Zaburi
92:12-15 “Mwenye haki atasitawi kama mtende, Atakua
kama mwerezi wa Lebanoni. Waliopandwa
katika nyumba ya Bwana Watasitawi katika nyua za Mungu wetu. Watazaa matunda
hadi wakati wa uzee, Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi. Watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili,
Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu katika Hekima yake, huwa anatumia vitu
vyenye uhai na visivyo na uhai wakati mwingine kwa kusudi la kutufundisha
maswala kadhaa sisi wanadamu, Miti kadhaa katika Biblia imeweza kutumiwa na
Mungu kwa kusudi la kutufundisha mambo ya kiroho sisi wanadamu, Moja ya Mti
ambao umetajwa sana katika Biblia ni pamoja na mti ujulikanao kama Mwerezi
wa Lebanon, Mti huu unaheshimika sana na ni hazina kubwa sana ya dunia,
Taifa la Lebanon limeweka mti huu katikati ya Bendera yake kama alama kuu ya
uchumi wa taifa la Lebanon, Leo tutachukua Muda kuutafakari mti huu kwa kina na
kisha kujifunza Maswala kadhaa katika vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Ufahamu
kuhusu mti wa Mwerezi
·
Mambo ya
kujifunza kutokana na Mwerezi
·
Kustawi kama
Mwerezi wa Lebanon
Ufahamu kuhusu mti wa Mwerezi.
Ni muhimu kufahamu
kuwa miti katika biblia mara kadhaa imetumika kuwakilisha watu au taifa katika lugha
ya kinabii, na mara kadhaa imetumiwa katika biblia kumaanisha watu, mtu au
taifa au mataifa, Kwa msingi huo miti inapotumiwa katika biblia hutumika
kuwakilisha jamii ya watu au aina ya watu na sifa zao, Sifa za mti fulani
kulingana na jinsi ulivyo unaweza kutumika katika kufundisha sifa ya mtu au
watu kutokana na tabia na mwenendo wao mfano, Sifa za Mwerezi zinaweza kufanana
kwa kiwango fulani na sifa za Mpingo kwa hapa Tanzania kutokana na ugumu wa mti
huo unaotumika kuchongea vinyago, miaka kadhaa Nyuma kulikuwa na Band inaitwa
Mchinga Sound wakiwa na kiongozi wao Muumini Mwinjuma waliwahi kuimba na kusema
maneno haya “Mimi Kisiki cha mpingo wamekuja wenye shoka unakuja na panga
unajisumbua” akionyesha ugumu wa mti huo na uimara wake ndivyo ambavyo
Mwerezi nao ulikuwa na sifa zake katika maandiko na Mungu ameutumia kutufunza
maswala kadhaa muhimu katika maisha yetu ya kawaida nay a kiroho.
Waamuzi
9:7-15 “Kisha walipomwambia huyo Yothamu, yeye akaenda,
akasimama juu ya kilele cha kilima cha Gerizimu, akapaza sauti yake, akapiga
kelele, na kuwaambia, Nisikieni mimi, enyi watu wa Shekemu, ili kwamba Mungu
naye apate kuwasikia ninyi. Siku moja miti ilitoka ili kuutia mmoja mafuta uwe
mfalme juu yao; ikauambia mti mzeituni, Tawala wewe juu yetu. Lakini huo
mzeituni ukaiambia, Je! Niache mafuta yangu, ambayo kwangu mimi watu wamheshimu
Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti? Kisha miti ikauambia
mtini, Njoo wewe, utawale juu yetu. Lakini huo mtini ukaiambia, Je! Niuache
utamu wangu, na matunda yangu mazuri, niende nikayonge-yonge juu ya miti? Kisha
miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe, utawale juu yetu. Huo mzabibu nao ukaiambia,
Je! Niiache divai yangu, ambayo humfurahisha Mungu na wanadamu, ili niende
nikayonge-yonge juu ya miti? Ndipo hiyo miti yote ikauambia mti wa miiba, Njoo
wewe, utawale juu yetu. Huo mti wa miiba ukaiambia miti, Kwamba ninyi mwanitia
mafuta niwe mfalme juu yenu kwelikweli, basi njoni mtumaini kivuli changu; na
kwamba sivyo, na utoke moto katika mti wa miiba na kuiteketeza mierezi ya Lebanoni”.
Unaona
katika kisa hiki Yothamu anajaribu kuwaelezea watu kwa kutumia miti, kwa msingi
huo miti kibiblia inaweza kutumika kuwakilisha taifa au watu, au jamii au maana
ya tabia na mwnendo wa mtu mmoja mmoja utaweza pia kuona katika vikiwakilishwa
na miti;-
Luka
21:29-31”
“Akawaambia mfano; Utazameni mtini na miti mingine yote.
Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno
yamekwisha kuwa karibu. Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea,
tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu.”
Hapa Yesu alikuwa
analizungumzia Taifa la Israel na mataifa mengine kuwa yatakapoanza kupata
uhuru basi tuelewe kuwa Ufalme wa Mungu unakaribia, hii ina maana gani mtini
unawakilisha Taifa la Israel na miti mingine inawakilisha mataifa mengine, Kwa
msingi huo leo tutachukua Muda kuuchambua mti wa mwerezi wa Lebanon kisha
tutaanza kuona namna mti huo unavyotufundisha kitu katika maisha ya kiroho.
Mwerezi ni mti wenye historia katika nchi
ya Lebanon. Hujulikana
sana kama (Mti wa Furaha na Neema n- the joy and Grace tree)
hukua mpaka kufikia futi 130 hivi na
matawi yake hunyooka vizuri, ni wa kijani siku zote kwa muda wa mwaka mzima.
Mizizi yake huenda chini sana Hosea
14:5-6 “Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye
atachanua maua kama nyinyoro, na kuieneza mizizi yake kama Lebanoni. Matawi
yake yatatandaa, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake
kama Lebanoni” Inasemekana kuwa matawi ya muerezi hunyooka kwa mfano
wa pyramid na kukua mpaka kufikia futi 30-50 hivi.
Historia ya
mwerezi wa Lebanon inaanzia miaka mingi nyuma kabla Yesu hajazaliwa, kwa mfano katika Isaya 2:13 Unatajwa kama moja ya miti
mirefu duniani Isaya 2:13 “Na juu ya mierezi
yote ya Lebanoni iliyo mirefu na kuinuka, na juu ya mialoni yote ya Bashani”
Ni mti unaostahimili hali zote za hewa yaani za baridi kali na joto pia. Inadumu duniani kwa zaidi ya miaka 1000-2000 maisha yake.
Mwerezi
hukua taratibu sana na hivyo kuufanya kuwa mti wenye mbao imara. Kwa sababu hiyo mierezi ya Lebanon
imekuwa ikikatwa kwa wingi tangu enzi za mfalme Suleiman (na wafalme wengine pia) Wakati wa Mfalme
Sulemani aliitumia mierezi ya Lebanon katika ujenzi wa hekalu la Yerusalemu hivyo ni Mti utumikao au uliotumika Kujenga
Nyumba ya Mungu.
Mierezi ya
Lebanon imekuwa pia ikitumiwa na wenyeji wake kutengenezea mashua ambazo ziliwawezesha kuwa wafanyabiashara wa kwanza
wa kimataifa. Mti huu Mzuri wenye kukua kwa mfano wa Pyramid kwa umbile lake, pia mafuta yake hutumika kutengenezea
manukato na pia picha yake wengi wameitumia kutengeneza Cheni za namna
mbalimbali na kuzivaa shingoni kama ishara ya furaha, nguvu na kilele cha
mafanikio.
Hata hivyo kutokana
na ukataji uliokithiri, mierezi imekuwa michache sana katika nyakati hizi. Kwa
mfano kusini mwa Lebanon ni ngumu hata kuamini kwamba kuliwahi kuwa na misitu
yenye miti mikubwa na kuiletea sifa nchi ya Lebanon. Imebaki miti michache
katika maeneo ya kaskazini karibu na mpaka wa Syria.
Kutokana na
historia iliyotukuka ya mwerezi, mti huo umewekwa katikati ya bendera ya nchi ya
Lebanon na kuwa miongoni mwa alama muhimu za taifa la Lebanon.
Nyakati za
Biblia mbao ya mwerezi wa Lebanon ilikuwa ndio mbao imara na yenye ubora ambayo
ilikuwa haiwezi kuharibika kwa haraka, wala kushambuliwa na wadudu, Nchi ya
Lebanon ndio ilikuwa maarufu kwa aina hii ya miti na misitu ya mti huo
mashuhuri wa kifahari na imara, mti huu ni mti mzuri sana, ni mti unaosifiwa
kwa uzuri katika biblia unatajwa kama mti mzuri kuliko miti yote kiasi ambacho
miti mingine inauonea wivu na inatamani kuwa kama mwerezi
Ezekiel
31:3-9 “Tazama, Mwashuri alikuwa mwerezi katika
Lebanoni, wenye matawi mazuri, na kifuniko chenye uvuli, na kimo kirefu; na
kilele chake kilikuwa kati ya matawi mapana. Maji yalimlisha, vilindi
vilimsitawisha; mito yake ilipita pande zote za miche yake; naye akapeleka
mifereji yake kwa miti yote ya kondeni. Basi kimo chake kilitukuzwa kuliko miti
yote ya kondeni, na vitanzu vyake viliongezeka; matawi yake yakawa marefu, kwa
sababu ya maji mengi, alipoyachipuza. Ndege wote wa angani walifanya vioto vyao
katika vitanzu vyake, na chini ya matawi yake wanyama wote wa kondeni walizaa
watoto wao, na chini ya uvuli wake mataifa makuu yote walikaa. Basi hivyo
alikuwa mzuri katika ukuu wake, katika urefu wa matawi yake; maana mizizi yake
ilikuwa karibu na maji mengi. Mierezi ya bustani ya Mungu haikuweza kumficha;
misunobari haikuwa kama vitanzu vyake, na miamori haikuwa kama matawi yake,
wala bustanini mwa Mungu hamkuwa na mti wo wote uliofanana naye kwa uzuri.
Nalimfanya kuwa mzuri kwa wingi wa matawi yake; hata miti yote ya Adeni,
iliyokuwa ndani ya bustani ya Mungu, ilimwonea wivu.”
Mwerezi wa
Lebanon umetajwa katika Agano la kale mara kadhaa sehemu nyingi mara 103, unawakilisha Utajiri na ufahari,
Mfalme yeyote maarufu wa nyakati za Biblia alijenga nyumba yake kwa kutumia
Mwerezi, Daudi alitumia mierezi kujenga Ikulu yake
2Samuel 5:11, 7:2 ona 5:11. “Kisha Hiramu,
mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na
maseremala, na waashi; nao wakamjengea Daudi nyumba”. 7:2 “mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa
katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.”
Mfalme Daudi aliona kuwa anakaa
katika nyumba ya kifahari iliyojengwa kwa kutumia mierezi na aliona kwanini
Sanduku la Bwana Mungu wake lisijemgewe nyumba, Mierezi hali kadhalika
ilitumika katika ujenzi wa HEKALU
maana yake ya kiroho tutaiona baadaye
1Wafalme 5:6 “Basi uamuru wanikatie mierezi ya
Lebanoni; na watumishi wangu watafuatana na watumishi wako; na ujira wa
watumishi wako nitakupa kama utakavyosema; kwa kuwa wajua ya kwamba hakuna
kwetu mtu ajuaye kukata miti kama Wasidoni. Ikawa, Hiramu aliposikia maneno
yake Sulemani, alifurahi sana, akasema, Na ahimidiwe Bwana leo, aliyempa Daudi
mwana mwenye akili juu ya watu hawa walio wengi. Hiramu akatuma watu kwa Sulemani, akasema, Nimeyasikia
yale uliyoniletea; nami nitafanya kila ulitakalo katika habari ya miti ya
mierezi, na miti ya miberoshi”
Mierezi
ilitumika kujengea mahali pote ambapo Sanduku la agano la bwana lilipaswa kukaa 1Wafalme 6:15-19 “Akazijenga
kuta za nyumba ndani kwa mbao za mwerezi; toka sakafu ya nyumba hata boriti za
juu, akazifunika ndani kwa mti; akafunika sakafu ya nyumba kwa mbao za
mberoshi. Akajenga mikono ishirini pande za nyuma za nyumba toka chini hata juu
kwa mbao za mwerezi; naam, ndani akaijengea chumba cha ndani, yaani, patakatifu
pa patakatifu. Nayo nyumba, ndiyo hekalu la mbele, ilikuwa mikono arobaini. Na
ndani ya nyumba, mlikuwa na mwerezi ulionakishiwa maboga na maua yaliyofunuka
wazi; mlikuwa na mwerezi mahali pote; wala mawe hayakuonekana. Akaweka tayari
chumba cha ndani katikati ya nyumba ndani, ili atie humo sanduku la agano la
Bwana.”
Wakati wa
ujenzi wa Hekalu la pili pia baada ya hekalu la Sulemani kubomolewa bado tena
Mwerezi ulitumika kulijenga tena upya hekalu Ezra 3:7 “Tena waliwapa waashi na maseremala
fedha; wakawapa watu wa Sidoni, na watu wa Tiro, chakula, na vinywaji, na
mafuta, ili walete mierezi kutoka Lebanoni mpaka Yafa kwa njia ya bahari, kwa
kadiri walivyopewa ruhusa na Koreshi, mfalme wa Uajemi.” Kama mtu alikuwa na mierezi mingi sana ilikuwa
ni ishara ya mafanikio makubwa sana, Daudi na Sulemani mwanae walitumia mierezi
katika ujenzi na hasa mierezi ya Lebanon kwa sababu huko ndiko ilikokuwa
inapatikana mierezi iliyo bora zaidi.
Ukweli ni
kwamba Mierezi ni zawadi kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu, ni sihara ya
uzuri, nguvu na wema, Mierezi ya Lebanon iliitwa miti ya Bwana aliyoipanda
mwenyewe Zaburi 104:16 “Miti ya Bwana nayo imeshiba, Mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.”
Kwa hiyo ni
muhimu vilevile kukumbuka kuwa hatupaswi kuwa na majivuo na kiburi kwa jambo
lolote ambalo ni zawadi au karama kutoka kwa Mungu, kwa msingi huo kama watu
watajivuna kama mierezi Mungu ameahidi kuwa atawakatilia mbali, Mungu ana nguvu
kubwa sana na sauti yake inaweza kuivunjilia mbali Mierezi hakuna mwenye nguvu
kumshinda Mungu hivyo mierezi haipaswi kujivuna Zaburi 29:5 “Sauti ya Bwana yaivunja mierezi;
Naam, Bwana aivunja-vunja mierezi ya Lebanoni;”
Ni kutokana
na ubora na ufahari na uzuri wa mti huu Nchi ya Lebanon inayoongozwa na Rais
Mkristo, na waziri mkuu muislamu, wa madhehebu ya Suni na spika wa bunge
muislamu wa madhehebu ya shia kwa mujibu wa sheria na mikataba yao, utaweza
kuona bendera ya taifa hili na nembo ya rais wa nchi hii ina alama ya mti wa
mwerezi.
Mwerezi
Kuna mierezi
ya aina nyingi sana Duniani Lakini Mwerezi wa Lebanon ndio pekee unaoweza kukua
na kufikia futi zipatazo 130 aidha
mataiw yake hukuwa kwa umbile la mfano wa pyramid kwa ukubwa wa kati ya futi 30-50 na hivyo kufanya msitu mkubwa na
mzito unaotegemewa na ndege na wanyama mbalimbali ,ni mti mkubwa na mnene na
imara sana Isaya 37:24, “Umemshutumu Bwana kwa watumishi wako, kwa kuwa umesema, Kwa
wingi wa magari yangu nimepanda juu ya vilele vya milima, mpaka mahali pa ndani
ya Lebanoni; nami nitaikata mierezi yake mirefu, na misunobari yake mizuri,
nami nitaingia ndani ya mahali pake palipoinuka, palipo mbali sana, msitu wa
shamba lake lizaalo sana.” Kibiblia mtu mwenye haki anafananishwa na
Mwerezi wa Lebanon, Mizizi ya Mwerezi huenda chini sana na hivyo kuufanya mti
huu pia kuwa na uwezo wa kwenda juu mno, Ukuwaji wake unafananishwa na ukuaji
wa mtu imara kiroho kama jinsi mtu anavyokua na kufika katika cheo cha kimo cha
utimilifu wa Kristo, ukuaji wake unafananishwa na ukuaji katika Nyanja zote za
mtu wa Mungu, kukua katika imani, kuikulia neema ya Mungu, kukua katika
unyenyekevu, kukua kwa kujikana na utii kwa Mungu na katika kumjua Yesu Kristo,
na kujitoa katika kumuelekea Mungu na
kuutafuta uso wake, aidha Mwerezi ni mti ambao haufi na una uwezo mkubwa sana
wa kuvumilia joto na baridi hii ni sawa na hali ya mtu wa Mungu aliyemuaminifu
ambaye hawezi kuondoshwa katika imani linapokuja swala la kumtegemea na
kumuamini Mungu.
Mambo ya kujifunza kutoka kwa Mwerezi.
1. Unawakilisha
watu wanaostahili kuwa Nguzo katika nyumba ya Mungu.
Mwerezi ndio
mti pekee imara uliotumika wakati wa Sulemani katika ujenzi wa Hekalu la Mungu 2Nyakati 2:1-9,16, “Basi Sulemani
alikusudia kujenga nyumba kwa jina la Bwana, na kuujengea ufalme wake nyumba.
Sulemani akahesabu watu sabini elfu wawe wachukuzi wa mizigo, na watu themanini
elfu wawe wachongaji milimani, na elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao.
Sulemani akatuma watu kwa Hiramu mfalme wa Tiro,akisema, kama ulivyomtendea
baba yangu Daudi, na kumletea mierezi, ajijengee nyumba ya kukaa, unitendee na
mimi.Angalia, najenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wangu, ili kumfanyia
wakfu, ya kufukizia mbele zake fukizo la manukato, na ya mkate wa wonyesho wa
daima, na ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na za siku za sabato,
na za mwezi mpya, na za sikukuu zilizoagizwa za Bwana, Mungu wetu. Hili ni
agizo la milele kwa Israeli. Nayo nyumba nitakayoijenga ni kubwa; kwa sababu
Mungu wetu ndiye mkuu juu ya miungu yote. Lakini ni nani awezaye kumjengea
nyumba, ikiwa mbingu hazimtoshi, wala mbingu za mbingu? Nami ni nani basi, hata
nimjengee nyumba, isipokuwa kwa ajili ya kufukizia fukizo mbele zake?
Unipelekee basi mtu mstadi wa kazi ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya
chuma, na ya urujuani, na nyekundu, na samawi, mwenye kujua kuchora machoro,
pamoja na wastadi walioko Yuda na Yerusalemu pamoja nami, aliowaweka baba yangu
Daudi. Niletee tena mierezi, na miberoshi, na miti ya msandali kutoka Lebanoni;
maana najua ya kwamba watumishi wako hujua sana kuchonga miti Lebanoni; na
tazama, watumishi wangu watakuwa pamoja na watumishi wako, ili wanitengenezee
miti kwa wingi; kwani nyumba nitakayoijenga itakuwa kubwa ajabu.”
Bila Mierezi Hekalu la suleimani lisingeliweza kusimama na kudumu kwa muda mrefu
Mierezi inawakilisha watu wenye sifa watu walio karibu na Yesu wanaojua ufunuo
tofauti na wengine kuhusu Yesu, wenye siri za kipekee kutoka kwa baba kuhusu
Yesu, waliojengeka walio imara ambao wanaweza kuliimarisha kanisa hawa
wanafananishwa na mwerezi
Ufunuo 3:7-12
7. “Na kwa
malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye
mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala
hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye. Nayajua matendo yako.
Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye
kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala
hukulikana jina langu. Tazama, nakupa walio wa sinagogi la Shetani, wasemao
kwamba ni Wayahudi, nao sio, bali wasema uongo. Tazama, nitawafanya waje
kusujudu mbele ya miguu yako, na kujua ya kuwa nimekupenda. Kwa kuwa umelishika
neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa
iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi. Naja
upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako. Yeye ashindaye,
nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo tena
kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu
wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina
langu mwenyewe, lile jipya.” Petro, Yakobo na Yohana walikuwa ni
wanafunzi wa Yesu walioimarika kwa viwango vya juu zaidi na hivyo walihesabika
kuwa Nguzo katika kanisa la Kwanza
Wagalatia
2:1-9 “Kisha,
baada ya miaka kumi na minne, nalipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na
Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja nami. Nami nalikwenda kwa kuwa
nalifunuliwa, nikawaeleza injili ile niihubiriyo katika Mataifa, lakini kwa faragha
kwa hao walio wenye sifa, isiwe labda napiga mbio bure, au nalipiga mbio bure.
Lakini Tito aliyekuwa pamoja nami, naye ni Myunani, hakulazimishwa kutahiriwa.
Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri; ambao waliingia kwa
siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, ili watutie
utumwani; ambao hata saa moja hatukujitia chini yao, ili kwamba kweli ya Injili
ikae pamoja nanyi. Lakini wale wenye sifa ya kuwa wana cheo; (walivyokuwa vyo
vyote ni mamoja kwangu; Mungu hapokei uso wa mwanadamu); nasema, hao wenye sifa
hawakuniongezea kitu; bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa
injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa;(maana yeye
aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi
kwenda kwa Mataifa); tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na
Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa
kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;”
Wanafunzi wenye sifa kuwa ni nguzo, walikuwa na
ufahamu wa Tofauti na wanafunzi wa kawaida, walimfahamu Yesu kwa viwango vya
juu zaidi na Sauti ya Mungu baba waliwahi kuisikia kwa ukaribu na uwazi,
waliweza kujua ufunuo wa Torati na manabii, walimjua Musa na Eliya
Mathayo 17:1-5 “Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na
Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; akageuka
sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama
nuru. Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye. Petro akajibu
akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa
vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.
Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti
ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu,
ninayependezwa naye; msikieni yeye. Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka
kifulifuli, wakaogopa sana. Yesu akaja,
akawagusa, akasema, Inukeni, wala msiogope. Wakainua macho yao, wasione mtu ila
Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema,
Msimwambie mtu ye yote habari ya maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka
katika wafu.”
Yesu Katika Utukufu wake akitokewa na Musa na Eliya, Petro, Yakobo na Yohana wenye sifa kuwa ni Nguzo pekee walilishuhudia tukio hili.
Kwa sababu
hiyo ili mtu awe nguzo katika kanisa la Mungu, mitume hawakuruhusu awe mtu
alkiyeokoka hivi karibuni, viongozi katika kanisa la Mungu ni nguzo wanapaswa
kuwa watu wenye uzoefu wa kutosha katika wokovu, kisha baadaye ndipo wateuliwe
kuwa viongozi 1Timotheo 3:6 “Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka
katika hukumu ya Ibilisi.” Mwerezi hauwezi kuwa na manufaa unapokuwa
mchanga, ni Muhimu kufahamu kuwa Mungu anataka watu waluioshiba neno lake
waliojengeka kwenye neno lake ambao sio watu wa kuyumbishwa yumbishwa na kila
aina fulani ya upepo, watu wenye msimamo watu wagumu katika imani, walimmeza
Yesu watu ambao Yesu kristo ameumbika ndani yao kwa wingi, wasio na uchanga,
waliokomaa hawa ndio waaweza kufananishwa na mwerezi wa Lebanon.
2. Unawakilisha
watu wanaoweza kustahimili katika mazingira yote.
Tunaendelea
kuuchimba na kujifunza kuhusu mti huu wa Mwerezi wa Lebanon ambao kitaalamu
unaitwa “Cedrus Libani” mti huu una
sifa nyingi na za kipekee ni alama ya Utakatifu, Amani, uvumilivu na umilele,
ni mti ambao pia kwa mujibu wa mwanamashairi maarufu wa Ufaransa Alphonse de Lamartine aliuita mti huu
Mnara mashuhuri wa asili Duniani, hapa sasa nataka kuzungumzia sifa ya mwerezi
katika eneo la uvumilivu au kustahimili.
Tumeelezwa
wazi kuwa mti wa Mwerezi katika sifa zake unauwezo mkubwa sana wa kustahimili
hali zote yaani wakati wa Baridi na wakati wa joto, majani yake huwa ya kijani
wakati wote, kiroho unawakilisha watu wanaoweza kustahimili katika hali zote,
ni mfano wa watu wanaoweza kusimama na Mungu aidha hali ikiwa njema ama ikiwa
mbaya wana uwezo mkubwa wa kustahimili mabaya na uvumilivu na kumkubali Mungu
katika hali zote, manabii wengi wa bwana walikuwa watu wa namna hii Yakobo 5:10-1 “Ndugu,
watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya,
na wa uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya
subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema,
mwenye huruma”. Ayubu alikuwa ni mfano wa watu waliostawi kwa Mungu
katika hali zote.
Alikuwa
Tajiri mno lakini utajiri wake haukuweza kumfanya amuache Mungu, aliendeleza
ibada na kumtanguliza Mungu, Utafiti unaonyesha kuwa wako watu ambao maisha
yakifanikiwa huwa Mungu anakuwa hana maana tena, mafanikio yanawapelekesha
kiasi ambacho Mungu anakuwa hana maana Ayubu alikuwa tajiri lakini hakumuacha
Mungu aliendelea kushikamana naye wakati wa Raha ona Ayubu 1:1-5 “Palikuwa na mtu katika nchi ya
Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu,
ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha walizaliwa kwake wana
saba, na binti watatu. Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia
elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa
nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote
wa upande wa mashariki. Nao wanawe huenda na kufanya karamu katika nyumba ya
kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakatuma na kuwaita maumbu yao watatu ili
waje kula na kunywa pamoja nao. Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao
zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na
mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa;
kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru
Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote.” Lakini sio
hivyo tu hata wakati wa misukosuko bado Ayubu aliendelea kushikamana na Mungu,
hakuweza kusema kuwa nataachana na Mungu kwa sababu eti anapitia magumu, tena
wakati wa Ayubu hakukuwa na ufunuo kama tulio nao kuhusu shetani kwani Ayubu
alijua kuwa kila baya lililompata lilikuwa limetoka kwa Mungu, Mateso yote
yalitoka kwa ibilisi japo Mungu alimruhusu ili kuonyesha kwake kuwa Ayubu ni
mtu mwenye msimamo na anayeweza kustahimili mazingira yote.
·
Alipatwa na
majaribu mfululizo Ayubu 1:13-19 “Ilitukia siku moja
hao wanawe na binti zake walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya
ndugu yao mkubwa, mjumbe akamfikilia Ayubu na kumwambia, Hao ng'ombe walikuwa
wakilima, na punda walikuwa wakilisha karibu nao; mara Waseba wakawashambulia,
wakawachukua wakaenda nao; naam, wamewaua hao watumishi kwa makali ya upanga,
mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali
akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka
mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke
yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena,
akatokea na mwingine, na kusema, Wakaldayo walifanya vikosi vitatu,
wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watumishi kwa makali ya
upanga; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa
akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wanao na binti zako walikuwa
wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa; mara, tazama, upepo
wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba pembe zake nne,
nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi
tu, kukuletea habari.”
·
Ayubu ni mtu
aliyeteseka mno kuliko mtu awaye yote “Ayubu 3:24-
26, “Kwani kuugua kwangu kwaja kana kwamba ni chakula, Na
kunguruma kwangu kumemiminika kama maji. Maana jambo hilo nichalo hunipata,
Nalo linitialo hofu hunijilia. Mimi sioni raha, wala situlii, wala kupumzika;
Lakini huja taabu.”
·
Alipata maumivu makali kiasi cha kuchagua
kufa kuliko aina ya maumivu aliyoyapata Ayubu
7: 15, “Hata nafsi yangu huchagua kunyongwa, Na
kuchagua kifo kuliko maumivu yangu haya.”
·
Ayubu aliugua na kuoza na kutoa harufu kwa
majipu mabaya Ayubu 13: 28, “Nijapokuwa ni kama kitu kilichooza,
kinachosinyaa, Mfano wa nguo iliyoliwa na nondo.”
·
Kila mtu
aliyemjua Ayubu hakumuheshimu tena na kila mtu alimkimbia hata mke wake Ayubu
19:13-21, “Amewaweka ndugu zangu mbali nami, Na
wanijuao wametengwa nami kabisa. Watu wa mbari yangu wamekoma, Na rafiki zangu
niwapendao wamenisahau. Wakaao nyumbani mwangu, na vijakazi vyangu, wanihesabu
kuwa mgeni; Mimi ni mgeni machoni pao.
Namwita mtumishi wangu, wala haniitikii, Ingawa namsihi kwa kinywa
changu. Pumzi zangu ni kama za mgeni kwa mke wangu, Nami ni machukizo kwa ndugu
zangu. Hata watoto wadogo hunidharau; Nikiondoka, huninena. Wasiri wangu wote
wanichukia; Na hao niliowapenda wamenigeukia. Mfupa wangu unagandamana na ngozi
yangu na nyama yangu, Nami nimeokoka na ngozi ya meno yangu tu. Nihurumieni, nihurumieni,
enyi rafiki zangu, Kwa maana mkono wa Mungu umenigusa”
·
Ngozi ya Ayubu iliharibiwa vibaya alikata
tamaa Ayubu30: 16-18,27-30 “Sasa nafsi yangu inamwagika ndani yangu; Siku za mateso
zimenishika.Wakati wa usiku mifupa yangu huchomeka ndani yangu, Na maumivu
yanayonitafuna hayapumziki. Kwa ugonjwa wangu kuwa na nguvu nyingi Mavazi yangu
yameharibika; Hunikaza kama shingo ya kanzu yangu,
Matumbo yangu yatokota, wala hayaachi; Siku za taabu zimenijilia.Ngozi
yangu ni nyeusi, nayo yanitoka, Na mifupa yangu imeteketea kwa hari”
·
Hata pamoja na majanga haya yote jamaa
alisimama na kuendelea kumuamini Mungu aliamini kuwa Mungu yu hai nay a kuwa
atamtetea siku moja na kuwa hata bila mwili wake atamuona Mungu Ayubu 19:25-27 “Lakini
mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya
nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili
wangu nitamwona Mungu; Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu
yatamtazama, wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu” unaona
Ayubu hakuwa mtu wa kuyumbishwa na hali zinazomzunguka alikuwa imara alisimama
kama mwerezi aliweza kustahinili hali zote hiki ndio Mungu anachokitafuta kwa
watu wake watu wa namna hii atawafanya kuwa nguzo katika nyumba ya Mungu.
Bendera
ya Jeshi la Ulinzi la Lebanon kukiwa na alama ya mti wa Mwerezi!
Mungu anajivunia
watu ambao wanaweza kustahimili hali zote, Mapema Bwana Yesu alipokuwa
akiwafundisha wanafunzi wake katika hutuba ya mlimani alihitimisha mafundisho
yake kwa kuonyesha kuwa anataka watu imara ambao wataimarika kwa Mafundisho
yake kiasi ambacho hawataogopa Dhuruba za aina yoyote Mathayo 7:24-27 “Basi kila asikiaye hayo
maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga
nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma,
zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba.
Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu,
aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga;mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo
zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa”.
Unaweza kuona Mungu
anapendezwa na watu imara watu wenye msimamo wasioyumbishwa katika imani kwa
sababu zozote zile, Ayubu anatajwa kuwa mfano wa watu hao kwa sababu alipokuwa
na kitu alionyesha imani kwa Mungu na hata kila kitu kilipoondolewa kwake bado
alisimama na Mungu, hakuweza kuyumbishwa kwa sababu zozote zile Yeye alistawi
katika Mungu katika mazingira yote watu wa namna hii katika imani ni Mwerezi wa
Lebanon,
watu wenye uwezo wa kumzalia Mungu matunda wakati wote bila kujali
ni mazingira gani yanawazunguka Yesu alitoa mfano wa watu hao kama mbegu
iliyomea kwenye mnchanga ilihali wale wasiona uwezo wa kustahimili haraka sana
majaribu yakija wanashndwa kusimama na kunyauka
Mathayo 13:3-8,20-21 “Akawaambia mambo mengi
kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda.Hata alipokuwa
akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa
na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina; na jua lilipozuka
ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. Nyingine zikaanguka penye
miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; nyingine zikaanguka penye udongo mzuri,
zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. “Naye aliyepandwa penye
miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini
hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili
ya lile neno, mara huchukizwa.”
Kustahimili
misukosuko na majaribu lilikuwa mojawaponya somo muhimu nyakati za kanisa la
kwanza, mitume waliwaeleza wazi wakristo kuwa imetupasa kuingia katika ufalme
wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi mno Matendo
14:21-22 “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji
ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya
imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba
imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.”
Nyakati
za kanisa la kwanza somo kuhusu nustahimilivu ndio lilikuwa somo kuu, somo
kuhusu kustahimili majaribu lilikuwa somo muhimu sana ilikuwa ndio injili,
lakini nyakati za leo watu wanataka kusikia utapata upenyo, mambo yako
yatakunyookea, pokea na kadhalika, Mwerezi ni watu wanaoweza kushahimili
mazingira yoyote, Leo hii watu wanaweza kumuacha Mungu kirahisi tu, wanashindwa
kuwa wavumilivu, wanaweza kuacha wokovu kwa sababu zilizo nyepesi sana zisizo
na uzito, Mungu anataka watu imara watakaosimama katika hali zote, na
kulitukuza jina lake hata katika saa ya
kujaribiwa, lazima imani yetu iwe thabiti katika kiwango cha kuwa imara, iwe
unaumwa au la! Hali yoyote ile, uwe umeolewa au la lazima ufikie wakati
tukubaliane kuwa Mungu anabaki kuwa Mungu tu na tuendelee kumuadhimisha
tukisubiri kwa uaminifu.
3. Unawakilisha
watu wenye subira au uwezo wa kuvumilia kwa muda mrefu.
Moja ya
tatizo kubwa ambalo limewasumbua watu wengi, hususani kanisa ni tabia ya kukosa
Subira, mwerezi wa Lebanon ni mti unaosubiri na unaelewa kuwa utakuwa mti mrefu
sana kuliko miti yote, lakini haukui kwa haraka, unachukua muda mrefu kukua na
kufikia katika kilele kinachompa Mungu utukufu mkubwa huku ukiwa ni mti imara
sana, Mwerezi huwa haunung’uniki kupitwa na miti mingine kwa haraka kwa sababu
hatima yake huwa mrefu kuliko miti mingine kwa hiyo hauogopi kupitwa, kitaalamu
mti wa mwerezi unakawia sana kukua unakua polepole na mpaka uweze kufaidika nao
inachukua miaka mingi inasemekana kuwa kitaalamu mti wa mwerezi hukua kwa
kiwango cha sentimita 6-12 kwa mwaka
hiki ni kiwango kidogo sana cha ukuaji na ni cha polepole mno, kumbuka kuwa mti wa mwerezi unafananishwa na
mtu mwenye haki katika zaburi ile ya 92 na mtu mwenye haki maana yake ni wale
wanaomuamini Mungu, wakimtegemea yeye na kufuata ahadi zake na mausia yake hawa
ni watu wanaosimama imara katika imani kwa maizingira yote, wakiwezeshwa kwa
neema ya Mungu kustahimili magumu yote na mpaka wakifikia ngazi ya kuzaa
matunda na kuonyesha uzuri katika maisha na kuonyeshwa lile kusudi la Mungu
lililokusudiwa kwao utakuja kugundua kuwa wanachukua Muda mrefu mno, hii ina
maanisha kuna maswala mengine katika ufalme wa Mungu na katika maisha ya
ukristo yanachukua muda mrefu mno na inaweza kuwa safari ya taratibu sana kwa
kweli kama mtu hana subira huwezi kusubiria matunda na kufaidika na mwerezi
hata kidogo katika eneo hili tunajifunza nini yako maswala kadhaa ya
kujifunza:-
Ni muhimu
kuwa na ufahamu kwamba kama ungepanda miti ya mierezi mpaka uje unufaike na
matunda yake inachukua muda mrefu sana, wako watu Mungu anapowaita katiia neema
ya wokovu na hata katika neema ya kumtumikia Mungu wanahitajinsana kuvumiliwa
mpaka wafikie hatua ya kumtumiakia Mungu katika viwango bora zaidi, Hakuna
mtumishi mzuri wa Mungu katika biblia ambaye aliibuka tu kama mchicha wengi
iliwachukua Muda mrefu mpaka kuwa watumishi wenye kufaa, Mungu alichukuliana
nao sana katika maswala ya udhaifu, na taratibu, aliendelea kuwavumilia kisha
baadaye wakawa wenye kufaa
John Mark
ambaye ndiye Mwandishi wa injili ya Marko aliambatana na Barnaba na Paulo Mtume
katika safari ya kwanza ya umisheni na kutokana na ugumu wa kazi za kimisheni
alikata tamaa na kurejea nyumbani
Matendo
13:13 “Kisha Paulo na wenziwe wakang'oa nanga
wakasafiri kutoka Pafo, wakafika Perge katika Pamfilia. Yohana akawaacha
akarejea Yerusalemu.” Yohana anayetajwa hapa alijulikana pia kama
Yohana Marko na baadaye ndiye aliyekuja kuwa mwandishi wa injili ya Marko,
kutokana na kuwaacha wamisionari na kurejea nyumbani Paulo hakufurahi na hivyo
katika safari ya pili ya umisheni Paulo hakutaka kuambatana naye lakini Barnaba
alitaka kuambatana naye hivyo ilibidi safari ya kimisheni igawanyike
Matendo 15:36-40 “Baada
ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa
tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali
gani. Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao. Bali Paulo
hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini. Basi
palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko
akatweka kwenda Kipro. Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na
wale ndugu apewe neema ya Bwana.” Unadhani nini kilitokea hapa?
ilivyo ni kwamba Barnaba alikuwa Mchungaji alikuwa nimlezi na Marko alikuwa ni
kijana mdogo ambaye Mungu alikuwa amekusudia kuja kuandika injili, Marko
alikuwa na kama mwerezi unaokuwa polepole alikuwa na madhaifu mengi, alikuwa
bado mchanga alipaswa kulelewa na kukuzwa kwa huduma ya Kichungaji, Paulo
alikuwa Mwinjilisti alitaka watu walioandaliwa na waliokuwa tayari kwa kazi
hivyo Barnaba alikuwa anajua kuwa Bado Marko alihitaji muda, Barnaba alikuwa na
Roho ya uvumilivu na subira alifahamu kuwa akimpa Muda Marko atakuja kuwa na
faida kubwa katika ufalme wa Mungu, kumbuka kuwa ni barnaba huyuhuyu ndiye
aliyemlea Paulo Mtume na ndie aliyemleta Antiokia na ndiye aliyemtambulisha kwa
Mitume, Barnabas alikuwa mtu maarufu nyakati za kanisa la kwanza kwa sababu ya
kuwajali wengine na kuwalea katika huduma anaonekana kwa mara ya kwanza katika
Matendo 4:36-37 “Na
Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi,
asili yake ni mtu wa Kipro, alikuwa na
shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume”. Hapo
Barnaba ambaye aliitwa Yusufu alianza kujulikana kuwa alikuwa ni mtu wa namna
gani, na mitume ndio waliompa jina hilo la Baranaba kwa maana alaikuwa mwana wa
faraja, alikuwa ni faraja kuwa katika kanisa, alijitoa kwaajili ya wengine, na
sio hivyo tu aliweza kuwavumilia watu na hasa wale waliokataliwa au ambao watu
walikuwa hawawaelewi ona
Matendo 9:26-29
“Na Sauli
alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa
wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa,
akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba
alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la
Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. Akahubiri kwa
jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao
wakajaribu kumwua”
Unaweza kuona kazi ya Barnaba namna na jinsi
alivyokuwa mwenye uwezo wa kuvumiliana na kuchukuliana na kupitia yeye moja ya
mitume waliofanya kazi mno kuliko mitume wote alilelewa vema kiimani na Barnaba
hata watu walipoona shaka naye yeye alisimama kumtetea, lakini kama haitoshi
alipoenda kuchunga kanisa kule Antiokia, alienda mpaka Tarso kumtafuta
Sauli/Paulo na kumleta Antiokia kwa hiyo
ni wazi aliweza kuwa mvumilivu na mwenye subira dhdi yaw engine kwa muda mrefu
yeye ndio sababu kuu ya kuonekana kwa Paulo mtume ona
Matendo 11:19-26 “Basi
wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano,
wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa
Wayahudi peke yao. Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao
walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri habari njema
za Bwana Yesu. Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini,
wakamwelekea Bwana. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa
lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia. Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya
Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Maana
alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka
upande wa Bwana. Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; hata alipokwisha
kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja
na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo”
Ni Barnaba
huyuhuyu aliyemvumilia Paulo ndiye aliyekuwa sasa anataka kulea Marko ili aweze
kuja kuwa mwenye kufaa baadaye angalia sasa baada ya miaka kadhaa mbele 2Timotheo 4:11 “Luka
peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa
kwa utumishi.” Unaona Paulo mtume baadaye akiwa mtu mzima anasema
Umtwae Marko umlete pamoja nawe maana ananifaa kwa utumishi, ni yeye aliyeona
kuwa Marko hafai lakini sasa anamkubali kwa sababu ya kazi ya Barnaba ya
kuwavumilia watu.Marko huyu huyu ndiye ambaye alikuja kuandika injiliya Marko
tunayoitumia leo kama injili ya kazi
Kaka zangu
dada zangu maranyingi sana tumewahukumu watu kwa haraka kutokana na udhaifu wa
kibinadamu, tumewahukumu kutokana na uchanga wao, tukawadhani kuwa hawafai,
tumewahukumu kwa sababu wanaanguka kana kwamba sisi ni wakamilifu,
tumewahukumu, tumewakomesha watu kana kwamba sisi tunamiliki funguo za
Mbinguni, mara kadhaa tumewehesabu watu kadhaa kuwa watu waioweza kufiti tena
hatukujua kuwa watu hao ni Mwerezi unakua kidogo-kidogo na kuwa baadaye unakuja
kuwa mti mkubwa, lazima ifikie ngazi ya kuyafumbia macho maswala kadhaa kwa kuwasamehe
watu makosa yaoa na kuendelea kuwaamini katika nafasi zilezile badala ya
kuwaondoa na kuwatupilia mbali kama kiytu najsisi na kisichofaa ni lazima tuwe
na uvumilivu kwa watu wengine na kutoa muda wa Malezi, kama mama anavyolea
mtoto kwa uvumilivu katika hatua zote za kichanga, kukaa, kutambaa, kusimama,
kutembea, lugha na kusoma na kuandika mpaka mtu anakuwa mtu mzima na kutambua
uwezo wao na kuwasapoti katika maisha yao mpaka wanakuja kuwa watu wenye kufaa.
Barnaba
alikuwa na uwezo wa kuona uweza alionao mtu na kugundua umuhimu wao na hivyo
alitaka kuwapa nafasi kubwa mno, ili waweze kukua na kuja kuwa wenye kufaa
baadaye,
1Petro 5:13 “Mwenzenu mteule
hapa Babeli awasalimu, na Marko mwanangu.” Marko alifanya kazi na
mitume wakubwa na alipata habazi za Yesu kwa usahihi na kuja kuwa miongoni mwa
waandishi wanne maarufu wa injili, huku injili yake ikimtaja Yesu kama
mtendakazi, au mtumishi wa Mungu mkuum, Yule aliyedharauliwa na kukataliwa sasa
anakubalika na kutajwa katika nyaraka
Wakolosai 4:10 “Aristarko, aliyefungwa pamoja nami,
awasalimu; na Marko, mjomba wake Barnaba, ambaye mmepokea maagizo kwa habari
yake; akifika kwenu mkaribisheni.”
Nini
tunaweza kujifunza kutokana na Marko na uvumilivu uluofanyika kupitia Barnaba,
Mpaka baadaye Marko anaonekana kuwa mtu muhimu katika kanisa na mitume wanataka
kufanya naye Kazi?
1. Makosa tuliyoyafanya nyuma hayamaanishi kuwa
sisi tutakuwa wakosaji milele!, Ni mungu ndiye anayefanya kazi ndani yetu, yeye
anayeukuza mwerezi taratibu anamkuza kila mmoja wetu taratibu ili tumkaribie
yeye, kazi ya kubadili mwenendo wa Mtu haifanyi na sisi inafanya na Mungu, ni
lazima tuwaache watu na Mungu wao ili kumruhusu Mungu kufanya kazi ndani yao
yeye ataendelea na kazi ya utakaso taratibu mpaka yule aliyemuita aona kuwa
amefaa
2. Kama mtu akikosea asifikiri kuwa hawezi
kuendelea na huduma, Marko alikuwa kama sisi wengine miongoni mwetu lakini
lazima ikumbukwe kuwa wakati mwingine Mungu huchukua miaka kadhaa kutengeneza
mtu wake wanaweza kuanguka mara nyingi sana kabla hawajafaa kwa huduma na
baadaye wanakuwa watumishi wazuri.
3. Bado tunaweza kuwarejesha tena wale ambao
tuliwaondoa katika mioyo yetu au waliokosea katika maisha yao kwani huwezi
kujua watakuwa muhimu kiasi gani baadaye.
4. Hatujachelewa kuwasamehe wale waliotukosea,
sisi sote tunatenda dhambi, sisi sote tunakosea na Mungu ametuvumilia mara
kadhaa je si jambo jema tukiwavumilia na sisi wale waliotuudhi, wakati mwingine
mtu anaweza akakosea na sisi tukafikiri kuwa hafai tena? Je wewe ndio
unaebadilisha watu? Wewe ndio Mungu? Wewe ndio seremala wa Nazarethi? Je wewe ndiye
mfinyanzi?, wakati mwingine watu wanaweza kwenda miaka na miaka wakimuhukumu
mtu kwa kudhani kuwa yuko vilevile na wanadhani hawezi kubadilika, lakini hebu
tuwakumbuke na kuwarejeza uone kama hawatakushangaza !
Achilia
wacha kuukata huo mti, uache ukue kama unakuwa taratibu nani ajuaye baada ya
miaka kadhaa utakuwa mti mkubwa na Mrefu kama mwerezi na kutumika kama Nguzo
katika nyumba ya Mungu, Mierezi inachukua muda kukua kiroho, haina haraka
inakuwa taratibu huwezi kula matunda yake kama utakavyo, Viongozi wengi wa
kanisa wamejiweka katika kiti cha hukumu cha Mungu na kudhani ya kuwa Mungu
amemaliza na mtu fulani, au fulani ndio basi tena nataka nikukumbushe usihukumu
mtu wa Mungu, wengina wanaweza kufikiri kuwa mtu fulani hana maana kwao kabisa
kwa sababu tu amehama dhehebu lao, huu ni uchanga wa kiroho, mtu kuhama dhehebu
lako haimaanishi kuwa ameahama mwili wa Kristo, wala haimaanishi kuwa huwezi
kumita na kumtumia, watu wamekuwa wajinga kiroho kwa sababu ya mitazamo duni
isiyo ya kimungu wala kiimaandiko, watu ambao ni mwerezi wanao uwezo wa kuwavumilia
wengine!
Uvumilivu ni
moja ya tabia ya uungu inayoashiria kuwa sisi tumekomaa na kukua ni pamoja na
kuwa na tabia kama zile tabia za Mungu, na kumzalia Mungu matunda, matunda
ambayo sisi tunapaswa kuyazaa yanatajwa katika Wagalatia 5:22-23 “Lakini tunda la Roho ni
upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi;
juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”
Neno uvumilivu hapo au subira
kwa kiingereza linatumika neno longsuffering yaani uwezo wa kuvumilia
Katika
maisha haya lazima tukue na kuwa na uwezo wa kuvumilia, hatuwezi kusema kuwa
tumekomaa katika upendo kama hatuna uwezo wa kuvumilia 1Wakoritho 13:1-7 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina
upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.Tena nijapokuwa na unabii, na
kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza
kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote
kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo,
hainifaidii kitu. Upendo huvumilia,
hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na
adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii
udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote;
hutumaini yote; hustahimili yote.”
Unaona
maandiko yanasema upendo huvumilia, tena yanakazia huvumilia yote, kisha
anamalizia hustahimili yote, Katika safari ya kwenda mbinguni ni lazima tuwe
wavumilivu, huwezi kuwa Mchungaji, au mwinjilisti au mwalimu wa neno la Mungu
kama hauna uvumilivu, vongozi wengi wa kanisa na hata washirika wameumiza wengi
makanisani kwa sababu ya kushindwa kuwavumilia, Kama kuna jambo kanisa tunapaswa
kuliomba kuwa tuweze kuwa nalo ni uvumilivu long suffering hii haiji hivi hivi ni lazima uwezeshwe na
Mungu hivyo hatuna budi kumuomba Mungu atusaidie
Wakolosai 1:11 “mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa
kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na
uvumilivu pamoja na furaha;”
unaona Paulo analiombea kanisa pamoja
na mimi na wewe kwamba tutiwe nguvu kwa kadiri ya utukufu wa Mungu tuwe na
uwezo wa kusubiri na kuvumilia tukiwa na furaha anapozungumzia kuvumilia maana
yake kuwa na uwezo wa kuwavumilia wengine, tuwe na uwezo wa kujidhibiti sisi
wenyewe ili tusimkosee Mungu lakini vilevile tusimkosee Mungu kwa kushindwa
kuwavumilia wengine, Maandiko
yanaonyesha wazi kabisa kuwa hatupaswi kukasirika kwa haraka Mithali 14:29 “Asiye mwepesi wa
hasira ana fahamu nyingi; Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu”
ukomavu wa kiroho katika Kristo unapimwa kwa uvumilivu
4. Unawakilisha
watu wasioweza kutikiswa, Kuyumbishwa na kuchukuliwa na kila aina ya upepo.
Biblia
inaelezea namna na jinsi ukuaji wa Mwerezi ulivyo, mwerezi ni mti unaokuwa
polepole na hivyo mizizi yeke huweza kwenda chini sana na hivyo kuufanya mti
huu kurefuka na kwenda juu sana, Mungu anamtarajia kila mtu aliyeokolewa kukua
na kufikia hatua ya juu sana ya kilele cha ukuaji wake kumfikia yeye aliye juu
ambaye ni Yesu Kristo, Biblia imekazia sana juu ya ukuaji wa kiroho 1Petro2:2 “Kama
watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili
kwa hayo mpate kuukulia wokovu;” Mungu anataka tuukulie wokovu,
tusiwe watoto wachanga wa kiroho wanaochukuliwa na upepo wa kila nammna wa
Elimu
Waefeso 4:11-15 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na
wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;kwa kusudi la
kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo
ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana
Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha
utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku,
na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja,
tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua
hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo”
Unaona
Neno la Mungu linakazia kukua Kiroho, ziko “levels” viko viwango ambavyo mtu
anatakiwa kukua kiroho, anapaswa kukua kiasi ambacho hataweza kuwa kama unyasi
unaotikiswa na upepo, watu wasioyumba kama Yohana mbatizaji, ambaye alikuwa
tayari kuingia Gerezani kwaajili ya kusimamia ukweli, ambaye alikuwa tayari
kukatwa kichwa kwaajili ya kusimama katika kweli ambaye alisema ukweli.,
hakumumunya maneno linapokuja swala la kusimamia kweli ya Mungu, ni ukweli
usiokanushika kuwa Yohana mbatizazi hakuwa unyasi unaotikiswa na upepo
Mathayo
11:7-9 “Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza kuwaambia
makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi
ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi
mororo? Tazama, watu wavaao mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme. Lakini
kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii? Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii”
Nyakati tulizo nazo ni nyakati ambazo watu huchukuliwa chukuliwa tu na kila
aina ya upepo wa Elimu hawaifahamu kweli halisi ya neno la Mungu, watu wamekuwa
wenye kutikishwa huku na kule sababu kubwa ni kuwa watu hawatulii darasani na
kujifunza kuhusu Yesu, tumekuwa na watu ambao hawakimbilii mahali kwa sababu
kuna mwalimu mzuri anaifundisha kweli ya Mungu bali wanakimbilia mahali kwa
sababu kuna miujiza, wanakimbilia mahali kwa sababu watatabiriwa mambo kadhaa
katika maisha yao wamesahau kuwa Yesu aliagiza kuwafanya watu kuwa wanafunzi na
sio watu wa mikate yaani watu wanaofuata miujiza huku na kule, si unakumbuka
Yesu alisema enendeni makwafanye watu kuwa wanafunzi, na sio wakimbilia
maombezi, leo hii watu wamekuwa wakihamia kila kanisa badala ya kutulia na
kujifunza kweli ya neno la Mungu ili wakue kama mwerezi na wafikie hatua ya
kuwa walimu wa wengine, mwerezi hukua taratibu huzamisha mzizi yake chini na hivyo
huenda juu sana na hauwi kama unyasi unaotikishwa na upepo unaona?
Waebrania 5:11-14 “Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida
kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia.
Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita),
mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi
mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye
maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula
kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua
mema na mabaya.”
Ni lazima tukue na kukomaa kiroho katika ngazi
ambayo hatutaweza kutikiswa na mtu awaye yote, hatutaogopa kufa, hatutaogopa
mabaya, tutakuwa na kiwango kikubwa cha imani kiasi ambacho, tutakuwa tayari
hata kufa kwaajili ya Kristo, na hatutaweza kudanganywa kutokana na kuimarika
katika ujuzi wa neno la Mungu. Tutakuwa kama Nehemia aliyeweza kusimama imara
katika kazi ya Ujenzi wa ukuta wa Yerusalem ambaye alikuwa na uwezo wa juu sana
wa kupambanua maandiko na kuwashinda kina Tobia na Sanbalati watu waliosimama
kama mwerezi hawawezi kutikiswa na uzushi, wala uongo wala imani potofu
haziwezi kuwaondoa katika kweli ya Kristo., Watu wenye sifa hizi katika
maandiko ndio wanaitwa mwerezi wa Lebanon., Kanisa leo limekuwa likishabikia
wahudumu wa injili kuliko kumshabikia yeye aliyetufia msalabani, unapoona watu
wanashambikia madhehebu, wanayatukuza madhehebu yao kuliko Yesu, wanashabikia
wahudumu wa injili kuliko Yesu mwenyewe, ujue wao bado hawajakomaa, bado ni
wachanga bado wanatabia za mwilini, hawajakua kama mwerezi. 1Wakoritho 3:1-7 “Lakini,
ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni,
bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika
Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza.
Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya
mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya
mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja
asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si
wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao
mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji;
bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali
Mungu akuzaye”. Watu waliokomaa kama mwerezi hawana muda wa
kushabikia wahudumu wa injli, haraka sana wanakuwa wanajua nini wanachotakiwa
kukifanya wana ukomavu wa hali ya juu, hawajali elimu ya mtu au mahubiri ya mtu
bali wao wenyewe kwa uungwana wao nao huchukua muda kuyachunguza maandiko ili
waijue kweli bila kujali yanahubiriwa na nani Matendo 17:10-11 “Mara hao ndugu wakawapeleka
Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi
la Wayahudi. Watu hawa walikuwa
waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa
uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo
ndivyo yalivyo.” Watu wa Beroya wanatajwa kuwa walikuwa waungwana
maana yake wenye hekima, waliyapokea mahubiri ya Paulo mtume kwa uelekevu wa
moyo, lakinoi vilevile walichukua muda kuyachunguza maandiko ili wajue au waone
kama mambo hayo ndivyo yalivyo, wakristo wazuri wanaofanananishwa na mwerezi,
wanapaswa kuwa wanafunzi wa maandiko, wanayachunguza wanajifunza wanachimba,
haijalishi cheti alichokuwa nacho Muhubiri., Paulo mtume alikuwa Muhubiri wa
viwango vya juu sana lakini hata hivyo bado watu wa Beroya walikuwa na muda wao
wa kuyachunguza aliyoyahubiri walikuwa wakiyapima maneno yake kama yako sawa na
kile wanachokijua na kukiamini, kizazi cha leo hakina muda huo, waoa
wanakimbizana na maombezi, kila siku wanaombewa hawakui kiroho, hawafikii ngazi
ya kujua au kujifunza kuomba hata wakaomba wao wenyewe na hata wao wakatumiwa
na Mungu kuwaombea wengine, na kutatua matatizo yaw engine kwa sababu ya
uchanga miaka inaenda miaka inarudi unaombewa tu wewe utaombea lini, Nyakati
zaKanisa la Kwanza sio mitume tu waliofanya ishara na maajabu, na nkuombea
wagonjwa hata watu wa kawaida walifungua makanisa, walihubiri injili, walifanya
kazi sawa na zile mitume walizifanya kwa sababu walikuwa wakidumu katika
fundisho na kuwa na uwezo uleule au hata zaidi ya ule na kazi ya Mungu ikakua kwa
kasi sana angalia
Matendo 6:8 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu
na ishara kubwa katika watu.” Matendo 8:4-8 “Lakini
wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka
akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja
wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara
alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao,
wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa
furaha kubwa katika mji ule” Matendo 11:19-21 “Basi
wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano,
wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa
Wayahudi peke yao. Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao
walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri habari njema
za Bwana Yesu. Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini,
wakamwelekea Bwana”.
Unaona nyakati za kanisa la kwanza watu wa
kawaida walitumiwa na Mungu, walitumiwa kufanya miujiza, walitumiwa kugfungua
makanisa walitumiwa katika kuhubiri injili hawa walikua walikomaa na kuwa kama
mwerezi, mimi sipingani na huduma zozote za maombezi, lakini swali kubwa la msingi
ni kuwa nini kinafuata baada ya maombezi na unabii je watu wanakomaa? Watu
wanakua kiroho? Watu wanafanyika kuwa wanafunzi wa Yesu? Wanaomaa kiroho ama
wanakuwa watu wa kuombewaaaa na kutolewa unabiii mpaka kuibuka nabii mwingine?
Je watu wanapata nafasi ya kupambanua na kuyapima mafundisho, je wala
tunaowaendea ili kutupa msaada wana malengo ya kutuombea siku zote au
kutupeleke akatika ngazi za juu za kiroho na kuwa na ukomavu unataotu pelekea
sisi tuwe kama wao?
5. Unawakilisha
kilele cha ujuzi, ufahamu na hekima ya juu!
Ile tabia ya
ukuaji wa mierezi na kufikia hatua ya juu kabisa kuliko miti mingine iliufanya
mti huu kuitwa Mfalme wa miti yote, ukuaji wake na uwezo wake wa kuipita miti
mingine unawakilisha ujuzi, ufahamu, hekima na maarifa ya juu zaidi kwa
binadamu, hivyo mtu mwenye hekima pia huitwa mwerezi wa Lebanon
1Wafalme 4:30-33 “Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki,
na hekima zote za Misri. Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko
Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa
zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka. Naye akanena mifano elfu tatu, na
nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano. Akanena habari za miti tangu mwerezi
ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za
ndege, na vitambaavyo, na samaki”
Ujuzi wa
hali ya juu, ufahamu na hekima na maarifa katika kumjua Mungu hukufanya kuwa
kama mwerezi, Mungu anataka kila mtu aliyeokolewa ajae hekima awe na Hekima
Yakobo 1:5 “Lakini
mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa
ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.”
Wote tunajua kuwa katika agano la kale na agano jipya na katika maisha
haya hekima ni ya muhimu sana kila mahali walipo wenye hekima watatatua
matatizo na kuleta suluhu ya mahitaji ya watu na kwa jamii, Kigezo kikubwa cha kupata viongozi
ambao wangetatua tatizo katika jamii na kanisa ni watu waliojaa Roho Mtakatifu
na Hekima Matendo 6:3 “Basi ndugu,
chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na
Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili;” ni wazi kuwa Petro
alishakuwa na ujuzi uliowazi kuwa wenye hekima hutatua matatizo ya jamii, wenye
hekima wana mawazo ya juu kabisa yenye kuweza kuisaidia jamii, wenye hekima ni
kama mwerezi Sulemani alikuwa ni mfano
wa mti wa mwerezi kwa hekima aliweza kutatua matatizo magumu yaliyomkumba mtu
yeyote na hata kutoa suluhu ya kilicho nyuma ya maswali yake tunaelezwa kuwa
Malkia wa Sheba alikwenda na maswali magumu aliposikia Hekima ya Suleiman na
kila alichokiuliza kilijibiwa na kuzidi 1Wafalme
10:1-8 “Na malkia wa Sheba aliposikia habari za
Sulemani juu ya jina la Bwana, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo.Akaingia
Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu
nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akazungumza naye mambo
yote aliyokuwa nayo moyoni. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala
hakukuwa na neno alilofichiwa mfalme asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona
hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga, na chakula cha mezani pake, na watumishi wake
walivyokaa, na kusimamia kwao wangoje wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake,
na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana, roho yake ilizimia.
Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za
mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata
nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe
umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako,
na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima
yako.” Unaweza kuona namna na jinsi
ambavyo hakukuwa na neno lililofichika katika maisha ya Suleimani aliweza
kufumbua mafumbo yote na magumu yote malkia aliyokuja nayo Biblia ya kiingereza
The Amplified Bible inasema katika mstari wa kwanza b “SHE
CAME TO TEST HIM WITH HARD QUESTIONS”
Yaani alikuja kumjaribu kwa Maswali magumu, Lakini unaweza kuona
Sulemani akiyatatua, Ndio maana kwa uwezo alionao Yesu aliweka wazi kuwa yeye
ni mkuu kuliko Sulemani Mathayo 12:42
“Malkia wa
kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu
kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili
asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.”
Yesu ni mkuu kuliko Suleiman yeye ndiye aliyemuumba na ni yeye ndiye aliyempa
Hekima Suleimani, Kanisa na watu wa nyakati za leo lazima tumuombe Mungu atupe
hekima, watu wengi leo hujiita wachungaji, hujiita mitume, hujiita manabii,
hujiita wainjilisti na hujiita Wachungaji na walimu maaskofu na kadhalika
lakini nataka kuwakumbusha kuwa Yesu alisema anatuma manabii na wenye hekima Mathayo 23:34 “Kwa
sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi;
na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika
masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji;” Nashangaa kusikia Yesu
ametuma manabii na waandishi yaani walimu na wengine lakini sisikii wenye
hekima? Wako wapi? Kanisa la Mungu lazima liwe na “wise men” lazima liwe na wenye hekima, Bila shaka Yesu anawatuma
wenye hekima anataka watu wenye hekima na wakiwemo watatatua matatizo ya jamii
hawa wanaitwa Mierezi ya Lebanoni., Muda usingeliweza kutosha kueleza habari za
Stephano ambaye Hekima yake iliwaazidi wapinzani wa injili mpaka wakaona hakuna
njia nyingine zaidi ya kumuua tu, waligundua ni mtu hatari kwa dini ya
kiyahudi, aliwazidi kwa hekima mpaka wakamsagia meno Matendo 6:8-10 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo,
alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa
sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na
la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini
hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.” Wako watu wanadai kuwa Stefano aliuawa kwa kukosa Hekima
hii sio kweli, maandiko yanaonyesha alikuwa amejaa Hekima aliuawa na watu
wajinga ambao hawakutaka kuiamini kweli aliyoiweka mbele zao, watu wa masinagozi
ya kisomi kutoka SIGAGOGI LA MAHURU, SINAGOGI LA WAKIRENE (LIBYA), SINAGOGI LA
ISKANDERIA (MISRI), SINAGOGI LA KILIKIA na ASIA, Hawa wote walishindana kwa
hoja wakakutana na mtu mwenye hekima mwerezi akawashinda wakaamua kumuua,
Biblia hijasema alikuwa nabii, au alikuwa mchungaji lakini alikuwa mwenye
hekima kama alivyosema Yesu kuwa atatuma wenye hekima na watawaua! Je leo wako
wapi Mungu anataka mierezi ya Lebanon ili aifanye kuwa nguzo katika nyumba ya
Mungu, anataka watu wenye uwezo wa kutatua matatizo ya wakristo,watu wenye
majibu watu wenye ufumbuzi watru watakaosimama kama waamuzi wa maswala mbali
mbali ya wakristo, Watu wengi wa Mungu wameumizwa makanisani kwa sababu tu ya
viongozi wabovu waliokosa hekima, walioshindwa kutatua matatizo yao kwa usahihi,
wakiitwa watu wengi waliachana katika ndoa zao, wakiitwa wengi waliohama
makanisa yao, wakiitwa wengi hata watumishi waliohama madhehebu yao, wakiitwa
na kuulizwa wengi waliokutana na changamoto hii au ile utagundua nkuwa sababu
zake nyingi ni kukosekana kwa watu wenye hekima, Mungu anataka kanisa liwe nao
hao ni muerezi wataweza kuwaweka wakristo pamoja na kuzima migogoro mikubwa ya
kikanisa, na kesi nyingi za kijinga na za hovyo hovyo, Hivi majuzi hapa
Tanzania kulitokea vipande vya video vilivyokuwa vikidaiwa kuwa ni vya Askofu
wa Kanisa la Ufufuo na uzima ukweli jambo hili liliwagusa watu wengi na
liliumiza wengi na lingeweza kuleta madhara makubwa sana kwa mwili wa Kristo
lakini aluipotokea Askofu wa Kanisa la full Gospel na kufundisha kwa muda mfupi
tu “USIKUBALI MASHITAKA DHIDI YA MZEE” mgogoro ule ulipotelea mbali na kuyeyuka
kabisa hii ni kwa sababu mwenye hekima alisimama aliamua kesi na kuzima fukuto
kubwa na bila shaka Hata askofu wa ufufuo na Uzima alipata mani na kibali,
sababu kubwa ni nini hali ilikuwa mbaya kwa sababu kanisa limejaa wajinga
limejaa watu wasio na hekima wengi walikuwa waliunga mkono, wengi labda
wangetamani afadhali Gwahima aharibikiwe na sijui ingekuwa ni kwa faida ya nani
lakini kile kilichofanywa na Kakobe kama ni kuamua Kesi ilikuwa ni sawa na ile
kesi Suleimani aliiamua kwa wanawake waawili waliokuwa wanagombania mtoto hii
ndio faida ya kuwa na wenye hekima katika kanisa, Paulo mtume alihopji je
kanisa kule Koritho halina watu kama hao? Kwanini watu wa Mungu wapeleke kesi
zao mahakamani je kanisa linakosaje wenye Hekina mahalia ambapo Roho Mtakatifu
yupo wanakosekaje waru wenye hekima? Tunahitaji watu wa aina hii watakaofikia
kilele cha hekima na kuwa kama mwerezi, mwerezi unawakilisha watu wenye hekima!
1Wakoritho 6:1-6 “Je! Mtu wa kwenu
akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si
mbele ya watakatifu?Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na
ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo?
Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya?
Basi, mkiwa na mahali panapohukumiwa mambo ya maisha haya, mwawaweka kuwa
waamuzi hao waliohesabiwa kuwa si kitu; katika kanisa? Nasema hayo nipate
kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima,
awezaye kukata maneno ya ndugu zake? Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena
mbele yao wasioamini”.
6. Unawakilisha
watu wanaoishi maisha matakatifu!
Ni muhimu
kufahamu kuwa Mungu ametuita kuishi maisha matakatifu lazima tuseme ukweli huu
ndio wito muhimu tulioitiwa UTAKATIFU, kama kuna jambo ambalo kanisa la Mungu
linakosa leo ni watu wanaoishi maisha matakatifu na sio tu wanaoishi maisha
matakatifu bali pia watu wanaohubiri utakatifu hawa wanaitwa mwerezi wa Lebanon
Ushahidi wa kimaandiko unaonyesha wazi kuwa katika Isaya 1:18 “Haya, njoni, tusemezane, asema
Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji;
zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.”
Ni muhimu kufahamu
kuwa asili ya neno hili la Isaya “Zitakuwa Nyeupe kama Theluji” neno hilo
Theluji analolitumia Isaya katika biblia ya kiibrania ni “LAWBAN” ambalo ni
sawa na neno LEBANON ambayo yote kwa pamoja maana yake ni NYEUPE au
THELUJI, Neno hili limetumika hasa
kutokana na Milima katika nchi ya Lebanon ambayo imejaa theluji na katika
milima hii ndiko ambako Mierezi ilistawi, kutokana na jambo hili mti wa Mwerezi
wa Lebanon pia unatumika kuelezea weupe au utakatifu.
Utakubaliana
nami kuwa mti wa mwerezi pia ulitumika katika kufanya kazi za utakaso hekaluni
au katika hema ya kukutania angalia Mambo
ya walawi 14:4-6 Biblia inasema “ndipo huyo kuhani
ataagiza kwamba watwae kwa ajili yake atakayetakaswa ndege wawili walio hai,
ambao ni safi, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo; kisha kuhani
ataagiza ndege mmoja achinjwe katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya
mtoni; kisha huyo ndege aliye hai atamshika, na huo mti wa mwerezi, na hiyo
sufu nyekundu, na hisopo, naye atavichovya hivyo, pamoja na yule ndege aliye
hai, katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa juu ya maji ya mtoni;” Unaona kile alichokisema Isaya kuhusu weupe kama
theluji na sufu kinakubaliana na ukweli kuwa anazungumzia mwerezi ambao
ulitumika kwa kazi za utakaso Hekaluni tuongeze maandiko
Mambo ya Walawi 14: 49-52 “Naye atatwaa ndege
wawili, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo, kwa kuitakasa hiyo
nyumba; naye atamchinja mmojawapo wa ndege hao katika chombo cha udongo kilicho
juu ya maji ya mtoni; kisha atatwaa huo mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu
nyekundu, pamoja na huyo ndege aliye hai, na kuvichovya vyote katika damu ya
huyo ndege aliyechinjwa, na katika hayo maji ya mtoni, na kuinyunyiza nyumba
mara saba; naye ataitakasa hiyo nyumba kwa damu ya ndege, na kwa maji ya mtoni,
na kwa huyo ndege aliye hai, na kwa mti wa mwerezi, na kwa hisopo, na kwa sufu
nyekundu;” Pia tunaweza kuona katika Hesabu 19:6 “kisha kuhani atatwaa mti wa
mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, na kuvitupa katika huo moto unaomchoma
ng'ombe.”
Unaona kwa msingi
huo kilele cha juu kabisa cha wito wa maisha yenye kumpendeza Mungu ni kuishi
maisha matakatifu, wakristo lazima tukumbuke kuwa tumeitiwa maisha matakatifu 1Petro 1:15-16 “bali
kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika
mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni
mtakatifu”. Ni muhimu kufahamu kuwa utakatifu ndio tulioitiwa, kila
mtu aliyeokoka anapaswa kuhakikisha ya kuwa anautafuta utakatifu kwa bidii na
kuwa na amani na watu wote kwani pasipo huo haiwezekani kumuona Mungu Waebrania 12:14 “Tafuteni
kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu
atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”
Watu wa Mungu lazima tuukubalia
utakatifu, tusikubali kuchukuliana na dhambi, tusikubali kuwa sisi ni ndhaifu,
Mungu hangetuagiza kuishi kile ambacho hatungekiweza najua kuwa mwanadamu ni
dhaifu lakini Yesu ana nguvu ya kubadilisha na kubadili mwenendo wetu wote wito
unatolewa wa kuacha dhambi, za kila aina tuzifanyazo, wito unatolewa kutubu,
tutubu na kuziungama dhambi zetu ili tusamehewe na kuishi maisha matakatifu
yanayompendeza Mungu, na tukiishi maisha ya usafi namna hii sisi mbele za Mungu
tutakuwa sawa na mwerezi wa Lebanon Mungu atatufanya kuwa nguzo katika nyumba
yake, Nyumba ya Mungu kanisa la Mungu haliwezi kushikwa na nguzo mbovu au za
waovu, Mungu anataka watu watakatifu wasimame katika imani na kulisimamia neno
la Mungu na kuwa tayari kusema mnifuate mimi kama ninavyomfuata Kristo, wakati
wa kuishi maisha ya kisanii umepita, wakati wa kuifuata kawaida ya ulimwengu
huu umepita lazima tuishi maisha matakatifu, lazima tuuuhubiri utakatifu lazima
tuhakikishe kuwa tunawaambukiza watu utakatifu na sio dhambi, Lazima ufikie
wakati tuutetee utakatifu badala ya kuitetea dhambi, Mungu ni mtakatifu watu
wake wanaomfuata yeye na kumtaja wanapaswa kuwa watakatifu watu waliojitenga na
maovu 2Wakoritho 6:14-18 “.Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo
sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika
gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari?
Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?Tena pana mapatano
gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye
hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao
nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni
kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami
nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi
mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike”,
Mwerezi wa Lebanon
unatumika kuelezea Mtu anayeishi maisha matakatifu ambaye yeye pia ni sababu ya
watu kuishi maisha matakatifu. Anauhubiri utakatifu analitaja jina la bwana
huku yeye aliwa ameuacha uovu 2Timotheo
2:19 “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama,
wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la
Bwana na auache uovu”. Ni vema kufahamu kuwa baada ya kuokolewa
Mungu anatutaka tuishi maisha matakatifu, watu ambao ni mwerezi wanapaswa
kuishi maisha matakatifu, hakuna namna nyingine tunaweza kumuona Mungu pasipo
utakatifu.
7. Unawakilisha
watu wanayoyatoa maisha yao kwaajili ya wengine!
Ni muhimu
kufahamu kuwa mierezi pia ilitumika kutengenezea Meli, na kutokana na teknolojia
ya wakati huo na hivyo kuifanya nchi ya Lebanon au Phoinecia wakati huo kuwa
nchi yenye mafanikio makubwa sana ya kibiashara,
1Yohana 4:10 “Hili
ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi,
akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu”
Kuja kwa Yesu Kristo Duniani ni matokeo ya upendo mkuu wa Mungu
kwa mwanadamu, ni matokeo ya juu kabisa ya upendo usioweza kupimika
Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu
aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele.”
Yohana 15:13:- “Hakuna
aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki
zake”.
Ni Muhimu kufahamu kuwa upendo unaotajwa hapa sio upendo wa
kawaida ni upendo wa kimungu ni upendo wenye huruma za kiungu sio upendo wa
kibinadamu kwa kawaida katika lugha ya kiyunani neno upendo lime gawanyika
katika tafasiri kuu nne za upendo ambazo ni Phileo, Storge, Eros, na Agape au
agapan:- aina hizi za upendo tunaweza kuzichambua kama ifuatavyo:-
·
PHILEO aina hii ya
upedno kwa kiingereza tunaiita “Companionable
love”yaani ni upendo wa Kirafiki, Ni upendo unaojengeka kutokana na
kushirikiana kuzungumza kukubaliana kupeana zawadi,kuendana na kadhalika huu ni
upendo wa kirafiki
·
STORGE aina hii ya
upendo kwa kiingereza tunaiita “Natural
affection love” yaani ni upendo unaotokana na kuweko kwa undugu wa damu,
unampenda mtu kwa sababu ni baba, mama, mwana, mjomba shangazi, dadam kaka na
kadhalika katika mahusiano ya kindugu na damu
·
EROS aina hii ya
upendo kwa kiingereza tunaiita “Erotic
love” yaani ni upendo unaotokana na mvuto wa kimapenzi, ni upendo unaohusu
jinsia tofauti na yako, unampenda mtu kwa sababu ya muonekano wake , umbile
lake na uzuri wake hii husababishwa na mvuto wa kimapenzi, body morphology is
concern Muonekana wa mwili au mvuto unahusika na upendo huu ni wa kihisia.
·
AGAPE aina hii ya
Upendo kwa kiingereza tunaiita “unconditional love” Yaani ni upendo wenye kupitiliza mipaka ya kibinadamu, ni
upendo ambao asili yake ni Mungu ni upendo unaomtakia mema kila mmoja awe adui
au ndugu upendo huunapita mipaka ya kawaida ya kibinadamu, hauangalii hali ya
hewa, unampenda Mungu au mtu bila kutarajia kitu kutoka kwake, bila kujali mtu
huyo ni mwema au mbaya, bila kujali ni wakati mzuri au mbaya, bila kujali ni
wakati wa matatizo au raha upendo huu unabaki vilevile na haubadilishwi na
matukio, Mungu anapoamuru kupendana au kumpenda Yeye katika maandiko
anamaanisha upendo huu wa Agape. Upendo huu pia hujulikana kama Sacrificial
love , upendo wenye kujitoa sadaka kwaajili ya wengine, ni upendo unaojali
kuwahudumia wengine zaidi ya sisi wenyewe, Huu ndio upendo ulioamriwa katika
1Wakoritho 13 upendo wa kiungu.
1. Daktari mmoja wa Uingereza aitwaye Will Pooley alikuwa ni moja ya
madaktari waliokuwa mstari wa mbele Nchini “Sierra Leone” huko walikuwa na wenzake wengi wakipambana na
wagonjwa wa EBOLA na virusi vyake
katika harakati hizo Madaktari
wengi sana na Manesi wengi sana wakiwemo wa Afrika Magharibi waliambukizwa
virusi vya ebola wakati walipokuwa wakiwauguza wagonjwa na wengi wao walikufa
Ugonjwa utokanao na kirusi cha Ebola ni ugonjwa hatari
wenye uwezo wa kusababisha kifo kwa asilimia 90. Shirika la afya duniani,
WHO katikatovuti yake inasema kwa mara ya kwanza ulibainika mwaka 1976
huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Sudan. Chanzo cha kirusi hiki
hadi sasa hakijulikani lakini popo aina ya (Pteropodidae) wanaonekana kuwa
wabebaji wa kirusi hicho, kwa mujibu wa ushahidi uliopo sasa.
Maambukizi hupatikana kwa kila aina ya majimaji
yanayotoka katika mwili wa binadamu ni ugonjwa hatari na unaoua kwa haraka na
hauna tiba
Will Pooley alipoupata ugonjwa huu alirejeshwa katika
ndege maalumu na kuanza kutibiwa chini ya uangalizi maalumu huko uingereza
Pichani Doctor Will Pooley Mwingereza aliyenusurika na Ebola!
Jambo la kushangaza ni kuwa baada ya kupona kwa bahati
tu Will Pooley alitangaza nia yake ya kurudi tena Sierra Leone kusaidiana na
wenzake kupambana na ugonjwa huo.
Mtu huyu aliwashangaza wengi sana na kuwaogopedha
wengi sana akiwa amepona kwa asilimia 100%alisema atarudi Africa kusaidia zaidi
maana alizaliwa kwaajili ya hayo, jambo hili lilimfanya aandikwe kama shujaa na
mwanadamu mwenye uwezo wa kujitoa kwa kiwango cha juu.
2. Maximilian Kolbe alikuwa ni Padre aliyetokea Poland aliuawa
kama mfungwa tarehe 14 August 14,1941, Jeshi
la wa NAZI waligundua kuwa baadhi ya wafungwa wamejaribu kutoroka na hivyo
waliamua kuwaua wafungwa kadhaa, walijaribu kuwaua kwa njia mbalimbali, na
hivyo walichagua wafungwa 10 ili wauawe na kifo chao kiliamuriwa kuwa kifo cha
njaa, wafungwa waliamuriwa kujitoa mmoja mmoja yeye mwenyewe na mfungwa wa
kwanza kuchaguliwa alijulikana kama Franciszek
Gajowinczek mfungwa huyu alipochaguliwa alilia kwa huzuni kubwa akimtaja
mkewe, watoto wake na familia yake na kusikitika kuwa hatowaona tena kutokana
na swala hili Maximillian alisimama na kusogea mbele na kuomba afe yeye kwa
niaba ya Franciszek ombi lake lilikubaliwa, wafungwa waliwekwa kizuizini kwa
muda wa siku kadhaa bila kula wengine walikunywa mikojo yao ili waweze kuishi,
Maximillian alikaa kwa wiki mbili bila kufa huku wengine wote wakiwa wamekufa,
walimchoma sindano ya kufa hakufa na hivyo waliamua kukata kichwa Pope John
Paul II alimtangaza kuwa Mtakatifu kutokana na moyo wake
Pichani Padre Maximilian Kolbe
3. Mifano hii
inatusaidia kujua kile ambacho Bwana wetu Yesu amekifanya Pale alipojibu kuwa
kwaajili ya haya Nalizaliwa alikuwa akimkumbusha Pilato kuwa yeye amekuja
kuwafia wanadamu, amekuja kuwaonyesha upendo wa Mungu jinsi ulivyo Isaya 53:1-5 “Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na
mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na
kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri
hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi,
ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala
hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni
zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali
alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa
juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
Huu
ni upendo mkubwa sana Yesu alikufa kwaajili yetu, Hatuna budi kuhakikisha kuwa
tunasimama upande wake siku zote za maisha yetu, tusihesabu damu yake ya
thamani kuwa kitu cha hovyo tudumu katika wokovu na kuwa wavumilivu kwaajili ya
Mungu wetu.
8. Unawakilisha
watu wenye msimamo usiotikisika.
Kutokana na
ukuaji wa mierezi na urefu wake kwenda juu na nuimara wake umeufanya mti huu
kuwa mti wenye msimamo ambao hautikisiki, au hauyumbishwi na upepo, hivyo kiroho
unawakilisha watu wenye msimamo
Wote
tunafahamu kuwa katika maisha haya kila mmoja anapitia au amewahi kupitia
maswala kadhaa ambayo yamewahi kutikisha maisha yake tunatikiswa katika kila
eneo la maisha yetu, misingi ya imani yetu, mashaka, kukata tamaa, kusalitiwa,
na kuvunjika moyo, huku tukiwa katika mchakato wa kujijenga kiimani ili kwamba
hata kutokee jambo la namna gani lisitufikishe katika hatua ya kuyumba
Maandiko
yanatufunza kupitia mwerezi kwamba tunapaswa kuwa imara na hatupaswi kuyumba
lazima tuwe tayari kukabiliana na majaribu ya aina mbalimbali yanayotujia ni
lazima tuwe na imani isiyotikisika
1. Hakuna ajuaye namna tunavyoweza kuitikia Majaribu
ya aina mbalimbali, tunaweza kukosa amani wakati wa majaribu lakini kila
tunapopitia aina yoyote ya hatupaswi kukata tamaa ni lazima mitikisiko ya kila
aina itukute kuwa tuko tayari na tuko zaidi ya kinachotarajiwa
Matendo 21:10-14 “Basi
tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka
kutoka Uyahudi. Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na
mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu
watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa
Mataifa. Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande
kwenda Yerusalemu. Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja
moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika
Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu. Alipokataa shauri letu,
tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke.”
Paulo mtume
alikuwa ni kama mwerezi alikuwa amekwisha kujengeka katika mfumo wa uwezo wa
kukabiliana na lolote lile kwa hiyo hata nabii agabo na wakristo wa nyakati za
kanisa la kwaza walipofunuliwa ju ya kile knachomkabili yeye alikuwa tayari
zaidi ya kile kinachomkabili.
Majaribu
humtikisha kila mwanadamu na wakati mwingine yanaweza kututupa nje kama
wanafunzi wa Yesu, Shetani ni mjaribu kama anavyotajwa katika maandiko Mathayo 4:3 “Mjaribu
akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe
mikate.” Mjaribu ambaye pia
alimjaribu Masihi, yeye ni adui yetu pia na atatujaribu atataka kujua mismamo
wa imani yetu kwa Mungu, amekuwa akiwajaribu wanadamu wengi kwa miaka mingi
hivyo anazo njia nyingi na uzoefu mkubwa wa ujuzi wa ni namna gani anaweza
kutuingiza katika majaribu 2Wakoritho
2:11 “Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana
hatukosi kuzijua fikira zake.”
Na Rev.
Innocent Kamote
Mkuu wa
wajenzi mwenye Hekima
0718990796.