Andiko La msingi: Luka 13:32 “Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika.”
Wengi wetu tutakuwa tunafahamu,
jinsi Mafarisayo walivyokua wapinzani wakubwa sana wa Bwana Yesu katika huduma
yake na kazi zake, Katika kifungu hicho hapo juu hatuna uhakika kama Mafarisayo
walikuwa wametumwa na Herode kweli, au walitunga uongo wao wenyewe ili kumtoa
Yesu katika KUSUDI kuu la kazi yake ambalo lilikuwa ni kuutangaza Ufalme wa
Mbinguni. Tunasoma hivi katika Mukhtadha mzima wa habari hii:-…
Luka 13:31-33 “Saa ile ile
Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali
pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha,
Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu
leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.”
Yesu alikuwa katika mipaka ya
galilaya wakati huu, Mafarisayo walimjia wakijifanya kama wanaurafiki na Yesu
na kuwa wanamtakia mema, wanataka kuokoa maisha yake wana uchungu na maisha
yake, walijifanya wana habari hizi kutoka kwa Herode kwamba Herode anataka
kukuua hivyo uondoke, Yesu alitaka kuwaonyesha Mafarisayo hawa kuwa kama
wamekubali kuwa wajumbe wa Herode yeye anawarejesha tena kwa Herode, na
anawatuma waende wapeleke taarifa hii maana wamekubali kutumiwa kama wambeya
sasa wamweleze wazi Herode na Yesu anatumia neno gumu
Nendeni Mkamwambie yule Mbweha!
Mbweha ni kijimnyama dhaifu sana na kioga ambacho kinafanana na Mbwa, ni
vinjinyama vinavyoishi mwituni vina uwezo wa kubweka lakini ni vioga, viongo na
vichafu na vimejaa hila,huwinda wanyama wengine ni mnyama asiye na Heshima wala
umaarufu na ni mnyama anayedharauliwa sana!
Yesu Kristo aliifahamu sheria
kuwa imeandikwa usimnenee mabaya mkuu wa watu wako, Hivyo Yesu kimsingi hakuwa
anamtukana Herode au kumnenea mabaya, Lakini alimuita mbweha kwa sababu Yesu alikuwa anatambua roho ya ukatili
aliyokuwa nayo Herode alikuwa anafahamu jinsi Herode alivyosumbua wengi kwa
ukatili wake, alitambua kuwa Herode alikuwa amepoteza umaarufu kwa wayahudi na
tena alikuwa ni kibaraka tu wa warumi na Kaisari, alikuwa muoga na mwenye hila
na aliyepoteza umaarufu kabisa,
Yesu alikuwa anajua kuwa Herode hataki yeye
awepo katika mipaka yake, na hivyo anataka kumtisha ili Yesu akimbilie mji
mwingine, Majibu ya Bwana Yesu yalikuwa ya kumuondoa wasiwasi huyu Mbweha
kuhusu huduma anayoifanya,
Yesu alikuwa anajua kusudi la kuwepo kwake na
hata saa ya kufa kwake, alikuwa anajua kusudi la Mungu katika maisha yake na
hivyo mbwembwe za Herode hazikuwa tishio
kwake, watu wengi walimuogopa Herode kama Simba lakini Yesu alimuona Herode
kama mbweha tu, Hivyo Yesu alitaka kumhakikishia Herode kuwa Yeye yupo kwa
mapenzi ya Mungu katika ardhi ya Mungu na kuwa anatimiza kazi ya baba yake tu,
na kuwa haogopi lolote! Aidha katika wakati huu Yesu alikuwa amepata umaarufu
mkubwa sana na watu wengi walikuwa wamemuamini na kwa vile Yesu ni wa ukoo wa
Daudi watu wengi walikuwa wameanza kujenga imani ya kuwa Yesu ndiye mfalme
ajaye na mwokozi wa Israel Yesu alitambua wazi kuwa Yeye hakuzaliwa kwa kusudi
la kutawala serikali ya wakti ule, Yeye alikuwa amekuja kufanya kazi ya
ukombozi wa Mwanadamu kwa kufa na kufufuka kwake na hivyo alitambua kusudi la
kuweko kwake!
Natoa Pepo na Kuponya wagonjwa!
Aidha Yesu alimtangazia Herode
kupitia wajumbe wake ukweli kuwa anaendelea kufanya kazi ya Mungu katika mipaka
ya Herode na kuwa ataendelea kufanya kazi ya Mungu, Ni kama Yesu alikuwa
anamwambia Herode kuwa Haogopi wala hana hofu yoyote ya njama za Herode, Badala
yake naendelea kutimiza kusudi la Mungu kwa kuwa yuko ndani ya majira na saa ya
Mungu na haogopi vitisho, aidha Herode hapaswi kuogopa kwa kuwa Yesu anafanya
kazi ya Mungu kwa muda mfupi tu,
Yesu Kristo ni kama alikuwa alikuwa
akimjibu Herode kuwa kutoa Pepo na kuponya wagonjwa na kuhubiri injili leo na
kesho tu (Kwa maana ya muda mfupi tu) kulikuwa na maana ya kuwa hakuwa anavunja
sheria, hakuna ubaya wowote ambao Yesu alikuwa akiutenda, kutoa pepo na kuponya
wagonjwa kwa siku chache tu, na kuwa Yesu baadaye angeondoka katika Mipaka yake
kwa wakati wa Mungu na sio wa Herode.
Siku ya tatu nakamilika
Yesu alikuwa akitoa Muda tu wa
kinabii kuwa siku ya tatu anakamilika, hii haikuwa na maana ya siku tatu katika
jimbo la Galilaya, hii ilikuwa na maana ya siku tatu katika mpango wa Mungu na
Muda wa Mungu, Yesu alikuwa anafahamu kuwa hakuna wa kumuua wala wa kumuondoa
mpaka Muda wa Mungu utakapowadia, Yesu alikuwa na ujuzi kuwa atakwenda
Yerusalem na huko ndiko atakakofia na kufufuka na kurudi katika enzi yake
Mbinguni.
Ndugu Momaji wangu Jambo lolote
lile linalokuja katika maisha yako, kukutisha na kukudhoofisha na kukutia woga
na kukuvunja moyo na kukukatisha tamaa ni MBWEHA!
Kama unaifanya kazi ya Mungu wewe
ni mtumishi au nabii mamlaka uliyo nayo kwa Mungu ni kubwa kuliko ya watawala
wa kisiasa, timiza kusudi la kazi uliyoitiwa bila kuogopa vitisho
Ndoto yako na maono yake
yasitishwe na mtu awaye yote.
Hatuishi duniani kwa kubahatisha
wala hatutimizi kusudi la kuweko kwetu kijinga, Mungu ndiye alpha na omega,
hatima ya maisha yetu haiku mikononi mwa mtu Fulani au kiongozi Fulani iko
mikononi mwa Mungu.
Wachawi ni Mbweha tu hawana
hatima ya maisha yetu, waganga ni mbweha tu, wambea ni mbweha tu, wazushi ni mbweha
tu, wafitinini mbweah tu, Kaaa katika kusudi la Mungu mtu awaye yote
asikutishe, Usiondoke katika kusudi lako la Utumishi, kusoma, kufanya biashara,
wokovu, malengo na mipango yako muhimu, ndoa yako na kadhalika, Kumbuka lolote
linalotaka kukutoa katika mpango wa Mungu ni Mbweha tu!
Ujumbe: Na Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote
kwa Mawasiliano, Maoni, ushauri na shukrani wasiliana nami:-
0718990796
0784394550
0626606608 SMS only
ikamote@yahoo.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni