1Wafalme 12:6-7 “Mfalme Rehoboamu akataka
shauri kwa wazee waliokuwa wakisimama mbele ya Sulemani, baba yake, alipokuwa
hai, akasema, Mwanipa shauri gani ili niwajibu watu hawa? Wakamwambia wakasema, Ukikubali kuwa mtumishi
wa watu hawa leo, na kuwatumikia, na kuwajibu, na kuwapa maneno mazuri, basi
watakuwa watumishi wako daima.”
Utangulizi:
Mojawapo ya maombi yanayompendeza
sana Mungu ni pamoja na kuomba Hekima, Mfalme Suleimani mara alipotawazwa kuwa
mfalme wa Israel, Mungu alimtokea na kumtaka amuombe lolote alitakalo, katika
namna ya kushangaza sana Mfalme Suleimani aliomba Hekima jambo ambalo
lilimpendeza sana Mungu hata akamjalia na mambo mengine mengi sana ambayo hakuyaomba
ona:-
1Wafalme 3:5-13 “Na huko Gibeoni Bwana
akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo
nikupe. Sulemani akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu,
kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu
wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa
kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza
niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo
tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya
watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi
yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu
watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa
watu wako walio wengi? Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani
ameomba neno hili. Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala
hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala
hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu; basi,
tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili;
hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama
wewe. Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na
mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.”
Kila siku katika maisha yetu
tunakabiliwa na swala la kufanya uamuzi, Hakuna jambo gumu sana duniani kama
kufanya uamuzi, maamuzi yetu tunayoyafanya leo yanaweza kuwa na faida kubwa
sana katika siku zetu zote za maisha yetu na ya watu wengine, lakini vilevile
yanaweza kutugharimu na kusababisha machungu katika maisha yetu au hata na ya
wengine kwa hiyo ni muhimu sana kumuomba Mungu atupe Hekima.
Yakobo 1:5 “Lakini mtu wa kwenu
akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala
hakemei; naye atapewa.”
Katika kifungu cha maandiko ya
msingi, tulichosoma tunamuona Mwana wa mfalme Sulemani aliyeitwa Rehoboamu akiwa
anakabiliwa na wakati wa kufanya maamuzi kwa mustakabali wa taifa lake mapema
tu katika siku za mwanzoni mwa utawala wake.
1Wafalme 12:1-5 “Rehoboamu akaenda Shekemu;
maana Israeli wote walikuwa wamekwenda Shekemu, ili kumfanya mfalme. Ikawa Yeroboamu
mwana wa Nebati alipopata habari (maana alikuwa akaliko Misri, huko
alikokimbilia awe mbali na mfalme Sulemani; Yeroboamu akakaa huko Misri,
wakapeleka watu kwenda kumwita); basi Yeroboamu na jamii yote ya Israeli
wakaenda, wakamwambia Rehoboamu, wakasema, Baba yako alilifanya zito kongwa
letu; basi sasa utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako, na lile
kongwa zito alilotutwika, nasi tutakutumikia. Akawaambia, Enendeni zenu hata
siku ya tatu, kisha mnirudie tena. Watu wakaenda zao.”
Wana wa Israel wanaonekana ya
kuwa walikuwa tayari kabisa kumtumikia mfalme Rehoboamu baada ya baba yake
Suleimani, lakini walikuwa na ombi kwamba wawarahisishie maisha maana wakati wa
baba yake hali ilikuwa ngumu sana walielemewa na kodi na utumwa mzito uliowanyima
furaha, Suleimani alikuwa amewatumikisha watu sana kwa utumwa mzito na Kodi
kwaajili ya fahari ya ufalme wake, Mfalme Rehoboamu aliwapa Muda ili kwamba
aweze kulitafakari ombi lao, jambo hili au hatua hii ilikuwa njema kwani
hakufanya haraka alikuwa na utulivu na hii ni hatua nzuri kila wakati
tunapotaka kufanya maamuzi, hatupaswi kufanya maamuzi kwa kufuata mihemko, ni
muhimu kutulia na ikiwezekana kuwa na wakati wa kumuomba Mungu ili kwamba atupe
hakima ya kufanya maamuzi mema yanayokusudiwa, Mungu akitupa hekima yake
tutakuwa na mafanikio makubwa sana yaani matunda mema kwa sababu hekima ya
Mungu ni safi, ya amani, ya upole, na inasikiliza watu hekima hii ina rehema,
na ina matunda mema haina fitina wala haina unafiki imetajwa hivyo katika maandiko;-
Yakobo 3:17-18 “Lakini hekima itokayo juu,
kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu,
imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki. Na tunda la haki
hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.”
Tunapotafakari haya tutaliangalia
somo hili katika vipengele vitatu vifuatavyo:-
1. Ushauri
wa wazee na ushauri wa vijana
2. Umuhimu
wa kufanya maamuzi yenye busara
3. Ukikubali
kuwa mtumwa utatumikiwa Daima
Ushauri wa wazee na ushauri wa vijana.
Kuna kitu cha kujifunza
tunapoangalia maamuzi yaliyofanywa na mfalme Rehoboamu, Maamuzi yake yanaletwa
kwetu na neno la Mungu ili tuweze kujifunza maswala halisi yanayoweza
kujitokeza kwetu katika maisha Mfalme
Rehoboamu alipotulia ili atake ushauri, alipata ushauri kutoka katika makundi
makuu mawili, kundi la kwanza lilikuwa kundi la wazee hawa walikuwa ni watu
waliokuwa na uzoefu na ujuzi (Experience) walikuwa wameona utawala uliopita wa wakati wa baba yake walijua mazuri na
machungu ya utawala huo, kwa kawaida Biblia inapotaja wazee wakati mwingine
huwa inazungumzia UZOEFU hawa walitoa ushauri wao kama hivi ona
1Wafalme
12:6-7 “Mfalme
Rehoboamu akataka shauri kwa wazee waliokuwa wakisimama mbele ya Sulemani, baba
yake, alipokuwa hai, akasema, Mwanipa shauri gani ili niwajibu watu hawa? Wakamwambia wakasema, Ukikubali kuwa mtumishi
wa watu hawa leo, na kuwatumikia, na kuwajibu, na kuwapa maneno mazuri, basi
watakuwa watumishi wako daima.”
Kundi hili ni kundi la watu
wanaojua wapi tunatoka na wapi tunakwenda, maandiko yanaonyesha kuwa walikuwa
ni washauri pia wa Mfalme Suleimani, maandiko yanasema waliokuwa wakisimama
mbele ya Sulemani alipokuwa hai, hawa waliona ukatili aliokuwa nao Sulemani na
ukali wake hunda kuna mambo walishauri na Sulemani kwa ubabe wake alikataa, na
sasa anapokuja mfalme mpya walimshauri kwamba akubali kuwa mtumwa yaani
mtumishi awajali watu awatumie watu lakini vilevile azungumze nao vizuri, awape
majibu akutane na haja za mioyo yao, na kuwapa maneno mazuri, walimwambia
akifanya hivyo watu hawa watamtumikia daima.
Kundi la Pili lilikuwa kundi la
vijana, vijana katika lugha ya kinabii ni watu wasio na uzoefu, hawana ujuzi wa
kutosha wa kupambanua mambo, wao walikuwa ni machipukizi bado hawana mizizi
kundi hili wao walimpa mfalme ushauri wa kuongeza ukatili na kutokuwahurumia
watu
1Wafalme 12:8-11 “Lakini akaliacha shauri
lile la wazee, walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye,
na kusimama mbele yake. Akawaambia, Mwanipa shauri gani ili tuwajibu watu hawa,
waliosema nami, wakinena Utufanyie jepesi kongwa lile alilotutwika baba yako?
Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale
waliokuambia, wakisema, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, bali wewe
utufanyie jepesi, uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko
kiuno cha baba yangu. Basi kama vile baba yangu alivyowatwika kongwa zito, mimi
nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi
nitawapigeni kwa nge.”
Mfalme Rehoboamu kwa bahati mbaya
alifuata ushauri wa vijana maana yake alifuata ushauri wa watu wasio na uzoefu,
wajanja wajanja ambao kimsingi walikuwa wakitarajia nafasi kadhaa katika utawala
mpya hivyo wasingekuwa na jipya zaidi ya kumpamba mfalme na kumpa maneno ambayo
walifikiri yangeweza kuwa na tija katika jamii matokeo yake wana wa Israel
waligawanyika makundi makundi na inchi ya Israel ikapoteza umoja na kuvunjika
katika falme mbili
1Wafalme 12:12-16 “Basi, Yeroboamu na watu
wote wakamfikia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema,
Mnirudie siku ya tatu. Mfalme akawajibu watu wale kwa ukali, akaliacha shauri
lile wazee walilompa; akawajibu kama vile walivyomshauri vijana, akasema, Baba
yangu alilifanya zito kongwa lenu, bali mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu
aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge. Basi mfalme hakuwasikia
wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa Bwana, ili alitimize neno lake, Bwana
alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa kinywa cha Ahiya Mshiloni. Basi
Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hakuwasikia, hao watu walimjibu mfalme,
wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa
Yese. Haya! Nendeni zenu hemani kwenu, enyi Israeli; sasa itunze nyumba yako
mwenyewe, Ee Daudi. Hivyo Israeli wakaenda zao hemani kwao.”
Umuhimu wa kufanya maamuzi yenye busara
Ni jambo la kusikitisha sana kuwa
Nchi ya Israel iligawanyika na watu walivunjika Moyo, mfalme hakuwajibu watu
kwa upole na badala yake aliwajibu watu kwa ukali na watu wakavunjika moyo kila
mmoja akarejea nyumbani kwake, Siku zote
katika maisha yetu hatuna budi kuhakikisha ya kuwa tunafanya maamuzi ambayo
yanampendeza Mungu maamuzi ambayo kwa namna yoyote ile hayatakuja yawaumize
watu na kuwakatisha tamaa, tusifanye uamuzi wowote wenye kuaibisha watu au
kudhalilisha, au kuumiza, tusifanye kwa mihemko yetu wala kwa ubinafsi wetu
wala kwa kutaka makuu, Mungu anatutaka watu wote tuwe na maamuzi yenye busara,
watu wa Mungu hawapaswi kuwa kama watu wa dunia hii, katika kanuni za kimungu
kuwatumikia watu ndio hatua ya juu zaidi itakayotupa heshima kwa Mungu, Bwana
Yesu ametufundisha kuwa namna hiyo
Mathayo 20:25-28 “Lakini Yesu akawaita,
akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao
huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa
mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza
kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali
kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”
Kumbe ni kanuni ya kibiblia
kabisa ya kuwa tunapaswa kuwatumikia
watu kwa maana nyingine tuwe wanyenyekevu na jambo hili litatupa faida kubwa
sana katika maisha yetu, Wazee walikuwa wamemshauri Rehoboamu namna njema ya
kufaulu walimtaka awe mnyenyekevu kwa watu, awe mpole azungumze nao kwa amani awe
mtumwa na kuwa watu wangemtumikia daima, kumbe katika maisha yetu tukitaka
kufanikiwa tukubali kuwa watumwa, tujinyenyekeze, tutii wazee, tusikilize
wakubwa, tusikilize walimu, tusikilize wazazi, na walezi, tusikilize wale wenye
uzoefu wanatuambia nini na wakati wote
tukatae hali ya kujifanya mabwana:-
1Petro 5: 1-3 “Nawasihi wazee walio kwenu,
mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa
utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na
kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa
kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya
mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.”
Ukikubali kuwa mtumwa utatumikiwa Daima!.
Huu ndio ushauri mwema kutoka
katika mapenzi ya Mungu, wazee walimshauri Rehoboamu kwamba ukikubali kuwa
mtumishi wa watu hawa watakutumikia daima, hii ndio kanuni ya msingi ya
kibiblia na ina faida nyingi sana kwa mujibu wa maandiko;-
1.
Ukijinyenyekesha
utainuliwa juu sana, unapokubali kuwa mtumwa Mungu atakuinua juu mno utapanda
katika viwango na watu wote watakutumikia ona Wafilipi 2:5-11 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia
ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye
hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali
alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa
wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo
kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.
Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila
jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya
duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI
BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba. Hii ni kanuni huru ya kibiblia Zaburi 147:6 “Bwana huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye
jeuri.” Bwana wetu Yesu Kristo alikubali kuwa mtumwa, aliwatumikia
watu, kumbuka alikuwa sawa na Mungu alikini alijinyenyekeza moyo wake ulijikita
katika kumtumikia Mungu na watu wake na hivyi Mungu alimuinua juu sana na kumpa
jina lipitalo majina yote na kutukuzwa sana mbinguni na duniani.
2.
Kujinyenyekeza
kunaongeza Neema ya Mungu, 1Petro 5:5-6 “Vivyo
hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu,
mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa
wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili
awakweze kwa wakati wake;” Hakuna jambo baya duniani kama
kupungukiwa neema, Mungu wetu ana upendo mkubwa sana aukipata neema mbele zake
utafanikiwa katika maisha yako, lakini kiburi ni sumu ya neema, kama
tukishindwa kujinyenyekesha haraka sana Mungu ataondoa neema yake kwetu! Na hivyo tutajisikia vibaya na kupatwa
na aibu.
3.
Kujinyenyekeza
kunaleta kukubaliwa na kujikweza kunaleta kukataliwa Luka 18:9-14 “Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni
wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni
kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba
hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine,
wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga
mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza
ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali
alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.
Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule;
kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.” Yakobo
4:10 “Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza.”
3Yohana 1:9 “Naliliandikia kanisa neno, lakini
Diotrefe, apendaye kuwa wa kwanza kati yao, hatukubali.”
4.
Mungu
huwasikiliza wanyenyekevu 2Nyakati 34:27 “kwa kuwa
moyo wako ulikuwa mwororo, nawe umejinyenyekeza mbele ya Mungu, uliposikia
maneno yake juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao, ukajinyenyekeza mbele zangu,
na kuyararua mavazi yako, na kulia mbele zangu; mimi nami nimekusikia, asema
Bwana.”
5.
Unyenyekevu
unaleta hekima na kutufanya tukubali kufundishika ona Zaburi 25:9 “Wenye upole atawaongoza katika hukumu, Wenye upole
atawafundisha njia yake”. na Mithali 11:2 “Kijapo
kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.”
6.
Huepusha
hasira ya Mungu na kutupa wokovu ona 2Nyakati 32:26 “Hata
hivyo Hezekia akajinyenyekeza kwa ajili ya huku kutukuka kwa moyo wake, yeye na
wenyeji wa Yerusalemu, hata haikuwajia hasira ya Bwana siku za Hezekia.”
na Zaburi 149:4 “Kwa kuwa Bwana awaridhia watu
wake, Huwapamba wenye upole kwa wokovu.”
7.
Ukijishusha
utakuwa mkubwa katika ufalme wa Mungu Mathayo 18:4 “Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe
kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.”
Kama Rehoboamu angejinyenyekeza
angeweza kupata thawabu kubwa na nyingi zinazotajwa katika mandiko, Bwana na
ampe neema kila mmoja wetu kujifunza umuhimu wa kunyenyekea na kujishusha ili
tuweze kuona faida na uzuri wa kanuni za kimungu sawa na namna Mungu anavyokusudia
katika Maisha yetu na tukumbuke siku zote ya kuwa ukikubali kuwa mtumwa
utatumikiwa Daima.
Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!