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu
kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za
mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye
juu.”
Kwa hiyo unaweza kuona na kugundua mapenzi ya
ibilisi, kuinua kiti chake kuliko cha Mungu, kuketi juu ya mlima wa mkutano,
kupaa juu kuliko Mungu na kufanana na aliyejuu, kwa hiyo yuko tayari kuharibu
lolote linalompa Mungu utukufu, yuko tayari, kuharibu mpango wa Mungu juu yako
na yangu, chochote ambacho Mungu amekijenga ndani yetu mpango wake ni
kukuharibu na kufutilia mbali programu zote za kiungu zilizoko ndani yako na
kuweka zake, na hali kadhalika mpango wowote wa ibada ya kweli unaomwelekea
Mungu.
5.
Shetani hana sura
mbaya - Ni muhimu kuwa na ufahamu katika hali ya
kawaida tu hakuna mahali tunaelezwa ya kuwa shetani ni mweye sura mbaya, au ana
mapembe kama tunavyoweza kuona katika michoro mbalimbali, ni kweli alikataliwa
na ni kweli alifukuzwa katika uwepo wa Mungu na matendo yake ni mabaya lakini
hata hivyo hii haimaanishi kuwa ana sura mbaya liko swali liliwahi kuulizwa ni
kwanini watu humuonyesha shetani au kumchora shetani akiwa na sura mbaya sana
na likajibiwa hivi kwa lugha ya kiingereza “Because it’s human nature to
venerate beauty, and denigrate ugliness. If we were to portray the Devil as
beautiful, then people might feel more inclined to venerate the Devil. Sadly,
in endorsing the denigration of ugliness the church has led us astray away from
the calling of Christ.” Tafasiri isiyo rasmi tafasiri yangu “kwa sababu ni
asili ya mwanadamu kuheshimu uzuri na kudhalilisha ubaya. Ikiwa tungemuonyesha
ibilisi kuwa mrembo basi huenda watu kuwa na muelekeo wa kumuabudu ibilisi na
kumkubali, lakini cha kusikitisha ni kwamba
katika kuunga mkono na kudharaulika kwa ubaya kanisa limepotiosha ukweli
kuhusu shetani mbali na wito wa Kristo” kwa majibu haya tunakubaliana ya kuwa
ubaya wa sura ya shetani umetiwa chumvi jambo ambalo kikristo haliko sahihi.
6. Shetani ana matakwa – Shetani ana matakwa kwaajili yetu anatamani kututumia, anatamani
kutushinda, ana tamani kutuharibu, anatamani kutudanganya, anatamani kutuua,
anatamani kutukomesha, anatamani kututoa nje ya mstari wa Mungu, anaweza
kutuzuia tusimtumikie Mungu katika njia inayoonekana kuwa inakubalika, tamu, au
njia sahihi, njia ya kistaarabu sana na ya kawaida au yenye sababu zinazokubalika,
anaweza kuzuia na anaweza kuchelewesha, anaweza kupinga na anaweza kushambulia
kwa matakwa yake
Luka 22:31 “Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi
apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako
isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.”
1Petro 5:8-9 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi,
kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni
huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa
kwa ndugu zenu walioko duniani.”
Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo
mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika
kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake
mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo”
7. Shetani ana kiburi – Shetani ana kiburi, hii ndio dhambi yake ya kwanza na kubwa
iliyosababisha akafukuzwa mbinguni, shetani anaposhindwa kukupata katika maeneo
mengine yote sindano muhimu atakayoitumia ili unajisikie ni kiburi, kwa kuwa
Shetani alikataliwa kwa sababu ya kiburi, njia ya kukubalika kwa Mungu ni
unyenyekevu, kama njia ya kushusha ni kiburi basi njia ya kupandishwa juu ni
unyenyekevu
Ezekiel 28:17 “Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu
hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya
wafalme, wapate kukutazama.”
Wafilipi 2:5-9 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani
ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona
kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya
kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena,
alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti,
naam, mauti ya msalaba.Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina
lile lipitalo kila jina;”
Shetani anatamani tuwe kama yeye, tuwe na
kiburi, wakati wowote kama kuna jambo ambalo sisi wakristo tunapaswa kujihami
nalo ni pamoja na kiburi, kiburi kinaweza kuharibu kila kitu tulicho nacho
ikiwa ni pamoja na utumishi wetu. Na ndio maana maandiko yanatuonya kuwa makini
tusijivune na kuanguka katika hukumu ya ibilisi yaani kukataliwa.
1Timotheo 3:6 “Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna
akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.”
8. Shetani ana hasira – Tofauti na utendaji wa kiungu ambao unasukumwa
na upendo katika kumuokoa mwanadamu, shetani anasukumwa na uchungu, hasira kali
sana au hasira kubwa sana, hasira iko moyoni mwake, ana ghadhabu kubwa sana nah
ii ndiyo inayomsukuma kwa uchungu mkubwa kushambulia watu.
Ufunuo 12:12 “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa
nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi,
akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”
Neno Hasira au ghadhabu nyingi katika
kiingereza great wrath, kwenye biblia ya kiyunani neno linalotumika hapo
ni “thumos” ambalo tafasiri yake ni “fierceness”, yaani
forceful and aggressive maana yake anasukumwa na uchungu mwingi sana kwa
hiyo hata kama humuoni shetani akitumia nguvu fahamu tu moyoni mwake ana
uchungu na wewe na mimi, anachukizwa na sisi sana, Hasira hii anayo siku zote
uchungu huu anao siku zote kwa hiyo shetani hafanyi jambo kwa kukuhurumia
ataendelea hivyo mpaka mwisho, kwa msingi huo kwa kadiri tunavyoendelea
kutembea na Mungu na kumtumikia yeye anachukizwa sana na ana uchungu mno na
wewe na mimi na kila kitu tulicho nacho. Jambo kubwa la kumshukuru Mungu ni
kuwa tunalindwa na nguvu za Mungu. Kumbuka kila anachokifanya shetani anafanya
akisukumwa na chuki na hasira na uchungu, tushukuru tunalindwa na nguvu za
Mungu na malaika zake wapo.
9. Shetani ni mwenye nguvu - angetamani sana atujaze kwa nguvu
zake ili tuyatende mapenzi yake, na anatoa nguvu Fulani kwa watu wake katika
kuhakikisha kuwa wanayatimiza mapenzi yake sawa tu na namna Mungu anavyotujaza
Roho wake Matakatifu tuwe mashahidi wake yeye anaweza kushusha aina Fulani ya
ushawishi au nguvu kwa mtu au chochote ili kutimiza mapenzi yake anawapa nguvu
ya uponyaji waganga, anawapa nguvu ya kudhuru wachawi, anawapa ushawishi
matapeli, anawapa ujanja, mbinu na mvuto makahaba na kadhalika anaweza kutoa
uwezo mwingi kwa watumishi wake ili kutekeleza matakwa yake duniani.
Ufunuo 13:1-4 “Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe
kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa
vyake majina ya makufuru. Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na
miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba,
yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi. Nikaona
kimoja cha vichwa vyake kana kwamba kimetiwa jeraha la mauti, na pigo lake la
mauti likapona. Dunia yote ikamstaajabia mnyama yule. Wakamsujudu yule joka kwa
sababu alimpa huyo mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule mnyama, wakisema, Ni
nani afananaye na mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye?”
10. Shetani ni Nafsi – Shetani ni nafsi iliyo hai na halisi, (Person) maandiko
yanavyomuelezea hayaelezei kama dhana au nguvu fulani, yanamuelezea kama “MTU”
hapa namaanisha nafsi iliyo hai na halisi kwa hiyo maandiko yanampa nafsi na ni
nafsi kweli sio nguvu hasi hii ni kwa sababu ziko dhana za falsafa fulani
duniani ambao huamini kuwa ziko nguvu mbili zinazoongoza ulimwengu yaani nguvu
hasi na nguvu chanya, au nguvu njema na nguvu mbaya kama wanavyoamini wabudha (yin
yan) nguvu chanya au njema ikiwa ni Mungu na nguvu hasi na mbaya ikiwa ni
Shetani, maandiko hayakubaliani na dhana hiyo na badala yake yanatuthibitishia
kuwa ni nafsi na kama nafsi ina sifa zifuatazo kujidhihirisha
a.
Anazungumza
– Ayubu 1:6-12 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha
mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Bwana akamwuliza Shetani,
Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika
kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.Kisha Bwana akamwuliza
Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja
aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na
kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu
yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba
yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali
yake imeongezeka katika nchi.Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote
aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako. Bwana akamwambia Shetani,
Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu
yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana.”
Kama shetani anaweza kuzungumza ni wazi kuwa pia hutoa maagizo kwa
watumishi wake ana uwezo wa kuwasiliana, kuamuru, kuagiza na kutekeleza maswala
kadhaa katika maisha ya ulimwengu wa roho na kupitia maajenti wake duniani
b.
Anaweza
kumjia mtu – Mathayo 4:3-11 “Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu,
amuru kwamba mawe haya yawe mikate. Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu
hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha
hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana
imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije
ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu
Bwana Mungu wako. Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha
milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa,
ukianguka kunisujudia.Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana
imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.Kisha Ibilisi
akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.”
Shetani kama nasfi inaweza kumjilia mtu au kumtokea mtu, na kufanya
mazungumzo hii inadhihirika wakati huu ambapo shetani alimtokea Yesu na Yesu
alizungumza naye kihalisia na kuchukuliana naye kwa uangalifu mkubwa sana na
hekima kubwa kwa hiyo tunajifunza ya kuwa shetani sio nguvu pinzani bali ni
mpinzani wa Mungu na wanadamu au watu wa Mungu na ya kuwa ikiwa Yesu
alimchukulia kwa tahadhari kubwa sana sisi nasi hatuna budi kumchukulia kwa
tahadhari kubwa zaidi
c.
Anaelezewa
kama Nafsi – Waandishi wa neno la Mungu karibu wote hawajawahi kumuelezea shetani
kama nguvu hasi bali wanamuelezea kama nafsi kiumbe halisi na matamko yake yako
hivyo hivyo
Zekaria 3:1-2 “Kisha
akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na
Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. Bwana akamwambia
Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na
akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni? ”
Yakobo 4:6-7 “Lakini
hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao,
bali huwapa neema wanyenyekevu.Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye
atawakimbia.”
Ufunuo 20:1-7 “Kisha nikaona
malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa
mkononi mwake. Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na
Shetani, akamfunga miaka elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri
juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na
baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache. Kisha nikaona viti vya enzi,
wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa
kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao
wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika
vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja
na Kristo miaka elfu. Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka
elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu
katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa
makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu. Na
hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake;”
d.
Anatajwa
kuwa ana moyo na ni mzuri sana kwa kuumbwa - Maandiko hayajawahi kumuelezea shetani kama kiumbe kibaya, japokuwa
alimuasi Mungu, ana kiburi, ni muasi lakini Luciferi hajaharibiwa kuwa na sura
mbaya na mapembe au kuwa mweusi na kama vile watu wanavyomchora, shetani
alikuwa mzuri sana na ni uzuri wake pia uliochangia kiburi chake na anguko
lake, ni hekima yake iliyochangia majivuno yake na tamaa yake maandiko yanamtaja
kuwa ana moyo japo ni kiumbe cha kiroho lakini kinapewa utu, kama Mungu
anavyopewa utu, Nimemwona Daudi mwana wa Yesu mtu aupendezaye moyo wangu, basi
shetani ana moyo
Isaya 14:13 “Nawe ulisema
moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota
za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za
kaskazini.”
Ezekiel 28:17 “Moyo wako
uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya
mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.”
Ezekiel 28:11-17 “Ulikuwa ndani
ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako,
akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na
yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na
filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa
tayari. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka
hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe
ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata
uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza
udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu
katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe
kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu
ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa
chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.”
Shetani amefukuzwa kutoka mbinguni kama kitu najisi, lakini hajaharibiwa
sura, wala nguvu wala hali ya kuwa na uwezo kama kerubi, na tunaona katika
maandiko Mungu akizungumza na ibilisi au shetani bila chuki, na Yesu pia
alizungumza na shetani bila chuki wala jazba wala hasira, sisemi kwamba watu
wasimchukie shetani lakini kazi yetu kubwa ni kumuelewa na kumjua na kuomba
neema ya Mungu na kujitegemeza kwake kwa sababu adui yetu sio wa kawaida ni
mwenye nguvu nasi tunahitaji nguvu za Mungu, ulinzi wake na msaada wake na
Mungu atatusaidia kwa sababu yeye anamuelewa na kumjua shetani kwa kina na
mapana na marefu kuliko sisi.
11. Shetani
ana nia – Ukiacha mpango wake wa kutaka kuabudiwa na kutaka kuwa kama
Mungu, kazi yake kubwa na nia yake kubwa ni kuiba, kuchinja na kuharibu, wakati
nia ya Kristo ikiwa ni kutupa uzima wa milele
Yohana 10:10 “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja
ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.”
Kwa nini shetani ana nia ya kuiba, kuchinja na
kuharibu? Hii ni kwa sababu ana chuki kubwa sana na uumbaji wa Mungu,
anachukizwa sisi kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kwa hiyo hana urafiki na
wanadamu, anachukizwa na ukweli ya kuwa tutakuwa na utukufu wa Mungu milele,
wakati yeye aliupoteza, ana wivu ana uchungu, ana wivu na furaha ya mielele
tutakayokuwa nayo, kumbuka kama alivyokokota theluthi ya malaika anataka pia
kukokota wanadamu wapatikane watakaokwenda naye kwenye ziwa la moto,
anachukizwa na sisi kwa sababu maelfu Rabbi mmoja wa zamani sana aliwahi kusema
“kwa wivu wa shetani kifo kiliingia ulimwenguni na wale wamfuatao wako
pamoja naye” mwisho wa kunukuu.
12. Shetani ana uwanda mpana wa utendaji – Shetani ana uwanda mpana sana katika utendaji wake wa kazi, na ndio
maana kanisa linapaswa kuwa macho, yeye hafanyi kazi tu miongoni mwa watu waovu
lakini ana daraja la juu sana katika utendaji wake kama malaika wa Nuru, kwa
kusudi la kushughulikia watu wa kanisani yeye pamoja na watumishi wake.
2Wakorintho 11:13-14 “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa
hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu. Maana Shetani
mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.”
Shetani pia ana mafundisho ambayo yako wazi na
yanajulikana kama mafundisho ya mashetani, lengo lake kuu ni kuchakachua na
kupoteza kabisa waamini na watumishi wa Mungu, anajihusisha na ibada za uongo,
watumishi wa uongo na mafundisho yake.
1Timotheo 4:1 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho
wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya
mashetani;”
Ufunuo 2:9-10 “Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua
na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la
Shetani. Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi
yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu
hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.”
Shetani pia anaonekana kuingia katika
makusanyiko ya kiimani wakati malaika wanapokusanyika
Ayubu 1:6-7 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda
kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao.Bwana akamwuliza
Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka
katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.”
Shetani anajua nguvu ya kanisa na mafundisho
ya kweli na kusanyiko la ibada na maombi na anajua kuwa akifanikiwa kuharibu
kanisa ambalo ndilo chumvi ya ulimwengu basi kila kitu kitazolewa kwa urahisi
kuelekea upande wake na kuwa mawindo yake.
13. Shetani ana mipaka - Pamoja na kutambua uweza na utendaji wa shetani na kukubali kuwa ana
akili na mjanja ni muhimu kufahamu kuwa shetani ni kiumbe na ana mipaka kila
mtu anayemuamini Bwana Yesu anahesabika kuwa amemshinda shetani, Shetani hana
kitu kwa Yesu mwenye nguvu zote, shetani hatawagusa wamwaminio Mungu mpaka kwa
ruhusa ya Mungu mwenyewe ama kwa mwamini kufungua mlango wa kushughulikiwa kwa
kukushitaki n ahata pamoja na hayo Yesu atasimama kututetea.
Yohana 14:30 “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu
wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.”
1Yohana 4:4-6 “Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda,
kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.Hao ni
wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia, Sisi twatokana na Mungu.
Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili
twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu.”
Yakobo 4:7-8 “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye
atawakimbia.Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu,
enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.”
Aidha shetani hana uwezo wa kusoma mawazo
yetu, Maandiko hayajawaho kuonyesha ya kuwa Shetani ana uwezo wa kusoma mawazo
yetu, Lakini badala yake ni Mungu pekee ndiye anayeweza kujua kile
kinachoendelea katika moyo wa mwanadamu
1Wafalme 8:39 “basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukasamehe,
ukatende, ukampe kila mtu kwa kadiri ya njia zake; wewe ujuaye moyo wake;
(maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu wote);”
Kwa hiyo ni Mungu peke yake ndiye aijuaye
mioyo ya wanadamu, Shetani hayuko mahali kote na huwategemea malaika zake
kukamilisha baadhi ya kazi zake, shetani hajui mambo yote ni kiumbe na sio
Mungu kwa hiyo ana mipaka katika utendaji wake, japo kuwa shetani anaweza
kukuingizia mawazo mabaya na kuotea na kusoma kile anachohisi anaweza kukitumia
kwa faida zake, ili kuweza kumshinda ni kumtii Mungu na kumpiga , kutumia neno
la Mungu na kukataa mawazo yoyote unayohisia na kujua kuwa yako kinyume na
mapenzi ya Mungu
14. Shetani ni adui wa injili – Pamoja na kazi zingine anazozifanya shetani usisahau hili, shetani ni
adui wa injili ni adui mkubwa sana wa injili, hataki injili iwafikie watu na
hataki mafundisho sahihi yawafikie watu anapambana kwa kila jinsi kuhakikisha
kuwa anaiharibu injili, anatumia mawazo mbadala, mafundisho potofu lakini pia
anapofusha fikra za watu wa ulimwengu huu ili isiwazukie nuru ya injili
2Wakorintho 4:3-4 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao
wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao
wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake
Mungu.”
1Wathesalonike 2:18 “Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya
kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia.”
Mathayo 13:19 “Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule
mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na
njia.”
15. Shetani anaweza kumtumia mtu – Ndio uko uwezekano wa shetani kumtumia mtu katika kushauri au kufanya
jambo ambalo liko kinyume na mapenzi ya Mungu, uko wakati Fulani ambapo Yesu
alimkemea Petro kwa kutokuwaza mapenzi ya Mungu na kufikiri kibinadamu, Yesu
alipofunua mpango wa Mungu kuhusu kufa kwake msalabani kwa ukombozi wa
mwanadamu Petro alimpinga Yesu na moja kwa moja Yesu alimkemea, Kimsingi Petro
hakuwa shetani lakini alitoa wazo ambalo kimsingi lilikuwa wazo la shetani la
kumtaka Kristo asitimize mapenzi ya Mungu, aidha katika mkakati wa kuhakikisha
Yesu anakamatwa na kusulubiwa kwa usaliti mkubwa tunaambiwa kuwa shetani
alimuingia Yuda ili kutekeleza mpango huo.
Mathayo 16:21-23 “Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya
kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa
makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua,
akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.Akageuka, akamwambia
Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya
Mungu, bali ya wanadamu.”
Luka 22:2-4 “Na wakuu wa makuhani na waandishi walikuwa wakitafuta njia
ya kumwua; maana walikuwa wakiwaogopa watu. Shetani akamwingia Yuda, aitwaye
Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara. Akaondoka, akaenda akasema na
wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao.”
Hatima ya shetani
Hakuna marefu yasiyo na mwisho au ncha, Maandiko yanaonyesha kuwa shetani
ana mwisho, na Mungu aliutangaza mwisho huo mapema mara baada ya kuingilia na
kujaribu kuharibu kusudi la Mungu kwa wanadamu
Mwanzo
3:14-15 “BWANA
Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko
wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na
mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo
mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda
kisigino.”
Unabii huu unaonyesha ya kuwa Yesu Kristo uzao wa mwanamke utamponda
kichwa Shetani anayewakilishwa na nyoka hapo.
Amefukuzwa kutoka mbinguni Ufunuo 12:9 “Yule joka
akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani,
audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa
pamoja naye.”
Wakati wa utawala wa Yesu Kristo wa millenum miaka 1000 shetani atafungwa
kwa muda huo na baada ya muda huo atatupwa katika ziwa la Moto milele na milele.
Ufunuo
20:2-3 “Akamshika
yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka
elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate
kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa
afunguliwe muda mchache.”
Ufunuo
20:9-10 “Wakapanda
juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa.
Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala. Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya,
akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa
uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.”
Na. Rev.
Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa
wajenzi mwenye hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni