Ufunuo 19:1-2 “Baada ya hayo nikasikia
sauti kama sauti ya makutano mengi, sauti kubwa mbinguni, ikisema, Haleluya;
wokovu na utukufu na nguvu zina BWANA MUNGU wetu. kwa kuwa hukumu zake ni za
kweli na za haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa
uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake.”
Utangulizi:
Timothy John Evans (20 November
1924-9 March 1950) alikuwa ni Dereva
wa Roli huko Welsh, aliwahi
kushitakiwa kwa kosa la kumuua mkewe Beryl
pamoja na binti yake mdogo Geraldine,
kwenye makazi yake huko Notting Hill,
London nchini Uingereza, January 1950
Evans alikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la mauaji ya Binti yake mdogo na
mke wake na tarehe 9 March 1950
alihukumiwa kunyongwa mpaka kufa, wakati wa Kesi hiyo Evans alilalamika kuwa jirani yake wa ghorofa ya chini Bwana John Christie ambaye alikuwa
ndiye shahidi namba moja wa mauaji hayo dhidi yake kwamba yeye ndiye muuaji wa
mkewe na binti yake.
Miaka mitatu baadaye baada ya
kunyongwa hadi kufa kwa Evance, ilikuja kubainika kuwa kweli muuaji alikuwa ni Bwana John Christie, ambaye pia aliuwa
wanawake wengine katika matukio yanayofanana na lile, katika nyumba ile ile, akiwemo mke wake Ethel, Bwana Christie alihukumiwa adhabu ya kifo, na alipokuwa anakaribia
kunyongwa alikiri kuwa ni kweli yeye ndiye pia alikuwa mtu aliyehusika na kifo
cha binti na mke wa Timothy John Evans,
Mahakama kuu ilikuja kupitia upya kesi ya Bwana Evans mnamo mwaka 2004 na kubaini kuwa alihukumiwa
kimakosa, na hivyo kubatilisha maamuzi
ya mtu ambaye alikwisha hukumiwa kifo na kunyongwa miaka 54 iliyopita!
Kwa nini nimeanza na habari hizi
za kusikitisha za Timothy Evans? ni kwa sababu nataka kukuthibitishia kuwa
katika moja ya maswala magumu sana duniani ni pamoja na swala la kusimamia haki
au swala zima la kutoa hukumu za kweli na za haki, akielewa swala hili na ugumu
wake huku akiwa na moyo wa kutaka kusimamia watu wa Mungu na kuwahukumu kwa
haki Mfalme Suleimani aliwaza sana juu ya swala hili na kuamua kuwa atamuomba
Mungu Hekima ili ahukumu watu hao kwa haki, Na Mungu alifurahishwa sana na ombi
la Suleimani kwa sababu Mungu hafurahii udhalimu
1Wafalme 3:4-10 “Basi mfalme akaenda
Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu.
Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile. Na huko
Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba
utakalo nikupe. Sulemani akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu
fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na
katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana
umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu
wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu;
nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa
wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa,
wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako
moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani
awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi? Neno hili likawa jema machoni pa
Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.”
Kutoa haki sio jambo rahisi
katika ulimwengu huu ulioharibika na unaotawaliwa na shetani, Mwanadamu ni
kiumbe chenye upungufu na kwa sababu hiyo sio rahisi sana wakati mwingine
mwanadamu kutoa haki, kwa sababu mtazamo wa kibinadamu unatofautiana sana na wa
Mungu. Maandiko yanaonyesha wazi kuwa ni Yesu Kristo pekee ndiye atakayekuja
kutoka hukumu ya haki kwa sababu Roho wa Bwana atakuwa juu yake, na haki itakuwa
mshipi wa viouno vyake ona:-
Isaya 11:2-5. “Na roho ya Bwana atakaa juu
yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya
kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa
kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa
masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa
dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya
midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu
mshipi wa kujifungia.”
Unaposoma kisa hicho hapo juu cha
Bwana Timothy John Evans utaweza
kubaini na kugundua kuwa sio watu wote walioko magerezani wako huko kwa haki,
wengine waliingia magerezani kwa uonevu na kwa sababu ya kuongozwa na waamuzi
ambao wanasukumwa na misisimko, hawana hekima, wanasikiliza upande mmoja ama
hawafanyi uchambuzi wa kina au kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi
unaojitosheleza, na kwa bahati mbaya hata makanisani ziko hukumu za namna
mbalimbali zinazotolewa na hasa katika makanisa ya kiroho, hukumu hizo hutolewa
wakati mwingine kwa misisimko na bila kuzingatia misingi ya haki na uongozi wa
Roho wa Mungu na matokeo yake kumekuweko na watu wengi sana walioumizwa na
kujeruhiwa mioyo, Lakini jambo mojawapo kubwa la kumshukuru Mungu ni kuwa Yeye
Mungu wetu Hukumu zake ni za kweli na za haki.
Zaburi 119:136-138 “Macho yangu yachuruzika
mito ya maji, Kwa sababu hawaitii sheria yako. Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye
haki, Na hukumu zako ni za adili.Umeziagiza shuhuda zako kwa haki, Na kwa
uaminifu mwingi.”
Tutajifunza somo hili Hukumu zake ni za kweli na haki kwa
kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
·
Kwa nini
wanadamu hawawezi kuhukumu kwa haki?
·
Hukumu
zake ni za kweli na haki!
Kwa nini wanadamu hawawezi kuhukumu kwa haki?
Mwanadamu ni kiumbe mwenye
upungufu na mipaka na kwa sababu hiyo katika kutoa hukumu anazingirwa na
vikwazo kadhaa vinavyopelekea kushindwa kutenda haki, hii ni tofauti na mtazamo
wa Mungu ambaye yeye hana mipaka ya kibinadamu na kwa sababu hiyo anaweza
kufanya hukumu za kweli na za haki kwa sababu yeye anajua yote na hana upungufu
wa wema yeye amejaa wema (Omnibenevole) na ni mkamilifu, hana upendeleo wala haendeshwi
na hisia, hana vikwazo vya kuona tofauti na wanadamu ambao wao wanaweza kuona kwa
mitazamo ya nje.
1Samuel 16:7 “Lakini Bwana akamwambia
Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi
nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama
sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.”
Tunaweza kujiuliza maswali ni kwa
nini Mwanadamu hawezi kuhukumu kwa haki? hapa kuna sababu kadhaa zinazomuathiri
mwanadamu na sababu ni kwanini mwanadamu hawezi kuhukumu kwa haki?
1.
Wanadamu wana ufahamu finyu
Tangu anguko la
mwanadamu mwanadamu amekuwa kiumbe mwenye mapungufu mengi na mojawapo ni ufinyu
wa maarifa na ufahamu, kwa sababu hiyo mwanadamu hawezi kufahamu kweli zote,
nia ya moyo wa mtu, msukumo wa mazingira
hali na ukweli wa mambo, moyo wa mwanadamu unatajwa katika maandiko kuwa
una ugonjwa wa kufisha, nia ya mwanadamu
inaweza kuwa sahihi machoni pake tu lakini zaidi ya yote hata pamoja na uwepo
wa Roho Mtakatifu maandiko yanakiri kuwa tunafahamu kwa sehemu tu mpaka wakati
ule utimilifu utakapokuja kwa sababu ya ufahamu huo finyu anaathirika kimaamuzi
Yeremia 17:9-10 “Moyo
huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye
kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu
kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.”
Mithali 14:12 “Iko
njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.”
1Wakorintho 13:12 “Maana
wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa
uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami
ninavyojuliwa sana.”
2.
Wanadamu
wana ubaguzi na upendeleo.
Wanadamu kwa
kawaida wanathiriwa na uzoefu wao, tamaduni zao, na historia zao, na wakati
mwingine hisia na chuki katika mioyo yao,
na ubaguzi usiokuwa rasmi, maswala kama haya ya kibinadamu
yanapotangulizwa mbele katika hukumu yanaweza kupelekea mwanadamu asitende haki
wakati wa kuhukumu, wakati mwingine mtu anaweza kuhukumiwa kwa sababu ya kabila
yake tu, kwa sababu wewe ni msonjo basi unaweza kufikiriwa kuwa u mkorofi, au
kwa sababu wewe ni mbondei unaweza kutafasiriwa kuwa una kiburi, au kwa sababu
wewe ni mgogo au mhaya mtu anaweza kuhitimisha tu kuwa u mzinzi na mpenda
ngono, au kwa sababu wewe ni mnyiramba unaweza kuhesabika kuwa u mtu katili na
kama wewe u mmachame unaweza kufikiriwa kuwa una roho mbaya hukumu ya mwanadamu
inaweza kutanguliwa na mitazamo mingi isiyo sahihi na ambayo sio ya kiungu na
ama wakati mwingine mtu anayetangulia kushitaki anaweza kufikiriwa kuwa ndio
yuko sahihi.
Yakobo 2:1-4 “Ndugu
zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa
kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu
na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi
mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali
pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu,je!
Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu?”
Mithali 18:17 “Ajiteteaye
kwanza huonekana kuwa ana haki; Lakini jirani yake huja na kumchunguza.”
3.
Mwanadamu
awaye yote ana asili ya dhambi.
Uwezo wa
mwanadamu wa kuhukumu umeathiriwa na dhambi, dhambi inaweza kutuelekeza katika
ubinafsi, hofu, ujinga na umimi, pia dhambi inaaathiri maisha yetu na kutufanya
tujawe na kiburi na hata hali ya kutokutenda haki, na kwa sababu hiyo mwenendo
wetu katika utoaji wa haki unaathiriwa na dhambi na kwahiyo wakati mwingi
tunashindwa kusimama katika haki na kutohukumu kwa haki na kweli
Warumi 3:10-12, 23 “kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna
afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna
mtenda mema, la! Hata mmoja.23 “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na
kupungukiwa na utukufu wa Mungu;”
Yakobo 4:12 “Ndugu,
msisingiziane; amsingiziaye ndugu yake, au kumhukumu ndugu yake, huisingizia
sheria na kuihukumu sheria. Lakini ukiihukumu sheria, huwi mtenda sheria, bali
umekuwa hakimu. Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye
kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine?”
4.
Mwanadamu
ana uoni hafifu
Uwezo wetu wa
kuona mambo kamwe hauwezi kufananishwa na namna Mungu anavyoona mambo, yale
tunayoyana sisi tunaona sehemu ndogo sana ya picha, wakati Mungu anaona picha
zima kuanzia mwanzo, kati hadi mwisho, lakini kama haitoshi anaiona dhamira kwa
mbali kwa sababu hiyo mwanadamu anakosa na kupoteza haki ya kuwa na hukumu za
kweli na za haki, Mungu anauwezo wa kumuona mtu akali mbali mwanadamu hana
uwezo huo
Ayubu 38:1-2 “Ndipo
Bwana akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Ni nani huyu atiaye
mashauri giza Kwa maneno yasiyo na maarifa? ”
Isaya 55:8-9 “Maana
mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. Kwa
maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi
juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.”
Luka 15:17-20 “ Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni
watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa
ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba,
nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye
kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. ALIPOKUWA ANGALI
MBALI, BABA YAKE ALIMWONA, AKAMWONEA HURUMA, akaenda mbio akamwangukia
shingoni, akambusu sana.”
5.
Mwanadamu
ana misukumo ya kihisia.
Kila mwanadamu
ameumbwa na misikuko ya kihisia kama hasira, woga, wivu, na kadhalika misukumo
hiyo ya kihisia inaweza kwa kiasi kikubwa sana kuathiri utoaji wa hukumu na
hivyo kumfanya mwanadamu asihukumu kwa haki na kweli, tofauti na Mungu ambaye
maandiko yanamtaja kuwa mwingi wa rehema na asiye mwepesi wa hasira
Mithali 29:11. “Mpumbavu
hudhihirisha hasira yake yote; Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.”
Yakobo 1:19-20 “Hayo
mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si
mwepesi wa kusema; wala kukasirika; kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi
haki ya Mungu.”
Zaburi 145:8-9 “Bwana
ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, Bwana
ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.”
6.
Wanadamu
wana viwango visivyowiana
Viwango
vya wanadamu kuhusu haki na uadilifu
havilingani au haviko katika uwiano sawa katika tamaduni moja na tamaduni
nyingine, wakati kule Sumbawanga, ukiingia katika shamba la mtu na kukata
mahindi ya kuchoma ukawasha moto na kujichomea ukala mwenye shamba akikukuta
hawezi kukudhuru kwa sababu anajua ulikuwa na njaa, jambo kama hilo huko
Muheza, Tanga, linaweza kuhesabika kuwa ni wizi unaoambatana na dharau ya hali
ya juu kwamba mahindi uibe afu kisha uchome humo humo ndani ya shamba, Mungu
anakusudia kila mwanadamu awe mtenda haki na haki kwake haiathiriwi na
mazingira au tamaduni, viwango vya Mungu vimenyooka havuathiriwi na geografia
wala mazingira.
Muhubiri 3:16-18 “ Zaidi
ya hayo, nikaona tena chini ya jua ya kwamba, Mahali pa hukumu upo uovu, Na
mahali pa haki upo udhalimu. Nikasema moyoni mwangu, Mungu atawahukumu wenye
haki na wasio haki; kwa kuwa kuna wakati huko kwa kila kusudi na kwa kila kazi.
Nikasema moyoni mwangu, Ni kwa sababu ya wanadamu, ili Mungu awajaribu, nao
waone ya kuwa wao wenyewe wafanana na wanyama.”
Mika 6:8 “Ee
mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila
kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!”
7.
Mwanadamu
anakosa upendo uliokamilika
Hukumu ya
mwanadamu wakati mwingine inapungukiwa na upendo uliokamilika na kwa sababu hiyo
wakati wa kuhukumu wanakosa rehema za Mungu, au rehema anayokuwa nayo Mungu
wakati wa kushughulika na wanadamu, ukweli tukikosa rehema na upendo tunapoteza
maana kabisa
1Wakorintho 13:1-3 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo,
nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri
zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha
milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha
maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii
kitu.”
Mathayo 7:2 “Msihukumu,
msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa;
na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa.”
8.
Mwanadamu
hufanya makosa
Wakati Mungu
huwa habadiliki wala hakosei, mwanadamu ana tabia ya kubadilika badilika na
kufanya makosa, kutokana na hali hii ya uanadamu mara kadhaa watu wamefanya
makosa, kumbuka kile kisa cha Timothy
John Evans ambaye alinyongwa licha ya kuwa yeye ndiye aliyepoteza mke wake
na binti yake mdogo, ona makosa yaliyofanyika! Kumbuka jinsi Pilato alivyonawa
mikono na kuwa na uhakika kuwa Yesu hakuwa na hatia lakini kumbuka kuwa ni yeye
aliyetoa hukumu ya Yesu kusulubiwa kwa sababu ya mashinikizo ya kisiasa na
ubinadamu, kwa kweli unapojihusisha na hukumu au maneno ya kusikia na mambo
tata na yasiyo na ushahidi, usikimbilie kuhukumu na badala yake tuiendee hukumu
kwa unyenyekevu mkubwa, tegemea hekima ya Mungu au muombe Mungu hekima kila
uwapo katika nafasi inayokuhusisha kufanya maamuzi, vinginevyo utakuja kujikuta
unajuta
Mithali 3:5-7 “Mtumaini
Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia
zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni
pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.”
Hesabu 23:19 “Mungu
si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda?
Iwapo amenena, hatalifikiliza?”
Mungu anatuagiza katika neno lake
kuacha kuhukumu kwa mitazamo ya kawaida, lakini Mungu anatutaka tuhukumu kwa
usahihi
Yohana 7:24 “Basi msihukumu hukumu ya macho
tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya haki” leo vilio vya haki
vinasikika kila kona watu wakiwa wameonewa na kutendewa visivyo haki, unapoona
leo hii utitiri wa makanisa pamoja na dini kugeuzwa kuwa biashara au kuwepo kwa
uamsho mkubwa lakini wengine
wameondoka katika makanisa yao na kupoteza haki zao zote kwa sababu ya
kuhukumiwa vibaya, katika kazi zetu hizi za kichungaji na kazi ya Mungu ndugu
wa uongo wako kila kona na unaweza wakati mwingine kwa sababu ya siasa za kidini,
ukachomekewa na kuonewa na kuhukumiwa pasipo haki na kwa kweli wakati mwingine
makosa ya kibinadamu hayo yamewafanya watu wengine kuishi maisha ya kuteseka na
kuumizwa sana huku wakisubiria wakati wa Mungu ufike, Je unamkumbuka Yusufu
Mwana wa Israel aliyewekwa gerezani kwa sababu ya kushutumiwa kuwa alitaka
kumbaka mke wa Potifa na ushahidi ulikuwa ni vazi lake aliloliacha chumbani ni
nani ambaye angeliweza kuingilia kati ili haki ya Yusufu ipatikane?
Ukweli ni kuwa yuko Mungu, Ni
Mungu peke yake ambaye Hukumu zake ni za kweli na za haki, uko wakati utafika
katika maisha yako uatamshangilia Mungu na kusema haleluya kweli nimetambua
kuwa hukumu zako ni za kweli na za haki. Abrahamu alimtambua Mungu kama mhukumu
ulimwengu na alipokuwa akiomba aliamini kuwa Mungu atatenda haki na atahukumu
kwa haki
Mwanzo 18:25-26 “Hasha usifanye hivyo,
ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; MHUKUMU
ULIMWENGU WOTE ASITENDE HAKI? BWANA akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki
hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao.”
Mungu anaweza kuwahukumu adui
zetu sawasawa na haki yake na neno lake, hata kama kuna wakati wanaonekana
kustawi usiogope washindanao na Bwana watapondwa kabisa Bwana ataihukumu miisho
ya nchi, naye atampa mfalme wake nguvu na kuitukuza pemba ya masihi wake Asante
sana Mungu mwingi wa rehema, asante sana Mungu mwenye haki asante sana kwa
fadhili zako asante sana kwa sababu kati kati ya miungu hakuna aliye kama wewe
ni wewe pekee yako mwenye rula isiyopinda, ni wewe peke yako unayeweza
kuishangaza dunia ni wewe peke yako uliyempa mtumwa wako uvumilivu, ni wewe
peke yako uliyempa mtumwa wako kuvumilia adui zake ni wewe peke yako uhukumuye
kwa haki fadhili zina wewe milele na milele!, haki imesimama na kisasi
kimelipwa na sasa Bwana utamwangalia mtumishi wake na kumrejeshea kila
kilichopotezwa na adui kwa sababu ya uonevu, Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana
Kwa maana hakuna yeyote ila wewe, wala hakuna mwamba kama Mungu wangu!,
walinena wakatakabari, walijivuna wakatoa maneno ya kiburi vinywani mwao Lakini
hawakujua kuwa Mungu ni mwingi wa maarifa
nay a kuwa matendo hupimwa nay eye, kwa mizani yake isiyo na upendeleo,
nguvu za waonevu zimevunjika, waliojikwaa wamepigwa hofu, walioshiba wanaona
njaa, Kwa sababu aliye mnyone amesimikwa na Bwana, yeye hulinda miguu ya
watakatifu, na hunyamazisha miguu ya wqaovu gizani, washinanao naye watapondwa
Bwana atawapiga kwa radi, yeye anaweza kuhukumu hata mwisho wan chi, yeye yu
aweza kumtukuza masihi wake! ni yeye pekee Mungu wetu na Mungu wangu, Mungu wa
baba zangu Mungu mwenye kuogofya Mungu ahukumuye kwa kweli na kwa haki, humu
zako zimenifurahisha, matendo yako yamependezwa nami ninakupenda kuliko wazee
wangu, maana rehema zako na fadhli zako ni za milele, hukumwacha mtakatifu wako
ane uharibifu! Wala mwenye haki wako aende kuzimu fadhili zina wewe milelele na
milele! Na hukumu zako nimezithibitisha haki kwako haipindi, kweli kwako
zimenyooshwa tuma malaika zako walitangaze hili, tuma makerubi walibandike na
maserafi waliimbe kwamba utukufu na nguvu zina wewe na hukumu zako ni za kweli
na za haki hata milele na milele! (Zaburi ya Mwandishi).
Hukumu zake ni za kweli na haki!
Ufunuo 19:1-2 “Baada ya hayo nikasikia
sauti kama sauti ya makutano mengi, sauti kubwa mbinguni, ikisema, Haleluya;
wokovu na utukufu na nguvu zina BWANA MUNGU wetu. kwa kuwa hukumu zake ni za
kweli na za haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa
uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake.”
Tofauti na Wanadamu ambao
tumejifunza kwamba kwa asili wanaathiriwa na maswala mengi hivyo uwezo wao wa
kutenda haki au kufanya hukumu za kweli na za haki hauwezi kukidhi vigezo na
utendaji wa Mungu, kwa upande wake yeye Mungu anaweza kufanya hukumu za kweli
na za haki kwa sababu zifuatazo;-
1.
Yeye
anajua yote – kwa asili Mungu anajua mambo yote (Omniscience), anajua kila kitu tangu wakati uliopita uliopo na
ujao, na zaidi ya yote anaijua nia ya mwanadamu moyo wake na mazingira yake,
ujuzi wake mkamilifu unamfanya asiwe na makosa katika uchunguzi wala upelelezi,
wakati mwanadamu anafungwa na mipaka na kuhitaji ushahidi Mungu yeye haitaji
ushahidi, yeye mwenyewe ana uwezo mkubwa sana wa kufanya uchunguzi na kumjua
mwanadamu katika kila jambo kuanzia kuingia kwake na kutoka kwake!
Zaburi 139:1-4 “Ee
Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe
wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote. Maana
hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana.”
2.
Yeye
ni mwema – Kwa asili Mungu ni mwema
na mwaminifu, wema wake hauna mipaka
(omnibenevolence) kutokana na tabia yake ya asili ya wema unamfanya yeye
Mungu kuwa mwenye haki katika njia zake zote bila dosari kama za kibinadamu, na
kwa sababu hiyo anaweza kufanya maamuzi yasiyo na utata, Licha ya kuwa mwema
yeye pia ni chanzo cha wema wote, ni chanzo cha upendo, na haki pia,
anapohukumu yeye anahukumu katika haki kwa sababu ya tabia yake na mwenendo
wake uliojawa na uadilifu, usio na hofu wala upendeleo, ulio na rehema na neema,
na wenye viwango vya juu kabisa vya haki
Zaburi 145:17 “Bwana
ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.”
Zaburi 100:5 “Kwa
kuwa Bwana ndiye mwema; Rehema zake ni za milele; Na uaminifu wake vizazi na
vizazi.”
3.
Yeye
hatazami kama wanadamu watazamavyo – Njia za Mungu ziko juu sana haziwezi
kamwe kulinganishwa na njia za wanadamu kwa sababu hiyo yeye hufanya mambo
katika njia na namna tofauti sana na ile inayodhaniwa au kukusudiwa na
wanadamu, Yeye ni mwenye haki na
wanadamu ni waongo
Isaya 55:8-9 “Maana
mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. Kwa
maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi
juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.”
Hitimisho!
Hukumu zake ni za kweli na za
haki ni usemi maarufu ambao umejirudia mara kadhaa katika maandiko ukionyesha
kuwa maamuzi ya Mungu ni ya kweli, ya haki ya adilifu, hii maana yake ni
kwakuwa yeye ni Mungu uweza wake wa kiungu unaaminika kukaa katika misingi ya
kutokuonea mtu wala kufanya mambo kwa upendeleo wala kupokea uso wa mwanadamu,
hakuna nafasi ya kutazama mambo kwa mtazamo usio sahihi kama wanadamu yeye
uhukumu kwa ukamilifu
Ufunuo 16:5-7 “Nami nikamsikia malaika wa
maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa
umehukumu hivi; kwa kuwa walimwaga
damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili.
Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na
za haki, hukumu zako.”
Zaburi 19:9-10 “Kicho cha Bwana ni
kitakatifu, Kinadumu milele. Hukumu za Bwana ni kweli, Zina haki kabisa. Ni za
kutamanika kuliko dhahabu, Kuliko wingi wa dhahabu safi. Nazo ni tamu kuliko
asali, Kuliko sega la asali.”
Kwa kujua jinsi ambavyo Mungu
uhukumu vizuri na kwa haki na kwa rehema Daudi alichagua kuangukia katika
hukumu ya Mungu kwa sababu alielewa Mungu atamhukumu kwa rehema
1Nyakati 21:9-13 “Naye Bwana akanena na
Gadi, mwonaji wake Daudi, akisema, Nenda ukanene na Daudi, ukisema, Bwana asema
hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya ujichagulie moja, nikutendee hilo.
Basi Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Bwana asema hivi, Kubali upendavyo;
miaka mitatu ya njaa; au miezi mitatu kuangamia mbele ya adui zako, ukipatwa na
upanga wa watesi wako; au siku tatu upanga wa Bwana, yaani tauni katika nchi,
na malaika wa Bwana akiharibu kati ya mipaka yote ya Israeli. Haya basi ufikiri
ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.Naye Daudi akamwambia Gadi,
Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na nianguke katika mkono wa Bwana; kwa
kuwa rehema zake ni nyingi sana; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.”
Siku zote wanadamu wanapokuhukumu
kwa njia isiyo halali usilalamike Mwambie Bwana uwasamehe kwa maana hawajui
walitendalo, Ni Mungu peke yake anapohukumu ndiye anayejua anachokitenda,
lakini wanadamu hawajui walitendalo wao wana mipaka najua wako watu wengi sana
wameumizwa serikalini, makanisani, mimi pia niliwahi kuumizwa, niliwahi
kuhukumiwa, niliwahi kusemwa vibaya wanadamu walinihukumu sawa na midomo ya
washitaki zangu, lakini nilinyamaza na namshukuru Mungu kwani amenifundisha
mengi sasa najua wazi kuwa Mungu wangu ni Mungu mwenye kuogopwa sana kwa sababu
Hukumu zake ni za kweli na za haki, kama Bwana alivyonitendea mimi akutendee na
wewe pia, naelewa na nilielewa tangu zamani ya kuwa hakumwacha mtu aliwatendea
haki wote walioonewa, Haki yako itapatikana kwa Mungu aliye hai usikate tamaa
endelea kumtumainia yeye na kumuachia yeye naye atakushangaza, amenishangaza
mara nyingi na namuomba Mungu akushangaze na wewe pia.
Zaburi 105:14-15 “Hakumwacha mtu awaonee,
Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala
msiwadhuru nabii zangu.”
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni