Jumapili, 24 Januari 2021

Nyumba juu ya Mwamba!


Mathayo 7:24-27Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.


Utangulizi:

Kristo Yesu alipokuwa duniani aliishi kama mtenda kazi awaye yote  katika Bwana akiwa na karama na vipawa mbalimbali vya Roho moja ya karama aliyokuwa nayo ilikuwa ni karama ya ualimu,uwezo wake na mamlaka aliyokuwa nayo katika kufundisha iliwafanya wale waliomsikiliza wakubwa kwa wadogo kushangazwa sana na uweza wake wa kufundisha ona

Mathayo 7:28-29 “Ikawa, Yesu alipoyamaliza maneno hayo, makutano walishangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi wao
”.

Makutano wengi walifurahishwa sana na kukubaliana na mafundisho yake, lakini sio wao tu hata watu wakubwa na wenye cheo na mamlaka walimkubali Yesu kuwa ni Mwalimu wa kweli na kuwa Mungu yuko pamoja naye ona

Yohana 3:1-2 “Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi.Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye.

Moja ya sifa kubwa sana ya Yesu Katika mafundisho yake ilikuwa ni uwezo wake wa kutumia mifano iliyo hai inayoeleweka vema kama daraja la kuwasaidia wpte waliomzunguka kumuelewa kwa wepesi, Mafundisho ya Yesu yalieleweka kwa watu wa kila Nyanja wakiwemo wasomo na watu wa kawaida, alitumia mifano mbali mbali iliyojumuisha maisha ya kila siku ya jamii yake nay a watu wake mfano alizungumza mifanyo ya Nyanja ya uvuvi, afya, mizabibu, mashamba, mbweha, matajiri na masikini, ndege, maisha ya kawaida, fedha lakini vilevile katika maswala ya ujenzi kama ilivyo katika mfano huu tutakaouchambua leo!

Makusudi makuu ya Yesu kutumia mifano ilikuwa ni kuleta uelewa wa ndani zaidi kwa wasikilizaji wake na kuleta matokeo makubwa ikiwemo kubadilisha maisha yao na kuwasaidia kuelewa makusudi ba mpango wa Mungu kwetu!

Mfano wa Mjenzi mwenye Hekima na Mjenzi mpumbavu.

Mfano huu Yesu aliweza kuuelezea kama kilele cha Mafunisho yake akitaka wale walioyasikia mafundisho yake waweze kuyafanyia kazi, kwa hiyo ulikuwa ni mfano unaosimama kama msumari wa moto kugongelea umuhimu wa kuishi kile ambacho yeye amekifundisha, Yesu alikuwa Carpenter yaani mjenzi alikulia na kujifunza maswala ya ujenzi, na hivyo alifahamu kuwa nyumba imara huwa inajengwa namna gani, uimara wa nyumba ni msingi wake  aidha uende chini sana au ujengwe juu ya Mwamba, lakini sio hivyo tu iwe na uwezo wa kustahimili mikimikiki ya Mafuriko, maji na pepo kali,

Yesu alikuwa akikazia mfano huu kuwataka wote wanaomuamini, wajue kuwa hawajamaliza kazi, Mwanafunzi makini wa Yesu Kristo ni yule anayejifunza kusikia na kutii au kuyafanyia kazi mafundisho ya Yesu Kristo ona

Luka 6:46-49
Na kwa nini mnaniita, Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo? Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake. Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri. Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa.

Neno la Mungu linatuagiza kuwa watendaji wa neno na sio wasikiaji tu, nykati za leo kumekuwepo na wimbi kubwa sana la wakristo ambao msingi wao hauko katika neno la Mungu, na wahubiri pia msingi wao uko katika miujiza tu na matyokeo yake wameendelea kuwa wachanga wakichukuliwa huku na huko na upepo wa kila namna wa Elimu, Kusudi la kuwepo kwa karama zote tano za huduma ni ili mwili wa Kristo ujengwe watu wakomae wafikie kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo wasiwe watu wa kuyumbishwa huku na kule ona

Waefeso 4:11-15
Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.” Unaona Karama zote za huduma zimetolewa kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, kwa kusudi la kuwajenga watu wakomae, Leo hii watu wengi wamekuwa wakifukuzia miujiza, akiinuka muhubiri huyu na miujiza wanahama huku na kule kwa sababu hawana msingi katika neno, lakini hata wahubiri pia wameshindwa kubalance/ kuweka sawa mzani sikatai kuwa miujiza ni ya muhimu sana na ndio maana hata Yesu aliifanya lakini kulitendea kazi neno la Mungu ni muhimu zaidi kuliko miujiza Biblia inaonya watu wanaofanya muujiza lakini hawayafanyi wala kuyaishi yale Kristo anayoyataka ona  maonyo ya yesu mwenyewe

Mathayo 7:21-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”
 

Kipimo kikubwa cha uendeleaji mwema wa Kikristo ni kulitendea kazi neno na sio vinginevyo, watu wanapaswa sasa kuwa na kiu ya kutafuta kujifunza neno la Mungu kuliko kuhangaika huku na kule wakitafuta miujiza ambayo ni ya kitoto tu kwani ni ya Muda mfupi na wale waitendao na hata wanaotenda hufariki dunia, Mkristo mkomavu ni yule anayejifunza neno la Mungu na kukaa katika neno huku akilifanyia kazi kinyume na hapo ni kujidanganya ona


Yakobo 1:22-25 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.”
  

Unaona neno la Mungu halitaki blaablaa wala unafiki linataka watu walitendee kazi, hiyo ndio akili kinyume cha hapo ni upumbavu, Neno la Mungu linatupa changamoto leo kuwa tusiwe wasikiaji tu bali tuwe watendaji, ni muhimu kujikumbusha kuwa kutoa pepo na kutoa unabii pekee hakutoshi, kwa kuingia katika ufalme wa Mungu wote tunapewa wito wa kulifanyia kazi neno, na kisha wote wenye karama za huduma yaani walimu, wachungaji, wainjilishi, manabii na mitume tumeitwa kuimarisha kanisa na kulijenga na sio kufanya miujiza peke yake, waamini nanyi mnapaswa kujifunza neno la Mungu na kukaa katika hilo, watu wanapaswa kumjua Yesu, huduma zetu zinapaswa kumtambulisha yesu zaidi kuliko sisi wenyewe, huduma zetu ziwaelekeze watu kwa Yesu, tusiwe busy kutafuta umaarufu au kufanya miujiza na hatimaye tukawa maarufu kumshinda Yesu, tunapaswa kuwa makini ili katika huduma zetu tufanyazo kipaumbele kisiwe sisi bali Yesu! Mkazo wetu uwe kuyatendea kazi yale Bwana aliyotuangiza hata kama si kwa ukamilifu lakini huo ndio uwe mwelekeo wetu Kama tunampenda Yesu tutazishika amri zake

Yohana 14:15 “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”
Mfano wa mjenzi ni mfano rahisi kueleweka kwamba mwanafunzi imara ni yule anayesikiliza na kutii walimu wake na kuyatendea kazi yake anayoagizwa, tukiishi hivyo na tukimuomba Mungu then Mungu atafanya sehemu yake na neema yake itakuwa juu yetu, Yohana 13;17 “ Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda.”

Mathayo 7:24-27Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!




Hakuna maoni: