Waebrania 1:1-3 “Mungu, ambaye alisema
zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho
wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena
kwa yeye aliufanya ulimwengu.Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa
ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya
utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;”
Utangulizi.
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu hufanya mawasiliano
yake na watu wake kwa njia nyingi na kwa namna mbalimbali, kama watu wa Mungu
watajifunza na kujua njia mbalimbali anazozitumia Mungu kuzungumza nao watakuwa
na amani kwa sababu watayajua mapenzi ya Mungu katika maisha yao, watu wengi
sana hujiuliza katika maisha nawezaje kujua kuwa jambo hili ni la Mungu au la?
Jibu lake ni rahisi tu utaweza kujua mapenzi ya Mungu endapo tu utakuwa na
ufahamu ni namna gani Mungu huwasiliana na watu wake, watu wengi nyakati za Biblia
waliweza kuyajua mapenzi ya Mungu kwa jinsi na namna walivyojua ni namna gani Mungu
anawasiliana na watu wake, Nyakati za Biblia watu waliyajua mapenzi ya Mungu
kwa sababu walizijua njia anazotumia kuzungumza nao.
Matendo 16:6-10 “Wakapita katika nchi ya
Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika
Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu
hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono
usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje
Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka
kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri
Habari Njema.”
Mungu huzungumza na wanadamu kwa njia nyingi
na kwa namna mbalimbali, anazungumza nasi kwa neno lake, katika maombi, kwa
Roho wake Mtakatifu, wakati wa maombi na ibada, lakini pia kupitia asili na
mazingira, watu, ndoto na maono, sauti ya ndani na hata sauti ya wazi, unabii,
manabii, ibadani na kadhalika, leo tutachukua muda kujifunza njia kadhaa ambazo
Mungu anazitumia kuzungumza nasi sawasawa na namna na jinsi zinavyofunuliwa
katika neno la Mungu yaani Maandiko matakatifu moja kwa moja, kujua njia hizi
kutatusaidia kuitambua sauti yake.
Mungu anazungumza nasi kwa njia mbalimbali.
1. Mungu huzungumza
nasi kwa sauti ya waziwazi – Kwa mujibu wa neno la
Mungu, tunathibitishiwa kuwa Mungu wakati mwingine huzungumza na wanadamu moja
kwa moja kwa sauti ya wazi bila kificho, Mungu huzungumza hivyo kama mtu
anavyozungumza na rafiki yake uso kwa uso na neno la Mungu linatufundisha hivyo
ona:-
-
Alizungumza hivyo na Musa Hesabu 12:6-8 “Kisha
akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, Bwana,
nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa
mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; Kwake
nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la Bwana
yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?”
-
Alizungumza hivyo na Adamu Mwanzo 3:9-12 “BWANA
Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako
bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani
aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza
usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa
matunda ya mti huo, nikala.”
-
Alizungumza hivyo na Abraham
Mwanzo 12:1-3 “BWANA akamwambia Abramu, Toka
wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi
nitakayokuonyesha;nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na
kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye
akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”
-
Alizungumza hivyo na Musa Kutoka 20:1-6 “Mungu
akanena maneno haya yote akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika
nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila
mimi.Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu
mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.
Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu
mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne
cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri
zangu.”
-
Alizungumza hivyo na Yoshua, Yoshua 1:1-3 “Ikawa
baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua, mwana wa
Nuni, mtumishi wa Musa, akasema, Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi,
ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi
niwapayo wana wa Israeli. Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu,
nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa.”
-
Alizungumza hivyo na Samuel, 1Samuel 3:8-10 “Bwana
akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi
hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita
yule mtoto. Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa,
akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli
akaenda akalala mahali pake. Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama
kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi
wako anasikia.”
2. Mungu huzungumza kwa
njia ya ndoto, Neno la Mungu linaonyesha pia mara kadhaa
Mungu akizungumza ujumbe wake kwa wanadamu moja kwa moja kwa njia ya ndoto,
Mungu hutumia njia hii kwa sababu wakati huu mwanadamu huwa katika wakati wa
utulivu na yeye kama Mungu hashindwi kuzungumza na watu wake wanapokuwa
wamelala, aidha Mungu huitumia njia hii kwa sababu mara kadhaa wakati wa mchana
tunakuwa katika shughuli zetu za kawaida na hivyo hutunyima muda wa utulivu wa kumsikiliza
yeye.
-
Alizungumza na Nebukadreza na kisha Daniel akaitafasiri ndoto yake –
Daniel 2:1-3 “Hata katika mwaka wa pili wa kumiliki
kwake Nebukadreza, Nebukadreza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika, usingizi
wake ukamwacha. Ndipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na
wasihiri, na Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake. Basi wakaingia,
wakasimama mbele ya mfalme. Mfalme akawaambia, Nimeota ndoto, na roho yangu
imefadhaika hata niijue tafsiri yake.”
-
Alizungumza na Yakobo kwa njia ya ndoto Mwanzo 28:10-15 “Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali
fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe
moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale
pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake
yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake.
Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu
baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na
uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na
mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa
zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila
uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata
nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.”
-
Alizungumza na Yusufu kwa njia ya ndoto - Mwanzo
37:5-11 “Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi
kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi
tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama,
na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake
wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi
kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto
nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na
tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na
ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je!
Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake
wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.”
-
Alizungumza na Sulemani kwa njia ya ndoto 1Wafalme 3:5 “Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya
usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe.”
-
Alizungumza na Yusufu mumewe Mariam kwa njia ya ndoto Mathayo 1:19-21 “Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki,
asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo,
tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa
Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho
Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye
atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”
-
Alizungumza na Mamajusi kwa njia ya ndoto Mathayo 2:11-12 “Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu
mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao,
wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane. Nao wakiisha kuonywa na Mungu
katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.”
3. Mungu huzungumza
kwa njia ya Maono – Maono hayatofautiani sana na ndoto, tofauti tu
ni kuwa Ndoto ni picha na mazungumzo yanayotokea usiku mtu akiwa amelala,
wakati maono ni picha na sauti zinazomtokea mtu wakati wa mchana akiwa katika
shughuli zake za kawaida, maandiko yamejaa mifano mingi pia ya watu waliotokewa
na maono au watu ambao Mungu alisema nao kwa njia ya maono mfano;-
-
Alizungumza na Musa kwa njia ya maono Kutoka 3:1-3 “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro
mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka
mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto
uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto,
nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya
makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei.”
-
Alizungumza na Kornelio Matendo 10:1-5 “Palikuwa
na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu
mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu
sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa
tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama
sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako
zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa,
ukamwite Simoni, aitwaye Petro.”
-
Alizungumza na Petro pia kwa njia ya maono Matendo 10:9-15 “Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia
mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana;
akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake
ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa,
inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi; ambayo ndani yake walikuwamo aina
zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani. Kisha
sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, Hasha,
Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia
mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi.”
-
Alizungumza na Paulo mtume na timu yake ya umisheni – Matendo 16:6-10 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na
Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia
wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia
wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia
amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie.Basi
alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa
tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.”
-
Alizungumza na Paulo huko Makedonia - Matendo 18:9-11 “Bwana akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali
nena, wala usinyamaze, kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu
atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji
huu. Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la
Mungu.”
4.
Mungu huzungumza kwa kutumia mawazo (trance) – Hali hii humtokea mtu akiwa katikati ya shughuli na usingizi au kuzimia
kwa muda (Half-conscious state)
ambao kwa kiyunani inaitwa “ekstasis”
moja ya mfano huu ni Jinsi Mungu alivyozungumza na Balaamu
-
Hesabu 24:3-6 “Akatunga mithali yake,
akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema; Asema,
yeye asikiaye maneno ya Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka
kifudifudi, amefumbuliwa macho; Mahema yako ni mazuri namna gani, Ee Yakobo,
Maskani zako, Ee Israeli!”
-
Hesabu 24:15-17 “Akatunga mithali yake
akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema, Asema,
yeye asikiaye maneno ya Mungu, Na kuyajua maarifa yake Aliye Juu. Yeye aonaye
maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho, Namwona, lakini si
sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya
enzi itainuka katika Israeli; Nayo itazipiga-piga pembe za Moabu, Na
kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia.”
5.
Mungu huzungumza kupitia sauti ya ndani – haya ni mawasiliano ya Mungu kwa mwanadamu bila ya sauti ya kusikika
inawezekana wakati unaomba Mungu anakupa muelekeo moja kwa moja kwenye moyo
wako au kupitia usomaji wako wa neno la Mungu au kupitia mawazo yako
anaingiza mpango wake na inakuwa sawa na nia yake
-
Wafilipi 3:15 “Basi sisi tulio wakamilifu na
tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lo lote, Mungu atawafunulia
hilo nalo.”
-
Wafilipi 2:13 “Kwa maana ndiye Mungu
atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake
Jema.”
6.
Mungu huzungumza nasi kwa kututokea – “Theophany” Hii ni hali
ya kutokea kwa kuonekana na kwa sauti ya Mungu kwa mwanadamu, kwa kitaalamu
Theophany neno la Kiyunani lenye misamiati miwili “Theo” yaani Mungu na
“Phainein” ambalo ni kuonekana, wakati makanisa ya ki Orthodox
wanapenda kutumia msamiati huu, makanisa ya kikatoliki ya magharibi wanatumia
neno “Epiphany” kwa hiyo ni tendo la Mungu kuonekana kihalisia huku
akiambatanisha na sauti ya wazi mfano:-
-
Kutoka 3:1-6 “Basi huyo Musa alikuwa
akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma
ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa BWANA
akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na
kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema,
Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki
hakiteketei.BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka
katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema,
Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama
ni nchi takatifu.Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu,
Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa
kumwangalia Mungu.”
-
Mwanzo 16:1-14 “Malaika wa BWANA akamwona
kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya
kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe
unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai.
Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono
yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala
hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi.Malaika wa BWANA akamwambia,
Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake
Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako. Naye atakuwa kama
punda-mwitu kati ya watu, mkono wake utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu
wote utakuwa juu yake, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote. Akaliita jina la
BWANA aliyesema naye, Wewe U Mungu uonaye, kwani alisema, Hata hapa nimemwona
yeye anionaye? Kwa hiyo kisima kile kiliitwa Beer-lahai-roi. Tazama, kiko kati
ya Kadeshi na Beredi.”
-
Mwanzo 18:1-3 “BWANA akamtokea Ibrahimu
karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana
wakati wa hari. Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama
mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema,
akainama mpaka nchi, akasema, BWANA wangu, kama nimeona fadhili machoni pako
nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako.”
7.
Mungu huzungumza kwa njia ya maandishi – Ziko nyakati Mungu huzungumza na watu wake kwa njia ya maandishi na
maandiko yaani neno lake linatuthibitishia hivyo, kwa mfano Mungu alimpa Musa
mbao mbili za mawe ambazo aliziandika yeye mwenyewe amri zake ili watu wake
wasome na kujikumbusha, lakini pia aliwahi kuzungumza na mfalme mkorofi kwa
kutumia kiganja cha mkono na kutafasiriwa na Daniel hii inaonyesha kuwa Mungu
anaweza kuzungumza nasi kupitia maandiko, lakini pia kupitia unabii ulioko
katika maandiko Mungu huzungumza nasi kuhusu mambo yajayo na mapenzi yake
aliyoyafunua kwetu.
-
Kutoka 31:18 “Hapo BWANA alipokuwa amekwisha
zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda,
mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda cha Mungu.”
-
Daniel 5:5-8 “Saa iyo hiyo vikatokea vidole
vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya
mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule
mkono ulioandika. Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha;
viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana. Mfalme akalia kwa
sauti kubwa, akaamuru waletwe wachawi, na Wakaldayo na wanajimu. Mfalme
akanena, akawaambia wenye hekima wa Babeli, mtu awaye yote atakayesoma maandiko
haya, na kunionyesha tafsiri yake, atavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na
kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atakuwa mtu wa tatu katika
ufalme. Basi wakaingia wenye hekima wote wa mfalme; lakini hawakuweza kuyasoma
yale maandiko, wala kumjulisha mfalme tafsiri yake.”
8.
Mungu huzungumza na watu kupitia matukio – Mungu anatumia matukio wakati mwingine pia kutoa ujumbe Fulani au
kufikisha ujumbe Fulani kwa njia ya uwazi kabisa kwa mfano wote tunakumbuka
tukio la kifo cha Anania na Safira, kifo cha Herode katika Matendo 12 na Uzza
na kadhalika vyote vilibeba jumbe kadhaa ambazo zinafundisha na kuonya na
kutujulisha mapenzi ya Mungu.
-
Matendo 5:1-11 “Lakini mtu mmoja jina lake
Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akazuia kwa siri sehemu ya thamani
yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume.
Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo
Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa
kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake
haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako?
Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaanguka,
akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya. Vijana wakaondoka,
wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika. Hata muda wa saa tatu
baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. Petro akamjibu,
Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo.
Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia,
miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe. Mara
akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa,
wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe. Hofu nyingi ikawapata kanisa lote
na watu wote walioyasikia haya.”
-
Matendo 12:20-23. “Naye Herode alikuwa
amewakasirikia sana watu wa Tiro na Sidoni; wakamwendea kwa nia moja, na
wakiisha kufanya urafiki na Blasto, mwenye kukitunza chumba cha mfalme cha
kulalia, wakataka amani; kwa maana nchi yao ilipata riziki kwa nchi ya mfalme.
Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika
kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni
sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa
sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.”
-
2Samuel 6:2-7 “Akaondoka Daudi akaenda
pamoja na watu wote waliokuwa naye, mpaka Baala wa Yuda, ili kulipandisha
kutoka huko sanduku la Mungu lililoitwa kwa jina, naam, jina la Bwana wa
majeshi akaaye juu ya makerubi. Wakaliweka sanduku la Mungu juu ya gari jipya,
wakalitoa katika nyumba ya Abinadabu, iliyoko kilimani; nao Uza na Ahio wana wa
Abinadabu wakaliendesha lile gari jipya. Wakalitoa katika nyumba ya Abinadabu
iliyoko kilimani, pamoja na sanduku la Bwana; na huyo Ahio akatangulia mbele ya
sanduku. Daudi na nyumba yote ya Israeli wakacheza mbele za Bwana kwa nguvu zao
zote, kwa nyimbo, na kwa vinubi, na kwa vinanda, na kwa matari, na kwa kayamba,
na kwa matoazi. Hata walipofika kwa uga ya Nakoni, Uza akalinyoshea mkono
sanduku la Mungu, akalikamata kwa maana wale ng'ombe walikunguwaa. Ndipo hasira
ya Bwana ikawaka juu ya Uza; naye Mungu akampiga huko kwa kosa lake; hata akafa
pale pale penye sanduku la Mungu.”
9.
Mungu huzungumza nasi kupitia uumbaji wa asili – Kwa ujumla uumbaji wa Mungu wa asili unatoa ujumbe Fulani kwa wanadamu,
unawafundisha kitu hata wale wanaokanusha kuwa hakuna Mungu, lakini unahimiza
sifa na utukufu wa Mungu kadiri unavyoufanyia uchunguzi uumbaji na kugundua
kuwa ufundi wote huu na fahari yake na mpangilio wake na utaratibu wake vyote
vinatangaza fadhili za Mungu na kutufundisha mambo mbalimbali, aidha Mungu
nanaweza kusema nasi kwa kutumia ndege wanyama na mimea yote ina ujumbe wetu
-
Zaburi 19:1-4 “Mbingu zauhubiri utukufu wa
Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake. Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa. Hakuna lugha wala maneno, Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. Katika
hizo ameliwekea jua hema,”
-
Matendo 14:16-17 “ambaye zamani zilizopita
aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe. Lakini hakujiacha pasipo
ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema, akiwapeni mvua kutoka mbinguni, na nyakati za
mavuno, akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha.”
-
Warumi 1:19 “Kwa kuwa mambo ya Mungu
yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia. Kwa
sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na
kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata
wasiwe na udhuru;”
10.
Mungu huzungumza nasi kupitia Malaika – Maandiko yamejaa matukio ya kishahidi yanayothibitisha jinsi na namna
Mungu anavyowatumia malaika kuleta ujumbe wake kwa wanadamu, kwa hiyo Mungu
husema nasi kupitia malaika au anaweza kusema nasi kupitia malaika
-
Mwanzo 19:1-3 “Basi, wale malaika wawili
wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona
akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi.Akasema, Bwana zangu, karibuni
nawasihi mwingie nyumbani mwa mtumwa wenu, mkalale, mkanawe miguu yenu, hata asubuhi
mwondoke na mapema mkaende zenu. Wakasema, Sivyo, lakini tutakaa uwanjani usiku
kucha. Akawasihi sana, nao wakaja, wakaingia nyumbani mwake. Akawafanyia
karamu, akawapikia mikate isiyochachwa nao wakala.”
-
Luka 1:26-31 “Mwezi wa sita, malaika Gabrieli
alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa
mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya
Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema,
Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili
ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika
akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama,
utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.”
-
Luka 2:8-11 “Na katika nchi ile ile
walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku.
Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote,
wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea
habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa
Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.”
-
Matendo 12:7-10 “Mara malaika wa Bwana
akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni,
akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika
akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia,
Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni
kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono.Na walipopita
lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini,
ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika
akamwacha.”
11.
Mungu huzungumza nasi kupitia dhamiri – Mungu amemuumba mwanadamu akiwa na dhamiri ambayo kimsingi inauwezo wa
kujua mambo mema na mabaya, dhamiri kwa vyo vyote vile ni zawadi ya Mungu,
mwanadamu hangeweza kuwa na uwezo wa kujua hili kuwa ni sawa na hili sio sawa
kama Mungu asingelikuwa aintumia dhamiri, kwa hiyo kupitia dhamiri mwanadamu
anaweza kuyajua mapenzi ya Mungu
-
Warumi 2:14-15 “Kwa maana watu wa Mataifa
wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na
sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao
waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia,
na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea;”
-
1Petro 3:16-17 “Nanyi mwe na dhamiri njema,
ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo
wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa
ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya.”
12.
Mungu huzungumza nasi kupitia miujiza – Miujiza hufunua uwepo wa
Mungu na nguvu za utendaji wa Mungu, Miujiza inasema na kutangaza au
kudhihirisha mamlaka ya kiungu na uthibitisho wa neno la Mungu na uweza wake wa
kutimiza ahadi
-
Marko 16:20 “Nao wale wakatoka, wakahubiri
kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa
ishara zilizofuatana nalo.] ”
-
1Wakorintho 2:4-5 “Na neno langu na kuhubiri
kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa
dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu,
bali katika nguvu za Mungu.”
-
Matendo 4:13-17 “Basi walipoona ujasiri wa
Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa,
wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu. Na wakimwona yule
aliyeponywa akisimama pamoja nao hawakuwa na neno la kujibu. Wakawaamuru kutoka
katika baraza, wakafanya shauri wao kwa wao, wakisema, Tuwafanyie nini watu
hawa? Maana ni dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya kwamba ishara
mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana.Lakini neno hili lisije likaenea
katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa jina hili.”
13.
Mungu
huzungumza kupitia Urimu na Thumin – Nyakati za agano la kale
ilikuwepo njia ya kuweza kuuliza kwa kuhani ili mtu aweze kuyajua mapenzi ya
Mungu, vyombo viwili kama coins vilivyokaa kifuani mwa kuhani vilisaidia kuwajulisha
watu mapenzi ya Mungu, hii urimu na thumim pia inafananishwa na kupiga kura
Mungu anaweza kuonyesha mapenzi yake kwa kupiga kura ni kama tu uchaguzi huo utakuwa huru na
haki
-
Hesabu 27:20-21 “Nawe utaweka juu yake
sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii.Naye
atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu
mbele za Bwana; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na
wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia.”
-
1Samuel 14:41-42 “Kwa hiyo Sauli akamwambia
Bwana, Mungu wa Israeli, [Kwani usimjibu mtumishi wako leo? Ikiwa dhambi i
ndani yangu, au ndani yake Yonathani mwanangu, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, utoe
Urimu; bali ukisema hivi, Dhambi i katika watu wako Israeli,] utoe Thumimu,
Basi Yonathani na Sauli wakatwaliwa, lakini watu wakapona. Basi Sauli akasema,
Sasa piga kati ya mimi na mwanangu Yonathani, [naye awaye yote ambaye Bwana
atamtwaa, atakufa. Nao watu wakamwambia Sauli, La! Sivyo hivyo; lakini Sauli
akawaweza watu. Nao wakapiga kati ya yeye na mwanawe Yonathani,]”
-
Matendo 1:23-26 “Wakaweka wawili, Yusufu,
aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya. Kisha wakaomba,
wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani
uliyemchagua katika hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu,
alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe. Wakawapigia kura; kura
ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.”
14.
Mungu huzungumza kwa njia ya kufungua mlango au
kufunga – wakati mwingine sauti ya Mungu huambatana na
kufunguka kwa mlango fulani au kufunga kwa mlango fulani, hapa tunazungumzia
nafasi, tunazungumzia mpenyo, tunazungumzia, njia iliyo wazi kwa sababu
tunaamini Mungu akizuia kitu hakuna anayeweza kukifungulia na Mungu akifungulia
kitu hakuna awezaye kukifunga, atakupa Amani au atakukosesha Amani ujue mapenzi
yake, hivyo kama yako mambo yamegoma katika maisha yako ujue Mungu ameweka
mkono wake endapo utakuwa umethibitisha kuwa sio shetani aliyezuia mpango wa
Mungu katika kusudia lako.
-
Isaya 22:22 “Na ufunguo wa nyumba ya Daudi
nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga
wala hapana atakayefungua.”
-
Ufunuo 3:8 “Nayajua matendo yako. Tazama,
nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa
kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”
15.
Mungu huzungumza kwa njia ya kuwa pamoja nasi – Mungu nanapokuwa pamoja nawe ni ishara ya kuwa uko katika sehemu muafaka
hata kama eneo hilo ni gerezani, au unakabliwa na magumu, Ishara ya kuwa Mungu
ana mpango wake na maisha yako ni kuwa pamoja nawe hata unapopita katika wakati
mgumu, na kule kuwa pamoja nawe kunaonyesha mapenzi yake, hivyo sio kila wakati
unapopita katika magumu huna Mungu au makuacha no.
-
Mwanzo 39:20-23 “Bwana wake akamtwaa Yusufu,
akamtia gerezani, mahali walipofungwa wafungwa wa mfalme, naye akawamo humo
gerezani.Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali
machoni pa mkuu wa gereza.Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote
waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye
aliyeyafanya.Wala mkuu wa gereza hakuangalia neno lililoko mkononi mwa Yusufu;
kwa kuwa BWANA alikuwa pamoja naye. BWANA akayafanikisha yote aliyoyafanya.”
-
Yoshua 1:2-5 “Musa mtumishi wangu amekufa;
haya basi, ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende
hata nchi niwapayo wana wa Israeli. Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za
miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa. Tangu jangwa hili na mlima
huu, Lebanoni, mpaka mto ule mkubwa, mto wa Frati, nchi yote ya Wahiti, tena
mpaka bahari ile kubwa upande wa machweo ya jua, hapo ndipo patakapokuwa mpaka
wenu. Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za
maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na
wewe; sitakupungukia wala sitakuacha.”
-
Isaya 41:10-13 “usiogope, kwa maana mimi ni
pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam,
nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote
walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe
watakuwa si kitu, na kuangamia.Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe;
watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu
yako. Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume,
nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.”
16.
Mungu huzungumza nasi kupitia watu – Mungu huwatumia watu kuzungumza nasi mapenzi yake katika hali ya kawaida,
anaweza kuweka Roho wake ndani yao wakatupa ujumbe, au kutufundisha kweli na
kututia moyo, katika historia ya kimaandiko mpaka leo bado tunaona Mungu
akiwatumia watu kusema nasi moja kwa moja juu ya mpango wake na mapenzi yake,
anawatumia wazee, wachungaji, walimu, manabii, wazazi, walezi, wapendwa
kuzungumza nasi moja kwa moja anaweza kutumia hata shuhuda zao na uzoefu wao na
wakasema nasi jambo na tukalifanyia kazi na likawa sawa na mapenzi ya Mungu au
tusipolifanyia kazi tukajikuta tunajuta
na kulia
-
Kutoka 18:13-24 “Asubuhi yake Musa akaketi
ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi
hata jioni. Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo
gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote
kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni? Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu
watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu; wakiwa na neno, hunijilia; nami
naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake.
Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema. Huna budi utadhoofika
wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako;
huwezi wewe kulitenda peke yako. Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na
Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe
umletee Mungu maneno yao; nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe
utawaonyesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya.
Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha
Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao,
wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi; nao
wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe,
lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata
nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe. Kwamba utafanya jambo
hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote
nao watakwenda mahali pao kwa amani. Basi Musa akasikiza neno la mkwewe,
akayafanya yote aliyokuwa amemwambia.”
-
2 Wafalme 6:1-4 “Kisha, wana wa manabii
wakamwambia Elisha, Angalia basi, mahali tukaapo mbele yako ni padogo kwetu.
Basi twende mpaka Yordani, twakuomba, tutwae huko kila mtu mti mmoja, ili
tujifanyie huko mahali pa kukaa. Akajibu, Haya! Nendeni. Mmoja wao akasema, Uwe
radhi, basi nakusihi, uende pamoja na watumishi wako. Akajibu, Nitakwenda.
Basi, akaenda pamoja nao. Nao walipofika Yordani, wakakata miti.”
-
Ruthu 3:1-5 “Kisha Naomi akamwambia mkwewe,
Je! Mwanangu, si vizuri nikutafutie raha, ili upate mema? Basi na huyu Boazi,
je! Siye wa mbari yetu, ambaye ulikuwapo pamoja na wasichana wake? Tazama,
usiku wa leo atakuwa akipepeta shayiri pale ugani. Basi wewe oga, ujipake
mafuta ujivike mavazi yako, kisha uende kwenye uga; walakini usijionyeshe kwake
mtu yule, ila atakapokwisha kula na kunywa. Nayo itakuwa wakati atakapolala,
utapaangalia mahali alalapo, nawe uingie, uifunue miguu yake ujilaze hapo; na
yeye atakuambia utakalofanya. Akamwambia, Hayo yote unenayo mimi nitayafanya.”
-
Matendo 21:10-13 “Basi tulipokuwa tukikaa huko
siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. Alipotufikia
akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu
asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye
mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa. Basi tuliposikia
haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu.Ndipo
Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha
ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake
Bwana Yesu.”
17.
Mungu huzungumza nasi kwa njia ya unabii – Mungu huzungumza na sisi kwa njia ya unabii ili kufunua mapenzi yake
kwetu, kutujenga na kututia moyo, unabii unajenga daraja kati ya Mungu na watu
wake, unabii hasa ni nini? Ni ujumbe unaoletwa na Mungu kupitia mtu aliyeokoka
kumuwezesha mtu huyo kupokea ujumbe kwa uweza wa Roho Mtakatifu na kuwaelezea
watu kile alichoambiwa na Mungu
Matendo 11:26-30 “hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa
muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi.
Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia. Siku zizo hizo manabii
walitelemka kutoka Yerusalemu hata Antiokia.Na tulipokusanyika akasimama mmoja
wao, jina lake Agabo, akaonyesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa
itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio. Na
wale wanafunzi, kila mtu kwa kadiri ya alivyofanikiwa, wakaazimu kupeleka
msaada kwa ndugu zao waliokaa Uyahudi.Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa
mikono ya Barnaba na Sauli.”
Mathayo 26:31-35 “Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili
yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi
watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.
Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa
kamwe. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo,
utanikana mara tatu. Petro akamwambia, Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe.
Na wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo.”
Hata hivyo unabii unapaswa kupimwa kama ilivyo kwa ndoto na maono na
sauti nyinginezo lazima zipimwe kama ujumbe unatoka kwa Mungu, mwanadamu au
shetani, sio hivyo tu upimwe kama unaendana sawasawa na neno la Mungu, upimwe
kama unamtukuza Kristo, upimwe kama unatuletea hofu au utatujenga, unaleta mafarakano
Amani, unatugawa au unatuunganisha au ni ujumbe hasi au halisi, unabeba matunda
ya Roho yaani kuna upendo, Amani. Unachochea ukuaji wa kiroho na unatufaa na
kuendana na wakati husika kisha ukiisha kupimwa unaweza kukubalika kama ujumbe
wa kiungu kwetu
Mungu anazungumza nasi kwa njia Maalumu.
18.
Mungu anazungumza nasi katika neno lake – Biblia ni ufunuo kamili wa neno la Mungu na mapenzi ya Mungu kwetu hii ni
njia maalumu ambayo Mungu huitumia kuzungumza nasi, tunaweza kumjua Mungu na
mapenzi yake kwa kusoma Biblia na kutiwa moyo na kujengwa na kuyatii mapenzi
yake kila siku tunaweza kujifunza na kupokea kutoka kwa Mungu kupitia neno lake.
-
2Timotheo 3:16-17 “Kila andiko, lenye pumzi
ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza,
na kwa kuwaadibisha katika haki;ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa
apate kutenda kila tendo jema.”
-
Waebrania 4:12-13 “Maana Neno la Mungu li
hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili,
tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani
yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe
kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni
pake yeye aliye na mambo yetu.”
-
Warumi 15:4-5 “Kwa kuwa yote yaliyotangulia
kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya
maandiko tupate kuwa na tumaini.Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunia
mamoja ninyi kwa ninyi, kwa mfano wa Kristo Yesu;”
19.
Mungu anazungumza nasi kupitia manabii – Manabii walitumiwa na Mungu na wanaendelea kutumiwa na Mungu kwaajili ya
maonyo, na hukumu itakayokuja, pia kwaajili ya kufariji, kujenga na kutia moyo
na kutujuza mapenzi ya Mungu, kutia moyo uvumilivu kutoa maelekezo, maagizo,
amri na mambo Mengine kuhusu Mungu
-
Waebrania 1:1 “Mungu, ambaye alisema zamani
na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi,”
-
Hesabu 12:6-8 “Kisha akawaambia, Sikizeni
basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, Bwana, nitajifunua kwake
katika maono, Nitasema naye katika ndoto.Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa;
Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote;Kwake nitanena mdomo kwa mdomo,
Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi
ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?”
-
Yohana 9:29-30 “Sisi tunajua ya kuwa Mungu
alisema na Musa; bali yule hatujui atokako. Yule mtu akajibu, akawaambia, Hii
ni ajabu! Kwamba ninyi hamjui atokako, naye alinifumbua macho!”
20.
Mungu anasema nasi kupitia Yesu Kristo – Yesu Kristo ni ufunuo kamili wa Mungu na mapenzi yake, kila kitu kuhusu
Mungu upendo wake, wokovu wake na namna anavyowajali wanadamu kumefunuliwa
kwetu wazi kupitia maisha ya mwanae
mpendwa Yesu Kristo, lakini pia Yesu anaweza kumtokea mtu moja kwa moja na
kuwasilisha ujumbe anaoukusudia kwa mtu huyo
-
Waebrania 1:1-3 “Mungu, ambaye alisema
zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho
wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena
kwa yeye aliufanya ulimwengu.Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa
ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya
utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;”
-
Yohana 1:1-3 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno,
naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako
kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote
kilichofanyika.”
-
Matendo 9:1-6 “Lakini Sauli, akizidi kutisha
na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua
za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii,
waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Hata alipokuwa akisafiri,
ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni.
Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi?
Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.
Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.”
-
Matendo 23:11 “Usiku ule Bwana akasimama
karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia
habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.”
21.
Mungu anasema nasi kwa Roho wake Mtakatifu - Anatajwa katika maandiko
kuwa anatuombea, ni msaidizi wetu, ni kiongozi wetu, ni Mwalimu ni mshauri kama
ilivyo kwa Mungu Baba na Mwana hawezi kufanya haya yote ndani yetu bila
mawasiliano na sisi
-
Yohana 14:16-17 “Nami nitamwomba Baba,
naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;ndiye Roho wa kweli;
ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali
ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.”
-
Yohana 16:7-15 “Lakini mimi nawaambia iliyo
kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi
hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.Naye akiisha kuja,
huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.Kwa
habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu
mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena; kwa habari ya hukumu, kwa
sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.Hata bado nikali ninayo
mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. Lakini yeye
atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa
maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena,
na mambo yajayo atawapasha habari yake.Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa
katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa
hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.”
-
Matendo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika
kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni
aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa
mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga,
Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.
Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha
waende zao.”
-
Matendo 16:6-10 “Wakapita katika nchi ya
Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika
Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu
hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono
usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje
Makedonia utusaidie.Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka
kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri
Habari Njema.”
-
Luka 2:25-34 “Na tazama, pale Yerusalemu
palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu,
akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa
ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa
Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto
Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe
alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu
mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu
wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa,
Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa
wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake.Simeoni akawabariki, akamwambia
Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio
katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.”
Hitimisho:
Hakuna jambo lenye faida kubwa sana kama
kumsikia Mungu akizungumza nasi, Mungu anapozungumza na wanadamu tunapata
muelekeo wa kina na wa ndani sana katika maisha, tunajua nini cha kufanya,
tunaelewa kipi cha kuchagua tunapata Amani, tunapata faraja, tunapokea maonyo,
tunaepushwa na hatari zisizoonekana , tunajengwa na kuimarishwa kiroho imani
yetu inakua, tunapata hekima, na mabadiliko makubwa ya Kiroho, hata hivyo ni
muhimu kukumbuka katika njia hizo zote ambazo Mungu anazitumia kuzungumza na wanadamu,
njia kuu zaidi ni NENO. njia hizo haziko kwaajili ya kulipuuzia neno la
Mungu wala kutufanya tujivune na kujifikiri kuwa sisi ni watu maalumu sana hapana,
Njia kubwa inayopendekezwa na neno la Mungu na Mungu mwenyewe ni neno la Mungu,
na nyingine zinaitwa makapi, hivyo unapojifunza jinsi, namna Mungu
anavyozungumza maana yake kila kitu kinapaswa kupimwa kwa NENO LA MUNGU ambalo
mwenyewe analisifia kuwa ni nyundo ivunjayo mawe vipande vipande.
Yeremia 23:24-29 “Je, mtu ye yote aweza
kujificha mahali pa siri, nisimwone? Asema Bwana. Je! Mbingu na nchi hazikujawa
nami? Asema Bwana. Nimesikia waliyoyasema manabii wanaotabiri uongo kwa jina
langu, wakisema, Nimeota ndoto; nimeota ndoto. Je! Mambo hayo yatakuwa katika
mioyo ya manabii wanaotabiri uongo hata lini, manabii hao wenye udanganyifu
katika mioyo yao wenyewe? Wanaodhania ya kuwa watawasahaulisha watu wangu jina
langu kwa ndoto zao, wanazomhadithia kila mtu jirani yake, kama vile baba zao
walivyolisahau jina langu, kwa ajili ya Baali. Nabii aliye na ndoto, na aseme
ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu.
Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. Je! Neno langu si kama moto?
Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?”
Isaya 55:6-11 “Mtafuteni Bwana, maadamu
anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu
asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa
Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa. Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala
njia zenu si njia zangu; asema Bwana. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu
sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo
yangu kuliko mawazo yenu. Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka
mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na
kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo
litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure,
bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”
Waebrania 4:12-13 “Maana Neno la Mungu li
hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili,
tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani
yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe
kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni
pake yeye aliye na mambo yetu.”
Na. Rev. Innocent
Samuel Kamote
Mkuu wa wajeni mwenye Hekima.
