Jumanne, 24 Desemba 2019

Siku ya Bwana !

Ufunuo 1:10 “Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, Kama sauti ya baragumu,



 
Utangulizi:
Leo nataka kuchukua muda wa kutosha pamoja na wewe msikilizaji na msomaji wangu kuzungumzia moja ya jambo muhimu la kibiblia litupasalo sisi kujifunza na hili lina uhusiano mkubwa na SIKU YA BWANA (JUMAPILI), Katika fungu la maandiko ya msingi utaweza kuona jambo la kushangaza kuwa Mtume Yohana japo alikuwa utumwani uhamishoni katika kisiwa kiitwacho Patmo kwaajili ya Mateso, Bado aliweza kuwa katika Roho siku ya Bwana! (JUMAPILI) Hili ni jamnbo la kushangaza sana na ni muhimu tukalipa kipaumbele kwani kuna kitu cha kujifunza:

Mtume Yohana alikuwa mzee wa siku nyingi sana na alikuwa amepelekwa uhamishoni mbali na ndugu jamaa na marafiki mbali na makanisa na mbali na wale wote waliokuwa naye katika imani, alitupwa katika kisiwa kikame chenye mawe katika inchi ya Ugiriki visiwani, ili asiweze kuendelea kuihubiri injili na wala kumuelezea Yesu Kristo kwa watu wengine, kwa ufupi alikuwa mfungwa kwaajili ya injili. Lakini pamoja na kutengwa mbali na jamaa zake na watu wake anaandika kuwa alikuwa katika “ROHO SIKU YA BWANA!” (Jumapili) hii maana yake nini? Alikuwa katika roho siku ya JUMAPILI! kama katika mazingira magumu namna hiii mtume Yohana alikuwa anakumbuka bila kalenda akiwa mbali akiwa porini akiwa kisiwani akiwa matesoni kuwa leo ni siku ya Bwana yaani ni jumapili, maana yake ni kuwa hatuna udhuru au sababu za kutosha kuacha kuipa umuhimu siku hii siku ya jumapili ambayo hujulikana katika maandiko kama siku ya Bwana.

Maana ya siku ya Bwana!

Ni muhimu kufahamu kuwa Neno siku ya Bwana linapotamkwa katika Kiswahili au linapoandikwa katika Kiswahili, linatunyima aina fulani ya upana wa kulizungumzia kwa raha inayokusudiwa hii ni kwa sababu katika kiigereza kuna maneno makuu mawili ambayo yanatumika kuelezea siku ya Bwana  mfano angalia “THE DAY OF THE LORD”  na angalia pia neno “THE LORDS’ DAY” Misamiati hii miwili yote kwa lugha ya  Kiswahili huitwa “SIKU YA BWANA” kwa misngi huo sasa  Ni muhimu kufahamu kuwa neno siku ya Bwana kinabii linaweza kuwa na maana pana sana tofauti na ile ninayotaka kuizungumzia leo, Neno siku ya Bwana kinabii  (THE DAY OF THE LORD) linamaanisha siku za mwisho, ama majira ya neema na majira ya hukumu kuanzia ujio wa Yesu Kristo mara ya Kwanza kwa wokovu mpaka ujio wake mara ya pili kwa hukumu, kipindi hiki kinabii kinaitwa vilevile siku ya Bwana.”THE DAY OF THE LORD” Kwa mfano

1.       Siku Mungu alipotangaza hukumu kwa watu wake Wayahudi au Israel kuwaonya au kuruhusu wavamiwe na maadui zao kinabii hii pia iliitwa siku ya Bwana Isaya 2:12 “Kwa maana kutakuwa siku ya Bwana wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini.” Unaona hapa siku ya Mungu kuhukumu watu wake kwa sababu kadhaa inaitwa siku ya Bwana yaani siku ya Hasira siku ya kuadhibu watu wake unaweza pia kuona katika Amos 5:18-20 “Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya Bwana; kwani kuitamani siku ya Bwana? Ni giza, wala si nuru.  Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma. Je! Siku ya Bwana haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga.”

2.       Siku ya Bwana kinabii vilevile ilimaanisha siku za mwisho yaani tangu ujio wa Yesu Kristo mara ya kwanza, alipozaliwa, umwagiko au ujio wa Roho Mtakatifu, unyakuo wa kanisa,  kuja kwa Yesu mara ya pili, kuja kuhukumu ulimwengu, na kuja kutawala  na mbingu mpya na nchi mpya au kipindi cha neema hiki pia manabii walikiita siku ya Bwana Yoel 2:31 “Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya Bwana iliyo kuu na itishayo.” Pia nunaweza kuona katika Matendo 2:14-20 “Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu. Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana; lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri. Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi. Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri.”

3.       Siku ya bwana kinabii pia humaanisha wakati wa kunyakuliwa kwa kanisa  na  kurudi kwa Yesu mara ya pili  na pia wakati wa hukumu ya watakatifu na mengineyo unaweza kuona katika 1Wathesalonike 5:2 “Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.” 2Wakoritho 1:14 “14. vile vile kama mlivyotukiri kwa sehemu, ya kwamba sisi tu sababu ya kujisifu kwenu, kama ninyi mlivyo kwetu sisi, katika siku ile ya Bwana wetu Yesu.”

Unaweza kuona kwa hiyo siku ya Bwana (The Day of The Lord) ni siku ya Bwana kinabii ina maana kdaa kama zilivyoainishwa hapo juu na siku ya Bwana (The Lords’ Day) inayotajwa pekee katika ufunuo 1:10 ni siku tofauti, ni siku ya jumapili ni siku ambayo katika somo hili ndio tutakayoizungumzia zaidi kwa kusudi la kuonyesha kwanini tunaabudu jumapili.

Siku ya Bwana tofauti na siku ya sabato!      

                       
               
Wengine hufikiri kuwa siku ya Bwana inaweza kuwa siku ya Sabato kwa sababu ni siku iliyotengwa na Mungu mwenyewe ili wanadamu wapate kumkumbuka na kumuabudu na kupumzika, siku hii inadhaniwa kuwa ni ile sabato ambayo Mungu aliwaamuru wana wa Israel waiadhimishe kwaajili kukumbuka ukombozi wao kutoka utumwani kule Misri!

Kumbukumbu la Torati 5: 14-15 “ lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng'ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako ye yote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe. Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa Bwana, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wako, alikuamuru uishike sabato.” 

Kwa kawaida sabato hii ya wayahudi huanzia ijumaa jioni na kuishia jumamosi jioni, siku hii ilikuwa ni siku ambayo Mungu aliamuru Israel wasifanye kazi yoyote, wao wala watoto wao wa kiume, wala binti zao,wala watumwa wao, wala wanyama wao, siku hii pia ilikuwa ni siku ya kuadhimisha kazi ya uumbaji wa Mungu na kuikumbuka kama siku ambayo Bwana mwenyewe anatajwa katika maandiko kuwa alipumzika au alistarehe! Na aliiitakasa siku hiyo:-

Mwanzo 2:2-3 “Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.” Ona pia

Kutoka 20:8-11 “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.  Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.”  Na pia

Kutoka 23:12 “Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng'ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika.”

Sabato ilikuwa ni ishara kwa wana wa Israel yaani wayahudi kwamba Mungu amewafanya kuwa taifa tofauti na mataifa mengine ili waweze kumcha Bwana Mungu wao. Lakini ni muhimu kufahamu kuwa hakuna mahali popote katika maandiko Sabato imewahi kutajwa kama siku ya Bwana hata kidogo, Sabato iliendelea kutajwa kama sabato katika Biblia agano la kale na agano jipya na sio siku ya Bwana  siku ya Bwana ni siku tofauti    

        
Mathayo 12:5 “Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? “ angalia pia;-

Yohana 7:23 “Basi ikiwa mtu hupashwa tohara siku ya sabato, ili torati ya Musa isije ikavunjika, mbona mnanikasirikia mimi kwa sababu nalimfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya sabato?”

Aidha kwa mujibu wa Mafundisho ya Mitume inaonekana wazi kabisa kuwa sabato ilikuwa ni kivuli, yaani “typology” kuhusu pumziko halisi la rohoni ambalo ni Yesu Kristo. Sabato ni alama ya kinabii kuhusu Pumziko halisi ambalo Mungu atalileta kwa watu wake, Neno Sabato kwa ufupi maara yake ni Raha, katika biblia ya kiingereza hutumika neno “Rest” au kustarehe raha zimatajwa katika biblia Mara sita mara tano ikiwa ni raha ya kinabii inayotabiriwa kuwa watapewa wanadamu baada ya taabu zao za hapa duniani jumla ya raha zote zinazotajwa katika maandiko ni pamoja na raha

1.       Raha au starehe ya Mungu mwenyewe Mwanzo 2:1-3 “Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote.      Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.”
Sabato hii ya Bwana ni sabato ya kinabii, katika kitabu cha Mwanzo Mungu mwenyewe alikuwa nabii kabla ya kutuma manabii, ana ametabiri maswala kadhaa yajayo, Mungu alitabiri kuhusu starehe ijayo kupitia sabato hii, hii ni sabato yake, juu ya kazi zake haitajwi tena popote au labda Musa aliiweka kwaajili ya mkazo wa sabato ya kiyahudi ili Israel waweze kujifunza kutoka kwa Mungu, lakini ni wazi kuwa Mungu hapumziki Yesu alisema baba yangu anatenda kazi hata sasa  Yohana 5:16-17 “Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwudhi Yesu, kwa kuwa alitenda hayo siku ya sabato.  Akawajibu, Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi.” Wayahudi walikuwa na fikra potofu kuhusu siku ya sabato, walifikiri Mungu anaopumzika Yesu alikuwa na ujuzi tofauti kuhusu pumziko hili la Mungu, Mungu hakustarehe hii ilikuwa ni alama ya kinabii ya kuja kuwaokoa watu wake na kuwapa sterehe ya kweli baada ya maisha na kazi ngumu za duniani 

  
2.       Raha au Starehe ya Sabato Kutoka 20:8-11” Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.” Mungu aliiweka sabato hii katika amri zake kwa kusudi la watu wa Mungu kuwa na nafasi ya Mungu katika mioyo yao, kwa nini ilikaziwa sana ilikuwa ni kivuli cha starehe halisi pumziko halisi ambalo ni Yesu Kristo.   

   
3.       Raha au starehe ya Ndoa Ruthu 3:1” Kisha Naomi akamwambia mkwewe, Je! Mwanangu, si vizuri nikutafutie raha, ili upate mema?” hii ni aina ya sterehe, au Pumziko ambalo kila mwanamke hutamani kuwa nalo katika maisha yake ndoa


4.       Raha au starehe ya kanaani iliyotolewa na Yoshua Waebrania 4:8 “Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingaliinena siku nyingine baadaye.Mungu aliwaahidi Israel waliokuwa wakipata shida Jangwani, aliwaahidi starehe aliwaahidi pumziko katika nchi ya kanaani pumziko ambalo Yoshua alikuwa amekabidhiwa kuwapa hii ni sabato ya kanaani, hata hivyo hawakuweza kustarehe, walipambana na maadui baada ya kufa kwake Joshua, raha ya kanaani ilikuwa ni ubnabii tu war aha kamili itakayoletwa na Yesu Kristo.

5.       Raha au Starehe ya wokovu ni raha ya nasfi inayotokana na kumpokea Yesu Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. nJitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”      Mtu akimuamini Bwana Yesu anapata starehe sabato, pumziko la nasfi hata sasa pamoja na taabu zote na changamoto za dunia liko pumizko katika mioyo ya watu waliomuamini Bwan wetu Yesu

6.       Raha au starehe ya watu wa Mungu wakati Mungu atakaposimamisha utawala wake hii ndiyo iliyokuwa imetabiriwa katika maandiko Waebrania 4:9 “Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu.Hii ndio sabato iliyo tabiriwa kwa watu wa Mungu itawapata watu wote waliomuamini Yesu Kristo huu utakuwa ni wakati ambapo masikani ya Mungu itakuwa pamoja na wanadamu milele.

Wakolosai 2:16-17 “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo”. Paulo anayazungumza haya akiwa na ufahamu kamili kuwa sabato ni KIVULI yaani TYPOLOGY  au unabii wa pumziko la mwanadamu, Raha hii iliyoahidiwa ndiyo ambayo watu wa Mungu wanapaswa kuhakikisha kuwa wanaingia hii ni raha ya Mbinguni. Ona:-

Waebrania 4:1-11 “Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile; kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu: Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo, Hawataingia rahani mwangu. Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao, aweka tena siku fulani, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo; kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo,kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu.Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingaliinena siku nyingine baadaye. Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu. Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake. Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi

Ni wazi kuwa sabato haijawahi kuitwa siku ya Bwana katika maandiko bali iliitwa sabato hivyohivyo na hii ilikuwa muhimu kwa wayahudi na sio mataifa mengine,  Wayahudi waliomuamini Masihi nyakati za kanisa la kwanza waliendelea kuitambua sabato kama siku takatifu kwa sababu ilikuwa mila na desturi yao, aidha ilikuwa ni siku ya makusanyiko na yangeliweza kufaa kwaajili ya kuihubiri injili na hata mataifa walioamini nyakati zile kwaajili ya ndugu zao wayahudi,kaka na dada zao waliendelea kuiheshimu Sabato kama njia ya kumuheshimu Mungu, kwa hiyo kumuabudu Mungu siku ya sabato sio tatizo, Mungu haangalia usahihi wa siku ya kuabudu bali huangalia usahihi wa msukumo wa Moyo kama mioyo yetu inasukumwa kuiheshimu na kuishika sabato kama sehemu ya kuishika sheria basi hapo moyo wako hauko sahihi mbele za Mungu  na tayari umetengwa na Kristo! Ona maandiko yanasema:-

Wagalatia 5:4 “Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema.

Kama dhamiri zetu ziko safi mbele za Mungu tuko huru kuabudu siku yoyote ile iwe jumamosi au jumapili au hata nyinginezo Mungu anapendezwa na dhamiri au mikao yetu ya moyo na sio siku, au kujitia chini ya Sheria, Mungu hapendezwi na watu wanaomuabudu yeye kwa midomo tu huku mioyo yao ikiwa mbali naye, awaye yote ambaye anakuja katika ibada kwa sababu tu ni lazima aje siku hiyo au kwa sababu ya sheria za kibinadamu moyo wake hauna nafasi katika Mungu bali uko mbali naye.

Isaya 29:13 “Bwana akanena, Kwa kuwa watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walicho nacho kwangu ni maagizo ya wanadamu waliyofundishwa;

Mathayo 15:7-9 “Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.    

          
Mungu hafurahishwi na watu wanaoshika sheria, maagizo na matakwa lakini anataka moyo unaowakwa kwa upendo kwake kama mtu anampenda Mungu na kwa moyo wake wote akaamua kuabudu siku yoyote iwe jumamosi, au jumapili, au jumatatu au jumanne au jumatano, au alhamisi au ijumaa Mungu ataukubali moyo wa Mtu huyo biLa kujaLi anaabudu lini!

Waebrania 12:28-29 “Basi kwa kuwa tunapokea ufalme usioweza kutetemeshwa, na mwe na neema, ambayo kwa hiyo tumtolee Mungu ibada ya kumpendeza, pamoja na unyenyekevu na kicho; maana Mungu wetu ni moto ulao”.

Zaburi 51:15-17 “Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, Na kinywa changu kitazinena sifa zako. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.                Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.”   

Unaona Mungu hataudharau moyo wa mtu mnyenyekevu, mwenye kumcha yeye moyo uliovunjika na uliojawa na shukurani kama moyo huo utamuendea siku yoyote ile kwa unyenyekevu bila kujali siku hiyo ni siku ya namna gani moyo wa aina hii Mungu atautazama
Isaya 66:2 “Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu

Neno siku ya Bwana katika Biblia ya kiyunani linasomeka kama neno (mia) limetumika mara nyingi zaidi katika injili kumaanisha siku aliyofufuka Yesu, siku hiii ndio ambayo wakristo wa nyakati za kanisa la kwanza waliiheshimu na kuitumia kwa ibada zaidi na ikijulikana kama siku ya Bwana, Msingi mkuu wa somo hili ni kuangalia sababu za kimaandiko na za kihistoria kwanini wakristo wameichagua siku ya Bwana yaani jumapili kuwa siku rasmi ya ibada na kwanini tunaabudu jumapili, huku hoja ya msingi ikibakia kuwa kwa Mungu siku zote ni sawa na Mungu humkubali awaye yote anayemuabudu kwa dhati bila kuacha kuzingatia kuwa siku hii Kristo alijifunua na anajifunua katika siku hii muhimu ambapo mauti ilimezwa kwa ushindi wa Kristo dhidi ya kifo katika siku ya kwanza ya juma!

Nalikuwa katika roho siku ya Bwana!

Baada ya kufahamu hasa maana ya siku ya Bwana na mapenzi ya Mungu kuhusu kuabudiwa kwake ni muhimu kufahamu kuwa  siku ya Bwana inayotajwa katika Ufunuo 1:10 ni siku ya Jumapili hili ni swala lililo wazi kimaandiko, siku hii ni siku ambayo wakristo wa nyakati za kanisa la kwanza waliadhimisha kila wiki kama siku muhimu aliyofufuka Yesu Kristo na ilijulikana kama siku ya kwanza ya juma, ni wazi kuwa  neno hili siku ya Bwana katika agano jipya linatajwa hapa tu, Lakini ni ukweli usiopingika kuwa Yohana alikuwa akiwandikia watu wakristo ambao walikuwa wanajua wazi kuwa akitaja siku ya Bwana namaanisha jumapili yaani siku ya kwanza ya juma, jambo ambalo wakristo wa nyakati za kanisa la kwanza walikuwa wakilijua wazi kwamba siku walizokuwa wakikutana kuabudu ilikuwa siku ya kwanza ya juma ambayo ni jumapili na sababu kubwa ni kuwa ilikuwa ndio siku ambayo Bwana Yesu alifufuka kutoka kwa wafu, siku hii iliitwa au kujulikana kama siku ya kwanza ya juma, ilikuwa ni siku ya namna gani kwa  mujibu wa maandiko na historia ya kanisa:-

1.       Ilikuwa ni siku ambayo Yesu alifufuka kutoka kwa wafu Mathayo 28:1-7 “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu. Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni, mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia.

Marko 16:1-6Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka. Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza; wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi? Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa kubwa mno. Wakaingia kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe; wakastaajabu. Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka

Luka 24:1 “Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari. Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi, Wakaingia, wasiuone mwili wa Bwana Yesu. Ikawa walipokuwa wakifadhaika kwa ajili ya neno hilo, tazama, watu wawili walisimama karibu nao, wamevaa nguo za kumeta-meta; nao walipoingiwa na hofu na kuinama kifudifudi hata nchi, hao waliwaambia, Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu? Hayupo hapa, amefufuka. Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa akaliko Galilaya,

2.        Baada ya kufufuka kwake iko wazi katika maandiko kuwa Yesu alikuwa na tabia ya kuwatokea wanafunzi wake katika siku hii ona:-

Marko 16:9 “Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba.”

Yohana 20:19 “  Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu.”

Yohana 20:26 “Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu.”
3.       Kuja maalumu na umwagiko wa Roho Mtakatifu ulifanyika jumapili siku ya kwanza ya juma  hii ni wazi kutokana na desturi kuwa Pentecost iliadhimishwa  siku ya 50  baada ya kukamilika kwa sabato saba sawa na agizo la

Walawi 23:15-16 “Nanyi mtajihesabia tangu siku ya pili baada ya Sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia Sabato saba; hata siku ya pili ya hiyo Sabato ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsongezea BWANA sadaka ya unga mpya.”

Neno Pentecost maana yake “50” Hamsa au hamsini siku hii ilihesabiwa siku 50 tangu baada ya pasaka yaani zikiisha kupita sabato saba siku ya pili yake waliadhimisha siku ya Pentecoste ni katika siku hii wanafunzi walipokuwa wamejifungiwa wakiwa wanaomba Roho Mtakatifu alikuja maalumu duniani na kuwajaza wote na kanisa lilianza rasmi katika siku hii ambayo kismingi nayo ilikuwa siki baada ya sabato yaani siku ya kwanza ya juma angalia katika

Matendo 2:1-4  Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.                 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”

4.       Nyakati za kanisa la kwanza watu walikutana kila siku kuabudu nyumba kwa nyumba angalia Matendo 2:46 -47 “Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe,  wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.

Hata hivyo kutokana na kuongezeka kwa majukumu mbalimbali katika maisha ya kila siku na kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi walifikia muafaka kuwa ni vema ikatengwa siku maalumu kama siku ya kuabudu na ikatengwa siku ya bwana kama siku ya kuadhimisha siku ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu, aidha pia ilikuwa ni maalumu kwa kuonyesha kuwa wakristo wako mbali au huru kutoka katika sheria za Musa na siku iliyofikiriwa ilikuwa ni siku ya bwana yaani jumapili, Kwa hiyo mitume akiwepo na Paulo waliiadhimisha siku hii na kuitumia kamasiku ambayo waamini wa Kikristo wangekutana na kumuabudu Mungu kwa pamoja

Matendo ya mitume 20:7 “Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane.”

1Wakoritho 16:2 “Siku ya kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja;

5.       Kitabu cha Ufunuo wa Yohana kilifunuliwa kuanzia siku ya Bwana yaani jumapili Ufunuo 1:10-19  Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, Kama sauti ya baragumu, ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia. Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu;  na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini. Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama mwali wa moto; na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana, kana kwamba imesafishwa katika tanuru; na sauti yake kama sauti ya maji mengi. Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume; na upanga mkali, wenye makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake; na uso wake kama jua liking'aa kwa nguvu zake. Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo.

Unaweza kuona ni katika siku hii ya Bwana yaani Jumapili Yohana akiwa anamuabudu Mungu akiwa amezama rohoni akikumbuka wazi kuwa ndio siku ya ushindi na ndio siku ambayo wakristo hukutana kuabudu yeye alikuwa katika roho akiungana nao kumuadhimisha Yesu na ndio unaona sasa Yesu akimtokea katika siku hii na kumuagiza aandike kitabu cha ufunuo ni wazi kabisa kuwa kibiblia siku hii sio ya kupuuzwa na uko umuhimu mkubwa wa kuabudu katika siku hii sawa na fundisho la mitume na kama yanenavyo maandiko

6.       Ushahidi wa Mababa wa kanisa
-          Ignatius aliandika hivi “hatupaswi kuihika sabato tena. Lakini tunapaswa kuishi sawa na siku ya Bwana ambayo nuru ya kweli iliangaza”
-          Justin mfia dini alisema alipokuwa akiutetea Ukristo “Jumapili ni siku ambayo sisi tu akusanyika kwa sababu ni siku ambayo Mungu alileta mabadiliko makubwa kwa kuondoa giza ulimwenguni na ndio siku ambayo Yesu Kristo mwokozi wetu alifufuka kutoka kwa wafu
-          Mafundisho ya mitume yaliyokusanywa Mwaka 105 AD ynasema hivi, “Mitume kwaajili ya hayo waliichagua siku ya Bwana siku ya kwanza ya juma kwaajili ya ibada na kwaajili ya kusoma maandiko na kushiriki Meza ya Bwana kwa sababu ni siku ya kwanza ya Juma ndipo Yesu alifufuka” 


-          Eusebous mwana historia aliyeheshimika sana nyakati za kanisa hata wakati wa mfalme Contantine  aliandika hivi “Tangu mwanzo wakristo walikusanyika siku ya kwanza ya juma kwa makusudi ya kuabudu kusoma maandiko, kuhubiri na kushiriki meza ya Bwana , kwa sababu Yesu alipata ushindi dhidi ya kifo siku hii na amakuwa wa kwanza katika cheo na hivyo anapaswa kuheshimiwa kuliko sabato ya kiyahudi”
               
7.       Yesu Kristo ndiye Bwana wa Sabato 

Ni muhimu kufahamu maana ya maneno haya Yesu ndiye Bwana wa Sabato, Meneno haya yamerejewa mara kadhaa katika injili za

Mathayo 12:8 “Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato”. na Marko 2:28 “Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.” Na Luka 6:5 “Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.”

Yalikuwa ni maneno ya Yesu mwenyewe kuwa Yeye ndiye bwana wa Sabato Yesu alikuwa anamaanisha nini kusema haya? Alikuwa akimaanisha Yeye ndiye mwenye mamlaka dhidi ya sheria zote na taratibu zote ikiwemo sheria ya Sabato, Yesu alisema kwa maneno mengine yeye ni mkuu kuliko sabato, yeye ni mkuu kuliko sheria , yeye ndiye mfanya sheria , Mafarisayo walikuwa wameikazia sheria na kutunga shetria zipatazo 39 za kuikazia zaidi siku ya sabato na kuisimamia kana kwamba wao ndio wafanya sheria Yesu alikuwa akiwaambia wazi kuwa yeye ndio  Muumba na ndio kwa asili mwanzilishi wa sabato hakuna mtu mwenye mamlaka ya kumuamrisha aitumiaje ilihali yeye ndiye mtawala wa kanuni hiyo 

Yohana 1:3 “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.” Ona pia

Waebrania 1:10 “Na tena, Wewe,Bwana,hapo mwanzo uliitia misingi ya nchi, Na mbingu ni kazi za mikono yako;”

 Yeye ni zaidi ya Mafarisayo na ndiye mwenye mamlaka ya kuwakosoa mila na desturi zao wanazofikiri kuhusu Matumizi ya sabato yeye ndiye mwenye mamlaka kamili ya kutafasiri matumizi sahihi ya sabato Yeye kama mtawala dhidi ya sheria zote ikiwemo sabato ana mamlaka ya kuitumia kama apendavyo yuko juu ya sheria hii, Yeye ndiye sabato yenyewe hakna mwanadamu anaweza kupata pumziko la kweli pasipo Yesu, yeye alikuja na kufa na kufufuka ili atukomboe nalaana yote ya torati ikiwemo mateso ya kuishika sabato, Wokovu tulio nao katika Kristo umeifanya sheria ya agano la kale ikiwemo sabato isiwe na maana tena  kimsingi sabato  ilifanyika yaani iliwekwa au ilikuwepo kwaajili ya mwanadamu na sio mwanadamu kwaajili ya sabato    

Marko 2:27 “Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato.”

maana yake sabato ilikuwa ni unabii kwaajili ya kuwapa wanadamu pumziko baada ya kufanya kazi kwa mikono yao wenyewe kwa siku sita, tafasiri sahihi ni kuwa hakuna mtu anaweza kujiokoa kwa kazi zake mwenyewe wokovu wa kweli na pumziko la kweli ljnatoka kwa Mungu, sasa tunaweza kustarehe katika neema yake badala ya kuhangaika kutafuta kibali cha Mungu kwa nguvu zetu wenyewe Yesu amkuja kuifanya kazi hiyo

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”

Sasa hapa Yuko mfalme na hapa iko katiba, hapa ziko mali na hapa yuko mtoa mali, hapa uko uhai na hapa yuko mtoa uhai, hapa iko sabato na yuko bwana wa sabato, wewe utachagua nini? Aliyeweka sheria au sheria yenyewe, wale wanaoadhimisha ibada siku ya jumapili wamemchagua Yesu mwenyewe na wale wanaoadhimisha sabato wamechagua sheria ya Musa 

Sabato, muandamo wa mwezi na kadhalika zilikuwa ni alama kivuli alama za kinabii zinazomuhusu Yesu Kristo na hivyo wakristo hawapaswi kuhukumiwa na mtu awaye yote kuhusu maswala hayo ambayo kwa sasa hayana maana, huku tukitilia maanani kuwa hatupaswi vilevile kuwahukumu wanaozing’ang’ania kama wana dhamiri safi na hakuna anayepaswa kumshambulia mwenzake muhimu ni Yesu Kristo

Wakolosai 2:16-17 “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo”.

Ikumbukwe pia wazi kuwa jumapili siku ya Bwana wala sio mbadala wa sabato, yaani kwa maneno mengine jumapili sio sabato ya wakristo, ni siku ya kumuabudu Yesu, pamoja na kuwa tunaweza kujichagulia siku yoyote kwa mapumziko na kumuabudu Yesu aliyekufa na kufufuka kwaajili yetu na sio kwa misingi ya Torati ya Musa,

Warumi 6:14-15 “Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema. Ni nini basi? Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi chini ya sheria bali chini ya neema? Hasha!

Watu waliookolewa wako huru kumuabudu Mungu siku yoyote na hakuna siku yenye maana kuliko nyingine awaye yote anayekuja na hoja ya kufikiri au kubishana kuhusu siku ni mpumbavu na hayajui maandiko, hakuna sababu ya kumuhukumu mtu awaye yote anayeabudu siku fulani kama anaabudu kwa moyo, cha msingi ni nani  anayeabudiwa na sio siku gani anaabudiwa, Mtu aliyekomaa kiroho hawezi kupata shida ya ipi ni siku ya kuabudu Paulo mtume alishafunga mjadala kuhusu siku ya kuabudu, lakini ni vema ikaeleweka wazi kuwa sabato ilisisitizwa kama alama kivuli cha starehe au raha ijayo ambayo ina uhususiano na raha ya wokovu na raha ya milele pumziko la kweli la wanadamu lililoandaliwa na Mungu.

Warumi 14:4-5 “Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha. Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe.”

Hitimisho:

Siku ya Bwana ni muhimu kwa sababu ndio siku ambayo Yesu alifufuka, ndio siku ambayo sabato halisi alitukomboa na kutuweka huru, ndio siku ambayo Yesu alikuwa akiwayokea wanafunzi wake, ndio siku ambayo tamaduni za kanisa la kwanza walikuwa wakikkutana kusoma neno, kuomba, kuumega mkate na kushirikiana na ndio siku ambayo mtume yohan a alikuwa katika roho, na ni siku ambayo inajitofautisha na wale waliomkataa Yesu wakiwemo baadhi ya wayahudi, ni siku ya kipekee inayoonyesha kuwa tuko huru mbali na sheria ya Musa na kongwa zima la sheria za kiyahudi ambazo haziwezi kuokoa ni siku ya neema ya Mungu! Mwenye masikio ya kusikia na asikie!

Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
0718990796

Maoni 2 :

Unknown alisema ...

Nimekuelewa mtumishi wa Mungu , nilikuwa natafuta maana ya siku ya bwana. Nimesoma na nimeelewa sana . mungu akubariki sana

Bila jina alisema ...

Mungu akubariki sana mtu wa Mungu kwa kunifungua ufahamu. Asante sana.