Jumapili, 25 Novemba 2018

Moto wa Kigeni!


Walawi 10:1-2Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni mbele ya BWANA, ambao yeye hakuwaagiza. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, nao ukawala, nao wakafa mbele za BWANA.”


Utangulizi:

Mojawapo ya matukio mazito ya kutisha ambayo yamerekodiwa katika Biblia hususani wakati wa agano la kale ni pamoja na tukio la kifo cha wana wa Haruni Nadabu na Abihu, Hili ni tukio lenye kutisha na kuogofya kama lilivyokuwa tukio la kifo cha Anania na Safira katika Agano jipya. Tukio hili kwa mujibu wa maandik lilisababishwa na tendo la Nadabu na Abihu kutoa Moto wa Kigeni mbele za Bwana, kutoa moto wa kigeni kuna maanisha nini hasa? Hili ndilo jambo la msingi na kuliangalia kwa undani na kujifunza katika nyakati zetu leo kuwa lina maanisha nini.

Maana ya Moto wa Kigeni.

Neno moto wa kigeni Katika Biblia ya kiebrania linatajwa kama “esh zarah” Kwa kiingereza “Alien Fire” yaani moto ulio tofauti na maagizo “Strange fire” Jambo ambalo liko kinyume na kawaida, Jambo lisiloagizwa, jambo lililo kinyume na mamlaka, Jambo lisilojali heshima au utukufu wa Mungu, tukio la aina hii ndilo limeitwa moto wa kigeni. Yaani wana wa Haruni walifanya jambo ambalo halikuagizwa na Mungu. Biblia ya kiingereza ya King James Version KJV na New American Standard Bible NASB yanatumia neno “Strange Fire” na Biblia ya kiingereza ya New International Version NIV inatumia neno “unauthorized fire” Kwa hiyo Mungu sio tu alikataa sadaka yao (Ibada yao) lakini aliwaangamiza kwa moto na kifo kwa kutokufuata maagizo yake.

Moto wa Mungu na Moto wa Kigeni.

Ni muhimu kufahamu kuwa Biblia imetaja aina mbili za Moto, kwanza kulikuwa na Moto uliotoka kwa Mungu na pili Nadabu na Abihu walitumia moto wa kigeni

Unaposoma maandiko katika Mambo ya walawi 9:22-24 “Kisha Haruni akainua mikono yake na kuielekeza kwa hao watu, akawabariki; kisha akashuka akisha isongeza sadaka ya dhambi, na sadaka ya kuteketezwa, na sadaka za amani. Kisha Musa na Haruni wakaingia ndani ya hema ya kukutania, kisha wakatoka nje, na kuwabarikia watu; na huo utukufu wa BWANA ukawatokea watu wote. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, na kuiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na yale mafuta juu ya madhabahu; watu wote walipouona huo moto wakapiga kelele wakainama kifudifudi.

Huu ulikuwa Moto ulioshuka kutoka kwa Mungu, Mto huu ulitokana na Musa na haruni pamoja na wanawe kufuata maelekezo yote ambayo Mungu alikuwa amewapa jinsi na namna ya kumuabudu, Moto huu ulileta Baraka kubwa sana kwa watu wa Mungu, Haruni kuhani mkuu aliwabariki watu, Mto huu uliposhuka watu waliuona walipiga kelele za utukufu kwa Mungu na waliinama na kumuabudu Mungu, Huu ulikuwa moto wa ushindi

Unaposoma maandiko Katika Mambo ya walawi 10:1-2 “Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni mbele ya BWANA, ambao yeye hakuwaagiza. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, nao ukawala, nao wakafa mbele za BWANA” 

Biblia haijaweka wazi kwamba Nadabu na Abihu walitumia aidha moto waliotumia walichukua kutoka nje au kama huu ulikuwa Moto uleule ambao ulishuka kutoka kwa Mungu lakini safari hii ulitumiwa na Nadabu na Abihu kwaajili ya kuwashia vyetezo vya kufukizia uvumba, Moto ukashuka kutoka kwa Munngu ukawaua nao wakafa, Moto huu ulisababishwa na Nadabu na Abihu kuasi na kutokufuata maelekezo ya Mungu na hivyo Haukuleta utukufu kwa Mungu na badala yake ulileta laana majuto na majonzi, ulikuwa ni moto wa hukumu, vyovyote vile kama walitumia moto wa Mungu au walitumia Moto kutoka nje ni wazi kuwa hawakuwa wanyenyekevu kutaka maelekezo kutoka kwa Mungu kwamba vyetezo vilipaswa kutumia moto wa aina gani, uwazi ni kuwa hawakuwa wamepokea maelekezo hivyo waliwasha moto usiamriwa na Mungu hawakufuata maelekezo,lakini pia kulikuwa na sababu kadhaa zifuatazo:-

Nabadu na Abihu waliuawa kwa sababu kadhaa zifuatazo za kibiblia.

1. Waliasi na kutokufuata maelekezo sahihi waliyopewa na Mungu na hivyo walishindwa kuonyesha heshima kwa Mungu Walawi 10: 3Ndipo Musa akamwambia Haruni, Jambo hili ni hilo BWANA alilolinena, akisema, Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu hao wote. Haruni akanyamaza kimya.”

2. Hawakumuheshimu Mungu; Walihudhuria ibada waliwa wamelewa na hivyo walishindwa kukumbuka maagizo ya Mungu kwa usahihi Walawi 10: 8-9 “Kisha BWANA akanena na Haruni, na kumwambia, Usinywe divai wala kileo cho chote, wewe, wala wanao pamoja nawe, hapo mwingiapo ndani ya hema ya kukutania, ili kwamba msife; amri hii itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyenu; kisha, mpate kupambanua kati ya yaliyo matakatifu na hayo yaliyo ya siku zote, na kati ya yaliyo najisi na hayo yaliyo safi;” Ni wazi kuwa tabia yao ya ulevi wa pombe na kuingia katika nyumba ya Bwana ndiko kulikopelekea wasitiikwa usahihi maagizo ya Mungu na Mungu aliwashughulikia kwa hukumu yenye kutisha iliyopelekea kufutwa kwao.

Fundisho:

Kwa kifo cha hukumu ya Nadabu na Abihu kwaajili ya Moto wao wa kigeni , Mungu anamfundisha kila mmoja wetu kuwa Mungu hakubalkiani na namna yoyote ya uasi na kuvunjamaagizo yake, Hatupaswi kuwa na kiburi na kujifikiri kuwa tuna hati miliki ya Mungu, Hakuna jambo baya duniani kama uasi, Biblia haikubaliana kabisa na uasi wa aina yoyote kwa sababu zozote zile, Mungu anataka atukuzwe na sisi au kupitia sisi katika mazingira yoyote yale, hakuna sababu yoyote ambayo inaweza kukubaliwa na Mungu ya kutufanya sisi tuasi, Hata kama tunaonewa Mungu yupo na atatulipia, lakini kuonewa kwetu kusiwe sababu ya kumuasi Mungu na kuacha Mungu atukanwe kupitia maisha yetu.

Mungu anaijua mioyo yetu vema Ni sadaka ya utii na unyenyekevu tu inayoweza kutuletea Baraka kutoka kwake na kuuleta utukufu wake, Lakini hatuwezi kumtolea Mungu Sadaka ya Kiburi na kutokutii kisha Mungu atuvumilie tu, Mungu huwapinga wenye kiburi na kuwapa neema wanyenyekevu, Tunaponyenyekea kwake na kumtii Mungu hutubariki na kutukubali, lakini linapokuja swala la Utukufu na Heshima yake Mungu hawezi kukubali kuona vinaharibiwa
Mungu anachukizwa sana na watu wasiofuata maelekezo yake , watu wasiofuata maelekezo ya Mungu maana yake wamekataa kuwa chini ya utawala wa Mungu na hivyo Mungu huwadhibu au kuwakataa.

1Samuel 15:22-23 “Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.” 

Popote pale unapoona watu wanachochea kuasi uongozi wa shule, au serikali, au wazazi au Mungu, au mamlaka fahamu kwa haraka kuwa hao wanatumia moto wa kigeni na kuwa hukumu ya Mungu haiko mbali, popote pale ambapo injili ya aina nyingine inahubiriwa na sio ile tuliyowahubiri mjue ya kuwa huo ni moto wa kigeni,Mafundisho potofu yaliyo kinyume na mpango halkisi wa Mungu ni moto wa kigeni, Mungu hatoruhusu Heshima yake iharibiwe kwa kufuata kile watu wanachokitaka na sio kile Mungu alichoagiza, Popote pale ambapo watu wanafungisha ndoa za jinsia moja au wanakubali kwa namna yoyote maswala ua ushoga na usagaji huo ni moto wa kigeni, Popote pale ambapo wanapinga watoto kuadhibiwa kwa fimbo, au walimu kushika fimbo kwaajili ya kuwaelekeza watoto sawasawa na neno la Mungu huo ni moto wa kigeni, ppopote pale wanapotumia mziki ambao sio wa kupiga moja kwa moja wakati wa kumsifu Mungu huo ni moto wa kigeni, popote pale ambapo watu wanaoongoza ibada wanavaa nusu uchi huo nao ni moto wa kigeni na utaharibu maisha yetu, utatuua hautaleta utukufu wa Mungu, kwetu utatunyima Baraka zilizokusudiwa kwetu, ni lazima tutubu kwa dhati na kumuomba Mungu atusamehe kila inapotokea mbegu ya uasi dhidi ya Mungu katikati yetu na kila linapotokea swala linalofanywa ambalo liko kinyume na Maagizo ya Mungu.

Musa alikuwa ni nabii aliyeheshimika sana na Mungu lakini Mungu hakumuachia aingie kanaani pale aliposhindwa kutii maagizo ya Mungu, ni lazima watu wa Mungu waogope kufuata maelekezo mengine ambayo sio ya neno lake.

Kumbukumbu 34:10 “Wala hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso;”

Pamoja na ukuu wote aliokuwa nao Musa aliadhibiwa vikali pale aliposhindwa kuyatii maagizo ya Mungu .

Hesabu 20: 7-13 “Bwana akasema na Musa, akinena, Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao. Musa akaitwaa hiyo fimbo kutoka mbele za Bwana kama alivyomwamuru. Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu? Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia. Bwana akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa. Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa Israeli waliteta na Bwana, naye alijionyesha kuwa mtakatifu kati yao”.

Mtu anayeweza kufurahia Baraka za Mungu kwa vyovyote vile atakuwa mtu yule ambaye anafuata maagizo ya Mungu na kuyashika vilevile bila kuangalia mkono wa kushoto au wa kiume, ni muhimu kukaza injili tuliyoipokea na kukaa katika utuu na maagizo ya Bwana, 

Joshua 1:5-8 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.” 

Mungu atupe neema leo kukumbuka kufuata maagizo ya Mungu na kuyatii katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth mwana wa Mungu aliye hai, Amen!

Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

0718990796

Hakuna maoni: