Jumatatu, 10 Julai 2023

Umuhimu wa kurudisha Shukrani wakati wa mavuno !


Mambo ya walawi 23:9-11. “Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapokuwa mmekwisha ingia hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu;  naye atautikisa mganda mbele za BWANA ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya Sabato kuhani atautikisa.”


Utangulizi:

Leo ni ni jumapili ya muhimu sana katika maisha yetu, kwa sababu ni siku ya Bwana ambayo ni maalumu kwa kumpa Bwana sadaka ya shukurani ni wakati wa kumshukuru Mungu kwa matendo yake makubwa na miujiza yake mikubwa mingi anayotufanyia ikiwa ni pamoja na kutupatia chakula mashambani mwetu.

Mungu alikuwa amewaelekeza watu wake kwamba walete sadaka ya shukurani, ambayo ingekuwa sababu ya Baraka kubwa sana kwao sadaka hii kwa lugha ya kiibrania iliitwa “BIKKURIM” kimsingi sadaka hii BIKKURIM maana yake waebrania waliita MBEGU YA MAMBO YAJAYO na sadaka hii ilijulikana kama MALIMBUKO.  Sadaka hii ilikuwa inaashiria kuwa mambo mazuri Zaidi yanakuja kama ukimshukuru Mungu, kwa hiyo walipolima mazao yao kabla hawajaanza kuvuna wao wala kula au walipokuwa wamevuna na kabla hawajaanza kutumia walichukua kiasi kulingana na ukarimu wa moyo wa mtu na wakakileta Hekaluni, ambako siku ya jumapili kuhani alipaswa kuiinua na kuitikisa na kuiombea na hapo mkulima huyu angeondoka kwa Imani kuwa Mungu atambariki tena.

Kwa nini Mungu aliagiza watu wamtolee shukurani ya mavuno? Kwa sababu mwanadamu alipewa kila kitu na Mungu ikiwemo mbegu, na ni Mungu ndiye anayefanya kazi ya kuziongeza, kwa hiyo mbegu sio zetu ni mali ya Mungu na chakula sio chetu ni mali ya Mungu na hivyo katika ibada ya shukurani tunamrudishia Mungu vile vinavyotoka kwake kwa hiyari yetu wenyewe

1Nyakati 29:9-14 “9. Ndipo hao watu wakafurahi, kwa sababu wametoa kwa hiari yao wenyewe, kwa sababu kwa ukamilifu wa moyo, kwa hiari yao wenyewe, wamemtolea Bwana; mfalme Daudi naye akafurahi kwa furaha kuu. 10. Kwa hiyo Daudi akamhimidi Bwana, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee Bwana, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele. 11. Ee Bwana, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee Bwana, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote.  12. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. 13. Basi sasa, Mungu wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. 14. Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea.” 

Kwa hiyo unapofika wakati wa kumtolea Mungu, tusifikiri kuwa sasa wachungaji wanatuchosha sasa utoaji umezidi hapana wakati wa kutoa ni wakati wa kupanda, ni wakati wa kurudhisha mbegu kwa Mungu na Mungu anapoipokea huizidisha Mungu hupima tu mioyo yetu na kutaka kuona shukurani zetu, Ndio maana wakati wa Daudi watu walipotoa yeye alikuwa na ujuzi kuwa vitu vyote vinatoka kwa Mungu na kuwa tunarudisha tu kwa mwenyewe  kwa sababu ya ukarimu wake mkuu. Tutajifunza somo hili umuhimu wa kurudisha shukurani wakati wa mavuno kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:- 

·         Sadaka ya Mavuno

·         Umuhimu wa kurudisha shukurani.

·         Jinsi ya kutoa sadaka ya shukurani. 


Sadaka ya mavuno.

Ni shukurani inayotolewa na watu waliomuamini Mungu, kwaajili ya kumshukuru Mungu kutokana na uwezo wake wa kuzizidisha mbegu za mazao alizotubarikia, Nyakati za Biblia kila mtu alimtolea Mungu kwa kadiri ya neema aliyopewa na Mungu, Jamii ya wafugaji walimtolea Mungu katika mifugo yao na jamii ya wakulima walimtolea Mungu kutoka katika mazao yao unaweza kuona 

 Mwanzo 4:3-4 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake;”

Kwa hiyo wafugaji wlitoa mzao wa kwanza na wakulima walitoa malimbuko yaani sehemu ya kwanza nay a muhimu ya mazao waliyopewa na Mungu, kwanini kwa sababu wanadamu hatuna uwezo wa kuzidisha wanyama wetu wala hatuna uwezo wa kuzidisha mazao yetu, muujiza huu hufanywa na Mungu kwa hiyo tunapokuwa na sadaka ya mavuno maana yake nini tunawapa watu nafasi au siku maalumu ambayo watakuja kumshukuru Mungu kwa muujiza wake wa kuwapa mazao na swala hili linakuwa ni akiba kwa Mungu kwaajili ya kuwakumbuka tena BIKKURIM yaani malimbuko au mbegu ya mambio yajayo , kazi ya mwanadamu inaweza kuwa kupanda au hata kumwagilia lakini mwenye kukuza na kuzidisha ni Mungu ona 

1Wakorintho 3:6-7 “Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye.” 

Unaona kwa hiyo siku ya mavuno ni siku ya kumshukuru yeye mwenye kukuza, huyu akuzaye ndiye wa muhimu sana yaani yeye mwenye kutuzidishia, kwa msingi huo tunapozungumzia sadaka ya mavuno tunazungumzia siku ya wakulima kumshukuru Mungu, Ni siku ya kuonyesha kuwa tunatambua mchango wa Mungu katika hiki tulichokipata wakati huu wa mavuno au kikiwa bado kiko shambani na kumshukuru Mungu kuna Baraka kubwa sana kama tunavyoweza kujifunza katika kipengele kifuatacho:- 

Umuhimu wa kurudisha shukurani.

1.       Kuna nguvu ya ufufuo na urejesho katika shukurani

 

Tunapomshukuru Mungu, kwa maneno yetu na sadaka zetu, tunatambua umuhimu wa utebndaji wake katika maisha yetu na Mungu hufufua au kurejesha kile tunachompa sio hivyo tu kila fursa ambayo inaonekana kufa katika maisha yetu inahuishwa kwa upya 

 

Yohana 11:41-44 “Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma. Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.”

Yesu alimshukuru Mungu tu na Lazaro akafufuka kutoka kwa wafu, hii maana yake tunapomshukuru Mungu, yeye anafufua firsa zote zilizokufa katika maisha yetu.

 

2.       Shukurani inakupa nguvu ya kuwashinda maadui.

 

Daudi alikuwa ni mfalme na Jemadari mpiganaji katika vita za aina mbalimbali na hajawahi kushindwa vita hata moja, moja ya siri kubwa ya ushindi wake dhidi ya maadui zake ni pamoja na kuwa na tabia ya kushukuru, inasemekana Daudi alikuwa na tabia ya kumshukuru Mungu mara saba kwa siku Zaburi 119:164 “Mara saba kila siku nakusifu, Kwa sababu ya hukumu za haki yakokutokana na tabia yake hii Mungu alimuahidi Daudi kuwa atampigania dhidi ya maadui zake

 

Zaburi 89:20-24 “Nimemwona Daudi, mtumishi wangu, Nimempaka mafuta yangu matakatifu. Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake, Na mkono wangu utamtia nguvu. Adui hatamwonea, Wala mwana wa uovu hatamtesa. Bali nitawaponda watesi wake mbele yake, Nitawapiga wanaomchukia. Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo, Na kwa jina langu pembe yake itatukuka

 

3.       Shukurani inaleta uponyaji mkamilifu.

 

Tunapomshukuru Mungu tunaruhusu uponyaji wa Mungu katika maeneo mbalimbali ya maisha yetu Yesu aliwaponya wakoma kumi katika Luka 17:11-19 jambo la kushangaza wakati wote wameambiwa wakajionyesha kwa makuhani njiani walipona lakini ni mmoja tu aliyerudi kutoa shukurani na aliporejea Yesu alimwambia kuwa Imani yako imakuponya, uponyaji huu ni uponyaji mkamilifu sio tu wa magonjwa bali na uchumi wetu tunapomshukuru Mungu tunapata uponyaji mkamilifu katika maeneo yetu yote

 

Luka 17:11-19 “Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya. Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika. Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.”

 

4.       Unapomshukuru Mungu unajipatia kibali Zaidi kwa Mungu.

 

Sadaka ya shukurani kwa mavuno, au wanyama, au kwa maneno au kwa fedha ina nguvu ya kutufungulia kibali kwa Bwana Mungu wetu hasa inapoletwa kwa moyo wa kudamiria na usio na manung’uniko, Mungu anapokukubali anasababisha mambo yako yanyooke, anasababisha ukubalike kila unakokwenda na kufanikiwa sana Neno lake limeagiza kumfanyi ayeye shukurani ili atupe kibali ona

 

Mambo ya Walawi 22:29 “Tena mtakapomchinjia BWANA dhabihu ya shukrani, mtamchinja ili mpate kukubaliwa.”

 

5.       Maandiko yameamuru Kushukuru

 

Kama mwanafunzi wa Yesu Kristo na mfuatiliaji wa neno la Mungu na watu tunaotafuta kuyafanya mapenzi ya Mungu utaweza kugundua kuwa unaposoma neno la Mungu utagundua kuwa Kushukuru ni agizo la kibiblia na ni mapenzi ya Mungu hasa ona 1Wathesalonike 5:18 “shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu

 

Zaburi 136:1-26 “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Mshukuruni Mungu wa miungu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Mshukuruni Bwana wa mabwana; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Yeye peke yake afanya maajabu makuu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Yeye aliyefanya mbingu kwa fahamu zake; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Yeye aliyeitandaza nchi juu ya maji; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Yeye aliyefanya mianga mikubwa; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Jua litawale mchana; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Mwezi na nyota zitawale usiku; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Yeye aliyewapiga Wamisri kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza wao; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akawatoa Waisraeli katikati yao; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Kwa mkono hodari na mkono ulionyoshwa; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akawavusha Israeli katikati yake; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akamwangusha Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Yeye aliyewaongoza watu wake jangwani; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Yeye aliyewapiga wafalme wakuu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akawaua wafalme mashuhuri; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Sihoni, mfalme wa Waamori; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Na Ogu, mfalme wa Bashani; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akaitoa nchi yao iwe urithi; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Urithi wa Israeli mtumishi wake; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Aliyetukumbuka katika unyonge wetu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akatuokoa na watesi wetu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Kila chenye mwili akipa chakula chake; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Mshukuruni Mungu wa mbingu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.”

Jinsi ya kutoa sadaka ya shukurani:

-          Andaa sadaka yako ya Mavuno ambayo unataka kuitoa hii ni tofauti na zaka, unaweza kuchukua kiasi unachotaka kulinga na neema ya Mungu aliyokupatia, unaweza kuibadili sadaka yako kuwa fedha hakuna ubaya na unaweza kuitoa kama ilivyo pia hakuna ubaya.

-          Ombea sadaka yako weka dua na maombi ambayo unataka Mungu akufanyie Zaidi kwa mwaka wa mavuno unaokuja

-          Iweke sadaka yako katika madhabahu unayopata neno la Mungu na unapoabudu

-          Mchungaji, kuhani na mashemasi wa kanisa husika watakapokuwa wnahitimisha ibada ya mavuno wataweka mikono juu ya sadaka hizo au wataziinua mbele za Mungu na kutamka Baraka kwaajili nya sadaka hizona kwaajili ya watu waliotoa


Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!



Hakuna maoni: