Jumapili, 15 Machi 2026

Akilishika neno la imani vile vile kama alivyofundishwa!


Tito 1:7-9 “Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu.bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.”



Utangulizi:

Mojawapo ya sifa muhimu za viongozi wa kanisa ni pamoja na kuwa waaminifu katika mafundisho sahihi ya imani yetu (Sound Doctrine) na neno la Mungu, Paulo mtume alikuwa amemuacha Tito mtenda kazi pamoja naye katika makanisa yaliyokuwa katika kisiwa cha Krete moja ya kisiwa kikubwa na maarufu sana katika nchi ya Ugiriki, kwa kusudi la kuweka viongozi zamani waliitwa wazee (yaani wachungaji) katika makanisa yaliyokuwako huko.

Tito 1:4-5 “kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu. Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;”

Hata hivyo katika sifa kadhaa zilizoainishwa na Paulo Mtume kwaajili ya kuchagua viongozi mojawapo ya sifa muhimu sana ilikuwa inahusu kuchagua au kuweka watu ambao watalifundisha neno la Mungu vile vile kama wao walivyofundishwa, hili ilikuwa ni agizo muhimu sana kwa sababu Mafundisho sahihi ni sawa kabisa na mlo kamili wa chakula chenye virutubisho vyote muhimu vinavyohitajika katika mwili wa mwanadamu na mafundisho sahihi vile vile ni ya muhimu katika kanisa la Mungu kwa mustakabali wa kanisa kuwa na Afya njema, ukuaji mzuri wa kiroho, uhakika wa wokovu, na ulinzi wa kanisa dhidi ya mafundisho potofu, kuwanoa waamini, kukuza umoja wa kanisa na kuutunza utakatifu na maisha ya haki kutendeka kwa kazi ya huduma. Kwa msingi huo Kanisa linapochagua watenda kazi, wanafunzi na wenye hekima linapaswa kuhakikisha kuwa watu hao wanateuliwa kwa sababu wameshiba mafundisho yaliyo sahihi na wako tayari kwa huduma na si kwa sababu wana cheo, pesa na heshima fulani huko duniani, kwa Msingi huo leo tutachukua muda kujifunza somo hili muhimu “Akilishika neno la Imani vile vile kama alivyofundishwa!”, na tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Maana ya kulishika neno la Imani vile vile.

·         Umuhimu wa kulishika neno la Imani vile vile kama ulivyofundishwa.

·         Akilishika neno la Imani vile vile kama alivyofundishwa!,

Maana ya kulishika neno vile vile.

Ni muhimu kufahamu kuwa kulishika neno la Mungu vile vile kama unavyofundishwa maana yake kwa Kiyunani  linatumika neno “antechomenon” au “antechomai” ambalo kwa kiingereza linatumika neno “holding fast to” au “adhering to” au “clinging” au “to hold firm” kwa lugha nzuri ya Kiswahili maana yake ni kushikamana, kung’ang’ania  au kutetea kwa uthabiti, kwa hiyo moja ya sifa ya kiongozi wa kanisa anapaswa kuwa king’ang’anizi, linapokuja swala la kushikamana na Mungu au mafundisho yake hapaswi kuwa mtu unayeyumbishwa, anapaswa kuwa mtu mwenye uwezo wa kusimamia kile unachokiamini kwa nguvu na hakuna mtu wa kukubadilisha.

Ayubu 2:9-10 “Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe. Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.”

Sifa ya kushikamana na mafundisho ya mitume au injili ya kweli na mafundisho yaliyo sahihi ilikuwa na umuhimu mkubwa sana nyakati za kanisa la kwanza kama ilivyo na umuhimu mkubwa zaidi katika nyakati za leo, kwa hiyo mtu aliyependekezwa kuwa kiongozi alipaswa kuwa na sifa ya kuenenda vile vile kama alivyofundishwa, hakuna uhuru wa kuibadili injili, kwa hiyo kiongozi alikuwa hawezi kupotoshwa wala kuyumbishwa na hawezi kuogopa au kusita kuukemea uwongo, Lengo la kuwafanya wakristo kuwa wanafunzi ni ili wasivutwe kufuata mafundisho ya uongo.

Waefeso 4:11-14 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.”

2Timotheo 4:2-4 “lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.”  

Nyakati za kanisa la kwanza walikuwa makini sana kuhakikisha kuwa mtu wanayemkaribisha anakuwa na imani ile ile iliyofundishwa na kukubalika na mitume, Mitume waliagiza kuwa hakukuwa na sababu ya kumchekea mtu ambaye hakai au haleti mafundisho yao, walikazia kuwa mtu wa namna hiyo ikiwezekana wasimkaribishe wala hata wasimsalimie, mwenye dhambi anaweza kubadilika hata pole pole, lakini mafundisho ya uongo hata salamu asipewe

2Yohana 1:8-11 “Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu. Maana yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu.”

Kanisa linapaswa kusimamia msimamo huu, kuhakikisha kuwa kila mtu anayekaribishwa katika kanisa letu anakuja na fundisho lililo sahihi, anakuja na msimamo ule ule waliokuwa nao mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo, au mtu anayechaguliwa kuwa kiongozi katika kanisa analishika neno la imani vile vile kama tulivyofundishwa na sio vinginevyo, mafundisho ya mitume yanapaswa kushikiliwa kama mila na desturi ya kanisa na kurithishwa katika kizazi kinachokuja hata akifufuka Paulo mtume leo atatukuta tukihubiri injili ile ile aliyoiacha na atatukuta hatujaichakachua injili wala hatuhubiri injili nyingine, na tutakemea kwa Mamlaka yote, kuonya na kukaripia. Kwa mafundisho yenye uzima. Haiwezekani Leo kiongozi mkubwa kabisa wa imani hatambui utatu na anachekewa

Umuhimu wa kulishika neno la imani vile vile kama ulivyofundishwa

Ni muhimu kufahamu kuwa mitume walikuwa wakali sana na swala zima la mfundisho ya uwongo kuliko tunavyofikiri, kwa bahati mbaya makanisa mengi leo wamekuwa wakali kwa dhambi jambo ambalo sio baya, kuliko kwa mafundisho potofu, dhambi inaweza kutubiwa na mwenye dhambi anaweza kubadilika, ukuaji wa kiroho ni mchakato na sio jambo la hatari kwa kanisa kwa sabahu Kristo alikuja kuokoa, lakini mafundisho potofu ni chachu na inaweza kubadilisha na kuathiri muelekeo mzima wa mwili wa Kristo na kwa sababu hiyo mitume walikuwa wakali sana na watu wanaofundisha uongo, Paulo mtume anamwagiza Tito kuwa makini kuwachagua watu wenye msimamo katika mafundisho yetu kwa sababu kisiwa cha Krete kilikuwa ni miongoni mwa sehemu zilizoathiriwa na mafundisho ya uongo kwa hiyo waliopendekezwa kuchaguliwa kuwa viongozi walipaswa kuwa watu hodari ambao wanauwezo wa kufundisha, kukemea, kuonya  na kuwazidi wale wanaowapinga au wale wanaoipinga kweli

Tito 1:4-5 “kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu. Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;”

Tito 1:7-9 “Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu.bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; AKILISHIKA LILE NENO LA IMANI VILE VILE KAMA ALIVYOFUNDISHWA, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.”

Kulikuwa na walimu wa uongo kule Krete, watu walikazia sheria ya Musa na mafundisho ya tohara, na pia watu walijitafutia mapato kupitia dini, kwa sababu hiyo suluhisho halikuwa miujiza bali suluhisho lilikuwa ni kupata watu sahihi watakaosimamia misingi ya Imani ya mitume na kuifundisha vile vile kama walivyofundishwa na wenye sifa ya kuweza kung’amua na kuyapinga au kuwashinda wale wenye kupinga kama alivyokuwa mtu wa Mungu Stefano, Paulo alikuwa anataka viongozi wawe wakali kwenye fundisho sahihi wenye sifa za ugumu wa kusimamia Imani na kupinga mafundisho ya uongo na kuwakemea waongo kwa nguvu zao zote, watu wenye uwezo wa kuwashinda wapingao na kuisimamia Imani kwa uaminifu hata kaa itawagharimu kufa 

Tito 1:10-14 “Kwa maana kuna wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, wadanganyaji, na hasa wale wa tohara, ambao yapasa wazibwe vinywa vyao. Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu. Mtu wa kwao, nabii wao wenyewe, amesema, Wakrete ni waongo siku zote, hayawani wabaya, walafi wavivu. Ushuhuda huo ni kweli. Kwa sababu hiyo uwakemee kwa ukali, ili wapate kuwa wazima katika imani; wasisikilize hadithi za Kiyahudi, wala maagizo ya watu wajiepushao na yaliyo kweli.”

Matendo 6:8-10 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano;lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.”

Kanisa linapaswa kuwa makini kuhakikisha kuwa linasimamisha watu waliojaa neno la Mungu, watu wenye injili iliyosahihi, watu wanaofunzwa vizuri ili kuirithisha Imani iliyosahihi kwa kizazi kinachokuja, leo hii kumejaa upuuzi wa kila aina kila kona kwa sababu ya uzembe wa Kanisa, Kanisa linafukuzana na mambo mengine na linaacha kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa neno la Mungu, ni lazima tuikabidhi injili kwa watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine vile vile kama walivyofundishwa, dunia ikijawa na mafundisho ya uongo leo sababu kubwa ni uzembe wa Kanisa kutokuwafundisha watu neno la Mungu, Kanisa ni lazima liwe kama shule ukiachanana maombezi na miujiza ambayo nayo ni ya muhimu lakini bila kusahau kuwafundisha watu neno, watu ni lazima wajae neno, dunia ni lazima ijawe na mafundisho yetu mpaka wakuu wa dini pinzani walalamike kama ilivyotokea kwa Masadukayo. 

2Timotheo 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.”

Matendo 5:27-29 “Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”

Kila kanisa ambalo linaamini kuwa lina mafundisho ya kweli basi lina wajibu wa kuijaza dunia na mafundisho hayo ya kweli kwa kuihubiri injili kila mahali, kufanya wanafunzi na kuijaza dunia na mafundisho yetu, kama hatufanyi kazi hiyo itafanywa kwa uaminifu na mashahidi wa Yehova, Mormonisim, Wasabato, na imani nyinginezo nyingi, injili za mafanikio, injili za neema iliyozidi, injili za sheria, na injili nyingine nyingi na usikasirike wakiwa na televisheni, magazeti na washuhudiaji wanapita nyumba kwa nyumba wakieneza mafundisho yao maana wewe hutaki na mafundisho yako lakini pembeni pembeni unadai una Imani ya kweli lakini umekaa nayo kimya na kazi yako ni kukosoa tu pembeni utasikia jihadharini na mafundisho ya mitandaoni, ahaaaa we ya kwako ya mitandaoni yako wapi na kwa nini hurushi? Kwa hiyo wadhani Kristo hana wanaohubiri kweli mitandaoni? Mwone kwanza lihubiri neno fundisha kweli eneza kweli kwa njia zozote, wafundishe washirika kupambanua mchele na chuya!   

Akilishika neno la Imani vile vile kama alivyofundishwa!.

Unadhani kuna faida gani ya kuwa na umati mkubwa wa watu, kuwa na sauti nzuri, kuwa na karama za kila aina, kutajirika na kubarikiwa sana na kuwa na walinzi na msafara wa magari lakini ukawa hauifundishi kweli? Kiongozi wa kweli wa imani ni lazima awe mwanafunzi mzuri wa neno la Mungu, awe mtetezi wa kweli wa imani, awe na uwezo wa kung’amua uongo na kuukemea kwa nguvu na kuukaripia au kuujibu kwa neno la Mungu, lakini zaidi sana awe mwaminifu kwa mafundisho ya mitume, na sio kwa sababu umerithi tu bali pia kwa sababu umelichunguza na kujithibitishia kuwa unaamini jambo lililo sahihi, mmesikia siku za Karibuni katika mitandao wahubiri wakubwa kabisa wenye umati mkubwa wa watu wakikanusha na kuushambulia na kupinga fundisho la utatu wa Mungu na watu wenye kweli wamekaa kimya tu hii ni mojawapo ya hatari iliyo wazi kuwa nyakati za leo tuna watu wengi tu wanaofuata mkumbo, kama watu wangekuwa wanafundishwa kweli ya Mungu kwa usahihi  na wakawa na uwezo mkubwa wa kupambanua nadhani siku ile wanamsikia kiongozi wao akisema hakuna Utatu ingekuwa ndio siku ya mwisho kuabudu hapo, lakini dunia imejaa vipofu, na viongozi wa vipofu, wala hawaoni kuwa hili ni tatizo kubwa!.

Kama kanisa tangu mwanzo lingezalisha watu wasioyumbishwa, imani yetu ingebaki kama ilivyokuwa nyakati za baba zetu, lakini siku za leo kumejaa nyumbu wengi makanisani ambao wanayumbishwa kila kukicha na Imani mbalimbali na imekuwa ngumu kwao leo kujua ipi ni sahihi na ipi ni potofu watu hawajui kupambanua. Mtu anayeishika Imani vile vile ni mtu asiyetikisika kwa sababu anajua alichokiamini na hawatikiswi na lolote wanashikamana na kile walichokiamini bila kujali wanapitia nini

-          2Timotheo 1:12-14 “Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile. Shika kielelezo cha maneno yenye uzima uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.”

 

-          Matendo 5:27-29. “Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”

 

Kanisa ni lazima tujikite katika kuandaa viongozi ambao watakuwa watata, wenye kumfuata Yesu na kukataa kuyachakachua maneno ya Mungu kwa gharama yoyote hata kama itawagharimu kuteseka na kuuawa, lazima tuzalishe viongozi mahiri wenye uwezo wa kumuigiza Yesu, kuwa hatukuja duniani kuwapendeza wanadamu bali tumekuja kuwatumikia watu kama yeye mwenyewe, lazima tuzalishe watu wenye nguvu, wenye akili wanaolijua neno ambao watasimama kuitetea Imani hata wakati wa mambo magumu na kuwasaidia watu kuijua kweli na kuisimamimai kwa gharama yoyote kwa sababu hiyo pamoja na sifa nyingine isisahahulike sifa hii muhimu ya kwamba imempasa askofu au kiongozi wa kanisa awe mtu anayeisimamia Imani vile vile kama alivyofundishwa .

Tito 1:7-9 “Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu.bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mqwenye Hekima

Hakuna maoni: