Ufunuo 3:7-8 “Na kwa malaika wa kanisa
lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa
kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye,
naye afunga wala hapana afunguaye. Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa
mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo
nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
maisha yetu kama wanadamu ziko nyakati ambazo tunaweza kujikuta katika dimbwi
la mawazo na hali ya kutokufahamu kutokana na mambo kadhaa katika maisha yetu
kutokuenenda kama tunavyotaka au kufikiri,
na mara nyingine tumejikuta hatuelewi au kuwa kama watu waendao gizani
kwa kupapasa kwa sababu tu ya kutokuyajua mapenzi ya Mungu katika maisha yetu,
tunaweza kudhani kuwa labda tuko katika maisha yaliyopoteza mwelekeo, au
yaliyopoteza tumaini, na kukosa msaada ya kiungu au hata wa kibinadamu wakati
mwingine unaweza kuwaza hata kufikiri kuwa labda una laana, au kuna mtu
amekuroga kwa sababu tu huoni mwelekeo wa hatima ile unayoitamani katika maisha
yako huu ni ule wakati ambapo tumekwama na kila mlango wa mpenyo tuliojaribu
katika maisha yetu unaonekana kama umefungwa au umepata kile ambacho hakilingani
na akili yako au mtazamo wako au kile ulichokitarajia! Mlango umefungwa!
Unaweza kufikiria kuwa umekataliwa kila mahali na ukadhania kuwa hustahili na
ni kama Mungu hausiki na maisha yako tena lakini Mungu anajua uliposimama na
ameahidi kufanya kitu kwako!
Isaya 22:19-22 “Nami nitakusukuma na
kukutoa katika mahali pako, naye atakushusha utoke hapa usimamapo. Na itakuwa
katika siku ile nitamwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia; nami
nitamvika vazi lako, nitamtia nguvu kwa mshipi wako, nami nitamkabidhi yeye
mamlaka yako; naye atakuwa baba kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa nyumba ya
Yuda. Na ufunguo wa nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala
hapana atakayefunga; naye atafunga wala hapana atakayefungua.”
Leo tutachukua muda kutafakari
mambo haya yanayotokeza katika maisha yetu kwa kuliangalia neno la Mungu
linasema nini pale tunapohisi kuwa labda mlango huu umefunga, labda jaribu hili
halitatoka, na pale unapohisi umekwama, leo tutajikumbusha kuwa neno la Mungu
linaonyesha wazi kuwa hakuna mwanadamu anaweza kukufunga wala mchawi anayeweza
kuzuia Baraka zako kwa sababu tunaye Mungu mwenye mamlaka ya kufunga na
kufungua milango na hakuna mtu anayeweza kufunga alichokifungulia wala hakuna
anayeweza kufungua alichokifunga, Yeye ndiye anayesema leo Tazama nimekupa mlango uliofunguliwa! Na tutajifunza somo hili kwa
kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya
mlango uliofunguliwa.
·
Tazama nimekupa
mlango uliofunguliwa.
·
Na huyu
ndiye mwenye mamlaka ya milango yote.
Maana ya mlango uliofunguliwa.
Kwa kawaida neno mlango
uliofunguliwa katika maandiko una maana
pana sana neno uliofunguliwa katika lugha ya kiebrania linatumika neno “Pāthah” na neno lingine la kiebrania ni “Gālāh” kwa kiyunani “Anoigō” Kwa hiyo neno Mlango
uliofunguliwa kwa kiyunani linasomeka “Anoigō
thura” neno hili lilitumika kumaanisha kupata mpenyo, kufunguliwa macho,
kufunguliwa kinywa, kufunguliwa masikio, kufunguliwa mlango, kupewa macho ya
kuona, kufunguliwa mbingu, kuwekewa wazi, kupata nafasi, kutoka, na kupata
muelekeo, kwa sababu hiyo Mlango katika lugha ya kiroho unawakilisha Nafasi
maalumu anayoitoa Mungu kwa mwanadamu kwaajili ya huduma, kusonga mbele, kutoka
katika changamoto inayokukabili katika maisha kwa msaada wa Mungu na anayesababisha milango hiyo ifunguke ni
Mungu mwenyewe na hufanya hivyo kwa watu wake ambao pia ni kondoo wa malisho
yake! Yesu alikwisha kutangaza kuwa yeye ndio mlango wa kondoo, awaye yote ambaye
anataka upenvyo wa aina yoyote katika maisha yake hawezi kutoka bila kupitia
Yesu!
Yohana
10:7-10 “Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin,
nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na
wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa
mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji ila aibe
na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.”
Kwa msingi huu katika maisha yetu
tunapoona kuwa kuna mambo hayaendi katika maisha yetu ya kila siku hatupaswi
kuzimia moyo kwa sababu uko mlango
uliofunguliwa kwaajili yetu na yuko mwenye mamlaka ya kufunga na kufungua,
hakuna mtu awaye yote anayeweza kuzuia usiolewe, hakuna mtu anayeweza kuzuia
usifanikiwe, hakuna mtu anayeweza kuzuia usizae, hakuna mtu anayeweza kuzuia
usipate kazi, hakuna mtu anayeweza kuzuia usifanikiwe, hakuna mtu anayeweza
kuzuia usipone, hakuna mtu anayeweza
kuzuia usijenge hakuna mtu anayeweza kuzuia usiendelee mbele, hakuna anayeweza
kuzuia usifaulu! Mungu wetu sio binadamu, hakuna mnyanyasaji asiyekuwa na
mwisho, hakuna adui asiyekuwa na mwisho, hakuna hali ngumu isiyokuwa na mwisho
kwa sababu uko mlango uliofunguliwa kwaajili yako, Mungu amekupa mlango
uliofunguliwa wengine wanaweza kuona giza lakini sivyo itakavyokuwa kwako wewe
na mimi wewe na mimi neno la Mungu linatuambia kuwa tunao mlango ulio wazi
nguvu ya mafanikio iko kwetu na Mungu anayeweza kutufanikisha yuko kwetu na yeye
ndio mlango wenyewe!
Tazama nimekupa mlango uliofunguliwa
Ni muhimu kuelewa kuwa wakati
tunapopitia changamoto na majaribu mbalimbali moja ya kazi kubwa anayoifanya
Shetani au adui ni kutufanya tusione njia, yaani ni kutupofusha tusipate ufunuo
wa mapenzi na makusudi ya Mungu na hii ndio inayotufanya tufadhaike na
kuvunjika moyo au kukata tamaa kwa sababu ya hali unayoipita kwa wakati ule,
lakini Neno la Mungu linasema kuwa kwa kila jaribu uko mlango wa kutokea, na
Mungu amekupa mlango uliofunguliwa!
2Wakorintho 4:3-4 “Lakini ikiwa injili yetu
imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii
amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake
Kristo aliye sura yake Mungu.”
1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata
ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye
hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na
mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”
Ufunuo 3:7-8 “Na kwa malaika wa kanisa
lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa
kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye,
naye afunga wala hapana afunguaye. Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa
mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo
nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”
Mungu ametupa mlango
uliofunguliwa, hakuna mtu wa Mungu ambaye anaweza kukwama milele, Mungu anapofunga
mlango mmoja huwa anafungua mlango mwingine, kila mwanadamu anayejitahidi
kukuzibia ataula wa chuya kwa uvivu wa kuchambua, hajui nguvu na uweza wa Mungu
wetu sisi tunao ufunguo wa Daudi, kila mahali palipofungwa tutatoboa tu, ni
lazima ufahamu ya kuwa wakati mwingine unapoona mambo yanakwama sio lazima iwe
umerogwa wewe haurogeki sio lazima uwe una laana wewe haulaniki, lakini wakati
mwingine ni sauti ya Mungu inafunga mlango mmoja ili kufungua mwingine, na
ukisikiliza katika ulimwengu wa roho kwa makini mlango uko wazi kwako na
kwaajili yako!
Matendo 16:6-10 “Wakapita katika nchi ya
Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika
Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu
hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono
usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje
Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka
kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri
Habari Njema.”
-
Walimfanyia fitini Yusufu, walimtupa shimoni,
walimuuza utumwani Misri, walimfitini tena na alitupwa gerezani, badala ya mema
ilionekana kana kwamba mambo yanamuendea vibaya lakini katika mpango wa Mungu, Mungu
alikuwa anatengeneza mlango uliofunguliwa wa kumuweka Yusufu katika ufalme
Mwanzo 41:40-44 “Basi
wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa.
Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe. Farao akamwambia Yusufu,
Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akavua pete yake ya muhuri
mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na
kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake. Akampandisha katika gari lake la pili
alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo
akamweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na
bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri.”
-
Walimdharau Daudi na kufikiri ya kuwa hafai
kabisa kuwa miongoni mwa watoto anayeweza kuwa mfalme na kupakwa mafuta,
alipigwa vita kila mahali, hakukubaliwa na baba wala hakukubaliwa na kaka zake,
na mfalme aliyekuwepo madarakani alimkataa na kutaka kumuua, alimwinda katika
mapango na kujaribu kwa kila jinsi na kila namna kumzuia asiwe mfalme, njia
ilionekana kuwa ngumu milango ilionekana kufunga lakini Mungu alikuwa na
sababu, hatimaye Yeye akawa ndiye mtu sahihi aliyeupendeza Moyo wa Mungu na
aliyewaongoza Israel kwa ukamilifu wa moyo, Mungu alimpa Daudi mlango
uliofunguliwa!
Zaburi 78:70-72 “Akamchagua
Daudi, mtumishi wake, Akamwondoa katika mazizi ya kondoo. Nyuma ya kondoo
wanyonyeshao alimwondoa, Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake.
Akawalisha kwa ukamilifu wa moyo wake, Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake.”
-
Walimfukuza Hajiri na Ishamel na kuwatupilia
jangwani, waliishiwa na mkate na waliishiwa na maji na hatari ya kifo ilikuwa
ikiwakabili, Hajiri alilia na Ishamel alilia Lakini Mungu ni Mungu ambaye
hakuwa na upendeleo aliwafungulia mlango wa uhai hata walipokuwa wametaka tamaa
jangwani Mungu alijidhihirisha kuwa ni Mungu mwenye kujali ni Mungu mwenye
upendo, ni Mungu asiye na upendeleo, Ni Mungu anayebariki na ni Mungu mwenye
kukuza sana aliahidi kumfanya Ishamel kuwa Taifa kubwa hakuna upendeleo kwa
Mungu!
Mwanzo 21:10-21 “Kwa
hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa
mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana
machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili
lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila
akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye
mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. Ibrahimu
akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri
akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika
jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini
ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa
mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza
sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita
Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu
amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike
mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho,
naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana.
Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa
mpiga upinde. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika
nchi ya Misri.”
Ndugu yangu Mungu ametupa mlango
uliofunguka, haijalishi sasa unapitia hali ya namna gani, au umesimama katika
hali inayoonekana kuwa ni ngumu na kama kila kitu hakionekani kuwa sawasawa
huna sababu ya kulalamika wala kunung’unika
Mungu anaweza kukufungulia mlango wa afya yako, masomo yako, visa yako,
safari yako, biashara zako, cheo chako, mshahara wako kuongezeka, mapato yako
kuchanua, kilimo na biashara kufanikiwa, walikuwa wakifukia visima vya Isaka
lakini aliendelea kuchimba vingine hakuna mtu anaweza kukufungia mlango, njia
za Mungu sio kama njia za wanadamu wala mawazo yake sio kama mawazo yetu yeye
huweza kufanya njia pasipo na njia leo Mungu amenituma nikukumbushe ya kuwa uko
mlango uliofunguliwa kwaajili yako, ndoa yako njema inakuhusu, mchumba anakuja
na yule aliyeondoka haikuwa mpango wa Mungu Mungu atakufungulia mlango
mwingine, kazi iliyopotea haikuwa mahali pako sahihi Mungu amekupa mlango ulio
wazi Mungu amekupa mlango uliofunguliwa na hakuna awezaye kuufunga.
Na huyu ndiye mwenye mamlaka ya milango yote
Ufunuo 3:7 “Na kwa malaika wa kanisa
lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa
kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye,
naye afunga wala hapana afunguaye.”
Yesu Kristo ndiye aliyejitangaza
ya kuwa anao ufunguo na kuwa mwenye kufunga ni yeye na mwenye kufungua ni yeye
na akifunga hapana afunguae na akifungua hakuna awezaye kufunga, huna sababu ya
kulalamika wala kulia unapoona mambo hayaendi, Yesu anabatiza kwa Roho
Mtakatifu, Yesu anamwaga neema juu ya neema, Yesu ndiye anayebariki, Yesu ndiye
anayefungua kurasa mpya wakati nyingine inapofunga yeye anayo mamlaka yote,
Yesu sio tu anafungua milango yote lakini pia anazo funguo za mauti na kuzimu
hakuna wa kukupeleka kaburini bila ruhusa yake na uwezo wake, watu wanaweza
kukuona umekwama lakini Yesu anakuona unaelekea anakotaka uko mlango na unaweza
kuwekwa wazi kwako katika ndoa yako, katika maisha yako, katika magonjwa yako,
katika familia yako, katika uponyaji wako, acha kuangalia milango iliyofungwa
mwangalie mwenye funguo mwangalie Yesu ambaye yeye ana mamlaka na wokovu wako,
na uponyaji wako na mafanikio yako ukimwangalia yeye kutoboa utatoboa katika
jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai kataa kuona giza, kataa mahangaiko
mwombe Bwana akufungulie mlango, Mwambie nipe kuona Malango uliofunguliwa
nionapo giza naye amekupa mlango uliofunguliwa tayari!
Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona,
nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu
yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami
nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo
za mauti, na za kuzimu.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!