Jumatatu, 24 Januari 2022

Ni nani atakayewashitaki wateule


Warumi 8:31-33 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.  Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?  Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya kazi muhimu anayoifanya shetani katika maisha yetu ya kila siku, ukiacha kututia majaribuni pia anafanya kazi ya kutushitaki mara tunapoangukia katika majaribu, yeye anaitwa Mshitaki wetu  na kazi hii huifanya usiku na mchana ona katika

Ufunuo 12:10 “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.”  Unaona Mwandishi wa kitabu cha ufunuo anaonyesha kushindwa kwa Mshitaki huyu katika ulimwengu wa roho, lakini ni wazi maandiko yanatukumbusha kuwa shetani nimshitaji wetu  kwa kiingereza  The Accuser” kwa hiyo waweza kuona wazi kuwa ibilisi ni mshitaki wetu, Petro anawaonywa Wakristo kuwa makini usiku na mchana ni kama anasema wasilale wawe waangalifu kwa sababu huyu mshitaki yuko kazini akituwinda kama Simba ona 1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Maana ya neno Mshitaki wetu:-

·         Ni nani atakaye washitaki wateule:-

·         Madhara ya kuwashitaji wateule:-

Maana ya neno mshitaki.

Ni muhimu kufahamu kuwa Paulo Mtume anaonyesha kwanza uwazi kuhusu ukarimu mkuu wa Mungu kwa wateule wake  na jinsi anavyotuhesabia haki na namna alivyotupenda ona

Warumi 3:23-26 “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake,ili aonyeshe haki yake ,kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa. apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.”

Na pia unaweza kuona katika Yohana 3:16-18 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”       

Upendo wa Mungu kwa wateule ni mkuu sana kiasi ambacho hakutuachilia mwanaye wa pekee asiyekuwa na dhambi kwaajili yetu na kwa sababu hiyo Mungu hashindwi, kutukarimia na mambo mengine lakini Paulo mtume anakwenda ndani zaidi katika lugha ya kimahakama kwamba licha ya rehema na upendo wa Mungu wa kutukomboa lakini vilevile sio rahisi mtu kufanikiwa kuwashitaki watele wa Mungu hii ni ile hali ya mtu kusimama mahakamani na kuendesha mashitaka ya kutaka wewe usikubaliwe na Mungu, Maneno yanayotumika hapo katika lugha ya Kiyunani ni Kategoros kwa kiingereza Prosecutor  -  A person who institutes legal proceedings against someone ! or a Person who claims that someone has committed an Offence or done something wrong , ni mtu anayeendesha mashitaka kwaajili ya mtuhumiwa ili ahukumiwe  na kuonekana na hatia , Nyakati za agano la kale  wayahudi waliamini hivyo ya kuwa shetani hufanya kazi ya kuwashitaki watu wa Mungu ili waonekane kuwa na hatia ona kwa mfano

Ayubu 1:6-11 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.

Unaweza kuona pia katika tukio linguine mfano Zakaria 3:1-7 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni? Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika. Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi. Nikasema, Na wampige kilemba kizuri kichwani pake. Basi, wakampiga kilemba kizuri kichwani pake, wakamvika mavazi; naye malaika wa Bwana akasimama karibu. Kisha malaika wa Bwana akamshuhudia Yoshua, akisema, Bwana wa majeshi asema hivi, Kama ukienda katika njia zangu, na kama ukishika maagizo yangu, ndipo utakapoihukumu nyumba yangu, nawe utazilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi ya kunikaribia kati yao wasimamao karibu.”

Kwa msingi huo wanadamu wengi wanakuwa na hofu, na kutembea kwa kutokujiamini kwa sababu wanajua kuwa wana hatia na kuwa shetani akiwashitani katika kesi ni kuwa hawatatoboa, sio hivyo tu lakini hata pale itakapotokea huna hatia kama Ayubu bado shetani atahakikisha kuwa anakuchongea kwa Mungu ili upate shida ni kwaajili ya haya Paulo mtume anauliza kwa hoja zenye nguvu kubwa sana kuwa ni nani atakayewashitaki wateule ?  nan i nani atawahukumia adhabu? Yesu yuko mkono wa Kuume wa Mungu na kwa bei ya mauti yake ametukomboa na anatutetea kwa baba yake ili wewe na mi mi tuokolewe!

Ni nani atakaye washitaki wateule:-

Kama jinsi tulivyoweza kuona maana ya Mshitaki, vilevile kugundua kuwa ni shetani lakini vilevile shetani hutumia sana mioyo yetu kutuhukumu, kule kujua kuwa tumetenda dhambi kunatuuma sana moyoni na wakati mwingine tunaweza kumfikiri Mungu vibaya kwa kudhani kuwa hataweza kutukubali na kutuhesabia haki, kutokana na namna na jinsi tulivyomkosea, sio hivyo tu wakati mwingine pia tunaweza kusikia mashitaka kutoka kwa wanadamu wenzetu wakituhukumu kutokana na kosa hili au lile

Yohana 8:2-7 “Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha. Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje?  Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe

Kwa hiyo shetani anaweza kutushitaki, mioyo yetu inaweza kutushitaki lakini hata watu wengine wanaweza kutushitaki na kisha kutuhukumu, Paulo sasa ana jenga hoja kwa kuwa Mungu ametupenda upeo akatuokoa na kutusamehe dhambi zetu ni nani atakaye washitaki wateule ?  Paulo anajenga hoja hii kwa vile anakumbuka kuwa mtu akimuamini Yesu hakuna hukumu iwayo yote inaweza kuwa na nguvu juu yake, kwa kufa kwa yesu pale msalabani hati za mashitaka na hukumu zimeharibiwa hivyio hakuna copy of judgement Wakolosai 2:13-15 “Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”

Mtu akimuamini Yesu Kristo dhambi zake zinasamehewa ya kale yanapita na tazama kila kitu kina kuwa kipya

2Wakoritho 5: 17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.”

Hii maana yake ni kuwa kila aina ya mashitaka kwa mtu wa Mungu au kwa watu wa Mungu lazima yataanguka na kusambara tika na hayatafanikiwa ni Mungu ndiye anayetuhesabia haki, Mungu muumba wa ulimwengu, ni yeye anayemtangaza mtu kuwa na haki, kwa malipo ya ukombozi unaotokana na kazi ya Yesu Pale msalabani, ambaye amekwishalipa gharama ya dhambi zetu, ni yeye aliyeteswa badala yetu ni yeye aliyekufa naye yuko mkono wa kuume wa Nguvu mbinguni hivyo kikla anayemuamini anahesabiwa haki, kwa hiyo hatusimami kwa sababu ya shetani, au mioyo yetu au watu, twasimama kwa sababu Mungu yuko pamoja nasi na anatutetea kupitia kazi ya Bwana Yesu Pale Msalabani.

Madhara ya kuwashitaji wateule:-

Watu wa Mungu hawashitakiwi, unapojaribu kuwashitaki watu wa Mungu ni wewe ndiye utakayeumbuka, ukimhukumu mtu wa Mungu wewe ndiye utakayekuja kuonekana una hukumu na hatia maandiko yanaonya vikali sana swala zima la kuhukumiana  na yana ahadi ya kuwa hakuna mtu atakayekuhukumu akafanikiwa :-

·         Isaya 54:17 “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”

·         Mtu wa Mungu hata kama unamuna anaharibu sio jukumu lako kuhukumu  ni hatari sana kumuhukumu mtu wa Mungu kwa Mungu mwenyewe biblia inaonya vikali ona Warumi 14:4 “Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha.”

·         Kushitaki na kumuhukumu mtu mwingine ni kujifanya wewe ni Mungu ni kuchukua nafasi ya Mungu ni kujikweza kuliko kukubwa sana ni kujifanya ya kuwa wewe ndiwe mwenye hatima ya maisha ya mtu mwingine Yakobo 4:12 “Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine? Maandiko ni kama yanaonya vikali sana swala zima la kuhukumu watu wengine na kuna madhara makubwa sana kwa kuwa wewe sio Mungu

·         Kuhukumu wengine kutakufanya ukataliwe  au uonekane sio kitu Warumi 11:1-3 “Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? Hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazao wa Ibrahimu, mtu wa kabila ya Benyamini. Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali.”

Ndugu yangu Mungu ni mkubwa kuliko mioyo yetu, hakuna sababu ya kutembea kwa huzuni iwapo moyo wako unamtegemea Yesu, makosa ya kibinadamu yanaweza kuweko lakini tukimuomba Mungu msamaha kwa neema yake ataturehemu, na zaidi sana Mungu ni muhimu kuendelea na Yesu, kumshika na kumuamini dhambi kubwa sana kuliko yote ni kukataa neema ya Mungu kwa kumkana Yesu Kristo Mathayo 10:32-33 “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”

Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni: