Jumapili, 22 Februari 2026

Kombeo la Daudi!


1Samuel 17:38-40. “Ndipo Sauli akamvika Daudi mavazi yake ya vita, akamtia chapeo cha shaba kichwani, akamvika dirii. Naye Daudi akajifunga upanga juu ya mavazi yake, akajaribu kwenda; maana alikuwa hajavijaribu. Daudi akamwambia Sauli, Siwezi kwenda na vitu hivi, maana sikuvijaribu. Basi Daudi akavivua. Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.”




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika maisha yetu duniani wakati mwingine adui zetu watatulazimisha kuingia katika vita hata kama sisi ni watu wa Amani, na ni muhimu kwetu kujua kuwa sisi ni askari wa Yesu Kristo kwa hiyo tuwapo duniani tunapigana, tunapigana vita vita inayoonekana na isiyoonekana na kwa sababu hiyo ni lazima kila mmoja wetu apigane vita vilivyo vizuri na kuilinda Imani, Paulo mtume alipokuwa anahitimisha kazi yake ya injili duniani alitoa taarifa kuwa amevipiga vita vizuri.

2Timotheo 4:7-8 “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.”

Katika vita zetu duniani ni lazima tuelewe kuwa Mungu ndiye anayetufundisha vita na kwa sababu hiyo ni muhimu kwetu kuwa makini na kujifunza kutoka kwake namna na jinsi tunavyoweza kupigana vita hizo ili tuweze kushinda.

2Samuel 22:33-35 “Mungu ndiye ngome yangu yenye nguvu; Naye huwaongoza wakamilifu katika njia yake. Huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu; Na kunisimamisha mahali pangu pa juu. Ananifundisha mikono yangu vita; Hata mikono yangu yaupinda upinde wa shaba.”

Zaburi 18:31-34 “Maana ni nani aliye Mungu ila Bwana? Ni nani aliye mwamba ila Mungu wetu? Mungu ndiye anifungaye mshipi wa nguvu, Naye anaifanya kamilifu njia yangu. Miguu yangu anaifanya kuwa ya kulungu, Na kunisimamisha mahali pangu pa juu. Ananifundisha mikono yangu vita, Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba.”

Zaburi 144:1-2 “Na ahimidiwe Bwana, mwamba wangu, Anifundishaye mikono yangu vita, Vidole vyangu kupigana. Mhisani wangu na boma langu, Ngome yangu na mwokozi wangu, Ngao yangu niliyemkimbilia, Huwatiisha watu wangu chini yangu.”    

Mungu huwafundisha watu wake vita na namna ya kupigana kwa jina la Bwana na kupata ushindi katika maisha yetu, Moja ya watu waliokuwa na uhodari katika vita ni pamoja na Daudi na watakatifu waliotutangulia wao walikuwa hodari katika vita kwa sababu Mungu aliwafundisha namna ya kupigana kwa usahihi katika maisha haya ya mapigano dhidi ya adui yetu mkuu ambaye ni shetani, maandiko yanawataja kuwa walikuwa hodari katika vita, sisi nasi Mungu na atupe kuwa hodari katika vita sawasawa na mapenzi yake katika jina la Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai

Waebrania 11:32-33 “Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii; ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni.”

Leo tutachukua muda kujifunza kutoka kwa Daudi jinsi Mungu alivyoweza kumtumia kuleta ushindi mkubwa kwa watu wa Taifa lake dhidi ya wafilisti kwa kutumia silaha duni na dhaifu maarufu kama kombeo, na tutajifunza somo hili Kombeo la Daudi kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-

·         Ufahamu kuhusu Kombeo

·         Kombeo la Daudi

·         Kanisa na kombeo la Daudi.


Ufahamu kuhusu Kombeo.

Mojawapo ya silaha ya zamani sana ambayo ilitengenezwa kwa kamba zilizofumwa vizuri au ngozi na kuwekewa kifuko cha ngozi katikati kwaajili ya kuwekea jiwe kisha kuzungushwa na kuliachia jiwe kwa kasi kubwa na kwa ufundi wa kulenga shabaha ni pamoja na kombeo, Kombeo kama silaha iliyotumiwa na Daudi kuleta ushindi dhidi ya Goliath sasa ina umri wa miaka kama 3000, silaha hiyo maarufu kwa lugha ya kiebania kama “Kela David”  au “Qela David” na kwa kiingereza “David Sling” Kiswahili inaweza kuitwa “Kombeo la Daudi” au “Manati ya Daudi”, ni silaha duni na ya zamani sana iliyotumiwa na watu masikini wasiokuwa na uwezo hata wa kununua panga au mkuki, ndiyo silaha iliyotumiwa na Daudi kumuua Goliathi kwa jina la Bwana wa majeshi Mungu wa Israel, jina lingine la kombeo ni teo.

1Samuel 17:43-45 “Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake.Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni. Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.”

Ni ukweli uliowazi kuwa  ushindi wa Daudi dhidi ya Goliath haukusababishwa na kombeo pekee bali Mungu alihusika nyuma ya ufundi, Imani na ujasiri wa Daudi, Daudi mwenyewe alikuwa na uelewa kamili kuwa Bwana angemtia Goliath katika mikono yake akiwa na uhakika kuwa Mungu haokoi kwa upanga wala mkuki bali kwa nguvu zake.

1Samuel 17:45-47 “Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu.”

Maneno  haya ya Daudi yanathibitisha kuwa kulikuwa na zaidi ya kombeo katika vita ile, watu wakati mwingine tunaweza kusema kuwa kombeo la Daudi pia linaweza kuitwa “kombeo la Bwana”, Mungu alihusika kwa asilimia zote kusababisha muujiza ule kupitia silaha duni na ya chini na ya kimasikini sana, Wakristo wakati mwingine tumepambana na maswala magumu sana duniani, na wakati mwingine na watu wakubwa sana  wenye nguvu, wenye akili, wenye utajiri na uwezo, wasemaji wazuri kuliko sisi lakini tunaweza kuwaangusha chini kwa silaha zetu duni na zenye kudharaulika endapo tutazitumia silaha hizo vema, ingawa silaha  za vita vyetu si za mwili lakini tunaelezwa katika maandiko kuwa zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome na kila kitu kinachijiinu kinyume na Mungu.

2Wakorintho 10:4-6 “(maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome ;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia.”

Pamoja na uduni wa kombeo moja ya sifa kubwa ya kombeo ilikuwa ni ni silaha ambayo kamwe haiko kwenye kundi la silaha ya kubahatisha na wale waliojifunza kuitumia wanakiri kuwa inapiga kwa ustadi na kwa umakini mkubwa, kwa hiyo Daudi alikuwa na uzoefu wa siri wa matumizi ya silaha hiyo ambayo aliitumia pia kuua dubu na simba kabla ya kujitokeza hadharani, wapendwa silaha za rohoni kama ukizitumia kwa ustadi zinalenga pale pale na kumaliza kabisa nguvu za adui bila kubahatisha, Kufunga na kuomba na matumizi sahihi ya neno la Mungu hakujawai hata siku moja kuwa kitu cha kubahatisha kama unataka kumpiga adui kwa usahihi basi tumia silaha hizo kwa usahihi.

Wajibu wa kutokuogopa silaha nzito:

Neno la Mungu limeonya kuwa hatupaswi kuogopa silaha za upande wa adui hata kama zitaonekana kuwa na ubora na manufaa kuliko silaha zetu, hatupaswi kuogopa farasi, wala magari ya vita, wala jeshi kubwa, Mungu amesema katika neno lake havipaswi kuogopewa, tunapoingia katika uwanja wa vita vya kiroho kamwe tusiogope nguvu za kibinadamu, wala teknolojia ya vita, wala ufundi wa maneno, wala takwimu ya jeshi kubwa wala uzoefu na ujuzi wa maadui, Mungu alitaka watu wake wamtegemee yeye tu yeye mwenyewe ndiye vita yetu, Mungu haokoi kwa wingi,

Kumbukumbu 20:1-4 “Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa Bwana Mungu wako, yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri. Na iwe, msongeapo mapiganoni, kuhani na akaribie na kusema na watu, awaambie, Sikizeni, enyi Israeli, hivi leo mwasongea mapiganoni juu ya adui zenu mioyo yenu na isizime; msiche, wala msiteteme, wala msiingiwe na hofu kwa ajili ya wao; kwa maana Bwana, Mungu wenu, ndiye awaandamaye kwenda kuwapigania juu ya adui zenu, ili kuwaokoa ninyi.”

Kumbukumbu 17:16 “Ila asifanye farasi wake kuwa wengi, wala asiwarudishe watu Misri, ili apate kufanya farasi kuwa wengi; kwa kuwa Bwana amewaambia, Tangu sasa msirudie tena njia ile.”

Yoshua 11:1-11 “Kisha ikawa, hapo huyo Yabini, mfalme wa Hazori, aliposikia habari ya mambo hayo, akatuma mjumbe aende kwa Yobabu, mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na mfalme wa Akshafu, na hao wafalme waliokuwa upande wa kaskazini, katika nchi ya vilima, na katika Araba upande wa kusini wa Kinerethi, na katika Shefela, na katika nchi zilizoinuka za Dori upande wa magharibi, na kwa Mkanaani upande wa mashariki, na upande wa magharibi, na kwa Mwamori, na Mhiti, na Mperizi na Myebusi katika nchi ya vilima, na kwa Mhivi pale chini ya Hermoni katika nchi ya Mispa. Nao wakatoka nje, wao na jeshi zao zote pamoja nao, watu wengi mno, kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi, pamoja na farasi na magari mengi sana. Wafalme hao wote wakakutana pamoja; wakaenda na kupanga mahema yao pamoja hapo penye maji ya Meromu, ili kupigana na Israeli. Bwana akamwambia Yoshua, Usiche wewe kwa ajili ya hao; kwani kesho wakati kama huu nitawatoa hali wameuawa wote mbele ya Israeli; utawatema farasi zao, na magari yao utayapiga moto. Basi Yoshua akaenda, na watu wote wa vita pamoja naye, ili kupigana nao hapo penye maji ya Meromu ghafula; wakawaangukia. Bwana akawatia mkononi mwa Israeli, nao wakawapiga, na kuwafukuza hata kufikilia Sidoni ulio mkuu, na hata kufikilia Misrefoth-maimu, tena hata kufikilia bonde la Mispa upande wa mashariki; wakawapiga hata wasiwasaze hata mtu mmoja aliyesalia. Yoshua akawafanyia vilevile kama Bwana alivyomwamuru; akawatema farasi zao, na magari yao akayapiga moto.”

Wakati wote Mungu alifanya vita na adui za watu wake katika namna ya kushangaza sana, na Mungu aliwaonya watu wake kutokuzitumainia silaha za kimataifa na za kifalme, aliwataka watu wake kumtegemea yeye, aliwataka watu wake wawe na ujuzi kuwa sio wingi wa farasi unaookoa, wala sio wingi wa watu unaookoa wala sio ukubwa wa jeshi, tena aliwataka hata wasiombe msaada wa kivita kwa majirani hasa Misri  na hata wakiteka mateka aliwambia farasi zao wazikate mishipa na magari yao ya vita wayachome moto, Mungu anajua kuwa ziko silaha zizisooenakana kwa macho na hata zile zinazoonekana kwa macho na zikadharauliwa na kuonekana kuwa ni silaha duni, Ni ukweli ulio wazi, kuwa Mungu anazitumia nyuma ya mambo kufanya mambo makubwa ya kutisha na kushangaza, Mungu hakutaka watu wajisifie wingi na uwezo wao alitaka watu waelewe na wajue ya kuwa ushindi unatoka kwa Mungu.

Waamuzi 7:1-2 “Kisha Yerubaali, yaani Gideoni, na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka na mapema, wakapiga kambi yao karibu na kijito cha Harodi; na kambi ya Midiani ilikuwa upande wao wa kaskazini, karibu na mlima wa More, bondeni. Bwana akamwambia Gideoni, Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno hata nikawatie Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa.”

Mungu aliwapunguza wanajeshi waliotoka na Gideoni kutoka 32,000 hadi kufikia mia tatu 300 na alimkataza Gideoni kusudi Israel wasijivunie kuwa ushindi walioupata umetokama na wingi wao, katika vita za Bwana wingi haumtishi, wala hauhusiki na wokovu wake, Mungu aweza kutumia silaha duni na watu wachache kusababisha ushindi kwa utukufu wake na kwaajili ya jina lake ili sifa na utukufu zielekezwe kwake!

Zaburi 33:16-17 “Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu. Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake.”

Zaburi 20:6-7 “Sasa najua kuwa Bwana amwokoa masihi wake; Atamjibu kutoka mbingu zake takatifu.Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu.” 

Isaya 31:1-3 “Ole wao watelemkao kwenda Misri wapate msaada, na kutegemea farasi; watumainio magari kwa kuwa ni mengi, na wapanda farasi kwa kuwa ni hodari sana; lakini hawamwangalii Mtakatifu wa Israeli, wala hawamtafuti Bwana! Lakini yeye naye ana akili, naye ataleta uovu, wala hatayatangua maneno yake; Bali ataondoka juu ya nyumba yao watendao mabaya, na juu ya msaada wa hao watendao maovu. Basi Wamisri ni wanadamu wala si Mungu, na farasi zao ni nyama wala si roho; na Bwana atakaponyosha mkono wake, yeye asaidiaye atajikwaa, na yeye asaidiwaye ataanguka, nao wote pamoja watakoma.”

Isaya 54:15-17 “Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako.Tazama, nimemwumba mhunzi avukutaye moto wa makaa, akatoa silaha kwa kazi yake; nami nimemwumba mharibu ili aharibu. Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”                 

Kombeo la Daudi

Daudi alikuwa na ujuzi fulani kuhusu Mungu na maagizo yake katika Torati. Alikuwa amekwisha kujifunza kuwa Mungu haokoi kwa upanga wala mkuki, alikuwa na ujuzi kuwa Mungu haokoi kwa kutumia wingi, kwa hiyo alipomwendea adui yake alikuwa na mkoba wa ngozi na ndani yake alikuwa amekunja kombeo yake na alikuwa na mawe matano laini kutoka mtoni, yanaitwa mawe laini kwa sababu yalikuwa na uduara flani yaani yasiyoweza kukata au kuumiza kutokana na kudongoroshwa katika maji, lakini yalikuwa magumu sana, Wakati Goliath alikuwa na vifaa vya kisasa  vya vita, na katika Israel ni mfalme Sauli tu na mwanae Jonathan ndio waliokuwa na uwezo wa kumiliki upanga, watu wengine wote walikuwa na silaha duni na za kimasikini, Daudi alikuwa anatambua kuwa vita ni ya Bwana na kuwa Bwana angewaliwapigania watu wake kwa hiyo Kombeo la Daudi ilikuwa ni silaha inayoonekana ya Mungu asiyeonekana, kulikuwa na kitu cha ziada katika kombeo la Daudi, yeye alionekana ameshika fimbo tu mpaka pale alipoichomoa kombeo lake na kuchagua jiwe laini na adui alisambaratishwa kwa uwezo wa jina la Bwana kupitia jiwe lile moja tu kati ya mawe matano aliyokuwa ameyachagua, kwanini Daudi alikuwa na uhakika wa silaha ile duni kumpa ushindi mkubwa usiokuwa wa kawaida?

-          Daudi alikuwa amefundishwa kupigana, Mungu alimfundisha Daudi vita na matumizi ya silaha zile duni na zikaonyesha uwezo mkubwa akiwa nyikani, wakati akiwa anachunga kondoo wa baba yake alikuwa amekwisha kujifunza kutumia kombeo, na aliona kombeo ikiwashughulikia Dubu na Simba wanyama ambao ni wakali, aliweza kupambana nao na Mungu akimsaidia, Mungu alimuokoa na wanyama hao wakali

 

1Samuel 17:34-37 “Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai. Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe.”

 

-          Daudi hakutegemea silaha za kifalme, Kulikuwa na nyakati ambapo wafilisti walihodhi teknolojia ya usindikaji vyuma kwa kusudi la kuwazuia Waisrael wasitengeneze silaha, hii ilikuwa mbinu ya kimkakati ya adui ya kuwafanya Israel wawe dhaifu na tegemezi, kwa hiyo watu walioweza kumiliki silaha za vyuma walikuwa ni wafalme au watu matajiri sana wenye kipato cha hali ya juu, kwa hiyo mtu kama Daudi hakuwa na uwezo wa kumiliki silaha za chuma wala hakuwa na ujuzi katika hizo, ilikuwa mtu akitaka kunoa hata jembe ni lazima aende kwa wafilisti, kwa hiyo uhodari wa vita ulikuwa ni katika matumizi ya kombeo, fimbo mawe na vifaa vya shambani, wafilisti walitaka kuwanyima Israel maarifa na dhana za mapigano  ili kujihakikishia ushindi

 

1Samuel 13:19-22 “Basi, hakuonekana mhunzi ye yote katika nchi yote ya Israeli; kwa kuwa Wafilisti walisema, Waebrania wasije wakajifanyizia panga au mikuki; lakini Waisraeli wote hushuka kwa Wafilisti, ili kunoa kila mtu jembe lake, na mundu wake, na shoka lake, na sululu yake; ila walikuwa na tupa za kunolea sululu, na miundu, na mauma, na mashoka; na kwa kuinoa michokoo. Hivyo ikawa, siku ya vita, haukuonekana mkononi mwa mtu ye yote, miongoni mwa watu waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani, upanga wala mkuki; isipokuwa Sauli mwenyewe na mwanawe Yonathani walikuwa navyo.”

 

-          Daudi alikuwa na ufahamu kuwa vita ni ya Bwana, Daudi alikuwa na uelewa wa wazi kuwa wao walikuwa na silaha duni, na walinyimwa teknolojia na hata utengenezaji wa silaha za vita za chuma, watu waliokuwa na silaha katika Israel ni Sauli na mwanae Jonathani, hivyo Daudi aliweka tumaini lake lote kwa Mungu, alielewa kuwa kombeo ilikuwa ni silaha duni sana na haikuwa na mchango wowote kwa mtu ambaye amejivika vyuma mwili mzima lakini alielewa kuwa Mungu angekuwa nyuma ya kombeo na angeliongoza jiwe kupita popote palipo wazi hata kama ni kwenye jicho kwani alijifunza kuwa kombeo lililoongozwa na Bwana halitakosa kulenga shabaha, na mkuki na upanga kama Bwana hayuko navyo haziwezi kuwa silaha za kutisha kwake, watu waliojifunza kutumia kombeo au teo walikuwa na uwezo wa kuitumia kwa usahihi sana tangu nyakati za waamuzi watumiaji wa kombeo walikuwa wanauwezo wa kulenga hata unywele kwa jiwe  na wasikose shabaha kwa hiyo usahihi wa matumizi ya kombeo ulikuwa wa uhakika kwa kiwango cha juu, sana na kwa sababu hiyo Daudi hakuidharau silaha yake ndogo na duni akijua kuwa Mungu ataitumia  

 

1Samuel 17:45   Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.”

 

Waamuzi 20:14-16 “Lakini wana wa Benyamini wakakutanika huko Gibea kutoka katika miji yao, ili watoke kwenda kupiga vita juu ya wana wa Israeli. Hao wana wa Benyamini walihesabiwa siku ile kutoka hiyo miji, watu waume ishirini na sita elfu waliotumia upanga, zaidi ya hao waliokaa Gibea, ambao walihesabiwa watu wateule mia saba. Katika watu hao wote walikuwako watu waume mia saba waliochaguliwa, wenye shoto; kila mmoja alikuwa anaweza kuutupia unywele mawe kwa teo, wala asikose.”

 

Ni kutokana na umahiri wa silaha hii leo hii Idara ya ulinzi ya Israel Israel Defense Force (IDF) wameendeleza silaha ya kisasa kabisa inayoitwa kwa jina hili la kombel la Daudi “David’s Sling” ambayo ilianza kutumika kijeshi mwaka 2017 ikiwa na uwezo wa kuingilia kati na kuharibu mifumo ya ushambuliaji ya maadui kama wakitumia ndege, drones, na mabomu ya mashambulizi ya kisasa Ballistics missiles za uwezo wa aina mbalimbali kuanzia kilomita 40 mpaka 300 katika mifumo ya kivita ya kisasa ya israel      

Kanisa na kombeo la Daudi.

Mungu katika mpango wake hata leo bado ameendelea kulifundisha kanisa lake na kulihimiza, kuendelea kuweka tumaini letu kwake katika maeneo yote, Pamoja na maendeleo ya kitaaluma na teknolpojia iliyoko leo na mpanuko mkubwa wa elimu Bado Mungu anataka tumpe yeye kipaumbele na katika nguvu zake na hekima ya Mungu kuliko nyenzo za kisasa zilizoko duniani, kuhudumu kwetu na kufundisha kwetu na kuhubiri kwetu kamwe kusiangukie katika hekima ya kibinadamu bali tuendelee kuzitegemea nguvu za Mungu katika maisha yetu yote Paulo mtume alikuwa msomi, mwanasheria mkubwa na mwanafalsafa aliyebobea hata hivyo, alimtegemea sana Mungu katika huduma yake kuliko Elimu yake  na uwezo wake wa kushawishi, Mungu hutumia Imani  yetu katika jina lake na upako  hata kuliko vyeti vyetu vya kitaaluma, sio vibaya kuwa na taaluma lakini tusisahahu upako una sehemu muhimu katika maisha yetu ya huduma na utumishi, jumbe zangu zote zinatokana na muongozo wa Roho Mtakatifu kwanza kisha taaluma hufuata baadae katika maandalizi, lakini Mungu Roho Mtakakatifu ni namba moja kwangu.

1Wakorintho 2:4-5 “Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.”   

Paulo mtume alikuwa na ujuzi ya kuwa Mungu anaweza kuwatumia wenye cheo na wenye hekima ya dunia hii, lakini alitahadharisha kuwa Mungu huyatumia mambo manyonge na madhaifu na yaliyodharauliwa, na wadhaifu, kwa sababu Mungu hataki watu wajisifie mbele zake kwa sababu ya uwezo wa kibinadamu, bali kwaajili ya jina lake.

1Wakorintho 1:26-29 “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu.”

Paulo alikuwa na ujuzi ya kuwa Mungu anaweza kumtumia mtu kwa rehema zake na neema yake tu na ya kuwa juhudi za kibinadamu haina mchango wowote katika kutupatia kibali cha Mungu, wala jitidaha za kibinadamu hazina mchango wa kuleta rehema za Mungu kwetu wala matakwa yetu

Warumi 9:10-16 “Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu,(kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye), aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo. Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia.Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha! Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.”

Neno la Mungu linatufundisha kuwa kuna namna ambapo Mungu asipohusika kwenye jambo lolote hata tujihusishe vipi jambo hilo haliwezi kuwa na maanikio bila ya mkono wake   na jambo hili ndio liko kwenye siri ya kombeo la Daudi           

Zaburi 127:1 “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure.”  

Yohana 15:4-5 “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.”

Tunajifunza kuacha kuzitegemea Pesa kuliko Mungu kuingilia kati maswala yetu, kuacha kutegemea miundo mbinu bila kumruhusu Roho Mtakatifu katika shughuli zetu, kuacha kutegemea wingi wa watu kuliko uwepo wa Mungu, tulitegemee neno la Mungu kama upanga wa roho kwaajili ya ushindi katika maisha yetu, tuyategemee maombi yetu kuleta matokeo kuliko akili zetu na tumtegemee Mungu kwa Imani hata katika mambo madogo yasiyotatrajiwa, tutumie kile ambacho Mungu amekiweka ndani yetu kwa utukufu wake na tunataona ushindi mkubwa katika maisha yetu na hilo ndio kombeo la Daudi, Bila uwepo wa Mungu kombeo lisingeweza kuwa sababu ya ushindi wa Daudi.

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: