Mathayo 12:3-6 “Akawaambia, Hamkusoma
alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? jinsi alivyoingia katika
nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila
wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati,
kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini
nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu.”
Utangulizi:
Nyakati za agano la kale Hekalu
la Mungu lilichukua nafasi muhimu na kubwa
sana katika maisha ya wanadamu hususani Wayahudi, katika uhusiano wao na Mungu,
Hekalu ilikuwa ni nyumba pekee ambayo ilikuweko Yerusalem ambapo watu wangeweza
kuabudu, kutoa dhabihu na kukutana na Mungu, Lakini katika namna ya kushangaza
sana Yesu Kristo kwa maneno na vitendo alitangaza wazi kuwa yeye ni mkuu kuliko
Hekalu!, Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kwa vipi
Yesu ni mkuu kuliko Hekalu na hii ina maana gani kwa sisi kama wakristo!,Usemi
huu sio tu kuwa una mapinduzi makubwa ya kiibada lakini una kitu cha maana sana
cha kujifunza kuhusu Yesu Kristo, Tutajifunza somo hili Hapa yupo aliyemkuu kuliko Hekalu! Kwa kuzingatia vipengele vitatu
muhimu vifuatavyo:-
·
Umuhimu
wa Hekalu katika jamii ya Wayahudi
·
Hapa yupo
aliyemkuu kuliko Hekalu
·
Mambo ya
msingi ya kujifunza katika kanisa
Umuhimu wa Hekalu katika jamii ya Wayahudi.
Neno Hekalu kwa kiingereza “temple” katika kiibrania linatumika
neno HEKHAL au BAYITH kwa kiyunani HIERON ambalo kimsingi ndio lilikuwa
jina la Jumba la kifahari lililojengwa Pale Yerusalem kwaajili ya Ibada za
Mungu wa Israel. Yako mahekalu
mengine mengi duniani yaliyokuwa yamejengwa kwa miungu mingine, Lakini hekalu
maarufu zaidi lilikuwa hekalu hili la Mungu wa Israel Lililojengwa na Mfalme
Sulemani na hili ndilo tunalolizungumzia kwa kuunganisha na Neno la Yesu
Kristo.
Wote tunafahamu kuwa Hekalu la
Mungu kule Yerusalem lilikuwa ndio kiini kikubwa cha ibada za kiyahudi na
lilishika sehemu kubwa sana ya maisha yao ya kiimani na kitamaduni, kwa
wayahudi hekalu lilikuwa ni zaidi ya jengo la kawaida la kifahari, wao
waliamini na ndivyo ilivyokuwa kwamba ni mahali ambapo Mungu alipachagua ili aweke
jina lake hapo, hivyo palikuwa ni mahali akaapo Mungu pa kidunia, ambapo kwa
mujibu wa torati iliwalazimu waende hapo, kwa kuwa ndipo alipopachagua Bwana
Mungu wa Israel kama ilivyoagizwa mapema katika torati ya Musa.
Kumbukumbu 12:5-6 “Lakini mahali
atakapochagua Bwana, Mungu wenu, katika kabila zenu zote, apaweke jina lake,
maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe wende huko; pelekeni huko
sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya
kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa
wa kwanza wa makundi yenu ya ng'ombe na ya kondoo;”
Tofauti na masinagogi, Hekalu
lilipaswa kuwa moja tu, tena Pale Yerusalem na ndipo mahali ambapo pekee pali ruhusiwa
kutolewa dhabihu za kuteketezwa, kwaajili ya upatanisho wa dhambi, Hapo ndipo
mahali ambapo Mungu alichagua kuwekeza uwepo wake mahali hapo, Palikuwa ni
mahali patakatifu panapounganisha mbingu na inchi.
1Wafalme 8:10-13 “Ikawa, makuhani
walipotoka katika patakatifu, nyumba ya Bwana ikajaa wingu; hata makuhani
hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa
nyumba ya Bwana ilikuwa imejaa utukufu wa Bwana.Ndipo Sulemani akanena, Bwana
alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa,
iwe mahali pa makao yako milele.”
Hekaluni ndipo mahali ambapo
dhabihu za kuteteketezwa na sadaka za upatanisho kwaajili ya dhambi
zilifanyika, wakati ibada hizo zilikuwa haziwezi kufanyika popote wala kwenye
masinagogi, kwa lugha nyingine Israel wasingeliweza kupata msamaha wa dhambi na
kupatanishwa na Mungu pasipo kufanyika kwa ibada hizo hekaluni peke yake, kwa
hiyo hekalu pekee lilikuwa lango la mbingu
Bwana Mungu wa Israel alikuwa
amepakubali mahali pale na kutoa ahadi nyingi sana kuhusu Nyumba ya Bwana kwa
watu wake, alipakubali kama mahali pa dhabihu, alipakubali pawe mahali pa
makimbilio, alipakubali pawe mahali pa kupoza vita, mapigo na matukio yoyote
magumu, na alipakubali pawe mahali ambapo mtu yeyote duniani akiomba lolote
kuelekea hapo Mungu angesikia dua yake na kuponya kwa ujumla ni mahali muhimu
sana kwa wote waliomuhitaji Mungu na wanaomuhitaji Mungu
2Nyakati 7:12-16 “Bwana akamtokea Sulemani
usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa
nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula
nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina
langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao
mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya
nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya
watu waombao mahali hapa. Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili
kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo
wangu daima.”
Kwa hiyo Hekalu lilikuwa ni
sehemu muhimu ya Imani, Dini, tamaduni, utaifa na umoja wa wana wa Israel na
wayahudi wote kutokana na mafundisho yao, kila wakati na kila mwaka zilikuwepo
sikukuu muhimu sana ambazo ziliwakutanisha wayahudi pamoja kama hija
zikiwapeleka Yerusalem na hivyo kuwa alama kubwa sana ya umoja wa kitaifa na
kiimani, kitamaduni na kihistoria na sehemu muhimu ya utambulisho wa Mungu wa
Israel kwa dunia nzima. Kuna maandiko mengi na zaburi nyingi zinazoonyesha umuhimu
mkubwa wa nyumba hii ya Bwana na uweza na nguvu na mamlaka aliyokuwa ameiwekeza
hapo kwa hiyo kwa ujumla:-
1.
Hekalu
lilikuwa ni kiini cha Imani ya wayahudi wa kale na sehemu muhimu kwa ibada ilikuwa ni mahali ambapo watu walilia na
kupakumbuka sana walipokosa uhusiano na mahali hapo au walipokuwa mbali na
mahali hapo
Zaburi 42:2-4 “Nafsi
yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai, Lini nitakapokuja nionekane mbele
za Mungu? Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi
wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako. Nayakumbuka hayo nikiweka
wazi nafsi yangu ndani yangu, Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano, Na
kuwaongoza nyumbani kwa Mungu, Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa
sikukuu.”
Zaburi 137:1-5 “Kando
ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti
iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka
Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo
za Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni? Ee Yerusalemu,
nikikusahau wewe, Mkono wangu wa kuume na usahau.”
Zaburi 122:1-2 “Nalifurahi
waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana. Miguu yetu imesimama Ndani ya
malango yako, Ee Yerusalemu.”
2.
Palikuwa
ni mahali ambapo waliweza kutoa dhabihu, kuondoa au kuweka nadhiri kumuita
Mungu na kupokea fadhili za Mungu
Zaburi 66:13-20 “Nitaingia
nyumbani mwako na kafara; Nitaondoa kwako nadhiri zangu; Ambazo midomo yangu
ilizinena; Kinywa changu kikazisema nilipokuwa taabuni. Kafara za vinono
nitakutolea, Pamoja na fukizo la kondoo waume, Nitatoa ng'ombe pamoja na mbuzi.
Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu, Nami nitayatangaza aliyonitendea
roho yangu. Nalimwita kwa kinywa changu, Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulimi
wangu. Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, Bwana asingesikia. Hakika Mungu
amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu. Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa
maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake.”
3.
Hekalu
palikuwa ni mahali ambapo kila mtu wa Mungu nyakati za agano la kale alipaonea
shauku au alipaonea hamu
Zaburi 23:6 “Hakika
wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani
mwa Bwana milele.”
Zaburi 27:4-5 “Neno
Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa
Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari
hekaluni mwake. Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri
katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba.”
Zaburi 122:1-2 “Nalifurahi
waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana. Miguu yetu imesimama Ndani ya
malango yako, Ee Yerusalemu.”
4.
Palikuwa
ni mahali ambapo Israel walitembelea kila mwaka wakati wa sikukuu akiwepo Bwana
Yesu mwenyewe alipokuwa kijana mdogo, na hii ilikuwa ni kwa mujibu wa maagizo
ya torati ya Musa
Kumbukumbu 16:16-17 “Mara tatu kwa mwaka na watokee wanawaume wako wote mbele
za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa
chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; wala
wasitokee mbele za Bwana mikono mitupu. Kila mtu na atoe kama awezavyo, kwa
kadiri ya baraka ya Bwana, Mungu wako, alivyokupa.”
Matendo 2:5-11 “Na
walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini
ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na
fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si
Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?
Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia,
Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na
wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa
wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.”
Luka 2:41-51 “Basi,
wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na
alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya
sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto
Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao
wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa
wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu,
huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati
ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia
fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake
akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa
tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa
imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo
alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na
mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.”
5.
Palikuwa
ni mahali maalumu kwaajili ya maombi na ibada kwa wayahudi wote kokote waliko
au sehemu maalumu ya muelekeo wa maombi (Prayer direction)
Isaya 56:5-7 “Nitawapa
hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema
kuliko kuwa na wana na binti; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa
mbali. Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la
Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana
agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha
katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya
madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.”
Daniel 6:10 -11 “Hata
Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia
nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa
kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru
mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo. Basi watu hao
wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.”
6.
Palikuwa
ni Mahali ambapo utukufu wa Mungu ulikaa – tangu nyakati za safari ya wana
wa Israel Jangwani uwepo wa Mungu ulishuka katika nyumba ya Bwana iliyokuweko
jangwani iliyojulikana kama Hema la kukutania, kimsingi Hema ya kukutania
lilikuwa ni hekalu la muda linalohamishika na walipofika katika nchi ya kanaani
Hekalu lilijengwa kwa mfano wa ile hema ya kukutania, uwepo huo wa Mungu
ulionekana kwa jinsi ya macho ya kibinadamu kama wingu la utukufu ambalo kwa
kiibrania lilitwa Shekinah
Kutoka 33:9-10 “Ikawa
Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa
ile hema; naye BWANA akasema na Musa. Watu wote wakaiona nguzo ya wingu
ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu
mlangoni pa hema yake.”
Sio hivyo tu
wakati mwingine malaika wa Bwana alijitokeza akijiunganisha na nguzo ile ya
wingu, na malaika huyu wakati mwingine ilionekana wazi kuwa alimuwakilisha
Bwana mwenyewe, na mara nyingi malaika huyu alijitokeza akiwa na mamlaka ya
kiungu na Pengine alikuwa ni Yesu mwenyewe katika agano la kale
Kutoka 14:19 “Kisha
malaika wa Mungu, aliyetangulia mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akaenda
nyuma yao; na ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao, ikasimama nyuma yao;”
Wingu la utukufu
wa Mungu wakati wote lilikuwa linawakilisha uwepo wa Mungu, Na ilikuwa ni
shauku ya Mungu kuwa pamoja na watu wake, na uwepo huu ulijirudia kulikalia
Hekalu lilipokuwa limejengwa na kuwekwa wakfu, aidha wakati mwingine ulionekana
kama moto ulioshuka kutoka mbinguni na hii inaweza kutupa picha pana kuwa uko
uwezekano kuwa kile kijiti alichokiona Musa kinawaka moto lakini hakiteketei
ulikuwa ni uwepo huu wa Mungu na ule uliokaa usoni kwa Musa na kuufanya uso
wake kung’aa
2Nyakati 7:1 “Basi
Sulemani alipokwisha maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza
sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa Bwana ukaijaza nyumba. Wala
makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa Bwana, kwa kuwa utukufu wa Bwana
umeijaza nyumba ya Bwana.”
Kimsingi uwepo
huu wa Mungu uliokuwa ukionekana na kukaa katika hekalu na hema ya kukutania alikuwa
ni Mungu mwenyewe, nahii iko wazi kwa
mujibu wa injili ya Yohana kuwa kumuona Yesu ni kuuona utukufu wa Mungu, Kristo
anatafasiriwa kuwa ndiye mng’ao huo wa utukufu wa Mungu ndiye Shekinah
mwenyewe, ambaye hakalu halina maana bila uwepo wake.
Yohana 1:14 “Naye
Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama
wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”
Waebrania 1:1-3 “Mungu,
ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia
nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa
mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa
utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake,
akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;”
Nyumba hii ya Mungu ilikuwa ni ya
Muhimu sana, na ilijengwa katika mlima wa Moriah mahali ambapo Inasadikiwa kuwa
Ibrahimu alitaka kumtoa Isaka kama sadaka ya kuteketezwa, mahali ambapo Mfalme
Daudi alipanunua lilipokuwa Shamba la Arauna Myebusi, ili aweze kutoa dhabihu
hapo na kumjengea Mungu madhabahu, kihistoria Hekalu lilijengwa mara tatu La
kwanza likiwa limejengwa na Suleimani, na baadaye Zerubabel na mwisho Herode
mkuu alilikarabati na kulijenga kwaajili ya wayahudi na hili ndilo Hekalu
ambalo Yesu alilitumia na baada ya kupoteza umuhimu wake na kuharibiwa ndipo
mahali ambapo sasa inasimama nyumba ya kiislamu iitwayo Masjid Al - Aqsa ambayo iko
chini ya utawala wa Hashemites au Bani Hashem ukoo ambao ni uzao wa
waarabu wanaotokana na ukoo wa Makuresh moja ya kabila za wana wa Ishmel mwana wa Ibrahimu, ambapo ndio ufalme wa
Jordan leo. Yako mambo mengi sana ambayo tungeweza kuzungumza kuhusu hekalu
lakini natamani kumzungumzia Yeye aliye mkuu kuliko Hekalu lenyewe kwa sababu
huyo ni wa Muhimu sana sasa kuliko hekalu halisi lililokuwako Yerusalem kwa
wakati huo.
Hapa yupo aliyemkuu kuliko Hekalu
Wote tunaweza kuona jinsi Hekalu lilivyokuwa
ni nyumba muhimu sana kwa Wayahudi, na sasa Bwana wetu Yesu Kristo anapokuja na
kukiri au kutangaza ya kuwa yeye ni Mkuu kuliko Hekalu maana yake anatamka kitu
kikubwa sana cha kushangaza ambacho hatuna budi kutoa kipaumbele na kuliangalia jambo hili kwa umakini mkubwa kwa
sababu kwa tamko lake maana yake sheria zote na maswala yote ya msingi kuhusu
Hekalu yanapoteza maana zake na mwelekeo mzima unaelekea kwake, wayahudi
walikuwa wakifikiri kuwa hekalu ndilo lililokuwa linabeba uwepo wa Mungu kwa
ukamilifu wake na sasa Yesu anaonyesha ya kuwa Uwepo ule wa Mungu sasa ni yeye
mwenyewe.
1. Hii
ilikuwa na maana ya moja kwa moja kuwa Yesu ni Mungu – Hekalu ilikuwa ni mahali
ambapo Mungu alipachagua kuweka jina lake hapo na uwepo wake ili aweze kuwa
katikati ya watu au ili aweze kutimiza mpango wake wa kukaa pamoja na wanadamu
yaani Mungu pamoja nasi.
Mathayo 1:21-23 “Naye
atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa
watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na
Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa
mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.”
Hekalu lilikuwa
linaufunga uwepo wa Mungu mahali pamoja lakini Yesu alikuwa akiufungua uwepo wa
Mungu kwa ulimwengu mzima, yeye ni uwepo halisi wa Mungu na ndiye neno halisi
la Mungu, watu walikuwa wakienda Hekaluni kumuabudu yeye na sasa kama yeye
mwenyewe yupo maana yake uwepo wa ibada sasa hauna budi kuelekezwa kwake na yeye
ndiye lango la Mbinguni, na ndiye kiini cha ibada na kumtukia yeye ni kuufikia
uwepo wake.
Yohana 1:1-3, 14 “Hapo
mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye
hakikufanyika cho chote kilichofanyika. 14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa
kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa
Baba; amejaa neema na kweli.”
2.
Yesu
alikuwa akijitambulisha kuwa yeye ndio ukamilifu wa sadaka za dhabihu na ndiye
kuhani mkuu halisi – Yesu alikuwa ndio dhabihu halisi na vile vile kuhani
mkuu milele na milele, aliyatoa maisha yake mwenyewe kuwa dhabihu timilifu kwa
ulimwengu na hivyo kukomesha mahitaji ya dhabihu za kawaida za wanyama
zilizokuwa zikitolewa Hekaluni, kwani dhabihu yake yenye maana ingeweza kuwa
dhabihu ya milele itakayofanya upatanisho wa moja kwa moja wa dhambi kwa
wanadamu wote duniani bila kuhitaji hekalu
Waebrania 9:11-14 “Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani
mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi,
isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu
ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika
Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi
na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu
hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba
kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa,
itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?”
Waebrania 10:8-12 “Hapo
juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi
hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo
aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili
kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa
mwili wa Yesu Kristo mara moja tu. Na kila kuhani husimama kila siku akifanya
ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa
dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo
hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu;”
3.
Yesu
ndiye njia ya kufikia uwepo wa Mungu – Wakati hekalu ndio ilikuwa njia ya
kumfikia Mungu, Yesu anaonyesha kuwa yeye ndio njia ya moja kwa moja ya
kuufikia uwepo wa Mungu, kupitia yeye tunaweza kukifikia kiti cha rehema cha
Mungu kwa ujasiri na kupata rehema bila kupitia kokote.
Waebrania 4:14-16 “Basi,
iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na
tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana
nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi
katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa
ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”
Pazia katika
hekalu lilipasuka katikati vipande viwili wakati Yesu anakata roho pale
msalabani hii ilikuwa ikitufundisha wazi kuwa kikwazo kilichokuwa kinamzuia
kila mmoja wetu kumfikia au kuufikia uwepo wa Mungu kimeondolewa na sasa kila
mtu kwa wakati wake na kwa nafsi yake anaweza kumfikia Mungu kwa Imani katika
damu ya Yesu na kukutana na mahitaji yake
Mathayo 27:50-51 “Naye
Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia
la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka;
miamba ikapasuka;”
4.
Yesu
alikuwa akijitambulisha kuwa yeye ndiye mng’ao wa utukufu wa Mungu (Shekinah)
Yohana 1:14 “Naye
Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama
wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”
Waebrania 1:1-3 “Mungu,
ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia
nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa
mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa
utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha
kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;”
5.
Yesu
alikuwa akitukumbusha ya kuwa sisi ndio Hekalu halisi na kuwa yeye anakaa ndani
yetu – Waandishi wa nyakati za karne ya kwanza nyakati za kanisa,
waliendelea kutumia lugha ya hekalu si kwa kumaanisha jengo tena na badala yake
walianza kumaanisha kuwa hekalu ni watu wa Mungu kila mtu aliyeokolewa ni kipande cha tofali katika hekalu hilo, ni
sehemu ya kiungo katika mwili wa Kristo.
1Wakorintho 6:19-20 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu
aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana
mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu”
Badala ya watu
kwenda kuutafuta uwepo wa Mungu kule Yerusalem lilikokuweko Hekalu, sisi kama
hekalu la Mungu sasa tunapaswa kuubeba uwepo wa Mungu na kuupeleka duniani kote
pale tulipo mpaka Yesu arudipo.
Mambo ya msingi ya kujifunza katika kanisa.
1.
Kumuabudu
Mungu katika roho na kweli – Ibada ya kweli haiitaji tena mahali Fulani pa
ibada, hapa sisemi watu waache kwenda Kanisani, lakini namaanisha kuwa
hatuhitaji tena kwenda hija Yerusalem kwaajili ya ibada kwani Mungu ni Roho na
anapatikana kokote, kwa hiyo kila mtu anapaswa kuufungua moyo wake na kuuelekeza
kwa Yesu kwaajili ya kumuabudu, kumuomba na kupeleka mahitaji yetu, aidha
huitaji kweda milimani ingawa hakuna anayekuzuia kwenda huko kwaajili ya
kutafuta utulivu na kuutafuta uso wa Mungu lakini ni lazima uelewe kuwa Mungu
anapatikana popote pale na yuko karibu
na yeyote yule maadamu tu utauelekeza uso wako kwake.
Yohana 4:23-24 “Lakini
saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho
na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo
yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”
2.
Kuzingatia
umoja – Hekalu lilikuwa likiwaunganisha wayahudi wote duniani, kumkumbuka
Mungu wao, tamaduni zao na utaifa wao na kuwakumbusha kuwa wao ni kitu kimoja,
sisi nasi kupitia Yesu Kristo kama Kanisa tunapaswa kuelewa kuwa sisi ni kitu
kimoja
Wagalatia 3:26-28 “Kwa
kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.
Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala
Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi
nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.”
3.
Hakuna
mauti tena hekaluni – Mara kadhaa tumesoma katika maandiko ya agano la kale
kuwa wako watu ambao walikufa au walifia hekaluni kwa sababu ya kukiuka maswala
mbalimbali na kanuni mbalimbali za hekaluni, Lakini Yesu anatangaza sasa kuwa
kama jinsi ambavyo Daudi na wenzake, waliweza kula mikate ya wonyesho bila kufa
(Kwa Sababu Daudi alikuwa na Yesu viunoni mwake) hali kadhalika kila amwendeaye
Yesu tatapata uzima na uzima wa milele na hakuna mauti kwa mtu amwaminiye Yesu
ambaye ni mkuu kuliko Hekalu
Mathayo 12:3-6 “Akawaambia,
Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? jinsi
alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si
halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala
hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi
sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko
hekalu.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima.