Jumapili, 25 Novemba 2018

Hata sasa Bwana ametusaidia!


1Samuel 7:12 “Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akisema, Hata sasa Bwana ametusaidia.


Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa wana wa Israel, waliwahi kupigwa vibaya sana na kusambaratishwa mbele ya adui zao, swalala Israel kushindwa lilikuwa swala la aibu kubwa sana katika maisha yao, Wao walitambua kuwa Mungu yuko pamoja nao na hivyo isingeliweza kuwa rahisi kwao kushindwa vita, lakini bilia inaonyesha kuwa Israel walipigwa vibaya na wazee walifikiri kuwa endapo watalileta sanduku la agano labda huenda wangeweza kupata ushindi hata hivyo safari hii walipigwa vibaya na hata sanduku la agano lilichukuliwa mateka
1Samuel 4:1-11 “[Ikawa siku zile Wafilisti walikusanyika ili kupigana na Israeli,] nao Waisraeli wakatoka juu ya Wafilisti kwenda vitani;wakatua karibu na Ebenezeri ,nao Wafilisti wakatua huko Afeki. Nao Wafilisti wakajipanga juu ya Israeli; na walipopigana, Israeli wakapigwa mbele ya Wafilisti; wakauawa watu wa jeshi lao lililokuwa uwandani wapata watu elfu nne. Hata watu walipofika kambini, wazee wa Israeli wakasema, Mbona Bwana ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Twende tukalilete sanduku la agano la Bwana toka Shilo hata huku, lije kati yetu, na kutuokoa katika mikono ya adui zetu. Basi wakatuma watu kwenda Shilo, nao wakalileta toka huko sanduku la agano la Bwana wa majeshi, akaaye juu ya makerubi; na Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwako huko pamoja na sanduku la agano la Mungu. Na sanduku la agano la Bwana lilipoingia kambini, Israeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikavuma. Nao Wafilisti waliposikia mshindo wa zile kelele, walisema, Maana yake nini mshindo wa kelele hizi kubwa katika kambi ya Waebrania? Wakatambua ya kuwa sanduku la Bwana limefika kambini. Wafilisti wakaogopa, maana walisema, Mungu ameingia kambini. Wakasema, Ole wetu! Kwani halijawa jambo kama hili tangu hapo. Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa na mkono wa miungu hawa walio hodari? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamisri kwa mapigo ya kila namna jangwani. Iweni hodari, na kufanya kiume enyi Wafilisti, msije mkawa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa watumwa wenu; fanyeni kiume, mkapigane nao. Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu. Hilo sanduku la Mungu Likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa.”
Unaweza kuona tukio hili la kusikitisha ambalo lilitokea kabla Samuel hajawa Mwamuzi wa Israel, lilikuwa tukio la kusikitisha na lililoleta simanzi kubwa sana kwa wana wa Israel, jambo hili liliwapa kujitafakari kwa nini wamepoteza ushindi katika maisha yao! Israel waligundua siri ya kushindwa kwao vibaya katika vita hii na hivyo chini ya Samuel walijipanga tena kuutafuta uso wa Mungu wa Israel, kwani sababu ilikuwa wazi kuwa kushindwa kwao kulitokana na maisha yao ya kuabudu miungu na kumuacha Mungu wa kweli, sasa Israel walitambua kuwa wamekosa na hivyo walianza kutafuta ushindi. Kanuni za ushindi.

Mungu aliweza kuwajilia tena baada ya kufuata kanuni kadhaa na kuweza kuwasaidia na kuwapa Ushindi.
1Samuel 7:3-12Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia Bwana kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee Bwana mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti. Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia Bwana peke yake. Samweli akasema, Wakusanyeni Israeli wote Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa Bwana. Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za Bwana; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia Bwana dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa. Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, mashehe wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti. Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia Bwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti. Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea Bwana sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia Bwana kwa ajili ya Israeli; Bwana akamwitikia. Hata Samweli alipokuwa akiitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti wakakaribia ili kupigana na Israeli; walakini Bwana akapiga ngurumo, mshindo mkubwa sana, juu ya Wafilisti siku ile, akawafadhaisha; nao wakaangamizwa mbele ya Israeli.Nao watu wa Israeli wakatoka Mispa, wakawafuatia Wafilisti, wakawapiga, hata walipofika chini ya Beth-kari. Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akisema, Hata sasa Bwana ametusaidia. Hivyo Wafilisti walishindwa, wasiingie tena ndani ya mipaka ya Israeli; na mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Wafilisti siku zote za Samweli. Nayo miji ile Wafilisti waliyokuwa wamewapokonya Waisraeli ilirudishwa tena kwa Israeli, tokea Ekroni mpaka Gathi; na Waisraeli wakauokoa mpaka wake mikononi mwa Wafilisti. Tena kulikuwa na amani kati ya Israeli na Waamori. Naye huyo Samweli akawaamua Israeli siku zote za maisha yake.”
Unaweza kuona Israel walipata ushindi mkubwa baada ya kuchukua hatua za kurejea katika kanuni za kimungu zilizowapa ushindi.
1. Waloimrudia Bwana kwa Moyo yaani walitubu na kuacha dhambi zao hususani za kuabudu miungu.
2. Walimtumikia Mungu yaani walimuabudu kwa moyo safi.
3. Waliteka maji na kuyamimina mbele za Bwana – kumimina maji ni lugha ya fumbo ambayo maana yake ni kuanguka chini na kuomba Zaburi 22:14 “Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu.” Hivyo Israel walianguka chini na kufanya maombi ya unyenyekevu yaliyoambatana na kufunga.
4. Walimuomba Samuel Nabii awaombeee kwa Mungu na kuwa asiache kuwa mwombezi katikati yao Samuel aliwaombea na Mungu alimjibu.
5. Kisha Maadui wa Israel waliinuka tena na safari hii walipigwa vibaya na kutolewa nje kabisa.
Ni ukweli ulio wazi kuwa Mungu aliwasaidia sana Israel, katika mji uleule mahali walipopigwa vibaya waliwashinda adui zao na kuwapiga vinbaya na kujikomboa, ni ukweli uliowazi kuwa Samuel alijua kuwa Mungu nsasa ameanza kuwasaidia watu wake, na alitaka kuweka kumbukumbu ya ushindi ule kwa jiwe alilolisimamisha na Kupaita mahali Pale EBEN-EZER yaani hata sasa Mungu ametusaidia.
Je maisha yako ni ya ushindi? Ni wapi umekwama Mungu anakupa nafasi ya kumrudia yeye na kuumimina moyo wako kwake, ni muhimu kukumbuka kuwa tunaye mwomnbezi, Yesu Kristo yeye ni Jiwe lililo hai, yeye ni muombezi wetu anatuombea na atatupa ushindi tukiwa naye hakuna kitu kitaweza kusimama mbele yetu, Israel waliwezakupata ushindi na adui hakuweza kusimama mbele yao siku zote za Samuel, Tunaweza kuwa na ushindi tukiwa na kuhani mwombezi aliyeketi mkono wa kuume wa Mungu baba naye anatuombea siku zote yeye ndiye kipatanisho kati yetu na Mungu, yeye ndiye chanzo cha ushindi wetu, Yeye ni Ebenezaer Jiwe la ushindi wetu, hata kama kulikuwa na historia ya kushindwa yeye Mungu wetu atatupa ushindi, na kuifuta historia ya kushindwa kwetu na kuwa ushindi wetu.
Na Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: