Jumanne, 20 Septemba 2022

Ukikubali kuwa mtumwa utatumikiwa Daima !


1Wafalme 12:6-7 “Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee waliokuwa wakisimama mbele ya Sulemani, baba yake, alipokuwa hai, akasema, Mwanipa shauri gani ili niwajibu watu hawa?  Wakamwambia wakasema, Ukikubali kuwa mtumishi wa watu hawa leo, na kuwatumikia, na kuwajibu, na kuwapa maneno mazuri, basi watakuwa watumishi wako daima.”



Utangulizi:

Mojawapo ya maombi yanayompendeza sana Mungu ni pamoja na kuomba Hekima, Mfalme Suleimani mara alipotawazwa kuwa mfalme wa Israel, Mungu alimtokea na kumtaka amuombe lolote alitakalo, katika namna ya kushangaza sana Mfalme Suleimani aliomba Hekima jambo ambalo lilimpendeza sana Mungu hata akamjalia na mambo mengine mengi sana ambayo hakuyaomba ona:-

1Wafalme 3:5-13 “Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi? Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili. Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu; basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe. Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.”

Kila siku katika maisha yetu tunakabiliwa na swala la kufanya uamuzi, Hakuna jambo gumu sana duniani kama kufanya uamuzi, maamuzi yetu tunayoyafanya leo yanaweza kuwa na faida kubwa sana katika siku zetu zote za maisha yetu na ya watu wengine, lakini vilevile yanaweza kutugharimu na kusababisha machungu katika maisha yetu au hata na ya wengine kwa hiyo ni muhimu sana kumuomba Mungu atupe Hekima.

Yakobo 1:5 “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.”

Katika kifungu cha maandiko ya msingi, tulichosoma tunamuona Mwana wa mfalme Sulemani aliyeitwa Rehoboamu akiwa anakabiliwa na wakati wa kufanya maamuzi kwa mustakabali wa taifa lake mapema tu katika siku za mwanzoni mwa utawala wake.

1Wafalme 12:1-5 “Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekwenda Shekemu, ili kumfanya mfalme. Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari (maana alikuwa akaliko Misri, huko alikokimbilia awe mbali na mfalme Sulemani; Yeroboamu akakaa huko Misri, wakapeleka watu kwenda kumwita); basi Yeroboamu na jamii yote ya Israeli wakaenda, wakamwambia Rehoboamu, wakasema, Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako, na lile kongwa zito alilotutwika, nasi tutakutumikia. Akawaambia, Enendeni zenu hata siku ya tatu, kisha mnirudie tena. Watu wakaenda zao.”

Wana wa Israel wanaonekana ya kuwa walikuwa tayari kabisa kumtumikia mfalme Rehoboamu baada ya baba yake Suleimani, lakini walikuwa na ombi kwamba wawarahisishie maisha maana wakati wa baba yake hali ilikuwa ngumu sana walielemewa na kodi na utumwa mzito uliowanyima furaha, Suleimani alikuwa amewatumikisha watu sana kwa utumwa mzito na Kodi kwaajili ya fahari ya ufalme wake, Mfalme Rehoboamu aliwapa Muda ili kwamba aweze kulitafakari ombi lao, jambo hili au hatua hii ilikuwa njema kwani hakufanya haraka alikuwa na utulivu na hii ni hatua nzuri kila wakati tunapotaka kufanya maamuzi, hatupaswi kufanya maamuzi kwa kufuata mihemko, ni muhimu kutulia na ikiwezekana kuwa na wakati wa kumuomba Mungu ili kwamba atupe hakima ya kufanya maamuzi mema yanayokusudiwa, Mungu akitupa hekima yake tutakuwa na mafanikio makubwa sana yaani matunda mema kwa sababu hekima ya Mungu ni safi, ya amani, ya upole, na inasikiliza watu hekima hii ina rehema, na ina matunda mema haina fitina wala haina unafiki imetajwa hivyo katika maandiko;-

Yakobo 3:17-18 “Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki. Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.”

Tunapotafakari haya tutaliangalia somo hili katika vipengele vitatu vifuatavyo:-

1.       Ushauri wa wazee na ushauri wa vijana

2.       Umuhimu wa kufanya maamuzi yenye busara

3.       Ukikubali kuwa mtumwa utatumikiwa Daima

Ushauri wa wazee na ushauri wa vijana.

Kuna kitu cha kujifunza tunapoangalia maamuzi yaliyofanywa na mfalme Rehoboamu, Maamuzi yake yanaletwa kwetu na neno la Mungu ili tuweze kujifunza maswala halisi yanayoweza kujitokeza kwetu katika maisha  Mfalme Rehoboamu alipotulia ili atake ushauri, alipata ushauri kutoka katika makundi makuu mawili, kundi la kwanza lilikuwa kundi la wazee hawa walikuwa ni watu waliokuwa na uzoefu na ujuzi (Experience) walikuwa wameona utawala uliopita wa wakati wa baba yake walijua mazuri na machungu ya utawala huo, kwa kawaida Biblia inapotaja wazee wakati mwingine huwa inazungumzia UZOEFU hawa walitoa ushauri wao  kama hivi ona

 1Wafalme 12:6-7 Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee waliokuwa wakisimama mbele ya Sulemani, baba yake, alipokuwa hai, akasema, Mwanipa shauri gani ili niwajibu watu hawa? Wakamwambia wakasema, Ukikubali kuwa mtumishi wa watu hawa leo, na kuwatumikia, na kuwajibu, na kuwapa maneno mazuri, basi watakuwa watumishi wako daima.”

Kundi hili ni kundi la watu wanaojua wapi tunatoka na wapi tunakwenda, maandiko yanaonyesha kuwa walikuwa ni washauri pia wa Mfalme Suleimani, maandiko yanasema waliokuwa wakisimama mbele ya Sulemani alipokuwa hai, hawa waliona ukatili aliokuwa nao Sulemani na ukali wake hunda kuna mambo walishauri na Sulemani kwa ubabe wake alikataa, na sasa anapokuja mfalme mpya walimshauri kwamba akubali kuwa mtumwa yaani mtumishi awajali watu awatumie watu lakini vilevile azungumze nao vizuri, awape majibu akutane na haja za mioyo yao, na kuwapa maneno mazuri, walimwambia akifanya hivyo watu hawa watamtumikia daima.  

Kundi la Pili lilikuwa kundi la vijana, vijana katika lugha ya kinabii ni watu wasio na uzoefu, hawana ujuzi wa kutosha wa kupambanua mambo, wao walikuwa ni machipukizi bado hawana mizizi kundi hili wao walimpa mfalme ushauri wa kuongeza ukatili na kutokuwahurumia watu

1Wafalme 12:8-11 “Lakini akaliacha shauri lile la wazee, walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, na kusimama mbele yake. Akawaambia, Mwanipa shauri gani ili tuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakinena Utufanyie jepesi kongwa lile alilotutwika baba yako? Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliokuambia, wakisema, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, bali wewe utufanyie jepesi, uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. Basi kama vile baba yangu alivyowatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge.”

Mfalme Rehoboamu kwa bahati mbaya alifuata ushauri wa vijana maana yake alifuata ushauri wa watu wasio na uzoefu, wajanja wajanja ambao kimsingi walikuwa wakitarajia nafasi kadhaa katika utawala mpya hivyo wasingekuwa na jipya zaidi ya kumpamba mfalme na kumpa maneno ambayo walifikiri yangeweza kuwa na tija katika jamii matokeo yake wana wa Israel waligawanyika makundi makundi na inchi ya Israel ikapoteza umoja na kuvunjika katika falme mbili

1Wafalme 12:12-16 “Basi, Yeroboamu na watu wote wakamfikia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu. Mfalme akawajibu watu wale kwa ukali, akaliacha shauri lile wazee walilompa; akawajibu kama vile walivyomshauri vijana, akasema, Baba yangu alilifanya zito kongwa lenu, bali mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge. Basi mfalme hakuwasikia wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa Bwana, ili alitimize neno lake, Bwana alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa kinywa cha Ahiya Mshiloni. Basi Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hakuwasikia, hao watu walimjibu mfalme, wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa Yese. Haya! Nendeni zenu hemani kwenu, enyi Israeli; sasa itunze nyumba yako mwenyewe, Ee Daudi. Hivyo Israeli wakaenda zao hemani kwao.”

Umuhimu wa kufanya maamuzi yenye busara

Ni jambo la kusikitisha sana kuwa Nchi ya Israel iligawanyika na watu walivunjika Moyo, mfalme hakuwajibu watu kwa upole na badala yake aliwajibu watu kwa ukali na watu wakavunjika moyo kila mmoja akarejea nyumbani kwake,  Siku zote katika maisha yetu hatuna budi kuhakikisha ya kuwa tunafanya maamuzi ambayo yanampendeza Mungu maamuzi ambayo kwa namna yoyote ile hayatakuja yawaumize watu na kuwakatisha tamaa, tusifanye uamuzi wowote wenye kuaibisha watu au kudhalilisha, au kuumiza, tusifanye kwa mihemko yetu wala kwa ubinafsi wetu wala kwa kutaka makuu, Mungu anatutaka watu wote tuwe na maamuzi yenye busara, watu wa Mungu hawapaswi kuwa kama watu wa dunia hii, katika kanuni za kimungu kuwatumikia watu ndio hatua ya juu zaidi itakayotupa heshima kwa Mungu, Bwana Yesu ametufundisha kuwa namna hiyo

Mathayo 20:25-28 “Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”

Kumbe ni kanuni ya kibiblia kabisa ya kuwa  tunapaswa kuwatumikia watu kwa maana nyingine tuwe wanyenyekevu na jambo hili litatupa faida kubwa sana katika maisha yetu, Wazee walikuwa wamemshauri Rehoboamu namna njema ya kufaulu walimtaka awe mnyenyekevu kwa watu, awe mpole azungumze nao kwa amani awe mtumwa na kuwa watu wangemtumikia daima, kumbe katika maisha yetu tukitaka kufanikiwa tukubali kuwa watumwa, tujinyenyekeze, tutii wazee, tusikilize wakubwa, tusikilize walimu, tusikilize wazazi, na walezi, tusikilize wale wenye uzoefu wanatuambia nini  na wakati wote tukatae hali ya kujifanya mabwana:-

1Petro 5: 1-3 “Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.”

Ukikubali kuwa mtumwa utatumikiwa Daima!.

Huu ndio ushauri mwema kutoka katika mapenzi ya Mungu, wazee walimshauri Rehoboamu kwamba ukikubali kuwa mtumishi wa watu hawa watakutumikia daima, hii ndio kanuni ya msingi ya kibiblia na ina faida nyingi sana kwa mujibu wa maandiko;-

1.       Ukijinyenyekesha utainuliwa juu sana, unapokubali kuwa mtumwa Mungu atakuinua juu mno utapanda katika viwango na watu wote watakutumikia ona Wafilipi 2:5-11 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;  tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba. Hii ni kanuni huru ya kibiblia Zaburi 147:6 “Bwana huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri.” Bwana wetu Yesu Kristo alikubali kuwa mtumwa, aliwatumikia watu, kumbuka alikuwa sawa na Mungu alikini alijinyenyekeza moyo wake ulijikita katika kumtumikia Mungu na watu wake na hivyi Mungu alimuinua juu sana na kumpa jina lipitalo majina yote na kutukuzwa sana mbinguni na duniani.

2.       Kujinyenyekeza kunaongeza Neema ya Mungu, 1Petro 5:5-6 “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;” Hakuna jambo baya duniani kama kupungukiwa neema, Mungu wetu ana upendo mkubwa sana aukipata neema mbele zake utafanikiwa katika maisha yako, lakini kiburi ni sumu ya neema, kama tukishindwa kujinyenyekesha haraka sana Mungu ataondoa neema yake kwetu! Na hivyo tutajisikia vibaya na kupatwa na aibu.

3.       Kujinyenyekeza kunaleta kukubaliwa na kujikweza kunaleta kukataliwa Luka 18:9-14 “Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.” Yakobo 4:10 “Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza.” 3Yohana 1:9 “Naliliandikia kanisa neno, lakini Diotrefe, apendaye kuwa wa kwanza kati yao, hatukubali.”

4.       Mungu huwasikiliza wanyenyekevu 2Nyakati 34:27 “kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe umejinyenyekeza mbele ya Mungu, uliposikia maneno yake juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao, ukajinyenyekeza mbele zangu, na kuyararua mavazi yako, na kulia mbele zangu; mimi nami nimekusikia, asema Bwana.”

5.       Unyenyekevu unaleta hekima na kutufanya tukubali kufundishika ona Zaburi 25:9 “Wenye upole atawaongoza katika hukumu, Wenye upole atawafundisha njia yake”. na Mithali 11:2 “Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.”

6.       Huepusha hasira ya Mungu na kutupa wokovu ona 2Nyakati 32:26 “Hata hivyo Hezekia akajinyenyekeza kwa ajili ya huku kutukuka kwa moyo wake, yeye na wenyeji wa Yerusalemu, hata haikuwajia hasira ya Bwana siku za Hezekia.” na Zaburi 149:4 “Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake, Huwapamba wenye upole kwa wokovu.

7.       Ukijishusha utakuwa mkubwa katika ufalme wa Mungu Mathayo 18:4 Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.”    

Kama Rehoboamu angejinyenyekeza angeweza kupata thawabu kubwa na nyingi zinazotajwa katika mandiko, Bwana na ampe neema kila mmoja wetu kujifunza umuhimu wa kunyenyekea na kujishusha ili tuweze kuona faida na uzuri wa kanuni za kimungu sawa na namna Mungu anavyokusudia katika Maisha yetu na tukumbuke siku zote ya kuwa ukikubali kuwa mtumwa utatumikiwa Daima.

Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: