Jumapili, 8 Machi 2026

Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa


2Timotheo 4:9-11 “Jitahidi kuja kwangu upesi. Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia. Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi.”



Utangulizi:

Ni maneno ya huzuni na masikitiko makubwa sana kutoka kwa mtume Paulo, akiwa kifungoni katika siku zake za mwisho, kabla kidogo ya kuhukumiwa kifo. Akiwa katika gereza lenye kutisha liitwalo “Mamertine Prison” akisubiria hukumu yake ya kifo, Katika wakati huo Mgumu anaachwa na mtenda kazi maarufu sana aliyewahi kuwa karibu sana na mtendakazi pamoja naye katika kazi ya injili aliyejulikana kwa jina la Dema, Ni katika namna ya kusikitisha sana Paulo akiwa katika maumivu hayo Dema anaamua kuachana na injili na kwenda katika jiji la Thesalonike Ugiriki ya leo, kwenda kuishi maisha ya kutanua na kustarehe, “Dema aliniacha akiupenda ulimwengu huu wa sasa”, ni ujumbe unaobeba fundisho muhimu sana kuhusu hatari ya kuanza vizuri na kumaliza vibaya! Wakati Paulo akiwa anafurahia kumaliza vizuri huduma yake Dema anamaliza vibaya kwa kurudi nyuma na kwenda kujirusha duniani.

Matendo 20:22-24 “Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja. Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu.”

Tuitajifunza somo hili Dema aliniacha akiupenda ulimwengu huu wa sasa kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Dema ni nani na alikuwa nani?

·         Dema aliniacha akiupenda ulimwengu huu wa sasa.

·         Mambo ya kujifunza kutoka kwa Dema.


Dema ni nani na alikuwa nani?

Jina Dema kwa asili limetokana na jina la Kiyunani Dēmos ambalo maana yake kwa kiingereza ni “The people”  mzizi mmoja na jina Nicodemus ambalo kwa kiingereza ni “Victory of the people” kwa hiyo jina Dema maana yake ni watu.  Na Nicodemo maana yake ushindi wa watu. Dema hakuwa mshirika wa kawaida tu kanisani na katika huduma, Yeye alikuwa ni Mtumishi wa Mungu katika timu ya umisheni pamoja na Paulo Mtume  na anatajwa pamoja na Luka yule tabibu mpendwa, mwandishi wa Injili ya Luka na kitabu cha Matendo ya mitume pamoja na kina Epafra mwanzilishi wa makanisa ya Kolosai, Laodikia na  Hierapoli.

Wakolosai 4:12-14 “Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu. Maana namshuhudia kwamba ana juhudi nyingi kwa ajili yenu, na kwa ajili ya hao walioko Laodikia, na kwa ajili ya hao walioko Hierapoli. Luka, yule tabibu mpendwa, na Dema, wanawasalimu.”

Maandiko yanamtaja Dema pamoja na watumishi wa Mungu wa ngazi ya juu kabisa wenye sifa njema, na wote tunajua jinsi ambavyo Paulo mtume alikuwa makini sana katika kuchagua watu wema wa kuambatana naye katika kazi ya injili, kwa hiyo iko wazi kuwa Dema alikuwa sehemu muhimu ya timu ya wamishionari na mtendakazi, Pamoja na Paulo mtume. Na alijulikana sana kuwa aliitenda kazi ya Mungu pamoja na watu wengine maarufu katika watendakazi wenza pamoja na Paulo mtume, Dema alikuwa pia katika timu moja na Marko mwandishi wa Injili ya Marko na pia Aristrarko, na wengineo, alikuwa muhubiri wa injili, alikuwa mmishionari, alikuwa mpanda makanisa kwa hiyo ni dhahiri kuwa alikuwa mtendakazi aliyeweza kustahimili magumu mengi katika safari ya injili, kimsingi aliianza kazi hii vizuri.

Filemoni 1:22-24 “Na pamoja na hayo uniwekee tayari mahali pa kukaa; maana nataraji ya kwamba kwa maombi yenu mtajaliwa kunipata. Epafra, aliyefungwa pamoja nami katika Kristo Yesu, akusalimu; na Marko, na Aristarko, na Dema, na Luka, watendao kazi pamoja nami.”

Hata hivyo katika mazingira ya kustaajabisha na ya kusikitisha sana mtumishi huyu wa Mungu maarufu namna hii tunataarifiwa kuwa alirudi nyuma alimuacha Mtume Paulo akiwa gerezani kisha akaenda zake jijini Thesalonike kwenda kufanya biashara zake akiupenda ulimwengu wa sasa hii maana yake ni nini? Hilo linatupa nafasi kutafakari kipengele cha pili cha somo hili Dema aliniacha akiupenda ulimwengu huu wa sasa, kama Dema angemuacha Paulo mtume na kwenda kuhubiri sehemu nyingine hiyo ingekuwa njema na Paulo asingelihuzunika lakini Dema aliupenda ulimwengu huu ni msiba hasa kwa Paulo kwa kuwa Dema hakwenda kuihubiri injili bali alirudi duniani huko Ugiriki.

Dema aliniacha akiupenda ulimwengu huu wa sasa.

Biblia haitoi maelezo mengi kwanini Dema alirejea nyuma, akiiacha kazi ya Mungu na mateso ya Mtume Paulo gerezani, lakini ufafanuzi wa maneno ya Paulo unatupa picha kubwa na ya kutisha  na kusikitisha kuhusu mkasa wa Dema, Kimsingi mstari wa “10” 2Timotheo 4:10 “Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia.” Unasomeka hivi katika Kiyunani “yáp Dēmas egkataleipō, agapaō ton nun aiona”  Katika maneno hayo ya Kiyunani neno Agapaō linamaanisha “sacrificial love” kujidhabihu kwa hiyo Dema alikuwa amejidhabihu kwa dunia badala ya kazi ya Mungu, hii maana yake aliipenda sana dunia, alikubali kuvutiwa nayo, alishikamana na dunia kwa moyo wake wote  na neno “Aiona” yaani ulimwengu wa sasa linamaanisha alishikamana na mfumo wa sasa wa dunia hii ikimaanisha kutafuta Heshima, kutafuta mali, na usalama wa kidunia Dema aliamua kufanya hivyo kwa sababu wakati huu ulikuwa ni wakati wa hatari sana kujitoa kwaajili ya injili, mateso kutoka utawala wa kirumi yalikuwa yamepamba moto kinyume na Ukristo na injili yake, wakristo walikuwa wanateswa, kuuawa na hata kufungwa kwa hiyo Dema aliogopa alikimbilia katika jiji kubwa la kibiashara la Thesalonike huko Ulaya Ugiriki ambako kulikuwa na kanisa letu huko lakini hakurudi kanisani na badala yake alirudi katika maisha yake ya kawaida na kufanya biashara akiishi maisha ya kawaida akiachana  na huduma ambayo kimsingi ilikuwa inagharimu maisha ya watu, aliogopa kuifia injili.

1Yohana 2:15-17 “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.”

Warumi 12:1-2 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”

Dema hakuwa mshirika wa kawaida alikuwa mtumishi wa Mungu alishiriki katika kazi ya injili, sio wakati wote mazingira yalikuwa rahisi lakini alivumilia kurudi nyuma kwa Mtumishi wa Mungu kama Dema ni swala la kusikitisha sana na ni swala lenye kuogopesha, Dema alikuwa askari wa mstari wa mbele, Kadiri tunavyokua na kuinuliwa katika imani  na kushinka nafasi za kitumishi hatunabudi kuongeza kiwango chetu cha kujitoa kwa Mungu na kumpenda Yesu, Shetani haogopi kuwa umefikia ngazi gani ya kiroho anaweza kukurejesha Duniani, kwa uwazi au kimya kimya.

Mambo ya kujifunza kutoka kwa Dema

Kumfuata Yesu kunahitaji kujikana nafsi – Leo tunamuhubiri Kristo na tunaweza tusisikie wahubiri wakirudi nyuma kwa sababu kwanza injili inalipa, watu wengi sana wamebarikiwa kutokana na kuihubiri injili katika wakati huu wa Amani, lakini yako mazingira ambapo mambo yanaweza kuwa magumu na mateso yakazidi hapo waoga wote wataondoka kwenye mfumo, tujikumbushe kuwa kumfuata Yesu kunahitaji kujikana  na kubeba Msalaba

 

Luka 9:23-25 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?

 

Kumfuata Yesu kunahitaji kuhesabu gharama – Yesu anawataka wanafunzi wake watambue kuwa kumfuata Yesu ni gharama ni sawa na mtu anayetaka kujenga mnara, ni lazima ukae upige hesabu na kufanya maandalizi ya kutosha ili usije ukawa dhihaka kwa kushindwa kukamilisha mradi wako, Dema alishindwa kukamilisha mradi.

 

Luka 14:28-30 “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.”

 

Kumfuata Yesu ni kama kuanzisha vita – taifa lolote linapoanzisha vita na taifa lingine au ufalme wowote unapoanzisha vita na ufalme mwingine ni lazima taifa hilo au ufalme huo ukae chini na kupiga hesabu zake vizuri na kufanya mashauri au upelelezi wa kutosha kama unaweza kupigana na upande wa pili na kupata ushindi na ukiona vita inakuwia ngumu basi omba agano la Amani

 

Luka 14:31-33 “Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali. Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”

 

Kumfuata Yesu ni kama kulima kwa jembe la kukokotwa na wanyama – Jembe la kukokotwa na wanyama kama ng’ombe kwa kawaida mtu anapolitumia kwenye kulima haliruhusu kusimama au kuangalia nyuma, mkulima wa jembe la kukokotwa na ngombe ni lazima aangalie pale anapolima ni lazima aangalie mbele asiondoe mawazo yake katika shughuli hiyo kwani kuangalia nyuma kunapoteza sifa ya mkulima wa aina hiyo hali kadhalika mtu anayemfuata Yesu

 

Luka 9:61-62 “Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.”

 

Kumfuata Yesu kunahitaji uaminifu hata kufa – Mungu kweli atatukoa wakati mwingine katika mitego ya adui, na vita za aina mbalimbali kama ilivyokuwa kwa Dema, tunakuwa salama wakati wote Bwana akiwa upande wetu hata hivyo yako mazingira kama haya ambayo Paulo mtume alikuwa anakabiliwa na kifo ni ukweli ulio wazi wengi walimuacha, kuna wakati tunapaswa kuwa waaminifu hata kufa lakini sio kila mtu anataka kifo, kuwa tayari kwa hilo kwaajili ya Kristo ni dhabihu ya hali ya juu sana ni kukubali kuwa shahidi wa Yesu Kristo uliye mwaminifu  

 

2Timotheo 4:16-17 “Katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba.”

 

Ufunuo 2:9-10 “Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani. Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.”

 

Matendo 21:10-14 “Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa. Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu. Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu. Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke.”             

 

Kumfuata Yesu kunahitaji uwe imara – Kila mwanafunzi wa Yesu anapaswa kukumbuka wakati wote kujiimarisha katika Imani ili kuhakikisha kuwa kila siku tunapiga hatua na kukua kiroho, hata pamoja na kuwa tunamtumikia Mungu, Dema alijisahau, Paulo mtume anasema hakujihesabu kuwa amefika lakini kila wakati alikuwa akiendelea na mazoezi muhimu ya kiroho ili asifanye kazi ya kuhubiri tu wengine kisha yeye akawa mtu wa kukataliwa, uzoefu na kurudi nyuma kwa Dema kunatukumbusha kwamba tunapaswa kuhakikisha kuwa tunajiimarisha kila iitwapo leo

 

Wafilipi 3:12-14 “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”

 

Mathayo 7:2-27 “Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”

 

Mathayo 13:20-21 “Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa.”

 

Watu wa Mungu tunaowajibu wa kuhakikisha kuwa tunamaliza vizuri, inasikitisha sana kuona mtu mkubwa aliyembatana na muhubiri mkubwa kama Dema akirudi nyuma, na kuipenda dunia, Shetani haogopi kuwa umefikia ngazi gani ya kiroho, kwa sababu hiyo kila wakati tujilinde katika neema ya Mungu, na kuendelea kujidhabihu na kutokukata tamaa kwa sababu ya dhiki na mambo mengineyo, na badala yake tujiimarishe katika Bwana ili kila mmoja wetu aweze kumaliza vizuri, tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima kipo na ni rahisi kuvutwa kwenye ulimwengu huu kama hatutashikamana na utimilifu wetu wa Imani mpaka mwisho.                


Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Maoni 2 :

Bila jina alisema ...

Ukiwa umefanya kazi maisha yako yote kujenga familia na urithi, huwezi kuruhusu kivuli cha mtu wa tatu kiiharibu katika miezi michache tu. Niligundua kuwa mabadiliko ya ghafla ya tabia ya mume wangu yalikuwa kuingiliwa kiroho, si tu mgogoro wa katikati ya maisha.

Niliwasiliana na Mystic Kakaa kwa ajili ya uingiliaji kati wa kibinafsi. Kazi yake ilikuwa ya upasuaji. Alitambua kivuli na kukiondoa kabisa bila drama yoyote ya umma. Ndani ya siku 5, umakini wa mume wangu ulirudi nyumbani kwetu na katika mustakabali wetu. Ikiwa unalinda maisha yenye thamani kubwa na unahitaji bwana anayeelewa busara, wasiliana naye kwa: dawnacuna314@gmail.com

WhatsApp: +2349046229159

Yeye ndiye kiwango cha dhahabu.
Kwa uchawi wa upatanisho wa uhusiano/ndoa.

Uchawi wa kumfanya mpenzi wako wa zamani/mwenzi wako aombe msamaha.

Uchawi wa kumrudisha mpenzi wako/kumvutia mpenzi mpya.

Uchawi wa kurejesha mali/pesa zilizoibiwa.

Mabadiliko ya umbo/Uchawi wa kutoweka.

Uchawi wa kushinda bahati nasibu/kesi ya mahakama. Na zaidi

Bila jina alisema ...

Nataka kutoa ushuhuda kuhusu jinsi nilivyopona kutokana na Virusi vya Herpes. Miezi michache iliyopita nilikuwa na dalili kadhaa. Nilienda kumuona daktari na vipimo vingi vya damu vilifanywa kwangu, baadaye niliambiwa nilikuwa na Herpes. Daktari wangu aliniambia kwamba hakuna tiba ya Herpes. Nilijisikia vibaya, niliingia mtandaoni nikitafuta tiba inayowezekana ya Virusi vya Herpes, niliona chapisho la Dkt. Dawn, daktari wa mitishamba anayewasaidia watu kupona kutokana na Herpes. Saratani. VVU na mengineyo. Niliwasiliana naye na kumwambia jinsi ninavyohisi. Alisema dawa yake ya mitishamba inaweza kuniponya. Alinitumia dawa kupitia huduma ya utoaji wa UPS na nilipokea dawa siku 6 baada ya kuituma, nilichukua dawa kama alivyoniagiza. Kabla sijakamilisha dawa dalili zilisimama. Nilienda kwa daktari na kufanya kipimo kingine cha damu, cha kushangaza nilikuwa hasi. Sijapata dalili tena. Dkt. Dawn ni mzuri na unaweza
kuwasiliana kwenye WhatsApp: +2349046229159
Gmail ( dawnacuna314@gmail.com )

Ikiwa unahitaji dawa za mitishamba kutibu magonjwa yoyote sugu au ya zinaa kama.
HERPES.
SARATANI.
VVU/UKIMWI na zaidi