Kutoka 14:5-8 “Mfalme wa Misri aliambiwa ya
kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake,
iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili
tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandalia
gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa magari mia sita
yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya magari hayo yote.
Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata
wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.”
Utangulizi:
Leo tutachukua Muda kutafakari
kwa kusudi la kujifunza na kupandisha imani zetu kwanini maandiko yanasema
Israel walitioka Misri kwa ujeuri? Jambo ambalo lilimfanya Farao kubadili
mawazo na kuamua kuwafuatilia wana wa Israel baada ya kikao cha Dharula cha
baraza la mawaziri na majeshi yake, kujadili kuwa imekuwaje wakawaachia Israel
waende zao? Na wasiwatutumikie tena? Uchumi wao utasimamaje bila watumwa? Kazi
zote ngumu za uzalishaji mali zitafanywa na nani? Kwanini tunawaachia watumwa waende
kwa uhuru hata bila kupigana nao? Au kutumia nguvu kuwarejesha? Baada ya hoja
nzito mswada ulipitishwa kuwa ni lazima watu hao warejeshwe utumwani vinginevyo
tutapata hasara kubwa sana!
Kutoka 14:5-10 “Mfalme wa Misri aliambiwa
ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi
wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili
tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandalia
gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa magari mia sita
yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya magari hayo yote.
Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata
wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.Wamisri
wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye
kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na
bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. Hata Farao alipokaribia,
wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao;
wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia BWANA.”
Leo tunapojifunza somo hili Roho
Mtakatifu ananiambia kuwa kuna watu watatoka kwa jeuri, wataondoka katika
mateso yao kwa mkono ulionyooshwa wa Bwana, watafunguliwa vifungo vyao kwa
nguvu na uweza wa Mungu wetu, watakombolewa kutoka katika mateso yao na maumivu yao na majonzi yao, na utumwa wa kila
aina unaoyazinga maisha yao, na kila kitu chenye kusononesha maisha yako leo kitakuwa
ndio mwisho wa utawala wake katika maisha yako nawe utaenda zako kwa jeuri,
Nasema leo utatoka kwa ujeuri katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye
hai haleluyaaa! Tutajifunza somo hili kutoka Misri kwa ujeuri kwa kuzingatia
vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya kutoka kwa jeuri
·
Nani ni sababu ya Jeuri yetu
·
Kutoka Misri kwa ujeuri
Maana ya kutoka kwa jeuri
Kutoka 14:8 “Na BWANA akaufanya moyo wake
Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu
wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.”
Katika kifungu hiki cha maandiko
tunajifunza namna na jinsi Mungu alivyoingilia kati swala zima la mateso ya
watu wake waliokuwa wanateseka kule Misri, Mungu alikuwa amechoshwa na utawala
katili wa Farao, asiyekuwa na shukurani ambaye aliwatumia watumishi wake na
wasimamizi wake kuwatesa wana wa Israel na kuwaletea msiba mkubwa na mateso
makubwa kiasi ambacho waliugua na kumlilia Mungu.
Kutoka 3:7-9 “BWANA akasema, Hakika
nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa
sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili
niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema,
kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na
Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa
Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.”
Wote tunakumbuka namna Mungu
alivyotekeleza mpango wake ambao mara kwa mara ulikuwa ukikataliwa na Farao
vilevile kwa jeuri aliyokuwa nayo, akigoma kabisa kuwaachia wana wa Israel na
kuwaongezea machungu na mateso makali zaidi huku akijaa kiburi na kujifanya
hamtambui Bwana na kuwa watu hao wana kauli za uongo na ni wavivu hivyo
akawakazia kazi ngumu zaidi.
Kutoka 5:1-9 “Hata baadaye, Musa na Haruni
wakaenda wakamwambia Farao, wakasema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Wape
watu wangu ruhusa waende, ili kunifanyia sikukuu jangwani.Farao akasema, BWANA
ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi
simjui BWANA, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao. Wakasema, Mungu wa
Waebrania amekutana nasi; twakuomba, tupe ruhusa twende safari ya siku tatu
jangwani, tumtolee dhabihu BWANA, Mungu wetu; asije akatupiga kwa tauni, au kwa
upanga. Mfalme wa Misri akawaambia Enyi Musa na Haruni, mbona mnawaachisha watu
kazi zao? Enendeni zenu kwa mizigo yenu.Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa
nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao. Na siku ile ile
Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema, Msiwape watu
tena majani ya kufanyia matofali, kama mlivyofanya tangu hapo; na waende
wakatafute majani wenyewe. Lakini hesabu ya matofali waliyokuwa wakifanya tokea
hapo, wawekeeni iyo hiyo, msiipunguze hata kidogo, kwa maana ni wavivu hao; kwa
hiyo wanapiga kelele, wakisema, Tupe ruhusa twende kumtolea Mungu wetu
dhabihu.Wapeni watu hao kazi nzito zaidi, waitaabikie; wala wasiangalie maneno ya
uongo.”
Jambo hili liliwapa uchungu wana
wa Israel zaidi, hali yao wakati wanadai uhuru wa ruhusa ilibadilika kuwa mbaya
na chungu zaidi, Jambo lilopelekea sasa Mungu kuanza kumuadhibu Farao kwa
mapigo mazito sana huku akiwapendelea wana wa Israel ambao walianza kupata
faraja kwa kutokuguswa na mapigo mazito, mapigo yaliyendelea mpaka lilipofika
pigo la kumi ambalo lilisababisha msiba mkubwa kuanzia kwa Farao mpaka kwa
wanyama wao na watumwa wao wote kila mahali walifiwa na mzaliwa wa kwanza jambo
lililopelekea kutoa ruhusa ya haraka haraka ili wana wa Israel waende zao
wakamuabudu Mungu kwa uhuru na pasipo hofu! Mungu mwenye nguvu YHWH alijionyesha uwezo wake na
kumtiisha mfalme mwenye kiburi awaachie watu wake ambao kimsingi nao waliondoka
kwa mikogo sana waliondoka kwa furaha na walindoka Misri kwa ujeuri ni nini
maana ya wana wa Israel kuondoka kwa Jeuri ambacho kimsingi kilimfanya Farao
abadilishe maamuzi? Hilo ndilo jambo la msingi ambalo tunataka kujifunza kwa
kila leo ili nasi tutoke kwa ujeuri katiika kila Nyanja ambayo ibilisi ameweka
mkono wake! tuchunguze andiko hilo kwa kina tena !
Kutoka 14:8 “Na BWANA akaufanya moyo wake
Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu
wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.”
Farao aliwafuta tena wana wa
Israel kwa kiburi kwa sababu wana wa Israel walitoka kwa ujeuri ni nini hasa
maana ya ujeuri unaozungumzwa hapo, kimsingi neno la kiebrania linalotumika
hapo ni “Rûm”
ambalo kimatamshi linatamkwa room neno
hili lina maana pana zaidi kama nitakavyokuonyesha kwanza tafasiri nyingine za
matoleo ya biblia ya kiingereza ili uweze kubaini misamiati tofauti tofauti
upate kufaidika na maana halisi ya neno hilo:-
-
King
James Version (KJV) – and the Lord hardened the
heart of Pharaoh king of Egypt, and he pursued after the children of Israel,
and the Children of Israel went out with and high hand
-
English
Standard version (ESV) - and the Lord hardened the
heart of Pharaoh King of Egypt, and he pursued after the people of Israel while
the people of Israel were going out defiantly.
-
The
Message Bible (MSG) – God made pharaoh king of
Egypt stubborn, determined to chase the Israelites as they walked out on him even without looking Back.
-
God’s
word translation (GW) – the Lord made pharaoh (the
king of Egypt) stubborn that he pursued the Israelites, who were boldly leaving Egypt.
-
Holman
Christian Standard Bible (CSB) – The Lord hardened
the heart of Pharaoh king of Egypt and he pursued the Israelites, who were
going triumphantly.
Sikutaka kutumia matoleo mengine
ambayo kimsingi yanaweza kuwa yamerudia neno mojawapo kama haya yaliyotumika
hapo juu, hivyo nimechagua matoleo ambayo yametumia misamiati mbali mbali
tofauti ili tuweze kujifunza kwa upana
1.
High
– hand – Mkono ulionyooshwa, kwa nguvu kwa mamlaka, bila kujali hisia zao
2.
Defiantly.
– Kwa lazima, kwa kuasi, bila kumtii au kumsikiliza Farao tena
3.
even
without looking Back – Bila kutazama nyuma, moja kwa moja bila kujali wala
kuhuzunikak
4.
boldly
leaving – Kwa ujasiri, Bila kuogopa, bila hofu, ukijua uendako,
5.
triumphantly
– Kwa shangwe, kwa furaha, kwa ushindi wa kufikia malengo
Rûm – Kwa ujeuri sasa maana
yake kwa mkono wa Bwana ulionyooshwa, Kwa nguvu na mamlaka ya Mungu, wakati wao
wanaomboleza kwa misiba, Israel anasonga mbele, Kwa lazima, kwa kuasi amri ya Farao,
bila matakwa yake, bila kumsikiliza, bila kumtii, kwa kuinuliwa juu
kulikopitiliza, bila kutazama nyuma, wala mpango wa kurejea tena, moja kwa moja
bila kujali ya nyuma, kwa ujasiri, bila woga wowote, wakiwa wanajua kule
wanakokwenda, sio kwa kubahatisha, kwa furaha na shangwe kwa mikogo, wakiwa na
ushindi wa kufikia malengo, wakijivunia walioinuliwa sana, kwa uchangamfu sio
kwa machozi. Kwa hiyo wana wa Israel kwao ilikuwa ni siku ya furaha kubwa sana
kila mmoja ilikuwa ni shauku yake kuwa ni lini Bwana atakuja kuwatoa watoke
katika hali waliyokuwa wakiipitia, walikuwa wamechoshwa na walikuwa sasa imani
zao zimepanda sana, Israel walitoka si kwa jeuri yao bali walikuwa wamejaa
matumaini, wametiwa nguvu, hawana hofu ya kurejea nyuma, Imani yao ilikuwa
imepanda sana saababu kubwa ikiwa ni Mungu wao na namna alivyojifunua kwao kwa
mkono wake uliohodari, mkono wa Bwana ulioonyooshwa, Bila hofu kwa ujasiri na
kwa kujiamini.
Waebrania 11:27-29 “Kwa imani akatoka
Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye
asiyeonekana. Kwa imani akaifanya Pasaka, na kule kunyunyiza damu, ili yule
mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wao.Kwa imani wakapita kati ya
Bahari ya Shamu, kama katika nchi kavu; Wamisri walipojaribu kufanya vivyo
wakatoswa.”
Nani ni sababu ya Jeuri yetu.
Israel walitoka kwa nguvu, kwa
mamlaka na uthabiti mwingi kama tulivyojifunza hapo juu, sababu kubwa ya ujeuri
huu haikuwa jeuri ya kibinadamu bali walikuwa wamejifunza jinsi Mungu alivyo
mwema katika njia zake, kadiri alivyojifunua kwao kwa mapigo yale yote kumi,
kila pigo lilikuwa ni shuhuda ya kuwa wanaye mtetezi ambaye hakuna anayeweza
kupambana naye, ujeuri huu ulikuwa unatokana na nguvu alizonazo Mungu, Mungu
wetu miujiza waliyokuwa wameiona ilikuwa imewapa imani thabiti kuwa wanaye Mkombozi,
na hivyo hawakua na mashaka naye.
Wamisri pamoja na mfalme wao
jeuri waliwasisitiza Israel kundoka maana hali yao ilikuwa mbaya na hawakujua
kama watasalimika waliona kuwa wameisha wote hivyo waliwataka waondoke haraka
Kutoka 12:29-33 “Hata ikawa, usiku wa
manane BWANA akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, tangu
mzaliwa wa kwanza wa Farao aliyeketi katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa
wa kwanza wa mtu aliyefungwa katika nyumba ya wafungwa; na wazaliwa wa kwanza
wote wa wanyama. Farao akaondoka usiku, yeye na watumishi wake wote, na Wamisri
wote; pakawa na kilio kikuu katika Misri; maana hapakuwa na nyumba hata moja
asimokufa mtu. Akawaita Musa na Haruni usiku, akasema, Ondokeni tokeni katika
watu wangu, ninyi na wana wa Israeli; enendeni, kamtumikieni BWANA kama
mlivyosema.Twaeni kondoo zenu na ng'ombe zenu kama mlivyosema, enendeni zenu,
mkanibariki mimi pia.Wamisri nao wakawahimiza watu, kuwatoa katika nchi kwa
haraka, maana walisema, Tumekwisha kufa sote.”
Mungu alikuwa pamoja nao na wala
hakuwaacha wakati wa mchana wala wakati wa usiku, hii iliwapa ujasiri mkubwa sana,
Mungu aliwashughulikia vikali maadui wa Israel na alionekana wazi kwa nguzo ya
wingu wakati wa mchana na alionekana wazi kwa nguzo ya moto wakati wa usiku na
ni yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa akiwaongoza njia, Jambo hili liliwapa ujasiri
mkubwa sana.
Kutoka 13:21-22. “BWANA naye akawatangulia
mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya
moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; ile
nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku,
mbele ya hao watu.”
Hakuna jambo linatupa kiburi kama
kujua ya kuwa Bwana yuko pamoja nasi, hakuna jambo linatupa ujasiri kama kujua
Neno la Mungu linasema nini juu yetu, hakuna kitu kinatupa kujiamini kama kujua
kuwa BWANA ni siri ya wokovu wetu, nuru yetu na ngao yetu, na ulinzi wetu, BWANA
ni kila kitu kwetu hakuna jambo linatupa nguvu na mamlaka kama kujua ya kuwa Bwana
anatupenda sana, na kuwa yuko upande wetu, hakuna jambo linatupa matumaini kama
kujua ya kuwa Mungu ni mtetezi wetu na ya kuwa yuko hai, na yuko pamoja nasi
kututetea na kutulinda na kutufunika !
Zaburi 27:1-3 “Bwana ni nuru yangu na
wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?
Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu,
Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu
hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”
Ayubu 19:25-27 “Lakini mimi najua ya kuwa
Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya
ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu;
Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine.
Mtima wangu unazimia ndani yangu.”
Warumi 8:33-39 “Ni nani atakayewashitaki
wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia
adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika
wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani
atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au
uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako
tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini
katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.
Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala
malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye
uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote
hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Israel walipata Jeuri kwa sababu
walijua kuwa Mungu ni Mungu anayesimamia neno lake, na agano lake akitamka kitu
ni sheria, lazima kiwe, Mungu wetu ni mwaminifu na hatatuacha, wala
hatatuangusha, andiko linasema na kila amwaminiye hatatahayari kamwe. Kama ni
hivyo kwanini shetani asituone tuna jeuri, kwanini wapinzani wako wasikuone una
jeuri? Kwanini wqasikuone una mikogo kwa sababu Bwana ndiye sababu yetu
Kutoka Misri kwa ujeuri
Neno la Mungu linatukumbusha ya
kuwa Mungu ni mwaminifu katika kazi yake ya ukombozi, na kuwa yeye yuko tayari
kumtoa kila mmoja katika hali yake ya utumwa, na kutupa ujasiri wa kusonga
mbele, wala tusiwe na mashaka naye, kila changamoto unayokutana nayo na
inayokutumikisha inataka kukuweka utumwani, na haitaki kukuachia kwa haraka kwa
sababu inataka uwe mtumwa wa hali hiyo jambo kubwa la Msingi ni kukumbuka kuwa
leo ni siku yako ya kutoka Misri kwa ujeuri, una shuhuda nyingi za jinsi Bwana
alivyoyapigania maisha yako na ya wengine
kwa hiyo hauna sababu ya kuogopa au kulia na kuomboleza hata adui akijaribu
kukufuata tena anachokitafuta kitampata, Farao alipojaribu kuwafuatia Israel
kwa sababu walitoka kwa jeuri maandiko yanasema alifutiliwa mbali yeye na
majeshi yake yote, katika biblia ya kiingereza inaonekana vizuri zaidi kuwa Farao
pia alifutiliwa mbali kabisa na majeshi yake yote na hakubakia hai ona
Zaburi 136:13-15 “Yeye aliyeigawa Bahari ya
Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akawavusha Israeli katikati yake;
Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akamwangusha Farao na jeshi lake katika
Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.”
Psalm 136:13-15 “to him who divided the Red
Sea asunder His love endures forever. And brought Israel through the midst of
it, His love endure forever, BUT SWEPT Pharaoh
and his army into the Red Sea; His love endure forever”
Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Majeshi
ya wamisri yalifutwa yote sawasawa na neno la Musa mtumishi wa Mungu hapo
aliposema hawa mnaowaona leo hamtawaona tena milele, Mwandishi maarufu wa
Historia ya wayahudi aitwaye Flavius
Josephus alisema kuhusiana na tukio hili nanukuu “And thus did all these men perish, so that there was not one man left
to be a messenger of this calamity to the rest of the Egyptians” kwa
tafasiri yangu “Na wote wakaangamia hata
kusiwepo hata mjumbe wa kuelezea yaliyowakuta wamisri” leo nataka utoke kwa
ujasiri katika kila kifungo kinachokuonea, leo nataka kifungo kinachokuonea na
kukandamiza kiwe mwisho, na usikione tena leo nataka utoke katika Misri inchi
yako ya utumwa kwa ujeuri, utoke nje ya uonevu wa mashetani, nje ya magonjwa,
nje ya huzuni, nje ya kila kinachopoteza tumaini la maisha yako, Nje ya utasa
wako, nje ya kansa, nje ya tezi dume, nje ya magonjwa ya kizee, nje ya
umasikini, nje ya uonevu wa wachawi, nje ya vifungo vya nguvu za giza, nje ya
mashambulizi na uonevu wa ibilisi, leo nakutangazia kwa mamlaka niliyopepewa
kama mtumishi wake kwa mafuta aliyonipaka kwayo nasema Toka kwa imani ukimtegema Mungu na kufahamu
ya kuwa hatakuangusha, mtegemee yeye katika maamuzi makubwa ya maisha, uwe na
ujasiri unapopita katika dhiki na shida, kabiliana na majaribu yako kwa Imani
ukijua wazi hatimaye Mwokozi atasimama karibu nawe na kukutoa katika hali unayoipitia
na kamwe usitazame nyuma, toka kwa ujeuri mbele kwa mbele usitazame tena jaribu
lako na nakuhakikishia halitakuwepo tena!, Bwana ameniambia kuwa fadhili zake
ni za milele, ikiwa aliwaokoa wana wa Israel wakatoka kwa Jeuri, leo ni zamu
yako kutoka kwa ujeuri katika hali iliyokusumbua kwa miaka mingi, katika jina
la Yesu Kristo pokea, mahitaji yako, pokea uzima wako, pokea ukombozi wako, pokea
uhai wako, nakufungua na kukuweka mbali na mauti katika jina la Yesu Kristo
nakutamkia uzima kwa mamlaka niliyo nayo katika jina la Yesu, pepo achia
wasomaji wangu, achilia wasikilizaji wangu, achilia watu wa Mungu katika jina
la Yesu, Nakutangazia kutoka kwa Jeuri na kumuacha Shetani akijuta na
kusikitika kwa kukuachia na akijaribu kukufuata ataangamia kama Farao katika
jina la Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai! Ramashakatariboso,
saparatashanda, rimosakata free sakata lota fakaseta rimoso pa taratshatata
parafata, katika jina la Yesu Amen!
Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Maoni 1 :
Asante nimepokea kwajina la Yesu amina
Chapisha Maoni