“Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake
waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea.Yesu akawageukia, akasema, Enyi
binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu.
Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo
yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. Ndipo watakapoanza kuiambia milima,
Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika
mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”
“Kama wakitenda Mambo
haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”
Utangulizi:
Leo nataka tuchukue Muda
kutafakari kwa kina kuhusu usemi huu wa Yesu Kristo, Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti
mbichi, itakuwaje katika mkavu?”
Usemi huu ambao ni usemi mzito sana na unaweza kuwa mgumu katika
kuutafasiri kwa namna nyepesi nyepesi, Usemi huu ni usemi wa kitaaluma katika
maswala ya semi za “Marabbi” na “Manabii” Ni usemi mzito uliojaa unabii,
maana na maonyo na ndani yake kuna maana nzito sana ukilinganisha na mfumo wa
maisha ya sasa tuliyonayo katika ulimwengu, lakini vilevile katika maisha ya
kila mmoja wetu, Bwana na atupe neema kuuangalia usemi huu kwa undani, hata
tuweze kupata, maana inayokusudiwa! Na kujifunza kutoka kwa Mwalimu mkuu Roho
Mtakatifu!Katika jina la Yesu Kristo Amen.
Maana ya mti mbichi.
Mstari wa 31 Kwa kuwa wakitenda
mambo haya katika mti mbichi, - Kimsingi
mti mbichi unaotajwa hapa na Yesu ni mti mwema mti wenye kuzaa matunda “Productive tree” mti ambao unaonekana
kuwa una faida kubwa sana kibiblia mti huu unaitwa mti wa uzima angalia Ufunuo 2:7 “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili
ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa
uzima, ulio katika bustani ya Mungu”. Ufunuo 22:2 “Katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa
ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa
matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.”
14, “Heri
wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa
milango yake”. 19 “Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii
wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na
katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.”
Mti mbichi hapa unawakilisha Yesu Kristo, ambaye ndio mti wa uzima, wenye kuzaa
matunda, kupitia kazi ya ukombozi na huruma zake amekuwa akiwaponya watu na
kuwatendea mema, amekuwa mzuri na mwenye moyo mzuri, aliwafundisha watu neno la
Mungu kwa huruma zake, aliwalisha watu wenye njaa, aliwaponya wenye ukoma,
vipofu, walemavu na watu wenye shida na maatatizo ya aina mbalimbali, lakini
pasipo huruma wakuu wa makuhani walimkabidhi kwa askari wa Kirumi watu wa
mataifa wasiotahiriwa, ili wamsulubishe japokuwa Pilato hakuona dhambi yoyote
ndani yake, hakuwa na hatia yoyote Yesu hakutenda dhambi yoyote lakini
alifanyiwa tukio baya sana, alipigwa mijeledi, alitemewa mate, alivunjiwa
heshima, alifedheheshwa, alinyanyashwa, alivishwa taji ya miiba japo kuwa
alikuwa mwema Pilato alitoa hukumu ya kifo dhidi ya mtu ambaye mwenyewe
alihakikisha kuwa hana hatia, lakini alitendewa mambo yasiyofaa, Yesu alikuwa
akiwawazia mema, alikuwa akiwapenda, alikuwa akiwahurumia lakini aliteswa na
kudhulumiwa uhai wake vibaya pasipo hatia yoyote, Yesu kristo alimtii Mungu kwa
viwango vya juu zaidi hakuwa na dhambi Yohana 8;46 “Je, kuna ye yote miongoni mwenu awezaye
kunithibitisha kuwa nina dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini?”
Kama Yesu Kristo mti wenye faida wenye kuzaa matunda wenye kutii na
kutenda mema wenye kweli yote amepita katika wakati mgumu namna hii siku ya mtu
mbaya au mti mbaya kupita katika hukumu utakuwa ni wakati mbaya sana, ikiwa
watu wa Mungu wanaokoka kwa shida, asiye wa Mungu atapata taabu sana 1Petro 4:18 “Na
mwenye haki akiokoka kwa shida, Yule asiyemcha Mungu na mwenye dhambi
ataonekana wapi? ”
Maana ya Mti mkavu.
31.b Itakuwaje kwa mti mkavu –
Kwa upande mwingine mti mkavu inazungumzia kibiblia mti usio na matunda na mti
usiozaa matunda “un Productive tree”
unawakilisha watu wasiomcha Mungu, mti usio na faida mti usiozaa matunda au mti
usiozaa matunda mazuri Mathayo 3:10
“Na shoka
limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri
hukatwa na kutupwa motoni.”
Luka 13:7-9 “Akamwambia mtunzaji wa shamba
la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu,
nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu
nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La,
usipozaa, ndipo uukate”.
Mti mkavu unawakilisha watu
waiozaa matunda, watu wabaya wasiomcha Mungu, wenye dhuluma waliojaa wivu kama
mafarisayo na wakuu wa makuhani waliomsulubisha Yesu Kristo, pamoja na wote
waliokataa neema ya Mungu lakini pia kwa lugha ya kinabii mti mkavu ni nabii wa
uongo na mpinga Kristo.
Onyo kwa wanaomkataa Yesu!
Luka 23:27-31 “27.Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa
wakijipiga vifua na kumwombolezea. 28. Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za
Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. 29. Kwa
maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo
yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. 30. Ndipo watakapoanza kuiambia milima,
Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni.
Lakini vilevile katika jamii
tunao watu wenye nia mbovu wasio wema ingawa wakati mwingine unaweza kushangaa
watu wema wakafanyiwa vitu vibaya sana vya kusikitisha na ukajiuliza je
itakuwaje kwa watu wabaya, Muda unakuja kwa wabaya pia kuhukumiwa na hukumu yao
itakuwa mbaya sana, kama Mungu anaweza kumuadhibu mwana wake mpendwa Yesu, na
kumuacha achinjwe kama kondoo wa kafara na watu wema wakawa wanamlilia na
kumuhurumia Yesu aliwaonya kuwa afadhali waache kumlilia yeye na waanze kulia
na kuomboleza kwaajili ya watoto wao, Yeye kristo anauawa kwaajili ya faida ya
watakaomwamini, kifo chake ni ushindi dhidi ya adui zake, kifo chake kinaleta
uzima wa milele na wokovu kwa wote
watakaomwamini, kwa sababu hiyo hakuna sababu ya kulia na kuomboleza kwaajili
ya Kristo, lakini iko sababu ya kulia na kuomboleza kwaajili ya nafsi zetu na
watoto wetu hususani kama tutaikataa neema ya Mungu.
Hata hivyo kinabii vilevile Yesu
alikuwa akizungumza na wayahudi ambao wangeuawa na kuteswa vibaya na Warumi hao
hao miaka michache kwa sababu ya kumkataa Yesu wayahudi walijuta sana kile
ambacho Yesu alikuwa amewaonya kilitimizwa mwaka wa 70 BK. Ilikuwa ni kilio na
kusaga meno. Ni muhimu kukumbuka kuwa kama mti mbichi na mti mkavu itatiwa moto
ukweli ni kuwa mti mkavu utawaka na kuteketea na kusahaulika ukilinganisha na
mti mbichi.
Ni ukweli ulio wazi kuwa baada ya
Yesu kutabiri hili kwenye mwaka wa 33BK tunaelezwa katika historia kuwa mwaka
wa 70 BK yaani (70-33=37) yaani miaka 37 baada ya maneno ya Yesu Askari wa
kirumi waliizingira Yerusalem na kuwanza kuwaua wayahudi chini ya utawala wa
Kaisari TITUS baada ya uasi wa mwaka 66 Israel walipotaka kuwa na serikali
huru, Yerusalem uliharibiwa vibaya, Hekalu lilichomwa kwa moto na halikujengwa
tena mpaka naandaa ujumbe huu, wayahudi waliuawa kila upande chini ya Jemadari
aliyeitwa Tiberius Julius Alexander , Wayahudi waliuawa kijiji kwa kijiji na
kumalizikia katika kijiji kilichoitwa Masada ambako wayahudi walijiua wenyewe
wakikataa kwenda utumwani, hali ilikuwa mbaya sana na wayahudi walitawanyika
dunia nzima mpaka mwaka wa 1949 may walipopata uhuru na kujitangaza tena kama
taifa pekee la kiyahudi lililoko hadi leo, hii ilikuwa ni hukumu mbaya na yenye
kutisha kama alivyoonya Bwana Yesu.
Wito wa Kimungu unamtaka kila mtu
duniani atubu, ajirekebishe aache dhambi, ikiwa Mungu aliruhusu mwana wake
Mpendwa Yesu Kristo achubuliwe na kudhihakiwa na kufa kifo kibaya na cha aibu
Msalabani, huku kwa hakika hakuwa mwenye dhambi, alikuwa mti mbichi sembuse
mimi na wewe leo, tusiofaa kitu, tulio mti mkavu, Bila unyenyekevu na toba ya
kweli ni wazi kuwa hatutaweza kustahimili siku ya kuadhibiwa kwetu, ni lazima
kama taifa tutubu, tuache uovu, tuzae matunda unabii huuwa Yesu Kristo bado
unafanya kazi hata sasa kwa kila mtu na kwa kila Taifa, Kama humuamini Yesu
wewe hutaweza kustahimili Hasira ya
Mungu, angalia dhuluma, uonevu, wizi, uasherati,zinaa, mmommonyoko mkubwa wa
uadilifu ulioko kwa dunia ya sasa, uovu unapoonekana akama sifa ya kujivunia.
Mataifa yaliyoendelea yaliyokuwa
yanajulikana kama mataifa ya Kikristo mabunge na viongozi na hata wa kidini
angalia walivyopigwa upofu kuruhusu ndoa za jinsia moja, kutokukemea matendo ya
usagaji na ushoga, angalia mataifa ya Kiislam yasiyotenda haki na kuruhusu
injili ya Kristo kuhubiriwa kwao, au kuruhusu uhuru wa kuabudu, utapeli
uliokithiri na ufisadi hizi zote zinatufanya kuwa mti mkavu ambao hautaweza
kustahimili, Hukumu ya moto wa Mungu itakapofika, kukandamiza wanyonge, dhuluma
kwa wajane na yatima, dhuluma za mipaka ya mashamba na viwanja, dhuluma za hati
za nyumba na viwanja, vilio kila mahali, mauaji yenye utata haya yote utafika
wakati ambapo Mungu mwenye haki hatoweza kuyafumbia macho, siasa makanisani,
uchawi, na ushirikina kampenzi za kimwili nyakati za chaguzi hata za kidini,
kuonewa na kudhulumiwa kwa watu wema haya yote yanaandaa mti mkavu kuwashwa
moto.
“Kama wakitenda Mambo haya katika
mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?” Yesu aliwaonya kina mama wa Yerusalem kuwa
wasilie kwaajili yake bali walilie nafsi zao na watoto wao, Dunia nakutangazia
ni wakati wa kujililia na kuililia nafsi za watoto wetu, leo ni taabu ukizaa
mtoto wa kiume tabu ukizaa wa kike taabu
Mungu na aingilia kati na kuwaponya watu wake, usijifikiri kuwa wewe
utapenya, hakuna upenyo dhiki ya Yerusalem iliwapata wema na waovu, lakini
zaidi sana wale waliomkataa Kristo, Kama humuamini Yesu ndugu wewe ni mti
mkavu, kama ungali unaishi katika dhambi ndugu wewe ni mti mkavu na kama
wametenda yale kwa mti mbichi itakuwaje kwa mti mkavu? Kristo anasema siku ile watu watasema heri matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha,watu wataiambia milima na vilima tuangukieni na kutufunika bila toba hali hii inaweza kumkuta mtu awaye yote.
“Kama wakitenda Mambo
haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye
Hekima.