1Timotheo 5:1-5 “Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote. Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli. Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu. Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku.”
Utangulizi:
Moja ya maswala ambayo nyakati za kanisa la kwanza yalipewa kipaumbele sana ni pamoja na kuwahudumia wanawake waliokuwa wajane kwelikweli, Swala zima la kuwakumbuka wajane lilipewa uzito mkubwa sana katika kanisa la kwanza kuliko ilivyo katika nyakati za leo, na inawezekana moja ya sababu kubwa inayofanya kanisa la leo kujisahau ni pamoja na kutokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu somo hili, Lakini kwa neema ya Mungu, Roho Mtakatifu Mwalimu mkuu leo anataka kutukumbusha tena namna na jinsi ya kuwaheshimu wajane kama tutakavyoweza kujifunza kwa kina na mapana na marefu katika siku hii ya leo.
Yakobo 1:25-27 “Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake. Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai.Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.”
Mungu anawajali sana wajane na kujihusisha sana na maisha yao na anatoa wito kwa kanisa lake na watu wake na jamii kufanya kitu kwaajili ya Wajane, Mungu aliwapa wajane kipaumbele kikubwa sana nyakati za agano la kale na kuwaweka katika uangalizi maalumu chini yake mwenyewe.
Zaburi 68:4-6 “Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mtengenezeeni njia ya barabara, Apitaye majangwani kama mpanda farasi; Jina lake ni YAHU; shangilieni mbele zake. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu.”
Kutokuwafikiria wajane nyakati za kale kulifikiriwa kuwa ni moja ya sababu ya kuleta maovu na changamoto katika maisha yako, na ndio maana unaweza kuona Yakobo akifikiri ya kuwa dini ya kweli ni lazima ihusishe kuwaangalia au kuwajali yatima na kuangalia mahitaji yao, Ayubu aliwahi kusema hivi alipokuwa akijitetea sababu ya changamoto zilizompata katika maisha yake na rafiki zake nay eye akadhani kuwa labda ni moja ya sababu ya mateso yake:-
Ayubu 31:15-17 “Je! Huyo aliyenifanya mimi ndani ya tumbo, siye aliyemfanya na yeye? Si yeye mmoja aliyetufinyanga tumboni? Ikiwa nimewanyima maskini haja zao, Au kama nimeyatia kiwi macho ya mwanamke mjane; Au kama nimekula tonge langu peke yangu, Mayatima wasipate kulila;”
Kwa hiyo ilieleweka wazi katika nyakati za waanzilishi wa Imani ya kuwa kutokuwajali yatima kunaleta mikosi na balaa kwa sababu kutokuwajali hao au kuwadhulumu na kutokuwapatia haki pamoja na yatima kunaweza kuwa sababu ya laana nyingi, na ndio maana utaweza kuona kuwa nyakati za kanisa la kwanza kulikuwepo na mgao maalumu wa mahitaji na chakula kwaajili ya wajane na hali kadhalika utaweza kuona katika kifungu chetu cha msingi Paulo Mtume akimuagiza Timotheo kuwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli.
Kumbukumbu 24:17-22 “Usipotoshe hukumu ya mgeni, wala ya yatima; wala usitwae mavazi ya mjane, yawe rehani; bali kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika Misri, Bwana, Mungu wako, akakukomboa huko; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili.Uvunapo mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda shambani, usirudi kuuchukua; na uwe wa mgeni, au yatima, au mjane; ili Bwana, Mungu wako, akubariki katika kazi yote ya mikono yako. Utakapochuma matunda ya mizeituni yako, usirudi kuchuma mara ya pili; yaliyobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane. Uchumapo zabibu katika shamba lako la mizabibu, usichume mara ya pili; zilizobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane.Nawe kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili.”
Kwa msingi huu leo tutachukua muda kujifunza sasa kwa kina na mapana na marefu namna na jinsi tunavyoweza kuwatambua na kuwatendea mema au kuwaheshimu wajane walio wajane kwelikweli na tutajifunza somo hili muhimu kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo:-
Maana ya neno Mjane
Ufahamu kuhusu changamoto wanazokutana nazo wajane
Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli
Maana ya neno Mjane
Neno mjane ambalo katika kiingereza linajulikana kama neno “widow” katika biblia ya kiibrania linatumika neno “almānāh” na katika maandiko ya kiyunani linatumika neno “Chēra” yote yakiwa na maana ya Mwanamke aliyepoteza mume wake kwa sababu ya kifo na ambaye hajaolewa tena, Mwanamke aliyeachwa baada ya kifo cha mumewe, Mwanamke aliyebaki peke yake, ni mwanamke ambaye mumewe amafariki na ameachwa mwenyewe na kwa sababu hiyo anakutana na changamoto kadhaa wa kadhaa katika jamii, ni mwanamke aliyefiwa lakini anakabiliwa na mapungufu, anakabiliwa na uhitaji, hana ulinzi wala msaidizi, hana hali nzuri ya kiuchumi na kihisia anapitia mambo magumu. Kutokana na hali hiyo nyakati za agano la kale wajane waliwekwa katika kundi la watu wanaohitaji msaada kama wakimbizi, masikini na yatima, au pamoja na kundi la walawi, waliokuwa watumishi.
Kumbukumbu 14:27-29 “na Mlawi aliye ndani ya malango yako usimwache, kwani hana fungu wala urithi pamoja nawe. Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba; ili kwamba Bwana, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo.”
Kuwajali wajane kama ilivyo kuwajali walawi, na yatima na wageni na masikini, katika maagizo ya Mungu kulikuwa kunafungua milango ya Baraka kubwa sana katika maisha ya wanadamu, maandiko yaaagiza kuwa watu hao waheshimiwe maana yake mtu asitumie nafasi ya ujane wao kuwadhulumu, kuwaonea na kuwafanyia jambo lolote lisilofaa, wakati mwingine katika hali ya ujane hivyo ziko mila na desturi mbaya miongni mwa jamii, na fikra potofu ambapo pia watu hao hufikiriwa kuwa wana nuksi, Mungu aliliona hilo na kulichungulia na anaweka katika utaratibu wa neno lake kuwa watu hao wapewe kipaumbele maalumu, aliwataka Israel hata wanapovuna chakula wabakize makombo ili yamkini watu hao duni wapate cha kuokoteza nyuma ya mashamba ya wenye uwezo. Pia Mungu aliweka sheria nyinginezo mbalimbali za kimila ili wajane warithiwe kwa kusudi la kuinua uzao wa Ndugu au kuwapa ulinzi na kadhalika hii yote ilikuwa ni kwa sababu ya kutafuta kuwatunza
Nyakati za kanisa la kwanza Mitume walikuwa na ufahamu kuhusu huduma kwa wajane na moja kwa moja tunaona nyakati za kanisa la kwanza kulikuwa na huduma maalumu ya chakula na mahitaji mengine na mgao wa kila siku kwaajili ya wajane
Matendo 6:1-4 “Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.”
Ufahamu kuhusu changamoto wanazokutana nazo wajane
Kabla ya kujifunza kwa kina na mapana na marefu, kwanini Mungu anawapa kipaumbele Wajane, ni muhimu kukumbuka kuwa wajane ni watu wanaopitia changamoto kadhaa wa kadhaa ambazo inawezekana watu wengi wakawa hawafahamu na au labda tu hatujawahi kutoa kipaumbele lakini mara tu baada ya mjane kupoteza mwenzi wake aliyeishi naye kwa muda mrefu, jambo ambalo linamuacha akiwa mpweke na mwenye msongo wa mawazo, na msiba unapoisha tu mjane huanza kujihisi kuwa ametelekezwa, au ametupwa na hapo ndipo neno la Mungu linatuagiza kujali na kutambua mahitaji yao na kuwatia moyo kwa kuwabebea mizigo wa moyoni.
Changamoto za kihisia – wote tunatambua kuwa hakuna jambo baya duniani kama kufiwa, linapokuja swala la msiba wewe lisikie kwingineko tu lakini omba Mungu lisikukute, kufiwa ni jambo zito zito zito mno, na kufiwa na mtu aliye karibu na mliyeishi naye kwa muda mrefu kunaacha mshituko mkubwa, simanzi nzito, kupoteza, upweke, kuachwa na kutelekezwa, linapokukuta swala la msiba wa mtu ambaye alikuwa ni kipenzi chako wa karibu haijalishi kuwa mlikuwa mkifarakana au kugombana ghafla unahisi kama umeadhibiwa, umeumbuka, ni kama una nuksi au dunia na Mungu amekukataa, hisia hizo zote zinakuwa juu ya mjane hata kama atakuwa ameachiwa mali nyingi kiasi gani, lakini kibinadamu linakuwa ni jeraha la kimaisha.
Kutelekezwa katika kiingereza linatumika neno abandonment ambalo maana yake ni leaving someone or ending or stopping something usually forever, kumuacha mtu, au kumtupa, au kumalizana naye au kumaliza uhusiano na yeye, au kuacha kuwasiliana naye na kwa kawaida milele, hili ni tukio baya sana ambalo kimsingi Mungu hawezi kuthubutu kulifanya.
Maombolezo 3:3-33 “Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.”
Kwa msingi huo inapotokea Mungu ameruhusu mwanadamu Fulani hasa mume kuondoka katika ulimwengu huu, mjane hupatwa na hisia za kutupwa, na hasa pale waombolezaji wanapoondoka na mfiwa anaanza kubaki mwenyewe, uhalisia wa msiba ndio unaanza, mfiwa anajikuta anajuta, anaanza kuhisi umuhimu wa yule aliyeonmdoka, pengo lake, na kama aliugua unaanza kuhisi kuwa labda ungempeleka hospitali Fulani ingekuwa kuna nafuu na kadhalika kwa hiyo simanzi huanza kuusonga moyo wa mjane. Kwa hiyo mara moja mwanamke anapofiwa na Mumewe watu wa Mungu hawana budi kujifunza namna ya kuwatetea wajane na kuwalinda jambo hili litawaletea Baraka kubwa sana
Isaya 1:16-17 “Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.”
Zekaria 7:9-10 “Bwana wa majeshi amesema hivi, ya kwamba, Fanyeni hukumu za kweli, kila mtu na amwonee ndugu yake rehema na huruma; tena msimdhulumu mjane, wala yatima, wala mgeni, wala maskini; wala mtu awaye yote miongoni mwenu asiwaze mabaya juu ya ndugu yake moyoni mwake.”
Changamoto za kiuchumi - Nyakati za Biblia kwa kiwango kikubwa sana au zamani wanawake wengi walikuwa wanawategema waume zao katika maswala ya kiuchumi, hata siku za leo pamoja na kuwa wanawake wengi wamepata mwamko mkubwa sana wa kujishughulisha hata hivyo bado ni jukumu la Mume kuitunza familia na kuitia moyo, kuisimamia kama kichwa cha nyumba na kama wanasaidiana ni njema sana sasa inapotokea mume amefariki bado inaleta mtikisiko mkubwa wa kiuchumi kwa mmoja anayesalia kwaajili ya kuitunza familia iliyobaki naye kwa hiyo changamoto za kiuchumi ni moja ya tatizo linalowakumba wajane, wanaweza kupoteza njia na namna ya kujikimu, na kwa sababu ni wanawake wakati mwingine hata kimila na desturi za baadhi ya watu wanaweza kuwaonea na hata kutaka kuwadhulumu wanawake hao wajane na ndio maana utaweza kuona Mungu aliweka sheria kali sana za kuwalinda wajane, kwani wakati mwingine pia walikabiliwa na madeni waliyoyaacha waume zao, au kupokonywa rasilimali na kadhalika
Kutoka 22:22-24 “Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa watu hao katika neno lo lote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima.”
2Wafalme 4:1-7 “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta. Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina. Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe,Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma. Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.”
Aidha Mungu aliagiza kuhakikisha kuwa unawasaidia wajane kwa masazo ya chakula hasa wakati wa mavuno ili na wao waweze kuokoteza na kukidhi mahitaji yao, kwa lugha nyingine Mungu anataka tuwakarimu wajane, tusiende kwao mikono mitupu, tuwasaidie tuwabebe kiuchumi, lakini tuwakumbuke katika maisha
Kumbukumbu 24:19-21 “Uvunapo mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda shambani, usirudi kuuchukua; na uwe wa mgeni, au yatima, au mjane; ili Bwana, Mungu wako, akubariki katika kazi yote ya mikono yako. Utakapochuma matunda ya mizeituni yako, usirudi kuchuma mara ya pili; yaliyobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane. Uchumapo zabibu katika shamba lako la mizabibu, usichume mara ya pili; zilizobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane.”
Changamoto za upweke – Wajane katika namna mbalimbali huwa wanahisi kukumbwa na upweke, kuondokewa na ulinzi na heshima, wanahisi wametengwa na jamii kwa kiwango kikubwa, mabadiliko makubwa na ya ghafla katika hali ya ndoa yanaingiwa na giza, na wakati mwingine katika jamii nyingine hufikiriwa kuwa ni mojawapo ya sababu ya vifo vya waume zao, na hivyo hulaumiwa jambo hili na sababu nyinginezo zinaweza kuchangia wao kuhisi kutengwa na jamii, kuwa wapweke, na kutoa mwanya mdogo sana kati ya changamoto za kihisia na upweke na kuongeza madonda mwilini, wanawake wengine hufikiriwa kuwa na nuksi au kusababisha balaa na wakati mwingine wanaume wengine hufikiri kuwa mwanamke huyu ana nuksi na husababisha vifo vya wanaume wengine.
Mwanzo 38:6-11 “Yuda akamwoza mke Eri, mzaliwa wake wa kwanza, na jina lake huyo mke ni Tamari. Naye Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mbaya machoni pa BWANA; na BWANA akamwua. Yuda akamwambia Onani, Uingie kwa mke wa nduguyo, ukamwoe, ukamwinulie nduguyo uzao. Onani alijua ya kwamba huo uzao hautakuwa wake, ikawa, alipoingia kwa mke wa nduguye, akamwagia chini asimpe nduguye uzao. Neno hili alilolifanya likawa baya machoni pa BWANA, basi akamwua yeye naye. Yuda akamwambia Tamari mkwewe, Ukae mjane nyumbani mwa baba yako hata Shela mwanangu atakapokuwa mtu mzima, maana alisema, Asipate kufa yeye kama nduguze. Basi Tamari akaenda, akakaa nyumbani mwa babaye.”
Tamari alikuwa moja ya wahanga wa ujane, alifiwa na waume wawili na Yuda aliahidi kumuoza mwanae mwingine aitwaye Shela, hata hivyo hakufanya hivyo kwa hofu kuwa mwanamke huyu ana nuksi huenda atasababisha kifo cha mwanaye mdogo, kwa hiyo Tamari alijilipizia kisasi kwa kulala na Yuda mwenyewe na ndipo ukoo wa Masihi ulipotokea kwa kumzaa Peresi Zera kupitia Yuda mwenyewe badala ya watoto wake, ujane una mitihani mingi, wako wanaolenga mali zao, wako wanaowafikiria kuwa labda ni wagonjwa na wanawaogopa hata kuwaoa wakijiuliza waume zao wamekufaje, wako wanaowamendea wawatweze, na wako wanaowatamani kuwatumia tu kimwili kutokana na kujua upweke walionao
Changamoto za kimalezi – Moja ya kazi ngumu sana kwa kina mama wajane ni malezi ya watoto, wote tunafahamu changamoto za kuwa mlezi peke yako, sauti ya mume ni sauti ya mamlaka ina nguvu katika makemeo ya watoto, haijalishi nani huwa ni mkali katika malezi lakini watoto hukaa vizuri sana wanapolelewa na pande zote mbili za wazazi, kwa hiyo kama wako watoto na mume amefariki mjane huwa na wakati mgumu sana wa kuwa mlezi pekee, kukabiliana na malimwengu inaweza kuwa rahisi kuliko kulea watoto peke yako bila mwenzi wako, watoto watahisi lile pengo ambalo baba yao angeweza kutosha, yako mambo ambayo baba anaweza kuwa alikuwa mzuri katika hilo kwa hiyo mama atatakiwa kufanya mara dufu kuweza kuziba, hofu kubwa ikiwa kila mtoto atajihisi sasa ni kiongozi kwa nafsi yake na hivyo mwanamke huyu atabaki anapambana kuhakikisha kuwa kila kitu kina kaa mahali pake. Ni kwaajili ya haya Mungu mwenyewe alibeba jukumu la kuwa baba wa yatima na mwamuzi wa wajane.
Zaburi 68:4-6. “Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mtengenezeeni njia ya barabara, Apitaye majangwani kama mpanda farasi; Jina lake ni YAHU; shangilieni mbele zake. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu”
Changamoto za kiroho – hali ya kupoteza mume huhesabika kama adhabu kubwa sana kwa mwanamke kwa hiyo wengi hugeuka kuwa wakali sana wakitetea maslahi yao na kwa Mungu wanakuwa na mgogoro naye, wanahisi Mungu amewaacha na kuwatelekeza hii ni fikira ya kawaida kwa wajane wengi na ndio maana Mungu akajiwahi katika maandiko kusimama kama mtetezi wao, wengi huwa na maswali mazito hata wakati wa Msiba huwa wanalia huku wakimuuliza Mungu kwanini kwanini, huwa wanahoji kwanini Mungu achukue mume wake, kwa nini maisha yawe hivi au vile baada ya wao kupoteza mume? Wanahisi kuwa maisha hayana maana na kupata maluwe luwe ya kiroho wengi huchanganyikiwa na kutokuwa sawasawa, ni ukweli ulio wazi kuwa wanapatwa na mshituko wa kiroho na kuwa katika wimbi kubwa la msongo wa mawazo, msongo wa mawazo wa mtu aliyefiwa na mume ni mara nne ya wale wenye ndoa yenye mgogoro, kama alimuombea sana mumewe amuokoe na mauti na bado akafa, mjane anaweza kumuona Mungu kuwa hana maana kabisa na kama asipojengwa vema kiroho anaweza kupoteza uwepo wa Mungu nahata kuvamiwa na pepo kwa sababau ya kuelemewa na huzuni na vita ya kiroho. Wakati mwingine wajane hufikiri kuwa Mungu anawakumbusha dhambi zao walizozifanya zamani pale wanapopata majaribu mengine ili hali wao ni wajane
1Wafalme 17:17-22 “Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena. Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu? Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake. Akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe. Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. Bwana akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka.”
Changamoto za kisaikolojia – Ni ukweli usiopingika ya kuwa wanawake wajane wanapitia changamoto nyingi sana za kisaikolojia, tafiti zinaonyesha hivyo japo kanisa linaweza lisiwe na utafiti wa kina au likawa linapuuzia hilo, lakini mgandamizo wa mawazo, mashaka, hofu na ugumu wa maisha na kukosa tendo la ngono kunatengeneza changamoto kubwa na nyingi za kisaikolojia, wajane watateseka kijamii, kiutamaduni, kiimani,kimila, kiuchumi, kiroho na kisheria na huku upande mwingine wakiwa hawana mume wanayapitia haya kimya kimya wakati mwingine jamii ikiwa haina hata taarifa, wanakutana na unyanyasaji wa kisaikolojia wa aina mbalimbali licha ya maneno wanayokutana nayo, ukweli ni kuwa sio rahisi sana kujua wajane wanapitia changamoto gani mpaka uwe makini, hatuwezi kushughulikia kila kitu wanachopitia lakini angalau tunaweza kuwapunguzia. Katika moja ya utafiti uliofanyika nchini kenya katika kaunti ya Kisumu wanawake 50 walifanyiwa utafiti wa kisayansi na kujulikana kuwa bila kujali kuwa waume zao walifariki katika namna ipi wanawake hao waligundulika kuwa na changamoto ya fadhaa kubwa, kukosa msaada, maumivu makali ya ndani, maombolezo yasiyokoma, hofu na woga, utafiti huo uliotumia njia mchanganyiko za maswali, na kuwahoji uso kwa uso, ukusanyaji wa taarifa na tafiti za kiushauri tafiti hizo zilizofanywa na Atindabilal, Bamford, Adatara, Nauko na Obenwa mwaka wa 2014 ulibaini kuwa changamoto wanazokutana nazo wajane kisaikolojia na kuzinukuu kama walivyoorodhesha kwa kiingereza “mental and emotional challenges such as grief, loneliness, isolation, anxiety, low self – esteem, denial, withdraw, sexual unfulfillment and depressed moody, kwa tafasiri yangu wanapata changamoto za kiakili, kihisia, kumezwa na huzuni, upweke, kutengwa, kujitenga, wasiwasi, kutokujithamini, kujikataa, kukosa ngono, na hisia zenye msongo kwa msingi huu kama matabibu wa kisaikolojia wanaweza kufanya utafiti huu na kugundua changamoto wanazozipitia wajane ukweli ni kuwa viongozi wa kiroho hususani watumishi wa Mungu wachungaji wanapaswa kujua pamoja na kanisa kuwa ujane sio tatizo dogo, na ndio maana nyakati za kanisa la kwanza lakini pia Mungu menyewe tumeona akijihusisha kutatua changamoto za wajane, dunia inakisiwa kuwa na wajane wapatao milioni 245 na kati ya hao wanaoishi kwenye umasikini wa kutupwa ni milioni 115 wengine wakiteseka kimila kama huko Nigeria ambako wengine huvamiwa na ndugu wa mume na wanachukua kila kilicho cha ndugu yao na kuwaacha wajane katika mazingira magumu sana kwahiyo unaweza kupata picha kuwa changamoto hii ni kubwa kwa kiasi gani, kwa hiyo kanisa haliwezi kukaa kimya na kuacha kuwa na huduma au kitengo na namna ya kuwahifadhi wajane sawa tu na mtazamo wa nyakati za kanisa la kwanza ulivyokua, tunaweza tusitimize mahitaji yao yote lakini tunaweza kuwapunguzia changamoto zao ili wasiwe na msiba juu ya msiba, Yesu alipunguza maumivu ya mwanamke mjane katika lango la mji wa Naini ambaye licha ya kuwa alifiwa na mumewe sasa watu wa mji walikuwa wakienda kumzika na mwanae wa pekee, hii ilikuwa huzuni juu ya huzuni ashukuriwe Mungu mwenye kujali, Yesu alimpunguzia mwanamke huyu majonzi
Luka 7:11-16. “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake.”
Sisi kama kanisa sasa tunaweza kufanya nini kwaajili ya kushughulika na changamoto hizi wanazokutana nazo wajane hili sasa linatuleta katika sehemu muhimu ya kutafakari kipengele cha tatu jinsi ya kuwahudumia wajane, na neno linalotumika ni kuwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli.
Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli
1Timotheo 5:1-5 “Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote. Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli. Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu. Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku.”
Ni muhimu kujiuliza kwanini Paulo mtume anamuagiza Timotheo kuwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli ni nini hasa maana yake?
Kuwaheshimu – Neno kuwaheshimu kwa kiyunani hapa ni “timaō” ambalo maana yake ni “fix a valuation upon” yaani kuwapa uthamani, uwathamini, wawe wamekidhi vigezo, wawe wamefuzu, uwatambue “Give them a proper recognition” uwape heshima inayostahili, kwa hiyo Paulo mtume alikuwa anamuagiza Timotheo kama mwangalizi wa makanisa kule Efeso kuweka orodha yenye vigezo rasmi vya wajane wanaostahili kutambuliwa na kusaidiwa na kanisa wajane hao walijihusisha na huduma ya kanisa moja kwa moja baada ya kufiwa na waume zao, walijihusisha na maombi kanisani, wajane hao walikuwa ni wale ambao Paulo anawaita wajane kweli kweli yaani ni wajane wasio na mtu wa kuwasaidia, na wajane hao walipitia katika mchujo wenye vigezo kadhaa, na wamefuzu mtihani wa maisha ya uaminifu
Wajane kweli kweli - walikuwa ni wale wasiokuwa na watoto wala wajukuu wala ndugu wa kuwasaidia kabisa
1Timotheo 5:3-4 “Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli. Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu. Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku.”
Walikuwa ni wajane ambao wanamtegemea Mungu na wanaishi maisha ya maombi kazi yao ni kuomba kwaajili ya kanisa, wanamuombea mchungaji, na huduma zote za kikanisa na hudumu katika huduma hiyo.
1Timotheo 5:5 “Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini Lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku.”
Luka 2:36-38 “Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.”
Walikuwa ni wajane ambao waliishi maisha matakatifu na kujiepusha na lawama hawakuruhusu miili yao iwake tamaa na hawakuwa na mpango wa kuolewa tena bali waliishi maisha ya utauwa, tumaini lao ni Yesu.
1Timotheo 5:5-7 “Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku. Bali, yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai.Mambo hayo pia uyaagize, ili wasiwe na lawama.”
Walikuwa ni wajane ambao sio wasichana sio wale wanaotamani kuolewa tena bali ni wajane ambao umri wao ni mkubwa na hawahitaji mume tena kwa hiyo Paulo alishauri ikiwezekana wawe na miaka sitini kwenda juu na wale wanaojisikia kuolewa tena alisema waolewe wawe na nyumba zao.
1Timotheo 5:9-14 “Mjane asiandikwe isipokuwa umri wake amepata miaka sitini; naye amekuwa mke wa mume mmoja; naye ameshuhudiwa kwa matendo mema; ikiwa amelea watoto, ikiwa amekaribisha wageni, ikiwa amewaosha watakatifu miguu, ikiwa amewasaidia wateswao, ikiwa amefuata kwa bidii kila tendo jema. Bali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao, maana, wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa; nao wana hukumu kwa kuwa wameiacha imani yao ya kwanza. Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizunguka-zunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa. Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu.”
Kutumia vibaya mazingira magumu ya wajane – Kuwaheshimu wajane pia kulikuwa na maana ya kutoyatumia vibaya mazingira yao ya uhitaji kwa faida, Yesu Kristo aliwahi kuwalaumu Mafarisayo ambao kwa sababu za kidini waliyatumia mazingira yao ya kidini kuwatembelea wajane na kuonyesha kama wanawahurumia lakini wakiwa na nia ovu, au nia ya kutumia mazingira ya kidini kufunika uovu uliokuwa katika mioyo yao, na katika namna ya wazi walikuwa wakisali sala ndeefu sana ili kujiziba kwa jamii ya kuwa wanawajali wajane lakini kumbe walikuwa wanataka kuyatumia mazingira yao magumu kwa nia ovu, kwa hiyo katazo la Kristo ni kuwa mafarisayo walikuwa wanaonekana kama wanajali na kuheshimu sana wajane lakini ukweli ni kuwa walikuwa wanatumia mazingira magumu waliyo nayo wajane kwa faida zao, aidha kwaajili ya kupikiwa na kuhudumiwa ili wale, au kwaajili ya kupata tiba za kihisia kutoka kwa wajane hao, na mengine hatuyasemi kwa sababu Yesu mwenyewe hakuyasema, kwa hiyo utembeleo wao kwa nje ungeonekana kuwa ni wa kidini lakini kwa ndani walikuwa wanatengeneza mazigira ya kuleta faraja zisizokuwa za kiungu, kwa msingi huo watu wa Mungu hatupaswi kuwatumia wajane kwa misingi ya kufaidika kwetu kutoka kwao bali kwaajili ya utukufu wa Mungu, ukimtembelea Mjane huku ukiwa una nia nyingine mume wao ambaye ni Mungu anakuona!
Mathayo 23:14 “[Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi.]”
Hitimisho:
Neno la Mungu limeonyesha mkazo mkubwa sana na wa muhimu kuhusu kuwahudumia wajane na kuainisha kundi la wajane wanaopaswa kuhudumiwa lakini vile vile limetoa vigezo kwa wajane wanaojulikana katikia maandiko kama wajane walio wajane kweli kweli, Maandiko yanaelezea kuwa wao ni wa Muhimu na kwamba wanahitaji kupendwa, kujaliwa, kusaidiwa, kutiwa moyo na kulindwa, kwa kuwa kanisa tumepewa wajibu na agizo la Mungu ni pana uko umuhmu wa kutokulisahau jambo hili na hivyo Roho wa Mungu anataka tulikumbuke hili ili tuweze kujipatia Baraka zinazokusudiwa, kwa kuwajali na kushughulika nao tunajiweka katika nafasi ya Kristo inayoonyesha kuwa kanisa linajali, kwa hiyo pamoja na maagizo mengine hatupaswi kujisahau kama kanisa na kufumbia macho swala ambalo Mungu amelipa kipaumbele, Mungu mwenyewe amejionyesha kujishughulisha na wajane katika namna ya kipekee, Mungu aliwahudumia wajane kadhaa kwa miujiza mikubwa ili kutimiza mahitaji yao, wajane wakikuombea mtumishi wa Mungu, ujue ya kuwa Mungu anaheshimu sana maombi yao na kuwasikiliza sana, kila mtumishi wa Mungu anahitaji kuwa na waombezi wanaomuombea usiku na mchana unapofikiri kuhusu watu wa kukuombea maana yake unapaswa kuwafikiri wajane. Jicho na sikio la Mungu linawasikiliza sana kama tu endapo watasimama katika zamu yao. Kwa hiyo unaweza kuwa na timu ya maombi na kupa jina Ana binti Fanuel na ukawa na wajane wanaofanya kazi ya kuombea huduma mbalimbali lakini zaidi sana Mchungaji wa kanisa la mahali pamoja bila kusahau maombi ya wengine.
Eliya alikaa pamoja na mjane wa sarepta, tukio ambalo hata Yesu alilithibitisha 1Wafalme 17:8-24 “Neno la Bwana likamjia, kusema, Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe. Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya. Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena. Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu? Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake. Akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe. Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. Bwana akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka. Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka orofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai. Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, na ya kuwa neno la Bwana kinywani mwako ni kweli.”
Elisha alimhudumia mjane aliyekuwa na deni 2Wafalme 4:1-7 “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa. Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta. Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina. Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma. Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.”
Na Yesu alimuhudumia mjane aliyekuwa na msiba Luka 7:11-16 “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye.Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake.Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake.”
Wewe na mimi tunafanya nini kuhusu wajane wanaotuizungika katika jamii ya kanisa la mahali pamoja Uongezewe neema
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni