Alhamisi, 6 Machi 2025

Hukumu zake ni za kweli na za haki


Ufunuo 19:1-2 “Baada ya hayo nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, sauti kubwa mbinguni, ikisema, Haleluya; wokovu na utukufu na nguvu zina BWANA MUNGU wetu. kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na za haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake.”



Utangulizi:

Timothy John Evans (20 November 1924-9 March 1950)  alikuwa ni Dereva wa Roli huko Welsh, aliwahi kushitakiwa kwa kosa la kumuua mkewe Beryl pamoja na binti yake mdogo Geraldine, kwenye makazi yake huko Notting Hill, London nchini Uingereza, January 1950 Evans alikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la mauaji ya Binti yake mdogo na mke wake na tarehe 9 March 1950 alihukumiwa kunyongwa mpaka kufa, wakati wa Kesi hiyo Evans alilalamika kuwa jirani yake wa ghorofa ya chini Bwana John Christie ambaye alikuwa ndiye shahidi namba moja wa mauaji hayo dhidi yake kwamba yeye ndiye muuaji wa mkewe na binti yake.

Miaka mitatu baadaye baada ya kunyongwa hadi kufa kwa Evance, ilikuja kubainika kuwa kweli muuaji alikuwa ni Bwana John Christie, ambaye pia aliuwa wanawake wengine katika matukio yanayofanana na lile,  katika nyumba ile ile, akiwemo mke wake Ethel, Bwana Christie alihukumiwa adhabu ya kifo, na alipokuwa anakaribia kunyongwa alikiri kuwa ni kweli yeye ndiye pia alikuwa mtu aliyehusika na kifo cha binti na mke wa Timothy John Evans, Mahakama kuu ilikuja kupitia upya kesi ya Bwana Evans mnamo mwaka 2004 na kubaini kuwa alihukumiwa kimakosa,  na hivyo kubatilisha maamuzi ya mtu ambaye alikwisha hukumiwa kifo na kunyongwa miaka 54 iliyopita!  

Kwa nini nimeanza na habari hizi za kusikitisha za Timothy Evans?  ni kwa sababu nataka kukuthibitishia kuwa katika moja ya maswala magumu sana duniani ni pamoja na swala la kusimamia haki au swala zima la kutoa hukumu za kweli na za haki, akielewa swala hili na ugumu wake huku akiwa na moyo wa kutaka kusimamia watu wa Mungu na kuwahukumu kwa haki Mfalme Suleimani aliwaza sana juu ya swala hili na kuamua kuwa atamuomba Mungu Hekima ili ahukumu watu hao kwa haki, Na Mungu alifurahishwa sana na ombi la Suleimani kwa sababu Mungu hafurahii udhalimu

1Wafalme 3:4-10 “Basi mfalme akaenda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile. Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi? Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.”

Kutoa haki sio jambo rahisi katika ulimwengu huu ulioharibika na unaotawaliwa na shetani, Mwanadamu ni kiumbe chenye upungufu na kwa sababu hiyo sio rahisi sana wakati mwingine mwanadamu kutoa haki, kwa sababu mtazamo wa kibinadamu unatofautiana sana na wa Mungu. Maandiko yanaonyesha wazi kuwa ni Yesu Kristo pekee ndiye atakayekuja kutoka hukumu ya haki kwa sababu Roho wa Bwana atakuwa juu yake, na haki itakuwa mshipi wa viouno vyake ona:-

Isaya 11:2-5. “Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.”

Unaposoma kisa hicho hapo juu cha Bwana Timothy John Evans utaweza kubaini na kugundua kuwa sio watu wote walioko magerezani wako huko kwa haki, wengine waliingia magerezani kwa uonevu na kwa sababu ya kuongozwa na waamuzi ambao wanasukumwa na misisimko, hawana hekima, wanasikiliza upande mmoja ama hawafanyi uchambuzi wa kina au kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi unaojitosheleza, na kwa bahati mbaya hata makanisani ziko hukumu za namna mbalimbali zinazotolewa na hasa katika makanisa ya kiroho, hukumu hizo hutolewa wakati mwingine kwa misisimko na bila kuzingatia misingi ya haki na uongozi wa Roho wa Mungu na matokeo yake kumekuweko na watu wengi sana walioumizwa na kujeruhiwa mioyo, Lakini jambo mojawapo kubwa la kumshukuru Mungu ni kuwa Yeye Mungu wetu Hukumu zake ni za kweli na za haki.

Zaburi 119:136-138 “Macho yangu yachuruzika mito ya maji, Kwa sababu hawaitii sheria yako. Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki, Na hukumu zako ni za adili.Umeziagiza shuhuda zako kwa haki, Na kwa uaminifu mwingi.”

Tutajifunza somo hili Hukumu zake ni za kweli na haki kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-


·         Kwa nini wanadamu hawawezi kuhukumu kwa haki?

·         Hukumu zake ni za kweli na haki!


Kwa nini wanadamu hawawezi kuhukumu kwa haki?

Mwanadamu ni kiumbe mwenye upungufu na mipaka na kwa sababu hiyo katika kutoa hukumu anazingirwa na vikwazo kadhaa vinavyopelekea kushindwa kutenda haki, hii ni tofauti na mtazamo wa Mungu ambaye yeye hana mipaka ya kibinadamu na kwa sababu hiyo anaweza kufanya hukumu za kweli na za haki kwa sababu yeye anajua yote na hana upungufu wa wema yeye amejaa wema (Omnibenevole)  na ni mkamilifu, hana upendeleo wala haendeshwi na hisia, hana vikwazo vya kuona tofauti na wanadamu ambao wao wanaweza kuona kwa mitazamo ya nje.

1Samuel 16:7 “Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.”

Tunaweza kujiuliza maswali ni kwa nini Mwanadamu hawezi kuhukumu kwa haki? hapa kuna sababu kadhaa zinazomuathiri mwanadamu na sababu ni kwanini mwanadamu hawezi kuhukumu kwa haki?


1.        Wanadamu wana ufahamu finyu

 

Tangu anguko la mwanadamu mwanadamu amekuwa kiumbe mwenye mapungufu mengi na mojawapo ni ufinyu wa maarifa na ufahamu, kwa sababu hiyo mwanadamu hawezi kufahamu kweli zote, nia ya moyo wa mtu, msukumo wa mazingira  hali na ukweli wa mambo, moyo wa mwanadamu unatajwa katika maandiko kuwa una ugonjwa wa kufisha,  nia ya mwanadamu inaweza kuwa sahihi machoni pake tu lakini zaidi ya yote hata pamoja na uwepo wa Roho Mtakatifu maandiko yanakiri kuwa tunafahamu kwa sehemu tu mpaka wakati ule utimilifu utakapokuja kwa sababu ya ufahamu huo finyu anaathirika kimaamuzi

 

Yeremia 17:9-10 “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.”              

 

Mithali 14:12 “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.”                

 

1Wakorintho 13:12 “Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.”

 

2.       Wanadamu wana ubaguzi na upendeleo.

 

Wanadamu kwa kawaida wanathiriwa na uzoefu wao, tamaduni zao, na historia zao, na wakati mwingine hisia na chuki katika mioyo yao,  na ubaguzi usiokuwa rasmi, maswala kama haya ya kibinadamu yanapotangulizwa mbele katika hukumu yanaweza kupelekea mwanadamu asitende haki wakati wa kuhukumu, wakati mwingine mtu anaweza kuhukumiwa kwa sababu ya kabila yake tu, kwa sababu wewe ni msonjo basi unaweza kufikiriwa kuwa u mkorofi, au kwa sababu wewe ni mbondei unaweza kutafasiriwa kuwa una kiburi, au kwa sababu wewe ni mgogo au mhaya mtu anaweza kuhitimisha tu kuwa u mzinzi na mpenda ngono, au kwa sababu wewe ni mnyiramba unaweza kuhesabika kuwa u mtu katili na kama wewe u mmachame unaweza kufikiriwa kuwa una roho mbaya hukumu ya mwanadamu inaweza kutanguliwa na mitazamo mingi isiyo sahihi na ambayo sio ya kiungu na ama wakati mwingine mtu anayetangulia kushitaki anaweza kufikiriwa kuwa ndio yuko sahihi.

 

Yakobo 2:1-4 “Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu,je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu?

               

Mithali 18:17 “Ajiteteaye kwanza huonekana kuwa ana haki; Lakini jirani yake huja na kumchunguza.”               

 

3.       Mwanadamu awaye yote ana asili ya dhambi.

 

Uwezo wa mwanadamu wa kuhukumu umeathiriwa na dhambi, dhambi inaweza kutuelekeza katika ubinafsi, hofu, ujinga na umimi, pia dhambi inaaathiri maisha yetu na kutufanya tujawe na kiburi na hata hali ya kutokutenda haki, na kwa sababu hiyo mwenendo wetu katika utoaji wa haki unaathiriwa na dhambi na kwahiyo wakati mwingi tunashindwa kusimama katika haki na kutohukumu kwa haki na kweli

 

Warumi 3:10-12, 23 “kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.23 “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;          

 

Yakobo 4:12 “Ndugu, msisingiziane; amsingiziaye ndugu yake, au kumhukumu ndugu yake, huisingizia sheria na kuihukumu sheria. Lakini ukiihukumu sheria, huwi mtenda sheria, bali umekuwa hakimu. Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine?      

 

4.       Mwanadamu ana uoni hafifu

 

Uwezo wetu wa kuona mambo kamwe hauwezi kufananishwa na namna Mungu anavyoona mambo, yale tunayoyana sisi tunaona sehemu ndogo sana ya picha, wakati Mungu anaona picha zima kuanzia mwanzo, kati hadi mwisho, lakini kama haitoshi anaiona dhamira kwa mbali kwa sababu hiyo mwanadamu anakosa na kupoteza haki ya kuwa na hukumu za kweli na za haki, Mungu anauwezo wa kumuona mtu akali mbali mwanadamu hana uwezo huo

 

Ayubu 38:1-2 “Ndipo Bwana akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Ni nani huyu atiaye mashauri giza Kwa maneno yasiyo na maarifa?

 

Isaya 55:8-9 “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.”

 

Luka 15:17-20 “ Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. ALIPOKUWA ANGALI MBALI, BABA YAKE ALIMWONA, AKAMWONEA HURUMA, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.”    

 

5.       Mwanadamu ana misukumo ya kihisia.

 

Kila mwanadamu ameumbwa na misikuko ya kihisia kama hasira, woga, wivu, na kadhalika misukumo hiyo ya kihisia inaweza kwa kiasi kikubwa sana kuathiri utoaji wa hukumu na hivyo kumfanya mwanadamu asihukumu kwa haki na kweli, tofauti na Mungu ambaye maandiko yanamtaja kuwa mwingi wa rehema na asiye mwepesi wa hasira

 

Mithali 29:11. “Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote; Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.”

 

Yakobo 1:19-20 “Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika; kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu.

 

Zaburi 145:8-9 “Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, Bwana ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.”

 

6.       Wanadamu wana viwango visivyowiana

 

Viwango vya wanadamu kuhusu haki na uadilifu  havilingani au haviko katika uwiano sawa katika tamaduni moja na tamaduni nyingine, wakati kule Sumbawanga, ukiingia katika shamba la mtu na kukata mahindi ya kuchoma ukawasha moto na kujichomea ukala mwenye shamba akikukuta hawezi kukudhuru kwa sababu anajua ulikuwa na njaa, jambo kama hilo huko Muheza, Tanga, linaweza kuhesabika kuwa ni wizi unaoambatana na dharau ya hali ya juu kwamba mahindi uibe afu kisha uchome humo humo ndani ya shamba, Mungu anakusudia kila mwanadamu awe mtenda haki na haki kwake haiathiriwi na mazingira au tamaduni, viwango vya Mungu vimenyooka havuathiriwi na geografia wala mazingira.

 

Muhubiri 3:16-18 “ Zaidi ya hayo, nikaona tena chini ya jua ya kwamba, Mahali pa hukumu upo uovu, Na mahali pa haki upo udhalimu. Nikasema moyoni mwangu, Mungu atawahukumu wenye haki na wasio haki; kwa kuwa kuna wakati huko kwa kila kusudi na kwa kila kazi. Nikasema moyoni mwangu, Ni kwa sababu ya wanadamu, ili Mungu awajaribu, nao waone ya kuwa wao wenyewe wafanana na wanyama.”              

 

Mika 6:8 “Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!

 

7.       Mwanadamu anakosa upendo uliokamilika

 

Hukumu ya mwanadamu wakati mwingine inapungukiwa na upendo uliokamilika na kwa sababu hiyo wakati wa kuhukumu wanakosa rehema za Mungu, au rehema anayokuwa nayo Mungu wakati wa kushughulika na wanadamu, ukweli tukikosa rehema na upendo tunapoteza maana kabisa

 

1Wakorintho 13:1-3 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.”       

 

Mathayo 7:2 “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa.”

 

8.       Mwanadamu hufanya makosa

 

Wakati Mungu huwa habadiliki wala hakosei, mwanadamu ana tabia ya kubadilika badilika na kufanya makosa, kutokana na hali hii ya uanadamu mara kadhaa watu wamefanya makosa, kumbuka kile kisa cha Timothy John Evans ambaye alinyongwa licha ya kuwa yeye ndiye aliyepoteza mke wake na binti yake mdogo, ona makosa yaliyofanyika! Kumbuka jinsi Pilato alivyonawa mikono na kuwa na uhakika kuwa Yesu hakuwa na hatia lakini kumbuka kuwa ni yeye aliyetoa hukumu ya Yesu kusulubiwa kwa sababu ya mashinikizo ya kisiasa na ubinadamu, kwa kweli unapojihusisha na hukumu au maneno ya kusikia na mambo tata na yasiyo na ushahidi, usikimbilie kuhukumu na badala yake tuiendee hukumu kwa unyenyekevu mkubwa, tegemea hekima ya Mungu au muombe Mungu hekima kila uwapo katika nafasi inayokuhusisha kufanya maamuzi, vinginevyo utakuja kujikuta unajuta                

 

Mithali 3:5-7 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.”

 

Hesabu 23:19 “Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?

Mungu anatuagiza katika neno lake kuacha kuhukumu kwa mitazamo ya kawaida, lakini Mungu anatutaka tuhukumu kwa usahihi

Yohana 7:24 “Basi msihukumu hukumu ya macho tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya hakileo vilio vya haki vinasikika kila kona watu wakiwa wameonewa na kutendewa visivyo haki, unapoona leo hii utitiri wa makanisa pamoja na dini kugeuzwa kuwa biashara au kuwepo kwa uamsho mkubwa lakini wengine wameondoka katika makanisa yao na kupoteza haki zao zote kwa sababu ya kuhukumiwa vibaya, katika kazi zetu hizi za kichungaji na kazi ya Mungu ndugu wa uongo wako kila kona na unaweza wakati mwingine kwa sababu ya siasa za kidini, ukachomekewa na kuonewa na kuhukumiwa pasipo haki na kwa kweli wakati mwingine makosa ya kibinadamu hayo yamewafanya watu wengine kuishi maisha ya kuteseka na kuumizwa sana huku wakisubiria wakati wa Mungu ufike, Je unamkumbuka Yusufu Mwana wa Israel aliyewekwa gerezani kwa sababu ya kushutumiwa kuwa alitaka kumbaka mke wa Potifa na ushahidi ulikuwa ni vazi lake aliloliacha chumbani ni nani ambaye angeliweza kuingilia kati ili haki ya Yusufu ipatikane?

Ukweli ni kuwa yuko Mungu, Ni Mungu peke yake ambaye Hukumu zake ni za kweli na za haki, uko wakati utafika katika maisha yako uatamshangilia Mungu na kusema haleluya kweli nimetambua kuwa hukumu zako ni za kweli na za haki. Abrahamu alimtambua Mungu kama mhukumu ulimwengu na alipokuwa akiomba aliamini kuwa Mungu atatenda haki na atahukumu kwa haki

Mwanzo 18:25-26 “Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; MHUKUMU ULIMWENGU WOTE ASITENDE HAKI? BWANA akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao.”

Mungu anaweza kuwahukumu adui zetu sawasawa na haki yake na neno lake, hata kama kuna wakati wanaonekana kustawi usiogope washindanao na Bwana watapondwa kabisa Bwana ataihukumu miisho ya nchi, naye atampa mfalme wake nguvu na kuitukuza pemba ya masihi wake Asante sana Mungu mwingi wa rehema, asante sana Mungu mwenye haki asante sana kwa fadhili zako asante sana kwa sababu kati kati ya miungu hakuna aliye kama wewe ni wewe pekee yako mwenye rula isiyopinda, ni wewe peke yako unayeweza kuishangaza dunia ni wewe peke yako uliyempa mtumwa wako uvumilivu, ni wewe peke yako uliyempa mtumwa wako kuvumilia adui zake ni wewe peke yako uhukumuye kwa haki fadhili zina wewe milele na milele!, haki imesimama na kisasi kimelipwa na sasa Bwana utamwangalia mtumishi wake na kumrejeshea kila kilichopotezwa na adui kwa sababu ya uonevu, Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana Kwa maana hakuna yeyote ila wewe, wala hakuna mwamba kama Mungu wangu!, walinena wakatakabari, walijivuna wakatoa maneno ya kiburi vinywani mwao Lakini hawakujua kuwa Mungu ni mwingi wa maarifa  nay a kuwa matendo hupimwa nay eye, kwa mizani yake isiyo na upendeleo, nguvu za waonevu zimevunjika, waliojikwaa wamepigwa hofu, walioshiba wanaona njaa, Kwa sababu aliye mnyone amesimikwa na Bwana, yeye hulinda miguu ya watakatifu, na hunyamazisha miguu ya wqaovu gizani, washinanao naye watapondwa Bwana atawapiga kwa radi, yeye anaweza kuhukumu hata mwisho wan chi, yeye yu aweza kumtukuza masihi wake! ni yeye pekee Mungu wetu na Mungu wangu, Mungu wa baba zangu Mungu mwenye kuogofya Mungu ahukumuye kwa kweli na kwa haki, humu zako zimenifurahisha, matendo yako yamependezwa nami ninakupenda kuliko wazee wangu, maana rehema zako na fadhli zako ni za milele, hukumwacha mtakatifu wako ane uharibifu! Wala mwenye haki wako aende kuzimu fadhili zina wewe milelele na milele! Na hukumu zako nimezithibitisha haki kwako haipindi, kweli kwako zimenyooshwa tuma malaika zako walitangaze hili, tuma makerubi walibandike na maserafi waliimbe kwamba utukufu na nguvu zina wewe na hukumu zako ni za kweli na za haki hata milele na milele! (Zaburi ya Mwandishi).

Hukumu zake ni za kweli na haki!

Ufunuo 19:1-2 “Baada ya hayo nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, sauti kubwa mbinguni, ikisema, Haleluya; wokovu na utukufu na nguvu zina BWANA MUNGU wetu. kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na za haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake.”

Tofauti na Wanadamu ambao tumejifunza kwamba kwa asili wanaathiriwa na maswala mengi hivyo uwezo wao wa kutenda haki au kufanya hukumu za kweli na za haki hauwezi kukidhi vigezo na utendaji wa Mungu, kwa upande wake yeye Mungu anaweza kufanya hukumu za kweli na za haki kwa sababu zifuatazo;-

1.       Yeye anajua yote – kwa asili Mungu anajua mambo yote (Omniscience), anajua kila kitu tangu wakati uliopita uliopo na ujao, na zaidi ya yote anaijua nia ya mwanadamu moyo wake na mazingira yake, ujuzi wake mkamilifu unamfanya asiwe na makosa katika uchunguzi wala upelelezi, wakati mwanadamu anafungwa na mipaka na kuhitaji ushahidi Mungu yeye haitaji ushahidi, yeye mwenyewe ana uwezo mkubwa sana wa kufanya uchunguzi na kumjua mwanadamu katika kila jambo kuanzia kuingia kwake na kutoka kwake!

 

Zaburi 139:1-4 “Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana.”

 

2.       Yeye ni mwema – Kwa asili Mungu ni mwema  na mwaminifu, wema wake hauna mipaka (omnibenevolence) kutokana na tabia yake ya asili ya wema unamfanya yeye Mungu kuwa mwenye haki katika njia zake zote bila dosari kama za kibinadamu, na kwa sababu hiyo anaweza kufanya maamuzi yasiyo na utata, Licha ya kuwa mwema yeye pia ni chanzo cha wema wote, ni chanzo cha upendo, na haki pia, anapohukumu yeye anahukumu katika haki kwa sababu ya tabia yake na mwenendo wake uliojawa na uadilifu, usio na hofu wala upendeleo, ulio na rehema na neema, na wenye viwango vya juu kabisa vya haki

 

Zaburi 145:17 “Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.”

 

Zaburi 100:5 “Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; Rehema zake ni za milele; Na uaminifu wake vizazi na vizazi.

 

3.       Yeye hatazami kama wanadamu watazamavyo – Njia za Mungu ziko juu sana haziwezi kamwe kulinganishwa na njia za wanadamu kwa sababu hiyo yeye hufanya mambo katika njia na namna tofauti sana na ile inayodhaniwa au kukusudiwa na wanadamu,  Yeye ni mwenye haki na wanadamu ni waongo

 

Isaya 55:8-9 “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.”               

Hitimisho!

Hukumu zake ni za kweli na za haki ni usemi maarufu ambao umejirudia mara kadhaa katika maandiko ukionyesha kuwa maamuzi ya Mungu ni ya kweli, ya haki ya adilifu, hii maana yake ni kwakuwa yeye ni Mungu uweza wake wa kiungu unaaminika kukaa katika misingi ya kutokuonea mtu wala kufanya mambo kwa upendeleo wala kupokea uso wa mwanadamu, hakuna nafasi ya kutazama mambo kwa mtazamo usio sahihi kama wanadamu yeye uhukumu kwa ukamilifu

Ufunuo 16:5-7 “Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi; kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili. Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako.”

Zaburi 19:9-10 “Kicho cha Bwana ni kitakatifu, Kinadumu milele. Hukumu za Bwana ni kweli, Zina haki kabisa. Ni za kutamanika kuliko dhahabu, Kuliko wingi wa dhahabu safi. Nazo ni tamu kuliko asali, Kuliko sega la asali.

Kwa kujua jinsi ambavyo Mungu uhukumu vizuri na kwa haki na kwa rehema Daudi alichagua kuangukia katika hukumu ya Mungu kwa sababu alielewa Mungu atamhukumu kwa rehema

1Nyakati 21:9-13 “Naye Bwana akanena na Gadi, mwonaji wake Daudi, akisema, Nenda ukanene na Daudi, ukisema, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya ujichagulie moja, nikutendee hilo. Basi Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Bwana asema hivi, Kubali upendavyo; miaka mitatu ya njaa; au miezi mitatu kuangamia mbele ya adui zako, ukipatwa na upanga wa watesi wako; au siku tatu upanga wa Bwana, yaani tauni katika nchi, na malaika wa Bwana akiharibu kati ya mipaka yote ya Israeli. Haya basi ufikiri ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na nianguke katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake ni nyingi sana; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.”

Siku zote wanadamu wanapokuhukumu kwa njia isiyo halali usilalamike Mwambie Bwana uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo, Ni Mungu peke yake anapohukumu ndiye anayejua anachokitenda, lakini wanadamu hawajui walitendalo wao wana mipaka najua wako watu wengi sana wameumizwa serikalini, makanisani, mimi pia niliwahi kuumizwa, niliwahi kuhukumiwa, niliwahi kusemwa vibaya wanadamu walinihukumu sawa na midomo ya washitaki zangu, lakini nilinyamaza na namshukuru Mungu kwani amenifundisha mengi sasa najua wazi kuwa Mungu wangu ni Mungu mwenye kuogopwa sana kwa sababu Hukumu zake ni za kweli na za haki, kama Bwana alivyonitendea mimi akutendee na wewe pia, naelewa na nilielewa tangu zamani ya kuwa hakumwacha mtu aliwatendea haki wote walioonewa, Haki yako itapatikana kwa Mungu aliye hai usikate tamaa endelea kumtumainia yeye na kumuachia yeye naye atakushangaza, amenishangaza mara nyingi na namuomba Mungu akushangaze na wewe pia.

Zaburi 105:14-15 “Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.”

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!