Ufunuo
3:14-19. “Na kwa malaika wa kanisa lililoko
Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu
na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. Nayajua matendo yako, ya kuwa hu
baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu
una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa
changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya
kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na
kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto,
upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane,
na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.Wote niwapendao mimi
nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.”
Utangulizi:
Katika kitabu cha Ufunuo 3:17 “Kwa kuwa wasema, Mimi ni
tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u
mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.”
Kutoka katika kifungu kikuu cha somo
letu tunakutana na maneno mazito ya Yesu Kristo kwa kanisa lililokuwako Laodikia.
Katika mstari huo Yesu anakemea na kutujulisha hali ya kiroho ya Kanisa
lililokuwako Laodikia ya kuwa wamepoteza kabisa hali yao ya kuwa matajiri wa
kiroho na badala yake wamekuwa wakijivunia utajiri wa mwilini na kusahau kile
ambacho wanatakiwa kukipa kipaumbele, katika maisha ya kiroho. Katika ujumbe
huu leo Roho Mtakatifu ambaye ndiye Mwalimu wetu mkuu anataka kutukumbusha
umuhimu wa maneno hayo kwa kutufundisha ili tuweze kujifunza na kuchukua
tahadhari katika siku zetu za leo, tutajifunza somo hili “Tajiri lakini masikini” kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-
·
Kwa
kanisa lililoko Laodikia
·
Hali
ya kiroho katika kanisa lililokuwako Laodikia
·
Tajiri
lakini Masikini
Kwa
Kanisa lililoko Laodikia
Laodekia ulikuwa ni moja ya miji
mikubwa sana na mizuri iliyokuwako katika Asia katika bonde la Lycos jimbo la Phrygia eneo ambalo yalikuwako makanisa saba yanayotawa katika
kitabu cha ufunuo ambayo kimsingi yalikuwako kijiografia katika Adia ndogo
yaani eneo la Asia linalopakana na ulaya iliko inchi ya Uturuki leo.au Eneo
lililojulikana kama Kapadokia, Eneo hilo lilibarikiwa sana nyakati za karne ya
kwanza kwa kuikubali injili na kuwa maeneo yenye utajiri wa Kikristo kutokana
na kuhudumiwa na mitume pamoja na watenda kazi waliokuwa wameiva vya kutosha
katika kuifanya kazi ya Bwana kwa kueneza injili na kufundisha.
Ufunuo
1:11 “ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo,
ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira,
na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia.”
Tofauti na historia ya miji mingine iliyotajwa
katika maaandiko hayo hapo, Laodekia ni mji uliojengwa na mfalme Antiochus II kati ya mwaka 261-246 BC Kabla ya Kristo, na mji huu
ukapewa jina la mke wa mfalme huyo Malikia aliyeitwa Laodikia, kwa kiingereza LAODICEA
na kwa kiyunani Laodikia, Jina Laodikia ni muunganiko wa maneno mawili
ya kiyunani “Laos” ambalo maana yake
ni Common People ambalo kwa
Kiswahili ni watu wa kawaida na neno “dike”
ambalo maana yake ni Justice kwa
Kiswahili haki kwa watu wa kawaida, Hiyyo maana kamili ya Laodikia ni watu wa haki au mtu mwenye haki, au Popular Judgement
au Popular Approval ambalo maana
yake mwenye kukubalika sana na watu wa kawaida, au wenye umaarufu, Mji huu
uliundwa kwa pamoja na mkusanyiko wa Wayahudi na Wasiria ambao walisafirishwa
kutoka Babeli mpaka katika miji ya Phrygia na Lydia huku Laodekia ukiwa ndio
mji uliokuwa katika njia kuu, Kutokana na makazi ya kijiografia ulilokuwa mji
huu, Mji ulikuwa na mafanikio makubwa sana kibiashara kiuchumi na viwanda, Kulikuwa
na maendeleo makubwa ya viwanda vya nguo, chuo cha madawa ya tiba na hasa dawa
za macho na dawa nyinginezo na mafanikio makubwa sana ya kiuchumi, Walaodikia
walikuwa na ufugaji wa kondoo wazuri waliozalisha manyoya yaliopelekwa
kiwandani na kuzalisha nguo za viwango vya juu sana, kwa hiyo watu wa Laodekia
pia walivaa vizuri sana na kuuza nguo za hali ya juu, pia walikuwa
watengenezaji wazuri wa Mazuria “Carpets”
jambo ambalo mpaka siku za leo Mazuria kutoka Uturuki yamekuwa na umaarufu
mkubwa sana duniani, kimsingi Laodekia pia ulikuwa ni mji wenye Benki kubwa
yenye utajiri mkubwa wa fedha katika Asia na ulikuwa ni mji wa watu wenye
mafanikio makubwa sana, Mji huu ulikuwa na bomba kubwa la maji yaliyotengenezwa
kutoka katika chemichemi iliyokuwa ikitoa maji ya moto huko Hierapolis mji ulioko maili sita hivi
kutoka Laodikia, maji hayo yalifika mjini na wanawake walikuwa wakichota maji
hayo na kupeleka majumbani mwao, maji yao yalifika nyumbani yakiwa vuguvugu, na
au wakati mwingine yakiwa yamepoa. Paulo Mtume aliwahi kuwaandikia waraka wakristo
waliokuwako Laodikia, katika kanisa lililokuwako huko na kuagiza kuwa wausome
kwa kubadilishana na ule wa Wakolosai, Hata hivyo kwa bahati mbaya waraka huo wa
Paulo Mtume kwa Walaodikia haukuweza kupatikana zaidi ya maelezo yake, kwa hiyo
inakisiwa ya kuwa waraka wa Paulo mtume kwa walaodikia huenda ulipotea au kuna
uwezekano ukawa ni pamoja na ule wa Wakolosai.
Wakolosai
4:15-16 “Wasalimuni ndugu walioko Laodikia, na
Nimfa, na kanisa lililo katika nyumba yake.Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu
fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia
usomwe na ninyi.”
Kutokana na Mafanikio makubwa ya ukazi
wa mji huu watu wake nao walifanikiwa sana na kuwa matajiri mno, Kanisa
lilipoanzishwa katika mji huu lilikuwa na washirika waliokuwa vizuri kifedha na
wenye mafanikio makubwa sana ya utajiri na umiliki wa mali za dunia, Kanisa
lilianzishwa hapa na moja ya watenda kazi pamoja na Paulo Mtume aliyeitwa Epafra, kwa hiyo wakati Paulo mtume
anaandika waraka kwa Wakolosai alikuwa bado hajautembelea mji huu wa Kolosai na
Laodikia na kanisa lililokuwako, Kama tunavyoweza kuona akitamani kuwatembelea
wale ambao hawakuwa wameuona uso wake, Paulo mtume wakati huu alikuwa Efeso kwa
hiyo ni wazi kuwa Epafra mtenda kazi pamoja naye alihubiri katika miji hiyo na kufungua makanisa katika Kolosai, Laodikia na Hierapoli na kutoa ripoti kwa Paulo
mtume ambaye aliamua kuwaandikia kwa kusudi la kuwatia moyo waamini wa eneo
hilo. Akifurahishwa na maendeleo yao kiroho na utumishi wa Epafra. Angalia:-
Wakolosai
1:3-8 “Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu
Kristo, siku zote tukiwaombea; tangu tuliposikia habari za imani yenu katika
Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote; kwa sababu ya tumaini
mlilowekewa akiba mbinguni; ambalo habari zake mlizisikia zamani kwa neno la
kweli ya Injili; iliyofika kwenu, kama ilivyo katika ulimwengu wote, na kuzaa
matunda na kukua, kama inavyokua kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu
sana neema ya Mungu katika kweli; kama mlivyofundishwa na Epafra, mjoli wetu
mpenzi, aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu; naye alitueleza
upendo wenu katika Roho.”
Wakolosai
2:1-3 “Maana nataka ninyi mjue jinsi ilivyo kuu
juhudi yangu niliyo nayo kwa ajili yenu, na kwa ajili ya wale wa Laodikia, na
wale wasioniona uso wangu katika mwili; ili wafarijiwe mioyo yao,
wakiunganishwa katika upendo, wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika,
wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo; ambaye ndani yake yeye hazina
zote za hekima na maarifa zimesitirika.”
Wakolosai
4:12-13 “Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu
Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake,
ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu.
Maana namshuhudia kwamba ana juhudi nyingi kwa ajili yenu, na kwa ajili ya hao
walioko Laodikia, na kwa ajili ya hao walioko Hierapoli.”
Kutokana na mafanikio waliyokuwa nao
watu hao walijiamini sana kwa sababu hata kanisa lilikuwa na hali nzuri ya
kifedha na kiuchumi, na kimsingi Mungu anapenda sana watu wake wafanikiwe wamiliki
fedha na uchumi kwa sababu kazi ya Mungu pia hufanikiwa sana kama tutakuwa na
waamini ambao wako vizuri kiuchumi na kifedha, watu wa Laodekia walikuwa watu
wavumilivu sana na waaminifu mno, mji wao ulikuwa na historia ya kukumbwa na
matetemeko, na uko wakati mji huu uliathiriwa vibaya na tetemeko kubwa na
kuharibiwa na uongozi wa Rumi ulitaka kuwapa msaada wa kifedha kwaajili ya
kuujenga tena mji huo, lakini wakazi wake waliamua kujichangisha wenyewe na
wakaujenga mji huo kwa ubora zaidi ya kwanza tukio hili lilikuwa ni kati ya mwaka wa 60-68 AD kwa hiyo unaweza kupata picha
kuwa walikuwa ni watu wanaojitosheleza na hawakuhitaji msaada hali iliyowapa
kujiamini sana. Kwa hiyo Kanisa la Laodikia walikuwa matajiri sana.
Hali
ya kiroho katika kanisa lililokuwako Laodikia
Kimsingi hali ya kanisa wakati
linaanzishwa ilikuwa ni nzuri na njema sana Epafra alimpa Paulo mtume taarifa
njema ya maendeleo ya makanisa hayo na Paulo Mtume alikubali na kuwandikia
waraka wa kuwatia moyo akiwaombea neema ya kupata kumjua Yesu zaidi, na kuwa na
hekima na ufahamu wa hazina zote za mbinguni, hata hivyo baada ya miaka mingi
baadaye kutoka mwaka wa 60 mpaka wakati kitabu cha ufunuo kinaandikwa yaani
mwaka wa 95-100 hivi Kanisa hili lilianza kuathiriwa na tabia za mkuu wa anga wa
mji ule, na hivyo kanisa lilianza kupoteza sifa njema lililokuwa nazo awali, na
ndio maana Yesu katika waraka wake kupitia Yohana kwenye kitabu cha ufunuo
aliwakemea ili aweze kuwarekebisha na kuwatia moyo ili waweze kuwa washindi
apate kukaa nao katika kiti cha enzi mbinguni, Kanisa lilianza kufunga mlango
kwa Kristo na kuamini ya kuwa wanajitosheleza kwa kila hali jambo lililopelekea
kubaki na utajiri wao wa kiuchumi lakini kuwa masikini sana katika maswala ya
kiroho na kuanza kutia aibu kama watu walio uchi mbele za Kristo.
Ufunuo
3:14-21 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia
andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa
kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala
hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una
uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa
changu.Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya
kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na
kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto,
upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane,
na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. Wote niwapendao mimi
nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.Tazama, nasimama mlangoni,
nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami
nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Yeye ashindaye, nitampa kuketi
pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi
pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.”
Katika kifungu hiki tunaweza kuona ni
changamoto gani ambazo zilikuwa zinalikumba kanisa la Laodikia na jinsi Yesu
Kristo alivyokuwa akishughulikia changamoto zao ambazo zilikuwa zikiwasumbua
1.
Ufahamu
finyu kuhusu Yesu Kristo – Kanisa la Laodikia lilikuwa
limeathiriwa na baadhi ya mafundisho ya waanostisizim na waariyan (Gnosticism and Arians) ambao kimsingi
walimuona Yesu Kristo kama ambaye hayuko sawa na Mungu, na kuwa Kristo ni Roho
iliyoumbwa na Mungu, na ambaye yuko juu kidogo ya wanadamu na malaika lakini
yuko chini ya Mungu, kwa hiyo kulikuwa na mashaka sana kuhusu uungu wa Yesu
Kristo, kama tu leo tunavyoweza kuona baadhi ya watumishi wa Mungu wakianza
kuropoka na kupoteza muelekeo kuhusu uungu wa Yesu Kristo, wao walianza vizuri
wakiamini katika uungu wa Yesu Kristo na katika hali duni na ya umasikini,
lakini walipofanikiwa kupitia jina la Yesu na kufanikiwa na kuwa matajiri na
kuwa na kila kitu, mavazi, magari, na kadhalika wanaaza kutamka wazi wazi na
kukanusha uwepo wa Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu wakilihesabu fundisho
hilo kuwa ni mapokeo, Mafanikio yoyote ya kimwili yakitupa kiburi na kuanza
kupuuzia misingi ya Imani ikiwepo uungu wa Yesu au utatu wa Mungu na kudhani
kuwa fundisho hili ni la kizushi huo ni mwanzo wa kujifikiria kuwa
tumetajirika, na kuwa tuna mavazi mazuri, na kuwa tuna akiba ya kutosha lakini
kwa Mungu ni uchi masikini na mnyonge na mwanzo wa kufilisika kiroho.
Yesu
aliwaeleza Walaodikia ya kuwa Yeye ni Amina, na ni shahidi aliye mwaminifu na
mwanzo wa kuumba kwa Mungu. Ona
Ufunuo 3:14 “Na
kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye
Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, MWANZO WA KUUMBA KWA MUNGU.”
Yesu
alikuwa na maana gani katika kifungu hiki? Yesu alikuwa anajifunua kwa
Walaodikia kwamba wanapaswa kumuamini yeye, wanapaswa kuamini fundisho la kweli
walilopata kulisikia kutoka kwa Mitume kuhusu Yesu ya kwamba yeye ni Bwana, kwa
hiyo hawapaswi kumpuuzia Yesu na kuanza kumfungia mlango kwa kudhani ya kuwa
Yesu, Yeye sio wa kuaminiwa, yeye yuko chini ya Mungu, na yuko juu ya malaika
kiasi tu, wao waliacha kumuona Yesu kama kiini cha Baraka zao na mafanikio yao
na hivyo waliweka Imani katika uchumi na maendeleo makubwa waliyokuwa
nayo. Kwa hiyo Yesu aliwajibu:-
a. Yeye ni Amina – Hali
ya kiroho ya washirika wa Laodikia ilikuwa mbaya wengi wa wanafunzi wake Pale
Laodikia walikuwa tayari wametia shaka kuhusu Yesu Kristo iwapo kweli yeye ni
Mungu? Licha ya mafanikio yao makubwa ya kimwili lakini hali yao ya kiroho
ilianza kuwa mbaya kwa sababu walianza kuukana uungu wa Yesu Kristo na
kumshushia thamani, Yesu akitaka kusema na watu hawa ili apate mwitikio wao
anajiita yeye ni Amina – Neno amina maana yake ni Hakika, Ni kweli, Kwa
hiyo Yesu alitaka kuwahakikishia kuwa anazungumza kweli na kuwathibitishia
ukweli kuwa Yeye ni Mungu, Licha ya kuwa yeye ni Mungu lakini pia ni Msema
kweli na kila kinachozungumzwa katika neno lake ni hakika na kweli na kila
kilichoahidiwa katika neno lake ni kweli, Yesu ni wa uhakika na hakuna
ubabaishaji kumuhusu yeye, Matumizi ya
Amina kwa Yesu Kristo yalikuwa ni uthibitisho ya kuwa yeye ni Mungu kamili na
wa kweli na ndio ufunuo mkamilifu na wa mwisho wa Mungu.Yeye kweli ni Alpha na
Omega.
2Wakorintho
1:20 “Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika
yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa
sisi.”
b. Shahidi aliye Mwaminifu – Yesu
alikuwa kweli anamwakilisha Mungu, yeye ni chapa ya nafsi ya Mungu akiwakilisha
asili na tabia ya uungu, Hakuna ufunuo mwingine zaidi wa Mungu Zaidi ya Yesu
Kristo, Mungu alizungumza na manabii kwa njia nyingi na namna nyingi lakini
siku hizi za mwisho amejifunua kwa Yesu Kristo, Yesu anaposema yeye ni Amina,
Shahidi aliye mwaminifu, alikuwa akifafanua ukweli kwamba hakuna Zaidi yake na
kuwa walaodikia wanapaswa kumuamini kwani Mungu hawezi kusema uongo. “Pistos martus” Shahidi mwaminifu, mfia
Imani wa kweli.
Waebrania
1:1-2 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu
katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi
amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye
aliufanya ulimwengu.”
Tito1:2
– “katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu
asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele;”
Wakolosai
1:13-15 – “Naye alituokoa katika nguvu za giza,
akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika
yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu
asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.”
Yohana
14:6 – “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli,
na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”
Yesu alikuwa akimaanisha kuwa kumfungia mlango
yeye ni kwenda upotevuni, kama kanisa linaamua kumuona Yesu kuwa sio kitu basi
ni lazima kanisa lielewe kuwa linajifungia njia ya kumfikia Mungu baba kwa
namna yoyote ile, Yesu anajiita Amina, na anajiita Shahidi aliye mwaminifu ili
kulithibitishia kanisa ya kuwa hakuna wokovu katika mwingine isipokuwa yeye, na
kuwa ni yeye aliye juu ya yote na hivyo wanapaswa kumuamini na kuonda shaka
kumuhusu. Kiongozi yeyote wa kanisa au kanisa lolote lile linalopunguza Heshima
ya Yesu Kristo linapunguza Heshima ya Mungu vile vile na ufunuo wa kweli ambao
Mungu amejifunua katika neno lake!
c. Mwanzo wa kuumba kwa Mungu – maneno
Mwanzo wa kuumba kwa Mungu na maneno Mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote yote
yana maana moja, waalimu wa uongo walieneza habari ya kuwa Yesu ni mwanadamu wa
kawaida tu na kuwa tofauti yake na viumbe wengine ni kuwa yeye aliumbwa kwanza,
Lakini Yesu alijitambulisha kuwa yeye ni
mwanzo wa kuumba kwa Mungu sawa tu na kusema ni mzaliwa wa Kwanza wa viumbe
vyote, kwa hiyo walaodikia waliamini kuwa Yesu hayuko sawa na Mungu wala sio
Mungu, bali ni kiumbe cha kwanza kuumbwa na Mungu, sawa na Adamu kama mwanadamu
wa kwanza kuumbwa na Mungu, Yesu aliliweka sawa fundisho hilo kwa kuwajibu kuwa
Yeye ni Mwanzo wa kuumba kwa Mungu ona:-
Ufunuo
3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia
andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa
kweli, MWANZO WA KUUMBA KWA MUNGU.”
Maneno hayo mwanzo wa kuumba kwa Mungu
yanasomeka hivi katika Biblia ya kiingereza ya King James Version (KJV) na Katika Biblia ya kiingereza ya New Internation Version (NIV)
Revelation
3:14 “And unto the angel of the church of
Laodiceans write; these this saith the Amen, the faithful and true witness, THE
BEGINNING OF CREATION OF GOD”
Revelation
3:14 “To the angel of the church in Laodicea write;
these are the words of the Amen, The faithful and true witness, THE RULER OF
GOD’S CREATION”
Na
yanasomeka hivi katika biblia ya kiyunani
Revelation
3:14 “Kai angelos ekklēsia Laodikeus grapho; hode
hēde tode lego Amēn, pistos kai alēthinos martus, archē ktisis theos”
Neno hilo
Archē maana yake ni Chief or rank or
application of order in terms of time and place
Sawa
na matumizi ya neno
Wakolosai
1:15 “naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa
wa kwanza wa viumbe vyote.” “Hos hē ho esti
eikōn aoratos Theos prōtotokos pas ktisis”
Kwa hiyo neno Archē ambalo ni Oder na
neno prōtotokos kwa kiingereza protocal
yanamaanisha WA KWANZA KATIKA
CHEO na sio wa kwanza kuumbwa kwa
hiyo Yesu ni Mungu ni kwa kwanza kuwepo kabla hata ya kuweko kwa Muda, yuko
juu ya kila kitu, Kwa hiyo Yesu ni Mungu sawa tu na yanavyoeleza maandiko,
Lakini watu wa Laodikia walikuwa wamedanganyika wakifikiri kuwa Yesu aliumbwa
kwanza na kwa hiyo walianza kupoteza
Imani na Yesu, walipoteza Imani kwa neno lake na wakidhani ya kuwa yeye sio
shahidi wa kweli, Kristo alikuwa akiwaonyesha ya kuwa yeye ni wakuaminiwa, na
alikuwa kwaajili ya kweli na kuwa yeye ni Mungu, “Mimi ni Amina, shahidi aliye muaminifu
mwanzo wa kuumbwa kwa Mungu”
Fundisho kuhusu uungu wa Yesu Kristo sio
fundisho la uzushi, wala fundisho hilo halikuingizwa kwa hila na mkutano wa
aina yoyote wa viongozi, fundisho kuhusu uungu wa Yesu ni fundisho la kibiblia
tangu wakati wa agano la kale na kuthibitishwa na wakati wa agano jipya,
malengo yote na kusudi lote la maandiko ni kumuhusu Yesu Kristo yeye ndio
Mwokozi wa wanadamu, wanadamu hawawezi kujikoa wenyewe, wanadamu wanahitaji
Mungu kwaajili ya wokovu. Na kwa sababu hiyo kama Yesu angelikuwa mwanadamu wa
kawaida asingeliweza kufaa kuwa mwokozi.
Maandiko yenyewe ndiyo yanayomuelezea Yesu
Kristo kuwa ni Mungu na jambo hili liko wazi hata bila kuhitaji ufafanuzi
mwingi kwa mfano nabii Isaya alipotabiri kuhusu kuzaliwa kwa masihi haya ndio
maneno yake ambayo kimsingi aliyatumia kumuelezea Yesu Kristo ona:-
Isaya
7:14 “.Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara.
Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake
Imanueli.”
Isaya
9:6-7 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa,
Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye
ataitwa Jina Lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme
wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti
cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na
kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda
hayo.”
Mfalme
Daudi anamuona Yesu kuwa sio mwanae bali ni Mungu ona
Mathayo
22:41-45 “Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu
aliwauliza, akisema, Mwaonaje katika habari za Kristo? Ni mwana wa nani?
Wakamwambia, Ni wa Daudi. Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika Roho kumwita
Bwana, akisema, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata
niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako? Basi, Daudi akimwita Bwana,
amekuwaje ni mwanawe? ”
Maandiko yanatuthibitishia kuwa Yesu ni Mungu,
na ni muumbaji wa kila kitu na kuwa kila kitu kilitokana na Yeye
Yohana
1:1-3,14 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno
alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.Huyo mwanzo alikuwako kwa
Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote
kilichofanyika.14 Naye Neno alifanyika
mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee
atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”
Kwa hiyo ni wazi kuwa Yesu alikuwa akijitambulisha
kama Mungu kwa Kanisa la Laodikia akiwataka wamuamini, Kristo alikuwa
akijimbainisha kuwa kanisa ni mali yake na kwa sababu hiyo ana mamlaka ya
kuwakemea na kuwarekebisha na kuwa anajua mapungufu yao na anawaona jinsi
ambavyo wamepoa kiroho na kuwa vuguvugu na kuwa na mapungufu Hakuna jambo la
hatari sana duniani kama kanisa lililopoa yaani wakristo wa kimwili, Kanisa au
wakristo waliopoa wanajijua kuwa wamepoa na wanaweza kutubu, lakini wale walio
vuguvugu hujihesabia haki na kujidhani ya kuwa hawahitaji kutubu, Yesu
analionya kanisa la Laodikia ambao wanajidhani kuwa wako salama wakijifikiri
kuwa ni matajiri wa kiroho lakini walikuwa wakijidanganya wenyewe, kwa sababu
katika uhalisia Yesu alikuwa anawaona kuwa Masikini, wanyonge na vipofu na uchi,
maana yake hawakuwa na vazi la haki ya Mungu, Mji wao waliokuwa wakiuishi na
mazingira yake yaliathiri hali zao za kiroho, hii ni wazi kuwa mkuu wa anga wa
eneo Fulani kwa sifa zozote alizonazo huathiri hali ya kiroho ya mazingira
yake, Laodikia uliitwa mji wa haki lakini Kanisa lilikuwa halina haki, Laodikia
ulikuwa na viwanda vya nguo Lakini kanisa Yesu analiona liko uchi, Laodikia
walikuwa hodari katika tiba hasa za macho, lakini Yesu analiona kanisa likiwa
kipofu, Kulikuwa na maji ya vugu vugu na chemichemi za maji ya moto, Lakini
Yesu alikuwa analiona kanisa liko vuguvugu, Laodikia ulikuwa mji wenye dhahabu
lakini Yesu aliwashauri kununua kwake dhahabu iliyo safi Zaidi, kiburi cha
mafanikio ya mwilini waliyokuwa nayo kiliwapiga upofu wa kiroho na wakajikuta
wanamfungia Kristo Yesu nje ya mioyo yao, Yesu alikuwa bado anawapenda na ndio
maana aliwakemea na bado aliahidi kuwa anaendelea kugonga mlango na kuwa wakikubali
kumfungulia ataingia kwao na kufanya makazi nao.
2.
Mimi
ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu;
Kanisa
la Laodikia lilikuwa katika eneo tajiri sana lililojulikana kwa Benki kubwa ya
fedha, viwanda vya nguo, shule za utabibu na madawa, jambo ambalo lilikuwa na
mchango mkubwa sana katika mafanikio ya kimaisha ya waamini wa kanisa pia, kwa
hiyo walijivunia Utajiri na walijiona kuwa hawahitaji kitu, hawahitaji msaada
Neno tajiri katika kiyunani linatumika kama neno “plousios” ambalo lina maana ya Material
wealth and abundance yaani utajiri wa mali na mafanikio mengi ya mwilini,
mafanikio haya yaliwapa kujiamini na kujiona kuwa wanatosha, jambo lililopelekea
wawe na upofu wa kujiona katika hali zao za kiroho, Yesu aliwakemea na
kuwajulisha kuwa walikuwa duni mno kuliko walivyokuwa wakijifikiri.
Ufunuo 3:17 “Kwa
kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe
hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.”
Yesu
aliwakemea kwa kiburi na majivuno ya mwilini kiroho walikuwa ni wanyonge, wenye
mashaka, na masikini na kipofu na uchi. Kimsingi walikuwa wanamuhitaji Yesu kwa
wingi kama alivyotamani Paulo mtume katika dua yake kwamba waijue siri ya Mungu
yaani Yesu Kristo. Lakini badala yake changamoto zifuatazo ziliwaandama
walikuwa:-
Wanyonge – Wretched - talaiporos - wenye
msiba na mateso, wasioridhika na wasio na Amani.
Wenye mashaka – Pitiable - eleeinos - wenye kutia huruma kwa sababu ya hali
yao
Masikini - Poor – Ptochos – masikini
wa kutupwa na mtu liyefilisika, chikoraa
Kipofu - Blind – typhlos – kipofu
asiyeweza kuona kwa macho wala kupambanua kwa akili
Uchi- Naked- gymnos – aliyewekwa
wazi aliyefumaniwa – akiwa hana nguo, kwa aibu
Wakati
kanisa la Laodikia wakizungukwa na mazingira yanayoonekana kuwa na mafanikio
makubwa kiukweli hali yao ya kiroho ilikuwa tofauti na mwonekao wao wa ndani,
Yesu alikuwa akiliona kanisa hili kama kanisa lililoathiriwa na majivuno na kiburi,
kwa sababu ya mafanikio ya nje wakati hali yao ya kutembea na Yesu ni mbaya
sana, hawakuwa na lolote ambalo Yesu aliliona na kulisifia tofauti na makanisa
mengine yale sita, Hali yao ya kujifikiri hawahitaji kitu iliwaongoza katika
kupoa kiroho na kuwa vuguvugu, kuchukuliana na mafundisho potofu, kutokuitetea
imani, na kupoa kiroho huku wakibaki na hali ya udunia uliokithiri jambo ambalo
lilipelekea Yesu awakemee.
Ufunuo 3:16 “Basi,
kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika
kinywa changu.”
Yesu
aliwataka watubu na kubadilika aliwataka waifahamu hali yao ya ndani ambayo ni
mbaya sana
Ufunuo 3:18 “Nakupa
shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na
mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya
kujipaka macho yako, upate kuona.”
Utajiri wa
kweli ni utajiri wa kiroho ambao unapatikana kwa Imani na uvumilivu, Yesu
anawashauri wanunue kwake vazi lililo bora, jeupe, waufunike uchi wao, Huku
akiwataka wapate dawa ya kuona vizuri kwani macho yao na akili zao
zimepofushwa, haki ya kweli ni ile inayopatikana kwa njia ya imani katika
Kristo Yesu, na ni kupitia yeye tunaweza kuangaziwa na kuiona nuru ya Mungu itakayotupa
ufahamu utakaotufanya tutembee kwa unyenyekevu. Haimaanishi kuwa Yeu yuko
kinyume na utajiri na mafanikio ya mwilini, Lakini Yesu alitaka hali yao ya nje
ingeanzia ndani yaani wangekuwa matajiri ndani katika roho zao kwanza lakini
badala yake ikawa kinyume, Bwana alipe neema kanisa la leo, kuwa na utajiri wa
rohoni na mwilini na mafanikio ya rohoni na mwilini pia.
Tajiri
lakini Masikini
Kanisa la Laodikia linaweza kuwa
linawakilisha mtu fulani au kanisa fulani, katika siku za leo watu huoanisha
mafanikio ya kimwili na mafanikio ya kiroho, wanadhani kumiliki mali na kuwa na
mafanikio ni kuwa sawa kiroho au ni kuwa na baraka kubwa za Rohoni, jambo
ambalo linawapelekea watu kuwa na kiburi na majivuno, Hali ya mafanikio ya
kimwili na kuwa na vitu vingi vya mwilini sio mbaya lakini vina mchango mkubwa
sana wa kutupa kiburi na majivuno na zaidi sana kuziba masikio yetu na macho
yetu ya rohoni yanayoweza kusaidia kuona uhalisia wetu na hali zetu za kiroho,
Lazima wakati wote tukumbuke kujipima kuwa ujasiri wetu unatokana na nini? mali
tulizo nazo au hali yetu ya kiroho, Yesu Kristo akiwa ndio mzabibu wa kweli?
Maneno ya Bwana Yesu yanamkumbusha
kila mmoja wetu leo kujipima kiroho chake na kujiangalia hali yake ya kiroho na
kutafuta kwa kina na mapana na marefu utajiri wa Rohoni, na uhusiano wenye
nguvu na Yesu Kristo Bwana wetu Bwana wa utukufu, hatuna budi kuwa na moyo mkubwa
wa kuutafuta mafanikio ya kiroho yaani utajiri wa imani na mengine yakawa ni
maswala yanayofuata tu
Yakobo
2:5 “Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu
hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme
aliowaahidia wampendao? ”
Mathayo
6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki
yake; na hayo yote mtazidishiwa.”
Yesu analitaka kanisa la Laodikia
kubadilika au kugeuka, toba maana yake ni kugeuka, na kuwa waendelee kuutafuta
uhusiano wao na yeye, ili waweze kuvikwa haki ya Kristo na kufuata muongozo
wake, na kupata ufahamu wa Rohoni, na kubaki wakiwa wanyenyekevu, kutambua kuwa
hakuna kitu wanahitaji na cha Muhimu duniani kama uhusiano wetu na Mungu,
Tunamuhitaji Mungu katika kila eneo la maisha yetu, sisi wenyewe na mali zetu
hatutoshi bila Mungu, tunamuhitaji Mungu. Mungu ndiye kila kitu katika maisha
yetu!
Mungu sio kuwa hafurahii mafanikio
Yetu, Mungu anafurahia sana sisi tufanikiwe lakini kamwe hatupaswi kumsahau
Mungu wakati wa mafanikio, tatizo kubwa la kanisa la Laodikia walimfungia Yesu
Mlango, walimuona hana maana tena, kwa sababu ya mafanikio yao kielimu,
kimazingira, na mavazi na madawa na mabenki na maendeleo ya viwanda na uchumi
imara na kila kitu hivyo walifikiri kuwa na hali zao za ndani zimebaki salama
walijiona ni matajiri kumbe walikuwa masikini sana na uchi, wanyonge na wenye
kuhitaji hifadhi, kujiona bora kuliko wengine ni kiburi na majivuno, kuwalaumu
wengine kwa sababu zozote zile ni kujiona una kila kitu, wako watu leo
wanaofikiri kuwa sasa hawamuhitaji Yesu kwa sababu wamejitosheleza katika kila
kitu lakini Yesu akiwaangalia ni masikini, wako uchi na ni wanyonge, lolote
lile ambalo linatupa kiburi katika maisha yetu lazima tuliweke kando na
kutembea kwa unyenyekevu, tukimtegemea Mungu, na kumuamini yeye kwaajili ya
mahitaji yetu yote.
Leo hii unawasikia watu wakisema Yesu
Sio Mungu na ni watumishi wa Mungu lakini wanapata wapi ujasiri wa kutamka hayo
leo hii ni kwa sababu sasa wametajirika kimwili, wameshiba ni kwa sababu
wamefanikiwa na kwa sababu wamekuwa maarufu, na wamekuwa maarufu mpaka kufikia
ngazi ya kupunguza umaarufu wa Yesu Kristo, lakini kiroho wamefilisika,
hawasomi biblia kwa kina na kujua ya kuwa maandiko yenyewe ndio yanayosema Yesu
ni Mungu na sio watu Fulani walioamua kuwa Yesu awe Mungu hiyo maana yake ni
nini ni kwa sababu wameshiba, wamefanikiwa, ni maarufu, wanajulikana sasa
wanaanza kumkufuru yeye aliyewaita na kumfungia mlango kaa nje Yesu wewe ni
kiumbe tu wewe sio Mungu! Kanisa la Laodikia linawakilisha kanisa la leo ambao walifikiri kuwa wanaweza
kujitosheleza, na Yesu alikuwa amefungiwa nje, ni wazi kuwa kanisa la Laodikia
linawakilisha kanisa la siku za mwisho kihistoria ambalo litakumbwa na
ukengeufu mkubwa, pamoja na kuwa na mafaniko ya kiuchumi na utajiri wa vitu
vyenye kuonekana.
Utajiri mwingine ambao watu
wanajivunia ni ule wa kufikiri kuwa wametimiza sheria yote ya Mungu na kuwa
hakuna kitu wamebakiza! Lakini Kristo anapowaangalia anaona kuwa kuna
changamoto kubwa zimebakia ndani yao.
Luka
18:18-24 “Tena, mtu mkubwa mmoja alimwuliza,
akisema, Mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu
akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye
Mungu. Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba
yako na mama yako. Akasema, Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu
aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo
vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate.
Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi. Yesu
alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu! ”
Hii ni aina nyingine ya utajiri, ni
utajiri ambao mafarisayo wengi walikuwa nao, sijui kama watu wa leo wanaweza
kuwa na utajiri huu, huu ni utajiri wa kujihesabia haki, kuishi maisha ya haki
ni mpango wa Mungu lakini hatupaswi kutembea katika kiburi cha kidini na
kudhani kuwa tunaweza kumnunua Mungu kwa matendo yetu, ni vigumu sana kujiona
namna tulivyo na kiburi lakini Mungu anakiona na kwa Roho wake Mtakatifu
anaweza kuikagua mioyo yetu na kuchunguza nia zetu na kutuonyesha namna na
jinsi tunavyojifikiria kuwa ni bora kwa sababu tumetimiza kila kitu ambacho
tunadhani ni matakwa ya sheria za kidini kama alivyokuwa mtu huyo hapo juu
lakini kumbe dhambi ya ubinafsi ilikuwa inamuandama na hakuweza hata kushinda
akionya juu ya tatizo hilo Yesu alitoa mfano huu kabla katika sura hiyo hiyo
Luka
18:9-14 “Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya
kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda
hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama
akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu
wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi
nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule
mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni,
bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye
dhambi.Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko
yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”
Hii ni aina nyingine ya mtu kujifikiri
kuwa amejitosheleza lakini Yesu akipima anaona kuna changamoto kubwa ya watu
kujihesabia haki, linapokuja swala la kuwa mbele za Mungu sisi ni masikini na
vipofu na uchi, ni haki yake Yesu Kristo tu inayotosha kutusaidia kufanya
kuhesabiwa haki mbele za Mungu na wala sio kwa juhudi zetu. Wakati unapojifikiria
kuwa u tajiri kumbe Yesu anakuona ni masikini, wakati unapofikiri kuwa u mwenye
haki, Yesu anakuona u uchi kabisa Bwana ampe neema kila mmoja wetu kumfanya
Yesu Kristo kuwa utoshelevu wetu katika jina la Yesu Kristo amen!
Na
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu
wa wajenzi mwenye hekima.