Jumapili, 15 Machi 2020

Kufungwa kwa Makanwa ya Simba!



Daniel 6:21-22Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno


Utangulizi:

Habazi za Daniel kutupwa katika tundu la simba inatukumbusha Jinsi ambavyo Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake na neno lake, hata katika wakati ambapo tunadhani kuwa kila kitu kimefikia mwisho kwa kukata tamaa, Ni ujasiri wa Daniel pakee na msimamo wake kuhusu Mungu ndio ambao baadaye uliweza kuliokoa taifa zima. Daniel anatajwa si katika njia ya moja kwa moja na mwandishi wa kitabu cha Waebrania kama moja ya mashujaa wa imani aliyefunga makanwa ya simba

Waebrania 11:32-35Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii; ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni. Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa.Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora;”

Unaweza kuona kumbe basi Daniel ni moja ya mashujaa wakubwa wa imani ambaye tunakitu cha kujifunza kuhusu ushujaa wake wa imani na utii wake kwa Mungu na jinsi Mungu alivyoweza kumtetea kwa sababu alikuwa mwaminifu kwake.

    
Daniel 6:1-5Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake.”


Mfalme Dario aliamua kuweka watawala juu ya ufalme wake na hivyo akachagua watu wenye sifa mwaliwali 120 au tunaweza kusema mawaziri 120 na hawa 120 juu yao aliweka watatu na katika hao watatu Daniel alikuwa ni mmoja wao, Sifa zake Daniel zikasikika sana kwa sababu Roho Bora ilikuwa inamkalia Roho Bora hapa maana yeke Roho Mtakatifu alikuwa juu yake, kutokana na sifa safi alizokuwa nazo maadui zake wakatafuta sana Makosa kuwa ni wapi atakosea ili wapate kushughulika naye lakini walikosa tumaini Lakini waliikosa kwa sababu alikuwa mwaminifu, shetani na watumishi wake wakati wote watatafuta Jambo la kutushitaki kwa Mungu au kwa wanadamu ili uweze kupoteza kibali

1Petro 5:8Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”

Mpango wa shetani ni kumuharibia kila mtu wa Mungu, ni kuhakikisha kuwa anatushitaki ili atumeze kwa msingi huo tunapaswa kukesha Daniel alikuwa makini sana na hivyo wapinzani hawakumuweza

Maadui wa Daniel walikosa sababu za uovu za kumshitaki Daniel lakini walijua kwa sababu anamtumikia Mungu wa Israel basi wanaweza kuipata sababu njema katika maswala ya kuabudu kwake, Hivyo walitengeneza sheria ya kumfurahisha mfalme na sheria hii ilikuwa kwamba kwa mwezi mmoja watu wasiabudu Mungu mwingine yeyote isipokuwa mfalme na kuwa kama endapo mtu ataabudu na kuitumikia miungu mingine isipokuwa mfalme atupwe kwenye tundu la simba wenye njaa kali ili mvunja sheria atafunwe

Daniel 6:6-9
Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele. Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba. Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika. Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku.

Ukweli kwa utawala wa waamedi na waajemi waoa walikuwa na utawala wa sheria, yaani utawala unaotukuza sheria zaidi, sheria ilikuwa na nguvu kuliko mfalme, ule wa Nebukadneza mfalme alikuwa na Nguvu, lakini wakati wa Dario sheria ilikuwa na nguvu ukipitishwa mswaada hakunalinaloweza kukunjwa kwa hiyo mazingira ya kuikwepa sheria hii yalikuwa magumu mno kibinadamu.
Daniel alielewa kila kitu lakini alidhamiria Moyoni mwake kuwa atasimama imara mno na aliamua kuomba na kumsifu Mungu, Daniel aliomba mara tatu kila siku akifungua madirisha ya chumba chake kuelekea Yerusalem, na adui walipoona walitoa taarifa za kumshitaji Daniel kwa mfalme mfalme alimpenda sana Daniel lakini kwa sababu ya sheria ilikuwa ni ngumu kuweza kumuokoa hivyomoyo wake ulipata taabu sana Daniel anashitakiwa kwa kosa la Kumcha na kumuabudu Mungu

Daniel 6:10-11Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo. Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.

Mfalme alihuzunika sana akijua kuwa haiwezekani kubadili sheria na kuwa Daniel ni lazima atatupwa katika tundu la simba na kweli Daniel alitupwa katika tundu la simba. Mfalme alisikitika sana kwani alielewa kuwa Daniel anamtumikia Mungu aliye hai daima na kuwa hili halikuwa kosa illa ulikuwa mtego tu ili Daniel asambaratike

Daniel 6:12-18Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika. Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku. Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa. Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na mfalme. Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya. Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli. Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa.”

Kufungwa kwa makanwa ya Simba.

Daniel 6:19-28Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake. Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu. Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, waliokaa juu ya uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu. Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danieli; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho. Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danieli na nguvu za simba. Basi Danieli huyo akafanikiwa katika enzi ya Dario, na katika enzi ya Koreshi, Mwajemi.”

Mambo ya kujifunza:
1.      Hakuna jambo linalipa duniani kama Kumuamini Mungu na kumtegemea, kama tukimtumaini Mungu atafanya mambo ambayo kibinadamu ni vigumu kufikiri kuwa yanaweza kufanyika

2.      Mungu atatulinda na mauti, alimlinda Daniel na mauti na alimfufua mwanaye kutoka kwa wafu Daniel alishitakiwa kwa wivu, Yesu naye alishitakiwa kwa wivu, Daniel alikuwa mwenye haki Yesu naye alikuwa mwenye haki, jiwe liliwekwa Muhuri na Yesu pia jiwe liliwekwa Muhuri Mungu aliwatuma malaika kumlinda Daniel, Mungu aliwatuma malaika kumlinda Yesu Kristo alipofufuka kutoka kwa wafu maisha ya Daniel yalikuwa ni maisha nya kinabii kuhusu Yesu Kristo, Mungu hatakuacha uaibike

3.      Simba hawa wanamuwakilisha Ibilisi ambaye wakati wote anatuwinda ili kutuharibu lakini ulizni wa Mungu ni mkubwa sana kwetu, Petro anasema nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu tunapomtegemea Mungu na kumtii yeye utakuwepo ulinzi wa kimungu katika maisha yetu na hivyo hatupaswi kwamwe kuogoa dhiki na mateso tusimamane na Mungu kwa gharama yoyote ile katika kweli yake naye atatutetea

4.      Mungu hatishiwi na sheria za kibinadamu, ni kweli kuwa ziko sheria za kibinadamu lakini kama sheria hizo za kibinadamu zinapingana na mapenzi ya Mungu biblia inatufunza lazima kumtii Mungu kwanza Matendo 5:29Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.” Daniel aliamua kumtii Mungu kwanza kisha binadamu baadaye Kama sheria za kibinadamu zinakinzana na mapenzi ya Mungu lazima tumuweke Mungu mbele kwa gharama yoyote, biblia inatutia moyo kuitii mamlaka lakini inatutaka tumtii Mungu kwanza

5.      Jina Daniel maana yake Mungu ni nguvu zangu, Kila mmoja anapaswa kudhihirisha kuwa Mungu ni nguvu zake katika kila eneo la maisha yake. Ni muhimu kumtiii Mungu hata kama itatugharimu kwa gharama yoyote ile.


Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
ikamote@yahoo.com/0718990796.

Hakuna maoni: