Jumatano, 23 Oktoba 2024

Hapa yupo aliyemkuu kuliko Hekalu!


Mathayo 12:3-6 “Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu.”



Utangulizi:

Nyakati za agano la kale Hekalu la Mungu lilichukua nafasi muhimu  na kubwa sana katika maisha ya wanadamu hususani Wayahudi, katika uhusiano wao na Mungu, Hekalu ilikuwa ni nyumba pekee ambayo ilikuweko Yerusalem ambapo watu wangeweza kuabudu, kutoa dhabihu na kukutana na Mungu, Lakini katika namna ya kushangaza sana Yesu Kristo kwa maneno na vitendo alitangaza wazi kuwa yeye ni mkuu kuliko Hekalu!, Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kwa vipi Yesu ni mkuu kuliko Hekalu na hii ina maana gani kwa sisi kama wakristo!,Usemi huu sio tu kuwa una mapinduzi makubwa ya kiibada lakini una kitu cha maana sana cha kujifunza kuhusu Yesu Kristo, Tutajifunza somo hili Hapa yupo aliyemkuu kuliko Hekalu! Kwa kuzingatia vipengele vitatu muhimu vifuatavyo:-

·         Umuhimu wa Hekalu katika jamii ya Wayahudi

·         Hapa yupo aliyemkuu kuliko Hekalu

·         Mambo ya msingi ya kujifunza katika kanisa


Umuhimu wa Hekalu katika jamii ya Wayahudi.

Neno Hekalu kwa kiingereza “temple” katika kiibrania linatumika neno HEKHAL au BAYITH kwa kiyunani HIERON ambalo kimsingi ndio lilikuwa jina la Jumba la kifahari lililojengwa Pale Yerusalem kwaajili ya Ibada za Mungu wa Israel. Yako mahekalu mengine mengi duniani yaliyokuwa yamejengwa kwa miungu mingine, Lakini hekalu maarufu zaidi lilikuwa hekalu hili la Mungu wa Israel Lililojengwa na Mfalme Sulemani na hili ndilo tunalolizungumzia kwa kuunganisha na Neno la Yesu Kristo.

Wote tunafahamu kuwa Hekalu la Mungu kule Yerusalem lilikuwa ndio kiini kikubwa cha ibada za kiyahudi na lilishika sehemu kubwa sana ya maisha yao ya kiimani na kitamaduni, kwa wayahudi hekalu lilikuwa ni zaidi ya jengo la kawaida la kifahari, wao waliamini na ndivyo ilivyokuwa kwamba ni mahali ambapo Mungu alipachagua ili aweke jina lake hapo, hivyo palikuwa ni mahali akaapo Mungu pa kidunia, ambapo kwa mujibu wa torati iliwalazimu waende hapo, kwa kuwa ndipo alipopachagua Bwana Mungu wa Israel kama ilivyoagizwa mapema katika torati ya Musa.

Kumbukumbu 12:5-6 “Lakini mahali atakapochagua Bwana, Mungu wenu, katika kabila zenu zote, apaweke jina lake, maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe wende huko; pelekeni huko sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng'ombe na ya kondoo;”

Tofauti na masinagogi, Hekalu lilipaswa kuwa moja tu, tena Pale Yerusalem na ndipo mahali ambapo pekee pali ruhusiwa kutolewa dhabihu za kuteketezwa, kwaajili ya upatanisho wa dhambi, Hapo ndipo mahali ambapo Mungu alichagua kuwekeza uwepo wake mahali hapo, Palikuwa ni mahali patakatifu panapounganisha mbingu na inchi.

1Wafalme 8:10-13 “Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya Bwana ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya Bwana ilikuwa imejaa utukufu wa Bwana.Ndipo Sulemani akanena, Bwana alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele.”

Hekaluni ndipo mahali ambapo dhabihu za kuteteketezwa na sadaka za upatanisho kwaajili ya dhambi zilifanyika, wakati ibada hizo zilikuwa haziwezi kufanyika popote wala kwenye masinagogi, kwa lugha nyingine Israel wasingeliweza kupata msamaha wa dhambi na kupatanishwa na Mungu pasipo kufanyika kwa ibada hizo hekaluni peke yake, kwa hiyo hekalu pekee lilikuwa lango la mbingu

Bwana Mungu wa Israel alikuwa amepakubali mahali pale na kutoa ahadi nyingi sana kuhusu Nyumba ya Bwana kwa watu wake, alipakubali kama mahali pa dhabihu, alipakubali pawe mahali pa makimbilio, alipakubali pawe mahali pa kupoza vita, mapigo na matukio yoyote magumu, na alipakubali pawe mahali ambapo mtu yeyote duniani akiomba lolote kuelekea hapo Mungu angesikia dua yake na kuponya kwa ujumla ni mahali muhimu sana kwa wote waliomuhitaji Mungu na wanaomuhitaji Mungu

2Nyakati 7:12-16 “Bwana akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa. Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima.”

Kwa hiyo Hekalu lilikuwa ni sehemu muhimu ya Imani, Dini, tamaduni, utaifa na umoja wa wana wa Israel na wayahudi wote kutokana na mafundisho yao, kila wakati na kila mwaka zilikuwepo sikukuu muhimu sana ambazo ziliwakutanisha wayahudi pamoja kama hija zikiwapeleka Yerusalem na hivyo kuwa alama kubwa sana ya umoja wa kitaifa na kiimani, kitamaduni na kihistoria na sehemu muhimu ya utambulisho wa Mungu wa Israel kwa dunia nzima. Kuna maandiko mengi na zaburi nyingi zinazoonyesha umuhimu mkubwa wa nyumba hii ya Bwana na uweza na nguvu na mamlaka aliyokuwa ameiwekeza hapo kwa hiyo kwa ujumla:-

1.       Hekalu lilikuwa ni kiini cha Imani ya wayahudi wa kale na sehemu muhimu kwa ibada  ilikuwa ni mahali ambapo watu walilia na kupakumbuka sana walipokosa uhusiano na mahali hapo au walipokuwa mbali na mahali hapo

 

Zaburi 42:2-4 “Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai, Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu? Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako. Nayakumbuka hayo nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu, Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano, Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu, Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu.”

 

Zaburi 137:1-5 “Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni? Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe, Mkono wangu wa kuume na usahau.”

 

Zaburi 122:1-2 “Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana. Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.”              

 

2.       Palikuwa ni mahali ambapo waliweza kutoa dhabihu, kuondoa au kuweka nadhiri kumuita Mungu na kupokea fadhili za Mungu

 

Zaburi 66:13-20 “Nitaingia nyumbani mwako na kafara; Nitaondoa kwako nadhiri zangu; Ambazo midomo yangu ilizinena; Kinywa changu kikazisema nilipokuwa taabuni. Kafara za vinono nitakutolea, Pamoja na fukizo la kondoo waume, Nitatoa ng'ombe pamoja na mbuzi. Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu, Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu. Nalimwita kwa kinywa changu, Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulimi wangu. Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, Bwana asingesikia. Hakika Mungu amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu. Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake.”

 

3.       Hekalu palikuwa ni mahali ambapo kila mtu wa Mungu nyakati za agano la kale alipaonea shauku au alipaonea hamu

 

Zaburi 23:6 “Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.”

 

Zaburi 27:4-5 “Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake. Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba.”

 

Zaburi 122:1-2 “Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana. Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.”

 

4.       Palikuwa ni mahali ambapo Israel walitembelea kila mwaka wakati wa sikukuu akiwepo Bwana Yesu mwenyewe alipokuwa kijana mdogo, na hii ilikuwa ni kwa mujibu wa maagizo ya torati ya Musa

 

Kumbukumbu 16:16-17 “Mara tatu kwa mwaka na watokee wanawaume wako wote mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; wala wasitokee mbele za Bwana mikono mitupu. Kila mtu na atoe kama awezavyo, kwa kadiri ya baraka ya Bwana, Mungu wako, alivyokupa.”

 

Matendo 2:5-11 “Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.”

 

Luka 2:41-51 “Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.”

 

5.       Palikuwa ni mahali maalumu kwaajili ya maombi na ibada kwa wayahudi wote kokote waliko au sehemu maalumu ya muelekeo wa maombi (Prayer direction)

 

Isaya 56:5-7 “Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema kuliko kuwa na wana na binti; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa mbali. Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.”        

 

Daniel 6:10 -11 “Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo. Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.”

 

6.       Palikuwa ni Mahali ambapo utukufu wa Mungu ulikaa – tangu nyakati za safari ya wana wa Israel Jangwani uwepo wa Mungu ulishuka katika nyumba ya Bwana iliyokuweko jangwani iliyojulikana kama Hema la kukutania, kimsingi Hema ya kukutania lilikuwa ni hekalu la muda linalohamishika na walipofika katika nchi ya kanaani Hekalu lilijengwa kwa mfano wa ile hema ya kukutania, uwepo huo wa Mungu ulionekana kwa jinsi ya macho ya kibinadamu kama wingu la utukufu ambalo kwa kiibrania lilitwa  Shekinah

 

Kutoka 33:9-10 “Ikawa Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye BWANA akasema na Musa. Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake.”

 

Sio hivyo tu wakati mwingine malaika wa Bwana alijitokeza akijiunganisha na nguzo ile ya wingu, na malaika huyu wakati mwingine ilionekana wazi kuwa alimuwakilisha Bwana mwenyewe, na mara nyingi malaika huyu alijitokeza akiwa na mamlaka ya kiungu na Pengine alikuwa ni Yesu mwenyewe katika agano la kale

 

Kutoka 14:19 “Kisha malaika wa Mungu, aliyetangulia mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akaenda nyuma yao; na ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao, ikasimama nyuma yao;”

 

Wingu la utukufu wa Mungu wakati wote lilikuwa linawakilisha uwepo wa Mungu, Na ilikuwa ni shauku ya Mungu kuwa pamoja na watu wake, na uwepo huu ulijirudia kulikalia Hekalu lilipokuwa limejengwa na kuwekwa wakfu, aidha wakati mwingine ulionekana kama moto ulioshuka kutoka mbinguni na hii inaweza kutupa picha pana kuwa uko uwezekano kuwa kile kijiti alichokiona Musa kinawaka moto lakini hakiteketei ulikuwa ni uwepo huu wa Mungu na ule uliokaa usoni kwa Musa na kuufanya uso wake kung’aa

 

2Nyakati 7:1 “Basi Sulemani alipokwisha maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa Bwana ukaijaza nyumba. Wala makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa Bwana, kwa kuwa utukufu wa Bwana umeijaza nyumba ya Bwana.”             

 

Kimsingi uwepo huu wa Mungu uliokuwa ukionekana na kukaa katika hekalu na hema ya kukutania alikuwa ni Mungu mwenyewe,  nahii iko wazi kwa mujibu wa injili ya Yohana kuwa kumuona Yesu ni kuuona utukufu wa Mungu, Kristo anatafasiriwa kuwa ndiye mng’ao huo wa utukufu wa Mungu ndiye Shekinah mwenyewe, ambaye hakalu halina maana bila uwepo wake.

 

Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”      

 

Waebrania 1:1-3 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;”

                               

Nyumba hii ya Mungu ilikuwa ni ya Muhimu sana, na ilijengwa katika mlima wa Moriah mahali ambapo Inasadikiwa kuwa Ibrahimu alitaka kumtoa Isaka kama sadaka ya kuteketezwa, mahali ambapo Mfalme Daudi alipanunua lilipokuwa Shamba la Arauna Myebusi, ili aweze kutoa dhabihu hapo na kumjengea Mungu madhabahu, kihistoria Hekalu lilijengwa mara tatu La kwanza likiwa limejengwa na Suleimani, na baadaye Zerubabel na mwisho Herode mkuu alilikarabati na kulijenga kwaajili ya wayahudi na hili ndilo Hekalu ambalo Yesu alilitumia na baada ya kupoteza umuhimu wake na kuharibiwa ndipo mahali ambapo sasa inasimama nyumba ya kiislamu iitwayo Masjid Al - Aqsa  ambayo iko chini ya utawala wa Hashemites au Bani Hashem ukoo ambao ni uzao wa waarabu wanaotokana na ukoo wa Makuresh moja ya kabila za wana wa Ishmel  mwana wa Ibrahimu, ambapo ndio ufalme wa Jordan leo. Yako mambo mengi sana ambayo tungeweza kuzungumza kuhusu hekalu lakini natamani kumzungumzia Yeye aliye mkuu kuliko Hekalu lenyewe kwa sababu huyo ni wa Muhimu sana sasa kuliko hekalu halisi lililokuwako Yerusalem kwa wakati huo.

Hapa yupo aliyemkuu kuliko Hekalu 

Wote tunaweza kuona jinsi Hekalu lilivyokuwa ni nyumba muhimu sana kwa Wayahudi, na sasa Bwana wetu Yesu Kristo anapokuja na kukiri au kutangaza ya kuwa yeye ni Mkuu kuliko Hekalu maana yake anatamka kitu kikubwa sana cha kushangaza ambacho hatuna budi kutoa kipaumbele  na kuliangalia jambo hili kwa umakini mkubwa kwa sababu kwa tamko lake maana yake sheria zote na maswala yote ya msingi kuhusu Hekalu yanapoteza maana zake na mwelekeo mzima unaelekea kwake, wayahudi walikuwa wakifikiri kuwa hekalu ndilo lililokuwa linabeba uwepo wa Mungu kwa ukamilifu wake na sasa Yesu anaonyesha ya kuwa Uwepo ule wa Mungu sasa ni yeye mwenyewe.

1.       Hii ilikuwa na maana ya moja kwa moja kuwa Yesu ni Mungu – Hekalu ilikuwa ni mahali ambapo Mungu alipachagua kuweka jina lake hapo na uwepo wake ili aweze kuwa katikati ya watu au ili aweze kutimiza mpango wake wa kukaa pamoja na wanadamu yaani Mungu pamoja nasi.

 

Mathayo 1:21-23 “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.”

 

Hekalu lilikuwa linaufunga uwepo wa Mungu mahali pamoja lakini Yesu alikuwa akiufungua uwepo wa Mungu kwa ulimwengu mzima, yeye ni uwepo halisi wa Mungu na ndiye neno halisi la Mungu, watu walikuwa wakienda Hekaluni kumuabudu yeye na sasa kama yeye mwenyewe yupo maana yake uwepo wa ibada sasa hauna budi kuelekezwa kwake na yeye ndiye lango la Mbinguni, na ndiye kiini cha ibada na kumtukia yeye ni kuufikia uwepo wake.

 

Yohana 1:1-3, 14 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. 14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”     

 

2.       Yesu alikuwa akijitambulisha kuwa yeye ndio ukamilifu wa sadaka za dhabihu na ndiye kuhani mkuu halisi – Yesu alikuwa ndio dhabihu halisi na vile vile kuhani mkuu milele na milele, aliyatoa maisha yake mwenyewe kuwa dhabihu timilifu kwa ulimwengu na hivyo kukomesha mahitaji ya dhabihu za kawaida za wanyama zilizokuwa zikitolewa Hekaluni, kwani dhabihu yake yenye maana ingeweza kuwa dhabihu ya milele itakayofanya upatanisho wa moja kwa moja wa dhambi kwa wanadamu wote duniani bila kuhitaji hekalu

 

Waebrania 9:11-14 Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?

 

Waebrania 10:8-12 “Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu. Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu;”

 

3.       Yesu ndiye njia ya kufikia uwepo wa Mungu – Wakati hekalu ndio ilikuwa njia ya kumfikia Mungu, Yesu anaonyesha kuwa yeye ndio njia ya moja kwa moja ya kuufikia uwepo wa Mungu, kupitia yeye tunaweza kukifikia kiti cha rehema cha Mungu kwa ujasiri na kupata rehema bila kupitia kokote.

 

Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

 

Pazia katika hekalu lilipasuka katikati vipande viwili wakati Yesu anakata roho pale msalabani hii ilikuwa ikitufundisha wazi kuwa kikwazo kilichokuwa kinamzuia kila mmoja wetu kumfikia au kuufikia uwepo wa Mungu kimeondolewa na sasa kila mtu kwa wakati wake na kwa nafsi yake anaweza kumfikia Mungu kwa Imani katika damu ya Yesu na kukutana na mahitaji yake

 

Mathayo 27:50-51 “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;”

 

4.       Yesu alikuwa akijitambulisha kuwa yeye ndiye mng’ao wa utukufu wa Mungu (Shekinah)

Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”      

 

Waebrania 1:1-3 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;”

 

5.       Yesu alikuwa akitukumbusha ya kuwa sisi ndio Hekalu halisi na kuwa yeye anakaa ndani yetu – Waandishi wa nyakati za karne ya kwanza nyakati za kanisa, waliendelea kutumia lugha ya hekalu si kwa kumaanisha jengo tena na badala yake walianza kumaanisha kuwa hekalu ni watu wa Mungu kila mtu aliyeokolewa ni kipande cha tofali katika hekalu hilo, ni sehemu ya kiungo katika mwili wa Kristo.

 

1Wakorintho 6:19-20 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu

 

Badala ya watu kwenda kuutafuta uwepo wa Mungu kule Yerusalem lilikokuweko Hekalu, sisi kama hekalu la Mungu sasa tunapaswa kuubeba uwepo wa Mungu na kuupeleka duniani kote pale tulipo mpaka Yesu arudipo.

 

Mambo ya msingi ya kujifunza katika kanisa. 

1.       Kumuabudu Mungu katika roho na kweli – Ibada ya kweli haiitaji tena mahali Fulani pa ibada, hapa sisemi watu waache kwenda Kanisani, lakini namaanisha kuwa hatuhitaji tena kwenda hija Yerusalem kwaajili ya ibada kwani Mungu ni Roho na anapatikana kokote, kwa hiyo kila mtu anapaswa kuufungua moyo wake na kuuelekeza kwa Yesu kwaajili ya kumuabudu, kumuomba na kupeleka mahitaji yetu, aidha huitaji kweda milimani ingawa hakuna anayekuzuia kwenda huko kwaajili ya kutafuta utulivu na kuutafuta uso wa Mungu lakini ni lazima uelewe kuwa Mungu anapatikana popote pale  na yuko karibu na yeyote yule maadamu tu utauelekeza uso wako kwake.

 

Yohana 4:23-24 “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

 

2.       Kuzingatia umoja – Hekalu lilikuwa likiwaunganisha wayahudi wote duniani, kumkumbuka Mungu wao, tamaduni zao na utaifa wao na kuwakumbusha kuwa wao ni kitu kimoja, sisi nasi kupitia Yesu Kristo kama Kanisa tunapaswa kuelewa kuwa sisi ni kitu kimoja

 

Wagalatia 3:26-28 “Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.”

 

3.       Hakuna mauti tena hekaluni – Mara kadhaa tumesoma katika maandiko ya agano la kale kuwa wako watu ambao walikufa au walifia hekaluni kwa sababu ya kukiuka maswala mbalimbali na kanuni mbalimbali za hekaluni, Lakini Yesu anatangaza sasa kuwa kama jinsi ambavyo Daudi na wenzake, waliweza kula mikate ya wonyesho bila kufa (Kwa Sababu Daudi alikuwa na Yesu viunoni mwake) hali kadhalika kila amwendeaye Yesu tatapata uzima na uzima wa milele na hakuna mauti kwa mtu amwaminiye Yesu ambaye ni mkuu kuliko Hekalu

Mathayo 12:3-6 “Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu.”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote 

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima.

Jumatano, 16 Oktoba 2024

Kutoka Misri kwa ujeuri!


Kutoka 14:5-8 “Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya magari hayo yote. Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.”

 



Utangulizi:

Leo tutachukua Muda kutafakari kwa kusudi la kujifunza na kupandisha imani zetu kwanini maandiko yanasema Israel walitioka Misri kwa ujeuri? Jambo ambalo lilimfanya Farao kubadili mawazo na kuamua kuwafuatilia wana wa Israel baada ya kikao cha Dharula cha baraza la mawaziri na majeshi yake, kujadili kuwa imekuwaje wakawaachia Israel waende zao? Na wasiwatutumikie tena? Uchumi wao utasimamaje bila watumwa? Kazi zote ngumu za uzalishaji mali zitafanywa na nani? Kwanini tunawaachia watumwa waende kwa uhuru hata bila kupigana nao? Au kutumia nguvu kuwarejesha? Baada ya hoja nzito mswada ulipitishwa kuwa ni lazima watu hao warejeshwe utumwani vinginevyo tutapata hasara kubwa sana!

Kutoka 14:5-10 “Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya magari hayo yote. Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia BWANA.”

Leo tunapojifunza somo hili Roho Mtakatifu ananiambia kuwa kuna watu watatoka kwa jeuri, wataondoka katika mateso yao kwa mkono ulionyooshwa wa Bwana, watafunguliwa vifungo vyao kwa nguvu na uweza wa Mungu wetu, watakombolewa kutoka katika mateso yao na maumivu yao na majonzi yao, na utumwa wa kila aina unaoyazinga maisha yao, na kila kitu chenye kusononesha maisha yako leo kitakuwa ndio mwisho wa utawala wake katika maisha yako nawe utaenda zako kwa jeuri, Nasema leo utatoka kwa ujeuri katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai haleluyaaa! Tutajifunza somo hili kutoka Misri kwa ujeuri kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-


·         Maana ya kutoka kwa jeuri

·         Nani ni sababu ya Jeuri yetu

·         Kutoka Misri kwa ujeuri

 

Maana ya kutoka kwa jeuri

Kutoka 14:8 “Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.”

Katika kifungu hiki cha maandiko tunajifunza namna na jinsi Mungu alivyoingilia kati swala zima la mateso ya watu wake waliokuwa wanateseka kule Misri, Mungu alikuwa amechoshwa na utawala katili wa Farao, asiyekuwa na shukurani ambaye aliwatumia watumishi wake na wasimamizi wake kuwatesa wana wa Israel na kuwaletea msiba mkubwa na mateso makubwa kiasi ambacho waliugua na kumlilia Mungu.

Kutoka 3:7-9 “BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.”

Wote tunakumbuka namna Mungu alivyotekeleza mpango wake ambao mara kwa mara ulikuwa ukikataliwa na Farao vilevile kwa jeuri aliyokuwa nayo, akigoma kabisa kuwaachia wana wa Israel na kuwaongezea machungu na mateso makali zaidi huku akijaa kiburi na kujifanya hamtambui Bwana na kuwa watu hao wana kauli za uongo na ni wavivu hivyo akawakazia kazi ngumu zaidi.

Kutoka 5:1-9 “Hata baadaye, Musa na Haruni wakaenda wakamwambia Farao, wakasema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Wape watu wangu ruhusa waende, ili kunifanyia sikukuu jangwani.Farao akasema, BWANA ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui BWANA, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao. Wakasema, Mungu wa Waebrania amekutana nasi; twakuomba, tupe ruhusa twende safari ya siku tatu jangwani, tumtolee dhabihu BWANA, Mungu wetu; asije akatupiga kwa tauni, au kwa upanga. Mfalme wa Misri akawaambia Enyi Musa na Haruni, mbona mnawaachisha watu kazi zao? Enendeni zenu kwa mizigo yenu.Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao. Na siku ile ile Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema, Msiwape watu tena majani ya kufanyia matofali, kama mlivyofanya tangu hapo; na waende wakatafute majani wenyewe. Lakini hesabu ya matofali waliyokuwa wakifanya tokea hapo, wawekeeni iyo hiyo, msiipunguze hata kidogo, kwa maana ni wavivu hao; kwa hiyo wanapiga kelele, wakisema, Tupe ruhusa twende kumtolea Mungu wetu dhabihu.Wapeni watu hao kazi nzito zaidi, waitaabikie; wala wasiangalie maneno ya uongo.”

Jambo hili liliwapa uchungu wana wa Israel zaidi, hali yao wakati wanadai uhuru wa ruhusa ilibadilika kuwa mbaya na chungu zaidi, Jambo lilopelekea sasa Mungu kuanza kumuadhibu Farao kwa mapigo mazito sana huku akiwapendelea wana wa Israel ambao walianza kupata faraja kwa kutokuguswa na mapigo mazito, mapigo yaliyendelea mpaka lilipofika pigo la kumi ambalo lilisababisha msiba mkubwa kuanzia kwa Farao mpaka kwa wanyama wao na watumwa wao wote kila mahali walifiwa na mzaliwa wa kwanza jambo lililopelekea kutoa ruhusa ya haraka haraka ili wana wa Israel waende zao wakamuabudu Mungu kwa uhuru na pasipo hofu! Mungu mwenye nguvu YHWH alijionyesha uwezo wake na kumtiisha mfalme mwenye kiburi awaachie watu wake ambao kimsingi nao waliondoka kwa mikogo sana waliondoka kwa furaha na walindoka Misri kwa ujeuri ni nini maana ya wana wa Israel kuondoka kwa Jeuri ambacho kimsingi kilimfanya Farao abadilishe maamuzi? Hilo ndilo jambo la msingi ambalo tunataka kujifunza kwa kila leo ili nasi tutoke kwa ujeuri katiika kila Nyanja ambayo ibilisi ameweka mkono wake! tuchunguze andiko hilo kwa kina tena !

Kutoka 14:8 “Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.”

Farao aliwafuta tena wana wa Israel kwa kiburi kwa sababu wana wa Israel walitoka kwa ujeuri ni nini hasa maana ya ujeuri unaozungumzwa hapo, kimsingi neno la kiebrania linalotumika hapo ni “Rûm” ambalo kimatamshi linatamkwa room neno hili lina maana pana zaidi kama nitakavyokuonyesha kwanza tafasiri nyingine za matoleo ya biblia ya kiingereza ili uweze kubaini misamiati tofauti tofauti upate kufaidika na maana halisi ya neno hilo:-

-          King James Version (KJV) – and the Lord hardened the heart of Pharaoh king of Egypt, and he pursued after the children of Israel, and the Children of Israel went out with and high hand

-          English Standard version (ESV) - and the Lord hardened the heart of Pharaoh King of Egypt, and he pursued after the people of Israel while the people of Israel were going out defiantly.

-          The Message Bible (MSG) – God made pharaoh king of Egypt stubborn, determined to chase the Israelites as they walked out on him even without looking Back.

-          God’s word translation (GW) – the Lord made pharaoh (the king of Egypt) stubborn that he pursued the Israelites, who were boldly leaving Egypt.

-          Holman Christian Standard Bible (CSB) – The Lord hardened the heart of Pharaoh king of Egypt and he pursued the Israelites, who were going triumphantly.   

Sikutaka kutumia matoleo mengine ambayo kimsingi yanaweza kuwa yamerudia neno mojawapo kama haya yaliyotumika hapo juu, hivyo nimechagua matoleo ambayo yametumia misamiati mbali mbali tofauti ili tuweze kujifunza kwa upana

1.       High – hand – Mkono ulionyooshwa, kwa nguvu kwa mamlaka, bila kujali hisia zao

2.       Defiantly. – Kwa lazima, kwa kuasi, bila kumtii au kumsikiliza Farao tena

3.       even without looking Back – Bila kutazama nyuma, moja kwa moja bila kujali wala kuhuzunikak

4.       boldly leaving – Kwa ujasiri, Bila kuogopa, bila hofu, ukijua uendako,

5.       triumphantly – Kwa shangwe, kwa furaha, kwa ushindi wa kufikia malengo

Rûm – Kwa ujeuri sasa maana yake kwa mkono wa Bwana ulionyooshwa, Kwa nguvu na mamlaka ya Mungu, wakati wao wanaomboleza kwa misiba, Israel anasonga mbele, Kwa lazima, kwa kuasi amri ya Farao, bila matakwa yake, bila kumsikiliza, bila kumtii, kwa kuinuliwa juu kulikopitiliza, bila kutazama nyuma, wala mpango wa kurejea tena, moja kwa moja bila kujali ya nyuma, kwa ujasiri, bila woga wowote, wakiwa wanajua kule wanakokwenda, sio kwa kubahatisha, kwa furaha na shangwe kwa mikogo, wakiwa na ushindi wa kufikia malengo, wakijivunia walioinuliwa sana, kwa uchangamfu sio kwa machozi. Kwa hiyo wana wa Israel kwao ilikuwa ni siku ya furaha kubwa sana kila mmoja ilikuwa ni shauku yake kuwa ni lini Bwana atakuja kuwatoa watoke katika hali waliyokuwa wakiipitia, walikuwa wamechoshwa na walikuwa sasa imani zao zimepanda sana, Israel walitoka si kwa jeuri yao bali walikuwa wamejaa matumaini, wametiwa nguvu, hawana hofu ya kurejea nyuma, Imani yao ilikuwa imepanda sana saababu kubwa ikiwa ni Mungu wao na namna alivyojifunua kwao kwa mkono wake uliohodari, mkono wa Bwana ulioonyooshwa, Bila hofu kwa ujasiri na kwa kujiamini.

Waebrania 11:27-29 “Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana. Kwa imani akaifanya Pasaka, na kule kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wao.Kwa imani wakapita kati ya Bahari ya Shamu, kama katika nchi kavu; Wamisri walipojaribu kufanya vivyo wakatoswa.”

Nani ni sababu ya Jeuri yetu.

Israel walitoka kwa nguvu, kwa mamlaka na uthabiti mwingi kama tulivyojifunza hapo juu, sababu kubwa ya ujeuri huu haikuwa jeuri ya kibinadamu bali walikuwa wamejifunza jinsi Mungu alivyo mwema katika njia zake, kadiri alivyojifunua kwao kwa mapigo yale yote kumi, kila pigo lilikuwa ni shuhuda ya kuwa wanaye mtetezi ambaye hakuna anayeweza kupambana naye, ujeuri huu ulikuwa unatokana na nguvu alizonazo Mungu, Mungu wetu miujiza waliyokuwa wameiona ilikuwa imewapa imani thabiti kuwa wanaye Mkombozi, na hivyo hawakua na mashaka naye.

Wamisri pamoja na mfalme wao jeuri waliwasisitiza Israel kundoka maana hali yao ilikuwa mbaya na hawakujua kama watasalimika waliona kuwa wameisha wote hivyo waliwataka waondoke haraka

Kutoka 12:29-33 “Hata ikawa, usiku wa manane BWANA akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao aliyeketi katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa mtu aliyefungwa katika nyumba ya wafungwa; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. Farao akaondoka usiku, yeye na watumishi wake wote, na Wamisri wote; pakawa na kilio kikuu katika Misri; maana hapakuwa na nyumba hata moja asimokufa mtu. Akawaita Musa na Haruni usiku, akasema, Ondokeni tokeni katika watu wangu, ninyi na wana wa Israeli; enendeni, kamtumikieni BWANA kama mlivyosema.Twaeni kondoo zenu na ng'ombe zenu kama mlivyosema, enendeni zenu, mkanibariki mimi pia.Wamisri nao wakawahimiza watu, kuwatoa katika nchi kwa haraka, maana walisema, Tumekwisha kufa sote.”

Mungu alikuwa pamoja nao na wala hakuwaacha wakati wa mchana wala wakati wa usiku, hii iliwapa ujasiri mkubwa sana, Mungu aliwashughulikia vikali maadui wa Israel na alionekana wazi kwa nguzo ya wingu wakati wa mchana na alionekana wazi kwa nguzo ya moto wakati wa usiku na ni yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa akiwaongoza njia, Jambo hili liliwapa ujasiri mkubwa sana.

Kutoka 13:21-22. “BWANA naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.”

Hakuna jambo linatupa kiburi kama kujua ya kuwa Bwana yuko pamoja nasi, hakuna jambo linatupa ujasiri kama kujua Neno la Mungu linasema nini juu yetu, hakuna kitu kinatupa kujiamini kama kujua kuwa BWANA ni siri ya wokovu wetu, nuru yetu na ngao yetu, na ulinzi wetu, BWANA ni kila kitu kwetu hakuna jambo linatupa nguvu na mamlaka kama kujua ya kuwa Bwana anatupenda sana, na kuwa yuko upande wetu, hakuna jambo linatupa matumaini kama kujua ya kuwa Mungu ni mtetezi wetu na ya kuwa yuko hai, na yuko pamoja nasi kututetea na kutulinda na kutufunika !

Zaburi 27:1-3 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”

Ayubu 19:25-27 “Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu.”

Warumi 8:33-39 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

Israel walipata Jeuri kwa sababu walijua kuwa Mungu ni Mungu anayesimamia neno lake, na agano lake akitamka kitu ni sheria, lazima kiwe, Mungu wetu ni mwaminifu na hatatuacha, wala hatatuangusha, andiko linasema na kila amwaminiye hatatahayari kamwe. Kama ni hivyo kwanini shetani asituone tuna jeuri, kwanini wapinzani wako wasikuone una jeuri? Kwanini wqasikuone una mikogo kwa sababu Bwana ndiye sababu yetu

Kutoka Misri kwa ujeuri

Neno la Mungu linatukumbusha ya kuwa Mungu ni mwaminifu katika kazi yake ya ukombozi, na kuwa yeye yuko tayari kumtoa kila mmoja katika hali yake ya utumwa, na kutupa ujasiri wa kusonga mbele, wala tusiwe na mashaka naye, kila changamoto unayokutana nayo na inayokutumikisha inataka kukuweka utumwani, na haitaki kukuachia kwa haraka kwa sababu inataka uwe mtumwa wa hali hiyo jambo kubwa la Msingi ni kukumbuka kuwa leo ni siku yako ya kutoka Misri kwa ujeuri, una shuhuda nyingi za jinsi Bwana alivyoyapigania maisha yako na  ya wengine kwa hiyo hauna sababu ya kuogopa au kulia na kuomboleza hata adui akijaribu kukufuata tena anachokitafuta kitampata, Farao alipojaribu kuwafuatia Israel kwa sababu walitoka kwa jeuri maandiko yanasema alifutiliwa mbali yeye na majeshi yake yote, katika biblia ya kiingereza inaonekana vizuri zaidi kuwa Farao pia alifutiliwa mbali kabisa na majeshi yake yote na hakubakia hai ona   

Zaburi 136:13-15 “Yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akawavusha Israeli katikati yake; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akamwangusha Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.”

Psalm 136:13-15 “to him who divided the Red Sea asunder His love endures forever. And brought Israel through the midst of it, His love endure forever, BUT SWEPT Pharaoh and his army into the Red Sea; His love endure forever

Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Majeshi ya wamisri yalifutwa yote sawasawa na neno la Musa mtumishi wa Mungu hapo aliposema hawa mnaowaona leo hamtawaona tena milele, Mwandishi maarufu wa Historia ya wayahudi aitwaye Flavius Josephus alisema kuhusiana na tukio hili nanukuu “And thus did all these men perish, so that there was not one man left to be a messenger of this calamity to the rest of the Egyptians” kwa tafasiri yangu “Na wote wakaangamia hata kusiwepo hata mjumbe wa kuelezea yaliyowakuta wamisri” leo nataka utoke kwa ujasiri katika kila kifungo kinachokuonea, leo nataka kifungo kinachokuonea na kukandamiza kiwe mwisho, na usikione tena leo nataka utoke katika Misri inchi yako ya utumwa kwa ujeuri, utoke nje ya uonevu wa mashetani, nje ya magonjwa, nje ya huzuni, nje ya kila kinachopoteza tumaini la maisha yako, Nje ya utasa wako, nje ya kansa, nje ya tezi dume, nje ya magonjwa ya kizee, nje ya umasikini, nje ya uonevu wa wachawi, nje ya vifungo vya nguvu za giza, nje ya mashambulizi na uonevu wa ibilisi, leo nakutangazia kwa mamlaka niliyopepewa kama mtumishi wake kwa mafuta aliyonipaka kwayo nasema  Toka kwa imani ukimtegema Mungu na kufahamu ya kuwa hatakuangusha, mtegemee yeye katika maamuzi makubwa ya maisha, uwe na ujasiri unapopita katika dhiki na shida, kabiliana na majaribu yako kwa Imani ukijua wazi hatimaye Mwokozi atasimama karibu nawe na kukutoa katika hali unayoipitia na kamwe usitazame nyuma, toka kwa ujeuri mbele kwa mbele usitazame tena jaribu lako na nakuhakikishia halitakuwepo tena!, Bwana ameniambia kuwa fadhili zake ni za milele, ikiwa aliwaokoa wana wa Israel wakatoka kwa Jeuri, leo ni zamu yako kutoka kwa ujeuri katika hali iliyokusumbua kwa miaka mingi, katika jina la Yesu Kristo pokea, mahitaji yako, pokea uzima wako, pokea ukombozi wako, pokea uhai wako, nakufungua na kukuweka mbali na mauti katika jina la Yesu Kristo nakutamkia uzima kwa mamlaka niliyo nayo katika jina la Yesu, pepo achia wasomaji wangu, achilia wasikilizaji wangu, achilia watu wa Mungu katika jina la Yesu, Nakutangazia kutoka kwa Jeuri na kumuacha Shetani akijuta na kusikitika kwa kukuachia na akijaribu kukufuata ataangamia kama Farao katika jina la Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai! Ramashakatariboso, saparatashanda, rimosakata free sakata lota fakaseta rimoso pa taratshatata parafata, katika jina la Yesu Amen!

 

Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Ijumaa, 11 Oktoba 2024

Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?


Yohana 6:65-69 “Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”




Utangulizi:

Je kuna watu wamewahi kukuacha na kuondoka katika maisha yako? Je kuna watu hawakupigii simu wala hawashughuliki tena na maisha yako? Je kuna watu mlikuwa karibu sana na siku hizi hawako karibu kama ilivyokuwa zamani? Je unahuzunika kwaajili yao? Je unalalamika kuwa hawakusalimii, hawatumi hata ujumbe na hawaulizi hata uko wapi na unafanya nini?, hawashughuliki hata kukusalimu?  kuna watu ulikuwa msaada mkubwa sana kwao, lakini sasa wako mbali na wewe? Je unahuzunika kwaajili yao? Kuna watu walikuwa faraja kubwa sana katika maisha yako, uliwapenda na wao wakakupenda, wakakufuata lakini sasa ni kama hawako na wewe, kuna wale mlisoma nao shule moja, darasa moja, kuna wale uliwasimamia harusi, kuna wale mlikuwa pamoja, mlicheza pamoja, kuna wale walikaa kwenu wakasomea kwenu, kuna wale ulisoma kwao ukakulia kwao, kuna wale ulikuwa msaada mkubwa kwao kiroho na kimwili na sasa ni kama hawataki kutambua mchango wako je unaumia kwaajili yao? Unalia kwaajili yao? Unasikitia kwaajili yao? Sikiliza wako watu ambao Mungu huwavuta kwetu na kuwaleta karibu nasi kwa makusudi maalumu, wako ambao Mungu amewaleta kwetu kama wenzi wetu, ndugu zetu, watoto wetu na ambao tunawafurahia hawa ni furaha yetu ni damu yetu ni watiifu kwetu hawawezi kutuacha kwa sababu Mungu alikusudia wawe nasi milele, kwa wakati mzuri na wakati mbaya, wako pamoja nasi hawana namna ya kujitoa kwetu, wao ni familia hawawezi kutuacha wala sisi hatuwezi kuwaacha. Lakini wako ambao Mungu huwaleta kwetu kwa sababu maalumu kama marafiki kwa kitambo, ni watu wema kwetu na wazuri kwetu lakini uko wakati ambao Mungu hufunga mlango na kuwaacha waende zao kwa sababu hawana shughuli kwetu tena, lile kusudi ambalo Mungu alikuwa amelikusudia kwa kuwaleta kwetu limeisha, Mlango umefungwa kwao kwaajili yetu, hawawezi tena kwenda unakoenda kwa hiyo Mungu hufunga mlango kwaajili yao, mchango wao wa kimwili na kiroho na kiushirika unakuwa umeishia hapo ambapo Mungu amekusudia uishie, huu ni ukweli ulio mchungu katika maisha, lakini hatuna budi kuukubali na kuujifunza na kujua kuwa ni mapenzi ya Mungu., Kama wana kazi nasi Mungu atawaleta tena Mara.

Muhubiri 3:1-8 “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa; Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa; Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena; Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.”

Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusiana na uhusiano uliofifia au uliokufa au ulioondoka na faida zake katika ufalme wa Mungu, tutajifunza namna unavyoweza kuelewa Mapenzi ya Mungu watu wanapokuacha na kuondoka zao katika maisha yako, Utajifunza namna na jinsi unavyopaswa kutokuhuzunika na kuwa na mashaka watu wanapokuacha na kukuona huna maana kwao, na kuona ya kuwa hawakuhitaji tena, hupaswi kulazimisha, wala hupaswi kujikomba komba, wewe umeumbwa kwa thamani kubwa sana  na; Ni Mungu tu aliyekuumba ndiye anayeijua thamani yako, kwa hiyo hatujifunzi kubomoa uhusiano hapa katika somo hili lakini tunajifunza kuwaachia watu wanaojiondoa katika maisha yetu wajiondoe, wataendelea kuwa rafiki zetu, na tutaendelea kuwapenda, lakini kama hawajihusishi na maisha yetu hatupaswi kuumia lazima ufikie wakati ukubali waende na ujue ya kuwa Mungu ameruhusu waende zao!, na kuna faida zake katika hilo, kwa hiyo hupaswi kulazimisha wakae, kwani unapojaribu kulazimisha kuwa na watu ambao wameshajiondoa katika maisha yako au Mungu amewaondoa katika maisha yako hii maana ni nini? Maana yake yake unajaribu kung’ang’ania, na kulazimisha kitu ambacho, Mungu ameshamalizana nacho katika maisha yako!, fahamu kuwa kila mtu ambaye Mungu alimleta kwako alimleta yeye kwa kusudi la kukujenga na kukupa changamoto na unapofika wakati mtu huyo au watu hao wanaondoka fahamu kuwa ni Mungu amewaondoa kwako kwa kusudi maalumu, kwa hiyo hupaswi kushangaa, kulalamika au kujifikiri kuwa una mapungufu na kulalamika na kuhuzunika na kulaani hapana!

Kifungu kile cha msingi tulichokisoma leo, ndicho ambacho kinabeba mafunuo yote ambayo Mungu amekusudia kutufundisha katika siku ya leo kwa mfumo wa kichambuzi (an Expository preachings) na tutakiangalia kupitia mstari kwa mstari tukizingatia vipengele husika katika somo hili hebu tukisome tena na kisha tutakifanyia uchambuzi wake

Yohana 6:65-69 “Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”

Tutajifunza somo hili “Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?” kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

·         Mungu ndiye mwanzilishi wa uhusiano.

·         Maumivu ya kuvunjika kwa uhusiano.

·         Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?

 

Mungu ndiye mwanzilishi wa uhusiano

Yohana 6:65 “Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.”

Katika kifungu hiki Yesu Kristo anatufunulia jambo ambalo sio tu linatokea katika maisha yake lakini vile vile linatokea katika maisha yetu kama watoto wa Mungu, Yesu alizungumza hili kuhusiana na wanafunzi wake akieleza kuwa hakuna mtu awezaye kuja kwake isipokuwa amejaliwa na baba yake wa Mbinguni, hili linatufunualia sisi nasi kuwa Ni Mungu ndiye anayeruhusu watu watukaribie na ni Mungu ndiye anayeruhusu watu waondoke,  Marafiki zetu wanaweza kuwa msaada mkubwa sana katika maisha yetu, wanaweza kutumiwa na Mungu kututia moyo, kutusaidia, kutujenga na kutupa ufahamu fulani katika safari zetu za kiroho na kimwili na kisaikolojia na kimakuzi, kwa hiyo marafiki ni neema ya Mungu, ni kupitia mahusiano ya kirafiki Mungu huwatumia marafiki kutuonyesha upendo, kutuonyesha namna na jinsi Mungu anavyojali, na hata kututia moyo na wakati mwingine huwatumia kutupa changamoto, kwa hiyo kila urafiki ni lazima utunzwe na kuchukuliwa kama zawadi ya Mungu katika maisha yetu na kuwa kupitia wao liko kusudi la Mungu, marafiki wengine huokoa maisha yetu kutoka katika maangamizi ya adui, wengine hutufundisha kuwa hata kama wako watu wanatuchukia bado wako ambao wanatuthamini sana na wanathamini mchango wetu na umuhimu wetu katika dunia hii, wengine hutusaidia kukua kiroho, na wengine tunawasaidia wao kukua kiroho na kadhalika kwa ujumla tunahitajiana na ndio maana tunahitaji ushirika.

1Samuel 18:1-5 “Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe. Sauli akamtwaa siku ile, wala hakumwacha arudi tena nyumbani kwa baba yake. Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake. Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia.”

Daudi hakukubalika sana kwa Sauli lakini hata hivyo mwana wa mfalme Yonathan alikuwa rafiki mwenye kufaa sana kwa Daudi, maandiko yanaeleza kuwa Yonathan alimkubali Daudi na na watu hawa walikuwa na agano la urafiki uliodumu sana hata baada ya maisha yao, ulikuwa ni urafiki wa kweli na wenye kufaa sana, ulikuwa ni urafiki wenye uhusiano wa kina kama uhusiano wa ndugu, Yonathan alikuwa mwelewa kwa rafiki yake Daudi, Yonathan aliyajua mapenzi ya Mungu yaliyokuwa juu ya Daudi, Yonathan hakuwa rafiki mwenye wivu wala hila, Yonathan alimtia moyo Daudi, alimpa mavazi ya kifalme aliyotumia mwenyewe, alimpa silaha, alimlinda alikuwa akimtakia mema, pamoja na kuwa baba wa Jonathan hakumpenda Daudi, alimchukia alimkusudia mabaya lakini haikuwa hivyo kwa Yonathan yeye alikuwa rafiki wa kweli. Na mtu ambaye aliangalia maslahi ya Mungu kwa upana. Hakuwahi kumponda wala kumchafulia sifa yake wala kutaka rafiki yake asipate kibali kwa mfalme, wakati wote Yonathan alikuwa faraja kubwa

1Samuel 19:4-6 “Naye Yonathani akamsifu Daudi kwa Sauli, babaye akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani, juu ya Daudi kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa mema sana. Kwa kuwa alitia uhai wake mkononi mwake, na kumpiga yule Mfilisti, naye Bwana akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo Daudi bure?Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo Bwana, yeye hatauawa.”

Kwa ujumla Yonathan alikuwa rafiki wa kweli kwa Daudi, alikuwa ni zaidi ya ndugu, alilinda uhai wa Daudi, na hakukubali maisha ya Daudi yawe hatarini wakati wote alitengeneza mazigira mazuri, ili raiki yake akubalike kwa baba yake asionekane kuwa muhalifu, alimtetea na kumtia Moyo na alimjulisha kuhusu hatari ambazo zingeweza kumkabili, kama tunataka kujifunza watu waliokuwa na urafiki wa dhati basi Daudi na Yonathani ni mfano wa kuigwa, Yonathani alikuwa ni rafiki aliyeambatana na Daudi na mwenye kufaa sana kuliko ndugu.

Mithali 18:24 “Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.”              

Marafiki zetu hawaji wenyewe kwetu huwa tunaletewa na Mungu na Mungu ndiye anayewavuta watu kuja kwetu, kama vile tu alivyowavuta wanafunzi kuja kwa Yesu Kristo, hakuna mtu awezaye kuja kwangu, isipokuwa amejaliwa na Baba yangu, Neno hilo kujaaliwa katika kiyunani linatumika neno “Didōmi” kimatamshi ni Did-o-mee ambalo maana yake “with the palm of hand” yaani ni tendo la Mungu kuushika mkono na kumleta mtu moja kwa moja na kushikisha katika kiganja cha mkono wa mwingine kama tu vile mtu anayemkabidhi bibi harusi kwa mumewe siku ya harusi yake, kwa hiyo Ni Mungu Baba ndiye anayetushika mkono na kutupeleka katika mikono ya Yesu, hali kadhalika ni Mungu ndiye anayewashika mkono wale waliokusudiwa kuwa rafiki zetu na kuwaleta katika mikono yetu, Kwa hiyo ni muhimu sana kutomchukulia kwa dharau mtu awaye yote anayetamani kuwa na urafiki na wewe kwa sababu kila unayeletewa au anayekujia analetwa kwako na Mungu kwa kusudi maalumu katika maisha yako na kwa ufalme wa Mungu, wakati wote watu wanapokuwa marafiki mioyo yao inaunganishwa kuwa kitu kimoja kwaajili ya mafanikio ya yule ambaye Mungu amemkusudia au kwa kufaidiana, na kila wakati Mungu huhakikisha kuwa pande zote mbili zinanufaika na urafiki huo, kwa hiyo wote mnajengana na kufaidiana kwani chuma hunoa chuma Mithali 27:17 “Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.” Marafiki zetu huletwa kwetu na Mungu kwa kusudi la kutusaidia na sisi kuwasaidia na wakati mwingine kwajili ya kufaidiana, kama Barnaba na Sauli au Paulo

Matendo 9:26-28 “Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka.”

Maumivu ya kuvunjika kwa uhusiano.

Yohana 6:66 “Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena.”

Hata hivyo Pamoja na kuwa Mungu huwaleta watu karibu nasi kama tulivyojifunza kutoka kwa Bwana Yesu ni jambo la kusikitisha kuwa, kuna wakati  mwingine wengine wataondoka kama ilivyokuwa tu kwa Yesu, watu au wanafunzi wengi siku hiyo waliamua kuondoka tena biblia inasema wasiambatane naye tena, hapa ni kwa sababu walishindwa kupokea mafundisho yake magumu katika akili zao, jambo hili linatufunza ya kuwa si kila mtu anayeanza safari pamoja nasi atakuwa pamoja nasi mpaka mwisho, na wakati huu ni wakati wa maumivu makali sana hakuna jambo linaumiza kama kuvunjika kwa mahusiano, yawe ya ndoa, yawe na ushirika, yawe ya kichungaji, kazini na kadhalika, lakini Mungu huruhusu watu hao waende na huo ndio unakuwa mwisho wa stori yao katika maisha yetu, inauma sana na inaumiza sana lakini hatuna budi kukubali, kama ilivyokuwa kwa Yesu Kristo ambapo wanafunzi wake walimuacha na hawakuambatana naye tena ndivyo ilivyo kwetu pia kuna kusudi kwa kila jambo katika maisha yetu,  wakati huo hakuna lolote tunaloweza kulifanya kuwafanya wabaki, Mungu tayari amekwisha kukusudia, wakuache wale wanaokupenda kwa dhati hawawezi kukuacha  watabaki na wewe iwe jua iwe mvua lakini wale ambao Mungu amekusudia waende wataenda tu hakua namna unaweza kulizuia hilo, hukuwaleta wewe kumbuka kwa hiyo  acha waende zao kwa amani, Kama Mungu ndiye aliyeamua waende hakuna unaloweza kulifanya wasiende?

Mungu ndiye mwenye funguo na mamlaka za kufunga na akifunga hakuna afunguaye, na akifungua hakuna anayeweza kufunga unaweza kujaribu kubembeleza na kujipendekeza kwa watu na ukajitahidi kuwapendeza na kufanya vizuri lakini kama Bwana hajaruhusu utakuwa unajisumbua bure, kile utakachokuwa unakitafuta ni kutafuta maumivu ya moyo tu, jaribu njia mpya na waache waende usiumie wala usikwazike ni Mungu ameruhusu, lazima tuamini kuwa Mungu ndiye anayedhibiti watu kuja na kuondoka katika maisha yetu na wengine huletwa kwetu kwa majira fulani tu kisha anawaondoa, unapoendelea kuwang’ang’ania watu ambao wamepoteza maana katika maisha yako maana yake unazuia kusonga kwako mbele au kukua katika kiwango kingine. Rafiki mimi ninajua uchungu wa kupoteza marafiki, ninapenda watu sana, sitaki kila ambaye amewahi kuwa rafiki yangu aniache, lakini uko wakati unalazimika kufanya hivyo, wako wapi uliosoma nao shule ya msingi, sekondari, vyuoni, na hata katika utumishi huu wako wapi? Wako wapi uliofanya nao kazi zamani,? Ulifika wakati waliondoka na Mungu aliwaficha na hukuweza kuwaona tena, kusudi la kuwepo kwao katika maisha yako lilikwisha kutimia na sasa Mungu anataka ufungue ukurasa mpya. Ona mfano wa maumivu yaliyomkuta Naomi:-

Ruthu 1:3-18 “Akafa Elimeleki, mumewe Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili. Nao wakaoa wake katika wanawake wa Moabu; na jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthu. Wakakaa huko yapata miaka kumi. Wakafa na Maloni na Kilioni wote wawili; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia. Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana huko katika nchi ya Moabu amesikia ya kwamba Bwana amewajilia watu wake na kuwapa chakula. Basi akatoka pale alipokuwapo, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda. Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; Bwana na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. Bwana na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia. Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako.Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa Bwana umetoka juu yangu. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.”

Tunasoma habari za Naomi, ambaye mumewe alifariki na kumuacha na watoto wawili ambao nao baadaye walioa, lakini vile vile walikufa katika nchi ya Moabu, kwa hiyo Naomi alibaki peke yake yeye na wakwe zake, Naomi aliamua kurudi kwao Yuda na aliwaeleza wakweze juu ya maamuzi yake mmoja aliitwa Orpa na mwingine Ruthu, Ruthu aliamua kubaki naye na Orpa aliamua kubaki katika inchi yake, wote walimpenda mkwe wao Naomi lakini Orpa aliamua kumbusu Naomi na kuondoka, Naomi hakuanza kulalamika kuwa Orpa anaondoka hata pamoja na wema wote aliomtendea na malezi yote aliyowapa Naomi alielewa kuwa huu ni msimu mpya ni msimu wa mabadiliko katika maisha kwa hiyo alikuwa na amani alipoachwa na Orpa alikubali kuwa Orpa aende na asiwe sehemu ya maisha yake tena, Mtu aliyekomaa kiroho/na kiufahamu huwaachia watu waende, unakubali Mungu awaondoe watu fulani katika maisha yako, Mungu ndiye anayefunga mlango au kufungua, lakini Ruthu aliamua kubaki na Naomi kwa gharama yoyote ile, hii ndio hali halisi, Yesu watu waliondoka na hakutikisika aliwauliza waliobaki naye je ninyi nanyi mwataka kuondoka? Aliendelea kuacha mlango wazi kwa kila anayetaka kumuacha, Naomi Orpa aliondoka ulikuwa wakati mgumu na wa maumivu makali sana, ulikuwa ni wakati mgumu ulikuwa ni wakati wa machozi lakini hakuna tunachoweza kufanya pale watu waliokuwa rafiki, waliokuwa ndugu waliokuwa jamaa zetu, waliokuwa wenzetu waliokuwa tunashinda nao, na kuzungumza nao wanapoamua kutuacha ni vema kukubali waende, Naomi alimbusu Orpa na kumuacha aende, kumbuka  hatuhitaji kufukuza mtu au kumaliza nao vibaya wala kuwa na uadui nao lakini sasa wanaondoka utafanya nini tuwaache waende zao kwa Amani huo ndio ukomavu wa kifikra na ukomavu kiroho na ujuzi, sio wewe tu utaacha wewe pia unaweza kuachwa na watu uliowapenda lakini wakawa hawakuhitaji tena huwezi kubadili pai isiwe 22/7  ni lazima ukubaliane na ukweli wa mambo hata kama ni mchungu kiasi gani waache waende! 

Yesu aliwahi kuwafundisha wanafunzi wake kuwa sio kila mahali watawakubali, ziko sehemu nyingine watu watakukataa hawatafungua mioyo yao kwako, watakukataa hawatakukaribisha unajua unachotakiwa kukifanya ni kukung’uta mavumbi ya miguu yako kisha enenda kule ambako watakukaribisha, hii sio kwa ugomvi ni sehemu ya kawaida kabisa katika maisha kwamba watu watakuja kwetu na kisha wataondoka na sisi halikadhalika.

Mathayo 10:13-14 “Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu.”

Matendo 18:6-8 “Walipopingamana naye na kumtukana Mungu, akakung'uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa. Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.”

Usijisumbue na watu ambao hawakutaki, watu ambao hawaoni thamani yako, wala usijaribu kuwashawishi, endapo utafanya hivyo utajichelewesha na utajipatia fadhaa bure, Ni kweli Mungu anaweza kuwabadilisha  kama watatakiwa kukuunga mkono lakini kamwe usijaribu kujilazimisha kuungana na watu wasiotambua uthamani wako, damu ya kifalme ya Yesu Kristo inatitiririka katika mwili wako wewe sio wa kawaida wewe ni mali ya Mungu na ndio maana Mungu alikuokoa na amekuumba kwa sura na mfano wake kwa hiyo usiwashawishi watu wakukubali kama mioyo yao imefungwa, Mungu ameandaa watu tayari wanaotambua uthamani wako, inaweza kuwa inauma sana lakini ndio ukubwa achana nao waache waende, katika maisha yetu wako Orpa wengi lakini vile vile wako Ruthu wengi ambao wamepangiwa kutokutuacha watakaokaa nasi, na kuambatana nasi wanaoondoka ni kuwa Mungu amemalizana nao katika kusudi lao kwako na wanaobaki ni wale ambao Mungu anataka ushirikiane nao Baraka zako, wale walio kama Ruthu watabaki kuwa waaminifu kwako  na hawatakuacha daima, hatupaswi kumfukuza mtu wala kumpiga teke mtu lakini acha wao watupige teke na kutufukuza na hapo neema ya Mungu ya urafiki wetu kwao itakuwa imefikia ukingoni  inasikitisha inaumiza sana lakini huu ndio ukweli katika maisha.

Matendo 15:36-40 “Baada ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani.Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao. Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini. Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro.Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe neema ya Bwana.”

Paulo na Barnaba walikuwa marafiki, waliitwa pamoja  na Roho Mtakatifu katika kazi ya huduma, waliihubiri injili kwa pamoja kimsingi Barnaba alikuwa ni kama Mchungaji wa Paulo mtume, ni yeye ndiye aliyemtambulisha kwa mitume na ni yeye aliye mpeleka Antiokia, walizoeana sana, waliitwa kwa pamoja na Roho Mtakatifu kwa kazi ya umisheni, lakini ulifika wakati wakaachana haikuwa kwa lengo baya wala kwa ugomvi, lakini ulifika wakati ambapo Mungu alikusudia kila mmoja awe na njia yake hili ni jambo la kawaida sana katika maisha wao tofauti yao ilikuwa ni Marko, nadhani inawezekana Marko alijisikia vibaya maana Paulo alimuona ni mtu dhaifu, Lakini Barnaba aliona Marko anahitaji malezi tu kwa hiyo kulitokea tofauti na kulitokea matengano, Lakini Mungu ni mmoja, miaka mingi baadaye, Paulo aliutambua umuhimu wa Marko na aliomba aungane naye maana anamfaa kwa huduma! Angalia:-

2Timotheo 4:10-11 “Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia. Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi.”

Paulo alimkumbuka Marko na kuagiza aletwe kwake kwa sababu ana faida nyingi sana kwa utumishi, kumbe kuna mtu anaweza asiwe na faida kwako leo, lakini akawa na faida kwako kesho, unaweza usimuhitaji mtu leo lakini ukamuhitaji mtu huyo kesho, Mungu ndiye anayehusika anaweza mtu asikufae kwa jua akakufaa kwa mfua na anaweza mtu asikufae kwa mvua akakufaa kwa jua hii ndio dunia ya Mola kwa hiyo tuheshimu mahuisiano sana  na kuyatunza isipokuwa pale to Mungu anapoamua huyu aende kule na huyu aje hapa kwa makusudi yake mema.

Wakati mwingine mafanikio yetu yanaweza kuwavuta watu wengi sana kwetu, na mapito yetu yanaweza kuwafanya wengi watukimbie, unapitia upweke? Wakati wa changamoto hakuna mtu wa kukutia moyo? Hii ilimpata Ayubu Maandiko yanasema watu wa nyumbani mwake walikuwa wengi sana ona

Ayubu 1:3 “Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, NA WATU WA NYUMBANI WENGI SANA; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.”

Unaona tunasoma kuwa watu wa nyumbani kwa Ayubu walikuwa wengi sana wakati wa mafanikio yake, lakini wakati wa dhiki yake watu wote walimuacha na kundoka zao, hata hivyo wakati wa mafanikio yake walirejea tena kwa wingi sana, hili nalo ni jambo la kawaida katika uanadamu kwa hiyo usivunjike moyo unapopitia upweke!  

Ayubu   42:10-12 “Kisha Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza. Ndipo wakamwendea nduguze wote, waume kwa wake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake; nao wakamlilia na kumtuza moyo katika habari za huo uovu wote Bwana aliouleta juu yake; kila mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja. Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu, na punda wake elfu.”

Wakati mwingine watu, na marafiki zako watakuacha kwa sababu tu unapita katika hali ngumu, lakini wanaweza kukurudia tena hali inapokuwa nzuri hili nayo ni jambo la kawaida katika maisha na hatuna budi kulielewa na kukubaliana nalo. Jambo kubwa la msingi ni kwamba mahusiano yanapaswa kutunzwa na kuwa na Amani na watu woe ni swala la smingi sana tuwapo duniani. lakini watu wanapoondolewa kwetu, tumshukuru Mungu kwaajili yao                                  

Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?

Yohana 6:67-69 “Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”

Yesu anatufundisha kuwa yeye alikuwa tayari kuwaacha watu waende zao, Kama wamechagua kwenda hakuwalazimisha kubaki nao lakini aliwapa uhuru wa kuondoka ili wafanye maamuzi yao wenyewe, waache waende zao kwa Amani, kama wamejisikia raha kuwa mbali na wewe wamejisikia Amani kukuacha acha waende! Na kama wamejisikia kubaki acha wabaki na wewe usiwalazimishe, kulazimisha watu wawe nawe wakati hawana Amani ya kuwa na wewe kutasababisha uchungu katika maisha yako, kukosa utulivu na majuto, lakini kama utawaacha waende watapata nafasi mpya na kujiamulia mambo yao wenyewe, wape watu uhuru wa kuamua  na Amani ya Mungu itaamua. Na huu ndio ukomavu wa kiroho, kiufahamu na kihekima. Let them go !

Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”

Amini katika kusudi la Mungu kwamba Mungu anaporuhusu watu waende zao na au wabaki na wewe ufahamu kuwa Mungu ana mpango mkubwa na mpya na kila mmoja, inaweza kuwa ngumu kuelewa lakini hatuna budi kuamini katika mpango wa Mungu kwa kuwa Mungu ni mwema, watu wanapoondoka katika maisha yako iwe kwa wema au kwa ubaya bado fahamu ya kuwa Mungu ana mpango mwema kwenu wote yeye huweza kuitumia njia yoyote ile katika kutokeza jambo lililo jema zaidi.

Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”              

Rafiki wa kweli ni yule atakayesimama na wewe hata katika hali ngumu, Petro na wale thenashara walichagua kubaki na Yesu, Petro alisema tuende wapi Bwana wewe una maneno ya uzima wa milele, wako marafiki watakaa na wewe kwa muda mfupi, au watajitokeza kwako katika wakati Fulani maalumu na kisha watakoma lakini marafiki kama Petro kwa Yesu Kristo watamaanisha kubaki na wewe, kwa hiyo ni Muhimu kutambua umuhimu wao na kumshukuru Mungu kwaajili yao. Wakati wote kumbuka kuwa uhusiano wowote ule uwe wa muda au ule wa kudumu una kitu cha kutufundisha katika maisha yetu, hatukutanishwi na watu kwa bahati mbaya, Mungu hakumuumba mwanadamu awe peke yake, tunahitajiana, Lakini Mungu huruhusu watu waje na kuondoka katika maisha yetu kwa kusudi maalumu,  jambo kubwa na la msingi ni sisi kuendelea kuwa waaminifu katika kila aina ya uhusiano ambao Mungu ametupa kumbuka mahusiano yanapovunjika inaleta maumivu makali sana lakini wale wanaoondoka waache waende na wale wanaobaki kaa nao kumbuka kuwa ni Mungu ndiye anayewashika mkono na kuwaleta kwetu kwa hiyo amini katika mchakato huo na utakubali ukweli huu mchungu katika maisha, wafurahie sana wale wote ambao Mungu anawaleta katika maisha yako ukijua kuwa ni sehemu ya mpango wa Mungu,  wakubali wale wote ambao Mungu ameruhusu waende zao mbali na wewe ukijua pia kuwa Mungu ana mpango mwema, thamini umuhimu na msingi wa marafiki  hususani wale wanaobaki kuwa waaminifu kwako hasa wakati wa majaribu na wakati wa mambo magumu, waheshimu wote wapende wakubali lakini usilazimishe mtu akupende au awe na wewe hii haimaanishi uwatendee watu kikatili hapana lakini jifunze kuwa kama Yesu, Yesu aliwahoji hata wale waliobaki je ninyi nanyi mwataka kuondoka?  

Hatima yako haiko mikononi mwa waliokuacha, wala Mungu haitaji lolote uliloliacha au chochote ulichopoteza kupitia marafiki walioondoka, jambo kubwa la msingi uwe na Amani lakini usilazimishe watu wakupende na kukubali au wakuamini, ukiona wamekuacha maana yake huwahitaji tena, wao sio sehemu ya mpango wa Mungu katika maisha yako tena na Mungu ana mpango mwema na wewe na hata wale wanaokusema vibaya waache waseme, mimi nimewahi kusikia habari za mtu anayenisema vibaya na nikaonyeshwa sijawahi kumkataza wala kumbeleza aniseme vizuri, ninajua tu kuwa Mungu ameruhusu wawepo watu watakaonisema vizuri na wawepo watu watakaonisema vibaya wote wana faida katika mapenzi ya Mungu, wanaonisema vibaya wananisaidia nisiwe na kiburi, nikumbuke kuwa mimi ni mwanadamu na nizidi kunyenyekea na wale wanaofaidika na huduma yangu watamshukuru Mungu kwaajili yangu, sina muda wa kumbembeleza mtu asiniseme vibaya, siumii tena na wanaosema vibaya wala siwezi kutukuka watu wakinisifu, ninanyenyekea kwa Mungu kwa sababu mimi ni udongo tu, sikuja duniani kusifiwa, nimekuja duniani kutimiza kile ambacho Mungu amekikusudia katika maisha yangu na hivyo kile nitapangiwa na Mungu kukifanya nitakifanya, Petro alitambua ya kuwa Yesu ana maneno ya uzima wa milele, na ya kuwa ni Mtakatifu wa Mungu yaani ni Masihi.

Bwana ampe neema kila moja wetu kuelewa makusudi ya somo hili kwa kina na mapana na marefu katika jina la Yesu Amen!

 

Na. Rev Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!