Mstari wa Msingi: Yeremia 1:19 “Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda;
maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe.”
Pichani ndege za Jeshi la Anga la
Israel (IAF) Israel Air Force tayari kwa
mashambulizi dhidi ya adui wa Israel
Utangulizi:
Nabii Yeremia alikuwa moja ya
manabii aliyepata ahadi nyingi sana za Mungu za kutia moyo, na sababu kubwa ni
kuwa pia alikuwa ni nabii aliyepitia changamoto nyingi sana katika maisha,
hususani upinzani mkubwa sana kwa ujumbe aliokuwa akiutoa, ambao kimsingi
haukuwa wake bali ulikuwa ni ujumbe kamili wa Mungu dhidi ya watu wake kwa
kinya cha nabii Yeremia.
Mungu mwenye upendo mwingi na
rehema alikuwa anajua wazi kuwa mtumishi wake atapitia changamoto, kubwa na
nyingi dhidi ya ujumbe wake wa kinabii aliokuwa anautoa ambao kimsingi
haungeweza kuwafurahisha watu wayahudi kwa vile huenda walidhani kuwa Yeremia
anatabiri kinyume na watu wa Mungu, mji wa Mungu na Hekalu la Mungu, aidha
alionekana kama anawatukuza wakaldayo ambao kimsingi walikuwa ni adui wa
Israelk na mataifa mengine.
Kutokana na ugumu wa kazi hii
mapema sana Mungu alimuahidi Yeremia kuwa atakuwa pamoja naye, Mungu kuwa
pamoja na Yeremia ulikuwa ni ujumbe wazi kuwa Mungu mwokozi wa wanadamu angekuwa
pamoja naye, hii ilieleweka wazi kwa Yeremia kuwa ushindi uko pamoja naye,
uwepo wa Mungu unapokuwa na mtu awaye yote ni vigumu sana kumshinda mtu wa
namna hiyo, Kama Mungu amesema mtu huyu niko naye tayari mtu huyo ni mshindi,
uwepo wa Mungu ni ushindi, uwepo wa Mungu ni ulinzi, uwepo wa Mungu bwana wa
majeshi ni ishara iliyowazi kuwa hata kuwe na jeshi kubwa namna gani
litasambaratika kabisa na hii ndio maana ya “ Immanuel” Isaya 7:14 “Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira
atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.” Unaweza
kuona Katika mstari wa Msingi Mungu alimuahidi Nabii Yeremia mambo ya msingi makuu matatu ambayo
anamuahidi kila mtu wake leo kama yeremia wa sasa au kama mtu unayepitia mambi
magumu au uko kwenye vita ngumu kama ile aliyokuwa akiipitia Yeremia.
1.
Watapigana
naye (au watashindana naye) Lakini hawatakushinda, watapigana nawe hii ina
maana ya Muungano mkubwa wa maadui, ya kwamba adui sio mmoja tu, wanaweza kuwa
wengi wanaweza kuwa ni timu kubwa ya watu walioungana kwa nia moja kuweza
kukufutilia mbali, na wewe unaweza kusalia peke yako, Hili lisikupe shida
lisikutese angalia Waamuzi 20:11 “Basi waume wote wa
Israeli walikutana pamoja juu ya mji huo, walikuwa wanashikamana pamoja kama
mtu mmoja.” Kuna wakati adui wataungana na kuwa kama mtu moja wakiwa
na lengo au kusudi la kupigana nawe hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Yeremia, Israel
na hata wewe pia lakini Mungu ameahidi kuwa
HAWATAKUSHINDA. 2Mambo ya nyakati 20:1- 15 “Ikawa
baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na pamoja nao baadhi ya Wameuni,
wakaja juu ya Yehoshafati vitani. Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati,
wakisema, Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng'ambo ya bahari;
na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio En-gedi).Yehoshafati akaogopa,
akauelekeza uso wake amtafute Bwana; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika
Yuda yote. Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute Bwana; hata kutoka miji yote
ya Yuda wakaja kumtafuta Bwana. Yehoshafati akasimama kati ya kusanyiko la Yuda
na Yerusalemu, nyumbani mwa Bwana, mbele ya ua mpya; akasema, Ee Bwana, Mungu
wa baba zetu, si wewe uliye Mungu mbinguni? Tena si wewe utawalaye falme zote
za mataifa? Na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu ye yote kusimama
kinyume chako. Si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele
ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Ibrahimu rafiki yako hata milele? Nao
walikaa humo, wamekujengea patakatifu pa jina lako humo, wakisema, Yakitujia
mabaya, upanga, hukumu, au tauni, au njaa, tutasimama mbele ya nyumba hii, na
mbele zako, (maana jina lako limo katika nyumba hii), na kukulilia katika shida
yetu, nawe utasikia na kuokoa. Na sasa, tazama, wana wa Amoni, na Moabu, na wa
mlima Seiri, ambao hukuwaacha Israeli waingie katika nchi yao, walipotoka nchi
ya Misri; lakini wakawageukia mbali, wasiwaharibu; tazama, jinsi wanavyotulipa,
wakija kututupa toka milki yako, uliyoturithisha. Ee Mungu wetu, je!
Hutawahukumu? Maana sisi hatuna uwezo juu ya jamii kubwa hii, wanaotujia juu
yetu; wala hatujui tufanyeje; lakini macho yetu yatazama kwako. Wakasimama Yuda
wote mbele za Bwana, pamoja na wadogo wao, na wake zao, na watoto wao. Ndipo
Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania,
Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya Bwana, katikati ya kusanyiko;
akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme
Yehoshafati; Bwana awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi
kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu.”
2. Hawatakushinda; Maana yake ni kuwa
hawataweza, hawatakuweza, yaani hata kama watatumia silaha kubwa na za kisasa
namna gani, yaani hata kama watatumia uchawi, yaani hata kama watajikita
na kuleketa watu waliobobea kiasi gani
Mungu ameahidi kuwa hawatakushinda Yeremia
15:20-21 “Nami
nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana
nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na
kukuponya, asema Bwana. Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami
nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha.” Unaweza kuona kumbe
hata adui awe mwenye kutisha kiasi gani Mungu ameahidi kutokoa na mikono ya
watu wabaya na kutukomboa kwa mkono wenye kutisha, licha ya ushindi mkubwa sana
Mungu atakaotupa dhidi ya adui zetu Pia mungu ameahidi kuwa watapata aibu
ambayo haitasahaulika hii ni kwa sababu
Mungu atakuwa pamoja nasi Yeremia 20:10-11. “Maana nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande
zote. Rafiki zangu wote, wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi
tutamshitaki, huenda akahadaika, nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake.
Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao
wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu
hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe.”
3.
Kwa
kuwa mimi nipo pamoja nawe: Siri kubwa ya ushindi ambayo kila muumini
anaweza kuwa nayo ni kwakuwa Bwana Mungu yuko pamoja naye Yeremia 1:8 “Usiogope kwa sababu ya hao maana
mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana.” Wakati wote Mungu
anapokuwa pamoja nasi uwepo wake unaleta ushindi katika maisha yetu, Mungu
anapokuwa pamoja nasi yeye anakuwa ndio ushindi wetu, na mlinzi wetu hatuna
budi kutembea kifua mbela tukijua kuwa Bwana yu pamoja nasi 2Timotheo 4:17-18 “Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia
nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie
Mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba. Bwana ataniokoa na kila
neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye
milele na milele. Amina.”
Hitimisho!
Ahadi hii kimsingi
haikuwa tu kwaajili ya Yeremia pekee, Ahadi hii ni agano kwa watu wote
wanaomtumaini Bwana, ni ahadi kwa Taifa la Israel na ni ahadi kwa kanisa na ni
ahadi kwa kila Mtu wa Mungu, Katika Israel wote tunakumbuka kuwa mara kadhaa
mataifa pinzani yanayoizunguka Israel wakiwahi kutaka kuifuta na kuikusudia
mabaya, Misri, Jordan, Lebanon, Syria na Iraq waliwahi kukusudia mabaya dhidi
ya Israel lakini walibamizwa vibaya na kusambaratishiwa mbali, watapigana nawe
lakini hawatakushinda, Ndugu mpendwa kama tunamtumaini Mungu na kutembea katika
uwepo wake hatupaswi kuogopa kitu, Hakuna atakayeweza kutushinda, hata kama
maadui wataungana na kuwa kundi kubwa la watu au jeshi kubwa litasambaratishwa
hatupaswi kuogopa kwa sababu tumemtumaini Mungu naye ametuahidi kuwa yuko
pamoja nasi ili atuokoe na wale waliotukusudia mabaya watotaoka wakiwa
wanatahayari, wamesambaratika, wamerudhishwa nyuma, Mpendwa liamini neno lake
uone kama Mungu ninayekuhubiri habari zake atakuaibisha, Muaminini Mungu
waaminini manabii wake ndipo mtakapothibitika.
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Rev. Innocent Kamote
0718990796/0781394550
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni