Waebrania 12:14-15 “Tafuteni kwa bidii kuwa
na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana
asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la
uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa
hilo.”
Utangulizi:
Moja ya kanuni za muhimu sana
katika ufalme wa Mungu ni pamoja na swala zima la kuhakikisha kuwa unakuwa na
amani na watu wote, Maandiko yanatoa wito wa kufanya bidii kutafuta Amani na
watu wote, Hili ni jambo la Msingi, Kwa kuwa tuko duniani kuzuka na kutokea kwa
migogoro ni swala la kawaida sana katika jamii hususani watu wanapoishi pamoja,
lakini hata hivyo kama watu wa Mungu au watu wenye ukomavu hatupaswi kuiacha
migogoro hiyo ikadumu kwa Muda mrefu na kuwatia unajisi watu wengine, Migogoro
katika maandiko inafananishwa na shina la uchungu, shina ni chanzo, na kwa
sababu hiyo mti wowote ambao shina lake litakuwa chungu, ni rahisi mti huo
kueneza uchungu katika matawi yake na au hata katika matunda yake na kwa sababu
hiyo katika ukuaji wa kiroho migogoro huathiri utiririkaji wa neema ya Mungu na
kuleta upungufu wa neema ya Mungu katika maisha ya waamini, Lakini tunapofanya
bidii ya kutafuta Amani tunazuia uchungu huo na kujiimarisha kuwa wana wa Mungu
Mathayo 5:9 “Heri wapatanishi; Maana hao
wataitwa wana wa Mungu.” Neno wapatanishi hapo katika lugha ya asili
ya kiyunani linasomeka kama “eirēnopoios” kwa kiingereza “peacemakers” wanaosababisha amani
itokee au iwepo hao ni watu wenye baraka kubwa, wamebarikiwa sana kama maandiko
yanenavyo na kiyume chake wanaosababisha makwazo wanaitwa ole yaani
waliolaaniwa na ambao adhabu kubwa sana inaweza kuwakabili.
Luka 17:1-4 “Akawaambia wanafunzi wake,
Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake!
Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe
baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni; kama ndugu
yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku
moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.”
Wakiyajua haya wazee wetu wa imani
zamani sio kuwa hawakuwahi kukutana na migogoro ya ina mbalimbali walikutana
nayo lakini walikuwa na bidii kuhakikisha kuwa wanarejesha amani au kuepusha
kabisa migogoro miongoni mwao wakitumia busara kubwa sana, kwa sababu hiyo
maandiko yanamtaka kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anatunza amani kila wakati
kunapotokea migogoro ya aina mbalimbali au kuzima kwa haraka migogoro na vyanzo
vinavyoashiria kutoweka kwa Amani kabla mambo hayajaharibika kabisa, Katika
maandiko iko mifano ya watu kama kina Abrahamu, Isaka, na Yakobo na wengineo
ambao kwa namna moja ama nyingine walifanya kila jitihada ya kuhakikisha kuwa
wanadhibiti migogoro na kutafuta Amani ya kudumu katika maisha yao ya uchaji
Mungu na uhusiano na watu wengine, tutajifunza somo hili umuhimu wa kuwa na
amani na watu wote kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Mifano ya
wazee waliotafuta kuwa na amani na watu wote
·
Baraka ya
kuwa na amani na watu wote
·
Umuhimu
wa kuwa na amani na watu wote
Mifano ya wazee waliotafuta kuwa na amani na watu wote.
Neno Amani linalotumika katika
maandiko kwa agano la kale linatumika neno la kiibrania “Shālōm”
na katika maandiko ya agano jipya linatumika neno “eirēne”
kimatamshi “Irene” maneno haya
katika tafasiri ya kiingereza maana yake ni
“it is a condition of being freedom from any kind of disturbance wether
outwardly or inwardly” yaani ni hali ya kuwa mbali na usumbufu wa aina
yoyote wa nje au wa ndani, usumbufu huu unaweza kuwa wa nafsi au familia, au
taifa na kadhalika, neno hilo Shālōm
pia lilitumiwa na Wayahudi kumtakia mtu mafanikio ya kimwili na kiroho na
lilitumika katika matumizi ya kila siku ya kumtakia mtu mema wakati wa salamu,
kwa hiyo hii hasa ndio Amani na utulivu au hali ya kutokuwa na vita au uhasama
au ugomvi na mtu na hii ndio Amani ambayo maandiko yanaagiza tuwe nayo na watu
wote, Amani hii ni msingi mkubwa wa mafanikio na ustawi mkubwa wa mwanadamu
popote alipo duniani.
Maandiko yana mifano mingi
inayoonyesha kuwa wazee wetu katika kusafiri kwao duniani walikutana na changamoto
za namna mbalimbali ambazo zingeweza kuharibu amani na maisha yao pia, lakini
katika namna ya kushangaza sana maandiko yanatuonyesha namna na jinsi wazee
wetu walivyokuwa na busara na hekima iliyopelekea wao kuepusha changamoto za
aina mbalimbali ambazo zingeweza kuwa sababu ya ukosefu wa amani katika maisha yao
duniani na kwa sababu hiyo walifanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa
wanapata Amani hata pale ilipotokea wamehitilafiana na mtu, hapa iko mifano
kadhaa ya watu walioitafuta Amani kwa bidi ona:-
Mfano wa Ibrahimu na Lutu.
Mwanzo 13:5-12 “Na Lutu aliyesafiri pamoja
na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng'ombe na kondoo, na hema. Na ile
nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata
wasiweze kukaa pamoja. Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na
wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa
katika nchi. Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya
mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu
ndugu. Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi;
ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume,
nitakwenda upande wa kushoto. Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la
Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora,
lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari. Basi
Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa
mashariki; wakatengana wao kwa wao. Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na
Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma.”
Wachungaji wa Abrahamu na Lutu
walianza kugombana kwa sababu mifugo yao ilikuwa imeongezeka sana kiasi ambacho
nchi ilikuwa haiwatoshi kwa sababu walikaa pamoja, Abrahamu aliona wazi kuwa
jambo hili lisingelileta matokeo mema na kwa sababu hiyo alimwita Lutu na kutoa
mapendekezo kwa kumsihi ajitenge naye, Abrahamu hakuwa na choyo wala ubinafsi
alimpa Lutu chaguo la kwanza kuchagua na kumueleza wazi kuwa endapo atachagua
kwenda kushoto yeye atakwenda kulia na akichagua kwenda kulia yeye atachagua
kwenda kushoto, hakukuwa na ubinafsi moyoni lakini msingi mkuu ulikuwa ni USIWEPO UGOMVI KATI YA MIMI NA WEWE MAANA SISI NI NDUGU, Abrahamu aliipa
Amani kipaumbele cha kwanza kuliko maslahi binafsi. Aliamini kuwa Mungu
atambariki vyovyote iwavyo bila kujali chaguo lake litamuathiri kwa kiwango
gani:-
Amani ya kweli haipatikani kwa
kushinda siku zote inapatikana kwa unyenyekevu na kuwa tayari kupoteza haki
zako na wakati mwingine hata mazuri tuliyokuwa tukiyatarajia kwa faida ya Amani
yenyewe kuliko mafarakano, Amani wakati mwingine inatutaka kumuachia Mungu na
sisi kujitoa ili Amani iwe faida ya pande zote mbili, kumpata ndugu yako ni kwa
muhimu sana kuliko faida za ubinafsi na tamaa ya moyo! Nyakati tulizo nazo leo
wako watu ambao wako tayari kupoteza ndugu na marafiki kuliko kuitafuta Amani,
Maandiko yanatufunza kuwa Amani ni ya muhimu kuliko kupoteza ndugu au rafiki na
hiki ndio Abrahamu anatufundisha katika maisha yake.
1Wakorintho 8:13 “Kwa hiyo, chakula kikimkwaza
ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu.”
Mfano wa Isaka na Wafilisti (wenyeji).
Mwanzo 26:12-22 “Isaka akapanda mbegu
katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na
mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya
kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na
vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye,
Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka,
Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi Isaka akatoka huko
akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua
vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale
Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita
majina kufuata majina alivyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika
lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari
wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita
jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima
kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko
akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake
Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi
katika nchi.”
Isaka alikuwa na mafanikio
makubwa sana alistawi mno, jambo hili liliamsha wivu kwa wenyeji yaani
wafilisti walijaribu kutafuta na kufukia siri ya mafanikio ya Isaka, Isaka
alikuwa akichimba visima yeye na Abrahamu baba yake walikuwa na ujuzi wa
kuchimba visima, Isaka alipata visima vilivyobubujisha maji na hivyo alivitumia
kwa umwagiliaji na unyweshaji wa mifugo na kwa sababu hiyo alifanikiwa na
kustawi sana, wenyeji waliona wivu, waliogopa mafanikio yake walimuogopa na
yeye pia lakini pia walimsumbua walianza kufukia visima hivyo kwa uchafu
wakimlazimisha kuchimba vingine, hata hivyo kila alipochimba kisima kingine
Wafilisti walikigombania na kudai kuwa kisima ni chao!
Isaka hakupambana nao wala
hakutaka kulipa kisasi wala kutafuta ushahidi kuwa visima vilikuwa mali ya baba
yake na badala yake alihama na kuchimba kisima kingine alifanya hivyo kila mara
walipofukia kisima chake au kukigombania kwa kudai kuwa ni mali yao, hatimaye
alichimba kingine tena na kingine tena na kingine tena na hatimaye mwisho
wakaona aibu wala hawakukigombania tena akakiita kisima hicho “Rehoboth” maana yake Bwana ametufanyia
nafasi, na wafilisti hawakukigombania tena.
Isaka aliipata Amani yake kwa
kukubali kuachilia na kupoteza, alijitahidi kila wakati kuepuka migogoro isiyo
na sababu za kimsingi ambayo yeye aliona itavuruga Amani na hivyo aliamua
kutumia nafasi ya kuachilia (withdraw) au kujiepusha, wakati mwingine ili
kuipata Amani itatugharimu kuachilia, itatugharimu kwenda mbali ili kuepusha migogoro
badala ya kusisitiza haki zetu, hatimaye Mungu ataongeza neema kwa wale
wanaotafuta amani kwa bidii na kwa mioyo yao
1Petro 3:10-12 “Kwa maana, Atakaye kupenda
maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake
isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; ATAFUTE AMANI, AIFUATE SANA. Kwa
kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi
yao; Bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya.”
Mfano wa Yakobo na Labani
Mwanzo 31:22-55 “Hata siku ya tatu Labani
akaambiwa ya kwamba Yakobo amekimbia, akatwaa ndugu zake pamoja naye, akamfuata
mwendo wa siku saba. Akampata katika mlima wa Gileadi. Mungu akamjia Labani,
Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno
la heri wala la shari. Labani akamfikia Yakobo, na Yakobo alikuwa amepiga hema
zake katika mlima, na Labani na ndugu zake wakapiga hema zao katika mlima wa
Gileadi. Labani akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti
zangu kama mateka waliotwaliwa kwa upanga. Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa,
wala hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwa furaha, na nyimbo, na
ngoma, na kinubi? Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi
umetenda upumbavu. Ninao uwezo mkononi mwangu wa kukufanyia madhara; lakini
Mungu wa baba yako usiku huu ameniambia, akisema, Ujihadhari, usimwambie Yakobo
neno la heri wala la shari. Basi sasa, umetoka kwa sababu umetamani sana nyumba
ya baba yako. Mbona basi umeiiba miungu yangu? Yakobo akajibu, akamwambia
Labani, Kwa sababu naliogopa, nikasema, Usije ukaninyang'anya binti zako kwa
nguvu. Awaye yote utakayemwona kuwa nayo miungu yako, yeye asiishi. Mbele ya
ndugu zetu ukitambue kilicho chako kwangu, ukakichukue. Maana Yakobo hakujua ya
kwamba Raheli ameiiba. Labani akaingia katika hema ya Yakobo, na hema ya Lea,
na hema ya vijakazi wawili, wala hakuiona. Akatoka katika hema ya Lea, akaingia
katika hema ya Raheli. Basi Raheli alikuwa amevitwaa vile vinyago ameviweka
katika matandiko ya ngamia, na kuvikalia. Labani akapapasa hema yote wala
hakuviona. Naye Raheli akamwambia babaye, Bwana wangu asikasirike kwa sababu siwezi
kuinuka mbele yako, maana nimeshikwa na mambo ya kike. Akatafuta, wala
hakuviona vile vinyago. Yakobo akakasirika, akagombana na Labani. Yakobo
akajibu, akamwambia Labani, N'nini hatia yangu? Nayo ni nini dhambi yangu, hata
ukanifuatia namna hii? Umepapasa-papasa vyombo vyangu vyote; ni kitu gani
ulichokiona cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya ndugu zangu, na ndugu
zako, wakaamue kati yetu. Miaka hii ishirini nimekaa kwako; kondoo zako wala
mbuzi zako wake hawakuharibu mimba wala waume katika wanyama wako sikuwala.
Kilichoraruliwa na hayawani sikukuletea, mimi mwenyewe nimetwaa hasara yake,
wewe umekidai katika mkono wangu, ikiwa kilichukuliwa mchana, au ikiwa
kilichukuliwa usiku. Hii ilikuwa hali yangu; mchana jua likanipata, na baridi
usiku, usingizi ukanitoka machoni mwangu. Miaka hii ishirini nimekaa nyumbani
mwako; nilikutumikia miaka kumi na minne kwa binti zako wawili, na miaka sita
kwa wanyama wako, nawe umebadili mshahara wangu mara kumi. Kama Mungu wa baba
yangu, Mungu wa Ibrahimu na Hofu ya Isaka, hangalikuwa pamoja nami, hakika sasa
ungalinifukuza mikono mitupu. Mateso yangu na kazi za mikono yangu Mungu
ameziona, akakukemea usiku huu. Labani akajibu, akamwambia Yakobo, Hao binti ni
binti zangu, na wana ni wanangu, na wanyama ni wanyama wangu, na yote uyaonayo
ni yangu; nami naweza kuwatendea nini leo binti zangu na wana wao waliowalea?
Haya! Na tufanye agano, mimi na wewe, liwe kwa ushahidi kati ya mimi na wewe.
Yakobo akatwaa jiwe akalisimamisha kama nguzo. Yakobo akawaambia ndugu zake, Kusanyeni
mawe. Wakatwaa mawe, wakafanya chungu, nao wakala huko karibu na ile chungu.
Labani aliiita Yegarsahadutha, lakini Yakobo aliiita Galedi. Labani akasema,
Chungu hii ni shahidi kati ya mimi na wewe hivi leo. Kwa hiyo likaitwa jina
lake Galedi, na Mispa, maana alisema, Mungu avizie kati ya mimi na wewe, wakati
tusipoonana. Ukiwatesa binti zangu, na ukitwaa wake zaidi ya binti zangu, wala
hapana mtu pamoja nasi, tazama, Mungu ni shahidi kati ya mimi na wewe. Labani
akamwambia Yakobo, Tazama chungu hii utazame na nguzo niliyoitia kati ya mimi
na wewe. Chungu hii na iwe shahidi, na
nguzo hii na iwe shahidi, ya kuwa mimi sitapita chungu hii kuja kwako, wala
wewe hutapita chungu hii na nguzo hii uje kwangu, kwa madhara. Mungu wa
Ibrahimu, na Mungu wa Nahori, Mungu wa baba yao, ahukumu kati yetu. Yakobo
akachinja sadaka katika mlima, akawaita ndugu zake waje wale chakula, nao
wakala chakula, wakakaa usiku kucha mlimani. Labani akaondoka asubuhi na
mapema, akawabusu wanawe na binti zake, akawabariki; kisha Labani akaenda zake,
akarudi kwao.”
Mgogoro wa Yakobo na Labani
ulikuwa mgogoro mkubwa sana Mtu ameishi kwa mjomba wake mwenye hila nyingi
ambaye amemfanyia uonevu wa kila aina, Maandiko yanaweka wazi kuwa Labani
alijaribu kumrubuni Yakobo mara nyingi sana huku akibadilisha mshahara wake
zaidi ya mara kumi, Hali ya maisha katika nyumba ya Labani ilikuwa ngumu mno
kiasi ambacho Yakobo aliamua kutoroka unaweza kuona na kuwaza mtu anamtoroka
mjomba wake kwa siri, huku hakukuwa kuachana kuzuri kwa watu ambao ni ndugu hata
hivyo Labani alibaini na kumfuatia Yakobo akiwa amejawa na hasira nyingi, bila
kujali kuwa amemrubuni Yakobo na kuyatumia maisha ya ujana wake wote kwa faida
zake.
Baada ya kukabiliana kwa maneno
makali hatimaye Yakobo na Labani waliamua kufanya agano ili kwamba asiwepo mtu
atakayempandia mwenzake kwa madhara, Waliamua kusimamisha jiwe kubwa kama
Ushahidi na kulitia mafuta kwamba hakuna mtu aatakayelivuka jiwe hilo kumuendea
mwenzake kwa madhara, Jiwe hilo liliwahakikishia Amani na usalama licha ya kuwa
walikuwa wamejeruhiana moyo kwa siku nyingi na kwa maumivu makubwa, lakini
waliamua kuiacha Amani ishinde na kila mmoja kuendelea na maisha yake.
Wakati mwingine ili Amani
ipatikane hatuna budi kukabiliana na mtu uso kwa uso, na kuyazungumza na kupata
suluhu na makubaliano, Amani inahitaji watu wasameheane, na kujiwekea mipaka
ili Amani iweze kuwepo, Haikuwa rahisi kuipata Amani ukiwa na mjomba kama
Labani, Lakini Labani licha ya kuonywa na Mungu alikumbuka kuwa Yakobo pia ni
mkwewe na mali alizonazo pia ni za wanae na wajukuu zake, waliamua kumaliza
tofauti zao.
Mfano wa Yakobo na Esau.
Mwanzo 32:6-11 “Wale wajumbe wakarudi kwa
Yakobo wakisema, Tulifika kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu
mia nne pamoja naye. Ndipo Yakobo akaogopa sana, na kufadhaika sana,
akawagawanya watu waliopo pamoja naye, na kondoo, na ng'ombe, na ngamia, wawe
matuo mawili. Akasema, Akija Esau kwa kundi la kwanza, akalipiga, kundi
litakalosalia litaokoka. Yakobo akasema, Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, na
Mungu wa baba yangu Isaka, BWANA, uliyeniambia, Rudi uende mpaka nchi yako, na
kwa jamaa zako, nami nitakutendea mema; mimi sistahili hata kidogo hizo rehema
zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nalivuka mto huo wa Yordani
na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa matuo mawili. Uniokoe sasa na mkono wa
ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi namwogopa, asije akanipiga, na mama
pamoja na wana. Walikuwa ni watu ndugu mapacha waliokuja kuumizana sana, Yakobo
alinunua kwa hila haki ya mzaliwa kwa kwanza ya Esau, kama haikutosha Yakobo
aliiba mbaraka wa mzaliwa wa kwanza waliachana kwa uchungu mkubwa sana Esau
akiapa kuwa atamuua Yakobo, baada ya miaka mingi sana Yakobo alipokuwa akirejea
alihofia kwamba Esau atalipa kisasi”
Yakobo na Esau waliachana vibaya
sana, ni mapacha ni ndugu wote wameokoka lakini Yakobo kwa hila alinunua haki
ya mzaliwa wa kwanza na baadaye kuchukua mbaraka wa mzaliwa wa kwanza, jambo
ambalo lilimuudhi sana Esau ambaye aliapa kuwa angemuua Yakobo, wakati Yakobo
anarejea nyumbani alipatwa na hofu kuwa huenda ndugu yake anakuja kumuua,
matukio mabaya na kuachana vibaya kuliweka jeraha kubwa sana katika maisha yao
Yakobo alimuomba Mungu kwaajili ya hofu hiyo.
Yakobo alitumia zawadi, alitumia
maombi kwa Mungu, na aliamua kujinyenyekeza sana na kuinama mbele ya Esau mara
saba kwa hiyo badala ya Esau
kumshambulia alimkimbilia na kumkumbatia na kisha wote wakapaza sauti na kulia,
bila kujali yaliyojiri, walihitimisha mkasa wao kwa kupatana, walichagua Amani
badala ya visasi na viapo vya kumalizana
Amani ya kweli ili ipatikane
inahitaji kujinyenyekeza, toba na kumuomba Mungu, sio hivyo tu na kuwa na bidii
ya kuitafuta, kumuomba Mungu ni kwa Muhimu kwa sababu Mungu anaweza kuponya
majeraha ya ndani kabisa na kujenga tena uhusiano mpya na kuponya majeraha yote
ya ndani tunapochukua hatua ya kuitafuta Amani. Fikiria namna Yakobo
alivyotanguliza zawadi nyingi na jinsi alivyojinyenyekesha sana na Fikiria Esau
alivyoahirisha mpango wake wa kumuua Yakobo, wakati mwingine ni lazima
kujishusha, kununua moyo na nduguyo kwa zawadi na kuonyesha heshima kubwa sana
gharama hizo ndio bidii inayotajwa katika maandiko ya kwamba sio kila wakati
kuitafuta Amani linaweza kuwa jambo rahisi. Lakini inatulazimu kuitafuta Amani
kama agizo la Mungu lilivyo.
Baraka ya kuwa na amani na watu wote
Kuwa na Amani na watu wote ni
jambo lenye Baraka kubwa sana, linaleta ustawi wa kimwili na kiroho kwa wale
wanaotafuta Amani, lakini kisaikolojia na kimwili kuwa na Amani kunapunguza
migandamizo ya mawazo, kunakupa Amani ya moyo inayokufanya kuendelea kukua
kiroho na kiakili, kujenga uhusiano mwema na watu, kuleta ukomavu na ukuaji wa
kiroho, kujenga furaha, kuondoa mashaka, kuleta utulivu na furaha, mawasilano
mazuri msamaha, na kujenga mazingira ya Amani na utulivu, ziko faida kadhaa za
kibiblia pia ambazo zinatokana na kuweko kwa Amani, kama ifuatavyo:-
1.
Uhusiano
wako na Mungu kuimarika - 1Yohana 2:9-11 “Yeye
asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.
Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo.
Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza,
wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.”
2.
Kukubaliwa
kwa sadaka zako – Mathayo 5:23-26 “Basi ukileta
sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu
yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu
yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati
uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi
akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe
hata uishe kulipa senti ya mwisho.”
3.
Kusikilizwa
kwa maombi yako – 1Petro 3:7 “Kadhalika ninyi
waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho
na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu
kusizuiliwe.”
4.
Kusamahehewe
dhambi zako – Marko 11:25-26 “Nanyi, kila msimamapo
na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni
awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu
aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.] ”
5.
Shina
la uchungu lisije likasumbua wengi – Shina la uchungu kwa kiyunani ni “Pikria” kwa kiingereza ni “bitterness” au uchungu, kwa kawaida
shina au mzizi ndio unaosambaza maji na virutubisho katika mmea na majani sisi
kama mwili wa Kristo ni kama mti, shina linapokuwa la uchungu, uchungu huo
unasambaa na kuwanajisi wengine, Neno la Mungu linatutaka tuwe na Amani na watu
wote ili kuepusha kuwanajisi wengine kwa sababu ya uchungu na ugomvi na
ushindani walio nao watu wengine, na kupungukiwa na neema ya Mungu katika
maisha yetu.
Waebrania 12:14-15 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao
hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie
neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu
wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”
6.
Kuonyesha
ujuzi wako wa kumjua Mungu - 1Yohana 4:8-12 “Yeye
asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Katika hili pendo la
Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili
tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali
kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.
Wapenzi ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. Hakuna
mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na
pendo lake limekamilika ndani yetu.”
Umuhimu wa kuwa na amani na watu wote.
Ni jambo la kusikitisha kuona na
kusikia kila mahali siku hizi watu wa Mungu wakiwa mstari wa mbele kwa
migogoro, kila mahali siku hizi inaumiza kusikia kuwa mtumishi huyu hapatani na
huyu, au askofu huyu ana bifu na huyu, Mchungaji huyu haviivi chungu kimoja na
yule, tungetarajia migogoro na
mafarakano kuwa kwa washirika wachanga au kwa watu wasiomjua Mungu, lakini
jambo la kusikitisha ni kuwa migogoro mingi leo inaongozwa na watu wa Mungu
tena wale ambao ni viongozi, au wako katika nafasi ya wao kuwa wapatanishi, au
waamuzi, Inasikitisha kuona leo Mshirika na Mchungaji wake wana ugomvi,
inasikitisha kuona mtu ana ugomvi wa miaka na miaka na mtu mwingine na
hawamalizi alafu ni watu wa Mungu inaumiza sana sana kuona watu wa Mungu wakiwa
hawataki suluhu leo, Najua kuwa maandiko
yanaeleza wazi kuwa siku za mwisho kutakuwa nyakati za hatari na tabia nyingi
mbaya zitajitokeza lakini hata hivyo hayo hayapaswi kuwatokea watu wa Mungu kwa
sababu maandiko yametujulisha kila kitu kwa uwazi lakini kama watu wa Mungu
watakuwa hivyo ni wazi kuwa hakuwezi kuwa na mbingu ya watu wenye mafarakano na
nadhani wote wanaweza kuachwa aliyekwazwa na aliyekwaza pia.
2Timotheo 3:1-5 “Lakini ufahamu neno hili,
ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye
kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye
kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa
kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda
mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;
wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.”
Haiwezekani watu wa Mungu
wanaolijua neno la Mungu na tena wanaolihubiri na kulifundisha kisha wakawa hawataki
Amani inasikitisha sana na tujifunze kutoka kwa wazee wetu wa Imani ambao wao
walikutana na changamoto mbali mbali lakini walihakikisha kuwa wanakuwa na
amani na watu wote, tukumbuke kuwa bila unyenyekevu sio rahisi kuwa na amani, bila
kujishusha na kukubali kupoteza haki zako na kuachilia hatuwezi kuwa na Amani,
kuipata Amani ni gharama, lakini kama tukiweka ubinasfi na maslahi yetu sio
rahisi kuipata Amani, tukikosa uvumilivu na subira ni ngumu kuwa na amani,
tukiwa hatuna msamaha na kuikiishi bila mipaka ni vigumu kwetu kuwa na amani, bila
kuachilia hatuwezi kuwa na Amani, bila kupoteza hatuwezi kuwa na Amani,
haijalishi nani mkubwa nani mdogo bila kuchukua hatua za kipatanishi na
maridhiano na urejesho ni vigumu kuwa na amani neno la Mungu limetuagiza kuwa
na amani na watu wote hivyo hatuna budi kulitii na kulifanyia kazi tafuta
Amani:-
Warumi 12:17-21 “Msimlipe mtu ovu kwa ovu.
Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae
katika amani na watu wote. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu
ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena
Bwana. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana
ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake.Usishindwe na ubaya, bali
uushinde ubaya kwa wema.”
Amani haiwezi kuja yenyewe ni
Lazima itafutwe, na ndio maana Mungu katika hekima yake anatuagiza katika neno
lake anawaagiza wenye haki waitafute Amani
Zakaria 8:16-23 “Haya ndiyo mtakayoyatenda;
kila mtu na aseme kweli na jirani yake; hukumuni kweli na hukumu ya amani
malangoni mwenu; wala mtu wa kwenu asiwaze mabaya moyoni mwake juu ya jirani
yake; wala msipende kiapo cha uongo; maana hayo yote ndiyo niyachukiayo, asema
Bwana. Tena neno la Bwana wa majeshi likanijia, kusema, Bwana wa majeshi asema
hivi, Saumu ya mwezi wa nne, na saumu ya mwezi wa tano, na saumu ya mwezi wa
saba, na saumu ya mwezi wa kumi, zitakuwa furaha na shangwe, na sikukuu za
kuchangamkia, kwa nyumba ya Yuda; basi zipendeni kweli na amani. Bwana wa
majeshi asema hivi, Itatokea halafu ya kwamba watakuja mataifa na wenyeji wa
miji mingi; wenyeji wa mji huu watauendea mji huu, wakisema, Haya! Twendeni
zetu kwa haraka tuombe fadhili za Bwana, na kumtafuta Bwana wa majeshi; Mimi
nami nitakwenda. Naam, watu wa kabila nyingi na mataifa hodari watakuja
Yerusalemu kumtafuta Bwana wa majeshi, na kuomba fadhili za Bwana. Bwana wa
majeshi asema hivi, Siku hizo watu kumi, wa lugha zote za mataifa, wataushika
upindo wa nguo yake yeye aliye Myahudi; naam, wataushika wakisema, Tutakwenda
pamoja nanyi, kwa maana tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nanyi.”
Amani ni ufunguo wa mafanikio na
ustawi wa mwanadamu kimwili na kiroho, unapokuwa na amani inakusaidia kuwaza na
kufikiri maswala ya maendeleo, na kuelekea kwenye ubunifu mkubwa na uzalishaji
katika maisha na kazi zetu na ndoa zetu na familia zetu, kila mtu anapaswa kuwa
na amani ya ndani na nje na mwanadamu anapokuwa na amani na kuitafuta sana
Amani inaleta mchango mkubwa wa ufanisi katika jamii na kutufanya tuishi kwa
furaa na amani, watu Fulani wanapoishi katika migogoro yao ni lazima wajue kuwa
migogori yao inatuumiza hata sisi tulio nje ya migogoro hiyo kwa sababu
hatufurahii kusikia migogoro hiyo upendo haufurahii udhalimu, kila mwenye mgogoro
na mtu malizana nao haraka, wako watu wamekufa wakiwa hawajatengeneza maasi na
maovu na uharibifu walioufanya kwa wenzao na kuwaumiza, wakafanya shingo zao
kuwa ngumu, wakafa wakiwa hawajatafuta Amani!
1Wakorintho 13:4-6 “Upendo huvumilia, hufadhili;
upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;haukosi kuwa na adabu;
hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu,
bali hufurahi pamoja na kweli;”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.
0719990897
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni