1Petro 2:6-8 “Kwa kuwa imeandikwa katika
maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye
heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.
Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe
walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni. Tena, Jiwe la kujikwaza
mguu, na mwamba wa kuangusha, Kwa maana hujikwaza kwa neno lile,wasiliamini,nao
waliwekwa kusudi wapate hayo.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa ni kwanini
mtume Petro anamtaja Yesu Kristo kama jiwe la kukwaza? (Stumbling block) Hili linaweza kuwa jambo lenye kushangaza sana, kwa
sababu kwa lugha rahisi hauwezi kudhani kuwa Mungu angeweza kukusudia Kristo
Yesu awe jiwe la Kukwaza pia, Katika hali ya kawaida tunapomuelezea Yesu Kristo
kama jiwe la Pembeni na lenye heshima inaweza kueleweka vema zaidi, lakini hata
hivyo kama tutaelewa kile kinacho maanishwa katika maandiko tunaweza kutoka
tukiwa na amani ya kutosha sana kumuhusu Yesu Kristo na sisi tuliomuamini.
Tutajifunza somo hili kwa kuzinagatia vipengele vifuatavyo vikuu viwili
vifuatavyo:-
·
Maana ya
jiwe la kukwaza.
·
Jiwe la
kukwaza katika Sayuni.
Maana ya jiwe la kukwaza.
Kibiblia neno jiwe la kukwaza au
kukwaza maana yake ni kukosesha kwa hila kwa kiingereza ni Stumbling Block yaani ukwazo, au makwazo ambalo kwa kiibrania
husomeka kama neno Miksol na kwa
kiyunani ni Skandalon ambalo maana
yake ni kukosesha au kutegea mtu ili aanguke na kupata madhara au jambo lolote
linaloweza kufanyika na kumfanya mtu afanye dhambi au apatikane na madhara na
kuhukumiwa sawa na kumuwekea mtu mtego ili aingie hatiani
Zaburi 140:4-5 “Ee Bwana, unilinde na
mikono ya mtu asiye haki; Unihifadhi na mtu wa jeuri; Waliowaza kuzipotosha
hatua zangu. Wenye kiburi wamenifichia mtego na kamba; Wametandika wavu kando
ya njia; Wameniwekea matanzi.”
Jambo hili kimaandiko sio jambo
jema na Katika lugha ya kinabii kukosesha mtu au kumkwaza mtu kulihesabika kuwa
ni tukio baya, hasa linapofanyika kwa mtu asiye na hatia, Mungu aliwaagiza
makuhani kutokuweka kwazo kwa mtu asiye na ufahamu au asiyeona (kipofu) kwani
kufanya hivyo lilionekana kuwa jambo baya na la kikatili sana
Walawi 19: 14 “Usimlaani kiziwi, wala
usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi BWANA.”
Kimsingi maandiko haya yalikuwa
na maana ya kutokusababisha makwazo kwa watu wanaohitaji kuelekezwa au
kufahamishwa, kwa hiyo kimsingi maonyo haya yanawahusu walimu wa neno la Mungu
kwamba wasitumie ufahamu wao kuwapotosha watu kwa hila kwa kufanya hivyo
kungeleta hukumu iliyokubwa sana au ya kutisha ona
Mathayo
18:6 “bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa
waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika
kilindi cha bahari.”
Unaweza kuona maandiko
yanatangaza hukumu kubwa sana kwa mtu atakayekosesha wengine au kwa lugha
nyingine anayesababisha makwazo au kwa lugha nyingine kufundisha watu uongo au
kumtia mwenye haki hatiani
Yakobo 3:1-2 “Ndugu zangu, msiwe waalimu
wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi. Maana twajikwaa sisi sote pia
katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu,
awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.”
Kwa msingi huo unaweza kupata
picha ya wazi kuwa kukosesha au kukwaza kamwe kibiblia halikuweza kuhesabiwa
kuwa la jambo zuri bali ni tukio baya na
lililoambatana na maonyo makali dhidi ya wale wote wanaosababisha makwazo ya
aina yoyote ile :-
Luka 17:1-2 “Akawaambia wanafunzi wake,
Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake!
Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe
baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa.”
Sasa ni katika namna ya
kushangaza sana unaweza kustaajabu kuona kuwa ujio wa Masihi Bwana wetu Yesu
Kristo unatajwa vilevile kuambatana na Heshima kwa wale watakaomwamini lakini
vilevile na kukwaza kwa wale
watakaomkataa au kutokumuelewa na kutokumuamini hii maana yake ni nini hilo
sasa linatuleta kutafakari kipengele kinachofuata kama ifuatavyo:-
Jiwe la kukwaza katika sayuni
Ni muhimu kufahamu kuwa kuja kwa
Yesu Kristo duniani, kulitabiriwa na manabii na kuwekwa wazi kuwa Yesu angekuja
kwa makusudi makuu mawili, yaani kuokoa wengi na kuwapa heshima kubwa lakini vilevile
kukwaza wengi hasa wale wasiomuamini au wasiomuelewa na kumkubali na
kusababisha hukumu kubwa sana kwao,
Yohana 3:16 -18 “Kwa maana jinsi hii Mungu
aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni
ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye
hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la
Mwana pekee wa Mungu.”
Kwa msingi huo ujio wa Yesu
Kristo una maswala makubwa mawili ya msingi kwa wanaomuamini na kwa
wasiomuamini, wanaomuamini hawatatahayarika lakini kwa wale wasiomuamini
watapata hukumu watakutana na mambo magumu sana sawa na alivyotabiri nabii
isaya ona.
Isaya 28:16 “kwa ajili ya hayo Bwana,
MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe
lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye
hatafanya haraka.”
Swala hili lilielezwa mapema
katika maandiko lakini vilevile nabii mwingine alimuelezea Mariamu mama yake Yesu
waziwazi mara baada ya kuzaliwa na walipokuwa wamempeleka kijana Yesu Hekaluni
kwa kubarikiwa ona katika
Luka 2: 25-34 “Na tazama, pale Yerusalemu
palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu,
akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa
ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa
Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto
Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe
alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu
mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu
wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa,
Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na
babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki,
akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka
wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.”
Kuna maneno kadhaa ambayo
watafasiri wa biblia ya Kiswahili waliyachanganya au kuyanukuu vibaya hasa
katika mstari wa 34 hapo ambao katika biblia ya Kiswahili Union Version
unasomeka hivi
Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa
kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.”
Mstari huo katika biblia ya kiingereza ya NIV yaani New International version
unasomeka hivi “Then
Simeon blessed them and said to Mary, his mother: This child is destined to
cause the Falling and rising of many in Israel, and to be a sign that will be
spoken against” kwa hiyo kwa tafasiri yangu mimi kifungu hiki
kilitakiwa kusomeka Simeoni akawabarikia
na kumwambia Mariam, mama yake, Mtoto huyu hatima yake itasababisha kuanguka
(Kujikwaa) na kuinuka (kuokolewa) kwa wengi katika Israel na kuwa Ishara itakayonenwa kinyume unaona Kwa msingi huo Petro anamuelezea
Yesu katika pande hizo mbili ya kuwa ni jiwe zuri sana la thamani na heshima
kwa wale walimuamini lakini vilevile ni jiwe la kukwaza kwa wale waliomkataa na
wasiomuelewa, au waliompuuzia, Wakati
wote Yesu alipokuwa duniani na kufanya kazi yake makundi mawili yalitokea wale waliomuamini na
wale wasiomuamini na wale wasiomuamini Kristo wamepata hasara kubwa sana Yohana 6:54-62 Petro anatoa ushauri kwa
waamini waendelee kumfuata Yesu kwa sababu yeye ni jiwe lililo hai, ni jiwe
teule, ni jiwe lenye heshima na kwa kufanya hivyo hakuna mtu atakayetahayari au
atakayeaibika kwa kumtegemea Yesu.
1Petro 2:4-9 “Mmwendee yeye, jiwe lililo
hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi
nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu,
mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. Kwa
kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la
pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika. Basi, heshima
hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi,
Limekuwa jiwe kuu la pembeni.Tena, Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa
kuangusha, Kwa maana hujikwaza kwa neno lile,wasiliamini,nao waliwekwa kusudi
wapate hayo. Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu,
watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke
gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;”
Petro anakazia katika ujumbe wake
sawa na neno la Mungu kwa vinywa vya manabii ya kuwa tumchague Yesu, yeye ni
jiwe lenye heshima ni teule limendaliwa na Mungu baba kwaajili ya ukombozi wetu
na kwamba ni fahari kumuamini Yesu na kumkubali na kuwa yeye hatatukataa na
kuwa hatutatahayari, yesu hatamuangusha mtu awaye yote anayemtumaini na
kumwendea yeye wakati wowote hata tuwapo majaribuni, hatatuangusha kwa hiyo
ukimuamini Yesu na kumtegemea katika maisha yako kutoboa katika jambo lolote
kuko nje nje lakini ukimpuuzia Yesu aibu na makwazo na hukumu zinakungoja ona
katika maandiko:-
Warumi 9:33 “kama ilivyoandikwa, Tazama,
naweka katika Sayuni jiwe likwazalo, na mwamba uangushao; Na kila amwaminiye
hatatahayarika.”
Kumwamini Yesu kunalipa na
kuliwapa faida kubwa wale waliomsadiki, lakini wale wanaojifanya wana hekima na
akili na wanaomtambua Yesu kama mtu wa kawaida watajikwaa, watu hawajikwai kwa
Yesu tu wanajikwaa hata kwa neno lake na kukataa ujumbe wake hata leo, Yesu
hatambuliki kwa historia ya kibinadamu tu na hekima ya kibinadamu tu huwezi
kumtambua Yesu kwa hisia tu, au kwa ujuzi wako binafsi, wako watu waliojikwaa
kwa sababu walimuona Yesu kuwa ni wa kawaida tu wakitimia akili zao na hekima
ya kibinadamu watu wengi wataingia dhambini na hatimaye kuingia mtoni kwa
sababu ya kutumia fahamu zao katika maswala ya kiungu, wako watu wenye dharau
kubwa sana kuhusu Mungu, na mambo ya Mungu huonekana kama ya kipumbavu kwao, na
wengine hulichukulia neno la Mungu kwa mazoea tu jambo hili litawagharimu gharama kubwa sana
kwa sababu watajikwaa na ukijikwaa hukumu itakupasa
Marko 6:1-3 “Akatoka huko, akafika mpaka
nchi ya kwao; wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipokuwa sabato, alianza
kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu
ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza
hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa
Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake
hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake.”
Hatuwezi kumtambua Yesu kwa akili
za kawaida na ujuzi wa kawaida Yesu alikuja ili wanyenyeevu watu waliovunjika
moyo waweze kumkubali na watu wenye kiburi waweze kukataliwa Yesu ataendelea
kuwa jiwe la kukwaza kwa watu wote wanaojidhani kuwa wana hekima ya mwilini na
watu wote wenye kiburi na wale wanaojihesabia haki na ndio maana Yesu alipokuja
duniani Mafarisayo ambao walifikiriwa
kuwa ndio wenye Haki waliumbuliwa na kujulikana kama wanafiki, wale waliokuwa
wakiitumainia haki yao wenyewe waliumbuka na kujiona kuwa sio kitu kila mtu
anayejitumainia na kujiamini mwenyewe Yesu kama jiwe la kukwaza litawasaga
tikitiki, watu wasio na akili huitegemea akili yao wenyewe, lakini Yesu
ameifanya hekima ya dunia hii kuwa ni upuuzi na kuifanya kuwa si kitu ni
kupitia kumwamini Yesu tu tunaweza kuokolewa na kuhesabiwa haki kutoka kwa
Mungu, kila anayemuami Yeye hatatahayari wala hatakwazika lakini kila
anayejitumainia atakwazika na kukengeuka na kuingia katika hukumu ya Mungu.
Mungu hawezi kueleweka kwa hekima ya kibinadamu, wengi waliokosa Baraka za
Mungu ni wale waliopuuzia neno la Mungu na kuona kama Yesu hana maana lakini
wale wanaomkubali wanazijua nguvu zake na uwezo wake
1Wakoritho 1:18-19 “Kwa sababu neno la
msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya
Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao
wenye akili nitazikataa.”
Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni